Jumatatu, 17 Oktoba 2022

Jinsi ya kukabiliana na mambo ya kutisha


1Samuel 17:4-11 Ndipo akatoka shujaa katika kambi ya Wafilisti, aliyeitwa Goliathi, wa Gathi, ambaye urefu wake ulikuwa mikono sita na shibiri moja. Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani, tena amevaa darii ya shaba; na uzani wake ile darii ya shaba ulikuwa shekeli elfu tano za shaba. Tena amevaa mabamba ya shaba miguuni mwake, naye alikuwa na mkuki wa shaba kati ya mabega; yake. Na mti wa fumo lake ulikuwa kama mti wa mfumaji; na kichwa cha mkuki wake kilikuwa shekeli mia sita za chuma uzito wake; na mtu aliyemchukulia ngao yake akamtangulia. Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupanga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi. Kama akiweza kupigana nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda yeye na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia. Yule Mfilisti akasema, Nayatukana leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane. Basi Sauli na Israeli wote waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana.”


Utangulizi:

Goliath ni moja ya watu wanaotajwa katika Biblia katika kitabu cha Samuel akielezewa kama jitu kubwa sana ambalo lilipigwa na kijana mdogo sana aitwaye Daudi, kwa silaha dhaifu sana, Kuja kwa Daudi ni matokeo ya Sauli pamoja na majeshi yake yote kufadhaika na kuogopa sana kupigana na askari huyo komandoo wa kikosi cha wafilisti, Leo hii stori ya Daudi na Goliath imekuwa ni moja ya mfano unaotumiwa sana katika kutia moyo watu wa kila aina kuondoa hofu na kukabiliana na tukio lolote gumu au linaloonekana lenye kutisha hata kama inaonekana kibinadamu kuwa tunakabiliana na kitu kigumu lakini tukiwa tuna Mungu aliye hai ndani yetu!

1Samuel 17:45 “Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana.”

Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo;-

·         Mambo ya kutisha

·         Jinsi ya kukabiliana na mambo ya kutisha!

·         Siri ya kukabiliana na mambo ya kutisha.

Mambo ya kutisha.

Tunapozungumzia mambo ya kutisha katika nyakati za leo, tunaweza kuzungumzia hali yoyote ngumu na ambayo kwa akili za kibinadamu ni ngumu kuikabili katika hali ya kawaida, hali hizo zote ngumu leo, au zenye kutisha na kuogopesha zinaweza kufananishwa na ukubwa aliokuwa nao adui wa Israel yaani Goliath, Kwa mujibu wa maelezo ya Biblia tunaambiwa kuwa Goliath alikuwa na urefu wa mikono sita na shubiri moja kwa vipimo vya leo ni kama Goliath alikuwa na urefu wa futi tisa na nusu, wakati watu wengine wanakisiwa kuwa na futi kama tano na inchi tatu au sita kwa wale wenye sifa ya urefu Gioliath alikuwa ni mrefu sana kwenda juu kuliko wanadamu wa kawaida hivyo lilikuwa jitu kwelikweli, lakini pia tunaambiwa alikuwa na Kofia ya kivita Chepeo ya shaba yenye uzito wa Paundi 66, kumbuka Paundi moja ni sawa na kilo 0.454 hivyo Paundi 66 ni sawa na Kilo 29 au 30, Pia jamaa alikuwa na koti la kivita dirii ya shaba yenye uzito wa Shekel 5000 sawa na Paundi 175 ambayo ni sawa na kilo 79 au 80 hivi, hali kadhalika mkuki wake kile kicha tu pekee kilikuwa na uzito wa Paundi 20 yaani sawa na kilo 9-10 na kumbuka huo ulikuwa ni kishwa tu cha mkuki wake, kwa kifupi tu Goliathi lilikuwa ni jitu la kutisha kimsingi Goliath alikuwa ni kama mashine ya kifo ambaye kwa kumuona tu huwezi kurusha mguu wako vitani, lakini kwa cv uzoefu wake huyu alikuwa mzoefu wa vita tangu utoto wake

1Samuel 17:33 “Sauli akamwambia Daudi, Huwezi wewe kumwendea Mfilisti huyu upigane naye; maana wewe u kijana tu; na huyu ni mtu wa vita tangu ujana wake.”

 Unaweza kuona na licha ya kuwa na uzoefu wa vita Goliath alikuwa anajiamini na alikuwa na maneno ya hivyo na ya jeuri na kila aliyemsikia na kumuona aliyeyuka moyo! Haya ni mambo ya kutisha, Yawezekana katika maisha yetu tukawa tunakutana na mambo magumu ambayo kwa akili ya kibinadamu hayawezi kukabilika wala hayaonyeshi upenyo, hayo ni mambo ya kutisha na hatupaswi kuogopa kwani neno la Mungu linatupa matumaini kuwa iko njia ya kushinda!. Tunapomuangalia Daudi tunaweza kugundua kuwa yako mambo Muhimu yaliyopelekea akubali kupambana na lijitu na akaweza kufanikiwa!

Jinsi ya kukabiliana na mambo ya kutisha!

1.       Alifikiri juu ya kulinda Heshima yake.

 

Daudi alifikiri juu ya kulinda heshima yake na na ya Mungu wake, Mfalme alikuwa ameahidi kuwa mtu atakayetoka na kumpiga mfilisti huyu kwanza angefanywa kuwa tajiri sana, pili angeinuliwa kwa kuingia katika familia ya kifalme na kuketi katika meza kuu pamoja na mfalme kwa kuozwa binti wa kifalme jambo ambalo linempa haki hiyo na zaidi ya hayo Familia yake ingekuwa huru katika maswala ya kulipa Kodi. Unaweza kuona

 

1Samuel 17:25-27Watu wa Israeli wakasema, Je! Mmemwona mtu huyu aliyepanda huko? Hakika ametokea ili awatukane Israeli; basi, itakuwa, mtu yule atakayemwua, mfalme atamtajirisha kwa utajiri mwingi, naye atamwoza binti yake, na kuifanya mbari ya baba yake kuwa huru katika Israeli., Daudi akaongea na watu waliosimama karibu, akisema, Je! Atafanyiwaje yeye atakayemwua Mfilisti huyo, na kuwaondolea Israeli aibu hii? Maana Mfilisti huyu asiyetahiriwa ni nani hata awatukane majeshi ya Mungu aliye hai? Nao watu wakamjibu vivyo hivyo, wakisema, Ndivyo atakavyofanyiwa mtu yule atakayemwua.”

 

Katika kila niia ya mafanikio kwa kawaida kuna jambo gumu linalosimama ambalo ni lazima upambane kuliangusha ndipo uweze kutoboa, Israel wasingeliweza kuingia katika inchi ya mkanaani nchi ya maziwa na asali bila kuwapiga wakazi wake, wakati wote njia ya mafanikio yako haiwezi kuwa nyepesi, lakini kumbuka kuna utajiri kuna heshima kuna uhuru ambao utapatikana kama tu jitu litaanguka, hivyo ni lazima ujipe moyo na ukubali kukabiliana na giant nani ajuaye ya kuwa wewe ndie utakayeikomboa Familia yako na taifa lako pigana kwaajili ya kuweka heshima, haiwezekani ukubali kupuuzwa pigana na kila kinachosimama mbele yako na Mungu atakuwa pamoja nawe!

 

2.       Alifikiri juu ya kulinda Heshima ya Mungu.

 

Israel lilikuwa ni taifa ambalo Mungu amewachagua ili waweze kuwa Baraka kwa mataifa yote, kushindwa kwa Israel ilikuwa ni sawa na kushindwa kwa Mungu wao na Mungu wa baba zao, Mungu wa Ibrahimu na Isaka na Yakobo angetukanwa, Mtu huyu anayetisha lisha ya kuwatukana waisrael lakini pia alimtukana Mungu aliye hai, wakati mwingine kushindwa kwetu, kuanguka kwetu, umasikini wetu na kushindwa kwetu kufanikiwa kunafanya ionekane kuwa Mungu wetu ameshindwa na jina lake kutukanwa Hivyo Daudi alikuwa akipigana kwaajili ya utukufu wa Mungu pia

 

1Samuel 17: 45-47 “Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana. Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli. Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana, naye atawatia ninyi mikononi mwetu.”

 

Kwaajili ya jina la Mungu wetu, ili kuitunza heshima yake hatuna budi kumuomba Mungu atukuzwe hata kupitia changamoto zinazotukabili, ijulikane ya kuwa changamoto unayoipitia hata kama inatisha kiasi gani ikishughulikiwa jina la Mungu wetu litatukuzwa na kuinuliwa Daudi aliona hana budi kushinda kwaajili ya jina la Mungu ili wafilisti waelewe kuwa Israel hata kama haina silaha wala nguvu inashinda kwa jina la Mungu aliye hai.

 

3.       Alifikiri juu ya kupoteza uhuru na kuwa watumwa.

 

Hakuna kitu kinauma duniani kama kuwa mtumwa au kupoteza Uhuru, wazee wetu waliopigania uhuru, walikataa kila aina ya ugandamizaji  na uonevu na ndio maana walidai uhuru kwa nguvu zao zote, sababu kubwa ilikuwa ni kukataa uonevu na kudhalilishwa, wapigania uhuru wote walikuwa na roho inayofanana, Jomo Kenyatta, Julius Nyerere, Patrice Lumumba, Kwame Nkuruma, Haile Selasie, Robert Mugabe, Keneth Kaunda, Abeid Karume, Samora Machel, Nelson Mandela, Oliva Tambo, Na mwimbaji Bob Marley walikataa dhana ya utumwa na kuwa na roho moja yenye kuitaka Afrika iweze kuwa huru kujitawala na kujiamulia mambo yake  na ndio maana Mungu aliwaamsha nia na mioyo yao  ili wawe na uchungu na kuwatetea ndugu zao, Mungu aliamsha hari ya Daudi na kukubali kuwa Mwamuzi na mwokozi wa ndugu zake kwa sababu hakutakamkukubali wawe watumwa wa wafilisti, masharti ya vita hii ilikuwa kama Goliath akimshinda yule ambaye Israel wangemtoa wangekuwa watumwa wa wafilisti na kama yule ambaye wangemtoa angemshinda basi wafilsiti wangekuwa watumwa wa Israel ona

 

1Samuel 17:8 -9 “Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupanga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi. Kama akiweza kupigana nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda yeye na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia.”

Siri ya kukabiliana na mambo ya kutisha.

-          Usikimbie vita na mambo ya kutisha – hakikisha kuwa unakabiliana na jitu lako lenye kutisha litokee kabiliaba nalo, jifunze kukabiliana na mambo ya kutisha na wakati mwingine sio lazima yakukabili bali unaweza hata kuyafuata 1Samuel 17:34-35 “Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo wa lile kundi, mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua.” Uko wakati ambako lazima umfuatilie adui na uambane naye kule aliko anaweza kukuvamia na kuchukua kila kilicho chako, kuna wakati katika maisha unaweza kudhulumiwa, adui akachukua kila kilicho chako, akachukua kipato chako, nyumba yako, familia yako, muda wako na hata afya yako, lazima uwe mkali usikubali kudhalilika pambana bila kujali ukubwa wa tatizo pambana kwa jina la Bwana wa majeshi, hakuha kukimbia wengine wakikimbia we baki pambana mpaka senti ya mwisho! 1Samuel 17:24 “Na watu wote wa Israeli walipomwona yule mtu wakakimbia, wakaogopa sana.” Huwezi kuwa kiongozi wa Bendi asiyependa Muziki.

 

-          Usiogope – Hata kama adui yako anaoneana mwenye kutisha kiasi gani haupaswi kuogopa neno usiogope katika Biblia limeandikwa mara 366 sawa na siku zote za mwaka mzima hii maana yake hatupaswi kuogopa, kuwaogopa na badala yake ujae imani umtegemee Mungu tu jua ya kuwa Mungu yuko nawe na atakusaidia 2Wafalme 1:15 “Malaika wa Bwana akamwambia Eliya, Shuka pamoja naye; usimwogope. Akaondoka, akashuka pamoja naye hata kwa mfalme.” Kuna wakati maandiko yanatuambia USIMUOGOPE hii kama inahusu mtu na pia inatuambia USIWAOGOPE kama  ni kundi kubwa

 

-          Kumbukumbu 20:1 “Utokapo kwenda vitani kupigana na adui zako, na kuona farasi, na magari, na watu wengi kuliko wewe, usiwaogope; kwa kuwa Bwana Mungu wako, yu pamoja nawe, aliyekukweza kutoka nchi ya Misri.”

 

-          Maandiko hayatutaki tuwe na hofu kwa sababu vitani tutaonekana kuwa ni sisi tunaopigana lakini ndani ya mioyo yetu anayepigana ni Bwana mwenyewe vita sio yako ni vita ya Mungu tunayemuamini na kumtumikia ona

 

2Nyakati 20:15 “akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; Bwana awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya Mungu.”

Hitimisho:-

Silaha zetu zina nguvu kubwa ya ajabu sana na hatupaswi kuogopa tunajifunza kutoka kwa Daudi ya kuwa hata iweje au adui aweje Mungu atatupa ushindi mkubwa sana, vita ni yake wala si yetu inawezekana unayakumbuka mamo haya yote lakini wakati mwingine tunapaswa kukumbushwa ili kibinadamu tusiogope, usiogope wakati vita vinakukabili kwa sababu zozote zile.Silaha alizochagua Daudi zilionakana kwa machio ya kibinadamu kuwa duni kwa kulinganisha na jitu alilokuwa anapigana nalo lakini Mungu alimpa ushindi

1Samuel 17: 49 “Daudi akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingilia kipajini, akaanguka chini kifudifudi.” Daudi alishinda kwa kutumia jiwe moja tu kati yam awe matano aliyokuwa nayo, silaha za vita vyetu zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome ona

2Wakoritho 10: 3-5 “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo;”    

Na Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!



Usibishane na Punda


Tito 3:9-11 “Lakini maswali ya upuzi ujiepushe nayo, na nasaba, na magomvi, na mashindano ya sheria. Kwa kuwa hayana faida, tena hayana maana. Mtu aliye mzushi, baada ya kumwonya mara ya kwanza na mara ya pili, mkatae; ukijua ya kuwa mtu kama huyo amepotoka, tena atenda dhambi, maana amejihukumu hatia yeye mwenyewe.”


Utangulizi:

“Mtu mwenye hekima ni yule anayejifanya mjinga wakati mtu mpumbavu anapojifanya kuwa ana hekima”

Siku moja Punda alimwambia Chui kwamba Majani yote yana rangi ya bluu!

Chui akajibu akamwambia Punda hapana Bwana majani yote ni ya Kijani!

Wakabishana sana huyu akisema ni bluu na huyu akisema ni kijani, mwisho waliona wamwendee mfalme wao ili waweze kuamua kwamba ni nani yuko sahihi,  Mfalme wao yaani mfalme wa Nyika Simba,  Kabla hawajafika msituni walimkuta mfalme wao yaani Simba akiwa ameketi na kutulia katika kiti chake cha ufalme !

Wakamsalimia wakisema Mtukufu mfalme Simba tuambie majani yana rangi ya kijani au yana rangi ya blue?

Simba akajibu, Kwa kweli majani yana rangi ya bluu!, Punda akadakia si nilikuambia chui majani yana rangi ya blue wewe ukanibishia  unasikia sasa? Lakini chui aliendelea kubisha na kusema kwa hakika jamani majani ni ya rangi ya kijani

Ndipo mfalme Simba akasema Natangaza adhabu kali kwa chui kuwa utapaswa kukaa kimya na kutokusema chochote kwa miaka mitano!, Punda aliruka juu na kufurahia sana kisha akaenda zake

Majani ni ya bluu?

Chui alikubaliana na adhabu aliyopewa lakini alitaka kumuuliza Mfalme swali moja wakiwa wamebaki peke yao!

Alimwambia Mtukufu Simba mfalme wa nyika kwanini unanipa adhabu kali ili hali unajua ukweli kabisa kuwa majani ni ya kijani?

Simba alimjibu chui kuwa ni ukweli usiopingika kuwa majani ni ya kijani!

Sasa kwa nini umeniadhibu aliuliza chui?

Simba alijibu!

Kwa habari ya kuwa majani ni ya kijani au ni ya bluu sijakuadhibu

Adhabu yako imekuja kwa sababu sio rahisi kwa mnyama mwenye akili kama wewe kupoteza muda wako kubishana na mnyama kama punda, zaidi ya yote kukubali kuja kwa mfalme na kumsumbua kwa maswali ya kijinga, huko ni kupoteza Muda kubishana na wajinga na wazushi, wasiojali ukweli wa mambo wala uhalisia wa vitu, zaidi wanajali tu washinde, waliamini katika uzushi na uwongo, kumbuka siku zote usipoteze muda wako kujadili mambo ya kipuuzi na yasiyo na maana wala kubishania mambo ya kipuuzi.

Kuna watu ambao huwa hawajali na huwa hawaoni, hata kama ushahidi uko wazi mbele yao na wanaona kwa macho yao hawana uwezo na moyo wa kukubali uhalisia, wao ni vipofu katika nafsi zao, wamepofushwa fikra zao, wabinafsi, wamejaa chuki na hila na wakati wote wanataka kuonekana kuwa wako sahihi hata kama ukweli ni kuwa hawako sahihi

Wakati ujinga unapounguruma, Hekima hukaa kimya, ukimya wa Hekima na mani ya hekima ni ya muhimu kuliko kujipotezea muda na wajinga!

“Mtu mwenye hekima ni yule anayejifanya mjinga wakati mtu mpumbavu anapojifanya kuwa ana hekima”

Translated and added value by

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!



Jumatatu, 10 Oktoba 2022

Vazi la Yusufu!


Mwanzo 37:23-24Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, wakamtwaa wakamtupa katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji.


Utangulizi:

Mojawapo ya viongozi wa kiroho ambao habari zao zimeandikwa kwa urefu sana katika maandiko ni pamoja na Yusufu, Yusufu anahesabika kama moya ya mababa wa Israel, ukiacha Abrahamu, Isaka na Yakobo, yeye ndio sababu kubwa kwa wana wa Israel kushuka Misri, kuna mambio mengi sana ya kujifunza katiika maisha ya Yusufu lakini moja wapo ya jambo la msingi na la muhimu sana tunalotaka kulizungumzia leo tena kwa kina ni pamoja na Vazi la Yusufu, vazi lake na nguo zake zinaonekana kuwa na mvuto wa kipekee na vilevile kuwa sababu ya mapito yake kuna nini kilipelekea hawa watu kumtenda machungu kisa kikianzia kwenye vazi? Maandiko yanasema hivi;-

Mwanzo 49:22-24 “Yusufu ni mti mchanga wenye kuzaa, Mti mchanga wenye kuzaa karibu na chemchemi, Matawi yake yametanda ukutani. Wapiga mishale walimtenda machungu, Wakamtupia, wakamwudhi, Lakini upinde wake ukakaa imara, Mikono yake ikapata nguvu, Kwa mikono ya Mwenye Enzi wa Yakobo; Kwa jina la mchungaji, yeye jiwe la Israeli,”

Maandiko hayatuambii kuwa Yusufu aliwakosea Ndugu zake, lakini yaonekana wazi kuwa ndugu zake walichukizwa naye na sababu kubwa inaweza kuwa ni wivu wenye uchungu na hasira kali juu yake, lakini Bwana alikuwa pamoja naye, matukio ya aina hii yanaweza pia kuwako katika jamii inayotuzunguka leo, tunaweza kujikuta katika wakati mgumu sana kwa sababu ya mafanikio ya aina mbalimbali na wakati mwingine kwa sababu ya kusudi la Mungu lililoko ndani yetu!  Na anayepingana na kusudi hilo kwa vyovyote vile ni adui Shetani ambaye wakati mwingine anaweza kuwatumia watu tena watu wa karibu.

Vazi la Yusufu!

Kisa cha kusikitisha cha maisha machungu ya Yusufu kinaanzia na namna Yusufu alivyonunuliwa na kuvishwa vazi la thamani kubwa sana na baba yake biblia inaelezea vazi hilo katika

Mwanzo 37:3-4 “Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani.”

Maandiko yanaelezea kuhusu kanzu hii ndefu, na matoleo mengine ya kibiblia yanaitaja kama nguo yenye rangi nyingi, vazi hili la thamani lilikuwa ni vazi la gharama kubwa na kwa mujibu wa historia ya kibiblia lilikuwa ni vazi lililoweza kumtambulisha mtu kuwa ni mwana mfalme au mwana wa kifalme (Prince au Princess)

2Samuel 13:18 “Naye alikuwa amevaa kanzu ndefu; kwa kuwa kwa nguo hizo huvikwa binti za mfalme waliokuwa wanawali. Ndipo mtumishi wake akamleta nje, akafunga mlango nyuma yake.”

Kanzu hii au vazi kinabii ilikuwa inaashiria kuwa Israel au Yakobo amekusudia kumpa heshima kubwa na ya tofauti mwanaye aliyeitwa Yusufu, na kuanza kumfunza Yusufu kuwa mtawala na mfalme, Vazi hili alilotengenezewa na baba yake lilikuwa ni ishara ya upendeleo, neema na heshima maalumu aliyokuwa ametunukiwa Yusufu aidha na baba yake au na Mungu lakini kwa vile baba yake alikuwa nabii alikuwa anaashiria kuwa Yusufu hakuwa mtu wa kazi ngumu yeye alikuwa ni msimamizi na mwangalizi na kazi zake ni usimamizi kwani vazi lile halikuwa vazi la kazi bali vazi la kitawala! Lilikuwa ni vazi la kibali, kupendwa na neema ya Mungu

Vazi maalumu kwa Yusufu!          

Kwa nini Yakobo alimtengenezea Yusufu vazi maalumu? Maandiko yanaonyesha kwanza kabisa Kuwa Yakobo alimpenda Raheli sana kuliko Lea, jambo hili linaweza kuwa lilionekana wazi kwa watoto wa Yakobo ambao waliona wazi kuwa mama zao hawakupendwa kama alivyopendwa mama yake Yusufu,

Mwanzo 29:30-31 “Akaingia kwa Raheli naye, akampenda Raheli kuliko Lea, akatumika kwa ajili yake miaka saba mingine. BWANA akaona ya kwamba Lea hakupendwa, naye akafungua tumbo lake; bali Raheli alikuwa hazai.”

Unaona kwa hiyo ni wazi kuwa kutokana na Yakobo kumpenda sana Raheli kuliko Lea ilikuja kuwa rahisi vilevile kwa Yakobo kumpenda Yusufu kuliko watoto wengine japo hii ni dhana tu ya kibiblia na kitheolojia  

Mwanzo 30:22-24 “Mungu akamkumbuka Raheli; Mungu akamsikia, akamfungua tumbo. Akapata mimba, akazaa mwana, akasema, Mungu ameondoa aibu yangu. Akamwita jina lake Yusufu, akisema, BWANA aniongeze mwana mwingine.”

Raheli alipokuja kumzaa Yusufu pia alimpa jina Yufufu ambalo maana yake Bwana ameniondolea aibu yangu, kwa msingi huo kinabii pia mtoto huyu alikuwa anahusika na kuondoa aibu ya mama yake wote tutakuwa tunakumbuka kuwa mara baada ya anguko la Mwanadamu katika bustani ya Edeni Adamu na Eva walijisikia aibu, walijiona wako uchi na Mungu aliwatengenezea vazi ili kuifunika aibu yao au kuwaondolea aibu kumbuka

Mwanzo 3:21 “BWANA Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika.” Yakobo alichokifanya kwa Mwanaye Yusufu, na jina alilopewa Yusufu na Vazi alilotengenezewa baadaye na Yakobo yalikuwa na maana sawa na kile Mungu alimfanyia Adamu na mkewe kwa kuwavika mavazi ya kuwaondolea aibu, maana yake Mungu aliwapa Heshima iliyokuwa imepotea na vilevile Yusufu kutengenezewa vazi lile maalumu ilikuwa ni Ishara ya Heshima kubwa kwake!,  na kinabii ni kijana ambaye angekuja kuiondolea aibu familia yake na kuiifadhi wakati wa dhiki, ukiacha heshima hii kijana huyu alikuwa mwadilifu na alijifunza mambo mengi kuhusu Mungu kutoka kwa baba yake na mara kwa mara ndiye aliyekuwa akitoa ripoti ya taarifa ya watoto wote wa Yakobo kwa  na kwa bahati mbaya wengi wao hawakuwa na tabia njema mwanzoni  ukilinganisha na Yusufu ona,

Mwanzo 37:2 “Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, aliyekuwa mwenye miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo pamoja na ndugu zake; naye alikuwa kijana pamoja na wana wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu akamletea baba yao habari zao mbaya.”

Kwa hiyo utaweza kuona kutokana na usafi wa Yusufu, alionekana kama kikwazo kikubwa cha matendo maovu ya kaka zake, pia alionekana kama mbeya kwa sababu angeleleza taarifa zao mbaya walizokuwa wakizifanya, achilia mbali Ndoto zake za kiutawala ambazo zilikuja kuongeza chuki kubwa kwani sio tu, baba yake alikusudia kumuheshimu sana Yusufu, lakini sasa inaonekana kuwa hata Mungu alikuwa amekusudia kumuheshimu sana Yusufu kuliko nduguze na kumuinua juu kiutawala ona.

Mwanzo 37:5-11 “Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake. Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia. Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi? Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili.”

Ndoto za Yusufu ulikuwa ni unabii maalumu kutoka kwa Mungu kuwa Mungu angemuheshimu sana Yusufu na kuwa kwa vyovyote vila angekuja kuwatawala nduguze, sawa tu na baba yake alivyomtengenezea vazi maalumu, ni wazi kuwa Mungu alikuwa amekusudia kumuheshimu Yusufu, kila mmoja wetu kuna jambo ambalo kwalo Mungu amekusudia kukufanya maalumu kuliko wengine kuna heshima ambayo Mungu ameikusudia kwako wakati wote Mungu ana mpango mwema kwaajili yako

Yeremia 29:11 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.”

Hata hivyo ni Muhimu kufahamu kuwa kama Mungu baba yetu wa Mbinguni amekusudia kutuheshimisha sisi, ieleweke wazi kuwa shetani atapambana kwa kila namna kuhakikisha ya kuwa heshima hiyo inaharibiwa vazi la heshima ambalo Mungu anataka kukuvisha linaweza kuwa sababu kubwa sana ya vita vyako duniani lakini kumbuka wakati wote kusudi la Mungu ndilo litakalosimama

Kuharibiwa kwa vazi la Yusufu!

Tumejifunza na kuona kuwa vazi hili tayari kinabii linaashiria heshima ambayo Mungu amekusudia Kumpa Yusufu, lakini vilevile ni heshima ambayo Mungu amekusudia kumpa kila mmoja wetu, ni muhimu kufahamu kuwa kusudi kubwa la ibilisi au shetani ambaye ni adui wa makusudi yote ya Mungu ndani yetu ni pamoja na kupambana na ile Heshima ambayo Mungu ameikusudia katika maisha yetu, na hii ni kutaka kuiharibu na kuichafua ile heshima ili yamkini aweze kupambana na kusudi la Mungu lililoko ndani yetu, ona mfululizo wa matukio magumu unaambatana na maisha ya Yusufu yote yakilenga kuharibu vazi lake kusalitiwa, kuchukiwa bila sababu, kupanwa kuuawa au kuuzwa uhamishoni  na jambo la kwanza ilikuwa ni kumbua lile vazi.

Mwanzo 37:23-24 “Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, wakamtwaa wakamtupa katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji.”

Unaweza kuona chuki dhidi ya Yusufu haikuwa juu yake mwenyewe tu lakini ilikuwa na juu ya ile kanzu, vita kali ilikuwa dhidi ya vazi la Yusufu, na Nduguze hawakuishia hapo tu walihakikisha kuwa wanaliharibu vazi lile na kumtumia salamu baba yake ili yamkini naye aweze kujuta kwa kumuandalia Yusufu vazi kama lile ona

Mwanzo 37:31-34 “Wakaitwaa kanzu ya Yusufu, wakachinja mwana-mbuzi, na kuichovya kanzu katika damu. Wakaenda nayo ile kanzu ndefu, wakamletea baba yao, wakasema, Tumeona hii; basi, utambue kama kanzu hii ni ya mwanao, ama siyo. Akaitambua, akasema, Ndiyo kanzu ya mwanangu, mnyama mkali amemla; bila shaka Yusufu ameraruliwa. Yakobo akararua mavazi yake, akajivika gunia viunoni, na kumlilia mwanawe siku nyingi.”

Unaona kimsingi chuki, na husuda juu ya Yusufu kwa ndugu zake haikutokana na nafsi zao tu kwani wao walimalizia hapo, lakini ni wazi kuwa chuki hii inatoka kwa yule adui, adui hana mpango mwema na vazi la Yusufu la aina yoyote ile fikiria kuwa ameuzwa ugenini utumwani, huko nako hakuna mtu anayeijua historia yake wala ndoto yake na kwa vile Mungu alikuwa amemkusudia kuwa msimamizi na kiongozi anajikuta utumwani ananunuliwa na Potifa naye anamfanya kuwa mtu mkubwa katika nyumba yake ona  

Mwanzo 39:1-18 “Basi Yusufu akaletwa mpaka Misri naye Potifa, akida wa Farao, mkuu wa askari, mtu wa Misri, akamnunua mkononi mwa hao Waishmaeli waliomleta huko. BWANA akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, yule Mmisri. Bwana wake akaona ya kwamba BWANA yu pamoja naye, na ya kuwa BWANA anafanikisha mambo yote mkononi mwake. Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake. Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo, BWANA akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka wa BWANA ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba. Akayaacha yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu cho chote chake, ila hicho chakula alichokula tu. Ikawa baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami. Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu. Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu cho chote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu?  Akawa akizidi kusema na Yusufu siku baada ya siku, lakini hakumsikia alale naye, wala aongee naye. Ikawa, siku moja, akaingia nyumbani atende kazi yake, wala hapakuwa na mtu katika watu wa nyumbani humo ndani; huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake, akakimbia, akatoka nje. Ikawa alipoona ya kwamba amemwachilia nguo yake mkononi mwake, naye amekimbia nje, akawaita watu wa nyumbani mwake, akasema nao, akinena, Angalieni, ametuletea mtu Mwebrania atufanyie dhihaka. Ameingia kwangu, ili alale nami, nikalia kwa sauti kuu. Ikawa, aliposikia ya kuwa nimepaza sauti yangu na kulia, aliiacha nguo yake kwangu, akakimbia, akatoka nje. Basi akaiweka ile nguo kwake hata bwana wake aje nyumbani. Naye akamwambia kama maneno hayo, akisema, Yule mtumwa Mwebrania uliyemleta kwetu, aliingia kwangu anidhihaki. Ikawa nilipopaza sauti yangu, nikalia, akaacha nguo yake kwangu akakimbia nje.”

Unapoendelea kufuatilia maisha ya Yusufu hata kule ugenini utakubaliana nani kwamba sio ndugu zake tu, lakini ni shetani anahusika kufuatilia vazi la Yusufu kwani hata watu wasiomjua wageni bado waliendelea kuandama nguo au vazi jingine la Yusufu katika nyumba ya Potifa ili waharibu kile ambacho Mungu amekikusudia,  makusudi ni kuwa maisha ya Yusufu yawe matatani na asipate nafasi kabisa ya kulitumikia shuri la Mungu, vazi la pili la yusufu linaingia matatani sasa Yusufu ana mavazi ya kifungwa gerezani hata hivyo bado neema ya Mungu ilikuwa pamoja naye hata akiwako kule gerezani  kwa kuwa yeye ana karama ya usimamizi ona

Mwanzo 39:21-23 “Lakini BWANA akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza. Mkuu wa gereza akawatia mkononi mwa Yusufu watu wote waliofungwa, waliomo gerezani; na yote yaliyofanyika humo ndiye aliyeyafanya. Wala mkuu wa gereza hakuangalia neno lililoko mkononi mwa Yusufu; kwa kuwa BWANA alikuwa pamoja naye. BWANA akayafanikisha yote aliyoyafanya

Yusufu katika vazi jipya

Hata pamoja na mapito yote aliyoyapitia Yusufu Bado Mungu alikuwa Pamoja naye, Mungu atakuwa pamoja nasi wakati wote katika kuhakikisha ya kuwa mpango wake unatimizwa kwetu, Yusufu hatimaye aliweza kutumia kipawa chake kutafasiri ndoto na hatimaye alitafasiri ndoto ya Farao ambayo ilimpatia nafasi kubwa sana na akalitimiza kusudi la Mungu

Mwanzo 41:39-44 “Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe. Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe. Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri. Farao akavua pete yake ya muhuri mkononi mwake, akaitia mkononi mwa Yusufu; akamvika mavazi ya kitani nzuri, na kumtia mkufu wa dhahabu shingoni mwake. Akampandisha katika gari lake la pili alilokuwa nalo. Na watu wakapiga kelele mbele yake, Pigeni magoti. Hivyo akamweka juu ya nchi yote ya Misri. Farao akamwambia Yusufu, Mimi ni Farao, na bila amri yako, mtu asiinue mkono wala mguu katika nchi yote ya Misri.”

Kumbe wote tunaweza kukubaliana wazi kuwa vazi la Yusufu lilikuwa lina uhusiano mkubwa sana na nafasi aliyokuwa nayo, Mungu alikuwa amekusudia kutimiza kusudi Fulani ndani yake Sasa sio baba yake tu wala sio Mungu pekee farao pia anamvika mavazi Yusufu kutoka gerezani saa anavikwa mavazi ya kifalme anapewa na mamlaka ili aweze kutimiza hivyo kusudi kubwa la Mungu

Mambo ya kujifunza kutoka katika vazi la Yusufu

1.       Vazi la sifa njema – Yusufu alitengenezewa vazi la kwanza na Baba yake kwa sababu alikuwa ni mtoto mwenye sifa njema kuliko wengine alipata kibali kwa baba yake, alipata neema ni vazi la upendeleo, ni sifa hii njema iliyoweza kuinua chuki na ibilisi alikusudia kuiharibu,

 

Mwanzo 37:3-4 “Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani.”

 

Yusufu alifanyiwa hila nyingi sana za kibinadamu kupitia ndugu zake lakini tunajifunza ya kuwa kusudi la Bwana ndilo litakalosimama, ikiwa Mungu amekukusudia Heshima hata iwe gerezani heshima yako itabaki pale pale

 

Mithali 19:21 “Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini shauri la Bwana ndilo litakalosimama.”Mavazi yake yalichafuliwa lakini Mungu alimvisha mavazi ya Kimisri na kumuinua juu akitumia farasi wa farao na Pete ya farao, Nataka nikuhakikishie ya kuwa ukisimama na Mungu hakuna mtu atafanikiwa katika hila yake ya aina yoyote.

 

2.       Vazi la utumwa – Ni ukweli ulio wazi kuwa vazi la Yusufu ilichanwa chanwa na kuharibiwa na kuchafuliwa kwa damu na Yakobo alionyeshwa ili atambue kama kanzu ile ni ya mwanaye Mwanzo 37:31-34 “Wakaitwaa kanzu ya Yusufu, wakachinja mwana-mbuzi, na kuichovya kanzu katika damu. Wakaenda nayo ile kanzu ndefu, wakamletea baba yao, wakasema, Tumeona hii; basi, utambue kama kanzu hii ni ya mwanao, ama siyo. Akaitambua, akasema, Ndiyo kanzu ya mwanangu, mnyama mkali amemla; bila shaka Yusufu ameraruliwa. Yakobo akararua mavazi yake, akajivika gunia viunoni, na kumlilia mwanawe siku nyingi.”

 

Yusufu alipata vazi lingine huko utumwani alinunuliwa kama mtumwa wa amrijeshi mkuu wa farao alivikwa mavazi ya kitumwa ili amtumikie mtu, lilikuwa vaza la anasa na lilikuwa vazi la tama lakini Yusufu aliishinda tamaa, aliushinda ulimwengu, alimuheshimu Mungu hata katika mazingira magumu nay a ugenini, Mungu huwaheshimu wale wanaomuheshimu  Yusufu alimuheshimu Mungu kila alipokuwepo, alitambua ya kuwa anapaswa kuwa mwaminifu kwa wanadamu na kwa Mungu pia, aliikataa dhambi nimtendeje Bwana Mungu wangu dhambi kubwa namna hii, aliamua kumuheshimu Mungu katika maisha yake alijihami na ubaya wa kila namna na kwa sababu hiyo hatimaye kwa uvumilivu mkubwa alivuna matunda yake yaliyokusudiwa

 

1Samuel 2:30 “Kwa sababu hiyo, Bwana, Mungu wa Israeli, asema, Ni kweli, nalisema ya kuwa nyumba yako, na nyumba ya baba yako itakwenda mbele zangu milele; lakini sasa Bwana asema, Jambo hili na liwe mbali nami; kwa maana wao wanaoniheshimu nitawaheshimu, na wao wanaonidharau watahesabiwa kuwa si kitu.”

 

3.       Vazi la Heshima – lolote linalotokea katika maisha yetu liko chini ya utawala wa Mungu hata pale watu wanapotutendea uovu na hila tukumbuke tu ya kuwa Mungu ndiye anayetawala, Pamoja na mapito yote uaminifu na uvumilivu ulimleta Yusufu katika heshima kubwa sana alivikwa mavazi ya kifahari na kuinuliwa na watu wote kuinamaa mbele zake ona

 

Mwanzo 41:41-42 “Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri. Farao akavua pete yake ya muhuri mkononi mwake, akaitia mkononi mwa Yusufu; akamvika mavazi ya kitani nzuri, na kumtia mkufu wa dhahabu shingoni mwake.”

Hitimisho:

Mungu anao mpango Madhubuti wa kumuheshimu kila mmoja wetu, ni wajhibu wako kuhakikisha ya kuwa unatunza sifa njema ulizonazo, huku ukitambua ya kuwa, Shetani atakupiga vita akiwatumia watu, jilinde na kuhakikisha kuwa unaendelea kuyatunza maisha yako, haijalishi ni mapitio magumu kiasi gani unayapitia.haijalishi uko sehemu ya ugenini ambako watu hawakuoni kumbuka ya kuwa Mungu anakuona na anataka wewe umuonyeshe heshima na Mungu atakuwa pamoja nawe  Mpango wake Mungu ni kutaka kukuheshimu na Mungu analo vazi, anao farasi anayo mavazi na anao watakaokutangaza pale utakapoitunza heshima inayokusudiwa kwako na Mungu na wazazi wako na ulimwengu , Bado Mungu anamkusudia kila mmoja wetu kuvikwa mavazi ya heshima kubwa

Esta 6:7-10 “Basi Hamani akaingia. Mfalme akamwambia, Afanyiziwe nini yule ambaye mfalme apenda kumheshimu? Hamani akasema moyoni mwake, Ni nani ambaye mfalme apenda kumheshimu kuliko mimi? Basi Hamani akamwambia mfalme, Yule ambaye mfalme apenda kumheshimu, na aletewe mavazi ya kifalme ambayo mfalme amezoea kuyavaa, na farasi ambaye mfalme humpanda mwenyewe, ambaye ametiwa taji ya kifalme kichwani; na yale mavazi na yule farasi akabidhiwe mkononi mmojawapo wa maakida wa mfalme aliye mstahiki; ili makusudi amvike yule ambaye mfalme apenda kumheshimu, na kumrakibisha juu ya farasi kuipitia njia kuu ya mjini, na kupiga mbiu mbele yake, kusema, Hivyo ndivyo atakavyofanyiziwa mtu yule ambaye mfalme apenda kumheshimu. Basi mfalme akamwambia Hamani, Hima! Twaa mavazi na farasi kama ulivyosema, ukamfanyizie vivyo hivyo Mordekai, Myahudi, aketiye mlangoni pa mfalme; lisipungue neno lo lote katika yote uliyoyasema.” Ni ahadi ya Mungu kwamba kila mtu atakayeshida tapata heshima kubwa sio hapa duniani tu bali na mbinguni pia

Ufunuo 3:5 “Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake.”

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Jumatatu, 3 Oktoba 2022

Haki yako ya Mzaliwa wa Kwanza!

Waebrania 12:16-17 “Asiwepo mwasherati wala asiyemcha Mungu, kama Esau, aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwa ajili ya chakula kimoja. Maana mwajua ya kuwa hata alipotaka baadaye kuirithi baraka, alikataliwa (maana hakuona nafasi ya kutubu), ijapokuwa aliitafuta sana kwa machozi.”



Utangulizi

Haki ya Mzaliwa ni haki ya kimila, kitamaduni na kiroho anayoipata mtu kutokana na kuzaliwa au mfululizo wa kuzaliwa kwake, Haki hizi zinaweza kumpa mtu, kwa mfano uraia kutokana na mahali ulipozaliwa au walipozaliwa wazazi wake, au kupokea sehemu ya mali na heshima kutoka katika familia yake kufuatana na mpangilio wa kuzaliwa kwake. Haki hii inaweza pia kumpatia mtu urithi wa kifalme kama anatokea katika familia za kifalme!

Katika maandiko Haki ya mzaliwa ilihusiana moja kwa moja na kijana wa kiume aliyezaliwa kwanza katika familia kuwa na haki ya kurithi mali au heshima na mamlaka ya baba yake mara mbili zaidi kuliko watoto wengine, Katika Israel, Kwa mfano kila mtoto alipokea sehemu fulani ya urithi wa mali za baba yake lakini mtoto wa kwanza alipokea mara mbili zaidi kuliko wengine pamoja na uongozi wa Familia.

Mwanzo 48:21-22 “Israeli akamwambia Yusufu, Angalia, mimi ninakufa, lakini Mungu atakuwa pamoja nanyi, naye atawarudisha mpaka nchi ya baba zenu. Nami nimekupa wewe sehemu moja zaidi kuliko ndugu zako, niliyoitwaa katika mikono ya Waamori, kwa upanga wangu na upinde wangu.”

Haki ya kuzaliwa kwanza kwa kawaida ilipaswa kuwa ya Mzaliwa wa kwanza hata kama umezaa na mwanamke usiyempenda, mtoto wa kwanza alihesabika kama mwanzo wa nguvu zako yeye ni Malimbuko ya uzao wako  kwa hivyo maandiko yaliagiza kutazamwa kwa jicho la tofauti kwa mzaliwa wa kwanza katika familia ona  

Kumbukumbu la Torati 21:15-17 “Akiwa mtu yuna wake wawili, mmoja ampenda, mmoja hampendi, nao wamemzalia watoto, ampendaye na asiyempenda wote wawili; na yule mzaliwa wa kwanza akiwa ni wa mke asiyependwa; ndipo itakapokuwa ya kwamba siku atakayowarithisha wanawe alivyo navyo, asimweke mwana wa ampendaye kuwa mzaliwa wa kwanza mbele ya mwana wa asiyempenda, naye ndiye mzaliwa wa kwanza huyu; lakini amkubali mzaliwa wa kwanza mwana wa yule asiyempenda, kwa kumpa mafungu mawili katika vyote alivyo navyo; kwa maana ndiye mwanzo wa nguvu zake; haki ya mzaliwa wa kwanza ni yake yeye.”

Neno Mzaliwa wa kwanza katika Lugha ya kiyunani ilihusiana zaidi na mfululizo wa kimamlaka kutoka juu kwenda chini mfululizo huu unaitwa itifaki, neno la kiyunani linalotumika kuelezea kuhusu mzaliwa wa kwanza ni “PROTOTOKOS”ambalo maana yake ni wa kwanza katika cheo, kwa hiyo mamlaka ya uzaliwa wa kwanza ingeweza kuhama hata kwa mtoto mwingine kama kijana wa kwanza hangekuwa na nidhamu, au angefanya mambo ya kipuuzi

Vita vya uzaliwa wa kwanza.

Katika ulimwengu wa kiroho shetani anapigana sana vita  na haki za mzaliwa wa kwanza kwa sababu Mzaliwa wa kwanza ndiye anayekuwa mlango wa Baraka kwa ndugu zake wote, kila mzaliwa wa kwanza alikuwa ni mali ya Mungu ona Hesabu 3:12-13 “Mimi, tazama, nimewatwaa Walawi na kuwatoa kati ya wana wa Israeli badala ya wazaliwa wa kwanza wote wafunguao tumbo katika wana wa Israeli; na hao Walawi watakuwa wangu; kwa kuwa hao wazaliwa wa kwanza wote ni wangu; katika siku ile niliyowapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri nikajiwekea wakfu wazaliwa wa kwanza wote wa Israeli, wa wanadamu na wa wanyama; watakuwa wangu; mimi ndimi Bwana.”

Kwa kuwa wazaliwa wa kwanza ni mali ya Mungu ni urithi wa Mungu, ni Makuhani, ni viongozi wa ibada, ni warithi wa Baraka za kifamilia, ni ishara ya mafanikio ya familia ni nguvu ya familia ni akiba, ni mtazamo wa baadaye wa familia nan i mali ya Mungu, kamwe shetani hangeweza kufurahia na kupenda kuona mpango wa Mungu unapitia kwa wazaliwa wa kwanza kwa hiyo kuna vita katika ulimwengu wa roho kwaajili ya wazaliwa wa kwanza, shetani angefurahia kuharibu kila mzaliwa wa kwanza kiadilifu, kitaaluma na kimafanikio ili kudhoofisha familia ambazo Mungu amekusudia kuzibarikia, kwa hiyo kila mzaliwa wa kwanza anapaswa kujua kuwa iko vita katika maisha yake.

Ni muhimu kufahamu kuwa kuupata urithi, kungehitaji uvumilivu mkubwa na mapambano ya hali ya juu, shetani anafahamu kuwa kuna urithi uolioko mbele yako na hivyo atahakikisha kuwa anapambana kwa kadiri awezavyo ili ikiwezekana upoteze, vita kati ya Mungu na Farao kule Misri kimsingi ilikuwa ni vita ya kugombea Mzaliwa wa Kwanza, Israel ni taifa ambalo lina haki ya mzaliwa wa Kwanza miongoni mwa mataifa ya dunia, lakini Farao hakutaka kuwaachia alitaka wawe watumwa wake awatumikishe hivyo kimsingi kulikuwa na vita kali kwaajili ya kumgombea mzaliwa wa kwanza  na ndio maana Mungu alimuonya Farao kumuachia Israel kwani vinginevyo angwewaadhibu wazaliwa wa kwanza wote wa mwanadamu na mnyama katika taifa la Misri ili Israel auweze kuwa huru ona

Kutoka 4:22-23 “Nawe umwambie Farao, BWANA asema hivi, Israeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wa kwanza wangu; nami nimekuambia, Mpe mwanangu ruhusa aende, ili apate kunitumikia, nawe umekataa kumpa ruhusa aende; angalia basi, mimi nitamwua mwanao, mzaliwa wa kwanza wako.”  

Mzaliwa wa kwanza alikuwa ni mlinzi wa mali au urithi wa mali za wazee wao kizazi hata kizazi na walipaswa kuhakikisha kuwa haki ile inatunzwa kwa gharama yoyote ili isipotee Shetani angetamani wakati wote Mzaliwa wa kwanza apoteze,

1 Wafalme 21:1-3 “Ikawa baada ya hayo, Nabothi Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu katika Yezreeli, karibu na nyumba ya kifalme ya Ahabu mfalme wa Samaria. Ahabu akasema na Nabothi, akamwambia, Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, maana ni karibu na nyumba yangu; nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu lililo zuri zaidi; au ukipenda, nitakupa fedha sawasawa na thamani yake. Nabothi akamwambia Ahabu, Bwana apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu

 Kila mtu aliyemwamini Bwana Yesu kuwa bwana na Mwokozi ni mzaliwa wa kwanza, na una haki na Baraka zilezile zilizokusudiwa kwa Ibrahimu, Isaka na Yakobo, kwa msingi huo Mwandishi wa kitabu cha waebrania alikuwa akiwaasa Wakristo wa kiyahudi, kutokurudia nyuma na kuiacha imani kwani kufanya hivyo kungekuwa hakuna tofauti na mwesherati au mtu asiyemcha Mungu kama ilivyokuwa kwa Esau.

Jinsi ya kuilinda haki ya mzaliwa wa Kwanza.

Kwa kuwa haki ya mzaliwa wa kwanza ni jambo linaloweza kuponyoka kutoka katika mikono ya mtu mmoja kwenda kwa mwingine  na tumeona wazi kuwa shetani kama mpinzani hangependa kuona makusudi ya Mungu yakitimizwa kwa wazaliwa wa kwanza hatuna budi kuhakikisha ya kuwa unailinda haki hiyo kwa gharama yoyote, Maandiko yanatuonya kuwa asiwepo mweshatari, wala mtu asiyemcha Mungu kama Esau aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwaajili ya chakula kimoja hii ina maana gani? Maana yake ni kuwa Esau sio kuwa alifanya uasherati lakini lugha inayotumika hapo inamaanisha kubadilisha kitu kikubwa sana na cha thamani kwa kitu kidogo sana kisicho na tamani, tabia ya aina hii inafananishwa na uasherati, uashetari unaweza kumuharibia mtu thamani yake na heshima yake kwa muda mfupi sana, maandiko yanatutaka tulinde kila kitu ambacho tunakiweka katika idadi ya vitu vya thamani sana duniani. Mambo yanayohitaji kupewa kipaumbele yapewe kipaumbele, Mfano watu wanapokuja shuleni, wazazi wanakuwa wamewekeza fedha ambazo wanazitafuta kwa hali na mali, ili mwanafunzi asome, lakini inasikitisha sana kama mwanafunzi badala ya kusoma yeye akawa anapoteza Muda na kucheza huku anapoteza fedha ya wazazi wake na kuharibu maisha yake ya baadaye kwa njia za kiupuuzi, mtu anaweza kufanya jambo la kijinga tu na likamkosesha kazi,  wakati wote tuyape kipaumbele maswala ambayo ni ya muhimu katika maisha yetu na kujihami na mambo yasiyo ya msingi, majukumu yoyote unayopewa hapa dunaini hakikisha kuwa unayatimiza na kuyatetendea haki kwa kujituma kwa gharama kubwa, mwenendo wako na uadilifu wako na tahadhari ni za muhimu sana katika kuhakikisha kuwa unatunza sana kile ambacho Mungu anakitarajia katika maisha yako! Biblia imejaa mifano ya watu waliopoteza haki yao ya uzaliwa wa kwanza kwa njia za kipuuzi na za kusikitisha sana ona :-

-          Mwanzo 9:20-26 “Nuhu akaanza kuwa mkulima, akapanda mizabibu; akanywa divai, akalewa; akawa uchi katika hema yake. HAMU, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje. Shemu na Yafethi wakatwaa vazi, wakalitanda mabegani mwao wote wawili, wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao; na nyuso zao zilielekea nyuma, wala hawakuuona uchi wa baba yao. Nuhu akalevuka katika ulevi wake, akajua mwana wake mdogo alivyomtendea. Akasema, Na alaaniwe Kaanani; Atakuwa mtumwa kabisa kwa ndugu zake. Akasema, Na atukuzwe BWANA, Mungu wa Shemu; Na Kaanani awe mtumwa wake.”

-           

-          Mwanzo 49:3-4 “REUBENI, u mzaliwa wangu wa kwanza, Nguvu zangu, na malimbuko ya uwezo wangu. Umewapita wengine kwa ukuu na kwa nguvu. Umeruka mpaka kama maji, basi usiwe na ukuu, Kwa sababu ulikipanda kitanda cha baba yako, Ukakitia unajisi; alikipandia kitanda changu.”

-           

-          Mwanzo 25:29-32 “Yakobo akapika chakula cha dengu. ESAU akaja kutoka nyikani, naye alikuwa amechoka sana. Esau akamwambia Yakobo, Tafadhali, unipe hicho chakula chekundu nile, kwa kuwa ninazimia mimi. Kwa hiyo walimwita jina lake Edomu.Yakobo akamwambia, Kwanza niuzie leo haki yako ya mzaliwa wa kwanza. Esau akasema, Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini haki hii ya uzazi?

Pigania urithi wako !

Wako watu wanaotajwa kama Mashujaa walioishi wakati wa Daudi watu hawa walikuwa Hodari sana katika kuutetea urithi wa bwana na kuhakikisha kuwa watu wengine wanafaidiaka kwa ujasiri wao, ni imani yangu Kuwa Mungu atakusaidia wewe na mimi tuweze kupigania kile ambacho Mungu ametukabidhi kwa gharama yoyote

2Samuel 23:8-12 “Haya ndiyo majina ya mashujaa aliokuwa nao Daudi; Yashobeamu Mhakmoni,mkuu wa maakida ;huyo aliliinua shoka lake juu ya watu mia nane waliouawa pamoja.Na baada yake kulikuwa na Eleazari, mwana wa Dodai, Mwahohi, mmojawapo wa wale mashujaa watatu waliokuwa pamoja na Daudi; walipowatukana Wafilisti waliokuwa wamekusanyika huko ili kupigana, na watu wa Israeli walikuwa wamekwenda zao; huyo aliinuka, akawapiga Wafilisti hata mkono wake ukachoka, na mkono wake ukaambatana na upanga; naye Bwana akafanya wokovu mkuu siku ile; nao watu wakarudi nyuma yake ili kuteka nyara tu. Na baada yake kulikuwa na Shama, mwana wa Agee, Mharari; nao Wafilisti walikuwa wamekusanyika huko Lehi, palipokuwapo konde lililojaa midengu; nao watu wakawakimbia Wafilisti; ila huyo alisimama katikati ya konde lile, akalipigania, akawaua Wafilisti; naye Bwana akafanya wokovu mkuu.”

 

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa Wajenzi Mwenye Hekima!