Wafilipi 3:4-11 “Walakini mimi ningeweza
kuutumainia mwili. Mtu ye yote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili,
mimi zaidi. Nalitahiriwa siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya
Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo,
kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo
kwa sheria sikuwa na hatia. Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu,
naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu
mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu,
Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu
kuwa kama mavi ili nipate Kristo; tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki
yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo
katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani; ili nimjue yeye, na uweza
wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake;
ili nipate kwa njia yo yote kuifikia kiyama ya wafu”
Utangulizi:
Kwa watu au kampuni zinazofanya
biashara neno hasara na faida ni maneno ya karibu sana katika misamiati ya kila
siku ya maisha ya biashara, Kila wakati wanajua mwenendo wa biashara zao endapo
wanapata faida au wanapata hasara, kusimama au kuendelea kwa Biashara yoyote ile
kunategemeana na faida inayopatikana au hasara inayopatikana, kuendelea kwa
biashara Fulani kunategemeana sana na jinsi biashara hiyo inavyoingiza faida,
Marabi wa kiyahudi wengi walikuwa wanafahamu swala hili la kibiashara nao wakalitumia katika kuainisha
jambo lililo na umuhimu na lisilo na umuhimu mfano utaweza kuona Mathayo 16:26 “Kwani atafaidiwa nini mtu
akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini
badala ya nafsi yake?”
Katika somo letu la msingi Paulo
mtume anatumia mtindo huo huo kuonyesha maswala ya msingi kwake na maswala
yasiyo ya msingi, Wafilipi 3:7-8 “Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu
kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote
kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana
wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa
kama mavi ili nipate Kristo;” Unapofanya uchunguzi wa kimaandiko
utaweza kuona kuwa hasara na faida inayozungumziwa hapa ni mambo ambayo ni ya
msingi na mambo ambayo sio ya msingi, na hii inatusaidia sisi nasi leo kujihoji
na kutafakari kuwa ni mambo gani tunayapa kipaumbele kama mambo ya msingi na
mambo yapi hatuyapi kipaumbele yaani mambo yasiyo ya msingi katika maisha!. Kwaajili
ya hayo hapo tutaweza kugundua mambo yaliyo na faida kwetu na mambo yasiyo na
faida kwetu, Paulo mtume aliyahesabu mambo yote yasiyo na faida kama hasara na kuyahesabu
kuwa kama mavi kutokana na faida ya kumpata Yesu. Ni mambo gani hayo ya msingi
ambayo aliyazingatia kisha baadaye akayaacha na kuona ni afadhali kupata hasara
iwa mambo ambayo mwanzoni alifikikuwa yana faida kwake:-
1.
Dini
za wazazi wetu.
Kama kuna jambo
litawapa hasara kubwa sana watu wengi ni pamoja na kung’ang’ania dini za wazazi
wao, hizi ni zile imani ambazo tumezirithi kutoka kwa wazazi wetu, imani hizi
zitatuleta katika hasara kubwa badala ya faida, Paulo Mtume alikuwa akipambana
vikali na watu waliokuwa wakihubiri dini ya kiyahudi na kufikiri kuwa ni dini
bora zaidi kuliko kumpata Yesu, ni ukweli ulio wazi na dhahiri kuwa hakuna
urithi wa kiroho, hali ya kiroho ya kila mtu inategemeana na yeye anavyokutana
na Mungu kwa binafsi na sio kwa sababu ya wazazi, wake nyakati za namna hiyo
kwa sasa haziko tena, watu wengi leo hii wako katika madhehebu au dini Fulani
kwa sababu tu eti babu yake baba yake na ndugu zake wote walizaliwaga humo, kwa
hiyo mtu yuko tayari kwenda Motoni na kutokumkubali Kristo kwa sababu tu
anaiona dini ya baba zake kuwa ina faida, Wayahudi wengi sana walidhani kuwa
Mungu atawahesabia haki kwa sababu wao ni watoto wa Ibrahimu, Yesu aliwajibu
wazi kuwa huwezi kuwa mtoto wa Ibrahimu kisha ukawa muuaji, kwa vyovyote vile
wayahudi hawakujua kuwa tayari wamekuwa na baba mwingine
Yohana 8:39-44 “Wakajibu,
wakamwambia, Baba yetu ndiye Ibrahimu! Yesu akawaambia, Kama mngekuwa watoto wa
Ibrahimu, mngezitenda kazi zake Ibrahimu. Lakini sasa mnatafuta kuniua mimi,
mtu ambaye nimewaambia iliyo kweli, niliyoisikia kwa Mungu. Ibrahimu hakufanya
hivyo. Ninyi mnazitenda kazi za baba yenu. Ndipo walipomwambia, Sisi
hatukuzaliwa kwa zinaa; sisi tunaye Baba mmoja, yaani, Mungu. Yesu akawaambia,
Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu,
nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma. Mbona
hamyafahamu hayo niyasemayo? Ni kwa sababu ninyi hamwezi kulisikia neno langu.
Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda.
Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna
hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu
yeye ni mwongo, na baba wa huo.”
Wayahudi wengi
walijifikiri wako sahihi kwa sababu baba yao ni Ibrahimu, walidhani hali ya
kiroho inaweza kurithiwa kwa jinsi ya mwili na kwa kushika mapokeo ya baba zao,
Lakini Yesu alikuwa akiwajulisha kuwa huwezi kurithi hali ya kiroho bila kuamua
kufuata mambo ya rohoni wewe mwenyewe, Paulo mtume anaonyesha hali kama hiyo
kuwa kabla hajamjua Yesu alifikiri kuwa ana haki zote vilevile kama wayahudi
wengine naye alikuwa mwenye bidii sana katika maswala ya imani akijua kuwa
yatampa faida kubwa sana kwa kumpendeza Mungu kupitia taratibu za baba zake na
mila za kwao na madhehebu ya kwao na kupitia vyuo vyao, lakini alipomfahamu
Yesu alifahamu kuwa yale mambo ya kwanza aliyokuwa akiyashikilia na kufikiri
kuwa na faida sasa anaachana nayo na kuyaiona kuwa ni hasara ukilinganisha na
uzuri wa kumpokea Kristo:-
Wafilipi 3:3-7 “Maana
sisi tu tohara, tumwabuduo Mungu kwa Roho, na kuona fahari juu ya Kristo Yesu,
wala hatuutumainii mwili. Walakini mimi ningeweza kuutumainia mwili. Mtu ye
yote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi.Nalitahiriwa
siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa
Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo, kwa habari ya juhudi,
mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na
hatia. Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa
ajili ya Kristo.”
Paulo anaonyesha
kuwa yeye kama ni kuitumainia Dini aliitumainia sana, alitahiriwa siku ya nane
kama dini yao ilivyoagiza, alikuwa ni
muisraeli yaani ni myahudi kama walivyo wayahudi wengine, alizaliwa katika
kabila la Benjamin, alikuwa mwebrania halisi, na alikuwa wa madhehebu ya
mafarisayo na aliishika torati, na aliliudhi kanisa na kuwatesa wakristo
akifikiri kuwa ni sawa kwa mujibu wa dini yao, na aliishika torati hasa na kuwa
kwa habari ya kuishika torati hakuwa na dhambi yoyote, Paulo anaonyesha jinsi
alivyokuwa jemadari wa kuishi maisha ya haki kwa niaba ya dini yake na aliipigania.
·
Aliishika torati tangu utoto, yeye alipitia
mafunzo ya sharia chini ya mkufunzi aliyeheshimika sana na wayahudi aliyeitwa
Gamaliel ona
Matendo 22:3 “Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa
Kilikia, ila nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa
sheria ya baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi
nyote mlivyo leo hivi;”
Matendo 5:34 “Lakini mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamalieli, mwalimu
wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza, akaamuru
mitume wawekwe nje kitambo kidogo,”
Gamaliel alikuwa ni Rabbi aliyeheshimika sana, kusoma kwake
ni kama kusoma chuo kikuu kilichoheshimika sana kwa wakati huo kwa kuwa alikuwa
ni Mwalimu wa sharia aliyebobea sana katika madhehebu ya mafarisayo, na Paulo
mtume alikuwa mwanafunzi wa mkufunzi huyu wa kiyahudi. Lakini hata hivyo alipompata
Yesu degree zake za dini ya kiyahudi alizihesabu kuwa si kitu au ni hasara
ukilinganisha na kumpata Yesu Kristo!
·
Alikuwa Farisayo yaani moja ya madhehebu
yaliyokuwa yakiheshimika sana kwa mitazamo mikali sana na iliyohesabika kama
dini sahihi zaidi Matendo 26:5 “wakinijua
sana tangu mwanzo, kama wakipenda kushuhudia, ya kwamba nalikuwa Farisayo kwa
kuifuata madhehebu ya dini yetu iliyo sahihi kabisa.”
·
Kwa habari ya wivu zeal yaani imani kali Paulo
alikuwa na imani kali kiasi cha kutumika kuliudhi kanisa ona
Wafilipi 3:6 “kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari
ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia”.
Matendo 8:3 “Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na
kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani.”
Matendo 9:1-2 “Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi
wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka ampe barua za kuenda Dameski
zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake,
awafunge na kuwaleta Yerusalemu”
·
Kwa asili alikuwa myahudi ni wa uzao wa Ibrahimu
·
Kwa asili alikuwa mbenjamin kabila mojawapo
halisi la kiyahudi
·
Kwa asili alikuwa mwebrania wa waebrania, yaani
alizaliwa akiwa mwebrania kweli kweli na kiutamaduni yeye ni mwebrania
kwelikweli ambapo napo hakuwa na sababu ya kubagulika Palulo mtume anaonyesha kuwa alikuwa
amekamilika idara zote kwa habari ya dini, yeye sio tu alimcha Mungu bali pia alikuwa
tayari kuuwa na kuwatesa na kuwafunga wale
wote aliodhani kuwa hawamchi Mungu kwa
mujibu wa dini yake, Paulo mtume alikuwa mtu aliyejitoa katika dini yake kuliko
kawaida huu ulikuwa ni wakati ambapo hakuwa amemjua Yesu, maisha yake ya awali katika dini yake
yalikuwa ya muhimu na ya faida kwa wakati huo akijua ya kuwa anaingiza kwake na
kwa Mungu wake, Lakini sasa alipobaini ya kuwa kwa Yesu kunalipa zaidi
akabadili kibao na kuhesabu yale ya zamani kuwa hayana faida kama kumpata Yesu
Wafilipi 3:7 “Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu
kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote
kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana
wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa
kama mavi ili nipate Kristo;”
Unaweza kuona wako watu ambao wanadhani imani walizozirithi
zina faida kubwa sana kwao na hawataki kuachana nazo kwa sababu ni mila, kwa
sababu ndugu zao wote ni wa aina hiyo, hawataki kuziachia wakidhani kuwa yana
faida kwao, wako wenye kuabudu mizimu, wako wenye kushika dini Fulani na
desturi za aina Fulani, au imani zao zimewafikisha mahali Fulani, labda
wamesomea maswala kadhaa katika imani zao, wana degree, wana phd, wana diploma
za aina mbalimbali, wana heshima, wana wivu kwaajili ya miungu yao,
wanaheshimika katika dini zao, wamepewa vyeo ni wazee wa kanisa, wamehiji maeneo
matakatifu wako karibu na viongozi wakubwa wa kidini wanaamini kuwa wamewekeza kwa faida na
kiwango kikubwa sana katika dini zao, vyovyote vile iwavyo Paulo mtume
alipobaini kuwa Yesu, analipa aliachana na kila kitu na kuyahesabu yote kuwa ni
hasara na kuwa faida kubwa ni kumpata
Yesu!
Paulo mtume alikuwa amejifunza ya
kuwa hakuna mtu anaweza kuokolewa kwa matendo yake mema au sifa zake za zamani,
Mungu hatuhesabii haki kwa sababu ya wema na matendo mazuri tuliyoyafanya
katika dini zetu
Warumi 3:20-24 “kwa sababu hakuna mwenye
mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua
dhambi huja kwa njia ya sheria. Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo
sheria; inashuhudiwa na torati na manabii; ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya
imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti; kwa sababu
wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki
bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu;”
Tunaishi katika ulimwengu wa
pongezi, na wengi wanadhani kwa kufanya vizuri wanaweza kukubalika kwa Mungu na
wanadamu pia lakini ukweli unabaki palepale kwamba mafanikio ya kiroho
yanapatikana kwa kumuamini Yesu tu, tunapofanya mema tukumbuke maelekezo ya
Yesu ya kuwa tumefanya tu yatupasayo kufanywa, Luka 17:10 “Vivyo hivyo nanyi,
mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na
faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya.” Kutumainia lolote nje ya
Yesu Kristo ni kutumainia hasara.
2.
Mila
na desturi za baba zetu.
Jambo linguine
kubwa litakalowatesa wengi na kuwapeleka Motoni ni kushika mila na desturi za
baba zao au babu zao, Jambo hili vilevile liliwaathiri wayahudi, walidhani ya
kuwa wanaweza kuokolewa kupitia mila zao na hivyo walishika sana mila zao na
desturi kiasi cha kusahahu kujua Mungu anataka nini kwao kuna watu wengi sana
leo wanayashika mapokeo ya madhehebu yao, mila na desturi za wazee wao na
kuacha kuliangalia neno la Mungu kwa undani hii ilikuwa shida kubwa kwa wayahudi
wa kawaida na kwa Paulo Mtume pia
Mathayo 15:1-3 “Ndipo Mafarisayo na waandishi toka
Yerusalemu walipomwendea Yesu wakisema, Mbona wanafunzi wako huyahalifu mapokeo
ya wazee, kwa maana hawanawi mikono walapo chakula. Akajibu, akawaambia, Mbona
ninyi nanyi huihalifu amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu? ” Yesu
alikemea vikali sana na kuiita tabia hii kuwa ni ya kinafiki alionya vikali
kutokuhubiri neno la Mungu na kuhubiri mila na desturi ambayo kwa lugha
nyingine aliyaita maagizo ya wanadamu au mapokeo ya wanadamu ona Mathayo 15:7-9 “Enyi
wanafiki, ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema, Watu hawa
huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure,
Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu” Nabii Yohana
aliwaonya vikali na mapema wayahudi kuwa kujifikiri ya kuwa wanaye baba ndiye
Ibrahimu bila kufungua mioyo yao na kumpokea masihi kwa imani ona Mathayo 3:7-10 “Hata
alipoona wengi miongoni mwa Mafarisayo na Masadukayo wakiujia ubatizo wake,
aliwaambia, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira
itakayokuja? Basi zaeni matunda yapasayo toba; wala msiwaze mioyoni mwenu
kwamba, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba Mungu aweza
katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto. Na shoka limekwisha kuwekwa penye
mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.”
Swala la mila na desturi lilisumbua mno nyakati za kanisa la kwanza na
linasumbua hata leo, watu wengi wameacha kweli ya neno la Mungu na
wanasumbuliwa na mafundisho na mapokeo ya wanadamu na hivyo wanaweza kujikuta
kuwa wanapata hasara kwa kufuata desturi za kidhehebu, kimila na taratibu
zilizowekwa na wanadamu, Paulo aliyashika sana mapokeo ya baba zake ona Wagalatia 1:14 “Nami
naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika
kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu.”
Hata hivyo baada ya kumjua Kristo aliliasa kanisa kuachana na aina hii ya Elimu
yenye kupotosha ambayo kismingi sio neno la Kristo Wakolosai 2:8 “Angalieni mtu asiwafanye
mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya
wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya
Kristo.” Ukristo utakuwa na nguvu kubwa sana kama watu wataacha
mapokeo ya kujifunza kulishika neno la Mungu ambalo kimsingi ni kumjua Yesu
Kristo jambo hili ndio lenye faida kubwa sana kuliko tunavyoweza kufikiri.
Faida kubwa iko katika kumjua Yesu Kristo
Tangu nyakati za nabii Yeremia
maandiko yalionyesha kuwa jambo lanye faida kubwa na la kujivunia ni kumjua
Yesu, Mungu anataka tujivunie kumjua yeye zaidi ya kitu kingine chochote!
Yeremia 9:23-24 “Bwana asema hivi, Mwenye
hekima asijisifu kwa sababu ya hekima yake, wala mwenye nguvu asijisifu kwa
sababu ya nguvu zake, wala tajiri asijisifu kwa sababu ya utajiri wake; bali
ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi, na kunijua, ya
kuwa mimi ni Bwana, nitendaye wema, na hukumu, na haki, katika nchi; maana mimi
napendezwa na mambo hayo, asema Bwana,”
Paulo anaiona faida kwa kumjua
Yesu Kristo Wafilipi 3:8 “Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara
kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa
ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate
Kristo;”
Hili ndio jambo lenye faida kubwa
mno, kumjua Yesu, kuwa na uhusiano naye na zaidi sana hata kutamani kwenda
kukaa naye milele na milele Wafilipi
3:9-10 “tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki
yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo
katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani; ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika
wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake;” Kumjua Yesu kristo
kuna faida kubwa sana, kumjua yeye kunaaanza na kusoma habari zake, ili
tuziamini na kwa kumuamini yeye tunakuwa na uzima tena uzima wa milele ona Yohana 20:30-31 “Basi
kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake,
zisizoandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini ya
kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina
lake”
Muhimu
Wafilipi 3:10-11 “ili nimjue yeye, na uweza
wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake;
ili nipate kwa njia yo yote kuifikia kiyama ya wafu.”
Kuna mambo mengi ambayo
tungependa kuyajua duniani kwa sababu tunataka kuitawala dunia,na kuyajua
mazingira yetu ya sasa na kukabiliana na changamoto za ulimwengi huu kila mmoja
ana mengi ambayo kwayo anaweza kuyaona kuwa yana faida nyingisana, hata katika
maisha tunatoa kipaumbele kwa mambo tunayodhani na kufikiri kuwa ni ya Muhimu
na yana faida kubwa sana kama ilivyiokuwa kwa Paulo mtume hata hivyo tunapaswa
kumuelewa kuwa kwa nini alitamani sana kumuona Kristo Paulo alikuwa na uelelewa
kuwa kumjua Yesu Kristo lilikuwa jambo lenye faida pan asana na hivyo
aliyahesabu mabo mengine yote kuwa ni hasara na kuyafafnanisha na mavi, ili
kumpata Kristo
Rev. Innocent Samuel Kamote
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni