Jumapili, 25 Desemba 2022

Kuokolewa katika mikono ya Herode!

 


Mathayo 2:12-16 “Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine. Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nalimwita mwanangu. Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi.”



Utangulizi.

Moja ya  wafalme aliyekuwa katili sana na mroho, mwenye tamaa na mbinafsi na muongo alikuwa ni mfalme Herode mkuu, kwa ujumla alikuwa ni mfalme mwenye kutisha sana, ni katili na muuaji aidha ni mwenye dhuluma, Huyu alikuwa tofauti sana na mfalme wetu Yesu Kristo, ambaye alikuja kwaajili ya ukombozi wa wanadamu, wakati Herode alikuwa na mpango wa kuangamiza na kuua, Mfalme Yesu alikuja na mpango wa wokovu, Herode alikuwa na mpango wa mateso, Yesu alikuja akileta matumaini na upendo, Herode alikuwa ni mkatili mwenye chuki na mwenye mpango wa kuangamiza, Kristo alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea tena alikuja ili watu wawe na uzima tena wawe nao tele, Katika wakati huu wa kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo hatuna budi vilevile katika wakati huu kujikumbusha Mambo ya msingi na ya muhimu yanayoyakabili maisha yetu na kisha kupata hekima ya kiungu namna ya kuokolewa katika mikon ya adui zetu.

Yesu alizaliwa wakati ambapo mfalme muovu na adui wa maisha yake alikuwa anatawala na mfalme huyu aliposikia habari kuwa Yesu Kristo amezaliwa ni ukweli ulio wazi kuwa badala ya kufurahi alifadhaika sana ona

Mathayo 2:1-3 “Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia. Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye.”

Mfalme Herode aliita baraza la wazee wa kiyahudi na wakuu wa makuhani na kufanya uchunguzi wa kina, na sio hivyo tu aliwahoji mamajusi na kutaka kujua kuwa ni kwa muda gani na wakati gani sahihi mtoto huyo atakuwa amezaliwa kufuatia mwenendo ya nyota waliyoiona nani wapi, na zaidi ya yote alitaka aletewe habari kamili kuhusu huyo mtoto kwa kusudi la kutaka kumuangamiza ona

Mathayo 2:4-8 “Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi? Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Uyahudi; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii, Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli. Kisha Herode akawaita wale mamajusi faraghani, akapata kwao hakika ya muda tangu ilipoonekana ile nyota. Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie.”

Ni muhimu kufahamu kuwa roho ya Herode inatenda kazi hata leo, katika ulimwengu wa kisiasa, makazini, duniani na hata makanisani, katika nyakati hizi za mwisho hatuna budi kuhakikisha kuwa wakati wote tunaendenda kwa hekima sana kwani hali halisi ya kiroho ya watu wengi imebadilika sana, wauaji wakubwa kabisa, wenye chuki, waharibifu, wabambikiaji, wasingiziaji, wenye siasa chafu, wachawi na watu wenye wivu wenye uchungu nyakati za leo hawako nje ya kanisa bali sasa wako ndani ya kanisa na hata madhabahuni, tunazungukwa na mbwa mwitu wakali huku wewe na mimi tukiwa kama kondoo tu, Bila kuweka tumaini letu kwa Mungu ni rahisi sana kujeruhiwa, kuumizwa na kutendewa kila aina ya ubaya na hata kuuawa kwa njia za ajabu au kuwekewa sumu, na watu ambao wala hatukuwahi kudhani kuwa wanaweza kuwa wasaliti na wenye kupingana na mpango wa Mungu katika maisha yetu, hali inatisha sana kwa sasa, watu wanatuma mpaka watu watushambulie, wako watumishi wa Mungu ambao sasa wamekuwa wachawi hata wokovu sijui waliuacha lini, wako washirikina pia hali inatisha hata hivyo Mungu aliye hai yuko macho na bila shaka atakuokoa na kila mpango mbaya wa ibilisi na maajenti wake katika maisha yako na yangu!

Herode alikuwa ni mtu wa namna gani?

Herode ambaye pia alijulikana kama Herode mkuu alikuwa ni mtawala wa Israel iliyokuwa chini ya utawala wa Warumi, Kimsingi yeye alizaliwa mwaka wa 72 kabla ya Kristo na kwa asili alitokea maeneo ya Idumeya yaani Eneo la Edomu wana wa Esau, Yeye na ukoo wake waliwekwa kuwa watawala vibaraka kwa niaba ya utawala wa warumi, Mwanzoni yeye alitawala Galilaya na uyahudi kabla ya utawala wa watoto wake watatu ambao waligawana majimbo baada ya kifo chake na Herode Akleo akatawala Idumeya, Uyahudi na Samaria na Herode Antipas alitawala Galilaya na Philip alitawaka huko Jordan, Kwa mujibu wa mwanahistoria maarufu wa kiyahudi wa  karne ya Kwanza Josephus, Herode mkuu alikuwa ni mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa sana ambaye ili kuongeza ushawishi wake alimuoa binti wa kuhani mkuu wa kiyahudi Kayafa na pia wakati wa utawala wake alilikarabati Hekalu la pili la Yerusalem na  kuliongezea eneo mlima wa Hekalu kwa upande wa kaskazini, Jambo lililopelekea yeye kukubalika na Wayahudi wengi.  Hata hivyo pamoja na umaarufu wake mkubwa hivyo ni jambo la kushangaza ya kuwa alipozaliwa Yesu Kristo Mfalme huyu alifadhaika na kugadhibika na ili aweze kujihakikishia usalama wake alihakikisha kuwa anawaua watoto wote wapatao miaka miwili kule Bethelehemu ili yamkini aweze kumuua Yesu Kristo ona

Mathayo 2:16 “Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi.”

Unaweza kuona Herode alikuwa ni mtu mwenye ghadhabu, mbinafsi na aliyekuwa hataki upinzani, alitamani kuwa yeye katika madaraka wakati wote, alitamani kuwa yeye abaki kuwa maarufu wakati wote, alikuwa mtu katili aliweza kuua watoto wote ili kujihakikishia usalama wake ni jambo la kusikitisha kuwa hii roho ya Herode ni roho inayotenda kazi katika nyakati zetu na katika kanisa la leo, Mara ngapi tumesikia viongozi wakubwa na maarufu wakiwaua wengine kisiasa na kuwachafua wengine kwa skendo za kutengeneza ili yamkini waweze kubakia wao tu madarakani, au wao tu waonekane kuwa ni safi na wenguine waonekane kuwa hawafai, au kuharibu umaarufu wa wengine  na wao tu waweze kuwa maarufu, hujawaona watu wenye kila kitu na wenye nguvu zote lakini wakifukuzana na watu masikini wasio na kitu wala nguvu yoyote wakitaka kuwazima ili yamkini wabakie wao tu hii ni roho chafu na mikono mibaya ya Herode, roho ya Herode ni roho ya watu wenye uchungu, hasira na tama mbaya wakiwa wamejawa na ubinafsi wa kila aina ni roho ya watu ambao hawawezi kufurahi nyota za wengine kung’aa lakini pamoja na hayo Bwana ana ujumbe muhimu leo Usiogope Bwana amenituma nikupe ujumbe huu kama nabii wake na kama malaika wake leo nakuletea habari njema ya kuwa wakati Herode anataka kusababisha misiba katika jamii, Mungu atakunusuru wewe na atakulinda na kukupa mlango wa kutokea mpaka atakapokufa Herode, Bwana atakuficha katika mikono yake nawe utakuwa salama hutaogopa madamu Mungu anakukubali, leo ziko habari njema kwaajili yako ona Yesu amezaliwa kwaajili yako na yeye ni mwokozi sio wa mtu mmoja tu wa ulimwengu mzima na hivyo amani inapaswa kutawala duniani kwa kila mtu ambaye Bwana ana mridhia najua wewe na mimi Bwana anaturidhia   

Luka 2:8-17 “Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku. Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang'aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng'ombe. Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema, Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia. Ikawa, malaika hao walipoondoka kwenda zao mbinguni, wale wachungaji waliambiana, Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu, tukalione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana. Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini. Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto.”

Kwaajili ya hayo ni imani yangu nani mpango wa Mungu ya kuwa pamoja na changamoto unazozipitia katika huduma, kazini ndoa na maeneo mengine Mungu hatimaye atatuokoa na mipango mikakakati ya heriode katika maisha yetu

Kuokolewa katika mikono ya Herode !

Mathayo 2:12-15 “Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine. Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize.  Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nalimwita mwanangu.”

Kila mtu mwenye mapenzi mema Mungu ana mpango mkakati ulio mwema na maisha yako na kwa jinsi Mungu alivyomwema anatuwazima mem, Mungu hana mpango wa kusababisha maombolezo katika maisha yetu wala hana malipizi anayotulipiza kwaajili ya maovu yetu, Mungu ni mwema mno yeye anatuwazia mema hana kisasi juu yetu yeye sio mwanadamu ana mpango mwema na mahususi kuliko mpango alionao Herode wako na wangu ona ;-

Yeremia 29:11-13 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote..”       

Vile adui zako na zangu wanavyotuwazia sivyo Mungu anavyotuwazia nataka kuanzia Christmas hii uweze kuelewa kuwa hakuna adui anayeweza kusimama mbele yako na kupingana au kushindana na mapenzi ya Mungu yaliyowekwa ndani yako, kila baya linalokusudiwa na adui dhidi yako Mungu ataligeuza kuwa Baraka, kila adui anayekutafuta akuangamize ataangamiza wengine na wewe utajikuta umefichwa; msomaji wangu nataka nikuhakikishie yakuwa ujumbe huu ni halisi katika maisha yako hakuna wa kukupata, hakuna atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako sio kwa Herode huyu tu lakini kwa kila mkono wa Herode yeyote atakayeinuka juu yako Mungu atakuokoa na mikono yake, wakati wa Petro alikuweko herode mwingine aliyaangamiza maisha ya Yakobo mtume na akataka kumuangamiza na Petro, lakini Mungu akawa mwaminifu akamfungua Petro kutoka katika mikono ya Herode Mungu huyu huyu atakufungua na wewe   atakuweka huru na Herode wako atatokwa na roho Hakuna herode aliyewafuatilia watu wa Mungu na kuwatesa na kuwaua ambaye  alibaki salama, Herode aliyetaka kumuua Yesu alikufa Yesu akiwa amefichwa Misri na herode aliyemuua Yakobo alipotaka kumuua Petro Mungu aklituma malaika wake ona

Matendo 12:1-23 “Panapo majira yale yale Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa. Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohana, kwa upanga. Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi akaendelea akamshika na Petro. Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa. Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka kumtoa na kumweka mbele ya watu. Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake. Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule ule Petro alikuwa analala katikati ya askari wawili, amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakailinda gereza. Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani, akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka mikononi. Malaika akamwambia, Jifunge, kavae viatu vyako. Akafanya hivyo. Kisha akamwambia, Jivike nguo yako, ukanifuate. Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua ya kuwa ni kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani kwamba anaona maono. Na walipopita lindo la kwanza na la pili, wakaja hata mlango wa chuma wa kuingilia mjini, ukawafungukia wenyewe. Wakatoka nje, wakapita katika njia moja; mara malaika akamwacha. Hata Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi. Na alipokuwa akifikiri haya akafika nyumbani kwa Mariamu, mamaye Yohana, ambaye jina lake la pili ni Marko; na watu wengi walikuwa wamekutana humo wakiomba. Naye alipobisha kilango cha lango, kijakazi, jina lake Roda, akaja kusikiliza.  Alipoitambua sauti ya Petro, hakukifungua lango, kwa ajili ya furaha, bali alipiga mbio, akaingia ndani akawaambia kwamba Petro anasimama mbele ya lango. Wakamwambia, Una wazimu. Lakini yeye akakaza sana, akasema ya kwamba ndivyo hivyo. Wakanena, Ni malaika wake. Petro akafuliza kugonga, hata walipokwisha kumfungulia wakamwona, wakastaajabu. Naye akawapungia mkono wanyamaze, akawaeleza jinsi Bwana alivyomtoa katika gereza. Akasema, Kampasheni Yakobo na wale ndugu habari hizi. Akaondoka, akaenda mahali pengine. Hata kulipopambauka askari wakaingiwa na fadhaa nyingi, amekuwaje Petro. Na Herode alipomtafuta, asimwone, aliwauliza-uliza wale walinzi, akaamuru wauawe. Kisha akatelemkia kutoka Uyahudi kwenda Kaisaria, akakaa huko. Naye Herode alikuwa amewakasirikia sana watu wa Tiro na Sidoni; wakamwendea kwa nia moja, na wakiisha kufanya urafiki na Blasto, mwenye kukitunza chumba cha mfalme cha kulalia, wakataka amani; kwa maana nchi yao ilipata riziki kwa nchi ya mfalme. Basi siku moja iliyoazimiwa, Herode akajivika mavazi ya kifalme, akaketi katika kiti cha enzi, akatoa hotuba mbele yao. Watu wakapiga kelele, wakisema, Ni sauti ya Mungu, si sauti ya mwanadamu. Mara malaika wa Bwana akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu utukufu; akaliwa na chango, akatokwa na roho.”

Hitimisho.

Ujumbe wangu wa Chrismas hii ni unabii, ni ujumbe ambao sio tu wa sikukuu hii lakini ni ujumbe wa maisha ya siku zote wote wanaoonewa na watu wenye nyadhifa zilizokubwa kupita wao wasiogope ni ujumbe wa matumaini na kukutia moyo ya kuwa Mungu yuko na anaifuatilia mipango ya Herode na ata shughulika naye ni ujumbe wa maonyo pia kama una roho ye herode lazima utubu na kubadilika Mungu hawezi kufurahia udhalimu, kusudi lake ni pana mno na yuko tayari kulilinda kusudi lake kwa gharama yeyote wewe sio wa Muhimu kuliko wanaochipukia uwe na roho ya malezi walee wengine na kuwainua na kuwaunga mkono usijidhanie ya kuwa uko mwenyewe au kuwa wewe ndiwe maalumu sana kwa Mungu, kujenga hekalu hakutakusaidia, kuoa mtoto wa kuhani mkuu hakutakusaidia, kuwa na wapelelezi hakutakusaidia, kuwa na jeshi hakukusaidiaa kitu Mungu wetu ni mwenye Nguvu na hekima yake ni kubwa kuliko hekima ya kibinadamu, hii ni Chrismas ya wokovu nani ya habari njema kwa wote wanaoonewa na maonyo  makali kwa waonevu! Kamwe asitokee mtu akashindana na kusudi la Mungu lililoko ndani yako kwani atapotea kama walivyopotea wakina herode na kusudi la Mungu ndilo litakalosimama.

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Maoni 1 :

Mkuu wa Wajenzi Mwenye Hekima alisema ...

Ukurasa huu umewekwa wakfu kwaajili ya Kuwaelekeza watu kwa Mungu ambaye ndiye msaada wetu mkuu, Maandiko yanasema Mungu kwetu sisi Ni kimbilio na Ngu vu msaada uonekanao tele wakati wa Mateso, hivyo kama yuko mwanadamu anatumia ukurasa huu, kujitangaza kuwa anaweza kuwasaidia wanadamu basi Mwanadamu huyo anamkufuru Mungu na ukurasa huu hautawajibika kwa mtu anayetegemea ushirikina badala ya kumtegemea Mungu, Maandiko yanasema amelaaniwa Mtu yule amtegemeaye mwanadamu na kumfanya kuwa kinga yake