Jumatatu, 11 Julai 2022

Mungu wa falme zote za Dunia !


2Wafalme 14-19 “Basi Hezekia akaupokea waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma; kisha Hezekia akapanda, akaingia katika nyumba ya Bwana, akaukunjua mbele za Bwana. Naye Hezekia akaomba mbele za Bwana, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia; wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi. Tega sikio lako, Ee Bwana, usikie; fumbua macho yako, Ee Bwana, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, ambayo amemtuma mtu aje nayo ili kumtukana Mungu aliye hai. Ni kweli, Bwana, wafalme wa Ashuru wamewaharibu mataifa na nchi zao, na kuitupa miungu yao motoni; kwa maana haikuwa miungu, bali ni kazi ya mikono ya wanadamu; ilikuwa miti na mawe tu, ndiyo sababu wakaiharibu. Basi sasa, Ee Bwana, Mungu wetu, utuokoe na mkono wake, nakusihi, ili kwamba falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe Bwana Mungu, wewe peke yako.”



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa Maandiko yanatufunduisha kuwa maombi ndiyo nyenzo pekee inayoweza kutusaidia  wakati wowote tunapokutana na changamoto za aina yoyote zile tuwapo duniani, Jambo lolote ambalo linaweza kukuletea fadhaa katika maisha yako au familia yako, au taifa lako, tunaelekezwa kuwa wakati wa changamoto hizo ziwe za kitaifa, au kifamilia au za taasisi au mtu mmoja mmoja kwamba tumtwike yeye fadhaa zetu zote  angalia

1Petro 5:7 “huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.”

Unaona sio fadhaa ya mtu mmoja mmoja tu bali hata fadhaa za kitaifa au kitaasisi au familia, Mungu anatuthibitishia wazi katika neno kuwa atasikiliza maombi yetu ona  2Nyakati 7:13-15 “Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.”

Ni kupitia maombi Mungu atakutana na mahitaji yetu yote  kwa kadiri ya utajiri alionao katika Kristo Yesu Wafilipi 4:19 “Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu.”

Katika kifungu cha maandiko ya msingi Mfalme Hezekiah anaomba Hekaluni Nyumbani mwa Bwana, Hezekia alikuwa ameletewa ujumbe kwa njia ya Barua kutoka kwa mfalme Senekarebu  ambaye alikuwa mfalme mkubwa na mwenye nguvu katika nyakati zile, mfalme huyu aliweza kuwa na historia ya kuwa mshindi kwa kila taifa ambalo lilipigana naye  alipiga kila taifa na kila ufalme pamoja na miungu yao na kuichoma moto na sasa mfalme huyu alikuwa anaukaza uso wake kumjia Hezekiah kwa maana nyingine kumjia Hezekia pamoja na Mji wa Yerusalem na Israel kwa ujumla, Lakini kabla ya kumjia aliamua kumpa taarifa ya kile alichokusudia kuja kukifanya ona

2Wafalme 18:28-37 “Kisha yule amiri akasimama akalia kwa sauti kuu kwa lugha ya Kiyahudi, akasema, Lisikieni neno la mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru. Mfalme asema hivi, Hezekia asiwadanganye; kwa maana, hataweza kuwaokoa katika mkono wake. Wala Hezekia asiwatumainishe katika Bwana, akisema, Hakika Bwana atatuokoa, wala mji huu hautatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru. Msimsikilize Hezekia; kwa sababu mfalme wa Ashuru asema hivi, Fanyeni suluhu na mimi, mkatoke mnijie; mkale kila mtu matunda ya mzabibu wake na matunda ya mtini wake, mkanywe kila mmoja maji ya birika lake mwenyewe; hata nije nikawachukue mpaka nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai, nchi ya chakula na mashamba ya mizabibu, nchi ya mafuta ya mzeituni na asali, ili mpate kuishi, msife; wala msimsikilize Hezekia, awadanganyapo, akisema, Bwana atatuokoa. Je! Yuko mungu mmoja wa mataifa aliyewaokoa watu wake wakati wo wote na mkono wa mfalme wa Ashuru? Iko wapi miungu ya Hamathi, na ya Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu, na ya Hena, na ya Iva? Je! Imeuokoa Samaria na mkono wangu? Katika miungu ya nchi hizi zote, ni miungu gani iliyookoa nchi yao na mkono wangu, hata Bwana auokoe Yerusalemu na mkono wangu?  Lakini hao watu wakanyamaza kimya; wala hawakumjibu hata neno moja; maana amri ya mfalme ilikuwa kwamba, Msimjibu neno. Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu, mwenye kuandika tarehe, wakaenda kwa Hezekia, na nguo zao zimeraruliwa, wakamwambia maneno ya yule amiri.”

Vitisho hivi vilikuwa vitisho vya kweli, Mfalme Senekarebu alikuwa ameshiba kiburi cha ushindi wake kila mahali alikopita, alipiga mataifa na miungu yao aliichoma moto,  Hezekia alikuwa  hana jinsi ya aina yoyote ya kufanya ilikuwa lazima akubali kushindwa na kuweka silaha chini na kukubali kulipa kodi kwa Mfalme Senekarebu, au aingie kwenye mapigano, ilikuwa ni rahisi katika wakati kama huu kwa Hezekia kutafuta ushauri wa kibinadamu, au kuuliza kwa wenye hekima, au aingize majeshi yake vitani  au awe tayari kuharibiwa  au kukutwa na jambo baya tu huku macho yake yakishuhudia, Hezekia aliwashauri watu wake wasijibu kitu, Moyoni mwake alikuwa anajua, Mungu wa Israel ni Mungu wa tofauti na kuwa Mungu wetu ndiye Mungu wa falme zote za dunia, hivyo hangeweza kutafuta msaada wa kibinadamu, au msaada wa kijeshi kutoka kwa mataifa rafiki, Yeye alijikita katika kuutafuta uso wa Mungu aliye hai Mungu wa falme zote za dunia, na hivyo Ndipo mfalme Hezekia alipoamua kumuomba Mungu na kupeleka zile nyaraka za vitisho alizoandikiwa  kwa Mungu wa Falme zote za dunia  kwa kuwa alimjua Mungu na kumtegemea alimsifia kutoka moyoni akitambua kuwa ni Mungu pekee mwenye uweza wa kumsaidia ona

2Wafalme 14-19 “Basi Hezekia akaupokea waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma; kisha Hezekia akapanda, akaingia katika nyumba ya Bwana, akaukunjua mbele za Bwana. Naye Hezekia akaomba mbele za Bwana, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia; wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi. Tega sikio lako, Ee Bwana, usikie; fumbua macho yako, Ee Bwana, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, ambayo amemtuma mtu aje nayo ili kumtukana Mungu aliye hai. Ni kweli, Bwana, wafalme wa Ashuru wamewaharibu mataifa na nchi zao, na kuitupa miungu yao motoni; kwa maana haikuwa miungu, bali ni kazi ya mikono ya wanadamu; ilikuwa miti na mawe tu, ndiyo sababu wakaiharibu. Basi sasa, Ee Bwana, Mungu wetu, utuokoe na mkono wake, nakusihi, ili kwamba falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe Bwana Mungu, wewe peke yako.”

Hezekia alikuwa anataka Mungu atukuzwe, alikuwa anataka Mungu ajidhihirishe mwenyewe kuwa yeye ni Mungu wa wote wenye mwili, na kuwa hakuna lisilowezekana kwake, Hezekia alimsifu Mungu, Hezekia hakuwa na woga alikuwa na ujasiri mkuu alimsihi Mungu aone yeye mwenyewe na kusikia maneno ya Senekarebu alionyesha ya kuwa anamtegemea Mungu tu na sio wanadamu, wala hekima ya kibinadamu, alimwambia Mungu ni kweli Senekarebu ameshambulia mataifa mengi na miungu mingi ameichioma moto na kuziharibu lakini hiyo haikuwa miungu na hayo mataifa hayakumjua Mungu aliye hai, lakini yeye alijitegemeza kwa Mungu mwenye uwezo mkubwa sana ambaye alimtambua kama Mungu wa falme zote za Dunia  nani ukweli kuwa Mungu alimjibu Hezekia kwa njia rahisi sana, Mungu ni Mungu anayesikia aliyasikia maombi ya Hezekiah na kuyajibu ona kwa kinywa cha Nabii Isaya

2Wafalme 19:32-34 “Basi Bwana asema hivi katika habari za mfalme wa Ashuru, Yeye hatauingia mji huu, wala hatapiga mshale hapa, wala hatakuja mbele yake kwa ngao, wala hatajenga boma juu yake. Njia ile ile aliyojia, kwa njia iyo hiyo atarudi zake, wala hataingia ndani ya mji huu, asema Bwana. Maana nitaulinda mji huu, niuokoe, kwa ajili yangu mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu.”

Wakati huu Mungu aliona afupishe safari ya mfalme Senekarebu kwa kumtumia malaika wake mmoja tu, ambaye aliwatandika jeshi zima na Senekarebu akarudi nyumbani kwake kwa njia ile ile aliyoijia sawa na lile neno ambali Bwana alinena kwa kinywa cha nabii Isaya, na kwenda kuuawa na watu wake mwenyewe ona katika ;-

2Wafalme 19:35-37 “Ikawa usiku uo huo malaika wa Bwana alitoka, akakiingia kituo cha Waashuri, akawapiga watu mia na themanini na tano elfu. Na watu walipoondoka asubuhi na mapema, kumbe! Hao walikuwa maiti wote pia. Basi Senakeribu mfalme wa Ashuru akaondoka, akaenda zake, akarudi akakaa Ninawi. Ikawa, alipokuwa akiabudu nyumbani mwa Nisroki, mungu wake, Adrameleki na Shareza wakampiga kwa upanga; wakaikimbilia nchi ya Ararati. Na Esar-hadoni mwanawe akatawala mahali pake.”

Ziko vita nyingine ambazo watu watadhani uko mwenyewe kumbe liko jeshi la malaika nani makomandoo, Mungu  na atume malaika wake akusaidie katika kila changamoto unazokutana nazo, Wakati huu Mungu alimtumia malaika mmoja tu aliyepiga watu 185000 kumbuka hii ilikuwa ni kwa watakatifu wa agano la kale, katika agano jipya tunaambiwa kuwa Malaika ni roho wanaotumwa kuwahudumia wale watakaourithi wokovu ona Waebrania 1:13-14 “Je! Yuko malaika aliyemwambia wakati wo wote, Uketi mkono wangu wa kuume Hata nitakapoweka adui zako chini ya nyayo zako? Je! Hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu? unaona umuhimu wa kumuomba Mungu msaada wako utakujaje Bwana anajua wewe tambua tu kuwa ndiye anayemiliki tawala zote za dunia, ninakuombea kwamba katika hali uliyo nayo Bwana Mungu na atume malaika wakabiliane na changamoto unazokutana nazo, wala usiogope liamini neno hili ambalo Bwana amenipa kwaajili yako nakuhakikishia hutalia tena wala hutafadhaika nina Mungu aliye hai kama wa Hezekia Na Mungu wangu atakutana na changamoto zako zote zinazokukabili kwa ushindi mkubwa, kisha wataaibika wanaoshindana nawe!

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote         

Mkuu wa wajenzi Mwenye hekima!

Hakuna maoni: