Mwanzo 37:23-24 “Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake,
wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, wakamtwaa wakamtupa
katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji.”
Utangulizi:
Mojawapo
ya viongozi wa kiroho ambao habari zao zimeandikwa kwa urefu sana katika
maandiko ni pamoja na Yusufu, Yusufu anahesabika kama moya ya mababa wa Israel,
ukiacha Abrahamu, Isaka na Yakobo, yeye ndio sababu kubwa kwa wana wa Israel
kushuka Misri, kuna mambio mengi sana ya kujifunza katiika maisha ya Yusufu
lakini moja wapo ya jambo la msingi na la muhimu sana tunalotaka kulizungumzia
leo tena kwa kina ni pamoja na Vazi la Yusufu, vazi lake na nguo zake
zinaonekana kuwa na mvuto wa kipekee na vilevile kuwa sababu ya mapito yake
kuna nini kilipelekea hawa watu kumtenda machungu kisa kikianzia kwenye vazi? Maandiko
yanasema hivi;-
Mwanzo 49:22-24 “Yusufu ni mti mchanga wenye kuzaa, Mti mchanga wenye
kuzaa karibu na chemchemi, Matawi yake yametanda ukutani. Wapiga mishale
walimtenda machungu, Wakamtupia, wakamwudhi, Lakini upinde wake ukakaa imara,
Mikono yake ikapata nguvu, Kwa mikono ya Mwenye Enzi wa Yakobo; Kwa jina la
mchungaji, yeye jiwe la Israeli,”
Maandiko
hayatuambii kuwa Yusufu aliwakosea Ndugu zake, lakini yaonekana wazi kuwa ndugu
zake walichukizwa naye na sababu kubwa inaweza kuwa ni wivu wenye uchungu na
hasira kali juu yake, lakini Bwana alikuwa pamoja naye, matukio ya aina hii
yanaweza pia kuwako katika jamii inayotuzunguka leo, tunaweza kujikuta katika
wakati mgumu sana kwa sababu ya mafanikio ya aina mbalimbali na wakati mwingine
kwa sababu ya kusudi la Mungu lililoko ndani yetu! Na anayepingana na kusudi hilo kwa vyovyote
vile ni adui Shetani ambaye wakati mwingine anaweza kuwatumia watu tena watu wa
karibu.
Vazi la Yusufu!
Kisa
cha kusikitisha cha maisha machungu ya Yusufu kinaanzia na namna Yusufu
alivyonunuliwa na kuvishwa vazi la thamani kubwa sana na baba yake biblia
inaelezea vazi hilo katika
Mwanzo 37:3-4 “Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana
ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba
yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye
kwa amani.”
Maandiko
yanaelezea kuhusu kanzu hii ndefu, na matoleo mengine ya kibiblia yanaitaja
kama nguo yenye rangi nyingi, vazi hili la thamani lilikuwa ni vazi la gharama
kubwa na kwa mujibu wa historia ya kibiblia lilikuwa ni vazi lililoweza
kumtambulisha mtu kuwa ni mwana mfalme au mwana wa kifalme (Prince au Princess)
2Samuel 13:18 “Naye alikuwa amevaa kanzu ndefu; kwa kuwa kwa nguo hizo
huvikwa binti za mfalme waliokuwa wanawali. Ndipo mtumishi wake akamleta nje,
akafunga mlango nyuma yake.”
Kanzu
hii au vazi kinabii ilikuwa inaashiria kuwa Israel au Yakobo amekusudia kumpa
heshima kubwa na ya tofauti mwanaye aliyeitwa Yusufu, na kuanza kumfunza Yusufu
kuwa mtawala na mfalme, Vazi hili alilotengenezewa na baba yake lilikuwa ni
ishara ya upendeleo, neema na heshima maalumu aliyokuwa ametunukiwa Yusufu
aidha na baba yake au na Mungu lakini kwa vile baba yake alikuwa nabii alikuwa
anaashiria kuwa Yusufu hakuwa mtu wa kazi ngumu yeye alikuwa ni msimamizi na
mwangalizi na kazi zake ni usimamizi
kwani vazi lile halikuwa vazi la kazi bali vazi la kitawala! Lilikuwa ni vazi
la kibali, kupendwa na neema ya Mungu
Vazi maalumu kwa
Yusufu!
Kwa
nini Yakobo alimtengenezea Yusufu vazi maalumu? Maandiko yanaonyesha kwanza
kabisa Kuwa Yakobo alimpenda Raheli sana kuliko Lea, jambo hili linaweza kuwa
lilionekana wazi kwa watoto wa Yakobo ambao waliona wazi kuwa mama zao
hawakupendwa kama alivyopendwa mama yake Yusufu,
Mwanzo 29:30-31 “Akaingia kwa Raheli naye, akampenda Raheli kuliko Lea,
akatumika kwa ajili yake miaka saba mingine. BWANA akaona ya kwamba Lea
hakupendwa, naye akafungua tumbo lake; bali Raheli alikuwa hazai.”
Unaona
kwa hiyo ni wazi kuwa kutokana na Yakobo kumpenda sana Raheli kuliko Lea ilikuja
kuwa rahisi vilevile kwa Yakobo kumpenda Yusufu kuliko watoto wengine japo hii
ni dhana tu ya kibiblia na kitheolojia
Mwanzo 30:22-24 “Mungu akamkumbuka Raheli; Mungu akamsikia, akamfungua
tumbo. Akapata mimba, akazaa mwana, akasema, Mungu ameondoa aibu yangu. Akamwita
jina lake Yusufu, akisema, BWANA aniongeze mwana mwingine.”
Raheli
alipokuja kumzaa Yusufu pia alimpa jina Yufufu ambalo maana yake Bwana
ameniondolea aibu yangu, kwa msingi huo kinabii pia mtoto huyu alikuwa
anahusika na kuondoa aibu ya mama yake wote tutakuwa tunakumbuka kuwa mara
baada ya anguko la Mwanadamu katika bustani ya Edeni Adamu na Eva walijisikia
aibu, walijiona wako uchi na Mungu aliwatengenezea vazi ili kuifunika aibu yao
au kuwaondolea aibu kumbuka
Mwanzo 3:21 “BWANA Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi,
akawavika.” Yakobo
alichokifanya kwa Mwanaye Yusufu, na jina alilopewa Yusufu na Vazi
alilotengenezewa baadaye na Yakobo yalikuwa na maana sawa na kile Mungu
alimfanyia Adamu na mkewe kwa kuwavika mavazi ya kuwaondolea aibu, maana yake
Mungu aliwapa Heshima iliyokuwa imepotea na vilevile Yusufu kutengenezewa vazi
lile maalumu ilikuwa ni Ishara ya Heshima kubwa kwake!, na kinabii ni kijana ambaye angekuja
kuiondolea aibu familia yake na kuiifadhi wakati wa dhiki, ukiacha heshima hii
kijana huyu alikuwa mwadilifu na alijifunza mambo mengi kuhusu Mungu kutoka kwa
baba yake na mara kwa mara ndiye aliyekuwa akitoa ripoti ya taarifa ya watoto
wote wa Yakobo kwa na kwa bahati mbaya
wengi wao hawakuwa na tabia njema mwanzoni ukilinganisha na Yusufu ona,
Mwanzo 37:2 “Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, aliyekuwa mwenye
miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo pamoja na ndugu zake; naye alikuwa
kijana pamoja na wana wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu
akamletea baba yao habari zao mbaya.”
Kwa
hiyo utaweza kuona kutokana na usafi wa Yusufu, alionekana kama kikwazo kikubwa
cha matendo maovu ya kaka zake, pia alionekana kama mbeya kwa sababu angeleleza
taarifa zao mbaya walizokuwa wakizifanya, achilia mbali Ndoto zake za kiutawala
ambazo zilikuja kuongeza chuki kubwa kwani sio tu, baba yake alikusudia
kumuheshimu sana Yusufu, lakini sasa inaonekana kuwa hata Mungu alikuwa
amekusudia kumuheshimu sana Yusufu kuliko nduguze na kumuinua juu kiutawala ona.
Mwanzo 37:5-11 “Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao
wakazidi kumchukia; akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota.
Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka
ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu.
Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi?
Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake. Akaota tena
ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto
nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia.
Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto
gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie
hata nchi? Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili.”
Ndoto
za Yusufu ulikuwa ni unabii maalumu kutoka kwa Mungu kuwa Mungu angemuheshimu
sana Yusufu na kuwa kwa vyovyote vila angekuja kuwatawala nduguze, sawa tu na
baba yake alivyomtengenezea vazi maalumu, ni wazi kuwa Mungu alikuwa amekusudia
kumuheshimu Yusufu, kila mmoja wetu kuna jambo ambalo kwalo Mungu amekusudia
kukufanya maalumu kuliko wengine kuna heshima ambayo Mungu ameikusudia kwako wakati
wote Mungu ana mpango mwema kwaajili yako
Yeremia 29:11 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni
mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.”
Hata
hivyo ni Muhimu kufahamu kuwa kama Mungu baba yetu wa Mbinguni amekusudia
kutuheshimisha sisi, ieleweke wazi kuwa shetani atapambana kwa kila namna
kuhakikisha ya kuwa heshima hiyo inaharibiwa vazi la heshima ambalo Mungu
anataka kukuvisha linaweza kuwa sababu kubwa sana ya vita vyako duniani lakini
kumbuka wakati wote kusudi la Mungu ndilo litakalosimama
Kuharibiwa kwa
vazi la Yusufu!
Tumejifunza
na kuona kuwa vazi hili tayari kinabii linaashiria heshima ambayo Mungu
amekusudia Kumpa Yusufu, lakini vilevile ni heshima ambayo Mungu amekusudia
kumpa kila mmoja wetu, ni muhimu kufahamu kuwa kusudi kubwa la ibilisi au
shetani ambaye ni adui wa makusudi yote ya Mungu ndani yetu ni pamoja na
kupambana na ile Heshima ambayo Mungu ameikusudia katika maisha yetu, na hii ni
kutaka kuiharibu na kuichafua ile heshima ili yamkini aweze kupambana na kusudi
la Mungu lililoko ndani yetu, ona mfululizo wa matukio magumu unaambatana na
maisha ya Yusufu yote yakilenga kuharibu vazi lake kusalitiwa, kuchukiwa bila
sababu, kupanwa kuuawa au kuuzwa uhamishoni
na jambo la kwanza ilikuwa ni kumbua lile vazi.
Mwanzo 37:23-24 “Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu
kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, wakamtwaa wakamtupa katika birika; na
hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji.”
Unaweza
kuona chuki dhidi ya Yusufu haikuwa juu yake mwenyewe tu lakini ilikuwa na juu
ya ile kanzu, vita kali ilikuwa dhidi ya vazi la Yusufu, na Nduguze hawakuishia
hapo tu walihakikisha kuwa wanaliharibu vazi lile na kumtumia salamu baba yake
ili yamkini naye aweze kujuta kwa kumuandalia Yusufu vazi kama lile ona
Mwanzo 37:31-34 “Wakaitwaa kanzu ya Yusufu, wakachinja mwana-mbuzi, na
kuichovya kanzu katika damu. Wakaenda nayo ile kanzu ndefu, wakamletea baba
yao, wakasema, Tumeona hii; basi, utambue kama kanzu hii ni ya mwanao, ama
siyo. Akaitambua, akasema, Ndiyo kanzu ya mwanangu, mnyama mkali amemla; bila
shaka Yusufu ameraruliwa. Yakobo akararua mavazi yake, akajivika gunia viunoni,
na kumlilia mwanawe siku nyingi.”
Unaona
kimsingi chuki, na husuda juu ya Yusufu kwa ndugu zake haikutokana na nafsi zao
tu kwani wao walimalizia hapo, lakini ni wazi kuwa chuki hii inatoka kwa yule
adui, adui hana mpango mwema na vazi la Yusufu la aina yoyote ile fikiria kuwa
ameuzwa ugenini utumwani, huko nako hakuna mtu anayeijua historia yake wala
ndoto yake na kwa vile Mungu alikuwa amemkusudia kuwa msimamizi na kiongozi
anajikuta utumwani ananunuliwa na Potifa naye anamfanya kuwa mtu mkubwa katika
nyumba yake ona
Mwanzo 39:1-18 “Basi Yusufu akaletwa mpaka Misri naye Potifa, akida wa
Farao, mkuu wa askari, mtu wa Misri, akamnunua mkononi mwa hao Waishmaeli
waliomleta huko. BWANA akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa
katika nyumba ya bwana wake, yule Mmisri. Bwana wake akaona ya kwamba BWANA yu
pamoja naye, na ya kuwa BWANA anafanikisha mambo yote mkononi mwake. Yusufu
akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka awe msimamizi juu ya
nyumba yake, na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake. Ikawa tokea wakati
alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo, BWANA
akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka wa BWANA ukawa juu
ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba. Akayaacha yote
aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu cho chote chake,
ila hicho chakula alichokula tu. Ikawa baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake
akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami. Lakini akakataa, akamwambia mke wa
bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na
vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu. Hakuna mkuu katika nyumba hii
kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu cho chote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe.
Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu?
Akawa akizidi kusema na Yusufu siku baada ya siku, lakini hakumsikia
alale naye, wala aongee naye. Ikawa, siku moja, akaingia nyumbani atende kazi
yake, wala hapakuwa na mtu katika watu wa nyumbani humo ndani; huyo mwanamke
akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi
mwake, akakimbia, akatoka nje. Ikawa alipoona ya kwamba amemwachilia nguo yake
mkononi mwake, naye amekimbia nje, akawaita watu wa nyumbani mwake, akasema
nao, akinena, Angalieni, ametuletea mtu Mwebrania atufanyie dhihaka. Ameingia
kwangu, ili alale nami, nikalia kwa sauti kuu. Ikawa, aliposikia ya kuwa
nimepaza sauti yangu na kulia, aliiacha nguo yake kwangu, akakimbia, akatoka
nje. Basi akaiweka ile nguo kwake hata bwana wake aje nyumbani. Naye akamwambia
kama maneno hayo, akisema, Yule mtumwa Mwebrania uliyemleta kwetu, aliingia
kwangu anidhihaki. Ikawa nilipopaza sauti yangu, nikalia, akaacha nguo yake
kwangu akakimbia nje.”
Unapoendelea
kufuatilia maisha ya Yusufu hata kule ugenini utakubaliana nani kwamba sio
ndugu zake tu, lakini ni shetani anahusika kufuatilia vazi la Yusufu kwani hata
watu wasiomjua wageni bado waliendelea kuandama nguo au vazi jingine la Yusufu
katika nyumba ya Potifa ili waharibu kile ambacho Mungu amekikusudia, makusudi ni kuwa maisha ya Yusufu yawe
matatani na asipate nafasi kabisa ya kulitumikia shuri la Mungu, vazi la pili
la yusufu linaingia matatani sasa Yusufu ana mavazi ya kifungwa gerezani hata
hivyo bado neema ya Mungu ilikuwa pamoja naye hata akiwako kule gerezani kwa kuwa yeye ana karama ya usimamizi ona
Mwanzo 39:21-23 “Lakini BWANA akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa
kibali machoni pa mkuu wa gereza. Mkuu wa gereza akawatia mkononi mwa Yusufu
watu wote waliofungwa, waliomo gerezani; na yote yaliyofanyika humo ndiye
aliyeyafanya. Wala mkuu wa gereza hakuangalia neno lililoko mkononi mwa Yusufu;
kwa kuwa BWANA alikuwa pamoja naye. BWANA akayafanikisha yote aliyoyafanya”
Yusufu katika
vazi jipya
Hata
pamoja na mapito yote aliyoyapitia Yusufu Bado Mungu alikuwa Pamoja naye, Mungu
atakuwa pamoja nasi wakati wote katika kuhakikisha ya kuwa mpango wake
unatimizwa kwetu, Yusufu hatimaye aliweza kutumia kipawa chake kutafasiri ndoto
na hatimaye alitafasiri ndoto ya Farao ambayo ilimpatia nafasi kubwa sana na
akalitimiza kusudi la Mungu
Mwanzo 41:39-44 “Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha
hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe. Basi wewe utakuwa juu ya
nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu
nitakuwa mkuu kuliko wewe. Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka juu ya
nchi yote ya Misri. Farao akavua pete yake ya muhuri mkononi mwake, akaitia
mkononi mwa Yusufu; akamvika mavazi ya kitani nzuri, na kumtia mkufu wa dhahabu
shingoni mwake. Akampandisha katika gari lake la pili alilokuwa nalo. Na watu
wakapiga kelele mbele yake, Pigeni magoti. Hivyo akamweka juu ya nchi yote ya
Misri. Farao akamwambia Yusufu, Mimi ni Farao, na bila amri yako, mtu asiinue
mkono wala mguu katika nchi yote ya Misri.”
Kumbe
wote tunaweza kukubaliana wazi kuwa vazi la Yusufu lilikuwa lina uhusiano
mkubwa sana na nafasi aliyokuwa nayo, Mungu alikuwa amekusudia kutimiza kusudi
Fulani ndani yake Sasa sio baba yake tu wala sio Mungu pekee farao pia anamvika
mavazi Yusufu kutoka gerezani saa anavikwa mavazi ya kifalme anapewa na mamlaka
ili aweze kutimiza hivyo kusudi kubwa la Mungu
Mambo ya
kujifunza kutoka katika vazi la Yusufu
1. Vazi
la sifa njema
– Yusufu alitengenezewa vazi la kwanza na Baba yake kwa sababu alikuwa ni mtoto
mwenye sifa njema kuliko wengine alipata kibali kwa baba yake, alipata neema ni
vazi la upendeleo, ni sifa hii njema iliyoweza kuinua chuki na ibilisi
alikusudia kuiharibu,
Mwanzo
37:3-4 “Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe
wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona
ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza
kusema naye kwa amani.”
Yusufu alifanyiwa hila nyingi
sana za kibinadamu kupitia ndugu zake lakini tunajifunza ya kuwa kusudi la
Bwana ndilo litakalosimama, ikiwa Mungu amekukusudia Heshima hata iwe gerezani
heshima yako itabaki pale pale
Mithali
19:21 “Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini
shauri la Bwana ndilo litakalosimama.”Mavazi yake yalichafuliwa lakini Mungu alimvisha
mavazi ya Kimisri na kumuinua juu akitumia farasi wa farao na Pete ya farao,
Nataka nikuhakikishie ya kuwa ukisimama na Mungu hakuna mtu atafanikiwa katika
hila yake ya aina yoyote.
2. Vazi
la utumwa – Ni
ukweli ulio wazi kuwa vazi la Yusufu ilichanwa chanwa na kuharibiwa na
kuchafuliwa kwa damu na Yakobo alionyeshwa ili atambue kama kanzu ile ni ya
mwanaye Mwanzo 37:31-34 “Wakaitwaa kanzu ya Yusufu, wakachinja mwana-mbuzi, na
kuichovya kanzu katika damu. Wakaenda nayo ile kanzu ndefu, wakamletea baba
yao, wakasema, Tumeona hii; basi, utambue kama kanzu hii ni ya mwanao, ama
siyo. Akaitambua, akasema, Ndiyo kanzu ya mwanangu, mnyama mkali amemla; bila
shaka Yusufu ameraruliwa. Yakobo akararua mavazi yake, akajivika gunia viunoni,
na kumlilia mwanawe siku nyingi.”
Yusufu alipata vazi lingine
huko utumwani alinunuliwa kama mtumwa wa amrijeshi mkuu wa farao alivikwa
mavazi ya kitumwa ili amtumikie mtu, lilikuwa vaza la anasa na lilikuwa vazi la
tama lakini Yusufu aliishinda tamaa, aliushinda ulimwengu, alimuheshimu Mungu
hata katika mazingira magumu nay a ugenini,
Mungu huwaheshimu wale wanaomuheshimu
Yusufu alimuheshimu Mungu kila alipokuwepo, alitambua ya kuwa anapaswa
kuwa mwaminifu kwa wanadamu na kwa Mungu pia, aliikataa dhambi nimtendeje Bwana
Mungu wangu dhambi kubwa namna hii, aliamua kumuheshimu Mungu katika maisha
yake alijihami na ubaya wa kila namna na kwa sababu hiyo hatimaye kwa uvumilivu
mkubwa alivuna matunda yake yaliyokusudiwa
1Samuel
2:30 “Kwa sababu hiyo, Bwana, Mungu wa Israeli,
asema, Ni kweli, nalisema ya kuwa nyumba yako, na nyumba ya baba yako itakwenda
mbele zangu milele; lakini sasa Bwana asema, Jambo hili na liwe mbali nami; kwa
maana wao wanaoniheshimu nitawaheshimu, na wao wanaonidharau watahesabiwa kuwa
si kitu.”
3. Vazi
la Heshima – lolote
linalotokea katika maisha yetu liko chini ya utawala wa Mungu hata pale watu
wanapotutendea uovu na hila tukumbuke tu ya kuwa Mungu ndiye anayetawala,
Pamoja na mapito yote uaminifu na uvumilivu ulimleta Yusufu katika heshima
kubwa sana alivikwa mavazi ya kifahari na kuinuliwa na watu wote kuinamaa mbele
zake ona
Mwanzo
41:41-42 “Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka
juu ya nchi yote ya Misri. Farao akavua pete yake ya muhuri mkononi mwake,
akaitia mkononi mwa Yusufu; akamvika mavazi ya kitani nzuri, na kumtia mkufu wa
dhahabu shingoni mwake.”
Hitimisho:
Mungu anao mpango Madhubuti wa
kumuheshimu kila mmoja wetu, ni wajhibu wako kuhakikisha ya kuwa unatunza sifa
njema ulizonazo, huku ukitambua ya kuwa, Shetani atakupiga vita akiwatumia
watu, jilinde na kuhakikisha kuwa unaendelea kuyatunza maisha yako, haijalishi
ni mapitio magumu kiasi gani unayapitia.haijalishi uko sehemu ya ugenini ambako
watu hawakuoni kumbuka ya kuwa Mungu anakuona na anataka wewe umuonyeshe
heshima na Mungu atakuwa pamoja nawe
Mpango wake Mungu ni kutaka kukuheshimu na Mungu analo vazi, anao farasi
anayo mavazi na anao watakaokutangaza pale utakapoitunza heshima inayokusudiwa
kwako na Mungu na wazazi wako na ulimwengu , Bado Mungu anamkusudia kila mmoja
wetu kuvikwa mavazi ya heshima kubwa
Esta
6:7-10 “Basi Hamani akaingia. Mfalme akamwambia,
Afanyiziwe nini yule ambaye mfalme apenda kumheshimu? Hamani akasema moyoni
mwake, Ni nani ambaye mfalme apenda kumheshimu kuliko mimi? Basi Hamani
akamwambia mfalme, Yule ambaye mfalme apenda kumheshimu, na aletewe mavazi ya
kifalme ambayo mfalme amezoea kuyavaa, na farasi ambaye mfalme humpanda mwenyewe,
ambaye ametiwa taji ya kifalme kichwani; na yale mavazi na yule farasi
akabidhiwe mkononi mmojawapo wa maakida wa mfalme aliye mstahiki; ili makusudi
amvike yule ambaye mfalme apenda kumheshimu, na kumrakibisha juu ya farasi
kuipitia njia kuu ya mjini, na kupiga mbiu mbele yake, kusema, Hivyo ndivyo
atakavyofanyiziwa mtu yule ambaye mfalme apenda kumheshimu. Basi mfalme
akamwambia Hamani, Hima! Twaa mavazi na farasi kama ulivyosema, ukamfanyizie
vivyo hivyo Mordekai, Myahudi, aketiye mlangoni pa mfalme; lisipungue neno lo
lote katika yote uliyoyasema.” Ni
ahadi ya Mungu kwamba kila mtu atakayeshida tapata heshima kubwa sio hapa
duniani tu bali na mbinguni pia
Ufunuo
3:5 “Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe,
wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina
lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake.”
Na
Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu
wa wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni