Jumatatu, 10 Februari 2020

Chochea Karama ya Mungu iliyo ndani yako!

2Timotheo 1:3-6Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana.  Nami natamani sana kukuona, nikiyakumbuka machozi yako, ili nijae furaha; nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo. Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu.”


Utangulizi:


Ni muhimu kufahamu kuwa kila mwanadamu amezaliwa kwa kukiwa na kusudi fulani au wajibu fulani wa kuutimiza ulioko ndani yake, na katika wajibu huo ili aweze kuutimiza ipaswavyo, Mungu huweka karama au kipawa kwaajili ya kumuwezesha mtu huyo kutimiza kusudi la Mungu lililowekwa ndani yake 


Hata hivyo karama au kipawa kinapokuwa ndani ya mtu kuna maswala kadhaa yanayopaswa kufanyika ili kiweze kukua au kukomaa au kujitokeza katika ubora wake swala hilo sio lingine ni kuchochea kipawa hicho kilichomo ndani ya mtu aliyekusudiwa na Mungu kutumiwa katika shughuli husika. Tutajifunza somo hili muhimu kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-



·         Maana ya kuchochea Karama
·         Jinsi karama zinavyochochewa!
·         Namna karama zinavyochochewa!


Maana ya kuchochea Karama 

Paulo mtume anamwandikia Muhubiri na kiongozi kijana na mchanga katika Imani na maongozi ili kumtia moyo wakati yeye akiwa anaelekea ukingoni wakati huu Paulo mtume alikuwa gerezani kwa sababu ya injili, akisubiri kuuawa kwake muda si mrefu kwa hiyo anaandikwa waraka huu akiwa na hisia kali sana akijua ya kuwa anatengwa na wapendwa wake lakini vilevile akijua kuwa Timothy atakabiliwa namaswala mengi ya kuhubiri injili, uongozi, nausimamizi wa kanisa na shughuli nyingunezo katika jamii, na sasa anataka kumtia moyo ili asimame kiume awe imara ahakikisha anafanya kazi kwa bidii na uaminifu na ndipoi anaposema manenoi haya “Kwa sababu hiyo nakukumbusha uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani kwa kuwekewa mikono yangu”Neno hili katika biblia ya kiingereza NKJV (New King James Version) linasomeka hivi “Therefore I remind you to stir up the gift of God which is in you trough the laying of my hands” Biblia  nyingine zimetumia neno “Keep a blaze the gift” na neno “rekindle the gift” Maneno ya kiyunani yanayotumika katika lugha hii ni “xesikono” yaani kuchochea mfano wa kusogeza vijinga vya moto ili moto wa kutumia kuni uweze kuendelea kuwaka, kwa kawaida moto wa kuni kama umewashwa na ukaachwa bila kuchochewa unaanza kuzimika na ili uendelee kuwaka vema unahitaji kuchochewa, Moto unapochochewa huwa na tabia ya kuendelea kuwaka na kubaki katika hali ileile na nguvu ileile au kuwaka zaidi.  Paulo anamtaka Timotheo aendelee kuwaka na kubaki katika hali ile ile na nguvu ileile au kuwaka zaidi, akiwa na imani ileile kama iliyokuwa kwa bibi yake loisi na mama yake Eunike nay eye mwenyewe aliwa kamawao na kuzidi. Kwa hiyo wale wanaotumia tafasiri ya kuchochea kwa maana ya kukoroga mfano wa sukari kwenye chai maana hjii ni ya kipuuzi kwa mujibu wa asili ya maandiko haya hayazungumzii kukoroga yanazungumzia kuongeza moto kuchochea kuhakikisha moto unabaki pale plale au unaendelea.


Hii ina maana gani? Matokeo makubwa katika jambo lolote tunalolifanya yatawezekana kama moto wetu hautazimika, Chakula kitaiva vizuri na Matunda yataonekana kama hakuna mtu anazimia moyo, Mungu amempa kila moja wetu karama na vipawa kwaajili ya shughuli mbali mbali, ili kufanikisha huduma na utumishi aliouweka ndani yetu na ndani ya kila mmoja wetu, Kama wewe ni mwana michezo mfano Bondia na umefanikiwa kuchukua mikanda mbalimbali ya kimataifa haupaswi kuishia hapo, Kama ni shule ya msingi au sekondari na imefanikiwa kiwilaya au kimkoa au kitafifa kushika nafasi nzuri ya juu kwa kufaulisha zaidi katika mitihani ya kitaifa haipaswi kuridhika na kubweteka na kukaa hapohapo tu, Kama ni kanisa limefanikiwa kuwahubiri injili watu maelefu kwa maelfu na kuwaleta kwaq Yesu hawapaswi kuridhika na kuishia hapohapo, kama Mungu amekupa nafasi ya kuwa Kiongozi mkubwa wanchi yaani Rais, au makamu wa Rais au waziri waziri mkuu, au  jaji mkuu au mkuu wa jeshi la pilisi, au Magereza, au uhamiaji, au zimamoto au kujenga taifa au mkuu wa majezi ya ulinzi na usalama,  spika wa bunge au mkuu wa mkoa au mbunge au mkuu wa wilaya na kadhalika na viongozi wengine wote na katika kanisa vilevile Hatupaswi kuishia hapo lazima tuichochee moto wa maendeleo na kuhakikisha kuwa kila tulifanyalo haliwi nguvu ya soda lazima tuchochee moto wa maendeleo na kuhakikisha kuwa tunasonga mbele na kupiga hatua kubwa sana hiki ndicho Mungu anachokitaka,  Mungu anataka moto uwe mkali zaidi, Nimeona pia katika nchji yetu Makocha wengi wa mpira wa miguu wanatoka katika nji nyingine kana kwamba hatuna makocha hodari hapa nyumbani Makocha wa nyumbani wanapaswa kuchochea uwezo wao na kujiapiza kuifunga kila timu yenye kocha mgeni mpaka wakubali kuwa nyumbani tunaweza hiki ndio kitu Mungu anataka, mpaka ulimwengu ugundue kuwa wako watu wanaweza, ikiwa wewe ni muhubiri hubiri injili kwa viwango na ufanisi mkubwa, ikiwa wewe ni mwanamuziki wa injili imba kwa mafundisho yaliyo sahihi huku wewe mwenyewe ukiwa ni kielelezo cha kila unachokihubiri, mwimbaji wa nyimbo za kawaida wekeza hisia zako zote kwa bidii, mchezaji wa mpira, bondia, mwanariadha, mwalimu, mwanafunzi, nakila mtu hata katika ndoa zetu hatuna budi kuhakikisha kuwa tunachochea upendo, uzalendo na mshikamano na kuhakikisha kuwa unawake na kuwa moto mkali sana na tutaona maendeleo makubwa katika taifa letu, Kila mmoja akichochea kipawa na karama aliyopewa na Mungu matunda yetu hayawezi kuzimika na kila sekta katika taifa letu itaonekana ikistawi kwa namna ya kipekee na ya tofauti, Na ndio maana Paulo mtume alikuwa anamtaka Timotheo aichochee karama ya Mungu iliyomo ndani yake, Leo mimi nawataka wananchi wote kwa pamoja tuchochee kila karama na kipawa kilichomo ndani yetu kila ambacho Mungu ametupa na kuwa tusizimie moyo wala tusiogope.

Paulo mtume alikuwa akimuomba Mungu na kutamani kuona Maisha ya Timotheo yanakwenda juu zaidi ya pale alipokuweko na kuwa imani yake inapaa na kuongezeka, Paulo alikuwa anajua kuwa Timotheo ana vipawa vingi na anajua kuwa zikichochewa atafanya na kuwa bora zaidi, Kila mtu na kila mmoja wetu ana kipawa fulani ndani yake na karama ambazo mungu ameweka ndani yetu kwa makusudi mbalimbali lakini hatuwezi kujigundua mpaka mtu mwingine aone, atuchochee na kututia moyo, Kila mwanadamu anahitaji kutiwa moyo, Hakuna mwanadamu anayefurahia kutukanwa kila siku na kukashifiwa na kuambiwa kuwa hana lolote, Ni lazima tuwe na tabia chanya yenye kuwajenga na kuwatia moyo wengine badala ya kuwa watu wenye kuonyesha kuwa wengine hawawezi ilihali kumbe ni sisi ndio hatuwezi, swala la kutia moyo mtu na kumuona mtu akifanya vema halihitaji kusomea saikolojia ni falsafa ya asili tu “Natural Philosophy” Mara kadhaa mtoto anapoanza kusimama katika mila na desturi zetu huwa tunawaimbia kamimama peke yake kwamakusudi la kuwatia moyo wasimame, kweli kweli  na hatimaye husimama, Wanamichezo wa soka na wa aina mbalimbali wanawahitaji sana washabiki wao kufika kwa wingi uwanjani ili kuwatia moyo na kuwashangilia jambo hili huwapa moyo na kuwafanya wafanye bidii na kufanikiwa, Mungu anapokuwa ameweka vipawa ndani yetu na karama za aina mbalimbali zinahitaji watu wenye ujuzi wa kututia moyo na kuhakikisha kuwa kwa namna chanya wanatujenga na kututia moyo ili kipawa na karama zisipotee na kufifia.


Jinsi Karama zinavyochochewa!


Ndani ya Timotheo kulikuwa na Huduma au karama ya Uongozi, yeye aliitwa na Mungu na kufanya kazi na Paulo mtume akisimamia makanisa alikuwa anapaswa kuyaongoza makanisa alikuwa nafanya kazi za kichungaji, alikuwa ni mwangalizi wa makanisa ya Mungu ni askofu kijana, alikuwa Muhubiri wa injili lakini kama binadamu alikuwa muoga kidogo, na alikuwa mwenye haiba ya aibu hivi na Paulo alifahamu jambo hili  na hivyo alitaka kumtia moyo asiogope kwani Mungu hakutupa roho ya woga ona 2Timotheo1:7Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.” Hii maana yake ni kuwa Mungu anaweza kutupa vipawa vikubwa sana ndani yetu lakini kuna madhaifu ya kibinadamu inaweza kuwa woga, inaweza kuwa tunaona aibu au tunakosa nidhamu na kadhalika au tunaweza kuwa waoga na kwa kujua hili ndipo Mungu huwapa watu wake Roho Mtakatifu ili kuwawezesha kuwa wajasiri na kukabiliana na kila aina ya upinzani na kuweza kujihami dhidi ya upinzani wowote tutakaokutana nao Luka 12:11-12 “Na watakapowapeleka ninyi mbele ya masinagogi na maliwali na wenye mamlaka, msifadhaike kwa kuwaza maneno yenu jinsi mtakavyojibu au kusema; kwa kuwa Roho Mtakatifu atawafundisha saa ile ile yawapasayo kuyasema”. Matendo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” na Warumi 8;26 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.” Mungu yupo kututia nguvu na kutuwezesha na kutupa nidhamu na kiasi kuweza kushinda changamoto mbalimbali tunazokabiliana nazo katika maisha, Roho Mtakatifu hutuombea na kutusaidia kwa sababu anajua udhaifu wetu na hivyo hatupaswi kuogopa, kwa hiyo kuchochea kwetu hapa ni pamoja na kumtanguliza Mungu mbele katika kila tunalolifanya na Roho Mtakatifu atakuwepo kutusaidia kwa dhamiri njema!


Namna karama zinavyochochewa


Kwa kuwa Karama na vipawa hutoka kwa Mungu, ni lazima Mungu atangulizwe mbele, katika karama za maongozi ya kanisa na vipawa vya roho mtakatifu kamwe hatuwezi kutumia akili zetu wenyewe wala hatupaswi kutumia ngubvu zetu Roho Mtakatifu hufanya kazi na sisi kama tutakubalia atutumia kwa hiyo lazima kwetu kuwekewa Mikono na watumishi wa Mungu ili watuombee neema ya Mungu katikalile tunalokwenda kulifanya 

1.       2Timotheo 1;6 “Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu.” 

     Viongozi wa kanisa wanapotuombea neema na kuweka mikono yao juu yetu kazi zile zilizowekwa mbele yetu zinapata kibali cha kiungu na karama zilizokuwa zimejificha huibuka, hekima na maarifa hutukalia na ndio maana mtu akiwekewa mikono na kubarikiwa mwenendo wa maisha yake huwa tofauti Matendo ya mitume 13: 1-3 “Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.” Mtu wa Mungu anapowekewa mikono na kuombewa neema kwaajili ya majukumu aliyopewa roho ya maarifa na hekima ya kutekeleza wajibu wake kwa uzuri hukaa juu yake Kumbukumbu la torati 34:9 “Na Yoshua, mwana wa Nuni, alikuwa amejaa roho ya hekima; maana Musa alikuwa amemwekea mikono yake juu yake; wana wa Israeli wakamsikiliza, wakafanya kama Bwana alivyomwamuru Musa.” Yoshua aliweza kuwa kiongozi shujaa na mwenye imani na akasikilizwa na wana wa Israel kwa kuwa aliwekewa mikono na Musa hivyo kwa kuwekewa mikono na kuombewa neema kamama zilizoko ndani yako zinaweza kuchochewa kwa msaada wa Roho Mtakatifu.


2.       Kubali kufundishwa 


1Timotheo 4:13 “Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha.Paulo Mtume pia alimwambia Timotheo afanye bidii sana katika kusoma, Tayari Timotheo alikuwa ni Muhubiri wa Injili na alikuwa ni mwangalizi wa makanisa lakini anatakiwa afanye bidii sana katika kusoma, uko ujuzi mwingi umejificha katika vitabu, lakini kutokana na watu wengi kuwa na uvivu wa kusoma na kuelimika wamezima moto au wameshindwa kuuchochea moto na kuchochea vipawa vyao, kila kitu duniani kinahitaji kujiongeza, wako watu wengi sana hawafurahii ndoa zao kwa sababu wanandoa wameridhika na hali ile ile na ujuzi uleule na hawataki kujaribu kujifunza na kutafuta mambo mengine kutoka vitabuni, wako wafanya biashara ambao biashara zao zimedumaa kwa sababu wana mbinu zilezile na mitindo ileile, wafanyakazi katika taasisi, walimu na kadhalika wanapaswa kujiongeza, serikali mara kadhaa katika sekta ya elimu wamebadili silabasi, mifumo ya mitihani, mbinu za ufundishaji bila kutoa semina  ya kutosha na kueleweka kwa kwa walimu, ili waendane na mfumo mpya na kuwapeleka katika ngazi ya juu, wapo wachungaji wamesoma zamani na mambo yamebadilika wanapaswa kupata semina elekezi katika Nyanja zao ili kujiongeza na kuchochea uelewa walio nao mpaka kuwapeleka ngazi nyingine kila ki[pawa karama na nafasi Mungu anayotupa inahitaji maarifa ya kutosha  na bidii katika kujifunza ili ifanyike kwa usahihi zaidi


Kuna baadhi ya karama na vipawa ambavyo Mungu ameweka ndani yetu ambavyo ili vifanye kazi na kunolewa na kutumika katika viwango vya juu lazima kusoma na kujisomea na kujiongeza kuhusike au mazoezi makali na miiko yake au nidhamu zake zihusike, siku hizi kumeibuka wimbi kubwa sala la watu wanaomtumikia Mungu huku wakiwa hawana mafunzo ya utumishi huo, huu ni msiba mkubwa sana nakubali kuwa utumishi ni huduma na ni karama na ni kipawa lakini kinaweza kufanya kazi vizuri kwa kupitia mafunzo aidha mafunzo rasmi au mafunzo yasiyo rasmi lakini ni muhimu kupitia mafunzo hayo kwa muda wa kutosha ili utumishi wetu uwe na ufanisi na hii ndio njia mojawapo ya kuichochea Karama, Mungu humtumia mtu vuziri zaidi baada ya kumuandaa kwa muda wa kutosha na mrefu zaidi Matendo ya Mitume 7:22Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa hodari wa maneno na matendo” Mungu alimtumia sana nabii Musa lakini Musa alikuwa msomi alifundishwa hekima yote ya wamisri na akawa Hodari wa maneno na matendo, ni kwa kusoma tunaweza kuchochea Karama zilizoko ndeani yetu na tukawa watu Hodari, lazima ufikie wakati tukubali kujifunza tuwasikilize walimu na kuwatii, tuwasikilize wazazi na kuwatii, tuwasikilize makocha na kuwatii, tujifunze kwa waliostaafu, tujifunze kwa waliotutangulia, tujifunze hata kwa walioshindwa kwa kuwauliza walishindwaje ili sisi tusipite katika njia ileile.  

Matendo 18:24-26 “Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu. Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi.                 

Maandiko yanaonyesha jinsi Apollo alivyokuwa mtu mwenye Elimu na alikuwa hodari katika maandiko na alikuwa Muhubiri hata hivyo alihitaji kujua maswala kadhaa kwa usahihi zaidi na mwalimu wa neno la Mungu Prisilla na Akila ambao walikuwa ni watumishi wa Mungu Pamoja na Paulo mtume wao walimfundisha njia ya bwana kwa usahihi zaidi ili kuichochea huduma yake, Tunapokubali kujifunza tunajiweka katika kutumiwa na Mungu katika viwango bora zaidi na kusaidia kupunguza makosa ya kibinadamu, hivyo unapobaini kuwa una kipawa fulani tafuta watu sahihi watakaosaidia kukinoa ili kukiweka kitaalamu zaidi, ili utumiwe vema na kwa ubora zaidi.

3.       Hakikisha unaonana na watu sahihi.

Mungu anapokuwa ameweka Karama au kipawa au aina fulani ya maono, mwanzoni ni rahisi sana watu kukataa kutambua kipawa au karama uliyo nayo na unaweza kujikuta uko katika mazingira ya watu ambao wanaweza kuua kile ulicho nacho kwa nia njema au mbaya lakini pia kwa kutokujua kuwa umebeba nini, Nilipotembelea taifa la Korea ya kusini mwaka 2016 niliwahi kukutana na wat kadhaa wanaotumia mkono wa kushoto kwa ubora sana kama mimi na watanzania wenzangu tunaotumia mkono wa kulia, Mkorea mmoja akaniambia kuwa watu wanaotumia mkono wa kushoto ni wenye akili sana na hapa Korea wako wengi mno, kwa haraka nilisikia uchungu moyoni kabla ya kujibu lolote niliwaza kuwa ina maana sisi tunaotumia mkono wa kulia hatuna akili? Lakini haraka sana jibu llikuja na nikamwamboa mkorea yule kuwa kama ni hiyo Afrika watu wengi wana akili sana kwa sababu kila mtoto anayezaliwa na niliowaona mimi wanatumia mkono wa kushoto lakini wazazi wetu hutuchapa na kutukemea kisha hutufundisha kutumia mkono wa kulia kwa sababu kwetu Afrika kutumia mkono wa kushoto kwa mila na desturi zetu sio jambo la busara na halna heshima, na mkorea yule aliacha majivuno yake,  kwa nini nimetumia mfano huu hapa unaweza kuwa na kipawa cha aina fulani na unaweza kuwa umezaliwa nacho unaweza kuwa unapenda kuchora na wazazi wanaweza kudhani unajisomea kumbe unachora na wakakukataza kuchora ili kwamba usome lakini kumbe wanaua kitu cha thamani ulichojaliwa na Mungu, Unaweza kuwa unapenda sana kucheza mpira lakini wazazi wakakukataza ili kwamba usije ukaumia au uweze kuweka mkazo katika kusoma lakini kumbe wakawa wanafifisha kipawa kilichoko ndani yako!  Mtu mwenye karama au kipawa ili aweze kukichochea hana budi kuhakikisha kuwa anaelekea mahali sahihi ili kupata mafunzo na kutiwa moyo zaidi kuhusu kipawa chake ona katika  

Luka 1:39-40 “Basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti.”

 Unaweza kujiuliza kuwa ni kwa nini Mariamu alipotaarifiwa  na Malaika Gabriel kuwa atakuwa na Mimba na atamzaa Masihi ambaye ni mrithi wa kiti cha enzi cha Daudi milele? Na tunaona Mariamu anafanya haraka kwenda kumtembelea Elizabeth na kukaa kwake miezxi mitatu wakati malaika anamwambia jambo hili Mariamu pia alimueleza jambo jingine kwa kusudi la kumtia moyo Mariamu maana alijiuliza inawezekanaje jambo hili kutokea naye hajui mume? Malaika alitaka kumuonyesha Mariamu kuwa Mungu hashindwi jambo na hata Elizabeth aliyeitwa tasa sasa ana ujauzito wa miezi sita ona:-

Luka 1:34-37 “Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.” 


Unaona Jambo hili lilimfanya Mariamu kwenda haraka sana kwa Elizabeth kwa sababu alikuwa amechanganyikiwa kwa maono makubwa ambayo malaika alisema naye ni kama malaika alikuwa amemuonyesha wazi kuwa mtu sahihi anayeweza kukusaidia kwa wakati huu ni Elizabeth ambaye naye Mungu amemfanyia mambo makubwa na magumu yaliyoshindikana kibinadamu Mariamu hangeweza kumwambia mama yake. Wala mwalimu wake au mtu yeyote aliyemjua alijua kuwa mtu aqnayeweza kumuelewa ni Elizabeth tu mtu mwenye maono na ndoto na muujiza na kipawa na karama kama zake 


Luka 1:36-37” Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.Mariamu alikuwa ametiwa moyo kupitia maneno haya alihitaji kujifunza kwa mtu sahihi aliyemtangulia alihitaji muongozo, alihitaji kupokea uzoefu, Elizabeth ndiye aliyekuwa mtu sahihi wakati huu wa kumtia moyo Mariamu, kumfundisha, kumuelekeza, kumuonyesha upendo na urafiki, kumpandisha imani na kumtetea ona maneno ya Elizabeth 

Luka 1:41-45 “Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi?  Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.”   


Unadhani Mariamu angeenda kwa mtu asiye sahihi ingekuwaje angeambiwa Mungu wangu ni nani atakayekuelewa umekwisha unaanzaje kumwambia mtu una mimba unawezaje kutimiza ndoto hii unawezaje kuifanya biashara hii, unawezaje kuandkia andiko maoni haya ndugu yangu hii ni kazi ngumu sana haiwezekani, vifaa vimepanda sana haiwezekani, ujenzi ni gharama mno hutaweza unapokuwa na karama au ndoto au maono enenda  kwa mtu sahihi Elizabeth anamwambia Mariamu tena akiwa amejaa Roho Mtakatifu Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.”   Elizabeth anamwambia mariamu ulichoambiwa na Mungu kitatimia tu na ni baraka kubwa kama utaamini, mwamini Mungu yeye anaweza ndipo Mariamu akamuadhimisha Mungu na kutulia kwa Elizabeth kwa miezi mitatu, Unapokuwa na njozi au hata mapito na majaribu enenda kwa watu wanaopitia majaribu kama yako mtazungumza lugha moja, unapokuwa na karama waone waliokutangulia  walio sahihi wenye kipawa kama chako jifunze kutoka kwao ambao lugha zao zitakuwa chanya watakuambia UTATOBOA TU, Mwanangu utatoka hii kitu nakuhakikishia utatoka kirahisi tu, hivyo ndivyo unavyoweza kuichochea karama iliyo ndani yako.


4.       Kuwa mkomavu.

Acha ulimbukeni, watu wengi sana wameua vipawa vyao kwa sababu ya ulimbukeni, vipawa vinapowapa mafanikio wanakuwa na mbwembwe nyingi, kiburi kinapanda na kujidai, wakijifikiri kuwa wao ni watu maarufu sana wanapoteza adabu na kujali utu, wanaongeza mbwembwe nyingi sana, wanakosa umakini,  na wanaacha kujilinda Kipawa ni zawadi ni uwakili ni amana ambayo Mungu amewekeza ndani yako lazima uilinde 2Timotheo 1:14 “Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu.”  Unawezaje kujilinda kuhakikisha kuwa uko vilevile au unazidi mno lazima ujilinde na kiburi, watu wenye mafanikio sana duniani wala hawajidai,  Hawana maringo, hawajifanyi wanajua, wanapokea ushauri, wanajali wengine. Ni vema tukajivika unyenyekevu kwa sababu njia ya Mungu ya kutupeleka juu ni kujishusha 1Petro 5:6 

Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;”  Kumbe kanuni ya Mungu ya kukukweza ni kujishusha na kuishi maisha ya unyenyekevu. Unyenyekevu ndio unaoonyesha ukomavu lakini tukiwa na kiburi ni muhimu kufahamu kuwa hatuko mbali na aibu Mitahli 11:2 “Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu; Bali hekima hukaa na wanyenyekevu. Watu wengi wenye vipawa na karama   wameharibu sifa zao kwa sababu ya kiburi na hivyo wamefupisha muda wao wa kumtumikia Mungu au kutimiza kusudi walilokusudiwa na Mungu duniani ni kutokana na kujinyenyekeza sana Yesu aliinuliwa sana hii ndio kanuni ya mafanikio ya kutunza kipawa chako mbele za Mungu na wanadamu nia nyenyekevu itakuweka juu kama ilivyomuweka yesu juu mno Wafilipi 2:5-11” Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.” 


5.       Usikubali kupoa
 

Tunaweza kuchochea karama vilevile kwa kuhakikisha kuwa hatuuzimi moto wa Mungu ulioko ndani yetu, usikubali kupoa au kuwa vuguvugu, Maandiko yanaonyesha kuwa Mungu akikupa amekupa na haondoi kipawa wala karama alizoweka ndani yetu lakini ni kwa nini watu hufulia na kuisha kabisa sababu kubwa ni kupoa au kuwa vuguvugu Mungu anachukizwa sana na watu vuguvugu maandiko yanaonyesha uwezo wa kupoa uko katika mikono yetu na uwezo wa kuwa Moto pia, Mungu ameweka karama ndani yako wewe ni wajibu wako kuhakikisha unabaki moto Ufunuo 3:15-16 “Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.” Unaona Mungu hapendezwi na watu vuguvugu hii maana yake anatujua vema anataka tuwe moto, au ukishindwa uwe baridi ijulikana umekwisha umepoa lakini kamwe Mungu hataki tuwe vuguvugu atakutapika ndio maana utaweza kuona watu wanaibuka kisha wanatokweka na karama na vipawa vinakwisha. 


6.       Usimzimishe Roho Mtakatifu.

Biblia inaeleza katika 1Wathesalonike 5:19 “Msimzimishe Roho;” Roho Mtakatifu ni Mungu na ndiye chanzo cha Karama na vipawa vyote anavyowapa wanadamu, Kumzimisha Roho Mtakatifu maana yake nini  Roho Mtakatifu kama Mungu Hakuna mtu anaweza kumzimisha  haiwezekani lakini sisi wenyewe tena tunaweza kuanza kumuhuzunisha Roho wa Mungu kutokana na mtindo wa maisha unaomuhuzunisha Roho Mtakatifu kama Mungu na kumfanya aondoe neema yake Waefeso 4:30 “Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi.”  Tunapofanya dhambi na uasi endelevu dhidi ya Mungu Roho wa Mungu anaweza kutuacha na ushujaa wetu utakuwa umefikia kikomo na ndio maana Daudi aliomba asiondolewe Roho Mtakatifu Zaburi 51:11 “Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee.” Kwa Msingi huo tukiishi mtindo wa maisha unaomnyima Mungu Roho Mtakatifu kutuongoza na kutusaidia huku yeye akiwa chanzo cha vipawa vyetu tutapoteza uwepo wake Napenda sana tafasiri ya Kiibrania ya neno Msimzimishe Roho wenyewe wanatumia neno “KABAH” sawa na kusema Msimkabe Roho Mtakatifu, Msimbanie, kiingereza Do note Expelled, au do not neglected  au Quench not,  Kwa maana hiyo sisi wenyewe ndio tunawajibu wa kujiachia katika neema ya Mungu, kwa kufunga, kuomba, kusoma neno, kuabudu, kujiweka karibu na Mungu kuutafuta uso wake kwa bidii, kutubu kwa haraka endapo tumekosea na tutaona Roho wa Mungu alkiendelea kukifungua kipawa kilichopo ndani yetu kidogo kidogo. Na kututumia kwa viwango vikunbwa na vya hali ya juu.

7.       Uwe hodari

Watu wenye vipawa wanapigwa vita sana wanapambana watu wenye wivu, Ibilisi pia hapendi kwa sababu karama ni silaha za maangamizi zinampa Mungu utukufu na kuharakisha kazi ya Mungu na kwa sababu hizo upinzani ni lazima, Karama na vipawa pia Mungu huzitumia kuinua maisha binaksi ya Muhusika kwaajili ya hayo ni lazima uwe hodari na uwe shujaa Yoshua 1:9 “Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.” Mungu anataka tuwe hodari na tuwe na moyo wa ushujaa kwa sababu anajua kuna changamoto mbele yetu, Kila mtu anayetaka kuzichochea karama akumbuke kuwa mbali na hofu na awe na ujasiri, kwa sababu kila utakapoitumia Karama uliyonayo kutainuka wasiopendezwa na watajaribu kwa kila jinsi na kila namna kupingana nawe kama nduguze Yusufu walivyochukizwa naye hata kutaka kumuua kwaajili ya ndoto  alizokuwa nazo  

Mwanzo 37:5-11 “Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia;  akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake. Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia. Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi?  Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili.Unaweza kuona Mungu anampa ndoto Yusufu kuwa mtawala, ana maono mazito kwaajili ya kuja kuisaidia familia yake ana karama ya maongozi, ana karana ya unabii na kipawa cha kutafasiri ndoto kipawa hiki kingembeba na kumpeleka kwenye kiwango kingine kingeisaidia jamii na ndugu nzake pia lakini wao ndio walikuwa wa kwanza kuona wivu na hata kutaka kumuua kabisa ona 

Mwanzo 37:18-20 “Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake.” 


 Unaweza kuona ndugu zake Yusufu walikusudia kumuua kwa sababun ya ndoto zake yaani ileile karama aliyopewa iliwavutia maadui, ningeweza kukupa mifano Mingi kama Daudi alivyotaka kuuawa na Sauli kwa sababu ya karama, ningeweza kukupa mfano wa Samsoni alivyowindwa na Wafilisti kutokana na ngvu zake na uwezo wake wa ajabu aliokuwa nao, ningekueleza jinsi Yesu alivyokuwa tishio kwa viongozi wa dini sio kwa sababu alikuwa mwovu bali kwa wema uliovutia watu kwa maelfu yao na miujiza mikubwa aliyoifanya, ningekuopa habari za Petro na Yohana walivyokutana na uopinzani kwa sababu ya muujiza mashuhuri walioufanya, sikwambii habari za Paulo aliyetumiwa kufanya miujiza na kuwavuta wengi kwa Yesu alivyotaka kuuawa,  sikwambii habari za Daniel ambaye alifanyiwa njama za kila namna kutokana na vipawa alivyokuwa navyo, sikwambii Michael Jakcson alivyochukiwa na wazungu na kufanyiwa kila aina ya hila kutokana na vipawa,  haya na mengineyo ni mifano ni mifano tu inayokutaka uwe makinina uhakikishe unakuwa na ushujaa na moyo mkuu ili kutokuizima ile karama iliyoko ndani yako! Kipawa na karana zina tabia ya kuvutia watu wema na wabaya  


Luka 11: 53-54 “Alipotoka humo, waandishi na Mafarisayo walianza kumsonga vibaya, na kumchokoza kwa maswali mengi, wakimvizia, ili wapate neno litokalo kinywani mwake.” Unaweza kuona namna na jinsi waandishi yaani walimu nwa sheria na Mafarisayo walivyokuwa wakimzongazonga Yesu na kumchokoza ili waweze kumsonga kwa maswali mengi kusudi lao kuu ni kupata neno la Kumshitaki, ili kumuharibia Mungu akupe hekima na Busara  kama alivyompa Yesu ili kujilinda na kujihami na maadui.

Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu

Na Rev. Innocent Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!

0718990796

Maoni 7 :

Unknown alisema ...

If you're looking to burn fat then you need to start using this totally brand new custom keto plan.

To produce this service, licensed nutritionists, personal trainers, and chefs united to develop keto meal plans that are efficient, convenient, price-efficient, and delicious.

Since their first launch in January 2019, thousands of people have already transformed their figure and health with the benefits a proper keto plan can provide.

Speaking of benefits; in this link, you'll discover eight scientifically-tested ones given by the keto plan.

Unknown alisema ...

nimebarikiwa saaaaana na nasaha zako katika mada hii. Ubarikiwe sana

Unknown alisema ...

Neno zuri...barikiwa

Unknown alisema ...

Neno zurii sana barikiwa

Unknown alisema ...

Hakika nimejifunza vyema mtumishi wa Mungu

Bila jina alisema ...

Hakika nimefurahi na somo lako

Bila jina alisema ...

Nimejifunza barikiwa sana