Jumapili, 2 Februari 2020

Mtu wa kumtendea Mema!



2Samuel 9:1-8 “Kisha Daudi akasema, Je! Amesalia mtu mmoja katika nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema kwa ajili ya Yonathani? Palikuwa na mtumishi mmoja wa nyumba ya Sauli, jina lake Siba, basi wakamwita aende kwa Daudi; na mfalme akamwuliza, Wewe ndiwe Siba? Naye akasema Mimi, mtumwa wako ndiye. Mfalme akasema, Je! Hakuna hata sasa mtu ye yote wa nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema ya Mungu? Siba akamwambia mfalme, Yonathani anaye mwana hata sasa, aliye na kilema cha mguu. Mfalme akamwambia, Yuko wapi? Siba akamwambia mfalme, Tazama, yumo katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari. Basi mfalme Daudi akatuma watu, akamwondoa katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari. Basi Mefiboshethi, mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli akaenda kwa Daudi, akaanguka kifudifudi, akasujudu. Daudi akasema, Mefiboshethi! Naye akaitika, Mimi hapa, mtumwa wako! Daudi akamwambia, Usiogope, maana bila shaka nitakutendea mema; kwa ajili ya Yonathani, baba yako, nami nitakurudishia mashamba yote ya Sauli, baba yako; nawe utakula chakula mezani pangu daima. Akasujudu, akasema, Mimi mtumwa wako ni nini, hata ukamwangalia mbwa mfu kama mimi?


Utangulizi:

Moja ya watu muhimu sana katika Biblia ambao tunaweza kujifunza mambo mengi sana kutoka kwao ni Pamoja na Mfalme Daudi mwana wa Yese, Huyu ni mtu mwenye moyo wa ajabu na roho nzuri sana alimpenda Mungu na aliwapenda wanadamu wengine, Maandiko yanaonyesha wazi kuwa Mungu alipendezwa naye angalia katika Matendo 13:22 “Na alipokwisha kumwondoa huyo, akamwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote.Mungu alipendezwa naye kwa sababu aliyatenda mapenzi ya Mungu yote.

Licha ya kuwa na madhaifu kama Mwanadamu Daudi alikuwa mtu mwema sana uwezo wake wa kutenda mema uliweza kuwashangaza wengi. Alikuwa ni mtu asiyelipiza kisasi hata kwa wale waliomfanyia mabaya, lakini vilevile alikuwa ni mtu aliyekumbuka na kushika ahadi/agano kama alivyopatana na Yonathan mwana wa Sauli, leo tutachukua Muda kutafakari kwa kina na mapana na marefu moja ya matukio ya kushangaza sana yaliyofanywa na mfalme huyu wa ajabu.

Mtu wa Kumtendea mema.!

Katika fungu la maandiko ya msingi utaweza kuona moyo wa Daudi, akiulizia swala la muhimu sana lenye kuonyesha kuwa alikuwa na moyo wa ajabu sana, Yeye baada ya kuziona fadhili za Mungu katika maisha yake naye alitaka kuonyesha fadhili zake kwa mtu anayeweza kumuhurumia 2Samuel 9:1 Kisha Daudi akasema, Je! Amesalia mtu mmoja katika nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema kwa ajili ya Yonathani?


a.       Je amesalia mtu mmoja katika nyumba ya Sauli? Daudi aliwahi kuuliza swali kama hili katika 1Samuel 7 wakati anawaza kufanya Jambo kwaajili ya Mungu, na anawaza kumjengea Mungu Hekalu, Sasa Daudi anauliza swali lingine Muhimu mtu wa kumtendea mema?

Swali la Daudi linaonyesha upendo mkubwa sana na wa ajabu mno, Ni wazi kuwa Sauli alitengeneza uadui mkubwa sana, na vita ya siku nyingi na Daudi,  2Samuel 3:1Basi kulikuwa na vita siku nyingi kati ya nyumba ya Sauli na nyumba ya Daudi; Daudi akaendelea akasitawi lakini Nyumba ya Sauli ikaendelea kudhoofika”Na ni wazi kuwa kwa mujibu wa tamaduni ya sheria za kifalme utawala mpya wa kifalme unapotawala unatakiwa kuwauwa na kuwateketeza kabisa ukoo wa mtawala aliyepita au awaye yote mwenye uhusiano na utawala uliopita ili utawala mpya uweze kuwa salama, Lakini katika habari hii tunamuona Daudi akifanya jambo la tofauti kabisa kinyume na kanuni za kawaida za kujilipizia kisasi dhidi ya uadui wa Sauli, lakini vile vile kanuni ya kujihami na kujihakikishia anatawala vema na kwa amani ilikuwa ni lazima kuimaliza kabisa Familia ya adui yake, lakini katika namna ya kushangaza mno Daudi yeye anatafuta mtu wa familia ya adui zake na kutafuta mtu wa kuwatendea mema!.

b.      Nipate kumtendea mema kwaajili ya Jonathan: Aidha Daudi pia alifanya hivi kwasababu alikumbuka agano alilolifanya na Jonathan pamoja na uhusiano mwema aliokuwa nao 1Samuel 20:14-15 “Nawe utanionyesha fadhili za Bwana, ili nisife, si wakati huu tu maadamu mimi ni hai; lakini pamoja na hayo, hata jamaa yangu pia hutawaondolea kabisa fadhili zako; la, hata wakati ule Bwana atakapokuwa amewaondoa kabisa adui za Daudi wote pia katika uso wa nchi.” Kwa hiyo wema wa Daudi haukuwa katika hisia zake pekee lakini pia ulikuwa kwaajili ya kukumbuka agano lake alilolifanya na Jonathan, Daudi alitaka kuwa mwaminifu kulitimiza agano lile kwa rafiki yake aliyempenda na kumuokoa na kifo kutoka kwa baba yake yaani Jonathan.


Kutenda wema katika mazingira magumu:

2Samuel 9: 2-4 “Palikuwa na mtumishi mmoja wa nyumba ya Sauli, jina lake Siba, basi wakamwita aende kwa Daudi; na mfalme akamwuliza, Wewe ndiwe Siba? Naye akasema Mimi, mtumwa wako ndiye. Mfalme akasema, Je! Hakuna hata sasa mtu ye yote wa nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema ya Mungu? Siba akamwambia mfalme, Yonathani anaye mwana hata sasa, aliye na kilema cha mguu. Mfalme akamwambia, Yuko wapi? Siba akamwambia mfalme, Tazama, yumo katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari.

a.       Siba aliyekuwa mtumwa wa Sauli alikuwa ndiye mtu pekee aliyekuwa anajua habari za uzao wa Sauli uliosalia na ndiye aliyekuwa anajua wapi walipo, Hii inamaanisha kuwa kijana pekee wa Uzao wa sauli aliyekuwa amebakia alikuwa amejificha kijana huyu alijulikana kama Mefibosheth


b.      Daudi alikua anamuhitaji mtu huyu ili kutunza agano alilofanya na Yonathan, ulikuwa sasa ni wakati wa kuonyesha wema wa Mungu, kwa Jonathan kutokana na agano lile kuwa Mungu atakapokuwa amemfadhili Daudi asiache kumkumbuka Yonathan na kumwacha hai juu ya uso wa nchi kwamba ni yeye au uzao wake huu ndio ulikuwa msingi mkubwa wa Daudi katika maamuzi yake alitaka mtu wa ukoo wa Sauli amuonyeshe wema wa Mungu kama jinsi Mungu alivyomfadhili yeye.


c.       Daudli alitaarifiwa na Siba kuwa yuko mwana wa Yonathan ambaye pia ni mlemavu wa miguu, Mwana huyu wa Yonathan alipata ulemavu wakati wa utoto, siku ya kifo cha baba yake na babu yake walipouawa vitani alipokuwa akikimbizwa mafichoni alipokuwa mdogo aliangushwa kwa bahati mbaya na kuwa mlemavu 2Samuel 4:4 “Naye Yonathani, mwana wa Sauli alikuwa na mwana aliyekuwa na kilema cha miguu. Alikuwa amepata miaka mitano, habari za Sauli na Yonathani zilipofika Yezreeli, na yaya wake akamchukua akakimbia ikawa, alipokimbia kwa haraka, huyo mtoto akaanguka, akawa kilema. Na jina lake aliitwa Mefiboshethi. Ni wazi kuwa Yaya wake alimchukua kijana ili kuokoa maisha yake kwa kukimbia baada ya kusikia kuwa Sauli na Yonathan wameuawa vitani, aliogopa na alikuwa anafahamu kuwa utawala mpya kwa vyovyote vile  wangewaua warithi wote wa ufalme wa Sauli kama zilivyo mila na Desturi.


d.      Mwana wa Yonathan kwa vyovyote vile Methibosheth ndiye aliyekuwa anatakiwa kuwa Mrithi wa kiti cha ufalme, Kijana wa Kwanza wa Sauli alikuwa ni Yonathan na  sasa Sauli na Yonathan walikuwa wameuawa vitani hivyo Methibosheth kama mzaliwa wa kwanza wa Yonathan ufalme ulikuwa una muhusu, Na Daudi alipaswa kuhakikisha kuwa anamuua kwanza Mefibosheth ili utawala wake uweze kuwa imara kwa mujibu wa mila na desturi za kifalme kwa sababu tishio kubwa la ufalme wa Daudi angekuwa ni Methibosheth

Katika kitabu cha 2Samuel 16:5-8 “Basi mfalme Daudi alipofika Bahurimu, tazama, kulitoka huko mtu wa jamaa ya nyumba ya Sauli, jina lake akiitwa Shimei, mwana wa Gera; alitoka, akalaani alipokuwa akienda. Tena akamtupia Daudi mawe, na watumishi wote wa mfalme Daudi; na watu wote na mashujaa wote walikuwako mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto. Na Shimei alipolaani, alisema hivi, Nenda zako! Nenda zako! Ewe mtu wa damu! Ewe mtu usiyefaa! Bwana amerudisha juu yako damu yote ya nyumba ya Sauli ambaye umetawala badala yake; naye Bwana ametia ufalme katika mkono wa Absalomu mwanao; kisha, angalia, wewe umetwaliwa katika uovu wako mwenyewe, kwa sababu umekuwa mtu wa damu.Maandiko yanaonyesha kuwa jamaa wa Sauli bado walikuwa wanapingana na Daudi na kuna uwezekano mkubwa watu wa aina hii walikuwa wengi katika Israel ambao hawakukubaliana na jambo hili la Daudi kutawala kwa sababu waliona kama ilikuwa ni halali na haki wana wa Sauli kutawala badala yake, mmojawapo ni huyu aliyeitwa Shimei. Aidha Ishbosheth ambaye alikuwa ni Mjomba wa Mefibosheth alianzaisha vita kali sana na Daudi kwaajili ya Ufalme katika Israel, kwa hiyo ilikuwa wazi kuwa Mefibosheth angeweza kufanya hivyo kwaajili ya ufalme.

Hali ya Methibosheth

Daudia liambiwa kuwa yuko katika Nyumba ya Makiri mwana wa Amiel, Hii inaonyesha wazi kuwa Mathibosheth alikuwa katika hali duni na mbaya na ya chini sana kimaisha, hakuwa hata na nyumba yake mwenyewe, alihifadhiwa katika nyumba ya mtu mwingine, Makiri mwana wa Amiel hata hivyo baadaye inaonekana alikuwa anampenda mfalme Daudi, na alikuwa muwazi na mkweli, Hata mwana wa Daudi Absalomu alipomuasi baba yake Makiri alikuwa upande wa kumsaidia Daudi hata hatari kubwa zilipomkabili ona 2Samuel 17:27-29 “Ikawa, Daudi alipofika Mahanaimu, Shobi, mwana wa Nahashi wa Raba, wa wana wa Amoni, na Makiri, mwana wa Amieli wa Lo-debari, na Barzilai, Mgileadi wa Rogelimu, wakaleta magodoro, na mabakuli, na vyungu, na ngano, na shayiri, na unga, na bisi, na kunde, na dengu, na asali, na siagi, na kondoo, na samli ya ng'ombe, wapate kula Daudi na watu waliokuwa pamoja naye; kwani walisema, Watu hao waona njaa, tena wamechoka, nao wana kiu huku nyikani.”

Maandiko yanaonyesha kuwa kijana huyu alikuwa mnyenyekevu mno aliweza kuonyesha unyenyekevu mkubwa sana kwa Mfalme Daudi ona mstari 5-6 “Basi mfalme Daudi akatuma watu, akamwondoa katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari. Basi Mefiboshethi, mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli akaenda kwa Daudi, akaanguka kifudifudi, akasujudu. Daudi akasema, Mefiboshethi! Naye akaitika, Mimi hapa, mtumwa wako!

a.       Mfalme Daudi alituma watu wakapate kumleta Mephibosheth nyumbani kwake kwa hakika tukio hili lilikuwa ni lenye kuogopesha sana kwake wakati watumishi wa Daudi wanagonga Hodi nyumbani kwa Makiri na kudai kuwa anaitwa kwa mfalme katika akili zake ilikuwa inaeleweka kabisa kuwa anakwenda kukutana na kifo kwa sababu ndivyo ilivyokuwa desturi ya kifalme kwaajili ya kujihami katika mamlaka zao,  Kitendo cha watumishi wa Daudi kwenda kwa Makiri na kumuhitaji Mephibosheth ilikuwa ni ishara wazi kuwa hawezi kujificha tena, na labda kama angejisikikia salama ni labda kwa kufikiri tu kuwa labda mfalme mpya hajui habari zake.

b.      Alijiinamisha na kumsujudia Mfalme: kwa mujibu wa tamaduni ni wazi kuwa mpaka wakati huu lazima kijana huyu alikuwa amejaa hofu ya hali ya juu na kwa hakika alikuwa na hofu kubwa isiyo na kifani yeye alikuwa amejificha tangu utoto wake na hajawahi kuwa na uhusiano wowote na Mfalme Daudi hivyo hakuwa na uhakika wa uzima wake ila alikiona kifo tu cha kihiyari bila ubishi.


c.       Mstari 7-8 Daudi alihakikisha anamuondolea Hofu Mephibosheth “Daudi akamwambia, Usiogope, maana bila shaka nitakutendea mema; kwa ajili ya Yonathani, baba yako, nami nitakurudishia mashamba yote ya Sauli, baba yako; nawe utakula chakula mezani pangu daima. Akasujudu, akasema, Mimi mtumwa wako ni nini, hata ukamwangalia mbwa mfu kama mimi? 
          

i.                     Usiogope: Daudi alimwambia Mephibosheth japo neno hili lingekuwa halina maana kama Daudi asingelisema kwa nini anafanya haya au anamwambia usiogope alimuhakikishia kumrejeshea mali za babu yake na kukaa pamoja naye katika kiti cha enzi cha utawala wake.

ii.                   Bila shaka nitakutendea mema kwaajili ya Yonathan baba yako, Daudi alimuhakikishia Mephibosheth kuwa alikuwa na agano na Yonathan baba yake 1Samuel 20 kwamba atamuonyesha fadhili za Mungu hata kwa uzao wake na hivyo Daudi pia alikuwa akitimiza agano hata kama Yonathan alikuwa amekufa.

iii.                  Nitakurudishia Mashamba yote ya Sauli: Daudi pia alimwambia Mephibosheth kwamba atapokea kila kilichokuwa mali yake, Inawezekana Mephoibosheth aliyajua haya  kuwa ni mali yake lakini alikuwa amejificha, alikuwa anaogopa, alikuwa anaishi maisha ya umasikini mkubwa uliokithiri, alijua ya kuwa amekwisha kupoteza kila kitu na kuwa hawezi kufanya lolote kwa uwazi, hangeweza kufanya kitu kuhusu Mashamba yake  kwa sababu kujitokeza kwake kungekuwa ni kuhatarisha maisha yake na kujiweka wazi kwa Daudi, Lakini Daudi kama mfalme mwema anakwenda kinyume na fikra za kitamaduni za wafalme wengine yeye anamtambua na kumfanyia wema mtu ambaye angekuwa hatari katika ufalme wake.

iv.                 Pia utakula mezani Pangu daima: hii nayo ilikuwa ni zaidia ya kawaida Mephibosheth anapewa heshima ya kuwa karibu sana na Mfalme anakaa mezani kwa mfalme hii ni heshima kubwa sana nikama anatawala pamoja naye ahadi kama hii Yesu aliwaahidi wale wamuaminio, Yesu aliwaambia wanafunzi wake kuwa watakula na kunywa Mezani pake huko mbinguni Luka 22:30mpate kula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu; na kuketi katika viti vya enzi, huku mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli.”

Muitikio wa Mephibosheth

Mtumwa wako ni nani hata ukamwangalia mbwa mfu kama mimi?:

Ni ukweli ulio wazi kuwa kijana huyu mjukuu wa Sauli hakujifikiri hata kidogo kuwa anastahili kitu, ni wazi kuwa hakustahili ukarimu mkubwa namna ile, Yeye alijifananisha na mbwa mfu tu!, yaani mbwa mfu ni kiumbe asiye na umuhimu wala thamani yoyote, kama vile mwanadamu anapoona njiani mbwa aliyekufa, huwa hakuna anayeonyesha kujali zaidi ya kupita kando na kutema mate, Yeye alikuwa amejificha siku zote za maisha yake, akiogopa na huku akiwa amezungukwa na umasikini mkubwa sana akijua wazi kuwa anastahili kuuawa iweje leo afikiriwe kwa kiwango kikubwa namna ile?

Maelekezo ya Mfalme Daudi kwa Siba 9-12

Ndipo mfalme akamwita Siba, mtumwa wa Sauli, akamwambia, Mali yote yaliyokuwa ya Sauli na ya nyumba yake nimempa mwana wa bwana wako. Nawe utamlimia nchi hiyo, wewe, na wanao, na watumwa wako; nawe utamletea mwana wa bwana wako matunda yake, apate chakula ale; lakini Mefiboshethi, mwana wa bwana wako, atakula chakula mezani pangu sikuzote. Basi huyo Siba alikuwa na wana kumi na watano na watumwa ishirini. Ndipo Siba akamwambia mfalme, Mimi, mtumwa wako, nitatenda hayo yote kama bwana wangu, mfalme, alivyoniamuru. Na kwa habari za Mefiboshethi, mfalme alisema, Atakula mezani pangu, kama mmojawapo wa wana wa mfalme. Huyo Mefiboshethi alikuwa na mwana mdogo, jina lake akiitwa Mika. Na watu wote waliokaa nyumbani mwa Siba walikuwa watumwa wa Mefiboshethi.

a.       Wewe na wanao na watumwa wako mtafanya kazi kwaajili yake, Ardhi ambayo Daudi alimpa Mephbosheth aliamuriwa siba na familia yake wamlimie na kuitunza kwaajili ya chakula cha Familia ya Mephibosheth kwa sababu yeye sasa anakula katika meza ya mfalme

b.      Yeye atakula mezani kwangu kama moja ya wana wa Mfalme, Mephibosheth alikuwa na furaha kujua kwamba Daudi hakuwa na mpango wa kumuua na alishangaa kupewa zawadi na kufanyiwa mambo makubwa ya kushangaza.


c.       Daudi aliitimiza ahadi yake kwa Mephibosheth na alikaa Yerusalem japo alikuwa mlemavu wa miguu, Hakuweza kujificha tena wala kumuogopa mfalme, familia ya Sauli sasa waliishi wazi miongoni mwa watu wa Mungu, alikula siku zote katika meza ya mfalme, hakuwa masikini tena maisha yake yalikuwa mazuri, alitawala pamoja na Daudi lakini alikuwa mlemavu wa miguu

Neema ya Daudi na wema wake kwa Methibosheth ni unabii wa Neema ya Mungu kwetu, sisi ndio Methibosheth wa leo

·         Sisi ni masikini, tumejificha, tuna hofu, ni vilema na tunamuogopa Mungu tumejificha mbali na uso wake kabla Yesu hajatutafuta, tumejificha kwa sababu ni wenye dhambi tunastahili kifo, hatuko katika ufalme wa Mungu
·         Tumetengwa na Mungu wetu kwa sababu ya makosa na dhambi za wazazi wetu, tangu kuzaliwa
·         Tumejificha mbele za Mungu kwa sababu hatuujui wema wake wala hatuujui upendo wake kwetu
·         Mungu anatufikiri sisi kabla ya sisi kumfikiri yeye
·         Wema wa Mungu umetufikia kwa sababu ya wema wa mtu mwingine Ni kwaajili ya Yesu Mungu ametupa neema Kama ilivyokuwa kwaajili ya Yonathan Mefibisheth alipata neema
·         Wema wa Mungu umekuja kwetu kwa sababu ya agano alilolifanya ba baba zetu
·         Tunapaswa kuupokea wema wa Mungu kwa unyenyekevu mkubwa!
·         Mungu ameturudishia kila kilichopotea, na kutupa zaidi ya kile tulichopoteza
·         Mungu amerudisha zaidi ya tulivyotegemea
·         Mungu ametukaribisha mezani pake sasa tuko karibu naye na tutakuwa na ushirika wa kudumu na yeye
·         Tunapewa watumwa wa kututumikia

·         Heshima aliyotupa Mfalme yaani Mungu wetu haiondoi ukweli kuwa sisis ni walemavu lakini ni neema na tunapaswa kusimama katika neema na kubadilisha mtazamo wa namna tunavyojiona

Somo kutoka kwa Daudi

·         Tuwatafute maadui zetu na kuwatendea mema.
·         Tuwatatute masikini, dhaifu na wenye ulemavu waliojificha na kuwabariki
·       Tuwabariki hata wale wasiostahili, tuwabariki wengine pia kwa sababu ya wengine tuwaonyeshe wema wa Mungu wetu wengine Dini ya kweli ni kuwaangalia wale wasiojiwezana kukutana na mahitaji yao, Yakobo 1:27 “ Dini iliyo safi, Isiyo na taka, mbele za Mungu Baba ni hii, kwemda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao na kujilinda na dunia pasipo mawaa.” Ni jambo la kusikitisha sana kuwa watu wengi siku hizi hasa waliomwamini Yesu wameacha kutenda mema, aidha watu wengi wanapopata madaraka makubwa huyatumia madaraka hayo kuhakikisha kuwa wengine hawainuki tena, watahakikisha wanamshughulikia kila wanayefikiri ni adui yao, watahakikisha kuwa wale walio tishio kwao wanawakandamiza mpaka wapotee, watahakikisha kuwa maisha ya wengine yanaharibika, Daudi hakuwa mtu wa namna hiyo, Mungu alipomuonyesha fadhili, aliwafadhili wengine hususani wale waliokuwa na hofu, waliokuwa wamejificha, waliokuwa wamepoteza kila kitu, waliokuwa hawana furaha Kama vile Yesu alivyosema sikuja kuwaita watu wema wapate kutubu bali wenye dhambi maana walio na afya hawahitaji Daktari, bali wale wasio na afya, Ni muhimu kujiuliza leo kuwaunaitumiaje nafasi iliyo nayo kwa manufaa ya wengine? Je wewe unaye mtu wa kumtendea mema?
Na. Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni: