Mathayo 21:1-5 “Hata walipokaribia Yerusalemu, na kufika Bethfage, katika
mlima wa Mizeituni, ndipo Yesu alipotuma wanafunzi wawili akiwaambia, Enendeni
mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mara mtaona punda amefungwa, na mwana-punda
pamoja naye; wafungueni mniletee. Na kama mtu akiwaambia neno, semeni, Bwana
anawahitaji; na mara huyo atawapeleka. Haya yote yamekuwa, ili litimie neno
lililonenwa na nabii, akisema, Mwambieni binti Sayuni Tazama, mfalme wako
anakuja kwako, Mpole, naye amepanda punda, Na mwana-punda, mtoto wa punda.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kwamba tukio
la Yesu Kristo kupokelewa kwa shangwe jijini Yerusalem, lilikuwa ni tukio la
kipekee sana lililofanywa na watu, sawa kabisa na namna watu wanavyompokea
mfalme, tukio hili halikuwa tukio la bahati mbaya kwani vilevile lilikuwa ni
sehemu ya kutimizwa kwa maandiko ya kinabii kuhusu kuja kwa mfalme wa kipekee
ambaye angejibu mahitaji yote ya wanadamu Nabii Zekaria alilitabiri tukio hili
miaka 400 kabla ya kuzaliwa kwa Yesu ona;-
Zecharia 9:9 “Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti
Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana wokovu;
Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto wa punda.”
Swali moja kubwa ambalo wanafunzi
wengi wa maandiko hupenda kujiuliza ni kwamba, iko wazi kuwa Yesu alipokelewa
Yerusalem kwa shangwe kubwa sana watu walimfurahia kwa matawi ya mitende na
hata kutandaza nguo zao njiani, lilikuwa ni tukio la kipekee sana ambalo hakuna
mfalme amewahi kufanyiwa,Mungu roho Mtakatifu aliinua mioyo ya watu na
wakasangilia kwa nguvu sana kuingia kwa Maishi pale Sayuni, lakini swali kubwa
kwanini mfalme huyu awe amepanda punda?
Hili ndio swali kubwa na la Muhimu kwa kila mmoja wetu kujiuliza na
kutafuta majibu.
Wafalme huja na Majibu ya mahitaji ya watu!
Moja ya Kazi kubwa sana ya
wafalme wa zamani na labda huenda hata sasa ilikuwa ni pamoja na kutawala mfalme
alipaswa kuwa na majibu ya aina yoyote dhidi ya mahitaji ya watu wake, wafalme
walitakiwa kutatua changamoto zilizowakabili watu hata kuamua kesi za aina
mbalimbali mfano;-
1Wafalme 3:16-28 “Ndipo wanawake wawili,
makahaba, walimwendea mfalme, wakasimama mbele yake. Na mwanamke mmoja akasema,
Ee bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunakaa katika nyumba moja; nami nalizaa
nilipokuwa pamoja naye nyumbani. Kisha, siku ya tatu baada ya kuzaa kwangu,
ikawa mwanamke huyu naye akazaa; na sisi tulikuwa pamoja; hapakuwa na mtu
mwingine pamoja nasi nyumbani, isipokuwa sisi wawili tu. Na mtoto wa mwanamke
huyu akafa usiku, maana alimlalia. Akaondoka kati ya usiku, akamwondoa mtoto
wangu ubavuni pangu, mimi mjakazi wako nilipokuwa usingizini, akamweka kifuani
pake, na mtoto wake mwenyewe, aliyekuwa amekufa, akamweka kifuani pangu.
Nilipoondoka asubuhi nimnyonyeshe mtoto wangu, kumbe? Amekufa. Hata asubuhi
nilipomtazama sana, kumbe! Siye mtoto wangu niliyemzaa. Ndipo yule mwanamke wa
pili akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wangu ndiye aliye hai, na mtoto wako
ndiye aliyekufa. Na mwenzake akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wako ndiye
aliyekufa, na mtoto wangu ndiye aliye hai. Ndivyo walivyosema mbele ya
mfalme. Ndipo mfalme akasema, Huyu
anasema, Mtoto wangu yu hai, na mtoto wako amekufa. Na huyu anasema, Sivyo
hivyo; bali mtoto aliyekufa ni wako, na mtoto aliye hai ni wangu. Mfalme akasema,
Nileteeni upanga. Wakaleta upanga mbele ya mfalme. Mfalme akasema, Mkate mtoto
aliye hai vipande viwili, kampe huyu nusu, na huyu nusu. Ndipo mwanamke yule,
ambaye mtoto aliye hai ni wake, akamwambia mfalme kwa maana moyoni mwake
alimwonea mtoto wake huruma, akasema, Ee bwana wangu, mpe huyu mtoto aliye hai,
wala usimwue kamwe. Lakini yule mwingine akasema, Asiwe wangu wala wako; na
akatwe. Ndipo mfalme akajibu, akasema, Mpe huyu wa kwanza mtoto aliye hai,
maana yeye ndiye mama yake. Na Israeli wote wakapata habari za hukumu ile
aliyoihukumu mfalme wakamwogopa mfalme; maana waliona ya kuwa hekima ya Mungu
ilikuwa ndani yake, ili afanye hukumu.”
Wafalme walitakiwa kujibu hoja
zozote ngumu za watu wao waliowatembelea kuhitaji msaada katika maeneo
mbalimbali ya maisha yao 1Wafalme 10:1 “Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani juu ya
jina la Bwana, alikuja ili amjaribu kwa maswali ya fumbo.” Biblia ya
kiingereza inatumia maneno “she came to
test her with HARD questions” Hata
hivyo Mfalme Suleimani pia aliweza kutoa majibu ya maswali yote aliyouliza
malikia wa Sheba. Hata hivyo maandiko pia yanatueleza kuwa kuna wakati ambapo
wafalme walikosa majibu na uwezo wa kutatua changamoto kadhaa na hivyo walilia,
na kufunga na kuvaa magunia au kurarua mavazi yao. Angalia kwa mfano:-
2Wafalme 6:25-30 “Njaa ikawa kuu huko
Samaria; na tazama, wakauhusuru, hata kichwa cha punda kikapata kuuzwa kwa
vipande themanini vya fedha, na kibaba cha mavi ya njiwa kwa vipande vitano vya
fedha. Ikawa mfalme wa Israeli alipokuwa akipita ukutani, mwanamke mmoja akamwita
akisema, Unisaidie, bwana wangu, mfalme. Akasema, Bwana asipokusaidia,
nikusaidieje mimi? Ya sakafuni, au ya shinikizoni? Mfalme akamwambia, Una nini?
Akajibu, Mwanamke huyu aliniambia, Mtoe mtoto wako, tumle leo, na mtoto wangu
tutamla kesho. Basi, tukamtokosa mtoto wangu, tukamla; nikamwambia siku ya
pili, Mtoe mtoto wako, tumle; naye amemficha mtoto wake. Ikawa, mfalme
alipoyasikia maneno ya huyo mwanamke, aliyararua mavazi yake; (naye alikuwa
akipita juu ya ukuta;) na watu wakaona, na tazama, alikuwa amevaa magunia ndani
mwilini mwake.”
Unaona kwa msingi huo Mfalme
alikuwa na kazi ngumu ya kutatua changamoto za maisha ya watu, ukiacha swala la kutatua changamoto ya maisha
ya watu, mfalme pia alitakiwa kuwa mtu wa vita na mwenye uwezo wa kutwatetea watu
wake dhidi ya adui zao kwa kupigana kwa silaha na kwa uwezo wa kujihami,
wafalme walipaswa kuwa watu wa vita, Heshima ya mfalme ilikuwa kupitia uwezo
wake wa kuamua mambo na kuwapigania watu wakena kuwashindia dhidi ya adui zao,
mfano
1Samuel 17:1- 11. Wakati huo Wafilisti walikusanya majeshi yao kwa vita,
nao wakakusanyika huko Soko, ulio mji wa Yuda, wakatua kati ya Soko na Azeka,
katika Efes-damimu. Naye Sauli na watu wa Israeli wakakusanyika, wakatua katika
bonde la Ela, nao wakapanga vita juu ya hao Wafilisti. Wafilisti wakasimama juu
ya mlima upande huu, na Waisraeli wakasimama juu ya mlima upande huu, napo
palikuwa na hilo bonde katikati. Ndipo akatoka shujaa katika kambi ya
Wafilisti, aliyeitwa Goliathi, wa Gathi, ambaye urefu wake ulikuwa mikono sita
na shibiri moja. Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani, tena amevaa darii ya
shaba; na uzani wake ile darii ya shaba ulikuwa shekeli elfu tano za shaba.
Tena amevaa mabamba ya shaba miguuni mwake, naye alikuwa na mkuki wa shaba kati
ya mabega; yake. Na mti wa fumo lake ulikuwa kama mti wa mfumaji; na kichwa cha
mkuki wake kilikuwa shekeli mia sita za chuma uzito wake; na mtu aliyemchukulia
ngao yake akamtangulia. Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli
akawaambia, Mbona mmetoka kupanga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si
watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi. Kama akiweza kupigana
nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda yeye na kumwua,
ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia. Yule Mfilisti akasema, Nayatukana
leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane. Basi Sauli na Israeli wote
waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana.”
Mfalme juu ya Punda !
Sasa moja ya tukio la kushangaza
ni kuwa pamoja na kuwa wafalme walikuwa ni watu waliotakiwa kujibu hoja na
mahitaji ya watu ya aimna mbalimbali na kuwashindia watu vita dhidi ya adui
zao, ni muhimu kufahamu kuwa wafalme walipotaka kuonyesha nguvu zao na ukuu wao
wakati wote walitumia farasi katika kusafiri kwao, Farasi ilikuwa ni alama ya
vita na ufahari na utajiri, kwa hiyo kila mfalme aliyekuwa anataka kuonyesha
ufahari wake alitumia farasi, farasi ni mnyama anayeonyesha uhodari, wakati
punda ni mnyama anayeonyesha huduma, kama watu walikuwa wakijivuna walijivunia
magari yao ya farasi kwani hayo ndio yalikuwa yakidhihirisha nguvu na uwezo wao
Zaburi 20:1-9 “Bwana akujibu siku ya dhiki,
Jina la Mungu wa Yakobo likuinue. Akupelekee msaada toka patakatifu pake, Na
kukutegemeza toka Sayuni. Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu
zako. Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kuyatimiza mashauri yako
yote. Na tuushangilie wokovu wako, Kwa jina la Mungu wetu tuzitweke bendera
zetu. Bwana akutimizie matakwa yako yote. Sasa najua kuwa Bwana amwokoa masihi
wake;Atamjibu kutoka mbingu zake takatifu.Hawa wanataja magari na hawa farasi,
Bali sisi tutalitaja jina la Bwana, Mungu wetu. Wao wameinama na kuanguka, Bali
sisi tumeinuka na kusimama. Bwana, umwokoe mfalme, Utuitikie siku tuitayo.”
Watu wanachohitaji ni kuokolewa
kutoka katika changamoto zinazowakabili, haijalishi mfalme anakuja namna gani,
anaweza akaja na magari ya farasi lakini akawa hana majibu ya kutosheleza mioyo
ya watu wake Zekaria alitabiri kuwa anakuja mfalme mnyenyekevu, mpole hana
majivuno wala majigambo wala hana nia ya kutafuta kiki au ufahari yeye anakuja
na wokovu anakuja na kifurushi kitakachotuletea amani ni mfalme wa tofauti
mwenye uwezo wa kutatua changamoto za watu kwa kiwango kikubwa sana yeye
anatabiriwa kuwa angekuja akiwa amepanda punda na mwana punda mtoto wa punda,
hii ilikuwa ni ishara madhubuti ya kumtambua mfalme huyo mwenye nguvu zote
lakini mnyenyekevu!
Zakaria 9:9-10 “Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti
Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana wokovu;
Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto wa punda. Na gari la
vita nitaliondoa liwe mbali na Efraimu, na farasi awe mbali na Yerusalemu, na upinde
wa vita utaondolewa mbali; naye atawahubiri mataifa yote habari za amani; na
mamlaka yake yatakuwa toka bahari hata bahari, na toka Mto hata miisho ya dunia.”
Maandiko yanaonyesha kuwa mfalme
huyu
o Atakomesha
vita
o Silaha
za vita kama upinde utaondolewa mbali
o Hatakuja
na majeshi
Yeye atatangaza amani kwa mataifa
yote na ufalme wake utakuwa ni wa dunia nzima, Luka 2:14 “Atukuzwe Mungu juu mbinguni,
Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.” Mfalme atakayeingia
Yerusalem, yaani katika mlima wa Sayuni akiwa juu ya Punda, ni simple but
powerful ni mnenyekevu na mpole lakini ana majibu yote yeye atatoa suluhu ya
mahitaji yetu yote na hivyo tunachopaswa kusema ni Hosana mwana wa Daudi,
mfalme mwenye majibu ya wokovu wako haji na vifaru, haji na ufahari wowote
anakuja na mwana punda, humble but very powerful, huyu ndiye mfalme
aliyetabiriwa na Zekaria na Mathayo anatudhihirishia kuwa Yesu ndiye mfalme
huyu ambaye amekuja kulitimiza andiko, ana hekima kuliko suleimani na ana nguvu
kuliko Daudi, yeye atatupigania na hakuna kinachoweza kusimama mbele yake yeye
ndiye mtetezi wa adui zetu na mkombozi wetu dhidi ya unyonge si mwingine ni
Yesu !
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni