1Samuel 17:4-11 “Ndipo akatoka shujaa katika kambi ya Wafilisti, aliyeitwa
Goliathi, wa Gathi, ambaye urefu wake ulikuwa mikono sita na shibiri moja.
Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani, tena amevaa darii ya shaba; na uzani wake
ile darii ya shaba ulikuwa shekeli elfu tano za shaba. Tena amevaa mabamba ya
shaba miguuni mwake, naye alikuwa na mkuki wa shaba kati ya mabega; yake. Na
mti wa fumo lake ulikuwa kama mti wa mfumaji; na kichwa cha mkuki wake kilikuwa
shekeli mia sita za chuma uzito wake; na mtu aliyemchukulia ngao yake
akamtangulia. Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia,
Mbona mmetoka kupanga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa
Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi. Kama akiweza kupigana nami na
kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda yeye na kumwua, ninyi
mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia. Yule Mfilisti akasema, Nayatukana leo
majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane. Basi Sauli na Israeli wote waliposikia
maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana.”
Utangulizi:
Goliath ni moja ya watu
wanaotajwa katika Biblia katika kitabu cha Samuel akielezewa kama jitu kubwa
sana ambalo lilipigwa na kijana mdogo sana aitwaye Daudi, kwa silaha dhaifu
sana, Kuja kwa Daudi ni matokeo ya Sauli pamoja na majeshi yake yote kufadhaika
na kuogopa sana kupigana na askari huyo komandoo wa kikosi cha wafilisti, Leo
hii stori ya Daudi na Goliath imekuwa ni moja ya mfano unaotumiwa sana katika
kutia moyo watu wa kila aina kuondoa hofu na kukabiliana na tukio lolote gumu
au linaloonekana lenye kutisha hata kama inaonekana kibinadamu kuwa
tunakabiliana na kitu kigumu lakini tukiwa tuna Mungu aliye hai ndani yetu!
1Samuel 17:45 “Ndipo Daudi akamwambia yule
Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia
wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana.”
Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo;-
·
Mambo ya
kutisha
·
Jinsi ya
kukabiliana na mambo ya kutisha!
·
Siri ya
kukabiliana na mambo ya kutisha.
Mambo ya kutisha.
Tunapozungumzia mambo ya kutisha
katika nyakati za leo, tunaweza kuzungumzia hali yoyote ngumu na ambayo kwa
akili za kibinadamu ni ngumu kuikabili katika hali ya kawaida, hali hizo zote
ngumu leo, au zenye kutisha na kuogopesha zinaweza kufananishwa na ukubwa
aliokuwa nao adui wa Israel yaani Goliath, Kwa mujibu wa maelezo ya Biblia
tunaambiwa kuwa Goliath alikuwa na urefu wa mikono sita na shubiri moja kwa
vipimo vya leo ni kama Goliath
alikuwa na urefu wa futi tisa na nusu, wakati watu wengine wanakisiwa kuwa na
futi kama tano na inchi tatu au sita kwa wale wenye sifa ya urefu Gioliath
alikuwa ni mrefu sana kwenda juu kuliko wanadamu wa kawaida hivyo lilikuwa jitu
kwelikweli, lakini pia tunaambiwa alikuwa na Kofia ya kivita Chepeo ya shaba yenye uzito wa Paundi 66, kumbuka Paundi moja ni sawa na kilo
0.454 hivyo Paundi 66 ni sawa na Kilo 29 au 30, Pia jamaa alikuwa na
koti la kivita dirii ya shaba yenye uzito wa Shekel 5000 sawa na Paundi
175 ambayo ni sawa na kilo 79 au 80 hivi,
hali kadhalika mkuki wake kile kicha tu pekee kilikuwa na uzito wa Paundi 20 yaani sawa na kilo 9-10 na kumbuka huo ulikuwa ni
kishwa tu cha mkuki wake, kwa kifupi tu Goliathi lilikuwa ni jitu la kutisha
kimsingi Goliath alikuwa ni kama mashine ya kifo ambaye kwa kumuona tu huwezi
kurusha mguu wako vitani, lakini kwa cv uzoefu wake huyu alikuwa mzoefu wa vita
tangu utoto wake
1Samuel 17:33 “Sauli akamwambia Daudi,
Huwezi wewe kumwendea Mfilisti huyu upigane naye; maana wewe u kijana tu; na
huyu ni mtu wa vita tangu ujana wake.”
Unaweza kuona na licha ya
kuwa na uzoefu wa vita Goliath alikuwa anajiamini na alikuwa na maneno ya hivyo
na ya jeuri na kila aliyemsikia na kumuona aliyeyuka moyo! Haya ni mambo ya
kutisha, Yawezekana katika maisha
yetu tukawa tunakutana na mambo magumu ambayo kwa akili ya kibinadamu hayawezi
kukabilika wala hayaonyeshi upenyo, hayo ni mambo ya kutisha na hatupaswi
kuogopa kwani neno la Mungu linatupa matumaini kuwa iko njia ya kushinda!.
Tunapomuangalia Daudi tunaweza kugundua kuwa yako mambo Muhimu yaliyopelekea
akubali kupambana na lijitu na akaweza kufanikiwa!
Jinsi ya kukabiliana
na mambo ya kutisha!
1. Alifikiri juu ya kulinda Heshima yake.
Daudi alifikiri
juu ya kulinda heshima yake na na ya Mungu wake, Mfalme alikuwa ameahidi kuwa
mtu atakayetoka na kumpiga mfilisti huyu kwanza angefanywa kuwa tajiri sana,
pili angeinuliwa kwa kuingia katika familia ya kifalme na kuketi katika meza
kuu pamoja na mfalme kwa kuozwa binti wa kifalme jambo ambalo linempa haki hiyo
na zaidi ya hayo Familia yake ingekuwa huru katika maswala ya kulipa Kodi.
Unaweza kuona
1Samuel 17:25-27 “Watu wa Israeli wakasema, Je! Mmemwona mtu
huyu aliyepanda huko? Hakika ametokea ili awatukane Israeli; basi, itakuwa, mtu
yule atakayemwua, mfalme atamtajirisha kwa utajiri mwingi, naye atamwoza binti
yake, na kuifanya mbari ya baba yake kuwa huru katika Israeli., Daudi akaongea na
watu waliosimama karibu, akisema, Je! Atafanyiwaje yeye atakayemwua Mfilisti
huyo, na kuwaondolea Israeli aibu hii? Maana Mfilisti huyu asiyetahiriwa ni
nani hata awatukane majeshi ya Mungu aliye hai? Nao watu wakamjibu vivyo hivyo,
wakisema, Ndivyo atakavyofanyiwa mtu yule atakayemwua.”
Katika kila niia
ya mafanikio kwa kawaida kuna jambo gumu linalosimama ambalo ni lazima upambane
kuliangusha ndipo uweze kutoboa, Israel wasingeliweza kuingia katika inchi ya
mkanaani nchi ya maziwa na asali bila kuwapiga wakazi wake, wakati wote njia ya
mafanikio yako haiwezi kuwa nyepesi, lakini kumbuka kuna utajiri kuna heshima
kuna uhuru ambao utapatikana kama tu jitu litaanguka, hivyo ni lazima ujipe
moyo na ukubali kukabiliana na giant nani ajuaye ya kuwa wewe ndie
utakayeikomboa Familia yako na taifa lako pigana kwaajili ya kuweka heshima,
haiwezekani ukubali kupuuzwa pigana na kila kinachosimama mbele yako na Mungu
atakuwa pamoja nawe!
2.
Alifikiri
juu ya kulinda Heshima ya Mungu.
Israel lilikuwa
ni taifa ambalo Mungu amewachagua ili waweze kuwa Baraka kwa mataifa yote,
kushindwa kwa Israel ilikuwa ni sawa na kushindwa kwa Mungu wao na Mungu wa
baba zao, Mungu wa Ibrahimu na Isaka na Yakobo angetukanwa, Mtu huyu anayetisha
lisha ya kuwatukana waisrael lakini pia alimtukana Mungu aliye hai, wakati
mwingine kushindwa kwetu, kuanguka kwetu, umasikini wetu na kushindwa kwetu
kufanikiwa kunafanya ionekane kuwa Mungu wetu ameshindwa na jina lake kutukanwa
Hivyo Daudi alikuwa akipigana kwaajili ya utukufu wa Mungu pia
1Samuel 17: 45-47 “Ndipo
Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na
mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi
ya Israeli uliowatukana. Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami
nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na
wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya
kuwa yuko Mungu katika Israeli. Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba
Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana, naye atawatia
ninyi mikononi mwetu.”
Kwaajili ya jina
la Mungu wetu, ili kuitunza heshima yake hatuna budi kumuomba Mungu atukuzwe
hata kupitia changamoto zinazotukabili, ijulikane ya kuwa changamoto
unayoipitia hata kama inatisha kiasi gani ikishughulikiwa jina la Mungu wetu
litatukuzwa na kuinuliwa Daudi aliona hana budi kushinda kwaajili ya jina la
Mungu ili wafilisti waelewe kuwa Israel hata kama haina silaha wala nguvu
inashinda kwa jina la Mungu aliye hai.
3.
Alifikiri
juu ya kupoteza uhuru na kuwa watumwa.
Hakuna kitu
kinauma duniani kama kuwa mtumwa au kupoteza Uhuru, wazee wetu waliopigania
uhuru, walikataa kila aina ya ugandamizaji
na uonevu na ndio maana walidai uhuru kwa nguvu zao zote, sababu kubwa
ilikuwa ni kukataa uonevu na kudhalilishwa, wapigania uhuru wote walikuwa na
roho inayofanana, Jomo Kenyatta, Julius Nyerere, Patrice Lumumba, Kwame
Nkuruma, Haile Selasie, Robert Mugabe, Keneth Kaunda, Abeid Karume, Samora
Machel, Nelson Mandela, Oliva Tambo, Na mwimbaji Bob Marley walikataa dhana ya
utumwa na kuwa na roho moja yenye kuitaka Afrika iweze kuwa huru kujitawala na
kujiamulia mambo yake na ndio maana
Mungu aliwaamsha nia na mioyo yao ili
wawe na uchungu na kuwatetea ndugu zao, Mungu aliamsha hari ya Daudi na
kukubali kuwa Mwamuzi na mwokozi wa ndugu zake kwa sababu hakutakamkukubali
wawe watumwa wa wafilisti, masharti ya vita hii ilikuwa kama Goliath akimshinda
yule ambaye Israel wangemtoa wangekuwa watumwa wa wafilisti na kama yule ambaye
wangemtoa angemshinda basi wafilsiti wangekuwa watumwa wa Israel ona
1Samuel 17:8 -9 “Naye
akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka
kupanga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli?
Jichagulieni mtu, akanishukie mimi. Kama akiweza kupigana nami na kuniua, sisi
tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda yeye na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa
wetu, na kututumikia.”
Siri ya kukabiliana na mambo ya kutisha.
-
Usikimbie
vita na mambo ya kutisha – hakikisha kuwa unakabiliana na jitu lako lenye
kutisha litokee kabiliaba nalo, jifunze kukabiliana na mambo ya kutisha na
wakati mwingine sio lazima yakukabili bali unaweza hata kuyafuata 1Samuel 17:34-35 “Daudi
akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na
alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo wa lile kundi, mimi
hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia,
humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua.” Uko wakati ambako lazima
umfuatilie adui na uambane naye kule aliko anaweza kukuvamia na kuchukua kila
kilicho chako, kuna wakati katika maisha unaweza kudhulumiwa, adui akachukua
kila kilicho chako, akachukua kipato chako, nyumba yako, familia yako, muda
wako na hata afya yako, lazima uwe mkali usikubali kudhalilika pambana bila
kujali ukubwa wa tatizo pambana kwa jina la Bwana wa majeshi, hakuha kukimbia
wengine wakikimbia we baki pambana mpaka senti ya mwisho! 1Samuel 17:24 “Na watu wote wa Israeli
walipomwona yule mtu wakakimbia, wakaogopa sana.” Huwezi kuwa
kiongozi wa Bendi asiyependa Muziki.
-
Usiogope
– Hata kama adui yako anaoneana mwenye kutisha kiasi gani haupaswi kuogopa
neno usiogope katika Biblia limeandikwa mara 366 sawa na siku zote za mwaka
mzima hii maana yake hatupaswi kuogopa, kuwaogopa na badala yake ujae imani
umtegemee Mungu tu jua ya kuwa Mungu yuko nawe na atakusaidia 2Wafalme 1:15 “Malaika
wa Bwana akamwambia Eliya, Shuka pamoja naye; usimwogope. Akaondoka, akashuka
pamoja naye hata kwa mfalme.” Kuna wakati maandiko yanatuambia USIMUOGOPE hii kama inahusu mtu na pia
inatuambia USIWAOGOPE kama ni kundi kubwa
-
Kumbukumbu
20:1 “Utokapo kwenda vitani kupigana na adui zako,
na kuona farasi, na magari, na watu wengi kuliko wewe, usiwaogope; kwa kuwa
Bwana Mungu wako, yu pamoja nawe, aliyekukweza kutoka nchi ya Misri.”
-
Maandiko hayatutaki tuwe na hofu kwa sababu
vitani tutaonekana kuwa ni sisi tunaopigana lakini ndani ya mioyo yetu
anayepigana ni Bwana mwenyewe vita sio yako ni vita ya Mungu tunayemuamini na
kumtumikia ona
2Nyakati 20:15 “akasema,
Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; Bwana
awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani
vita si yenu bali ni ya Mungu.”
Hitimisho:-
Silaha zetu zina nguvu kubwa ya
ajabu sana na hatupaswi kuogopa tunajifunza kutoka kwa Daudi ya kuwa hata iweje
au adui aweje Mungu atatupa ushindi mkubwa sana, vita ni yake wala si yetu
inawezekana unayakumbuka mamo haya yote lakini wakati mwingine tunapaswa
kukumbushwa ili kibinadamu tusiogope, usiogope wakati vita vinakukabili kwa
sababu zozote zile.Silaha alizochagua Daudi zilionakana kwa machio ya
kibinadamu kuwa duni kwa kulinganisha na jitu alilokuwa anapigana nalo lakini
Mungu alimpa ushindi
1Samuel 17: 49 “Daudi akatia mkono wake
mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti
katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingilia kipajini, akaanguka chini
kifudifudi.” Daudi alishinda kwa kutumia jiwe moja tu kati yam awe
matano aliyokuwa nayo, silaha za vita vyetu zina uwezo katika Mungu hata
kuangusha ngome ona
2Wakoritho 10: 3-5 “Maana ingawa tunaenenda
katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si
za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha
mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na
tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo;”
Na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni