Jumatatu, 24 Mei 2021

Jinsi ya kutupilia mbali aibu!!


Isaya 54:4 “Usiogope; maana hutatahayarika; wala usifadhaike; maana hutaaibishwa; kwa kuwa utaisahau aibu ya ujana wako, pia mashutumu ya ujane wako hutayakumbuka tena.”



Utangulizi:

Moja ya changamoto kubwa inayotukumba wanadamu tangu anguko la mwanadamu kutokea  katika bustani ya Edeni ni pamoja na changamoto ya aibu, au kuona aibu, au kutahayari. Aibu ni moja ya fedheha kubwa sana katika maisha ya mwanadamu, Hakuna mtu awaye yote anayependa kuaibishwa, Mpango wa shetani wakati wote ni kutuleta katika aibu, na kwa sababu hiyo kuna changamoto nyingi sana ambazo ibilisi huzifanya ili kutuleta katika aibu!, moja ya changamoto inayotuleta katika kuona/Kupata aibu ni pamoja na dhambi kama maandiko yasemavyo ona


Mwanzo 3:9-10 “BWANA Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha.”


Adamu na Eva wazazi wetu wakubwa sana waliokuwa karibu sana na Mungu walipofanya dhambi, walijisikia aibu, kule kujiona kuwa wako uchi na kujificha ilikuwa ni ishara ya aibu kwao kwamba wamevunja sheria ya Mungu wao, ni ukweli usiopingika kuwa dhambi ni aibu ya watu wote ona


Mithali 14:34 “Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote.”tunapofanya maovu kwa njia ya siri tunaweza kujifikiri kuwa ni wajanja na washindi, lakini dhambi zetu zinapofuniliwa na wengine wakazijua kwetu linaweza kuwa jambo la aibu, kwa msingi huo ni wazi kuwa aibu inaleta fadhaaa kubwa!. Na hakuna mwanadamu anayependa kuaibishwa!


Aibu hasa ni nini? Aibu ni tatizo la kisaikolojia na kisosholojia (Kijamii)- (Psychosocial-Problem) linaloendeshwa na hisia, hasi zinazotokana na dhamiri ya mwanadamu kujihuhukumu kuwa hajaenenda sawa na jinsi alivyopaswa kuenenda, ni hali ya kujitathimini kihisia na kujithaminisha katika hali ya chini na hivyo kupelekea kujitoa, kujificha, kujihukumu, kukosa furaha, kutokujitokeza, kutokujiamini, kukosa nguvu na kujiona hufai! Ni hofu ya kuogopa kuwekwa wazi kwa mambo yetu yasiyofaa tuliyoyafanya sirini, na wakati mwingine hutupelekea kuwashutumu wengine kwa kusudi la kuficha mambo yetu! Neno aibu kwa kiyunani ni Aischuno ambalo maana yake ni kuvuliwa nguo hadharani Yesu analishughulikia swala hilo la mtu kuvuliwa nguo kwa kutoa ushauri wa kutoa mavazi yatakayo ficha aibu hiyo ya kuwa uchi ona “Ufunuo 3:18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.” Hakuna mwanadamu awaye yote mwenye akili kamili na timamu ambaye atafurahia kuwekwa uchi hadharani, jambo kama hili ni aibu kwetu na kwa kila mwanadamu mwenye akili timamu.


Aibu ni moja ya tatizo linalohitaji kutatuliwa kiroho, Mungu katika Hekima yake na mpango wake wa ukombozi alikusudia pia kutukomboa kutoka katika aibu.  Yeye kama Muumba wa Mbingu na sisi anatujua vema namna na jinsi tunavyoteswa na aibu na hivyo aliwasaidia wazazi wetu wa kwanza kuwa mbali na aibu kwa kumwaga damu ya Mnyama ili awatengenezee mavazi ya ngozi na kuwavika hii ilikuwa ni ishara ya kinabii ya kuvikwa vazi la kutuondolea aibu yetu ona Mwanzo 3:21 “BWANA Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika.Kwaajili ya hayo nabii Isaya anatupa ujumbe kwamba tusifadhaike wala tusiogope na kwamba hatutatahayari wala kuaibishwa na kuwa Mungu mwenyewe ataifutilia mbali aibu yetu, hakuna wa kutushutumu wala hatutakumbuka tena aibu! Milele! Kwa hivyo ni ahadi ya Mungu kutuondolea Mauti, ni ahadi ya Mungu kutufuta machozi lakini vilevile ni ahadi ya Mungu kuiondoa aibu ya watu wake milele angalia Isaya 25:8-9 “Amemeza mauti hata milele; na Bwana MUNGU atafuta machozi katika nyuso zote; na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote; maana Bwana amenena hayo. Katika siku hiyo watasema, Tazama, huyu ndiye Mungu wetu, Ndiye tuliyemngoja atusaidie; Huyu ndiye Bwana tuliyemngoja, Na tushangilie na kuufurahia wokovu wake.”  

             

Yesu alikuja kuiondoa aibu yetu!

Moja ya majukumu makubwa ya waamuzi,wafalme na manabii nyakati za agano la kale ilikuwa ni pamoja na kuwaondolea watu aibu, kuna aibu za aina nyingi sana, kushindwa vita ni aibu, kufungwa magoli mengi ni aibu, kufeli ni aibu, ndoa kuvunjika ni aibu, kuziniwa mkeo au mumeo ni aibu, kufukuzwa kazi ni aibu, kufanya uzembe ni aibu, kuomba omba ni aibu, kufumaniwa ni aibu, kuugua magonjwa mabaya ni aibu, kufiwa na mtu mnayemtegemea sana ni aibu, kusemwa vibaya ni aibu, kuvuliwa nguo ni aibu, kusutwa ni aibu, kudhalilishwa ni aibu, kufanyiwa ukatili wa kijinsia ni aibu, kushindwa vita ni aibu, kutengwa kanisani ni aibu na maswala mengi kadhaa wa kadhaa yenye kuumiza moyo, kwa ujumla hakuna mwanadamu anayependa aibu, Na ndio maana watakatifu waliotutangulia nyakati za agano la kale walimkimbilia Mungu ili wasiabike milele Zaburi 31:1 “Nimekukimbilia Wewe, Bwana, Nisiaibike milele. Kwa haki yako uniponye,” Tunapokuwa tumefunikwa na aibu tunakosa ujasiri wa kufanya mambo kwa ufasaha hata katika kumtumikia Mungu, vijana wengi sana hunifuata kwa siri na kwa kuwa mimi pia ni mkuu wa shule na mchungaji, hivyo wanafunzi wengi wa kiume hunifuata na kunieleza wazi wazi, kuwa mchungaji mimi napenda sana kumtumikia Mungu na ni kweli unaweza kuona ni vijana wenye vipawa mbalimbali vya utumishi na lakini unaweza kuwaona wanakwepa kufanya huduma zao walizopewa na Mungu nao huniambia tunasumbuliwa na tatizo la kupiga punyeto na ingawa tatizo hili linafanyika kwa siri lakini dhamiri zao zinawafanya wajisikie aibu na kukosa ujasiri wa kutumika ipwaswavyo, nami huwa ninawajibu na kuwasaidia katika namna na hekima ile ambayo Mungu hunipa niwahudumie, lakini Napata jibu kuwa kama tuna mambo ya aibu hata kama watu hawajayajua, ni ya sirini yanapunguza ufanisi wetu kwa kiwango kikubwa, kuna changamoto nyingi mno zinazofanana na hizo ambazo huwanyima watu kuutumia uwezo waliopewa na Mungu kwa kuwa ndani ya mioyo yao wana hisia za aibu, na zinakuwa mbaya zaidi zinapofunuliwa katika jamii na hivyo wengi wanashindwa kujiamini, Habari njema ni kwamba Yesu ndiye mwamuzi mkuu, ndiye nabii, mkuu na ndiye mfalme mkuu, Yeye ukiacha kushughulika na maswala mengine pia alikuja kwaajili ya kutuondolea aibu, tunapokuwa na aibu tunashindwa kufanya mambo lakini tunapokuwa na ujasiri tunaweza kufanya mambo makubwa sana, Nisikilize Mungu anataka tumuone Bwana wetu Yesu Kristo kama sababu ya ujasiri wetu, wakati mwingine vilevile tunaogopa kukosea, tunatetemeka hatujiamini kwa sababu ya mambo ya aibu ya sirini au kwa sababu tunaogopa kuwamba tutakosea hatutafanya kwa ufasaha na kusababisha aibu hivyo tunaona aibu hata kabla hatujajaribu, huu ni uonevu wa ibilisi kwetu, Biblia inatuita kwamba tunapokuwa na hali kama hiyo na 

unapolemewa na aibu Mtazame Yesu –  Waebrania 12:2-3 “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu.”


Unapolemewa na aibu Kisogelee kiti cha rehema  - Waebrania 4;15-16 “Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”


Ujasiri wetu ni katika kumtumainia Kristo – Waefeso 3:11-12 “kwa kadiri ya kusudi la milele alilolikusudia katika Kristo Yesu Bwana wetu. Katika yeye tunao ujasiri na uwezo wa kukaribia katika tumaini kwa njia ya kumwamini.”


Kumbuka kuwa sisi wenyewe hatutoshi – 2Wakoritho 3:4-6 “Na tumaini hilo tunalo mbele za Mungu kwa njia ya Kristo. Si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lo lote kwamba ni letu wenyewe, bali utoshelevu wetu watoka kwa Mungu. Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha.”   

     

Mtumaini Bwana – Warumi 5:3-4 “Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi;  na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini; na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.” Tunapoweka tumaini letu kwake Mungu wetu hatatuacha tuaibike wala hatawaacha adui zetu wafurahi Zaburi 25: 1-3 “Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu, Ee Mungu wangu, Nimekutumaini Wewe, nisiaibike, Adui zangu wasifurahi kwa kunishinda. Naam, wakungojao hawataaibika hata mmoja; Wataaibika watendao uhaini bila sababu.”


Tumuombe yeye atufunike – Mwanzo 3:21 “BWANA Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika.Mungu anaijua aibu yetu anaelewa kioa kitu tuko wazi mbele zake hatuwezi kujificha Adam hata kabla hajaomba Mungu alijua fedhea ya Adamu alieleza wazi kuwa amejificha waliposikia sauti ya Mungu kwa sababu yuko uchi, Mungu alifanya mavazi kwaajili ya Adamu na mkewe akawavika, Yesu kama mwokozi anajua kwamba anawajibika kutufunika , tukimwamini hatutaaibika kamwe Warumi 10:11 “Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika.” Yaani kila amwaminiye hataaibika unaona


Tumtumikie yeye wala tusiache yeye atatusitiri – Zaburi 91:1-4 “Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi. Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini. Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo. Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao.” na Zaburi 27:4-5 “Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake. Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, Atanisitiri katika sitara ya hema yake, Na kuniinua juu ya mwamba.”


Hakuna wa kukushitaki Yesu ndiye mtetezi wetu – Zakaria 3:1-4 “Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa Bwana, na Shetani amesimama mkono wake wa kuume ili kushindana naye. Bwana akamwambia Shetani, Bwana na akukemee Ewe Shetani; naam, Bwana, aliyechagua Yerusalemu, na akukemee; je! Hiki si kinga kilichotolewa motoni? Basi, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu sana, naye alikuwa akisimama mbele ya malaika. Naye huyo akajibu, akawaambia wale waliosimama mbele yake, akisema, Mvueni nguo hizi zenye uchafu. Kisha akamwambia yeye, Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi.”    

          

Jinsi Yesu alivyoiondoa aibu yetu!

Maandiko kadhaaa hapo yametutia moyo kwamba hatupaswimkuogopa, na kuwa tunapaswa kuwa na ujasiri, kwa nini kwa sababu Kama Mungu alivyoshughulika na aibu ya adam na Eva na vilevile malaika wa bwana alivyoshughulika na aibu ya Yoshua kuhani mkuu ni ufunuo wa kimaandiko ulio wazi kuwa Yesu Kristo anashughulika na mambo yetu yote ya aibu na dhambi, Yeye alipoishughulikia dhambi pale msalabani na kuaibishwa aliaibihwa kwa niaba yetu, na kwa mateso yake akaimwaga damu yake pale msalabani ni wazi kuwa damu yake inafunika dhambi zetu na sio kufunika tu inaziondilea mbali kabisa, Yesu aliwaendea watu waliokuwa ni aibu kabisa katika jamii, wasio na matumaini wala kufikiri mkwamba itakuja itokee siku kuna mtu atawajali lakini wote aliwavuta kwake na kuwaingiza katiia mpango wake wa ukombozi, tunapozungumza wiokovu wetu ni pamoja na kufutiwa aibu yetu, hatupaswi mkuogopa wala kujidharau na kufikiri kuwa sisi hatufai hata kidogo, wala hatupaswi kuwalaumu watu, tunaye Mungu ambaye anajua kushughulika na aibu zetu kwa huruma zake na rehema zake atatufunika tunachotakiwa ni kumjia na kumueleza kuwa Bwana Yesu mimi sifai hata kidogo, nisamehe nisafishe kwa damu yako na kwa kazi yako uliyoifanya pale msalabani, na kwa njia rahisi sana weka imani kuwa amekusamehe na kukuelewa Mungu anatuelewa vizuri kuliko kiongozi yeyote wa kidini, hatupaswi kujificha, hupaswi mkuaxcha kuimba, hupaswi mkuacha kuhudhuria ibada na kumtumikia Mungu, Mwambie Bwana Yesu afanye kazi na wewe kwa utukufu wake akufiche chini ya ushindi wake akufunike kwa neema yake, usitishiwe na mtu yeyote kwa sababu wote biblia imesema wote ni wenye dhambi, wote tunaokolewa bure kwa neema kwa njia ya imani, asikutishe mtu kazi ya ukombozi sio mya mwanadamu wala haifanywi kwa vitisho vya kidini na viongozi wa kidini, wala kwa kukutenga imefanywa na Yesu pale msalabani nani yeye ndiye anayeweza kutuhukumu na kutuhesabia haki na sio mwingine, hakuna mamlaka yoyote inayoweza kukutenga na upendo wa Kristo, hata malaika hawawezi, viongozi wa dini hawawezi,  wako watu wanajipa mamlaka hata za kutenga au kukabidhi mtu kwa shetani, ni wajinga tu mwana akiwaweka huru mnakuwa huru kwelikweli watafunga hewa watatenga hewa mimi na Yesu tunaendelea kuwasiliana milele anaendelea kunibariki anaendelea kunitumia na wataisoma namba viongozi vipofu wa vipofu,  majoka wana wa majoka kuta zilizopakwa chokaa hakuna mtu wa kututenga na upendo wa Kristo, hakuna mtu mwenye hati miliki ya Mungu, ni watu waliojaa kiburi na jeusi wanaochukua nafasi ya Mungu tu wanaoweza kujifanya wana mamlaka ya kufunga lolote au kufungua lolote, nataka ujue ya kuwa mamlaka hiyo umepewa wewe na mimi, wakifunga nafungua mwenyewe wakifungua nafunga mwenyewe, wakikufukuza kwenye dhehebu lao na kuweka zengwe nenda linguine, wakikukataa anzisha la kwako liite hata kwa jina lako Muhubiri Yesu anza hata na mkeo na mwanao ahaaaaa, mpaka walalamike kuwa madhebu yamezidi utawajibu na vilabu vimezidi, acha kusikitika wanapokuaibisha kata aibu Yesu yuko kutupilia mbali uonevu Warumi 8:33 -35 “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? ” kisha 38-19 “Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima !    

Hakuna maoni: