Yohana 20:19-23 “Ikawa jioni, siku ile ya
kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya
Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye
akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale
wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana. Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe
kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha
kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote
mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi,
wamefungiwa.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa katika
ubinadamu wetu, mara kadhaa tunaweza kuwa na wakati wa amani na vilevile
tunaweza kuwa na wakati, tukapoteza amani na kuwa na mashaka kutokana na
majaribu ya aina mbalimbali na changamoto za aina mbalimbali tunazokutana nazo,
wakati mwingine tunaweza kujawa na hofu na mashaka hata kufikia kiwango cha
kujifungia, kwa woga na hofu huku tukiwa hatujui hatima yetu, ni katika hali ya
namna kama hiyo wanafunzi wa Yesu Kristo walikuwa na wakati mgumu sana wakati
Yesu alipokamatwa na kuteswa kwa kusulubiwa na kufa na kuzikwa, kulikuwa na
hali ya mashaka makubwa mno, huku taarifa za kufufuka kwake zikiwa bado
hazijathibitika kwa uwazi kwa wanafunzi wote, lakini vilevile Bado kulikuwa na
wasiwasi kama wayahudi watawaacha salama wanafunzi ama walianza na Kristo kisha
wamalizie kundi lake hivyo walipoteza matumaini kabisa! Na kukata tamaa! Wakiwa
katika hali kama hiyo maandiko yanasema Yesu akasimama katikati yao!, kumbe
Yesu anaposimama katikati hali inakuwa tofauti, huyu ni Yesu aliyefufuka mara
baada ya kusulubiwa na kufa na kuzikwa:-
o Yesu
akisimama katikati mahali ambapo watu wamepoteza tumaini, matumaini yanarejea
o Yesu
akisimama katikati mahali penye hofu hofu inaondoka
o Yesu
akisimama katikati mahali ambapo watu wamepoteza amani, amani inarejea
o Yesu
akisimama katikati mahali penye changamoto za aina mbalimbali, changamoto hizo
zinatoweka
o Yesu
akisimama katikati wakati watu wanapopata shida na kuingilia kati, shida hizo
zinaondoka
o Yesu
akisimama katikati anabadilisha hali ya mashaka na kuyaondoa kabisa, kwanini
Yesu husimama katikati ni kwa sababu
anajali na kuguswa sana na mahitaji yetu:-
Maandiko yanasema na tumtwike
yeye fadhaa zetu zote maana yeye hujishughulisha sana na mambo yetu,
1Petro 5:7” huku
mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo
yenu.”
Ni muhimu kukumbuka hili ya kuwa Mungu wetu ni Mungu muelewa
sana wakati mambo yanapoonekana kuwa ni yenye kuvunja moyo, yeye husimama
katikati na kubadilisha hali ya hewa, Tuna Mungu anayejali, na mambo huwa
tofauti wakati wote anapojitokeza, wakati
wa pasaka unapoadhimisha kufufuka kwa Yesu ni vema ukakumbuka kuwa Yesu
aliyefufuka ni wa tofauti yeye anauwezo wa kuibuka katikati ya shida yako na
kuyafanya mambo kuwa tofauti, Krito alipokuwa katika mwili alikuwa na tabia
hiyohiyo ya kuingilia kati na kubadili hali ya hewa pale mambo yanapoharibika
kwa wanadamu, Yesu anauwezo wa kubadilisha Msiba kuwa furaha, anauwezo wa
kuhahirisha mazishi na kurudisha furaha na amani iliyopotea ona:-
Luka 7:11-16 “Baadaye kidogo alikwenda
mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na
mkutano mkubwa. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti
anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini
wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia,
Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama.
Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza
kusema. Akampa mama yake. Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema,
Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake.”
Yesu anauwezo wa kutuliza dhoruba
ya aina yoyote itakayojitokeza katika maisha yetu na kutuondolea wasiwasi
Marko 4:36-41 “Wakauacha
mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine
vilikuwako pamoja naye. Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga
chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala
juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia?
Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma,
kukawa shwari kuu. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?
Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari
humtii? ”
Yesu aliweza kuyafanya hao
alipokuwa katika hali yake ya kawaida ya mwilini hapa duniani tena akiwa na
mipaka katika Israel, Lakini Yesu aliyefufuka hana mipaka na haitaji mlango
ufunguliwe yeye anauwezo wa kuingilia kati mahali popote pale na kufanya lolote
lile iwe mashariki au magharibi, kasikazini au kusini yeye anaposimama katikati
hubadilisha hali ya mambo:-
Yesu anaposimama katikati ya hali Fulani yeye anafanya nini kuna mambo
ya kujifunza kutoka katika kifungu hiki
1.
Anaonyesha
Makovu, unajua kwanini Yesu huonyesha makovu,? Mimi ninalo kovu Fulani
katika mkono wangu wa kushoto ambalo nililipata Tarehe 01/05/2000 kule Dodoma nilipokuwa naelekea chuo cha biblia,
nilivamiwa na majambaza zaidi ya nane na wakanikaba na kuniumiza kisha wakapora
kila nilichokuwa nacho wakati huo nilipopoteza fahamu kwaajili ya uvamizi ule,
kila ninapoliona lile kovu nakumbuka tukio lile na ninakumbuka namna Mungu
alivyoniokoa na mauti, lakini kama Haitoshi Tarehe 01/05/2015 Binti yangu wa kwanza Irene alizaliwa hivyo kwenye
Tarehe ile ambayo nilipaswa kukumbuka tukio baya sasa ninakumbuka tukio zuri la
kuzaliwa kwa binti yangu, kovu lile limekuwa historia, Yesu aliwaonyesha makovu
yake wanafunzi wake ili kwamba wajue kuwa mateso yake yamebaki historia tu,
Yesu amefufuka yu hai haijalishi aliumizwa kwa kiwango gani,
Yohana 20:20 “Naye
akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale
wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana.”
Mungu anajua
hali unayoipitia na Yesu aliyefufuka anakuthibitishia kuwa hali unayoipitia
itakuwa historia tu, Mungu atakufanyia muujiza mkubwa wa kupita kawaida kinyume
kabisa na matarajio ya maadui zako, watuoenee wanavyoweza kutuonea, watutese
wanavyoweza kututesa lakini hali yeyote unayoipitia sasa itakuwa Historia tu
unaweza usiwe na majeraha na makovukatika mwili wako lakini unaweza kuwa na
majeraha na makovu makubwa katika moyo wako, Yesu alityefufuka anapoonyesha
makovu namaanisha mashaka yako na mateso yako na majeraha yako atayabadili kuwa
historian a wewe utakuwa na kiwango kingine tunapoadhimisha kufufuka kwa Yesu
tukumbuke pia kuwa atatuonyesha makovu yake nah ii ni sihara ya kuwa mauti na
mateso na majeraha yetu yatabakia kuwa historia tu!.
2.
Anatangaza
Amani, Ni muhimu kufahamu kuwa Mstari wa 19 na wa 21 Yesu anasema Amani iwe
kwenu, hawa walikuwa wamepoteza amani, walikuwa na fadhaa, walikuwa na woga,
walikuwa na hofu, Yesu alikuwa amewaambia mapema kuwa anawapa amani na
akarudia tena amani iwe kwenu!, kwa nini alifanya alitangaza vile ni kwa sababu
alikuwa anataka kuwaondolea haki ya kuchanganyikiwa na hali ya hofu na woga
ambao uliwaondolea amani, kumbuka amani hii ni maalumu kutoka kwa Mungu
Yohana 14:27 “Amani
nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo.
Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.”
Amani itokayo
kwa Mungu ni zawadi ni tofauti na amani ya dunia hii neno la kiebrania
alilolitumia Yesu ni Shalom! Au Irene kwa kiyunani ambayo ni amani ya kipekee
itokayo kwa Mungu, amani hii huilinda mioyo yetu kwa kiwango cha hali ya juu
Paulo mtume anaiita amani hii kuwa inapita akili za kibinadamu amani hii
inauwezo wa kutulinda na kutuhifadhi!
Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue
kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na
kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili
zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”
Amani ipitayo
akili zote itatuhifadhi hii ni amani inayotumika kuhifadhi na kuilinda mioyo
yetu isijeruhiwe hali yoyote ya kuchanganyikiwa na kutokuelewa kwamba hali
itakuwaje hali hiyo na hofu hiyo inaondolewa na Yesu Kristo aliyefufuka,
wanafunzi walikuwa wamejifungia na hawajui itakuwaje, walikuwa
wamechanganyikiwa na hali ngumu ya kuuawa kwa Mwalimu wao kupitia mateso mazito
lakini zaidi na habari tata ya kwamba Yesu yuko hai au la au mwili wake umeibiwa
je amefufuka kwelikweli au hali ikoje? Kusimama katikati kwa Yesu kristo na
kuwatangazia amani kuliondoa mashaka yote, Yesu atatuondolea mashaka yote yanayotukabili
maishani.
3.
Yesu
anatupa Mamlaka, Yohana 20:22-23 “Naye akiisha
kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote
mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi,
wamefungiwa”.
Ni muhimu kufahamu kuwa Yesu anaposimama
katikati, hofu zetu, katikati ya mashaka yetu, katikati ya changamoto zetu,
katikati ya mateso yetu, katikati ya shida zetu, katikati ya vifungo vyetu,
katikati ya mashaka yetu, katikati ya masomo yetu katikati ya jambo lolote lile
maombi yetu yanajibiwa na kupata ufumbuzi lolote lile majibu ya maswali yetu
katika maisha, na Mungu anageuza kila
kitu kwa njia ya kutisha, anajibu maombi, anafanya kwa wakati wake, anatikisa,
anaweka huru anaokoa, anawezesha, anapatanisha anaweka mambo yote kuwa sawa,
anavunja magereza, na minyororo analainisha malango yanafunguka ana
anatetemesha na anaokoa!
Matendo 16:22-31 “Na walipokwisha kuwapiga
mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana.
Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga
miguu kwa mkatale. Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa
wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa
wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza
ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa.
Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza
imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia.
Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi
sote tupo hapa. Akataka taa ziletwe, akarukia ndani, akitetemeka kwa hofu,
akawaangukia Paulo na Sila; kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa
nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka
pamoja na nyumba yako.”
Namuomba Mungu asimame katikati
katika maisha yako na kuleta majibu ya maombi yako na kukutana na haja ya moyo
wako, wakati wote tunapopita katika changamoto za aina mbalimbali ni muhimu
kwetu tukakumbuka kuliitia jina la Bwana na kumtwika yeye fadhaa zetu zote,
naye ataingilia kati maisha yetu kwa kusimama katikati yetu na kutupa ufumbuzi
wa mahitaji yetu ! uongezewe neema
Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima