Waebrania 12:16-17 “Asiwepo mwasherati wala asiyemcha Mungu, kama Esau, aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwa ajili ya chakula kimoja. Maana mwajua ya kuwa hata alipotaka baadaye kuirithi baraka, alikataliwa (maana hakuona nafasi ya kutubu), ijapokuwa aliitafuta sana kwa machozi.”
Utangulizi
Haki ya Mzaliwa ni haki ya
kimila, kitamaduni na kiroho anayoipata mtu kutokana na kuzaliwa au mfululizo
wa kuzaliwa kwake, Haki hizi zinaweza kumpa mtu, kwa mfano uraia kutokana na mahali
ulipozaliwa au walipozaliwa wazazi wake, au kupokea sehemu ya mali na heshima
kutoka katika familia yake kufuatana na mpangilio wa kuzaliwa kwake. Haki hii
inaweza pia kumpatia mtu urithi wa kifalme kama anatokea katika familia za
kifalme!
Katika maandiko Haki ya mzaliwa
ilihusiana moja kwa moja na kijana wa kiume aliyezaliwa kwanza katika familia
kuwa na haki ya kurithi mali au heshima na mamlaka ya baba yake mara mbili
zaidi kuliko watoto wengine, Katika Israel, Kwa mfano kila mtoto alipokea
sehemu fulani ya urithi wa mali za baba yake lakini mtoto wa kwanza alipokea
mara mbili zaidi kuliko wengine pamoja na uongozi wa Familia.
Mwanzo 48:21-22 “Israeli akamwambia Yusufu,
Angalia, mimi ninakufa, lakini Mungu atakuwa pamoja nanyi, naye atawarudisha
mpaka nchi ya baba zenu. Nami nimekupa wewe sehemu moja zaidi kuliko ndugu
zako, niliyoitwaa katika mikono ya Waamori, kwa upanga wangu na upinde wangu.”
Haki ya kuzaliwa kwanza kwa
kawaida ilipaswa kuwa ya Mzaliwa wa kwanza hata kama umezaa na mwanamke
usiyempenda, mtoto wa kwanza alihesabika kama mwanzo wa nguvu zako yeye ni
Malimbuko ya uzao wako kwa hivyo
maandiko yaliagiza kutazamwa kwa jicho la tofauti kwa mzaliwa wa kwanza katika
familia ona
Kumbukumbu la Torati 21:15-17 “Akiwa mtu
yuna wake wawili, mmoja ampenda, mmoja hampendi, nao wamemzalia watoto,
ampendaye na asiyempenda wote wawili; na yule mzaliwa wa kwanza akiwa ni wa mke
asiyependwa; ndipo itakapokuwa ya kwamba siku atakayowarithisha wanawe alivyo
navyo, asimweke mwana wa ampendaye kuwa mzaliwa wa kwanza mbele ya mwana wa
asiyempenda, naye ndiye mzaliwa wa kwanza huyu; lakini amkubali mzaliwa wa
kwanza mwana wa yule asiyempenda, kwa kumpa mafungu mawili katika vyote alivyo
navyo; kwa maana ndiye mwanzo wa nguvu zake; haki ya mzaliwa wa kwanza ni yake
yeye.”
Neno Mzaliwa wa kwanza katika
Lugha ya kiyunani ilihusiana zaidi na mfululizo wa kimamlaka kutoka juu kwenda
chini mfululizo huu unaitwa itifaki, neno la kiyunani linalotumika kuelezea
kuhusu mzaliwa wa kwanza ni “PROTOTOKOS”ambalo
maana yake ni wa kwanza katika cheo, kwa hiyo mamlaka ya uzaliwa wa kwanza ingeweza
kuhama hata kwa mtoto mwingine kama kijana wa kwanza hangekuwa na nidhamu, au
angefanya mambo ya kipuuzi
Vita vya uzaliwa wa kwanza.
Katika ulimwengu wa kiroho
shetani anapigana sana vita na haki za
mzaliwa wa kwanza kwa sababu Mzaliwa wa kwanza ndiye anayekuwa mlango wa Baraka
kwa ndugu zake wote, kila mzaliwa wa kwanza alikuwa ni mali ya Mungu ona Hesabu 3:12-13 “Mimi,
tazama, nimewatwaa Walawi na kuwatoa kati ya wana wa Israeli badala ya wazaliwa
wa kwanza wote wafunguao tumbo katika wana wa Israeli; na hao Walawi watakuwa
wangu; kwa kuwa hao wazaliwa wa kwanza wote ni wangu; katika siku ile
niliyowapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri nikajiwekea wakfu
wazaliwa wa kwanza wote wa Israeli, wa wanadamu na wa wanyama; watakuwa wangu;
mimi ndimi Bwana.”
Kwa kuwa wazaliwa wa kwanza ni
mali ya Mungu ni urithi wa Mungu, ni Makuhani, ni viongozi wa ibada, ni warithi
wa Baraka za kifamilia, ni ishara ya mafanikio ya familia ni nguvu ya familia
ni akiba, ni mtazamo wa baadaye wa familia nan i mali ya Mungu, kamwe shetani
hangeweza kufurahia na kupenda kuona mpango wa Mungu unapitia kwa wazaliwa wa
kwanza kwa hiyo kuna vita katika ulimwengu wa roho kwaajili ya wazaliwa wa
kwanza, shetani angefurahia kuharibu kila mzaliwa wa kwanza kiadilifu,
kitaaluma na kimafanikio ili kudhoofisha familia ambazo Mungu amekusudia
kuzibarikia, kwa hiyo kila mzaliwa wa kwanza anapaswa kujua kuwa iko vita
katika maisha yake.
Ni muhimu kufahamu kuwa kuupata
urithi, kungehitaji uvumilivu mkubwa na mapambano ya hali ya juu, shetani
anafahamu kuwa kuna urithi uolioko mbele yako na hivyo atahakikisha kuwa
anapambana kwa kadiri awezavyo ili ikiwezekana upoteze, vita kati ya Mungu na Farao
kule Misri kimsingi ilikuwa ni vita ya kugombea Mzaliwa wa Kwanza, Israel ni
taifa ambalo lina haki ya mzaliwa wa Kwanza miongoni mwa mataifa ya dunia,
lakini Farao hakutaka kuwaachia alitaka wawe watumwa wake awatumikishe hivyo
kimsingi kulikuwa na vita kali kwaajili ya kumgombea mzaliwa wa kwanza na ndio maana Mungu alimuonya Farao kumuachia
Israel kwani vinginevyo angwewaadhibu wazaliwa wa kwanza wote wa mwanadamu na
mnyama katika taifa la Misri ili Israel auweze kuwa huru ona
Kutoka 4:22-23 “Nawe umwambie Farao, BWANA
asema hivi, Israeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wa kwanza wangu; nami
nimekuambia, Mpe mwanangu ruhusa aende, ili apate kunitumikia, nawe umekataa
kumpa ruhusa aende; angalia basi, mimi nitamwua mwanao, mzaliwa wa kwanza wako.”
Mzaliwa wa kwanza alikuwa ni
mlinzi wa mali au urithi wa mali za wazee wao kizazi hata kizazi na walipaswa
kuhakikisha kuwa haki ile inatunzwa kwa gharama yoyote ili isipotee Shetani
angetamani wakati wote Mzaliwa wa kwanza apoteze,
1 Wafalme 21:1-3 “Ikawa baada ya hayo,
Nabothi Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu katika Yezreeli, karibu na
nyumba ya kifalme ya Ahabu mfalme wa Samaria. Ahabu akasema na Nabothi,
akamwambia, Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, maana ni
karibu na nyumba yangu; nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu lililo
zuri zaidi; au ukipenda, nitakupa fedha sawasawa na thamani yake. Nabothi
akamwambia Ahabu, Bwana apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu”
Kila mtu aliyemwamini Bwana
Yesu kuwa bwana na Mwokozi ni mzaliwa wa kwanza, na una haki na Baraka zilezile
zilizokusudiwa kwa Ibrahimu, Isaka na Yakobo, kwa msingi huo Mwandishi wa
kitabu cha waebrania alikuwa akiwaasa Wakristo wa kiyahudi, kutokurudia nyuma
na kuiacha imani kwani kufanya hivyo kungekuwa hakuna tofauti na mwesherati au
mtu asiyemcha Mungu kama ilivyokuwa kwa Esau.
Jinsi ya kuilinda haki ya mzaliwa wa Kwanza.
Kwa kuwa haki ya mzaliwa wa
kwanza ni jambo linaloweza kuponyoka kutoka katika mikono ya mtu mmoja kwenda
kwa mwingine na tumeona wazi kuwa
shetani kama mpinzani hangependa kuona makusudi ya Mungu yakitimizwa kwa
wazaliwa wa kwanza hatuna budi kuhakikisha ya kuwa unailinda haki hiyo kwa
gharama yoyote, Maandiko yanatuonya kuwa asiwepo mweshatari, wala mtu asiyemcha
Mungu kama Esau aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwaajili ya chakula
kimoja hii ina maana gani? Maana yake ni kuwa Esau sio kuwa alifanya uasherati
lakini lugha inayotumika hapo inamaanisha kubadilisha kitu kikubwa sana na cha
thamani kwa kitu kidogo sana kisicho na tamani, tabia ya aina hii inafananishwa
na uasherati, uashetari unaweza kumuharibia mtu thamani yake na heshima yake
kwa muda mfupi sana, maandiko yanatutaka tulinde kila kitu ambacho tunakiweka
katika idadi ya vitu vya thamani sana duniani. Mambo yanayohitaji kupewa
kipaumbele yapewe kipaumbele, Mfano watu wanapokuja shuleni, wazazi wanakuwa
wamewekeza fedha ambazo wanazitafuta kwa hali na mali, ili mwanafunzi asome,
lakini inasikitisha sana kama mwanafunzi badala ya kusoma yeye akawa anapoteza
Muda na kucheza huku anapoteza fedha ya wazazi wake na kuharibu maisha yake ya
baadaye kwa njia za kiupuuzi, mtu anaweza kufanya jambo la kijinga tu na
likamkosesha kazi, wakati wote tuyape
kipaumbele maswala ambayo ni ya muhimu katika maisha yetu na kujihami na mambo
yasiyo ya msingi, majukumu yoyote unayopewa hapa dunaini hakikisha kuwa
unayatimiza na kuyatetendea haki kwa kujituma kwa gharama kubwa, mwenendo wako
na uadilifu wako na tahadhari ni za muhimu sana katika kuhakikisha kuwa
unatunza sana kile ambacho Mungu anakitarajia katika maisha yako! Biblia imejaa
mifano ya watu waliopoteza haki yao ya uzaliwa wa kwanza kwa njia za kipuuzi na
za kusikitisha sana ona :-
-
Mwanzo
9:20-26 “Nuhu akaanza kuwa mkulima, akapanda
mizabibu; akanywa divai, akalewa; akawa uchi katika hema yake. HAMU, baba wa
Kanaani, akauona uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje.
Shemu na Yafethi wakatwaa vazi, wakalitanda mabegani mwao wote wawili, wakaenda
kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao; na nyuso zao zilielekea nyuma, wala
hawakuuona uchi wa baba yao. Nuhu akalevuka katika ulevi wake, akajua mwana
wake mdogo alivyomtendea. Akasema, Na alaaniwe Kaanani; Atakuwa mtumwa kabisa
kwa ndugu zake. Akasema, Na atukuzwe BWANA, Mungu wa Shemu; Na Kaanani awe
mtumwa wake.”
-
-
Mwanzo
49:3-4 “REUBENI, u mzaliwa wangu wa kwanza, Nguvu
zangu, na malimbuko ya uwezo wangu. Umewapita wengine kwa ukuu na kwa nguvu.
Umeruka mpaka kama maji, basi usiwe na ukuu, Kwa sababu ulikipanda kitanda cha
baba yako, Ukakitia unajisi; alikipandia kitanda changu.”
-
-
Mwanzo
25:29-32 “Yakobo akapika chakula cha dengu. ESAU
akaja kutoka nyikani, naye alikuwa amechoka sana. Esau akamwambia Yakobo,
Tafadhali, unipe hicho chakula chekundu nile, kwa kuwa ninazimia mimi. Kwa hiyo
walimwita jina lake Edomu.Yakobo akamwambia, Kwanza niuzie leo haki yako ya
mzaliwa wa kwanza. Esau akasema, Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini
haki hii ya uzazi?”
Pigania urithi wako !
Wako watu wanaotajwa kama
Mashujaa walioishi wakati wa Daudi watu hawa walikuwa Hodari sana katika
kuutetea urithi wa bwana na kuhakikisha kuwa watu wengine wanafaidiaka kwa
ujasiri wao, ni imani yangu Kuwa Mungu atakusaidia wewe na mimi tuweze
kupigania kile ambacho Mungu ametukabidhi kwa gharama yoyote
2Samuel 23:8-12 “Haya ndiyo majina ya
mashujaa aliokuwa nao Daudi; Yashobeamu Mhakmoni,mkuu wa maakida ;huyo
aliliinua shoka lake juu ya watu mia nane waliouawa pamoja.Na baada yake
kulikuwa na Eleazari, mwana wa Dodai, Mwahohi, mmojawapo wa wale mashujaa
watatu waliokuwa pamoja na Daudi; walipowatukana Wafilisti waliokuwa
wamekusanyika huko ili kupigana, na watu wa Israeli walikuwa wamekwenda zao;
huyo aliinuka, akawapiga Wafilisti hata mkono wake ukachoka, na mkono wake
ukaambatana na upanga; naye Bwana akafanya wokovu mkuu siku ile; nao watu
wakarudi nyuma yake ili kuteka nyara tu. Na baada yake kulikuwa na Shama, mwana
wa Agee, Mharari; nao Wafilisti walikuwa wamekusanyika huko Lehi, palipokuwapo
konde lililojaa midengu; nao watu wakawakimbia Wafilisti; ila huyo alisimama
katikati ya konde lile, akalipigania, akawaua Wafilisti; naye Bwana akafanya
wokovu mkuu.”
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa Wajenzi Mwenye Hekima!
Maoni 1 :
mimi kama mzaliwa wa kwanza nimejifunza vyema sana na nitabadilika na kuwa shujaa zaidi kuisimamia nafasi hii ya baraka niliyopewa na Bwana.
Chapisha Maoni