Jumatatu, 17 Oktoba 2022

Usibishane na Punda


Tito 3:9-11 “Lakini maswali ya upuzi ujiepushe nayo, na nasaba, na magomvi, na mashindano ya sheria. Kwa kuwa hayana faida, tena hayana maana. Mtu aliye mzushi, baada ya kumwonya mara ya kwanza na mara ya pili, mkatae; ukijua ya kuwa mtu kama huyo amepotoka, tena atenda dhambi, maana amejihukumu hatia yeye mwenyewe.”


Utangulizi:

“Mtu mwenye hekima ni yule anayejifanya mjinga wakati mtu mpumbavu anapojifanya kuwa ana hekima”

Siku moja Punda alimwambia Chui kwamba Majani yote yana rangi ya bluu!

Chui akajibu akamwambia Punda hapana Bwana majani yote ni ya Kijani!

Wakabishana sana huyu akisema ni bluu na huyu akisema ni kijani, mwisho waliona wamwendee mfalme wao ili waweze kuamua kwamba ni nani yuko sahihi,  Mfalme wao yaani mfalme wa Nyika Simba,  Kabla hawajafika msituni walimkuta mfalme wao yaani Simba akiwa ameketi na kutulia katika kiti chake cha ufalme !

Wakamsalimia wakisema Mtukufu mfalme Simba tuambie majani yana rangi ya kijani au yana rangi ya blue?

Simba akajibu, Kwa kweli majani yana rangi ya bluu!, Punda akadakia si nilikuambia chui majani yana rangi ya blue wewe ukanibishia  unasikia sasa? Lakini chui aliendelea kubisha na kusema kwa hakika jamani majani ni ya rangi ya kijani

Ndipo mfalme Simba akasema Natangaza adhabu kali kwa chui kuwa utapaswa kukaa kimya na kutokusema chochote kwa miaka mitano!, Punda aliruka juu na kufurahia sana kisha akaenda zake

Majani ni ya bluu?

Chui alikubaliana na adhabu aliyopewa lakini alitaka kumuuliza Mfalme swali moja wakiwa wamebaki peke yao!

Alimwambia Mtukufu Simba mfalme wa nyika kwanini unanipa adhabu kali ili hali unajua ukweli kabisa kuwa majani ni ya kijani?

Simba alimjibu chui kuwa ni ukweli usiopingika kuwa majani ni ya kijani!

Sasa kwa nini umeniadhibu aliuliza chui?

Simba alijibu!

Kwa habari ya kuwa majani ni ya kijani au ni ya bluu sijakuadhibu

Adhabu yako imekuja kwa sababu sio rahisi kwa mnyama mwenye akili kama wewe kupoteza muda wako kubishana na mnyama kama punda, zaidi ya yote kukubali kuja kwa mfalme na kumsumbua kwa maswali ya kijinga, huko ni kupoteza Muda kubishana na wajinga na wazushi, wasiojali ukweli wa mambo wala uhalisia wa vitu, zaidi wanajali tu washinde, waliamini katika uzushi na uwongo, kumbuka siku zote usipoteze muda wako kujadili mambo ya kipuuzi na yasiyo na maana wala kubishania mambo ya kipuuzi.

Kuna watu ambao huwa hawajali na huwa hawaoni, hata kama ushahidi uko wazi mbele yao na wanaona kwa macho yao hawana uwezo na moyo wa kukubali uhalisia, wao ni vipofu katika nafsi zao, wamepofushwa fikra zao, wabinafsi, wamejaa chuki na hila na wakati wote wanataka kuonekana kuwa wako sahihi hata kama ukweli ni kuwa hawako sahihi

Wakati ujinga unapounguruma, Hekima hukaa kimya, ukimya wa Hekima na mani ya hekima ni ya muhimu kuliko kujipotezea muda na wajinga!

“Mtu mwenye hekima ni yule anayejifanya mjinga wakati mtu mpumbavu anapojifanya kuwa ana hekima”

Translated and added value by

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!



Hakuna maoni: