Jumapili, 22 Mei 2022

Kwa sababu hawawezi kuvumilia Baraka zako !


Mwanzo 26:12-22 “Isaka akapanda mbegu katika nchi ile, akapata mwaka ule vipimo mia kwa kimoja, BWANA akambariki. Na mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana. Akawa na mali ya kondoo, na mali ya ng'ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu. Na vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Ibrahimu babaye, Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza kifusi. Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi. Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko.  Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu; naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye. Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika. Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna. Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi.”


 

Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa katika ulimwengu tulionao ni watu wachache sana tena wenye ukomavu wa kifikra wanaoweza kustahimili pale mtu mwingine anapobarikiwa, na wako wengi wenye kushangaza katika upande wa pili ambao hawawezi kuvumilia pale Mungu anapokubariki, Baraka za Mungu kwetu zina tabia ya kuvutia umati mkubwa sana wa watu, lakini pia zinauwezo wa kuvutia maadui kwa upande mwingine, kwa msingi huo kila mmoja anapokuwa amebarikiwa na mbaraka wa Mungu na mbaraka huo ukamtajirisha ni lazima aelewe kuwa atakuwa na maadui na hawa ni wale ambao hawawezi kuvumilia Baraka zako na hivyo wakati mwingine tunaweza kujikuta tunavuna Baraka lakini tunapata na changamoto za Baraka hizo, kimsingi Mungu katika mapenzi yake kamili alikusudia kuwa Baraka zake zisilete huzuni iwayo yote ona Mithali 10:22 “Baraka ya Bwana hutajirisha, Wala hachanganyi huzuni nayo.”   Lakini kwa sababu tuko duniani wakati mwingine Baraka hizo zitaambatana na huzuni au udhia kutokana na watu wanaotuzunguka kushindwa kustahimili kishindo cha Baraka za Mungu kwetu, ni muhimu kufahamu kuwa watu wanaweza kushindwa kustahimili Baraka za Mungu kwetu katika mazingira yafuatayo-

1.       Wakati mwingine Mungu anapotutakabali.

Watu wengine wanaweza kushindwa kuvumilia Baraka zetu tunapotakabaliwa na Mungu, kutakabaliwa na Mungu katika lugha ya kiingereza ni “When God looked us with favor” ni tukio la kukubalika kiibada Mungu kukubali au kusikiliza maombi yetu na dua zetu, wengine wanachukizwa kwa nini huyu amesikilizwa na Mungu, kwanini huyu ameolewa mie bado, kwanini huyu amejenga mie bado, kwa nini huyu ana mashamba mimi bado, kwa nini huyu ana watoto mimi bado wako watu wanashindwa kuvumilia wanapoona Mungu amekutakabali, wanaweza kuona wivu, wanaweza kukukasirikia na wanaweza hata kukuua.

 

Mwanzo 4:1-8 “Adamu akamjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa BWANA.  Akaongeza akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi. Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. BWANA akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani] Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye,akamwua.”

 

Habili alipoteza maisha kwa sababu ya kutakabaliwa na Mungu, kaini alijawa na wivu wenye uchungu na kumkusudia nduguye mabaya, unaweza kukusudiwa mabaya, unaweza kupigwa vita kwa sababu una huduma nzuri, unaweza kupigwa vita kwa sababu unahubiri vizuri, kwa sababu unaimba vizuri, kwa sababu una sura nzuri, kwa sababu uko vizuri katika kila eneo kwa nini inafanyika hivyo ni kwa sababu wako watu hawawezi kuvumilia Baraka zako!

               

2.       Wakati mwingine tunapopata kibali kuliko wao.

 

Watu wengine wanaweza kushindwa kuvumilia Baraka zako kwa sababu tu unakibali, unakubalika kuliko wao, kwa sababu ya wao kujiona duni “inferiority complex” kutokana na kukubalika kwako wataanza kukuchukia na kukuonea wivu na hata kukupiga vita kwanini kwa sababu hawawezi kuvumilia Baraka zako ona

 

Mwanzo 37:3-5 “Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani. Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia;”

 

Ndugu zake Yusufu walipoona kuwa Yusufu anapendwa zaidikuliko wao, na baba yake amemnunulia nguo nzuri anapiga pamba kali kuliko wao,  wanabadilishana mawazo na mzee Yakobo, Yusufu anatoa taarifa kwa baba yake kuhusu kila kitu nyumbani jamaa wakahisi anapendelewa walishindwa kuvumilia Baraka hii ya kibali na wakazidi kumchukia sana, wako watu wanaweza kuchukizwa nawe kwa wazi au mioyoni mwao na wakawa wanaumia tu kwa sababu wewe unapendwa, kwa sababu wewe una kibali, una kibali kazini, unakibali kwa bosi, una kibali kikubwa na ni Mungu amesababisha kibali hicho na wanaokuzunguka wakashindwa kuvumilia Baraka zako na wanaanza kuchukizwa nawe na kukuonea wivu kwa sababu hawawezi kuvumilia Baraka zako!

 

3.       Wakati mwingine tunapopewa sifa zaidi kuliko wao

 

Watu wengine wanaweza kushindwa kuvumilia Baraka zako kwa sababu tu umesifiwa kuliko wao unaupiga mwingi katika jamii kuwazidi, unaposifiwa zaidi au sana kuliko wao, wao wanaaza kujiona duni na kupoteza kujiamini na hivyo wanaweza kukuonea wivu na kujenga uadui na kuanza kukupiga vita tangu waliposikia sifa zako kwanini watafanya hivyo kwa sababu hawawezi kuvumilia Baraka zako!

1Samuel 18:6-9 “Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile     

 

Unaona ni Daudi ambaye kwa nia njema alikuja kumpiga Goliath ambaye alikuwa ni adui wa taifa zima alisumbua ati kwa hiyo shujaa wa wafilisti alipigwa na Daudi ambaye ndani yake kulikuwa na upako wa kiungu ambao ulimwezesha kuwatetea wana wa Israel na jina la Mungu likatukuzwa watu walipomsifu tayari Sauli alimuonea wivu na kuanza uadui na Daudi, wako watu wanaweza kuanzisha uadui na wewe na wakakuchukia na kukupiga vita lakini sababu kubwa ni kuwa hawawezi kuvumilia Baraka zako!, angalia kuwa Sauli akimuwa mfalme na Daudi alikuwa mchunga kondoo tu, dunia ni yenye kushangaza kwa sababu wakati mwingine mtu mkubwa na mwenye nguvu kuliko wewe anakupiga vita wewe uliye mdogo kwa nini kwa sababu hawawezi kuvumilia Baraka zako!

 

4.       Wakati Mwingine tunapopandishwa Cheo.

 

Wako watu ambao wanaweza kushindwa kuvumilia Baraka zako kwa sababu eti wewe umekuwa mkubwa kuliko wao kwa sababu wewe una cheo kikubwa kuliko wao, unajua watu wanadhani cheo ni kuukata au kuuchinja au kuula, lakini Mungu huwa anatupa majukumu ili tuwatumikie watu hivyo kutokana na Baraka za kiungu Mungu anaweza kusababisha uinuliwe juu sana na ukawa na sifa njema lakini jambo la kushangaza ni kuwa wako watu hawataweza kustahimili kuinuliwa kwako na kwa sababu hiyo wataanza kupanga mikakati ya kibinadamu kabisa ili wakumalize kwa sababu hawawezi kuvumilia Baraka zako!

 

Daniel 6:1-5 “Ilimpendeza Dario kuweka juu ya ufalme maliwali mia na ishirini, wawe juu ya ufalme wote; na juu yao akaweka wakubwa watatu, na Danieli alikuwa mmoja wao; ili maliwali hawa watoe hesabu kwao, mfalme asipate hasara. Basi Danieli huyo alipata sifa kuliko wakubwa na maliwali, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme akaazimu kumweka juu ya ufalme wote. Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake. Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo, tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu wake.”

 

Unaona watu wanapata taabu sana kwa sababu una cheo na unaupiga mwingi katika mamlaka uliyo nayo kwa hiyo zinatafutwa sababu ili wakukamate, uweze kutiwa hatiani, Daniel alianza kutafutia namna hii iko kila mahali, iwe ni makazini, au makanisani, na kwenye taasisi mbalimbali kuna watu ni waroho wa Madaraka wanatafuta kila linalowezekana wakuangushe tu na hawajisikii vizuri wewe ukitamalaki! Kwa nini  kwa sababu hawawezi kuvumilia Baraka zako!

 

5.       Wakati mwingine kwa sababu unajenga.

 

Wako watu wengine kwa sababu wewe uko kwenye ujenzi unajenga basi wivu unawainuka na wanatamani kupingana na kile unachikifanya, wakati nakumbuka nilipokuwa najenga nyumba yangu, wachwi walikuja na kufanya uchawi wao wa kusotea huu ni uchawi wa kuhakikisha kuwa nyumba inadumaa na haiwezi kujengeka kama unaishia kwenye linta inakuwa ni kwenye linta tu, lakini mimi nilimtegemea Mungu hata baada ya wachawi kusotea na kuacha kinyesi kwenye nyumba ile, nilimuomba Mungu na ujenzi ukaenda kwa kasi sana na nikafanikiwa na ndipo wachawi walipokuja waziwazi na kugombana na mimi kwa hasira kali sana kwa nini kwa sababu hawawezi kuvumilia Baraka zangu, Nehemia alipokuwa anaujenga ukuta wa Yerusalem maadui wa wayahudi walitoa maneno ya kufuru kwa sababu Nehemia na wayahudi walikuwa kwenye ujenzi ona

 

Nehemia 4:1-8 “Lakini ikawa, Sanbalati aliposikia ya kwamba tulikuwa tukiujenga ukuta, akaghadhibika, akaingiwa na uchungu sana, akawadhihaki Wayahudi. Akanena mbele ya nduguze na mbele ya jeshi la Samaria, akisema, Wayahudi hawa wanyonge wanafanyaje? Je! Watajifanyizia boma? Watatoa dhabihu? Au watamaliza katika siku moja? Je! Watayafufua mawe katika chungu hizi za kifusi, nayo yameteketezwa kwa moto? Basi Tobia, Mwamoni, alikuwa karibu naye, akasema, Hata hiki wanachokijenga, angepanda mbweha, angeubomoa ukuta wao wa mawe. Sikia, Ee Mungu wetu; maana tunadharauliwa; ukawarudishie mashutumu yao juu ya vichwa vyao, ukawatoe watekwe katika nchi ya uhamisho; wala usiusitiri uovu wao, wala isifutwe dhambi yao, mbele zako; kwa maana wamekukasirisha mbele ya hao wanaojenga. Basi tukaujenga ukuta; nao ukuta wote ukaungamanishwa kiasi cha nusu ya kimo chake; maana watu walikuwa na moyo wa kufanya kazi. Lakini ikawa, Sanbalati, na Tobia, na Waarabu, na Waamoni, na Waashdodi, waliposikia ya kuwa kazi ya kuzitengeneza kuta za Yerusalemu inaendelea, na ya kuwa mahali palipobomoka panaanza kuzibwa, basi wakaghadhibika mno; wakafanya shauri wote pamoja kuja kupigana na Yerusalemu, na kufanya machafuko humo.”

 

Unaona kuna watu wanaweza kutoa maneno ya kejeli kwako, au hata kughadhibika na kufanya machafuko lakini ukiangalia sababu kubwa ni kua hawawezi kuvumilia Baraka zako, wala usishangae, wala usifadhaike they can’t handle your blessing  wakati mwingine utajenga nyumba watasema ni nyumba basin i kakibanda tu ili mradi wakukatishe tama usiogope ni kwa sababu hawawezi kuvumilia Baraka zako!

 

6.       Wakati mwingine ili wakunyamazishe

 

Kuna watu wakati mwingine hawafurahii kuona ukivuma au ukisifiwa au jina lako likiwa na nguvu, au ukishangiliwa hivyo kutokana na wivu wanatamani wakunyamazishe, wanapoona unafanya vizuri unakubalika na una nafasi kubwa sana sifa zako zinaenea kila mahali utashangaa wanakunyamazisha au wanataka hata na watu wanaokusifia wanyamaze ona

 

Luka 19:37-40 “Hata alipokuwa amekaribia matelemko ya mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi wake walianza kufurahi na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo yote ya uwezo waliyoyaona, wakasema, Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu. Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako. Akajibu, akasema, Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele.”

 

Unaona wakati mwingine unaweza kujikuta unanyamazishwa ziko namna nyingi watu watataka wakunyamazishe kwa sababu sifa zako zinaenea na kukua kwa kasi na wanajisikia vibaya hawawezi kustahimili, kwa nini hii ni kwa sababu hawawezi kuvumilia Baraka zako.!

 

7.       Wanataka uwasujudie

 

Kuna watu wengine huwa wakipata cheo tayari wanageuka kuwa miungu watu na wanataka uwatetemekee na kuwasujudia na ikiwa hutetemeki wala kuwasujudia wanachukia sana na hiyo inaweza kuwa sababu ya kuanzisha mapambanao na wewe, na hata kukuangamiza ona

 

Esta 5:9-13 “Basi Hamani alitoka siku ile kwa furaha na ukunjufu wa moyo; lakini Hamani alipomwona Mordekai mlangoni pa mfalme, ya kwamba hasimami wala kutetemeka mbele yake, alijaa ghadhabu juu ya Mordekai. Walakini Hamani akajizuia, akaenda zake nyumbani kwake; akatuma kuwaita rafiki zake na Zereshi mkewe. Naye Hamani akawasimulia habari za fahari ya mali zake, na wingi wa watoto wake, nayo mambo yote pia ambayo mfalme amemfanikisha katika hayo, na jinsi alivyompandisha juu ya maakida na watumishi wa mfalme. Zaidi ya hayo Hamani akasema, Naye malkia Esta hakumkaribisha mtu ye yote pamoja na mfalme katika karamu aliyoiandaa, ila mimi peke yangu; hata na kesho pia nimealikwa naye pamoja na mfalme. Bali haya yote yanifaa nini, pindi nimwonapo yule Mordekai, Myahudi, ameketi mlangoni pa mfalme?

 

unaona ni kwanini Hamani pamoja na fahari yake aliyokuwa nayo alikuwa hajisikii raha ? kwa sababu alikuwa anataka asujudiwe, wako watu wanataka watetemekewe, wababaikiwe kwa sababu tu eti wana madaraka makubwa wa kutetemekewa ni Mungu tu yeye ndiye mwenye destiny Hatima ya maisha yetu, na sio mwanadamu

 

Esta 3:1-6 “Baada ya hayo mfalme Ahasuero alimwongezea cheo Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, akampandisha, akamwekea kiti chake juu ya maakida wote waliokuwapo pamoja naye. Nao watumishi wote wa mfalme, walioketi mlangoni pa mfalme, wakainama na kumsujudia Hamani, maana ndivyo alivyoamuru mfalme kwa habari zake. Bali Mordekai hakuinama, wala kumsujudia. Basi watumishi wa mfalme walioketi mlangoni pa mfalme wakamwambia Mordekai, Mbona wewe waihalifu amri ya mfalme? Ikawa, waliposema naye kila siku asiwasikilize, wakamwarifu Hamani, ili kuona kama mambo yake Mordekai yatasimama; maana alikuwa amewaambia ya kuwa yeye ni Myahudi. Hata Hamani alipoona ya kwamba Mordekai hainami wala kumsujudia, alighadhibika sana. Akaona si shani kumtia mikono Mordekai peke yake; maana wamemjulisha kabila yake Mordekai; kwa hiyo Hamani alitaka kuwaangamiza Wayahudi wote waliokuwa wakikaa katika ufalme wote mzima wa Ahasuero, yaani, watu wake Mordekai.”

 

Umeona wako watu wanadhani wewe huwaheshimu kwa sababu huwasujudii sie wengine ni wayahudi tunaheshimu kila mtu lakini hatuabudu watu, tunamwabudu Mungu peke yake kama maandiko yalivyotuelekeza Luka 4:8 “Yesu akajibu akamwambia, Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake  wakati mwingine visa na mikasa huinuka kwa sababu watu wanataka kuabudiwa, mtu unamuheshimu laki ni anataka kuvuka mipaka ya kiheshima na kwenda mbali zaidi, Mordekai aliyekuwa myahudi alikuwa amejifunza kuwa mwanadamu wa kawaida muheshimu lakini wakumuinamia  na kumtetemekea ni Mungu peke yake anayestahili kuabudiwa na kusujudiwa wengine wakiona hufanyi hivyo hawawezi kuvumilia kwa sababu hauabudu mwanadamu.!

 

8.       Wakati mwingine kwa sababu unatumiwa na Mungu kuliko wao

 

Kuna watu wakati mwingine hawafurahii kuona namna Mungu anavyokutumia katika karama na vipawa mbalimbali kuliko wao na kwa sababu hiyo watajisikia wivu moyoni na wakati mwingine watazusha maneno ya uwongo kwa kusudi la kukuchafulia huduma yako, wanaweza kusema unafanya mioujiza kwa kutumia nguvu za giza, wanaweza kusema wewe ni freemason, wanaweza kusema wewe ni mchawi, anaweza kusema wewe ni imani potofu, hutumii jina la Yesu na kadhalika hiii yota inafanyika kwa sababu hawawezi kuvumilia Baraka na upako ambao Mungu ameweka ndani yako ona

 

Mathayo 12:22-24 “Wakati ule akaletewa mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu akanena na kuona. Makutano wote wakashangaa, wakasema, Huyu siye mwana wa Daudi? Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo

 

Unaona Mafarisayo hawakufurahia Yesu kukubalika kutokana na ishara na miujiza aliyokuwa akiifanya, sisis nasi Yesu alituambia kuwa Mwanafunzi hawezi kumpita Mwalimu wake maana yake yale majaribu ambayo Mwalimu aliyapitia sisi nasi tutayapitia na kuzidi, tumetumwa kama Kondoo katikati ya mbwa mwitu, lazima adui wa Baraka za kiungu ndani yetu watajitokeza na kuleta kila aina ya upinzani katika jambo lolote ambalo kwalo Mungu ameweka mkono wake usiogope jambo kubwa na la msingi la kukumbuika ni kuwa hawawezi kuvumilia Baraka zako!

Tumeona katika Mstari wetu wa Msingi kuhusu baba yetu wa Imani nabii Isaka ya kuwa Mungu alimbariki upeo, ilikuwa kuna njaa katika nchi ya kanaani na ilikuwa ni kawaida kuwa kukiwa na njaa kama ilivyokuwa wakati wa Ibrahimu baba yake, wao walikimbilia Misri kwa sababu ya chakula, hata hivyo Mungu alimuonya Isaka kuwa asishuke kwenda Misri, na Mungu akaweka Baraka zake, Isaka na baba yake Ibrahimu walikuwa ni wataalamu wa kuchimba visima, walifahamu namna na jinsi ya kuchimba maji, na huenda pia Isaka alikuwa na ujuzi wa kumwagilia, njaa ilipokuwa kali yeye alipanda mbegu na bila shaka alimwagilia hivyo Mungu alimbariki na akampa kuvuna mara mia lakini sio hivyo tu mali yake iliongezeka na umaarufu wake ukawa mkubwa mno, hivyo akastawi na kuwa mtu mkubwa sana, wafilisti walianza kuona wivu, kila kisima alichokichimba wao walikigombea na kukifukia au kudai kuwa ni cha kwao, Biblia imeweka wazi kuwa wafilisti WAKAMHUSUDU yaani maana yake waluiona wivu tena wivu wenye uchungu, Isaka alikuwa mpenda amani hivyo aliwaachia na kuchimba kingine lakini walifanya fitina hii ama ile na mwisho wakaona haya Isaka akachimba na kingine na wakapata Maji na wakakiita kisima kile REHOBOTHI maana yake sasa Bwana ametufanyia nafasi, Isaka aliteseka kwa sababu ya Baraka zake, yako mateso mengine unayapitia na changamoto nyingine unazipitia sio kwa sababu umemkosea Mungu bali kwa sababu Mkono wa Mungu uko juu yako na wanaokuzunguka hawawezi kustahimili wala kuvumilia aina ya upako ulio nao, aina ya huduma uliyo nayo aina ya Baraka ulizoanazo, aina ya uimbaji unaoimba, aina ya mavazi unayovaa, aina ya uzuri ulio nao na kila aina ya Baraka kwa kawaida ina tabia ya kuvutia watu na maadui kwa nini ulipobarikiwa wengine walikukimbia ni kwa sababu hawawezi kuvumilia Baraka zako!, wako ambao hawatavumilia wewe kuzaa, hawatavumilia wewe kuolewa, hawatavumilia we kuwa na mtoto, hatawatavumilia wewe kufanikiwa au kua na ustawi wa aina yoyote ilekatika jamii kwa nini kwa sababu wako watu watakupoenda na kukusoegelea lakini wako wengine hawataweza kuvumilia Baraka zako! Bwana Mungu wa Baba zangu Ibrahim, Isaka na Yakobo na akufanyie nafasi, ili ufurahie Baraka zako bila usumbufu kutoka kwa maadui katika jina la Yesu nakuombea amen!

 

Na Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Maoni 1 :

Bila jina alisema ...

Barikiwa sana mtu wa Mungu aliye hai nimejifunza mengi kupitia ujumbe huu na mimi pia nitawafundisha wengine ujumbe huu. Ameeni