Jumanne, 1 Oktoba 2019

Bwana atawapigania nanyi mtanyamaza kimya!


Kutoka 14:10-14 “Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia BWANA. Wakamwambia Musa, Je! Kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri? Neno hili silo tulilokuambia huko Misri, tukisema, Tuache tuwatumikie Wamisri? Maana ni afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani. Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya”.


Utangulizi:

Kutoka kwa wana wa Israel katika nchi ya utumwa huko Misri ilikuwa ni kama ishara kuu ya mwanzo mpya wa taifa la Israel, ilikuwa ndio siku yao ya kupata uhuru chini ya uongozi shupavu wa Musa, Hii ilikuwa ni siku ya kukumbukwa mno, Mungu mwenyewe aliwaamuru waikumbuke siku ile; Siku waliyokula Kondoo wa Pasaka!, Siku waliyoondoka katika nchi ya utumwa huko Misri.

Kushushwa kwa Bendera za kikoloni katika Nchi nyingi za Afrika na kupandishwa kwa bendera huru za mataifa ya Afrika ulikuwa ni mwanzo mpya wa matumaini makubwa ya kuishi kwa furaha na amani na utulivu tukiwa na Uhuru wetu, Kuoa au kuolewa, kwa wengi wetu ulikuwa ni mwanzo wa maisha mapya ya matumaini, hali kadhalika kumaliza shule na kupata vyeti vyetu vya aina mbalimbali, ulikuwa ni mwanzo mpya wa matumaini ya maisha mapya ya ndoto zetu, kuanza biashara, na mipango mingine mingi na hata kuokoka na kuanza imani yetu kwa nguvu tukiwa na uhusiano mgumu wenye nguvu na Mungu kote kunatujengea matumaini mapya na mwanzo mpya wa furaha na amani nyingi. Hii ni hali ya kawaida katika maisha ya binadamu, bila matumaini hatuwezi kuwa na mwanga mpya unaotuongezea nguvu ya kuishi na kusonga mbele. Lakini kama ilivyokuwa kwa wana wa Israel siku ile walipotoka Misri na utumwani kwa furaha; Uhuru wao ulionekana kama sio uhuru kamili kwa sababu Farao mfalme wa wamisri alighairi mpango wake wa kumuachia Musa na wana wa Israel kuwa huru, na hivyo yeye na majeshi yake yote walikusudia kuwarejeza utumwani, katika nchi ile ya taabu kule walikoteseka mpaka wakamlilia Mungu ili awaokoe! Hebu kumbuka walivyolia mpaka Mungu akawasikia na kumtuma Musa


Kutoka 3:7-10 “BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa. Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri.

Hali ya wana wa Israel kule utumwani Misri ilikuwa mbaya, Misri wakati huu lilikuwa ndio taifa kubwa duniani (Super Power Nation), walikuwa na Teknolojia ya hali ya juu kwa wakati huo nguvu ya kijeshi na kiuchumi ya hali ya juu ya ulimwengu wa waakati ule, utaratibu wa Kalenda za mwaka, sayansi ya tiba lakini nguvu za kiuchumi na kijeshi hali kadhalika uwezo wa nguvu za giza, wachawi na uabudu miungu uliokithiri; hakukua na taifa lingeweza kuthubutu kupigania uhuru wa Israel kutoka Misri isipokuwa Mungu mwenyewe, Na kwa hakika Mungu aliwasaidia, Mungu alimuadhibu Farao kwa mapigo makubwa mazito kumi ambayo yalimpelekea Farao na kiburi chake chote kusalimu amri, na kuwapa ruhusa Israel waende zao, maandiko yanasema Israel walindoka kwa jeuri/kwa kujiamini wakiamini kuwa chini ya Mkono wa Mungu na Musa mtumishi wake hakuna linaloshindikana lakini wakiwa katika kilele cha kufurahia mapinduzi yaliyofanywa na Mungu kwaajili yao na uhuru mzima walioupata Misri, Farao alihairisha mpango wa Mungu wa kuruhusu Israel iweze kuwa huru na kufurahia amani, kujitawala na kujitegemea! Akaamua awafuatilie na kuwarejesha Misri. Angalia.

Kutoka 14:5-8 “. Mfalme wa Misri aliambiwa ya kuwa wale watu wamekwisha kimbia; na moyo wa Farao, na mioyo ya watumishi wake, iligeuzwa iwe kinyume cha hao watu, nao wakasema, Ni nini jambo hili tulilotenda, kwa kuwaacha Waisraeli waende zao wasitutumikie tena? Akaandalia gari lake, akawachukua watu wake pamoja naye; tena akatwaa magari mia sita yaliyochaguliwa, na magari yote ya Wamisri, na maakida juu ya magari hayo yote. Na BWANA akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata wana wa Israeli; kwa sababu wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri.

Mpango wa wana wa Israel wa kufurahia uhuru wao na mpango mpya wa Mungu ulikuwa katika mashaka makubwa sana Baada ya Farao na majemadari wake kufikiri vinginevyo! Ni swala la kawaida sana kwa wanadamu kufikiri na kupanga mipango na mara tunapoiona mipangp hiyo imenyooka huwa tunajawa na furaha kubwa sana, tunakuwa na matumaini makubwa sana, na kuwaza maisha katika mwanga ulio bora!, je hujawahi kuona harusi kubwa na za kifahari zikifungwa? na nyingine kurushwa moja kwa moja katika vituo vya televisheni na watu mashuhuru wakihudhuria? Je huwa inachukua muda gani kuona ndoa hizo zikidumu na kukosa migogoro, ni mara ngapi tumeona na kushuhudia waliopendana wakitengana na kuanza kutumiana vijembe kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, mara ngapi watu wamekuwa na mipango mizuri ya kibiashara na wakaianza kwa ujeuri/kwa matumaini lakini inafikia kati kila kitu kinasambaratika? Mara ngapi tumewasaidia watu na kisha wakageuka kuwa mwiba katika maisha yetu, mara ngapi tumesalitiwa na tunaowapenda na kuwaamini? Mara ngapi ndoto zetu zimezimika na tukabaki tunalia na kutamani hata kufa? Mara ngapi tumejuta katika maisha yetu kuwa kama tungalijua yatupasayo kufanya tumgeweza kuyafanya hii ndio ilikuwa hali ya wana wa Israel walipotazama nyuma na kuona majeshi ya Farao yakiwakabili, ukweli ni kuwa walivunjika moyo na walikata tamaa sana, walimlilia Mungu lakini pia walimlaumu Musa, na waliona ilikuwa vema kama wangelikuwa watumwa wa wamisri kuliko kufia jangwani, walimlaumu Musa waliona kama mipango yake ilikuwa ikileta maumivu makubwa zaidi kuliko kule walikokuwa wakitoka walilia kwa kukata tamaa!

Kwa mujibu wa maelezo ya wataalamu wa Kijeografia eneo ambalo waisrael walikuweko lilikuwa ni eneo ambalo hawangeweza kwenda kushoto wala kulia wala kurudi nyuma, Nyuma ya Israel walikuwa wakikabiliwa na wamisri na mbele yao ilikuweko bahari ya shamu, kushoto na kulia kwao hakukuwa na upenyo ukweli walikuwa katika eneo dhahiri lisilo na upenyo, waliwekwa kwenye kona na ni wazi kabisa kilichokuwa kinawakabili kwa macho ya kawaida ilikuwa ni kifo tu, au kurudi utumwani, hawakuwa wamefunuliwa mpango kamili wa Mungu, hawakuwa wanajua kwamba kile alichokisema na kukifanya Mungu kulipaswa kuaminiwa kwa gharama yoyote ile  bali walikata tamaa! Tena walivunjika moyo na zaidi walilia machozi!

Hapa ninazungumza na watu ambao wamekata tamaa, matumaini yao ya kupona, kufanikiwa katika nyanja mbalimbali yanaonekana kama yamegonga ukuta, wale waliokuwa na ndoa zenye furaha na amani na mahusiano bora yaliyokuweko wakati wa uchumba wao sasa wanakutana na hali tofauti kabisa ndani ya ndoa zao, wale waliokuwa wakisomea fani za aina mbalimbali na kuwa na ndoto za kupata kazi na kuajiriwa sasa wametundika degree zao, hawana ujuzi wowote kila kazi wanayojaribu kuiomba wanaambiwa kuwa inahitajika mtu mwenye uzoefu, wengi wanajuta heri nisingechukua degree ya sheria, ualimu, uchumi, siasa, uongozi, miamba na kadhalika, Nchi nyingi za Afrika pia zimepitia katika hali kama hizi, watu walipopata uhuru walitegemea kuwa watakuwa na wakati mzuri wa kufurahia uhuru wao, walijua mambo yatakuwa mteremko baada ya kuwafukuza wakoloni, Japo wengi wamepiga hatua lakini wengi wanajuta na kusema heri tungeendelea kutawaliwa na wakoloni, hawajui mpango wa Mungu wa kutuacha tukawa huru, waliooa na kutana na changamoto wanajuta na kusema heri nisingeliolewa au heri nisingelioa, waliookoka wanaweza kusema heri nisingeliokoka, na hata walioitwa wanaweza kusema heri nisingelikubali wito wa kumtumikia Mungu, wengine wametumbuliwa, wengine wamepoteza umaarufu, wengine kila wakijaribu kutoka ni kama iko nguvu inawakandamiza chini ni kama hawaoni upenyo na wamekata tamaa wanalia kwa sababu hawazijui njia za Mungu,  waliojaribu biashara  wanasema ningejua nisingelijaribu biashara hii, waliotapeliwa na kulizwa wanajuta kwa kusema laiti ningelijua! Kuna majuto na kukata tamaa kila sehemu katika maisha yetu mambo hayapaswi kuwa hivyo!

Ni muhimu kuwa na ufahamu wa kutosha ya kwamba Mungu hataki tukate tamaa, Yeye anao mpango kamili juu ya maisha ya kila mmoja wetu, wakati mwingine Mungu anao mpango mzuri moyoni mwake na wakati mwingine anaweza kulifunua alifanyalo au atakalolifanya kwa kupitia watumishi wake au wale wanaotuongoza kisiasa lakini pia tunaweza kuyajua mapenzi yake kwa kuliangalia neno lake, Hakuna sababu ya kumlaumu Mungu, wala kuwalaumu viongozi wetu wala sera kadhaa za Taifa letu wala hatupaswi kujilinganisha na wengine tusikate tamaa Mungu hawezi kutuwazia mambo mabaya kama ilivyokuwa kwa wana wa Israel Mungu anatuwazia mema Neno la Mungu linasema katika
Yeremia 29:11 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho
.

Mungu alikuwa na mpango mwema kwa wana wa Israel alikusudia kuwaweka huru kweli kweli alikusudia kuwasambaratisha wamisri ili wasirejee tena tabia yao ya kuwafuata fuata watu wa Mungu lakini mpango huu haukuwa wazi kwa Israel wote hawakuelewa, machoni pao waliona kifo na hali ya kukatisha tamaa lakini Musa alikuwa ameelezwa wazi na Mungu na kwamba angeshughulika na Farao angalia

Kutoka 14:1-4 Biblia inasema hivi “BWANA akasema na Musa, akamwambia, Waambie wana wa Israeli, kwamba warudi na kupiga kambi yao mbele ya Pi-hahirothi, kati ya Migdoli na bahari, kukabili Baal-sefoni; mtapanga mbele yake karibu na bahari. Naye Farao atasema katika habari za wana wa Israeli, Wametatanishwa katika nchi, ile jangwa imewazuia wasitoke. Nami nitaufanya uwe mgumu moyo wa Farao, naye atafuata nyuma yao; nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote; na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Basi wakafanya hivyo.  

Unaona Mungu hakuwa amemweleza Musa kuwa atafanya nini lakini Mungu alikuwa amemthibitishia Musa wazi kuwa hali watakayoipitia wana wa Israel italeta utukufu mkubwa kwa Mungu! Na ndio maana walipokuwa wakilalamika na kuonyesha kukata tamaa kutokana na hofu kuu Musa alikuwa anajua wazi kuwa Mungu atafanya jambo, Mungu atafanya kitu katika maisha yao alifahamu wazi kuwa Bwana atawapigania na kuwa nao watanyamaza kimyaa, Mungu alimwambia Musa kuwa awaambie wana wa Israel wasonge mbele waendelee na mpango wa kuelekea kanaani bila kujali kuwa nini kinawakabili nyuma yao.

Tatizo kubwa la wana wa Israel walikuwa hawayajui kabisa Mapenzi ya Mungu, wala hawakujua kuwa walikuwa wanapaswa kufanya sehemu yao wao walipaswa kusonge mbele, walipaswa kuendelea kujaribu tena na tena bila kukata tamaa walipaswa tu kusonga mbele, nisikilize kuwa mjane hakumaanishi kuwa Mungu amekusudia uaibike, kuwa yatima haimaanishi kuwa Mungu amekusudia kukwamisha mpango wake kwako, kufilisika au kushindwa kulipa mkopo wako haimaanishi kuwa kila kitu kimeishia hapo, kutumbuliwa au kuondolewa madarakani hakumaanishi kuwa Mungu amemaliza na wewe Mungu ana makusudi mema na mpango na maisha yako wewe songa mbele Liko jambo jema usilolijua limefichwa nyuma ya jaribu lako na ushindi wake ni wewe kutokukata tamaa.
Iko mifano kadhaa ya watu ambao walikutana na changamoto mbalimbali katika maisha yao na walisonga mbele na wakawa watu wakubwa sana duniani na maarufu sana lakini waliishinda siri ya kukata tamaa, walishinda vikwazo, walishinda sauti za nje zinazowambia umekwisha, huwezi tena na kadhalika ni marufuku kabisa  kukata tamaa, ni mwiko usikate tamaa ni sumu yaw ewe kuinuka tena angalia mifano hii
1.      Mwana sayansi Thomas Edison tumtafakari!

Je umewahi kufeli katika maisha yako labda mara moja au mbili? Je mwalimu wako amewahi kukuita mjinga? Kwa sababu umeshindwa kujibu maswali rahisi tu ya somo la hisabati? Je umewahi kutimuliwa kazini zaidi ya mara moja? Hauko peke yako Sir Thomas Edison mgunduzi wa balbu yaani Taa za umeme hakuwa na akili kama unavyodhani alikuwa nazo, Yeye aliambiwa na mwalimu wake kuwa hana analoliweza na alipoteza matumaini, alisimama masomo akiwa na miaka 12, Mzazi wake akielezwa kuwa mtoto wake ni mbumbumbu wa mwisho hakuna mwalimu anaweza kumsaidia, Hata katika ugunduzi wake wa taa za balbu alikosea na kushindwa mara 1000, aliwahi kufukuzwa kazini mara kadhaa, lakini haya hayakuwahi kumkatisha tamaa hata siku moja badala yake alipuuzia kabisa kila aina ya kukoseolewa alikokutana nako hakuwahi kukata tamaa, Huyu ndiye aliyegundua taa za Umeme Duniani, unaonaje kama angekata tamaa Bado tungekuwa tunatumia mishumaa na vibatali duniani hata leo, “kila jaribio moja utakalolikosea linakupa hatua moja zaidi mbele” wewe pia mwisho wako bado usikubali kumuacha adui yako aone machozi yako, wala usikubali kushindwa kwa haraka namna hiyo je umejaribu mara 1000? Usikate tamaa!


Pichani mwansayansi Thomas Edison Mgunduzi wa taa za Umeme Duniani

2.      J.K. Rowling
Je unamjua mtu awaye yote ambaye ni tajiri kuliko Malikia wa uingereza? Kama hujui ni mwanamama JK. Rowling, mwandishi maarufu wa mtiririko wa Mashairi yaitwayo “Harry Potter”, Yeye ana utajiri unaozidi Pound Billion 1.  Hakuzaliwa akiwa anatumia hata kijiko cha fedha  mdomoni mwake, hakuwa bora kwa lolote katika maisha yake ya awali na kuna wakati aliishi katika nyumba za kupanga huko Edinburgh nyumba ambazo zilikuwa za watu wa hali ya chini  na zenye usumbufu mkubwa wa panya, alikuwa ni mama asiye na mume aliyepambana mpaka jasho lake la mwisho kupata mahitaji yake ya siku tunaweza kusema alikuwa na maisha mabaya ya dhiki mno, hakuwa na ajira yoyote, na hakustahili hata kulea mtoto wa Mchapaji “Typewriter” wa kazi yake ya ushairi wakati alipoanza kuchapa kitabu chake, na hakuweza kuwa hata na nafasi ya kuchapa kwa amani akiwa nyumbani kwake isipokuwa kwenda katika ofisi ya uchapaji tu, Ukiacha kuwa leo kuna vitabu vyake vingi tunavyosoma kitabu chake cha kwanza kilikataliwa mara 12, Lakini msimamo wake na kutokukata tamaa umemfanya sasa kuwa mwanamke aliyefanikiwa sana na kuwa mfano wa kuigwa.

Ndugu msomaji wangu inawezekana unapitia katika hali fulani ngumu mno na badala ya kusonga mbele unakaata tamaa; wana wa Israel walikata tamaa walilia walimlaumu Musa na Musa alimlilia Mungu lakini majibu ya Mungu ilikuwa waambie wana wa Israel wasonge mbele

Kutoka 14:15 “BWANA akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele.


Mungu atataka watu wasiokata tamaa watu watakao jaribu tena na tena kama Thomas Edison aliyegundua taa ya umeme alijaribu mara 1000 je wewe umejaribu mara ngapi, Mungu anakutaka usonge mbele, acha kuwalaumu viongozi wa kisiasa, acha kulaumu mfumo wa katiba na kudhani kuwa katiba mpya itakuwa suluhu ya matatizo yako,  acha kulaumu wazazi wako kuwa hawakukusomesha, acha kulaumu kuwa eti ulifukuzwa chuo , acha kulaumu kuwa ni kwa sababu hujaoa mke sahihi, au hujaolewa na mume sahihi, acha kulaumu kuwa ni kwa sababu ya talaka, acha kulaumu ni kwasabu etu ulidhulumiwa mirathi, acha visingizio, “Fumdi mbovu siku zote husingizia vifaa vyake “ hata kila kitu kikibadilishwa kama sisi hatutakuabali kufanya wajibu wetu hatuwezi kamwe kuona mambo mazuri ambayo Mungu ametuandalia katika dhiki na mateso tusiyoyajua, ni lazima tukubali kuzitumia changamoto tulizo nazo kama fursa, Hakuna ndege inaweza kupaa juu bila upinzani wa upepo, ili ndege ipae juu kwa urahisi inahitaji upinzani mkali sana wa upepo ndipo inapaa juu kabisa, Mungu anajua umuhimu wa changamoto katika maisha yetu na hivyo huziruhusu kwa utukufu wake

Mapito ya wana wa Israel haikuwa kitu kigeni kwa Mungu, Kwani yeye alikusudia moyo wa Farao uwe mgumu ili ajitwalie utukufu, sio hivyo tu aweze kukomesha kabisa Jeshi la Misri ili wasiwepo milele, ni wazi kuwa Misri na jeshi lote wangeendelea kuwepo wageweza kuwasumbua Israel hata kama wangefika kanaani kutokana na uwezo wao, hivyo Mungu alitaka ammalize adui kabisa ili Israel waende salama na waweze kuwa huru kwelikweli, Mungu alieleza mpango wake wazi kwa Musa katika


Kutoka 14:1-4 “BWANA akasema na Musa, akamwambia, Waambie wana wa Israeli, kwamba warudi na kupiga kambi yao mbele ya Pi-hahirothi, kati ya Migdoli na bahari, kukabili Baal-sefoni; mtapanga mbele yake karibu na bahari. Naye Farao atasema katika habari za wana wa Israeli, Wametatanishwa katika nchi, ile jangwa imewazuia wasitoke.  Nami nitaufanya uwe mgumu moyo wa Farao, naye atafuata nyuma yao; nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote; na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Basi wakafanya hivyo.”

Musa alikuwa anaufahamu mpango huu na kwa imani aliwatia moyo wana wa Israel kuwa wasiogope wasimame (Maana yake wasitikisike, maana yake wasonge mbele, maana yake wasiogope, maana yake wasione kuwa mwisho umefika, maana yake wasione kuwa Mungu hana mpango kamili dhidi yao) Mungu alikuwa amekusudia mema licha ya Israel kuwa na hofu Musa kama nabii alijua kuwa Mungu atafanya kitu alikuwa na imani kali sana alimuamini, yeye alishakuwa na uzoefu wa kutosha kuwa Mungu akisema lazima atatenda, aliamini kuwa Mungu hajawahi na hatawahi kuwmuangusha na alitabiri kuwa huo utakuwa mwisho wa majeshi ya Farao ingawa Musa hakuwa anajua kuwa Mungu atafanya kwa namna gani lakini imani yake ilikuwa juu sana kuwa kiko kitu Mungu atakifanya angalia maneno yake  katika


Kutoka 14:13-14 “Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya
.

Msomaji wangu nataka kukuhakikishia ya Kwamba Mungu yuleyule aliyeabudiwa na Musa na manabii, Mungu wa Israel ndiye Mungu wa Dunia nzima ndiye Mungu tunayemuabudu acha kuamini kelele za wapita njia acha kuangalia ukubwa wa mawimbi ya kipinzani au ukubwa wa majaribu yanayokukuta Mungu yule nimwabuduye ni mkuu kuliko tatizo lako, Nasimama leo kama nabii Musa wa katika kizazi hiki  kukutia moyo ya kwamba songa mbele acha kulia, Mtazame Bwana Yesu, Uko upenyo mkuu juu ya shida zako, uko ufumbuzi, liko jibu la changamoto yako, Mungu anao mpango kamili katika maisha yako endelea kupambana mpaka dakika ya mwisho muombe Mungu na msihi akufungulie milango na fanya kazi kwa bidii panga pamoja na Mungu naye atakutokea, Songa mbele lawamba na vilio havina majibu songa mbele. Mungu atakusaidia katika jina la Yesu!

Bwana Yesu mtumwa wako ninaomba kwaajili ya msomaji wangu, tafadhali usimuache katika hali aliyo nayo, kama ulivyowasaidia wana wa Israel chini ya Musa Mtumishi wako naomba umsaidie yeye naye ili kwaajili ya utukufu wako hali anayoipitia iweze kuwa historia ya maisha yake na umpeleke katika kiwango kingine, Mungu mwenye uwezo wa kuinua wanyonge kutoka jalalani na kuwaketisha na wakuu ufanye hivyo kwa kila mmoja wetu na watanzania kwa ujumla Katika jina la Yesu Kristo Amen!

Asante kwa sababu utaondoa na kuitowesha kabisa hali ya kukata tamaa inayomkabili kila moja kwa jinsi yake, Naikemea hali ya kukata tamaa ndani ya kila mmoja wetu katika jina la Yesu Kristo Amen!
USIKATE TAMAA WAKATI WA DHIKI!
Rev. Innocent Kamote Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima!..
0718990796

Maoni 2 :

Angetile Mwabdemange alisema ...

Aseee Mungu azidi kukutumia ujumbe mzito na wenye hekima ya kusonga mbele

Bila jina alisema ...

Mungu akubariki kwa masomo ukweli napiga hatua sana. Mungu akubariki.