Ijumaa, 18 Novemba 2022

Fikirini Maua ya Mashamba!


Mathayo 6:28-32 “Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba? Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini?  Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.


Utangulizi:

Katika moja ya hutuba yake nzuri na ya muhimu maarufu iama hutuba ya Mlimani, Yesu Kristo anatumia mfano wa Ndege wa angani na Maua ya kondeni, kutengeneza hoja za kifikra akilini (logic of comparison) kuonyesha namna Mungu anavyowathamini wanadamu kuliko ndege wa angani na maua ya kondeni na kama Mungu anaweza kujali sana vitu hivyo vidogo mno katika uumbaji wake basi kwa hakika anawajali sana wanadamu ambao ni kilele cha uumbaji wake, na ambao ameutawaza juu ya kazi zake zote

Zaburi 8:4-8 “Mtu ni kitu gani hata umkumbuke, Na binadamu hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; Umemvika taji ya utukufu na heshima; Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake. Kondoo, na ng'ombe wote pia; Naam, na wanyama wa kondeni; Ndege wa angani, na samaki wa baharini; Na kila kipitacho njia za baharini.

Katika nyakati za leo wasomaji wengi wa neno wanaweza wasielewe au isiingie akilini kwanini Yesu alitumia mfano huu na je watu wa nyakati zake waliweza kumuelewa?

Kwanini maua ya mashamba?

Kal Vahomer ni kanuni ya siri ambayo Yesu aliitumia, Neno la kiibrania KAL VAHOMER ni neno linalohusiana na kanuni ya kiualimu iitwayo kutoka wazo dogo kwenda wazo kubwa au kutoka wazo rahisi kwenda wazo gumu From minor to the Major au from simple to Complex hii ilikuwa ni moja ya kanuni iliyotumiwa na walimu wengi wa nyakati ya karne ya kwanza, kulikuwa na kanuni kama saba walizotumia marabi wa kiyahudi kutafasiri maandiko au mafundisho na KAL VAHOMER ilikuwa ni mojawapo kutoka jambo dogo kulinganisha na jambo Kubwa, kama Mungu anajali maua je si zaidi au je hatazidi, mtondo huu pia Yesu aliutumia katika sehemu nyingine za mafundisho yake au maneno yake mfano

Luka 23:31  Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

unaona kwa msingi huo ujengaji wa hoja alioutumia Yesu hapo unafanana na ule ujengaji wa hoja alioufanya katika mfano wa maua ya kondeni, ikiwa wanautendea mti mbichi hivi, itakuwaje kwa mti mkavu?, yaani kama mwenye haki anatendewa mambo kama haya itakuwaje kwa mtu asiye haki? kwa hiyo hapa yesu tena alitumia kanuni ya ufundishaji iliyoitwa KAL VAHOMER ambayo ilikuwa imeenea wakati huo na ilikuwa ya Muhimu sana Kwa hiyo ilikuwa ni rahisi kwa jamii ya nyakati za karne ya kwanza kuweza kuelewa jambo hili.

Fikirini Maua ya Mashamba!

Kimsingi Yesu Kristo alikuwa anazungumza na kundi la watu wa chini sana waliokuwa masikini na hata kufikia ngazi ya kukosa mahitaji yao ya kila siku kama chakula na mavazi ambayo kimsingi ni mahitaji ya msingi sana ya mwanadamu, Kristo anataka kuwaondoa watu hawa katika mawazo ya kufikiri kuhusu chakula na mavazi na kutaka kuwatia moyo waache kuhofu kuhusu hayo na badakla yake wamtegemee Mungu, kuhofu au kuogopa ni ibada, kama mtu atakuwa anawaza ale nini au avae nini mawazo yake yataelekea katika kuitumikia fedha ili apate mahitaji yake, Yesu anataka tuwe na imani tuisjisumbue, anataka kutujengea uwezo wa kuamini  kwamba Mungu anatujali sana kama maua hayafanyo kazi yoyote na Mungu huyavika na kuyafanya yapendeze sana hata kuliko fahari ya Sulemani, ikiwa Mungu huyavika maua kwa fahari kubwa ingawa kimsingi hayana maisha marefu ukilinganisha na mwanadamu lakini maua hayaogopi na kama Mungu anaweza kuyafanyia hivyo maua hashindi kutufanyia sisi wanadamu mahitaji yetu Maandiko yanatufundisha ya kuwa Mungu anajishughulisha sana na mambo yetu

1Petro 5:6-7 “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu. 

Kimsingi umasikini hauko katika chakula mavazi tu Yesu alizungumzia hayo kutokana na hadhiranya watu wa wakati ule ambao wengi walikuwa masikini, inawezekana katika jamii ya leo tukawa chakula na nguo kwetu sio jambo la kuhofia lakini watu wanahofia kodi za nyumba, wanahofia ada za shule za watoto, wanahofia mikopo ya chuo, wanahofia marejesho ya vikoba, weanahofia magonjwa na changamoto mbalimbali, wanahofia kupanda kwa bei za bidhaa kama mafuta na vyakula, wanahofia mmomonyoko mkubwa wa maadili, ziko fedhea na mizigo ya aina nyingi sana ambayo inaumiza watu katika maisha haya haya yote tunapoyaleta kwa Mungu wetu ambaye anatujali sisi kuliko anavyojali maua na ndege wa angani uwezekano wa Mungu kukutana na mahitaji yetu na kutuondolea hofu ni mkubwa kuliko hofu yenyewe

Mathayo 11:28-30 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”

Yesu anataka tuiweke mbali hofu ya aina yoyote katika maisha anataka kutupa Pumziko yeye mwenyewe ameonyesha ya kuwa kuhofia hakuwezi kutuongezea kitu hakuwezi hata kuongeza lisaa limoja la uhai wetu Luka 12:25 “Na yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? unaiona kwa msingi huo maandiko yanatuonyesha ya kuwa tunapoogopa tunapokutana na hofu watakatifu waliotutangulia hata katika hali ngumu na duni na stresses za maisha wao bado  waliweka tumaini lao kwa Mungu

Zaburi 118:5-7 “Katika shida yangu nalimwita Bwana; Bwana akanijibu akaniweka panapo nafasi. Bwana yuko upande wangu, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? Bwana yuko upande wangu, msaidizi wangu, Kwa hiyo nitawaona wanaonichukia wameshindwa.”

Kwa msingi huo hatupaswi kuhofia jambo lingione lolote na badala yake tuaxchie kila kitu katika mahitaji yetu kijulikana na Mungu, Mungu anawalisha ndege wa anagali na kuyavisha maua mavazi ya rangi mbalimbali za kupendeza na hayafanyi kazi yoyote wala hayana maisha marefu lakini kama Mungu anaweza kuyajali kiasi kile ni wazi na upana ya kuwa Mungu anatujali sisi kuliko tunavyoweza kufikiri, kwa msingi huo kila amwaminiye Mungu hapaswi kuishi kwa hofu na wasiwasi tumwamini Mungu kwa mahitaji yetu yote ya kiwmili na kiroho naye atashughulika maua hayafanyi kazi lakini afadhali sisis tunafanya kazi na Mungu katika mapenzi yake tukimtegemea na kumuomba atatujibu sawasawa na kuhitaji kwetu kwa mapenzi yake

Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!     

Hakuna maoni: