Jumatatu, 27 Septemba 2021

Hekima yao ikapate kuwa ubatili na maarifa yao yawe ujinga!



2Samuel 15:30-31 “Daudi akapanda akishika njia ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akilia alipokuwa akipanda; naye alikuwa amejifunika kichwa chake, akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia walipopanda. Mtu mmoja akamwambia Daudi ya kwamba, Ahithofeli yu katika hao waliopatana na Absalomu; Daudi akasema, Ee Bwana, nakusihi, uligeuze shauri la Ahithofeli liwe ubatili


Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa unapokuwa kiongozi wa ngazi yoyote ile, iwe kisiasa au kiimani, huwezi kupendwa na kila mtu, sio viongozi tu lakini hata katika maisha haya ya kawaida, wanakuwepo watu wanaotukubali sana na vilevile wako watu ambao hawawezi kutukubali, hili ni jambo la kawaida sana, hatuwezi kuwapendeza watu wote, sisi sio wema sana kama Masihi Yesu Kristo yeye alikuwa mwema mno kuliko mtu awaye yote lakini watu walimchukia na kufikia ngazi ya kumsulubisha Luka 15:18-20 “Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia. Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu.” Unaona Yesu hapa alikuwa anawafundisha viongozi, yaani hawa ni wale wanafunzi 12 wa Yesu ambao walikuwa kimsingi wanaandaliwa kuwa viongozi wa kanisa, si unakumbuka Yesu alikuwa na wanafunzi wengi? Ila wachache waliandaliwa kuwa viongozi, sasa kaka kiongozi kama Yesu aliongoza vizuri na wakamfanyia mabaya wakamuasi ni wazi kuwa sisi tutafanyiwa mabaya makubwa zaidi Luka 23:31 “Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?kulijua jambo hili mapema ni muhimu kwa sababu biblia inatufundisha vilevile namna ya kukabiliana na changamoto za aina hii na namna tunavyoweza kumuomba Mungu yanapotokea maswala magumu katika maisha yetu!, Leo tunachukua muda tena kujifunza kwa undani kuhusiana na jinsi Mungu alivyomtetea mtumishi wake Daudi alipokuwa kiongozi na alipokuwa akitimiza majukumu yake kwa Mungu! Namna na jinsi alivyomuomba Mungu kwa hekima na Mungu akamsikia.

 

2Samuel 15:30-31 “Daudi akapanda akishika njia ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akilia alipokuwa akipanda; naye alikuwa amejifunika kichwa chake, akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia walipopanda. Mtu mmoja akamwambia Daudi ya kwamba, Ahithofeli yu katika hao waliopatana na Absalomu; Daudi akasema, Ee Bwana, nakusihi, uligeuze shauri la Ahithofeli liwe ubatili

Katika mstari wetu wa msingi leo, tunajifunza mojawapo ya tukio gumu sana lililopata kumtokea Mfalme Daudi akiwa madarakani, Daudi alipata jaribu la kupinduliwa madarakani na kijana wake wa kumzaa aliyeitwa Absalom, hata hivyo uasi wake haukuwa na nguvu sana mpaka pale mtu mmoja muhimu mno katika utawala wa Daudi aliyeitwa Ahithofeli, alipoungana na upande wa uasi, Mtu huyu alikuwa ndiye mshauri mkuu wa Mfalme Daudi na alikuwa na sifa kubwa muhimu mno Maandiko yanasema uwezo wake wa kushauri ulikuwa sawasawa na Mtu anapouliza kwa Mungu ona.

2Samuel 16:23 “Na shauri lake Ahithofeli, alilokuwa akilitoa siku zile, lilikuwa kama mtu aulizapo kwa neno la Mungu; ndivyo yalivyokuwa mashauri yote ya Ahithofeli, kwa Daudi, na kwa Absalomu.”  

Unaweza kuona kwamba mtu huyu alikuwa na nafasi muhimu sana kwa mfalme na nafasi yake kama mshauri wa mfalme ilikuwa nafasi muhimu sana, Licha ya kuna na nafasi hii inasemekana pia Ahithopheli alikuwa na kijana wake ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa maakida yaani makomandoo  au mashujaa wanaotajwa kuwa waliokuwa mstari wa mbele katika majeshi ya Daudi Mfalme ona

2Samuel 23:34 “na Elifeleti, mwana wa Ahasbai, na Heferi, Mmaakathi, na Eliamu, mwana wa Ahithofeli, Mgiloni;

Unaona huyo Eliamu alikuwa ni kijana wa Ahithofeli kwa msingi hio kwa vyovyote vile lazima ieleweke wazi kuwa Ahithofeli alikuwa mtu muhimu na hakuwa mtu wa kawaida na katika mashauri na hekima alikuwa mtu muhimu kwa mfalme kwa miaka Mingi.

Hekima ya Ahithofeli

Wengi tunajiuliza ni nini kilimpata Ahithofeli kwanini alimchagua Absalom aliyeasi badala ya Daudi? Kwanini mtu huyu aliyekuwa na ujuzi wa kushauri na hekima ambayo inatajwa kuwa alikuwa akishauri, ushauri wake ulikuwa sawa na mtu kutafuta ushauri kwa Mungu? Nini kilimpa sifa kuwa anavyoshauri ni kama mtu akiuliza kutoka kwa Mungu? Watu wengi wanasema kuwa huenda ushauri wake kumwambia Absalom azini na wake za baba yake ulikuwa ushauri mbaya na usio wa kiungu, Binafsi ninakataa ushauri wake Ahithofeli ni kweli kabisa ulikuwa kama ushauri utokao kwa Mungu, Mapema sana Daudi alipofanya dhambi na kumtwaa mke wa Uria na kisha kufanya njama za kumuua Uria, Nabii Nathan alitumwa na Mungu kuja kumuonya Daudi dhidi ya dhambi zake na adhabu ambazo angepewa ona

2Samuel 12:1-13Ndipo Bwana akamtuma Nathani aende kwa Daudi. Naye akamwendea, akamwambia, Palikuwa na watu wawili katika mji mmoja; mmoja wao alikuwa tajiri, wa pili maskini. Yule tajiri alikuwa na kondoo na ng'ombe wengi sana; bali yule maskini hakuwa na kitu, ila mwana kondoo mmoja, mdogo, ambaye amemnunua na kumlea; naye akakua pamoja naye, na pamoja na wanawe; hula sehemu ya posho lake, na kukinywea kikombe chake, na kulala kifuani mwake, akawa kwake kama binti. Hata msafiri mmoja akamfikilia yule tajiri, naye akaacha kutwaa mmoja wa kondoo zake mwenyewe au mmoja wa ng'ombe zake mwenyewe, ili kumwandalia yule msafiri aliyemfikilia, bali alimnyang'anya yule maskini mwana-kondoo wake, akamwandalia yule mtu aliyemfikilia. Ndipo hasira ya Daudi ikawaka sana juu ya mtu yule; akamwambia Nathani, Aishivyo Bwana, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili kufa; naye atamrudishia yule mwana-kondoo mara nne, kwa sababu ametenda neno hili, na kwa sababu hakuwa na huruma. Basi Nathani akamwambia Daudi, Wewe ndiwe mtu huyo. Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nalikutia mafuta, uwe mfalme juu ya Israeli, nikakuokoa na mkono wa Sauli; nami nikakupa nyumba ya bwana wako, na wake za bwana wako kifuani mwako; nikakupa nyumba ya Israeli na ya Yuda; na kama hayo yangalikuwa machache, ningalikuongezea mambo kadha wa kadha. Kwa nini umelidharau neno la Bwana, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa wana wa Amoni. Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako. Bwana asema hivi, Angalia, nitakuondokeshea uovu katika nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako mbele ya jua hili. Maana wewe ulifanya jambo lile kwa siri; bali mimi nitalifanya jambo hili mbele ya Israeli wote na mbele ya jua. Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia Bwana dhambi. Nathani akamwambia Daudi, Bwana naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa.”

Uko uwezekano ulio wazi kabisa kwamba maelekezo haya yaliyotolewa na Nabii Nathani ambayo yalikuwa yanatoka kwa Mungu wakati yanatolewa Ahithofeli hakuwepo kabisa na mwandishi wa Kitabu anamuona Ahithofeli kama mshauri ambaye ushauri wake anapoutoa ni kama mtu anayeuliza kutoka kwa Mungu, kwanini kwa sababu ukiiangalia adhabu hii ambayo Mungu alikuwa ameitangaza Nathan Nabii kwa Daudi na ushauri aliokuwa anautoa Ahithofeli ilikuwa ni kama mtu anayetaka kulitimiza neno lililotoka kinywani mwa Bwana kupitia nabii wake

2Samuel 16:20-23 “Kisha Absalomu akamwambia Ahithofeli, Haya, toa shauri lako, tufanyeje. Naye Ahithofeli akamwambia Absalomu, Ingia wewe kwa masuria ya baba yako, hao aliowaacha ili kutunza nyumba; na Israeli wote watasikia ya kuwa umechukizwa kabisa na baba yako; ndipo itatiwa nguvu mikono yao wote walio pamoja nawe. Basi wakamtandikia Absalomu hema juu ya nyumba darini; naye Absalomu akaingia kwa masuria ya babaye machoni pa Israeli wote. Na shauri lake Ahithofeli, alilokuwa akilitoa siku zile, lilikuwa kama mtu aulizapo kwa neno la Mungu; ndivyo yalivyokuwa mashauri yote ya Ahithofeli, kwa Daudi, na kwa Absalomu.”

Unaweza kuona namna na jinsi Ahithofeli alivyokuwa na Hekima ya ajabu, na uwezo mkubwa wa kushauri sawa na mapenzi ya Mungu, Ahithofeli alikuwa na hekima na busara kubwa na alijua namna ya kuishawishi jamii, kitendo cha kumshauri Absalom alale na masuria wa baba yake hadharani kiliifanya kambi ya Absalom kupata nguvu kwani kiliwaaminisha kuwa ni ukweli ulio wazi kuwa kijana amemchukia baba yake waziwazi hivyo waliweza kuiteka mioyo ya watu, kiuadilifu ushuri huu haukuwa mwema lakini kinabii Ahithofeli alisaidia kutimia kwa unabii wa Nathan na ahadi ya Mungu ya kumuadhibu Daudi, na ndio maana mapema sana Absalom alipoasi alimuhitaji mtu huyu aliyekuwa Mshauri hodari, mwenye hekima na sio tu kuwa alikuwa mwenye hekima lakini vilevile alikuwa shujaa yaani alikuwa na ujuzi wa kivita kwa hivyo uasi wa Absalom ulipata nguvu kubwa sana alipompata Aithofeli, vita hiii ilikuwa moja ya vita ngumu sana kwa Daudi na uwezekano wa kushinda ulikuwa ni mdogo kama sio rehema za Mungu ona 

2Samuel 15:10-13. “Lakini Absalomu akapeleka wapelelezi katika kabila zote za Israeli kusema, Mara mtakaposikia sauti ya tarumbeta, ndipo mtakaposema Absalomu anamiliki huko Hebroni. Na watu mia mbili walioalikwa wakatoka Yerusalemu pamoja na Absalomu, wakaenda katika ujinga wao wasijue neno lo lote. Absalomu naye akatuma kumwita Ahithofeli Mgiloni, mshauri wake Daudi, kutoka katika mji wake, yaani, Gilo, alipokuwa akitoa dhabihu. Fitina yao ikawa na nguvu; maana watu waliokuwa pamoja na Absalomu wakazidi kuwa wengi. Mjumbe akamfikilia Daudi, akasema, Mioyo ya watu wa Israeli inashikamana na Absalomu.”

Kwa namna na jinsi Daudi alivyofahamu uwezo wa Ahithofeli alijua wazi kabisa kuwa vita imekwisha kuwa kali sana na kutoboa kwake kuko katika mazingira magumu mno, Daudi alitoroka ikulu akiwa miguu peku na akajitanda nguo kichwani akiwa analia kwani alihitaji rehema za Mungu tu, kumuokoa katika vita ile kali

2Samuel 15:30 “Daudi akapanda akishika njia ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akilia alipokuwa akipanda; naye alikuwa amejifunika kichwa chake, akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia walipopanda.”

Swali kubwa la kujiuliza ni kwanini Ahithofeli aliyekuwa na hekima namna hii, Hekima yake haikumuongoza kuungana na Daudi? Kulikuwa na dhida katika maisha ya Ahithofeli, Hekima yake ilimezwa na uchungu na moyo wake wa kutokusamehe na kuachilia! Na roho mbaya      

Hekima imemezwa kwa uchungu!

Ahithofeli Pamoja na kuwa alikuwa mtu muhimu na kuwa yeye na mwanaye wote kwa Pamoja walimtumikia Daudi katika kulitimiza shauri la Mungu, Na kuwa mtu mwenye hekima ya kupita kawaida tunaposoma maandiko mwanaye anatajwa kuwa ni Eliam

2Samuel 23:34 “na Elifeleti, mwana wa Ahasbai, na Heferi, Mmaakathi, na Eliamu, mwana wa Ahithofeli, Mgiloni;”

unapofanya uchunguzi wa kimaandiko inaonekana kuwa binti wa Eliam kijana wa Aithofeli ndiye Bathsheba ona vizuri katika maandiko haya

2Samuel 11:2-3Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho. Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti?

kwa maana hiyo sasa Ahithofeli alikuwa ni babu wa Bath-sheba, binti wa kijana wake Eliamu, kwa msingi huo basi Ahithofeli alitunza uchungu moyoni kwa kitendo alichofanyiwa mjukuu wake aliutunza uchungu huo kwa miaka mingi, hivyo alikuwa akimtumikia mfalme kwa unafiki, hivyo ndivyo uchungu ulivyoharibu maisha ya mtu mwenye hekima ya ajabu, uchungu uliweza kuharibu sio hekima yake tu hata maisha yake baadaye, uchungu huu ulifunuliwa sio tu kwa kuungana na Absalom lakini inaonekana katika ushauri wake alikuwa na nia ya dhati ya kumshambulia Daudi, sio tu akitumia Hekima yake lakini alikuwa tayari hata kumshambulia kwa mikono yake  na kumuua ona  shina la uchungu linapunguza neema ya Mungu kwetu na kutufanya tufanye mambo ya hovyo,

Waebrania 12: 14-15 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.”

Kutokana na kutunza uchungu kwa Muda mrefu Aithofeli sasa anapanga kumuua Daudi kwa mikono yake mwenyewe, anajiamini kuwa hakuna sababu ya kusumbua watu wala kumwaga damu ya watu wengi hapa ni kummaliza Daudi pekee na kazi imekwisha,

2Samuel17: 1-4 “Zaidi ya hayo Ahithofeli akamwambia Absalomu, Niache nichague watu kumi na mbili elfu, nami nitaondoka na kumfuatia Daudi usiku huu; nami nitamshambulia wakati atakaokuwa amechoka, na mikono yake imekuwa dhaifu, nami nitamtia hofu; na watu wote walio pamoja naye watakimbia; nami nitampiga mfalme peke yake; na hao watu wote nitawarejeza kwako; mtu yule umtafutaye ni kana kwamba wamerudi wote; na hivyo watu wote watakuwa katika amani. Shauri hili likawa jema machoni pa Absalomu, na machoni pa wazee wote wa Israeli.”

Unaweza kuona Ahithofeli alikuwa anajiamini sana hii ni wazi kuwa mtu huyu licha ya kuwa Mshauri na mtu mwenye hekima vilevile alikuwa anajua kupigana, kama kijana wake Eliamu alikuwa moja ya mashujaa wakubwa katika makomandoo wa Daudi ni wazi kuwa Ahithofeli alikuwa na uwezo mkubwa na mbinu kali za kivita alihitaji watu 12 elfu tu na angemuua Daudi tu na kazi ingekuwa imekwisha, ni wazi kabisa kumbe uchungu unapotunzwa moyoni watu wanatunza mauti,

Mathayo 5:21-22 “Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto.”  

Ni wazi kuwa uchungu na kisasi kinaweza kuharibu Hekima ile Mungu anayoikusudia kwetu maisha ya Aithofeli na maneno yake na mpango wake ulionyesha wazi kuwa ana uchungu mkubwa na Daudi na, Daudi ni kweli alikuwa amefanya dhambi na alikuwa kweli amejutia dhambi yake alitubu mbele ya Nathani Nabii na alikuwa ametamkiwa msamaha na kukubali adhabu zote ambazo Mungu alikuwa amezikusudia, hata hivyo kwa upande wa Pili Ahithofeli alikuwa hazijui njia za Mungu yeye aliendelea kuitegemea akili yake mwenyewe na kusahahu kuwa ziko njia za kiungu

Mithali 3:5-8 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu. Itakuwa afya mwilini pako, Na mafuta mifupani mwako.

Unaona Ahithofeli alikuwa ameacha kumtegemea Mungu wala hakumtumaini kwa lolote alizitegemea akili zake alikuwa mwenye hekima machoni pake mwenyewe, alichukulia poa kile kitendo cha kukubalika katika Israel na kusifiwa na wazee, hakumcha Mungu na kwa sababu hiyo hakujua kuwa uovu ulikuwa unammendea, uchungu ukamuharibu mtu mwenye hekima moyo wake ukajaa kulipiza kisasi na kutaka kuua mtu asiye na hatia kwa Mungu, Daudi alitambua njia za Mungu, alifahamu kuwa Mungu atamhurumia na kumpa rehema alimuomba Mungu na kumtegemea yeye, hata kabla ya kupanga vita na kupigana yeye alimuomba Mungu, Daudi alikuwa tayari hata kuwasamehe watu waliomtukana

2Samuel 16:5-12Basi mfalme Daudi alipofika Bahurimu, tazama, kulitoka huko mtu wa jamaa ya nyumba ya Sauli, jina lake akiitwa Shimei, mwana wa Gera; alitoka, akalaani alipokuwa akienda. Tena akamtupia Daudi mawe, na watumishi wote wa mfalme Daudi; na watu wote na mashujaa wote walikuwako mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto. Na Shimei alipolaani, alisema hivi, Nenda zako! Nenda zako! Ewe mtu wa damu! Ewe mtu usiyefaa! Bwana amerudisha juu yako damu yote ya nyumba ya Sauli ambaye umetawala badala yake; naye Bwana ametia ufalme katika mkono wa Absalomu mwanao; kisha, angalia, wewe umetwaliwa katika uovu wako mwenyewe, kwa sababu umekuwa mtu wa damu. Ndipo Abishai mwana wa Seruya, akamwambia mfalme, Mbona mbwa mfu huyu amlaani mfalme bwana wangu? Na nivuke, nakusihi, nikaondoe kichwa chake. Mfalme akasema, Nina nini na ninyi, enyi wana wa Seruya? Kwa sababu yeye analaani, na kwa sababu Bwana amemwambia, Mlaani Daudi, basi, ni nani atakayesema, Mbona umetenda haya? Daudi akamwambia Abishai, na watumishi wake wote, Angalieni, huyu mwanangu, aliyetoka viunoni mwangu, anautafuta uhai wangu; si zaidi Mbenyamini huyu sasa? Mwacheni alaani, kwa sababu Bwana ndiye aliyemwagiza. Labda Bwana atayaangalia mabaya yaliyonipata, naye Bwana atanilipa mema kwa sababu ya kunilaani kwake leo.” Daudi alizifahamu njia za Mungu, alisamehe hata waliomlaani, akijua wazi kuwa Mungu atazigeuza laana zao kuwa Baraka!, Daudi alimtegemea Mungu kwa asilimia 100 na hakuzitegemea akili zake tu, Daudi alimlilia Mungu!

Ee Bwana, nakusihi, uligeuze shauri la Ahithofeli liwe ubatili   

Daudi alitumia njia ya kiungu, Yeye mwenyewe alikuwa shujaa wa vita, lakini alikuwa na uzoefu kuwa hakuna vita ambayo alipigana peke yake, alijua kuwa siri kubwa ya ushindi wa vita yake ni Bwana, tangu ujana wake alipompiga Goliathi alimpiga kwa jina la Bwana wa majeshi ya Israel, na kila wakati alihitahi fadhili za Mungu ziweze kumpigania na alihitaji kujua kuwa bwana yuko upande gani, kumbuka Daudi alikimbia ikulu akiwa analia alipaza Sauti yake juu akilia kwa uchungu na kurusha mavumbi juu alikuwa akimlilia Mungu aweze kuingilia kati

2Samuel 15:30 “Daudi akapanda akishika njia ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akilia alipokuwa akipanda; naye alikuwa amejifunika kichwa chake, akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia walipopanda.”

 Akiwa katika hali hii ya kuomba Daudi alielezwa kuwa Mshauri wake muhimu sana wa kutegemewa alikuwa amejiunga na uasi wa Absalom, huyu ndiye Ahithofeli alikuwa sasa amemsaliti alikuwa ni mtu wa karibu sana kwa Daudi lakini amemgeuka,Huenda hii ndio sababu ya Daudi kuimba zaburi hii

Zaburi 41:9 “Msiri wangu tena niliyemtumaini, Aliyekula chakula changu, Ameniinulia kisigino chake.”

Pamoja na mambo mengine Daudi alimuomba Mungu dua muhimu sana iliyoleta ushindi katika maisha yake Daudi alisema maneno haya

2Samuel 15:30-31 “Daudi akapanda akishika njia ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akilia alipokuwa akipanda; naye alikuwa amejifunika kichwa chake, akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia walipopanda. Mtu mmoja akamwambia Daudi ya kwamba, Ahithofeli yu katika hao waliopatana na Absalomu; Daudi akasema, EE BWANA, NAKUSIHI, ULIGEUZE SHAURI LA AHITHOFELI LIWE UBATILI

Daudi aliyalaani maarifa na hekima ya Ahithofeli tangu wakati ule iwe ubatili, aliibatilisha hekima yake haithofeli ikapate kuwa ubatili, na Maarifa yake yawe ujinga, hii ilikuwa duwa Muhimu sana inayoweza kutupa ushuindi katika maisha yetu hata katika wakati huu tulio nao, tunapokuwa na vita zozote za kiroho, tunapokabiliwa na majanga mazito na maadui wanaotafuta kutuua au kutuangamiza au kutuumiza au kutujeruhi, maombi pekee tunayoweza kumuomba Mungu ni kuifanya hekima yao maadui zetu kuwa ubatili ma maarifa yaio kuwa ujinga Daudi alikuwa anajua kuwa Mungu wa Mbinguni ana uwezo wa kutangua mashaurui ya watu wabaya, anauwezo wa kuharibu mikono ya watu waovu isitimize makudui yao na kuzinasaa hekima zao kuwa hila na mashauri yao kuharibika kwa haraka

Ayubu 5:12-13 “Yeye huyatangua mashauri ya wadanganyifu, Mikono yao isipate kuyatimiza makusudi yao. Yeye huwanasa wenye hekima katika hila yao wenyewe; Na mashauri ya washupavu yaharibika kwa haraka.”

 Ni tabia ya Mungu kugeuza mashauri ya wanaojidhani kuwa wana hekima, au maarifa ni kazi yake kuwatia wazimu, kuwarudisha nyuma na kuyafanya maarifa yao kuwa ujinga

Isaya 44:24-25. “Bwana, mkombozi wako, yeye aliyekuumba tumboni, asema hivi; Mimi ni Bwana, nifanyaye vitu vyote; nizitandaye mbingu peke yangu; niienezaye nchi; ni nani aliye pamoja nami? Nizitanguaye ishara za waongo, na kuwatia waganga wazimu; niwarudishaye nyuma wenye hekima, na kuyageuza maarifa yao kuwa ujinga;”

Watu wasiotembea katika njia za Mungu wamejaa chuki, hawana upendo, wamejaa kisasi, kila wakati wanatafuta mabaya watu hao hawatoboi, Mungu anaigeuza Hekima yao kuwa upumbavu

Warumi 1:21-22. “kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza. Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika;”

Mungu yuko tayari kuiharibu hekima ya watu wenye hila hekima ya dunia hii na amaeahidi katika neno lake kuwa ataiharibu hekima yao wanaojidhani kuwa wana hekima na atazikataa akili zao wanaojidhania kuwa wana akili na hekima ya kidunia itafanywa kuwa upumbavu

1Wakoritho 1:19-20. “Kwa kuwa imeandikwa, Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, Na akili zao wenye akili nitazikataa. Yu wapi mwenye hekima? Yu wapi mwandishi? Yu wapi mlete hoja wa zamani hizi? Je! Mungu hakuifanya hekima ya dunia kuwa ni upumbavu?

Aithofeli alikuwa amemezwa na uchungu, hivyo Hekima na akili yake ilikuwa sio ya kungu bali ilikuwa ya dunia hii hekima iliyojaa ugomvi na kuondoa amani hii ndiyo Mungu anaibatilisha

Yakobo 3:14-18. “Lakini, mkiwa na wivu wenye uchungu na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme uongo juu ya kweli. Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani. Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya. Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki. Na tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.”

Mungu aliishikia Maombi ya Daudi

Katika namna ya kushangaza sana Daudi alimtuma mshauri wake mwingine rafiki yake wa karibu aliyeitwa Hushai kwamba aende kwenye kambi ya maadui, awe miongoni mwa washauri wa Absalom na atumike kutangua ushauri wa Aithofeli, kwa kuwa tayari Ahithofeli alikuwa amejawa na uchungu na moyo wa kisasi na kutokusamehe, lakini zaidi sana kuwa na chuki dhidi ya mpakwa mafuta wa Bwana na hata kukusudia kumuua , Mungu aliutumia ushauri wa Hushai na kwa mara ya kwanza ushauri wa Aithofeli ulikataliwa na hapo ndipo mtu huyu mwenye kiburi alipokimbia nyumbani na kwenda kujiua mwenyewe

2Samuel 17:1-14 .”Zaidi ya hayo Ahithofeli akamwambia Absalomu, Niache nichague watu kumi na mbili elfu, nami nitaondoka na kumfuatia Daudi usiku huu; nami nitamshambulia wakati atakaokuwa amechoka, na mikono yake imekuwa dhaifu, nami nitamtia hofu; na watu wote walio pamoja naye watakimbia; nami nitampiga mfalme peke yake; na hao watu wote nitawarejeza kwako; mtu yule umtafutaye ni kana kwamba wamerudi wote; na hivyo watu wote watakuwa katika amani. Shauri hili likawa jema machoni pa Absalomu, na machoni pa wazee wote wa Israeli. Ndipo Absalomu akasema, Basi, mwiteni Hushai, Mwarki, naye, tukasikie atakayosema yeye pia. Basi Hushai alipofika kwa Absalomu, Absalomu akamwambia, akasema, Ahithofeli amesema hivi; je! Tufanye kama alivyosema? Kama sivyo, sema maneno yako. Hushai akamwambia Absalomu, Shauri hili alilolitoa Ahithofeli si jema wakati huu.Hushai akafuliza kusema, Wamjua baba yako na watu wake, ya kuwa ni watu mashujaa hawa, nao wana uchungu katika mioyo yao, kama dubu aliyenyang'anywa watoto wake nyikani; tena baba yako ni mtu wa vita, hatalala pamoja na watu wake.Angalia, amefichwa sasa katika shimo, au penginepo; kisha itakuwa, watakapoanguka baadhi yao mwanzo, kila mtu atakayesikia, atasema, Kuna machinjo katika watu wanaofuatana na Absalomu. Basi hata yeye aliye shujaa, mwenye moyo kama moyo wa simba, atayeyuka kabisa; maana Israeli wote wanajua ya kuwa baba yako ni shujaa, na ya kuwa watu wale walio pamoja naye ni mashujaa. Kwa hiyo shauri langu ni hili, Waisraeli wote toka Dani mpaka Beer-sheba wakusanyike kwako, kama mchanga wa bahari kwa wingi; na wewe uende vitani mwenyewe. Hivyo tutamfikia mahali po pote atakapoonekana, na kumwangukia kama vile umande uangukavyo juu ya nchi; wala hatutaacha hata mmoja wao, yeye na watu wote walio pamoja naye. Tena, ikiwa amejitia katika mji uwao wote, basi Israeli wote wataleta kamba, na kuuendea mji ule, nasi tutaukokota mpaka mtoni, wala halitaonekana huko hata jiwe dogo moja la mawe yake. Naye Absalomu na watu wote wa Israeli wakasema, Shauri la Hushai, Mwarki, ni jema kuliko shauri la Ahithofeli. Kwa maana Bwana alikuwa amekusudia kulivunja shauri jema la Ahithofeli, ili Bwana alete mabaya juu ya Absalomu.” Unaona hivi ndivyo Mungu alivyomtetea Mtumishi wake Daudi na kubatilisha shauri la Aithofeli hebu na tuone yaliyomkuta sasa

2Samuel 17:23Naye Ahithofeli alipoona ya kuwa shauri lake halikufuatwa, akatandika punda wake, akaondoka, akaenda nyumbani kwake, mjini mwake, akaitengeneza nyumba yake, akajisonga; akafa, akazikwa kaburini mwa babaye.”

Ahithofeli anamwakilisha Yuda, kama jinsi ambavyo Yuda alimsaliti Yesu na kisha alipopata uchungu alikwenda akajiua yeye mwenyewe, Hekima yake ya kumuza Yesu iliishia kuwa mauti, hatuna budi kuhakikisha kuwa wakati wote tunafanya mambo katika hekima ya kiungu, tunapamba kwa kutumia hekima ya Mungu na tujue namna ya kumuo,ba Mungu katika maisha yetu abatilishe kila makusudi mabaya ya adui zetu ama wale wanaotutakia mabaya na wale wenye hekima za dunia hii zilizojaa hila na uchungu tujifunze kumtegemea Mungu katika mambo yote wala tusizitumainie akili zetu wenyewe, Bwana atupe neema yake ili tuweze kuzijua njia zake na Mungu wangu na bwana wangu na aifanye hekima ya adui zetu kuwa ubatili na maarifa yao kuwa upumbavu katika jina la yesu Kristo Amen

Rev. Innocent Samuel Kamote


Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!

#0718990796#




Hakuna maoni: