Isaya 63:9-10 “Katika mateso yao yote yeye aliteswa, na malaika wa uso
wake akawaokoa; kwa mapenzi yake, na huruma zake, aliwakomboa mwenyewe;
akawainua, akawachukua siku zote za kale. Lakini wakaasi, wakamhuzunisha Roho
yake Mtakatifu; kwa hiyo akawageukia, akawa adui, akapigana nao.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu
wetu ni mwingi wa rehema huruma na neema, Sifa za Mungu wetu kamwe haziwezi
kulinganishwa na mwingine awaye yote, Musa alipotaka kumjua Mungu Mungu
alijifunua kwake kwa sifa nzuri zenye kuwavutia sana wanadamu zinazoashiria
kuwa Mungu ni mwema mno ona
Kutoka 34:6-7 “BWANA akapita mbele yake,
akatangaza, BWANA, BWANA, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa
hasira, mwingi wa rehema na kweli; mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu,
mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu
kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao, na wana wa
wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne.”
Unaona tunamwabudu na kumtumikia
Mungu mwenye huruma nyingi, mwenye fadhili, na si mwepesi wa Hasira mwingi wa
rehema na kweli nani mwenye kuonea watu huruma hii ni sifa kubwa sana ya Mungu
aliye baba na muumba kwetu sifa hii na tabia hii ya uungu iko kwa Mungu etu
ambaye amejifunua kwetu kama Baba, mwana na Roho Mtakatifu, yeye ni mwingi wa
huruma kama maandiko yanenavyo
Zaburi 145:7-9 “Watalihubiri kumbukumbu la
wema wako mkuu. Wataiimba haki yako. Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, Si
mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, Bwana ni mwema kwa watu wote, Na rehema
zake zi juu ya kazi zake zote.”
Hata hivyo pamoja na wingi huu wa
rehema na neema na huruma za Mungu wetu, ni ukweli ulio wazi kwamba maandiko
yanatuonya sana sana sana kutokumkosea ROHO
MTAKATIFU Onyo hili limerudiwa tena na tena kama tahadhari kubwa sana
katika maandiko ya kwamba katika maisha yetu kama mtunataka kufurahia neema ya
Mungu na uwepo wake basi katika ufunuo wa Mungu wetu hasa kuhusiana na ROHO MTAKATIFU tunaonywa sana kutokumfanyia
dhambi au kasirani ROHO MTAKATIFU
hii maana yake ni nini maana yake mtu anaweza kutengeneza uadui na Roho
Mtakatifu na akajikuta yuko matatani. Katika
nafsi hizi tatu kwa mujibu wa mafundisho ya Yesu mwenyewe tunaweza kumkosea
Mungu baba na Mwana pia na mlango wa neema ukapatikana lakini tahadhari kubwa
inatolewa kuhusu kumkosea ROHO
MTAKATIFU.
Mathayo 12:31-32 “Kwa sababu hiyo
nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa
kumkufuru Roho hawatasamehewa. Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya Mwana
wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu
hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao.”
Unaona maneno hayo ni maneno ya
Bwana wetu Yesu Kristo ambaye anatuonya sana namna ya kujihadhari ili tusiweze
kuwa na uadui na Roho Mtakatifu kwani tunaweza kujikuta katika wakati
Mgumu hii maana yake ni nini maana yake
tunaweza kujikuta tunamtenda dhambi Mungu Roho Mtakatifu na akageuka na kuwa
adui yetu na kupigana nasi!
Namna ya kutengeneza uadui na Roho Mtakatifu.
Taasisi nyingi leo zinazomtaja
Mungu, na zilizokuwa na nguvu sana duniani zilianza kupoteza umaarufu wake mara
baada ya kuanza kupingana na kazi za Roho Mtakatifu na kufanikiwa kutengeneza
uadui naye, ni jambo la kusikitisha kwamba katika nchi nyingi za ulaya na
ikiwemo Uingereza makanisa mengi sana yaliyokuwa taasisi kubwa yamebakiwa na
majengo ambayo mengine yamenunuliwa na kuwa misikiti au kuwa maduka au majumba
ya makumbusho na pia kuwa makasino lakini ukichunguza kwa kina chanzo kikubwa
cha kufikia hatua hiyo ni kupoteza uamsho na kufikia ngazi ya kufanikiwa kuwa
na uadui na Roho Mtakatifu! Uwepo wa Roho Mtakatifu una nafasi kubwa sana
katika maisha yetu na mafanikio yetu ya kimwili na kiroho hata hivyo hatuna
budi kuzingatia tahadhari zilizotolewa na Mungu kwa neno lake kuhusu Mungu Roho
Mtakatifu ni namna gani tunaweza kutengeneza uadui na Roho Mtakatifu
1. Angalieni msimtie Kasirani - kumtia kasirani maana yake ni kumuudhi kwa
sababu ya manunguniko na malalamiko na kutokuamini, wakati tunapokuwa
tumeokolewa hatuna budi kufahamu kuwa ni kazi ya roho Mtakatifu kutuongoza na
kutusaidia yeye ni msaada ulio karibu sana anafanya kazi katika kiwango kile
kile ambacho angekifanya Kristo akiwa katikati yetu yeye huitwa msaidizi Yohana 14:16 – 18 “Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi
mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu
hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua,
maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. Sitawaacha ninyi yatima; naja
kwenu.”
Unaona Mpango
wake Mungu ni kuwa pamoja nasi, Pamoja na kuwa Yesu alipaa Mbinguni lakini
hakutuacha yatima ametuletea Msaidizi yaani Roho Wake mtakatifu ili akae nasi
ni rafiki wa karibu na ni kiongozi wetu hivyo hatupaswi kumtia kasirani ona
Kutoka 23:20-22 “Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele
yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea.
Jitunzeni mbele yake, mwisikize sauti yake; wala msimtie kasirani; maana,
hatawasamehe makosa yenu; kwa kuwa jina langu limo ndani yake. Lakini
ukiisikiza sauti yake kweli, na kuyatenda yote ninenayo mimi; ndipo mimi
nitakuwa ni adui wa adui zako, na mtesi wa hao wakutesao.”
Ni muhimu
kufahamu kuwa malaika anayetajwa hapa na Bwana kwamba atawaongoza wana wa
Israel na kuwa wajihadhari wasimtie Kasirani ni ROHO MTAKATIFU Yeye katika agano la kale anaitwa malaika wa uso
wake kama unavyoweza kuona katika andiko la Msingi
Isaya 63:9-10 “Katika mateso yao yote yeye aliteswa, na
malaika wa uso wake akawaokoa; kwa mapenzi yake, na huruma zake, aliwakomboa
mwenyewe; akawainua, akawachukua siku zote za kale. Lakini wakaasi,
wakamhuzunisha Roho yake Mtakatifu; kwa hiyo akawageukia, akawa adui, akapigana
nao.”
Unaweza kuona
maonyo ya kibiblia kwamba tunaweza kumkosea ROHO MTAKATIFU kwa kumtia kasirani na hatimaye akageuka na kuwa
adui na kupigana nasi, haya yalifanywa na wana wa Israel walipookolewa kutoka
Misri lakini njiani mara kwa mara walimkosea Mungu Roho Mtakatifu kwa kufanya
maovu ambayo yaliwafanya waangamizwe jangwani
ona
1Wakoritho 10:1-11 “Kwa maana,
ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya
wingu; wote wakapita kati ya bahari; wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu
na katika bahari; wote wakala chakula kile kile cha roho; wote wakanywa
kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata;
na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. Lakini wengi sana katika wao, Mungu
hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani. Basi mambo hayo yalikuwa mifano
kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani.
Wala msiwe waabudu sanamu, kama wengine wao walivyokuwa; kama ilivyoandikwa,
Watu waliketi kula na kunywa, kisha wakasimama wacheze. Wala msifanye
uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu ishirini na
tatu elfu. Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu,
wakaharibiwa na nyoka. Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika,
wakaharibiwa na mharabu. Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa
ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani”
Unaona? Wana wa
Israel kwa rehema na huruma za Mungu waliokolewa kutoka utumwani Misri kwa nia
nzuri ya upendo wa Mungu ili kusudi awapeleke katika nchi ya mkanaani akawape
raha na maziwa na asali na kila walichokitamani, hata hivyo katika namna ya
kushangaza sana utaweza kuona walimuhuzunisha Mungu na kumtia kasirani Roho wa
Mungu na hatimaye wakaangamizwa jangwani.
Ni kwa sababu ya
somo hili Paulo mtume anasema mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano ili
kutuonya sisi tuliofikiwa na miisho ya zamani hizi yaani zamani hizi ni zama
hizi ambapo ROHO MTAKATIFU Yuko
kazini hapa duniani akifanya kazi pamoja nasi, kwa msingi huo basi kanisa au
taasisi yoyote inayomtaja Mungu kama haitajali kutunza uwepo wa ROHO MTAKATIFU kwa heshima kubwa ni
ukweli ulio wazi kuwa tutakuwa na uadui naye!
2. Wala Msimuhuzunishe - Namna nyingine
ambayo tunaweza kujenga uadui na Roho Mtakatifu ni Pamoja na kumuhuzunisha ona Waefeso 4:30 “Wala
msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata
siku ya ukombozi.” Kumuhuzunisha ROHO MTAKATIFU huambatana na kumkasirisha neno la kiyunani linalotumika kuhusiana na
kumuhuzunisha ROHO MTAKATIFU Katika
kiyunani ni LYPEITE Kwa kiingereza
ni Cause Grief Ambalo maana yake ni
kumsababishia MAJONZI hili ni wimbi
zito la masikitiko na kukasirishwa kunakotokana na kupingwa kunakosababishwa na
ugumu wa mioyo ya watu kwa makusudi jambo la namna hii lilimtokea Masihi pale
watu walipiokuwa wanataka asiponye mtu kwa sababu ni siku ya sabato Marko 3:4-5 “Akawauliza,
Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya? Kuponya roho au
kuiua? Wakanyamaza. Akawakazia macho pande zote kwa hasira, akiona huzuni kwa
ajili ya ugumu wa mioyo yao, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Naye
akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena.” Katika taasisi
mbalimbali na madhehebu mbalimbali ya Kikristo wakati mwingine wamekuweko watu
ambao kwa makusudi kabisa wanapinga na kazi za Roho Mtakatifu katika taasisi au
maisha ya mtu, wako watu wanaweza kupinga maombi, wanaweza kupinga uponyaji au
hata ustawi wa tabia njema iliyoko ndani ya Mtu ambayo imetokana na kazi za ROHO MTAKATIFU shughuli kama hizo
zinamuhuzunisha sana Mungu Pale katika Marko
5:6 ukisoma utaona viongozi wa dini sio tu walichukizwa na Yesu kuponya
siku ya sabato lakini vilevile walikuwa na makusudi ya kumuangamiza! Wako watu
pia wanaopinga na mahubiri, au muhubiri au kazi zinazofanywa na wahubiri wa
Injili, nimefanya kazi ya kichungaji
miaka 12, na kufundisha vyo vya Biblia miaka 12 na pia kuongoza taasisi ya
kielimu kwa shule ya seminari miaka 10 na mara kadhaa nimeona watu wakishindana
na ROHO MTAKATIFU wazi wazi na
wakati mwingine nilidhani wananichukia mimi jambo ambalo nimeshalizoea lakini
kumbe niligundua baadaye kuwa kazi ile ambayo Roho wa Mungu ameiweka ndani
yangu ilikuwa inapingwa vikali, sio hivyo tu mahali popote ambako watu wanaishi
kwa MANENO MAOVU, UCHUNGU, GHADHABU, HASIRA KELELE NA MATUKANO NA UBAYA WA KILA
NAMNA Hayo nayo hayo nayo ni sababu
kubwa ya kusababisha MAJONZI kwa ROHO
MTAKATIFU hili ndio tukio lililopelekea Paulo Mtume kuwataka Kanisa la
Efeso wawe mbali na maswala ya aina hiyo kwani ndiyo yanayopelekea kuhuzunika
kwa Majonzi kwa ROHO MTAKATIFU jambo
ambalo litapelekea aliache kanisa, aondoke au asifanye kazi tena na hapo uadui
nay eye huwa unaweza kufikia kikomo. Waefeso
4:29-31 “Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani
mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia.
Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri
hata siku ya ukombozi.Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano
yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya;”
3. Msimzimishe Roho – 1Wathesalonike 5:19 “Msimzimishe Roho;”
Ni muhimu kukumbuka kuwa katika
kumueleze ROHO MTAKATIFU moja ya alama zinazotumika keelezea
utendaji wa Roho Mtakatifu ni pamoja na MOTO,
wote tunaweza kuwa na ufahamu juu ya umuhimu wa Moto katika maisha ya
Mwanadamu, tunajua kuwa maendeleo makubwa ya mwanadamu yalichangiwa pia na
ugunduzi wa Moto, Roho wa Krito vilevile hufanya kazi kama Moto katika maisha
ya waaminio
Isaya 4:3-4 “Tena
itakuwa ya kwamba yeye aliyebaki katika Sayuni, na yeye aliyeachwa ndani ya
Yerusalemu, ataitwa mtakatifu; yaani, kila mmoja aliyeandikwa miongoni mwa hao
walio hai ndani ya Yerusalemu; hapo Bwana atakapokuwa ameuosha uchafu wa hao
binti za Sayuni na kuisafisha damu ya Yerusalemu kati yake, kwa roho ya hukumu
na kwa roho ya kuteketeza.”
Unaona maandiko yanatufundisha wazi kuwa
utendaji wa Roho Mtakatifu ni kama mfano wa Moto hufanya kazi ya kuichoma mioyo
yetu na kuteketeza yasiyofaa ndani yetu ili tuweze kuwa watakatifu, upendo wa
Mungu huwaka ndani yetu, upendo wa kuhubiri, kuabudukumtumikia Mungu kwa
uaminifu, kufanya maombi, kuwasaidia wengine moto huo wa kihuduma ndani yetu
huwashwa na ROHO MTAKATIFU tangu
anapokuja ndani yetu ona Matendo 2:3-4 “Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto
uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa
lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.”
Unaona hii ni
Ishara ya Roho wa Mungu kuwasha moto wa uamsho ndani yetu ili tumpende Mungu na
wenzetu, kwa msingi huo hatupasw kamwe kuuzima moto huo, Neno linalotumika
katika maneno ya kiyunani kuhusu
KUZIMA ni neno SBENNUMI – “sben-noo-mee”
kwa kiingereza to extinguish ambalo maana yake ni tendo endelevu la kuzima
moto, msimzimishe ROHO kanisa ua
taasisi au mtu binafsi anaweza kuendelea kuuzimisha moto wa Roho Mtakatifu kwa kukosa
furaha, kuacha kuomba, kuacha kushukuru, kupinga unabii, kupinga mapenzi ya
Mungu, kupinga mambo mema na kutokujitenga na uovu au ubaya wa kila namna haya
ndio mojawapo ya maswala yanayochangia kumzimisha ROHO WA BWANA ona 1Wathesalonike
5:14-22 “Ndugu, twawasihi, waonyeni wale wasiokaa
kwa utaratibu; watieni moyo walio dhaifu; watieni nguvu wanyonge; vumilieni na
watu wote. Angalieni mtu awaye yote asimlipe mwenziwe mabaya kwa mabaya; bali
siku zote lifuateni lililo jema, ninyi kwa ninyi na kwa watu wote. Furahini
siku zote; ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi
ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu. Msimzimishe Roho; msitweze unabii; jaribuni
mambo yote; lishikeni lililo jema; jitengeni na ubaya wa kila namna.” Unaona kwa mujibu wa maelezo na maonyo
ya Mtume Paulo matukio yote hayo yakifanyika kwa waamini na taasisi za kidini
tunamfanya Roho wa Mungu auzunike na kwa sababu hiyo tunatengeneza uadui na
Mungu nay eye atatutapika na matokeo yake taasisi au watu binafsi wanapoa ona
Ufunuo 3:13-22 “Yeye
aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Na kwa
malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye
Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu. Nayajua
matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa
baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto,
nitakutapika utoke katika kinywa changu. Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri,
nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na
mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi. Nakupa shauri, ununue kwangu
dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa,
aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate
kuona. Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.
Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua
mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. Yeye
ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi
nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi. Yeye
aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”
Unaona kwa
msingi huo kama watu watauzima moto wa Roho kwaajili ya sababu mbalimbali
tulizojifunza hapo juu ni ahadi ya ROHO
MTAKATIFU mwenyewe ya kuwa watatutapika, yeye hapenzi watu vuguvugu, yeye
anatutaka tutubu na kama hatutafanya hivyo hakuna kingine tunachoweza kuzawadiwa
bali tutapoteza Rehema na neema yake na kujikuta tumeunda uadui na Roho
Mtakatifu. Nisikilize Mungu habadiliki, tabia ya Mungu ni ileile sisi wanadamu
hubadilika Kabla ya gharika ya wakati wa Nuhu iliyofutilia mbali wanadamu wengi
na kumuacha Nuhu na familia yake wanadamu walitenda maovu, walijaa uovu
waliacha kumsikiliza ROHO MTAKATIFU
kwa kufanya uovu na kuwaza kufanya mabaya kila wakati hivyo walimuhuzunisha na
walimzimisha pia na walishindana naye
nadhani ni pale alipokuwa akiwashauri kuwa wema na wao wakapuuzia Mwanzo
6:3-6 “BWANA
akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni
nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini. Nao Wanefili walikuwako
duniani siku zile; tena, baada ya hayo, wana wa Mungu walipoingia kwa binti za
binadamu, wakazaa nao wana; hao ndiyo waliokuwa watu hodari zamani, watu wenye
sifa. BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila
kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote. BWANA akaghairi kwa kuwa amemfanya
mwanadamu duniani, akahuzunika moyo” unaona madhara watu
waliposhinda ana Roho ya Mungu, miaka ya kuishi mwanadamu ilipunguzwa, Mungu
aklijuta kumuumba mwanadamu, rehema zake na huruma zake zikafikia mpaka
akahuzunika akawafuta wanadamu, watu wanaopinga ana mapenzi ya Mungu, taasisi
zinazopigana na kusudi la Mungu, na watu wenye tabia endelevu ya kushinda ana
kazi ya Mungu kupitia roho Mtakatifu watapunguziwa maisha, watafutwa kwa sababu
wameamua kuwa adui wa Mungu
4.
Msimpinge
Roho Mtakatifu – Matendo 7:51-52 “Enyi wenye shingo
gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama
baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo. Ni yupi katika manabii ambaye
baba zenu hawakumwudhi? Nao waliwaua wale waliotabiri habari za kuja kwake yule
Mwenye Haki; ambaye ninyi sasa mmekuwa wasaliti wake, mkamwua;” Namna nyingine ya kuwa adui wa
Roho Mtakatifu ni kumpinga ni neno gumu na lenye kusikitisha sana kadiri
nilipokuwa naendelea kujifunza somo hili nilikuwa nawaza maoyoni hivi somo hili
ni sehemu ya INJILI kweli au kuwatisha watu? Lakini Roho Mtakatifu
akanikumbusha maeno ya BWANA YESU na
haya ya STEFANO kwa habari ya ROHO MTAKATIFU maonyo ya kucheza naye
hayana utani wala mchezo kabisa, hakuna mzaha linapokuja swala la kucheza na
Roho Mtakatifu lugha ya kimaandiko ni kali na ngumu na haina mzaha! Kumpinga
Roho Mtakatifu ni dhambi nyingine ambayo wanadamu wanaweza kumtendea Mungu
aidha walioamini au hata wasioamini maadamu tu utaingia kwenye anga zake na
kumpinga madhara yake yatakuhusu, Kumpinga Roho Mtakatifu katika lugha ya
kiyunani linatumika neno ANTIPIPTO ambalo
kiingereza chake ni resist au oppose kwa kuwa Roho Mtakatifu hawezi kuonekana
kwa macho ya kibinadamu
Yohana 14:16-17 “Nami
nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele;
ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala
haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.”
Sasa unawezaje
kumpinga yeye usiyemuona kwa macho, ukweli ni wazi kuwa kumpinga ROHO MTAKATIFU Huambatana na kuwapinga
watumishi wake, wale wanaobeba ujumbe wake NI YUPI KATIKA MANABII AMBAYE BABA ZENU
HAWAKUMWUUDHI Wayahudi walipinga ana Musa, walipinga ana manabii,
walimpinga yesu Kristo waliwapimga mitume na hata kuwaua walipinga maneno yale
na ujumbe ule ambao waliubeba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, Roho wa Mungu leo
anaweza kugeuka adui na akapigana nasi kama tu tunazuia kazi mzake na kupinga
ujumbe wake huku tukiwadharau na kuwapiga na kuwapinga watumishi wake na
kushindana na kazi yake hiki ndicho ambacho mafarisayo na Masadukayo
walikifanya na wayahudi wengi wenye wivu walishindana sana na wajumbe wa injili
hata wakitaka wasihubiri wala kumtaja Yesu ona
Matendo 4:1-10 “Hata
walipokuwa wakisema na watu wale, makuhani na akida wa hekalu na Masadukayo
wakawatokea, wakifadhaika sana kwa sababu wanawafundisha watu na kuhubiri
katika Yesu ufufuo wa wafu.Wakawakamata, wakawaweka gerezani hata asubuhi; kwa
kuwa imekwisha kuwa jioni. Lakini wengi katika hao waliosikia lile neno
waliamini; na hesabu ya watu waume ikawa kama elfu tano.Hata asubuhi wakubwa na
wazee na waandishi wakakusanyika Yerusalemu, na Anasi Kuhani Mkuu, na Kayafa
pia, na Yohana na Iskanda, na wote wale waliokuwa jamaa zake Kuhani
Mkuu.Walipowaweka katikati wakawauliza, Kwa nguvu gani na kwa jina la nani
ninyi mmefanya haya? Ndipo Petro, akijaa Roho Mtakatifu, akawaambia, Enyi
wakubwa wa watu na wazee wa Israeli, kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema
alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu
wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi
mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama
ali mzima mbele yenu.”
Matendo 5:14-39 “walioamini
wakazidi kuongezeka kwa Bwana, wengi, wanaume na wanawake; hata ikawa katika
njia kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka juu ya majamvi na magodoro, ili Petro
akija, ngawa kivuli chake kimwangukie mmojawapo wao. Nayo makutano ya watu wa
miji iliyoko kandokando ya Yerusalemu wakakutanika, wakileta wagonjwa, nao
walioudhiwa na pepo wachafu; nao wote wakaponywa. Akaondoka Kuhani Mkuu na wote
waliokuwa pamoja naye, (hao ndio walio wa madhehebu ya Masadukayo), wamejaa
wivu, wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza; lakini malaika wa Bwana
akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema, Enendeni mkasimame
hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya Uzima huu. Nao waliposikia wakaenda
alfajiri hekaluni, wakaanza kufundisha. Akaja Kuhani Mkuu nao waliokuwa pamoja
naye, wakawakutanisha watu wa baraza, na wazee wote wa wana wa Israeli, wakatuma
watu gerezani ili wawalete. Hata watumishi walipofika hawakuwaona gerezani,
wakarudi wakatoa habari, wakisema, Gereza tumeikuta imefungwa salama, nao
walinzi wamesimama mbele ya mlango; lakini tulipoufungua hatukukuta mtu
ndani. Basi jemadari wa hekalu na wakuu
wa makuhani waliposikia haya, wakaingiwa na shaka kwa ajili yao, litakuwaje
jambo hilo. Mtu mmoja akaja akawapasha habari ya kwamba, Watu wale mliowaweka
gerezani wako ndani ya hekalu, wamesimama wakiwafundisha watu. Ndipo yule
jemadari akaenda pamoja na watumishi, wakawaleta, lakini si kwa nguvu, kwa
maana waliogopa watu wasije wakawapiga kwa mawe. Walipowaleta, wakawaweka
katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza, akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa
nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu
mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu. Petro na mitume
wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Mungu wa baba zetu
alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti. Mtu huyo Mungu
amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba
na msamaha wa dhambi. Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu
ambaye Mungu amewapa wote wamtiio.Wao waliposikia wakachomwa mioyo yao;
wakafanya shauri kuwaua. Lakini mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamalieli,
mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza,
akaamuru mitume wawekwe nje kitambo kidogo, akawaambia, Enyi waume wa Israeli,
jihadharini jinsi mtakavyowatenda watu hawa. Kwa sababu kabla ya siku hizi
aliondoka Theuda, akijidai ya kuwa yeye ni mtu mkuu, watu wapata mia nne
wakashikamana naye; naye aliuawa na wote waliomsadiki wakatawanyika wakawa si
kitu. Baada ya mtu huyo aliondoka Yuda Mgalilaya, siku zile za kuandikiwa
orodha, akawavuta watu kadha wa kadha nyuma yake, naye pia akapotea na wote
waliomsadiki wakatawanyika. Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa, waacheni;
kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu, itavunjwa, lakini
ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na
Mungu.”
Wakati wote
unaposoma kitabu cha Matendo ya Mitume ambacho kimsingi ndio tunasoma kwa kina
na mapana na marefu utendaji wa Roho wa Mungu ndio utaweza kuona jinsi watu
kadha wa kadhaa walivyoweza kupinga ana kazi ya Mungu na wajumbe wa ile kazi na
hiki ndicho anachokikemea STEFANO na
kuwaonya wayahudi kwamba waache kumpinga ROHO
MTAKATIFU ikiwa ni pamoja na
kushupaza shingo zao. Kumpinga Roho Mtakatifu na kazi zake au watumishi wake
leo limekuwa moja wapo ya Dhambi inayopelekea Mungu kuwaacha watu wake Roho
Mtakatifu leo anapingwa sana na waliokoka na wasiookoka yako mashirika leo na
wako watu leo wamefilisika kiroho na wanafanya kila jitihana waweze kuinuka
tena lakini inashindikana sababu kubwa ni kupinga ana Roho wa Mungu, watu
wanapinga uamsho, wanapinga ujazo wa Roho, wanapinga miujiza, wanapinga wajumbe
wa Mungu, wanahakikisha kuwa mnakuwa na usumbufu na mnakosa utulivu ili mradi
tu kuharibu hali ya kiroho na injili. Ukitaka kuwa adui wa ROHO MTAKATIFU hakikisha kuwa unapinga anaye, yeye aliye na sikio
na alisikie neno hili.
5.
Usimwambie
uongo Roho Mtakatifu - Matendo 5:3-5 “Petro akasema,
Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na
kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja? Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali
yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako?
Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu,
bali Mungu. Anania aliposikia maneno haya akaanguka, akafa. Hofu nyingi
ikawapata watu wote walioyasikia haya.” Kumwambia uongo ROHO MTAKATIFU ni mojawapo
ya dhambi mbaya ambayo nyakati za kanisa la kwanza ilisababisha watu kufa mara
moja, lakini hata leo watu wanaweza kutengeneza uadui na ROHO WA MUNGU kwa mtindo unaofanana na Anania na Safira kimsingi
watu hawa walifanya unafiki, walikuwa wakiigiza jambo ambalo sio sahihi mbele
za Mungu kwanza tuichambue asili ya dhambi yao
Kulikuwa na
mpango wa watu kuishi kwa umoja na kwa pamoja na kwaajili ya kanisa watu wengi
walikuwa wakiuza mali zao na kukabidhi kwa mitume kwa kusudi la kuwasaidia
wengine moja ya watu waliofanya hayo na kupata umaarufu na sifa kubwa katika
kanisa ni Barnabas ona
Matendo 4:34-37 “Wala
hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye mahitaji; kwa sababu watu wote
waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile
vilivyouzwa,wakaiweka miguuni pa mitume; kila mtu akagawiwa kwa kadiri ya
alivyohitaji. Na Yusufu, aliyeitwa na mitume Barnaba, (maana yake, Mwana wa
faraja), Mlawi, asili yake ni mtu wa Kipro, alikuwa na shamba akaliuza,
akaileta fedha, akaiweka miguuni pa mitume.”
Nadhani ni
kutokana na watu kadhaa kusifiwa na mitume kwa moyo wao wa utoaji tayari Anania
na Safira nao walipata msukumo wa kufanya hivyo lakini nadhani wakiwa na nia ya
kujipatia sifa tu, kutoa mali zako na kuziuza kwaajili ya utoaji wa kanisa
halikuwa tatizo, na hata kuzuia sehemu ya fedha kwaajili ya familia haikuwa
tatizo, kama Petro Mtume alivyohoji
Matendo 5:4 “Kilipokuwa
kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake
haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako?
Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu.”
Swala kubwa
lilikuwa kumdanganya ROHO MTAKATIFU na
kumjaribu, Shetani alikuwa ameshamjaza Anania na mkewe nia ovu nia yao ilikuwa
ni kutaka sifa, kutoka katika jamii ya kanisa, wao waliwaambia mitume kuwa
wametoa vyote kumbe kuna ambacho walijifichia, walikuwa wakijaribu kuwadanganya
watu hasa wa jamii ya kanisa kumbe kiuhalisia walikuwa wakimdanganya ROHO MTAKATIFU ona
Matendo 5:3-5 “Petro
akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho
Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja? Kilipokuwa kwako,
hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa
katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia
uongo mwanadamu, bali Mungu. Anania aliposikia maneno haya akaanguka, akafa.
Hofu nyingi ikawapata watu wote walioyasikia haya.”
Mungu alikusudia
kanisa lake liwe kama mfano wake yeye aliyetuumba ni agizo la kibiblia kwamba
tuuvue kabisa utu wa kale na kuacha kabisa kuambiana uongo angalia Wakolosai 3:9-10 “Msiambiane
uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake; mkivaa utu
mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba.”
Leo hii sio
ajabu watu kuambiana uongo, kumekuwa na watu waogo na wadanganyaji kuliko
nyakati za kanisa la Kwanza, kumekuwa na wimbi kubwa la watu wanafiki na
wanaotaka sifa na kujijengea jina katika jamii kupitia umaarufu feki, vyovyote
iwavyo kusema uongo ni ishara iliyo wazi kuwa Ibulisi ambaye ni baba wa uongo
anatawala ona
Yohana 8:44 “Ninyi
ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye
alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo
kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye
ni mwongo, na baba wa huo.”
Kwa misingi hii
unaweza kuona ya kuwa kama unadanganya watu na kutaka sifa na kudanganya
watumishi wa Mungu ni wazi kuwa unatengeneza uadui na ROHO MTAKATIFU jambo ambalo litakugharimu.
6.
Kumfanyia
Jeuri Roho wa Neema – Waebrania 10:26-29 “Maana,
kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena
dhabihu kwa ajili ya dhambi; bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha, na
ukali wa moto ulio tayari kuwala wao wapingao.Mtu aliyeidharau sheria ya Musa
hufa pasipo huruma, kwa neno la mashahidi wawili au watatu. Mwaonaje?
Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na
kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, NA KUMFANYIA
JEURI ROHO WA NEEMA?” Nyakati za agano la kale mtu aliyeivunja
sharia ya Musa aliuawa pasipo huruma
Hesabu 15:30-35 “Lakini
mtu afanyaye neno lo lote kwa kusudi, kama ni mzalia, kama ni mgeni, huyo
amtukana Bwana; na mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake. Kwa sababu
amelidharau neno la Bwana, na kuyavunja maagizo yake; mtu huyo atakatiliwa
mbali, uovu wake utakuwa juu yake. Kisha wakati huo wana wa Israeli
walipokuwako jangwani, wakamwona mtu mmoja akikusanya kuni siku ya Sabato. Hao
waliomwona akikusanya kuni wakamleta kwa Musa na Haruni, na kwa mkutano wote.
Nao wakamweka kifungoni, maana, lilikuwa halijasemwa atakalotendwa. Bwana
akamwambia Musa, Mtu huyo lazima atauawa; mkutano wote watampiga kwa mawe huko
nje ya marago.”
Agano jipya ni
agano lililobora zaidi ya lile la agano la kale kama mtu angeliweza kuuawa
kwaajili ya kuvunja sharia katika agano la kale ni zaidi sana mtu anapoivunja
sharia ya kifalme katika agano jipya kama asemavyo mwandishi wa kitabu cha
Waebrania, Mwandishi anatoa maonyo makali sana kuhusiana na ukengeufu, kurudi
nyuma na kumkana Yesu Kristo jambo ambalo ni kinyume na utendaji mzima wa Roho
Mtakatifu ambaye hufanya kazi ya kuwapa watu neema ili watubu na kumuamini Yesu
kwa msingi huo mtu anapoifanya shingo yake kuwa ngumu na kutukana maswala
kadhaa ya wokovu na kuukana anajiweka kwenye uadui na Roho wa Kristo nani sawa
kabisa na kumfanyia Jeuri ROHO WA NEEMA
kwa msingi huo kufanya dhambi kusudi, kunaleta hukumu yenye kutisha kwa sababu
kufanya hivyo ni kumfanyia jeuri yeye.
7.
Kumkufuru
Roho Mtakatifu. – Kilele cha juu zaidi katika dhambi zinazoweza kumfanya
mtu kuwa na uadui na Roho Mtakatifu ni kumkufuru, neno Kukufuru katika lugha ya
Kiyunani linatumika neno Blasphemia – sawa na neno Blasyphemy katika kiingereza
ambalo maana yake ni kusema maneno mabaya au kuzungumza vibaya kuhusu Mungu,
jambo hili limezungumzwa na Bwana wetu Yesu Kristo Mwenyewe
Mathayo 12:31-32 “Kwa
sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa
wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa. Naye mtu ye yote atakayenena
neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho
Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao.”
Dhambi ya
kumkufuru Roho Mtakatifu ndio dhambi pekee ambayo haina msamaha kwa mujibu wa
maelekezo ya Yesu kristo, na ndio maana utaweza kuona kumekuweko na maonyo ya
kutosha kuhusu kuacha kutenda dhambi kinyume na mapenzi ya ROHO MTAKATIFU, ukimkufuru
Roho umefanya dhambi ya milele, kukufuru
ni hali ya kuzungumza mabaya, au kutukana na kuudhi maswala yote Matakatifu
yanayohusiana na Mungu Yesu alitoa maonyio ya namna hii katika mazingira ambayo
mafarisayo walikuwa wanapinga kazi zote za Mungu alizokuwa akizifanya hata
kufikia ngazi ya kutukana na kusema ya kuwa kazi hizo za kiungu zinafanywa na
shetani kupoitia Yesu ona
Mathayo 12:22-32 “Wakati
ule akaletewa mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu
akanena na kuona. Makutano wote wakashangaa,
wakasema, Huyu siye mwana wa Daudi? Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema,
Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo. Basi Yesu akijua mawazo yao,
akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena
mji au nyumba yo yote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama. Na Shetani
akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje?
Na mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, je! Wana wenu huwatoa kwa nani? Kwa sababu
hiyo hao ndio watakaowahukumu. Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi
ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. Ama awezaje mtu kuingia ndani ya nyumba ya
mtu mwenye nguvu na kuviteka vyombo vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye
nguvu? Ndipo atakapoiteka nyumba yake. Mtu asiye pamoja nami yu kinyume changu;
na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya. Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila
dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho
hawatasamehewa. Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa,
bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu
wa sasa, wala katika ule ujao.
Matendo na maneno
yote anayosemewa na kutendewa Roho Mtakatifu kilele chake kinakamilika katika
kumkufuru na hivyo kila wakati inapotokea anahuzunishwa, anazimishwa,
anaongopewa, anapingwa, anafanyiwa jeuri, anafanyiwa kasirani kielele chake ni
kuondoka, kuacha, kutokujishughulisha na ninyi tena na kutokusababisha moyo wa
toba utokee na hatimaye kusababisha kuhesabika kana kwamba umekufuruau
umemkufuru, Ndio maana leo tunaweza kuiona watu wengi, makanisa mengi na
taasisi nyingi zimechwa na ROHO WA BWANA
kwa sababu hawakuzingatia maswala kadhaa yanayimuhuzunisha Mungu ROHO MTAKATIFU na kumfikisha katika hatua ya kuondoka na
kwenda mbali nasi.
Hitimisho:
Kuondoka kwa Roho Mtakatifu
katika maisha yetu sio tu kunatutengenezea uadui naye lakini inshara ya
kuondoka kwa utukufu wa Mungu, mar azote maandiko yameeleza kuwa wanadamu
wamepungukiwa na utukufu wa Mungu mara baada ya kutenda dhambi Warumi 3:23 “kwa sababu wote
wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;” Utukufu wa
Mungu unakuwepo kwetu kwa ukamilifu wakati ambapo Roho wa Mungu akiwa hai ndani
yetu, akiwa anatenda kazi akiwa anatuongoza, ikiwa tunamsikiliza, lakini
tunaelezwa kuwa tunapomuasi anageuka anakuwa adui anapigigana nasi, kwa kuwa
Roho Mtakatifu ni Mungu ieleweke wazi kuwa nafsi hii katika utatu wa Mungu
inapokasirishwa na kufikia hatua ya kupigana nasi ujue hakuna mwamuzi tena
1Samuel 2:22-25. “Basi Eli alikuwa mzee
sana; naye alisikia habari za mambo yote ambayo wanawe waliwatenda Waisraeli;
na jinsi walivyolala na wanawake waliokuwa wakitumika mlangoni pa hema ya
kukutania. Akawaambia, Mbona mnatenda mambo kama hayo? Maana nasikia habari za
matendo yenu mabaya kwa watu hawa wote. Sivyo hivyo, wanangu, kwa maana habari
hii ninayoisikia si habari njema; mnawakosesha watu wa Bwana. Mtu mmoja
akimkosa mwenzake, Mungu atamhukumu; lakini mtu akimkosa Bwana, ni nani
atakayemtetea? Lakini hawakuisikia sauti ya baba yao, kwa sababu Bwana
amekusudia kuwaua.”
Inapofikia ngazi Mungu mwenye
rehema na neema nyingi mwingi wa huruma na asiye mwepesi wa Hasira anafikia
ngazi ya kumuua mtu ujue jambo hilo limekuwa machukizo makubwa kwa Mungu wetu,
unapokuwa na uadui na Mungu kinachofuata ni kifo na wakati huo huo Mungu
anaweza kuamua kukuacha na kuondoa utukufu wake hakuna jambo baya duniani kama
kupungukiwa na utukufu wa Mungu. Israel walipokuwa wamemtenda dhambi ukweli ni
kuwa utukufu wa Mungu ulikuwa ukiondoa hatua kwa hatua na hatimaye ukaenda
katika inchi ya mbali ona katika kitabu cha Ezekiel uwepo wa Mungu ulikuwa
ukiondoka taratibu kutoka katika patakatifu hata kwenye kizingiti, kutoka
kizingitini hata ukutani, kutoka ukutani hata mlimani na kutoka mlimani hata
ukaldayo katika nchi ya utumwa
Ezekiel 10: 4. “Utukufu wa BWANA ukapaa
kutoka kwa kerubi yule, ukasimama juu ya kizingiti cha nyumba; nayo nyumba
ikajazwa na lile wingu, na ua ulikuwa umejaa mwangaza wa utukufu wa BWANA.,”
Ezekiel 10:18-19. “Kisha huo utukufu wa
BWANA ukatoka pale juu ya kizingiti cha nyumba, ukasimama juu ya makerubi.Nao
makerubi wakainua mabawa yao, wakapaa juu kutoka katika dunia machoni pangu,
hapo walipotoka nje, nayo magurudumu yakawa kando yao; wakasimama mahali pa
kuingilia pa mlango wa upande wa mashariki wa nyumba ya BWANA; na utukufu wa
Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao.”
Ezekiel 11:23-25. “Utukufu wa BWANA ukapaa
juu toka katikati ya mji, ukasimama juu ya mlima wa upande wa mashariki wa mji.
Na roho hiyo ikaniinua, ikanichukua katika maono, kwa nguvu za roho ya Mungu,
hata Ukaldayo, kwa watu wale wa uhamisho. Basi maono niliyoyaona yakaniacha. Ndipo
nikawaambia watu wa uhamisho habari ya mambo yote aliyonionyesha BWANA.”
Kadiri watu wa Mungu wanapofanya
machukizo ya aina mbalimbali, Mungu huupunguza utukufu wake na kuondoka kidogo
kidogo utukufu wa Mungu ni sihara ya uwepo wa Mungu ni uwepo wa Roho wake
Mtakatifu, Israel walipotenda ya kuchukiza uwepo huo uliondoka na kwenda
utumwani Babeli na ndipo sa unapoweza kuona watu waliokuwa utumwani walikuwa na
nguvu na uwezo mkubwa sana wa Kiroho na Mungu alitukuzwa lakini Israel panyewe
pakabaki ukiwa, Mtu wa Mungu wewe ndio hekalu la Mungu je utukufu wa Mungu
umeondoka na kufikia ngazi gani kama utukufu umekuacha na kwenda Babeli huna
budi kulia na kutubu, Leo hii mtakapoisikia sauti yake msiifanye mioyo yenu
kuwa Migumu. Chunga sana hakuna jambo baya duniani kama kutengwa mbali na uso
wa Mungu hakuna jambo linatisha duniani kama kumuasi Roho Mtakatifu na kumuacha
akawa adui yetu na kupoigana nasi Bwana ampe neema kila mmoja wetu asiwe adui
wa ROHO MTAKATIFU KATIKA JINA LA YESU AMEN.
Na. Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima.