Jumatatu, 2 Mei 2022

Shika sana ulichonacho!


Ufunuo 3:10-12 “Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi. Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako. Yeye ashindaye, nitamfanya kuwa nguzo katika hekalu la Mungu wangu, wala hatatoka humo tena kabisa, nami nitaandika juu yake jina la Mungu wangu, na jina la mji wa Mungu wangu, huo Yerusalemu mpya, ushukao kutoka mbinguni kwa Mungu wangu, na jina langu mwenyewe, lile jipya.”


Utangulizi:

Wito unatolewa kwa kanisa na kila mwanadamu mmoja mmoja kushika sana au kwa lugha nyingine kutunza sana kile alichonacho, asije mtu akaitwaa taji yako, Hii ni kwa sababu kuja kwa Yesu kunakaribia, lakini sio hivyo tu kuna misukumo mingi sana duniani na nguvu kubwa ya upinzani ambayo iko kinyume na kile ambacho Mungu amekubarikia kwacho katika maisha haya, Yesu Kristo alikuwa akizungumza na kutoa ujumbe wake kwa makanisa saba yaliyokuwepo katika Asia ndogo huko uturuki, akiyaonya na kuwatia moyo katika maswala mbalimbali na hapa anazungumza na kanisa la Filadelfia ambalo kimsingi lilikuwa na mambo mazuri ukilinganisha na mengine na Yesu anawataka wajitunze, wawe makini ili wasije wakapoteza kile walicho nacho ambacho ni kizuri, kimsingi sina mpango wa kuzungumzia Makanisa yale saba,wala nyakati zile saba za historia ya kanisa kwani vyote vinaweza kutumika kuzungumza na kanisa, lakini Mpango wangu ni kuzungumza na wewe au na hata mimi mwenyewe, ya kwamba mara kadhaa Mungu ametubariki kwa mambo mengi mazuri, mfano, Kazi nzuri, Ndoa nzuri, kibali, mambo mema, vipawa, kujulikana, na kadhalika ziko zawadi nyingi na nafasi nyingi nzuri ambazo Mungu ametubarikia nazo katika maisha yetu lakini wengi wetu huwa tunajikuta nafasi zile, vipawa vile, zawadi zile na Baraka zile hatuna uwezo wa kuzitunza, au tunazipoteza kabisa hii ni kwa sababu shetani anavutiwa sana na kila jambo jema ambalo Mungu amewekeza katika maisha yetu na hivyo anakusudia kutuharibia, wakati mwingine tunapambana kufa na kupona na kumwaga jasho letu jingi kwaajili ya jambo Fulani lakini unapokuja wakati wa mavuno adui anakuja na kutuharibia na kuvuruga kabisa mpango wa Mungu katika maisha yetu, hapa ndipo mahali Yesu anatutaka tushike sana kile tulichonacho!  Hali mkama hii iliwasumbua sana Israel wakati wa waamuzi kabla Gideoni hajaitwa ona!;- 

Waamuzi 6:2-6,11 “Mkono wa Midiani ulikuwa na nguvu juu ya Israeli; tena kwa sababu ya Midiani wana wa Israeli walijifanyia hayo mashimo yaliyo milimani, na hayo mapango, na hizo ngome. Basi ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamepanda mashamba, Wamidiani wakakwea, na Waamaleki, na hao wana wa mashariki; wakakwea juu yao; wakapanga marago juu yao, na kuyaharibu hayo maongeo ya nchi, hata ufikapo Gaza, wala hawakuacha katika Israeli riziki ziwazo zote; kondoo, wala ng'ombe, wala punda. Kwa maana walikwea na ng'ombe zao na hema zao, wakaja mfano wa nzige kwa wingi; wao na ngamia zao pia walikuwa hawana hesabu; nao waliingia katika hiyo nchi ili kuiharibu. Israeli walitwezwa sana kwa sababu ya Wamidiani; nao wana wa Israeli wakamlilia Bwana. Malaika wa Bwana akaenda akaketi chini ya mwaloni uliokuwa katika Ofra, uliokuwa mali yake Yoashi, Mwabiezeri; na mwanawe Gideoni alikuwa akipepeta ngano ndani ya shinikizo, ili kuificha machoni pa Wamidiani.”

Unaona shetani atasubiri umetaabika sana na pale unapokuwa unatarajia kuwa utapumzika utagundua kuwa ndio kwanza vita inaanza upya na ni kama hakuna kulala na endapo utajisahau shetani atachukua mateka kila kitu na kukuacha ukiwa unalia na kulalamika wakati kilikuwa mikononi mwako na kiko kwenye uwezo wako!

o   Maana ya neno taji

o   Shika sana kile ulichonacho!

Maana ya neno taji:

Neno taji katika lugha ya kiyunani linasomeka kama neno “STEMMA” kwa kiibrania ni “TIARA” ambayo maana yake ni kwa kiingereza “Top”, au “Climax”, au “The highest” au “Uppermost point” au “surface of something”, au “Exeed”  kwa hivyo neno taji maana yake ni kilele cha ubora, ni ile hali ya kuwa juu, kama ni nyota kuwa na mwangaza mkubwa zaidi kuliko wengine, au hali ya kuwa na kitu cha ziada kinachozidi wengine, ni kilele cha furaha yako, kwa hiyo neno la Mungu linatuonya kutunza kile kilichobora ambacho Mungu ametupa kwa sababu adui yetu shetani hawezi kufurahia kile ulicho nacho au kile ambacho ndio shauku yako uweze kukifikia, Mungu anatutaka kutokudharau na kufikiri kuwa kile tulichonacho sio bora wakati kuna watu wanatamani ukipoteze ili wakipate, kwa msingi huo ni muhimu kufahamu kuwa tunapokuwa duniani tuko kwenye uwanja wa vita ambapo kuna mapambano ambapo, kile ulichonacho ambacho wewe unaweza kuwa huujali na wala haumshukuru Mungu ya kuwa unacho kuna wengine wanakitamani na watapigana wakipate kwa msingi huo lazima ujue namna ya kukitunza taji yako inaweza kuchukuliwa na akapewa mtu mwingine ona:-

2Samuel 12:29-31 “Basi Daudi akawakusanya watu wote akaenda Raba, akapigana nao, akautwaa. Kisha akamnyang'anya mfalme wao taji toka kichwani pake; na uzani wake ulikuwa talanta ya dhahabu, nayo ilikuwa na vito vya thamani ndani yake; akavikwa Daudi kichwani. Akazitoa nyara za huo mji, nyingi sana. Naye akawatoa watu waliokuwamo, akawaweka kwenye kazi ya misumeno, na sululu za chuma, na mashoka ya chuma, akawatumikisha, tanuuni mwa matofali ndivyo alivyoifanya miji yote ya wana wa Amoni. Kisha Daudi akarudi na watu wote Yerusalemu.”

Ni muhimu kukumbuka kuwa kile unachokitamani wewe kuna na wenzako wanakitamani na kama utakuwa dhaifu kuna watu watapita mbele yako na watakichukua, usifikiri kuwa kuna mtu atakubeba au kukuhurumia, hakuna wa kukubeba lazima wewe mwenyewe upambane, Mungu anaweza kuachilia Baraka Fulani, lakini ni jukumu letu sisi kulinda, ukitegemea wanadamu wakubebe kumbuka nao wana mahitaji yao watakuacha utasota sana watapita mbele yako na watachukua kile wewe unatamani kuwa nacho na kukuacha unalalamika tu

Yohana 5:2-7 “Na huko Yerusalemu penye mlango wa kondoo pana birika, iitwayo kwa Kiebrania Bethzatha, nayo ina matao matano. Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza, [wakingoja maji yachemke. Kwa maana kuna wakati ambapo malaika hushuka, akaingia katika ile birika, akayatibua maji. Basi yeye aliyeingia wa kwanza baada ya maji kutibuliwa, akapona ugonjwa wote uliokuwa umempata.] Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane. Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu.”

Wakati wote unaweza kuona kama kuna kitu unakitamani ni lazima uchukue hatua wewe mwenyewe na usisubiri mwanadamu aje akusaidie, lazima upambane kuhakikisha kuwa unafikia kilelelcha furaha yako au hakikisha kuwa unamuita Yesu na kumuomba akusaidie haja ya moyo wako!.

Mungu anapokuwa amekubariki kwa kitu Fulani adui wakati wote anavutiwa na kitu hicho, na atainuka kupigana na kitu ambacho Mungu anataka au amekufanyia, wakati wote adui  atakuja wakati mambo yanapokaribia kuwa mazuri, baada ya wewe kutaabika sana ndipo anapokuja kuteka na kumbuka wakati wote utakuwa mwenyewe ukipambana ukifanikiwa watu wengi sana watakuzunguka, ukifeli kila mmoja atakukimbia, watu hawatakushambulia kwa sababu uko kama wao watakushambulia kwa sababu una taji, una kitu cha ziada umewazidi, una mambo mazuri, una nyumba nzuri, una gari nzuri, una cheo kizuri, una mshahara mzuri, una mafanikio, una kibali, una mvuto, una mke mzuri, una mume mzuri, una kipato kizuri, unazalisha mazao, unafanya vizuri, au hata una umbo zuri, kaa duniani na usifanye lolote lile uone kama kuna atakayepambana na wewe, watu watakushambulia kwa sababu una mafanikio na Mungu ameweka mkono wake kwako kwa hiyo utapigwa vita ili uwaondokee hawataki uwe una ushuhuda wa Baraka za Mungu kwako!

Daniel 6:1-4 “Ilimpendeza Dario kuweka juu ya ufalme maliwali mia na ishirini, wawe juu ya ufalme wote; na juu yao akaweka wakubwa watatu, na Danieli alikuwa mmoja wao; ili maliwali hawa watoe hesabu kwao, mfalme asipate hasara. Basi Danieli huyo alipata sifa kuliko wakubwa na maliwali, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme akaazimu kumweka juu ya ufalme wote. Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake.”     

Unaona wakati wote unapokuwa na kitu cha ziada wewe ndio utakuwa unatafutwa, ili ushuhuda wa Mungu kuwa amekutendea mema uweze kupotea kwa sababu wengine watasikia na kumtukuza Mungu kwa yale ambayo Mungu amekufanyia sasa adui akufurahie kwa sababu gani? Shetani akufurahie wewe kwa lipi?

Shika sana ulichonacho!

Ni jukumu lako kuhakikisha kuwa wakati wote unapambana kulinda kile ambacho Mungu amekubariki kwacho, Baraka za Mungu katika maisha yetu zinavutia maadui hivyo wakati wote lazima ujifunze kujihami na kujilinda Yesu aliliambia kanisa la Filadelfia kuwa kwa kuwa umeishika sana subira yangu nani nitakulinda, ziko kanuni ambazo kwazo zinauwezo wa kutulinda

1.       Lazima tutumaini Mungu na kumtegemea yeye Zaburi ya 91:1-9 “Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi. Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini. Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo. Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao. Hutaogopa hofu ya usiku, Wala mshale urukao mchana, Wala tauni ipitayo gizani, Wala uele uharibuo adhuhuri, Ijapo watu elfu waanguka ubavuni pako. Naam, kumi elfu mkono wako wa kuume! Hata hivyo hautakukaribia wewe. Ila kwa macho yako utatazama, Na kuyaona malipo ya wasio haki.  Kwa kuwa Wewe Bwana ndiwe kimbilio langu; Umemfanya Aliye juu kuwa makao yako.”

 

2.       Uwe mwaminifu Daniel 6:16-22 “Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, wakamtupa katika tundu la simba. Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Mungu wako unayemtumikia daima, yeye atakuponya. Likaletwa jiwe, likawekwa mdomoni mwa lile tundu; naye mfalme akalitia muhuri kwa muhuri yake mwenyewe, na kwa muhuri ya wakuu wake, lisibadilike neno lo lote katika habari za Danieli. Kisha mfalme akaenda nyumbani kwake, akakesha usiku kucha, akafunga; na vinanda havikuletwa mbele yake; na usingizi wake ukampaa. Asubuhi mfalme akaondoka mapema, akaenda kwa haraka mpaka penye lile tundu la simba. Naye alipolikaribia lile tundu, akamlilia Danieli kwa sauti ya huzuni; mfalme akanena; akamwambia Danieli, Ee Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu wako, unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa? Ndipo Danieli akamwambia mfalme, Ee mfalme, uishi milele. Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno.”            

 

3.       Usikubali kupeleka ibada kwa mwanadamu, maandko yako wazi kuwa amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu na kumfanya mwanadamu kuwa kinga yake, wokovu wa kweli kwetu hautoki kwa mwanadamu mtumaini Mungu na kumtegemea yeye tu naye atakusaidia

 

Daniel 3:12-27 “Wako Wayahudi kadha wa kadha uliowaweka juu ya mambo ya wilaya ya Babeli, yaani, Shadraka, na Meshaki, na Abednego; watu hawa, Ee mfalme, hawakukujali wewe; hawaitumikii miungu yako, wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha. Basi Nebukadreza akatoa amri kwa hasira na ghadhabu, waletwe hao Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Basi wakawaleta watu hao mbele ya mfalme. Nebukadreza akajibu, akawaambia, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa makusudi hata hammtumikii mungu wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuru iwakayo moto; naye ni nani Mungu yule atakayewaokoa ninyi na mikono yangu? Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hamna haja kukujibu katika neno hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.Ndipo Nebukadreza akajaa ghadhabu, na sura ya uso wake ikabadilika juu ya Shadraka, na Meshaki, na Abednego, basi akatoa amri watie moto ile tanuru mara saba kuliko desturi yake ya kutiwa moto. Kisha akawaamuru baadhi ya watu mashujaa wa jeshi lake kuwafunga Shadraka, na Meshaki, na Abednego, na kuwatupa katika ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto. Basi watu hao wakafungwa, hali wamevaa suruali zao, na kanzu zao, na joho zao, na mavazi yao mengine, wakatupwa katikati ya ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto. Basi kwa sababu amri ya mfalme ilikuwa ni kali, na ile tanuru ilikuwa ina moto sana, mwako wa ule moto ukawaua wale watu waliowashika Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Na watu hao watatu, Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakaanguka, hali wamefungwa, katikati ya ile tanuru iliyokuwa inawaka moto. Ndipo Nebukadreza akastaajabu, akainuka kwa haraka; akanena, akawaambia mawaziri wake, Je! Hatukutupa watu watatu, hali wamefungwa, katikati ya moto? Wakajibu, wakamwambia mfalme, Kweli, Ee mfalme. Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu. Kisha Nebukadreza akaukaribia mdomo wa ile tanuru iliyokuwa inawaka moto. Akanena, akasema, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye juu, tokeni, mje huku. Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakatoka katika ule moto. Na maamiri, na manaibu, na maliwali, na mawaziri, waliokuwa wamekusanyika pamoja, wakawaona watu hao, ya kuwa ule moto ulikuwa hauna nguvu juu ya miili yao, wala nywele za vichwa vyao hazikuteketea, wala suruali zao hazikubadilika, wala harufu ya moto haikuwapata hata kidogo. Nebukadreza akanena, akasema, Na ahimidiwe Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego; aliyemtuma malaika wake, akawaokoa watumishi wake waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa miili yao ili wasimtumikie mungu mwingine, wala kumwabudu, ila Mungu wao wenyewe. Basi mimi naweka amri ya kuwa kila kabila ya watu, na kila taifa, na kila lugha, watakaonena neno lo lote lisilopasa juu ya huyo Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watakatwa vipande vipande, na nyumba zao zitafanywa jaa; kwa kuwa hakuna Mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.”



Hakikisha kuwa unafanya sehemu yako, unapambana, na Mungu atakusaidia, tambua ya kuwa una kitu cha ziada, na usisubiri mwanadamu akutetee, mtegemee Mungu mwangalie yeye, kumbuka ya kuwa una kitu cha ziada, usikubali kwa namna yoyote ile kupoteza ulichonacho kwa njia rahisi, Pambana kwa kumtegemea Mungu yeye aliyekuweka! Mshike Yesu tu yeye ndio msaada wetu mkubwa na anayeweza kutusaidia usiwategemee wanadamu.

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!


Hakuna maoni: