Jumatatu, 25 Novemba 2019

Kizazi kisichomjua Mungu!

Waamuzi 2:10 “Tena watu wote wa kizazi hicho nao walikusanywa waende kwa baba zao; kikainuka kizazi kingine nyuma yao, ambacho hakikumjua Bwana, wala hawakuijua hiyo kazi ambayo alikuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli.” 

 
Wayahudi wa Madhehebu ya Orthodox huhakikisha kuwa watoto wao wanajua historia yao, dini yao mila zao na desturi zao, na kila mtoto huweza nkuelezea kuhusu familia yake hata vizazi kumi vilivyopita!

Utangulizi!


Katika moja ya tatizo kubwa ambalo jamii kubwa ya leo tumefeli duniani ni eneo la Malezi ya watoto, ni wazazi wachache sana ambao leo wamefanikiwa kuwaelekeza watoto wao na wakawa kama vile Mungu pamoja na wazazi walivyokusudia. Leo hii watu wengi sana wanalia na wameshindwa kuwadhibiti watoto, Namshukuru Mungu kuwa ameniita katika huduma ya kuwahudumia watoto, kwa miaka kadhaa sasa nimekuwa mkuu wa shule ya Sekondari Living Stone Boys’ Seminary, huku vilevile nikiwa Mchungaji wao, Najua na nimeona jinsi vijana wengi wanavyopoteza muelekeo hasa kwa sababu, ya kukosa malezi, wazazi wengi leo wako busy na utafutaji wa mali, wako busy na simu na ufuatiliaji wa Tamthilia na wameshindwa kujihusisha hata kidogo na maisha ya watoto, na wakati mwingine wamewasukumia shuleni, ili kwamba sisi walimu tuhangaike na watoto hawa ambao mimi huwaita kizazi cha ma-house girl Kizazi cha wadada wa kazi. Hili ni tatizo kubwa mno.


Tofauti ya kizazi wakati wa Joshua na kizazi wakati wa waamuzi.  


Kitabu cha waamuzi ni kitabu cha nyakati za mpito wa historia ya wana wa Israel baada ya uongozi wa Yoshua, tunakumbushwa katika maandiko na katika kitabu hiki kuwa watu walimtumikia Mungu wakati wote wa Yoshua, Na kuwa Mungu aliwabariki watu wake, 

Yoshua 24:31 “Nao Israeli wakamtumikia Bwana siku zote za Yoshua, na siku zote za hao wazee walioishi baada ya kufa kwake Yoshua, hao walioijua kazi yote ya Bwana, aliyowatendea Israeli.” 

Lakini kwenye kitabu hiki watu waliitumikia miungu na kuabudu sanamu, waliziacha kabisa njiia za Mungu na walisahahu kabisa matendo ya Mungu wala hawakujua matendo yake wala njia zake, Ndio maana biblia inasema kikainuka kizazi kingine kisichomjua Mungu! 

Waamuzi 2:10 “Tena watu wote wa kizazi hicho nao walikusanywa waende kwa baba zao; kikainuka kizazi kingine nyuma yao, ambacho hakikumjua Bwana, wala hawakuijua hiyo kazi ambayo alikuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli.” 


Kwanini tunaona tofauti kati ya kizazi kile na kizazi hiki? Hawa wote walikuwa wana wa Israel, wote walilellewa na kukulia katika historia ya matendo ya Mungu, kuna tofauti kadhaa


1.       Kizazi kile kilichomtumikia Mungu walikuwa chini ya uongozi wa Yoshua ambaye alimtumikia Mungu kwa moyo wake wote na waliona matendo makuu ya Mungu

a.       Waliona Israel wakivuka mahali pakavu wakati mto wa Yordani ukiwa umefurika
b.       Waliona kuta za Yeriko zikianguka kwa uwezo mkubwa wa Mungu na melekezo yake
c.       Waliona Mungu akiwapigania dhidi ya wafalme watano wa waamori na Mungu akiwashushia matofali ya moto
d.       Waliona Mungu akiongeza Muda kwa Joshua na majeshi yake kwa kusimamisha jua
e.       Maadui walitiishwa dhidi yao, kilikuwa ni kizazi kilichojua na kuyaona matendo ya Mungu
f.        Walipitia magumu mengi na kujitoa sana, kilikuwa ni kizazi cha mashujaa waliojipatia ardhi ya mkanaani.

2.      Kizazi kilichofuata kilikuwa ni kizazi kingine ambachoi hawakumjua Mungu wala matendo yake

a.       Walisikia tu Historias ya matendo ya zamani, waliona tu nguzo za kumbukumbu za baba zao kuwa walipita pakavu Jordani
b.       Waliona tu Magofu ya mji wa Yeriko na walisikia tu kuwa ukuita ulianguka
c.       Walijishughulisha tu kuendeleza nchi ambayo Mungu aliwapa baba zao na wakasahu mambo ya Mungu mwenyewe
d.       Walikaa katika miji ambayo wala hawakuihangaikia, walikula matunda ya mizabibu ambayo hawakuilima
e.       Walikuwa wakifurahia tu utajiri na mafanikio ambayo baba zao waliyapata kutoka kwa maadui kama nyara walizoteka
f.        Hawakujua habari za Mungu kuigawa bahari ya shamu, hawakujua habari za Mungu Kushuka katika mlima wa Sinai na kuwapa amri kumi na sheria na taratibu nyingine


Sababu kuu ya kizazi hiki kutokumjua Mungu.


Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu hapa sio tatizo, lakini kizazi kile kilichopita ndio kilikuwa tatizo, waoa hawakufanya yaliyo wajibu wao kwa Bwana, Mungu alikuwa amekusudia Israel wawafundishe watoto wao njia zake zote na kuwakumbusha matendo yake yote 


Kumbukumbu la Torati 6:1-14 “ Na hii ndiyo sheria, na amri, na hukumu, alizoziamuru Bwana, Mungu wenu, mfundishwe, mpate kuzitenda katika nchi ile mnayoivukia kuimiliki; upate kumcha Bwana, Mungu wako, kushika amri zake zote, na sheria zake, ninazokuamuru, wewe na mwanao, na mwana wa mwanao, siku zote za maisha yako; tena siku zako ziongezwe. Sikiza basi, Ee Israeli, ukaangalie kuzitenda; upate kufanikiwa, mpate kuongezeka sana, kama Bwana, Mungu wa baba zako, alivyokuahidi, katika nchi ijaayo maziwa na asali. Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako. Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako. Tena itakuwa atakapokwisha Bwana, Mungu wako, kukuleta katika nchi aliyowaapia babu zako, Ibrahimu na Isaka na Yakobo, ya kuwa atakupa; miji mikubwa mizuri usiyoijenga wewe,  na nyumba zimejaa vitu vyema vyote usizojaza wewe, na visima vimefukuliwa usivyofukua wewe, mashamba ya mizabibu na mizeituni usiyoipanda wewe, nawe utakula na kushiba; ndipo ujitunze, usije ukamsahau Bwana aliyekutoa nchi ya Misri, nyumba ya utumwa. Mche Bwana, Mungu wako; ndiye utakayemtumikia, na kuapa kwa jina lake. Msifuate miungu mingine katika miungu ya mataifa wawazungukao;”


Musa ni kama alikuwa ana wa zoom wana wa Israel aliwaonya mapema kwa neno la Mungu kuwa ni lazima wawaelimishe watoto wao na kuhakikisha kuwa wanampenda Mungu, ilikuwa ni kwa namna mbalimbali Mungu alitaka maswala haya ya msingi yakumbukwe, kizazi na kizazi walipaswa kufundishana kwa bidii matendo yote na maneno yote ya Mungu na kuwa kila kizazi wakumbuke, kile ambacho Mungu alikuwa amekikusudia wampende na kumtumikia. Mungu alirejea jambo kama hili kwa Yoshua kwa sababu Moyonimwake Mungu alikuwa anataka kizazi kipya kiyajue matendo yake ili wamuabudu


Yoshua 4:1-8 “Ikawa, hapo hilo taifa zima lilipokuwa limekwisha vuka Yordani, ndipo Bwana akanena na Yoshua, akamwambia, Haya, twaeni watu waume kumi na wawili katika hao watu, kila kabila mtu mmoja, kisha uwaamrishe, kusema, Twaeni mawe kumi na mawili, hapo katikati ya Yordani, mahali hapo miguu ya hao makuhani iliposimama imara, mwende nayo mawe hayo, mkayaweke nchi kambini, hapo mtakapolala usiku huu. Basi Yoshua akawaita hao watu kumi na wawili, aliokuwa amewaweka tayari tangu hapo, katika wana wa Israeli, kila kabila mtu mmoja; naye Yoshua akawaambia, Haya, piteni ninyi mtangulie mbele ya sanduku la Bwana, Mungu wenu, mwende pale katikati ya Yordani, mkatwae kila mtu wenu jiwe moja begani mwake, kwa kadiri ya hesabu ya kabila za wana wa Israeli; ili kwamba jambo hili liwe ishara kati yenu, hapo watoto wenu watakapowauliza ninyi katika siku zijazo, wakisema, Ni nini maana yake mawe haya? Ndipo mtakapowaambia, Ni kwa sababu maji ya Yordani yalitindika mbele ya sanduku la agano la Bwana; hapo lilipovuka Yordani, hayo maji ya Yordani yalitindika; na mawe haya yatakuwa ni ukumbusho kwa wana wa Israeli milele. Basi wana wa Israeli walifanya vile vile kama Yoshua alivyowaamuru, nao wakatwaa mawe kumi na mawili pale katikati ya Yordani, kama Bwana alivyomwambia Yoshua, sawasawa na hesabu ya kabila za wana wa Israeli; wakayachukua wakavuka nayo hata mahali pale walipolala, nao wakayaweka nchi kuko huko.” 


Unaweza kuona mkakati wa Mungu ni kuwa kila kizazi kiyajue matendo yake, watu wazima wawafundishe vija nana watoto kumjua Mungu, kuyajua matendo yake ili kwamba wampende Mungu na kumtumikia na kuacha kuabudu miungu, tatizo kubwa la kuibuka kwa kizazi kisichomjua Mungu ni kizazi kile kilichokuwa kikifurahia baraka za Mungu na kusahau kabisa wajibu wa kuwafunza watoto, leo hii dunia imejaa mafunzo ya ajabu mno, watu wanaohusika na ushoga wameandaa vijitabu vya kuwafundisha watoto ushoga mapema ili wauone kuwa ni kitu cha kawaida katika kizazi hiki, kanisa limepuuza maswala mazima ya kuwafundisha vijana na watoto, dini zimejikita katika maswala ya mafanikio utafutaji wa fedha na kutokushughulika na watoto ili kumtegenezea Yesu kanisa la baadaye matokeo kama haya na makosa kama haya ni sawa na yale waliyoyafanya wayahudi wakati wa waamuzi na matokeo yake wana wa Israel walijifunza tabia mbaya na kuabudu miungu na kumuacha Mungu aliye hai huku wakifanya maovu  angalia 

Waamuzi 2:11-13 “Wana wa Israeli walifanya yaliyokuwa ni maovu mbele za macho ya Bwana, nao wakawatumikia Mabaali. Wakamwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha Bwana, akaghadhibika. Wakamwacha Bwana, wakamtumikia Baali na Maashtorethi.” 


Leo hii kanisa linalia na manabii wa uongo, vuingozi wa kiroho wahuni, wasio na uadilifu, kuuzwa kwa mafuta, maji, sabuni, unga, chumvi, udongo na soda bangili za upako na kadhalika pamoja na kuweko kwa mafundisho ya ajabu ajabu tatizo kubwa sio wao tatizo kubwa ni kanisa lenyewe liliweka msingi gani katika kuwaandaa viongozi wa kiroho walio waadilifu? Unapolia na manabii wa uongo kumbuka kulina na walimju wa uongo waliowalea, kanisa lilikuwa wapi, wazazi walikuwa wapi jamii ilikuwa wapi wakati watoto wetu wanaharibika ? nani anawajibika? Ni sisi wenyewe Hatukujali mafundisho. Leo hii watu wametoa kipaumbele katika swala zima la kutafuta mafanikio ya kimwili na kusahau kujenga msingi wa kuifunza jamii juu ya swala zima la kumtafuta Mungu na kumpenda na kumpa kipaumbele na kumuabudu yeye na kuwa na hofu yake kamwe tusisahahu kuwa hukumu ya Mungu ipo  


2Petro 2:9-10 “basi, Bwana ajua kuwaokoa watauwa na majaribu, na kuwaweka wasio haki katika hali ya adhabu hata siku ya hukumu; na hasa wale waufuatao mwili katika tamaa ya mambo machafu. na kudharau mamlakaEndapo kanisa na wazazi hawatajali maswala mazima kuhusu ya kukilela kizazi kijacho katika njia za Mungu na uadilifu wake basi tujue kuwa hatutaweza kuiepuka hukumu ya Mungu, Zamani tulikuwa tunasema mauti imo sufuriani lakini sasa iko mdomoni ni lazima tuamke na kuwasaidia jamii yetu kujiandaa kumcha Mungu.

 
Jinsi ya kufanya ili kizazi kijacho kimjue Mungu


Wana wa Israel walikuwa na changamoto ambayo tunaweza kuigawa
·         Kizazi cha kwanza kioona matendo ya Mungu
·         Kizazi cha pili kilisikia matendo ya Mungu na
·         Kizazi chaa tatu hata kusikia hawakusikia 

1.       Tuwafundishe  kujenga na kuimarisha uhusiano na Mungu  Mungu alimchagua Ibrahimu kuwa rafiki yake kwa sababu alijua kuwa Ibrahimu atakuwa mwalimu mwema Mwanzo 18:17-19 “BWANA akanena, Je! Nimfiche Ibrahimu jambo nilifanyalo, akiwa Ibrahimu atakuwa taifa kuu, hodari, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa? Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya BWANA, wafanye haki na hukumu, ili kwamba BWANA naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake.” 

    Kanisa, mzazi na walimu wanaotaka kuwa rafiki wa Mungu ni wale watakaokuwa wanajali kuwafundisha watoto na kizazi kijacho njia ya Mungu. Lazima kizazi kimoja kiwaeleze kizazi kijacho na kizazi kijacho kielezee wale wanaokuja  

      Yoel 1:2-3 “Sikieni haya, enyi wazee; Sikilizeni, enyi wenyeji wote wa nchi. Je! Mambo haya yamekuwako katika siku zenu, Au katika siku za baba zenu? Waarifuni watoto wenu habari yake, Watoto wenu wakawaambie watoto wao, Na watoto wao wakakiambie kizazi kingine.”


2.       Hakikisha kuwa unawaelimisha watoto kwa ghama yoyote Mithali 4:13 “Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako” kkatika kuhakikisha kuwa vijana wanapata Elimu na uadilifu ni lazima tukumbuke kuwa kuna walimu wakuu wanne, 1 Wazazi hawa ndio walimu wa kwanza, wao ndio msingi wa maisha ya kila kitu unapoona mwanao unajiona wewe waoni picha ya nyumbani kwao, 2. Shuleni, unampeleka katika shule ya aina gani, walimu wake wakoje ja wanamcha Mungu. Hakikisha kuwa watoto wanaosma kama huna ada fanya kazi na muombe Mungu aliyekupa hao watoto kwamba afungue mlango wa ada ili waende shule wasome, je ni nani anataka kuzaa house girl nani anataka kuzaa kuli, nani anataka kuza machinga, nani anataka kuzaa wazurulazi, wauza mayai tuwasomeshe tuwapatie elimu  3 Ibadani mwanao ataabudu wapi huyu ndio mwalimu wa ngazi ya juu kabisa hivyo lazima tuchague mahali sahihi kwa vija na wetu kujifunza mambo ya Mungu pia, 4 Shetani nimwalimu mbaya mno atawanyoosha wote ambao hawakuweka msingi unaoeleweka kwa vijana, kama kuna kitu tunapungukiwa Watanzania ni kutokuwaelimisha watoto wetu, Rafiki yangu mmoja alisema Japan ni inchi Tajiri na iliyoendelea sana kwa sababu waliwekeza katika elimu lakini hawana rasilimali nyingi kama tulionazo, na Tanzania ni inchi yenye rasilimali nyingi sana lakini tumepigwa na ukwasi kwa muda kwa sababu hatukuwa na maarifa ya kutosha, watoto wetu wanazaliwa na vipawa na karama na majaliwa makubwa sana lakini tunaweza kuyadidimiza kwa sababu tu tumeshindwa kuyachohcea kwa kutokuwapa maarifa yanayohitajika, tusiwapeleke watoto mbali na Mungu Yesu anawahitaji waje kwake Mathayo 19:14 “Lakini Yesu akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao.”


3.       Usimnyime mtoto mapigo. 


Maandiko matakatifu yanataka kwanza tuutangulize upendo tuwapende vijana na watoto wetu kwa viwango ambavyo wataelewa kuwa tunawapenda, lakini tusiwadekeze, lazima watutii na watuheshimu, Biblia imesema lazima tufanye hayo, Padre mmoja aliyeitwa Don Bosco alisema atakwenda mtaani atakusanya vija na walioshindikana na atawakusanya na kuwapa elimu bila kuwachapa kiboko na watamtii, Padre huyu kutokana na mafanikio yake makubwa shule nyingi sana zimeanzishwa duniani na zinaitwa kwa jina lake Don Bosco kukumbuka uwezo wake mkubwa sana katika maswala ya nidhamu, lakini hata hivyo kama watoto hawasikii biblia imesema wapigwe viboko, sheria inayokataza watoto kuchapwa ni ya kishetani, kila dini inasema watoto waadhibiwe kuna sheikh hapa? Mtume Muhamad (SAW) alichapwa, alikuwa hajui kusoma na kuandika malaika jibril alipomtokea katika pango alimlazimisha asome na akariri kwa jila la mola wake “Iqraa bism rabik laz kalaaq” alilazimishwa mpaka aliugua aliumwa! Baada ya kulazimishwa kusoma, wewe lunasema viboko ni haramu? Mungu anasema  wacharazwe 

Mithali 13:24 “Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe; Bali yeye ampendaye humrudi mapema.”  Kila tabia mbaya tutakayoiona kwa watoto tuiondoe mapema kwa kuwacharaza, kuna matumaini kama tutawachapa kwa upendo bila kuzidi kiasi na kuwaumiza au tukiwa na hasira 

Mithali 19:18 “Mrudi mwanao, kwa maana liko tumaini; Wala usiikaze nafsi yako kwa kuangamia kwake.” Maandiko yanasema kuna matumaini tukiwadhibu kuna matumaini tukiwarudi, tena biblia inasema kwa kuwaadhibu tunaodoa ujinga ndani ya akili zao na mioyo yao na tunawaopa maarifa 

Mithali 22:15 “Ujinga umefungwa ndani ya moyo wa mtoto; Lakini fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali.” Bilia inaonyesha kuwa fimbo itafukuzilia mbali ujinga kwa hiyo tusiwanyime adhabu tusiwanyime mapigo  

Mithali 23:13-14. “Usimnyime mtoto wako mapigo; Maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa. Utampiga kwa fimbo, Na kumwokoa nafsi yake na Kuzimu.Biblia inasema hatakufa ukimchapa bali utaiokoa nafsi yake na kuzimu, ni fimbo ndio itaweka nidhamu, ni fimbo ndiyo itakayompa hekima na akili 

Mithali 29:15-17 “Fimbo na maonyo hutia hekima; Bali mwana aliyeachiliwa humwaibisha mamaye. Waovu wakiongezeka, maasi huongezeka; Bali wenye haki watayatazama maanguko yao. Mrudi mwanao naye atakustarehesha; Naam, atakufurahisha nafsi yako 

mtoto wako akiisha kujua nini mzazi anakitaka mapema sana atayashika mausia yako na utakuwa ni muongozo mkubwa utakaomsaidia kijana wako, atajua lipi jema na lipi baya, lazima tuwe na muda na watoto wetu na kuwaelekeza, na kuwafundisha utii, walekeze kuamkia watu wazima, walekeze kujilinda na maadui, waelekeze dalili za kujua mtu mwema na mtu mbaya, waelekeze kujisomea wewe mwenyewe ukiwa kielelezo cha hayo, mara nyingi watu hulaumu viongozi wa dini kuwa hawa jamaa wanahubiri tu lakini hawatendi sawa na kuhubiri kwao, haya yameanzia majumbani mzazi anamkataza mtoto wake kunywa pombe yeye mwenyewe anakunywa, unamkataza asivae mavazi ya kikahaba wewe mwenyewe unavaa, Lazima tujikite katika kuwalea waoto wetu kwa hali na mali, wasipotusikiliza baada ya hayo tutakuwa na uwezo wa kutoa Hesabu kwa Mungu, kuwa sisi tulijitahidi kufanya kila tuliloliweza kwaajili yao, lakini sehemu nyingine nilikuachia wewe Mungu na sitawajibika kama baba au mama aliyeshindwa kumpatia mtoto kile alichopaswa!


Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote
0718990796

Maoni 2 :

Unknown alisema ...

Kwenye swala la kanisa.je ni kanisa lenye misingi gani lina roho wa mungu au ni kweli

IJM alisema ...

Ipo Vizuri