Kumbukumbu La Torati 8:15-16 “aliyekuongoza
katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu
isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu, aliyekulisha jangwani
kwa mana, wasiyoijua baba zako; apate kukutweza, apate kukujaribu, ili
kukutendea mema mwisho wako.”
Utangulizi:
Wakati mwingine ili Mungu aweze
kutuimarisha na kutukomaza ili kutupeleka katika kusudi lake alilolikusidia
basi hutupitisha katika majaribu ya aina mbalimbali kwaajili ya kutufundisha
hali kama hii hututokea katika siku za maisha yetu tuwapo duniani na zaidi sana
katika maisha ya shuleni, maisha ya uanafunzi huwa yanahitimishwa kwa mitihani,
huwezi kumtenganisha mwanafunzi na mitihani hata kidogo, mtihani ndio unaoamua
hatima ya mwanafunzi na kumpeleka katika kiwango kingine cha kusudi la utumishi
wake duniani.
Ni msimu mwingine tena wa
mitihani, kwa majuma kadhaa sasa wanafunzi wetu watakuwa wanakaa kwaajili ya
mitihani yao, ambayo kimsingi vilevile itaamua hatima ya maisha yao ya baadaye,
kwa hivyo wote tunakubaliana kuwa ni wakati muhimu sana, Mitihani ni sehemu ya
kipimo cha yale tuliyojifunza na uwezo wetu wa kuelewa lakini sio hivyo tu
ndiyo inayotupeleka juu kuelekea hatua nyingine ya kielimu katika maisha, kwa
msingi huo kama wanafunzi tutakuwa tumewahi kukutana na mitihani ya aina
mbalimbali kama hii tunayokutana nayo sasa, Pamoja na uzuri na umuhimu wa
mitihani wakati wa mitihani ndio wakati ambao wanafunzi wengi hujikuta katika
msongo mkubwa wa mawazo na kufikiri itakuwaje, Je tunawezaje kuikabili mitihani,
Neno la Mungu linatupa kanuni za kutusaidia namna na jijnsi ya kushinda wakati
wa mitihani Roho wa Mungu aliniambia nisema haya kwa wanafunzi wanofanya
mitihani wakati huu.
1.
Hesabia
kuwa ni wakati wa furaha #
Yakobo 1:2 “Ndugu
zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali;”
Hapo Biblia inazungumzia kufurahi wakati tunapopitia katika majaribu ya aina
mbalimbali, Biblia inazungumzia kihalisia habari ya changamoto kadhaa katika
maisha ya ukristo na maisha ya duniani kwa ujumla, lakini kwa vile imesema
majaribu mbalimbali mimi nataka kuweka majaribu kama mtihani, nataka kuitumia
kanuni ileile ya jambo lile-lile ambalo huwa ni jaribu katika maisha huwa ni
changamoto huwa linatuhuzunisha na kutuondolea furaha kuwataka wanafunzi
wafahamu kuwa wakati wa mitihani japo wanatumia sana akili, na wanapaswa
kuongeza umakini mkubwa, wanakesha bongo zinachoka lakini wafahamu vilevile
kuwa sio wakati wa kuhuzuinika ni wakati wa kufurahi, ni wakati wa kujiachia
katika neema ya Mungu na kuondoa hofu kabisa kila mmoja akijua kuwa mtihani una
faida kubwa na kuwa utampeleka katika ngazi ya juu zaidi hivyo wakati kama huo
sio wa kulia na kuumia bali ni wakati wa furaha relax.
2.
Fanya
kwa utukufu wa Mungu.
Maandiko
yanatufundisha kuwa lolote tulifanyalo kwa neno au kwa tendo, tulifanye kwa
utukufu wa Mungu
1Wakoritho 10:31 “Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote,
fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.”
Hatufanyi mtihani kwaajili ya
mashindano, hatushindani na mtu, tunafanya lolote tulifanyalo kwaajili ya kumpa
Mungu utukufu, kwa msingi huo hakikisha kuwa Mungu anakwenda kutukuzwa kwa kile
unachokwenda kukifanya, acha mashindano, usishindane na mtu, wala shule yako
isifanye mashindano na shule nyingine,usiogope pia unapoona mwenzako ameandika
sana na kujaza kurasa haimaanishi kuwa ndio amejaza point, usiogope, mwenzako
anapoongeza booklet ya kujibia usipasuke moyo na kudhani kuwa labda mambo ni
mazuri kwake wala na wewe usiige kwa sababu balada ya kwenda kwenye point
unaweza kujikuta unajaza blaablaa kwa sababu ya kutaka kuwa kama Fulani kumbuka
kuwa unafanya mtihani kwa kusudi la kumpendeza Mungu, hivyo usijilinganishe na
mwingine endapo wasimamizi wa mtihani wanaruhusu mtu kutoka haraka wewe usitoke
kwa haraka unapoona kuna mtu kamaliza wewe fuata muda uliopangwa katika ratiba
na mtihani wako ukikumbuka kuwa wewe uko pale kwa kusudi la kumpendeza Mungu na
sio wanadamu
2Wakoritho2:9 “Kwa hiyo, tena, ikiwa tupo hapa, au ikiwa hatupo hapa,
twajitahidi kumpendeza yeye.”
Vyovyote vile jitahidi kuufanya
mtihani wako kwa kusudi la kumpendeza Mungu, Mungu anakuona, anajua hitaji
lako, anajua wazazi wako wamewekeza kiasi gani anajua walimu wako wamejitahidi
kiasi gani sasa wakati wa mtihani hakikisha kuwa unafanya mtihani kwa kusudi la
kumpendeza yeye, na kusudi lako kubwa liwe kwamba Mungu atukuzwe kwa matokeo
mema ya mtihani wako!
3.
Mwamini
Mungu!
Sisi hatuingii
katika chumba cha mtihani kama wapagani,au kama watu wasio na imani au
matumaini tunaingia tukiwa na Mungu aliye hai, ni lazima tumtangulize Mungu
mbele na ili tumpendeze yeye lazima tuwe na imani naye Maandiko yanasema pasipo
imani haiwezekani kumpendeza, kwa hiyo
ingia katika chumba chako cha mtihani ukiamini na kujua wazi kuwa yuko Mungu na
kuwa hatakuacha
Waebrania 11:6 “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu
amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale
wamtafutao.”
Mafanikio yetu na kuthibitika kwetu kutakuja tu endapo
tutamuamini Mungu, na kwa kuwa sisi tunamtumaini yeye ni dhahiri kuwa tutafanikiwa
2Nyakati 20:20 “Wakaamka
asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa
wakitoka, Yehoshafati akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa
Yerusalemu; mwaminini Bwana, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini
manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.”Hakuna mtu amemuamini Mungu
kisha Mungu akamuacha hivihivi tu!
4.
Fanya
mtihani kwa jina la Yesu
Mtu anaweza
kujiuliza Je naweza kutumia jina la Yesu kufanya mtihani ndio Jina la Bwana ni
ngome imara mwenye haki huikimbilia akawa salama ona
Mithali 18:10 “Jina la Bwana ni ngome
imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama.” Yesu mwenyewe alisisitiza kuwa tukiomba lolote kwa
jina lake baba wa Mbinguni atalitenda ona
Yohana 14:13-14 “Nanyi mkiomba lo lote kwa jina
langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo
lote kwa jina langu, nitalifanya.” Tunaweza kulitumia Jina la Yesu
kila wakati katika taabu yoyote naye atatusaidia, hili ndio jila lenye kuleta
msaada ndio jina linaloweza kutuokoa bila kujali historia zetu au wapi
tumetokea Biblia inasema kila, nakazia tena KILA, yaani bila kujali wewe ni nani, ni wa kabila gani, ni wa ukoo
gani, ni wa taifa gani, ni wa dini gani bila kujali haki yako unapoliitia jina
hili litaleta wokovu ulio sawa na mahitaji yako ona
Matendo 2:21 “Na itakuwa kila atakayeliitia
jina la Bwana ataokolewa.” Wengine wanaweza wasikubaliane nami
kwamba tunaweza kulitumia jina la Yesu katika mambo mazito sio kulichezea katika
mitihani, nisikilize mitihani ndio inayoamua hatima ya maisha yetu, hivyo
wakati wa mitihani sio wakati wa mchezo, tunamuhitaji Mungu na tunamuhitaji Bwana
Yesu wakati wa mitihani yetu kwa msingi huo ni muhimu kwetu tukafanya mtihani
huo kwa jina la Yesu, Biblia imesema lolote tufanyalo nakazia tena LOLOTE tufanyalo ukiwemo mtihani
tulifanye kwa jina la Yesu ona
Wakolosai
3:17 “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo,
fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.”
Unaona kumbe maandiko yanatutia Moyo kuwa tunaweza kufanya kila
tunachokifanya kwa jina la Yesu, iwe kwa neno au kwa tendo, ikiwa watakatifu
waliotutangulia katika agano la kale walifanya vita kwa jina la Bwana je kuna
dhambi gani kufanya mtihani kwa jina la Bwana wa majeshi?
5.
Usiibe/.
Wala usifanye udanganyifu!.
Kutoka 20:15-16 “Usiibe,
Usimshuhudie jirani yako uongo.” Ni amri mbili ambazo zinafuatana
katika maandiko, na katika amri Kumi, wote tunajua madhara ya udanganyifu,
tunafahamu namna dunia ilivyoingia katika huzuni kubwa sana kwa sababu ya
udanganyifu, shetani alipofanikiwa kumdanganya hawa alisababisha uharibifu
mkubwa, wakati wa mitihani shetani hatakosa kuwajaribu watu walio dhaifu,
usikubali kujaribiwa, usikubali kumpa shetani nafasi, Biblia inasema wala
msimpe ibilisi nafasi, nafasi moja tu inaweza kusambaratisha na kuharibu maisha
yako, hairuhusiwi kufanya udanganyifu wa aina yeyote wakati wa mtihani, Mungu
anataka tuwe waaminifu tu, hivyo basi jitahidi kutumia akili zako na kumtegemea
Mungu, hakuna msaada unaoweza kupewa na walimu wako wala mtu yeyote wala mzazi
wako zaidi ya msaada ule waliokusaidia kukulipia ada na kukufundisha, hivyo uwe
na bidii, ukaufanye mtihani ule kwa akili zako mwenyewe na kwa msaada wa Mungu
aliye hai, wala usiibe wala usifanye udanganyifu ambao unaweza kuwa na madhara
makubwa kwako, lakini vilevile kwa shule yako na kwa wenzako, na pia
kusababisha hasara kwa taifa na kuitia dosari wilaya yako mkoa wako na
kadhalika, hivyo tusijaribu kwa namna yoyote ile kufanya udanganyifu kwaajili
ya utukufu wa Mungu!, Mungu atatukuzwa vipi kama tumeibia, Mungu atatukuzwa tu
kama tulisoma kwa bidii, tukamuomba , tukamtegemea na kumuamini naye
akatusaidia basi.
6.
Muombe
Mungu!
Wako watu ambao
wanadharau maombi, wanadhani kuwa hayana msaada wowote wala kitu chochote cha
ziada hususani linapokuja swala la Mtihani, dhana hii ni ya kijinga, Hatupaswi
kuzitumainia akili zetu wenyewe japokuwa kutumia akili sio dhambi, akili ni
karama ya kwanza ambayo mwanadamu amepewa na Mungu, tuna haki ya kuitumia,
lakini ni kosa kubwa sana kukataa masaada wa Mungu wakati wa jaribio lililoko
mbele yetu, Neno la Mungu linasema tusijisumbue katika jambo lolote bali kwa
kuomba ona
Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa
kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na
amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika
Kristo Yesu.”
Maombi ni
silaha ya kipekee ambayo tunaweza kuitumia katika nyakati zote na kwa jambo
lolote, hatuna budi kuliamini neno la Mungu na kuomba, Yesu mwenyewe alipokuwa
anakabiliwa na Mtihani wa kufa msalabani aliomba na malaika wa Bwana wakaja
kumtia nguvu, inawezekana mtihani wenyewe ukawa sio tatizo lakini hofu yetu,
kukosa kwetu amani, kuogopa kukawa ndio tatizo kwa hiyo ni muhimu kuomba ili
tuhifadhiwe mioyo yetu na nia yetu na amani ya Mungu ipitayo akili zote
itatuhifadhi.
7.
Usiogope
Hofu ya mitihani
ni moja ya maumivu na homa kubwa sana ya wanafunzi wakati wa mtihani, wakati wa
mtihani watu wengi hujiuliza itakuwaje, mioyo inawadunda watu wanaogopa, namimi
pia nimefanya mitihani katiika viwango mbalimbali vya msingi, sekondari, vyuoni
na katika kozi nyinginezo, nimejiona na nimeona pia watu wengi wakiogopa
mitihani, Hata wachungaji katika vyuo vya Biblia huogopa mitihani, woga sio
mzuri, woga unaweza kuchelewesha kufikia kusudi la Mungu ndani yako, katika Kiwango
“level” ya chuo nilipokuwa na chukua digrii ya ualimu, ilikuwa ni ruhusa
kutokufanya mtihani kama unaona hauko tayari na maandalizi yako sio mazuri,
lakini pia ilikuwa ruhusa kurudia mtihani ukifeli, sikupenda kurudia mtihani
nilitamani kufaulu mara moja nitakapoufanya mtihani wangu, lakini mara kadhaa
niliahirisha kufanya mtihani kwa kutokujiamini kuwa laba maandalizi yangu
hayatoshi hivyo nilihairisha mara kwa mara,lakini mwisho nikaona mbona ninapoteza
Muda, mbona ninajichelewesha kufikia kusudi la Mungu analotaka kunitumia kwalo?
Nikamuamini Mungu nikaomba, Mungu aliponitia nguvu kufanya nilikasirika na
kuamua kuifanya yote bila kujali nilifanikiwa kuimaliza kwa wepesi sana, hata
hivyo nilikuja najishangaa kwa nini niliogopa sasa, niliogopa nini kumbe mbiona
inawezekana, ni kwa sababu waliita chuo kikuu kwa hiyo nilidhani sio mahali pa
mchezo na kuwa kila kitu ni kigumu kumbe inawezekana kama wengine walivyoweza.
Kuogopa kunaweza kuchelewesha lile ambalo Mungu alikuwa amelikusudia kwetu,
Hofu ni mbaya, wana wa Israel walipoogopa walishindwa kuirithi nchi ya kanaani
kwa wakati iliokusudiwa na hivyo ikawagharimu miaka mingi,
Hesabu 14:1-9 “Mkutano wote wakapaza sauti
zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule. Kisha wana wa Israeli wote
wakamnung'unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama
tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika
jangwa hili. Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake
zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri? Wakaambiana,
Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri. Ndipo Musa na Haruni wakaanguka
kifudifudi mbele ya mkutano wa kusanyiko la wana wa Israeli. Na Yoshua mwana wa
Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi,
wakararua nguo zao; wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi
ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. Ikiwa
Bwana anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi
yenye wingi wa maziwa na asali. Lakini msimwasi Bwana, wala msiwaogope wale
wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao
umeondolewa, naye Bwana yu pamoja nasi; msiwaogope.”
Wakati wote
linapokuja swala lolote linalotupa changamoto Fulani hatupaswi kuogopa,
tunapaswa kuona kama Kalebu na Yoshua kuwa kama Bwana yuko pamoja nasi hakuna
linaloweza kusimama kinyume nasi, tunaliitia jina la Bwana katika shida zetu na
tunaingia katika chumba cha mtihani tukiwa na imani kuwa yuko pamoja nasi
Zaburi 118:5-9 “Katika
shida yangu nalimwita Bwana; Bwana akanijibu akaniweka panapo nafasi. Bwana
yuko upande wangu, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? Bwana yuko upande
wangu, msaidizi wangu, Kwa hiyo nitawaona wanaonichukia wameshindwa. Ni heri
kumkimbilia Bwana Kuliko kuwatumainia wanadamu. Ni heri kumkimbilia Bwana.
Kuliko kuwatumainia wakuu.”
Unaona mwandishi wa zaburi ana ushujaa
mwingi sana kwa sababu ana uhakika kuwa Bwana yuko upande wake sisi nasi Mungu
yuko pamoja nasi kwa hiyo hatupaswi kuogopa na ushindi ni dhahiri kuwa utakuwa
upande wetu ona
Warumi 8:31 “Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu,
ni nani aliye juu yetu?”
8.
Fanya
kwa bidii.
Kama jinsi
ambavyo tumeiona kuwa mtihani ni nafasi, ni nafasi kwa sababu ndio unaoamua
hatima ya maisha yetu, na kutupeleka kule kwenye utume ambao Mungu ametuitia
kuufanya duniani kwa hiyo “it is an
opportunity” ni fursa kwa msingi huo hatuna budi kuhakikisha kuwa
tunaufanya vizuri sana
Muhibiri 9:10 “Lo lote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa
nguvu zako; kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko
kuzimu uendako wewe.”
Unaona maandiko yanatutia moyo kufanya kila
kitu kwa ufasaha, hakikisha unaandika vizuri, unapangilia vizuri, unaonyesha
machakato wa namna na jinsi ulivyopata majibu, nenda kwenye pointi kama hakuna
cha kuelezea usipige blaablaa nyingi, kumbuka huufanyi mtihani kwaajili ya kuwapendeza
wanadamu bali kwaajili ya utukufu wa Mungu, hivyo mambo ya Mungu hayapaswi
kufanywa kwa upuuzi, hivyo fanya kazi yako vema.
9.
Jipumzishe! (Relax)
Mwanzo 2:1-3 “Basi
mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza
kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake
yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika
siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na
kuifanya.”
Kama tumemuomba Mungu na kuzingatia yote yale ambayo
Mungu ametupa kuyafanya yaani tumejisomea sana, tulikesha sana, tulifunga na
kuomba, tunamuamini Mungu hatuogopi tuna uhakika kuwa Mungu yuko upande wetu
basi “Relax” usijisumbue pumzisha akili zako acha kuwa na msongo wa mawazo, uwe
na utulivu, wala hata usijadili kitu na mtu utakapotoka nje hasa kwa mtihani
ambao umekwisha kuumaliza, tafakari na utulie na upumzike hii nayo ni kanuni ya
kiungu unapomaliza kufanya assignment ambayo Mungu amekupa unahitaji kupumzika “Relax”
Yona 4: 5-6 “Ndipo
Yona akatoka mjini, akaketi upande wa mashariki wa mji, akajifanyia kibanda
huko, akakaa chini yake uvulini, hata aone mji ule utakuwaje. Na Bwana Mungu
aliweka tayari mtango, akaufanya ukue juu ya Yona, ili uwe kivuli juu ya kichwa
chake, na kumponya katika hali yake mbaya. Basi Yona akafurahi sana kwa sababu
ya ule mtango.”
10.
Chochea
karama iliyoko ndani yako kwa kuwekewa Mikono
Nilitaka
kumalizia mahubiri yangu na poit namba 9 tu lakini Roho wa Mungu akanitaka
niweke hii ya kuwekewa Mikono, unapofika wakati wa Mtihani kama hivi ni muhimu
kufahamu kuwa kila mtu, kila kijana kila mtoto, Mungu ameweka kitu ndani yake,
lakini wakati mwingine hakiwezi kujitokeza bila kuwekewa Mikono, hii ni sihara
ya maombezi yenye kuleta neema kubwa sana japo sio lazima, lakini ni kanuni
bora ya kimaandiko, kama sio tatizo mchungaji na aweke mikono juu ya wale
wanaokwenda kufanya mitihani yao, inahitajika neema, kuwekea mikono mtu hufanya
hekima na maarifa ya kiungu yawe juu yake ona
Kumbukumbu la Torati 34:9 “Na Yoshua, mwana
wa Nuni, alikuwa amejaa roho ya hekima; maana Musa alikuwa amemwekea mikono
yake juu yake; wana wa Israeli wakamsikiliza, wakafanya kama Bwana
alivyomwamuru Musa.”
Mmmh kumbe basi mtu anapowekewa Mikono karama
zilizojificha ndani yake huibuka na kumpa neema ya kuwa na hekima na maarifa kama
ilivyokuwa kwa Musa alimuwekea mikono Yoshua na Paulo mtume alimuwekea mikono Timotheo,
mtu anapowekewa mikono aidha roho ya woga huondoka na amani ya Mungu humkalia
hivyo uko umuhimu wa kuwawekea mikono watahiniwa endapo mazingira na muda
unaruhusu kufanya hivyo kwa watumishi husika Kama Paulo alivyofanya kwa
Timotheo. ona
2Timotheo 1:6-7 “Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu,
iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu. Maana Mungu hakutupa roho ya woga,
bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.”
Uongezewe neema!
Rev. Innocent Kamote
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni