Jumamosi, 18 Machi 2023

Usifanye neno lolote kwa Upendeleo !


1Timotheo 5:21 “Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, na mbele za malaika wateule, uyatende hayo pasipo kuhukumu kwa haraka; usifanye neno lo lote kwa upendeleo.”


 

Utangulizi:

Mojawapo ya agizo Muhimu sana alilopewa Timotheo, Kama mwangalizi wa makanisa yaliyokuwako Efeso katika waraka alioandikiwa na Paulo Mtume Pamoja na maagizo mengine ni pamoja na kuhakikisha kuwa asifanye neno lolote kwa upendeleo, Upendeleo katika nyakati za leo limekuwa mojawapo ya tatizo kubwa sana katika jamii, jambo linalopelekea kutokutendeka kwa haki, kumekuwepo na tatizo la upendeleo kila mahali leo, Katika mazingira ya kibiashara, mazingira ya kisiasa, katika michezo, na hata makanisani, katika familia, ndugu, serikalini na hata kwenye ndoa, Bila ya aibu yoyote leo hii watu wanaweza kufanya upendeleo na kusahau kabisa kuwa kufanya upendeleo ni dhambi nani kinyume na sheria ya kifalme.

Yakobo 2:8-9 “Lakini mkiitimiza ile sheria ya kifalme kama ilivyoandikwa, Mpende jirani yako kama nafsi yako, mwatenda vema. Bali mkiwapendelea watu, mwafanya dhambi na kuhukumiwa na sheria kuwa wakosaji.”            

Sisi kama wakristo tunapaswa kumfuata Kristo kama mfano wetu, Yesu Kristo hakuwahi kupendelea watu, sisi tunaomfuata yeye kamwe hatupaswi kuonyesha upendeleo maandiko yanatukataza kufanya hivyo, kuonyesha upendeleo ni moja ya tatizo kubwa sana katika jamii nani kinyume na haki ya Mungu, kama mtu anasema ni mkristo na anamwamini Mungu na hata kama sio mwamini awaye yote ambaye ana moyo wa kutenda haki hawezi kuruhusu upendeleo.

 Yakobo 2:1 “Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu.”

Kwa bahati mbaya mambo hayako kama maandiko yanavyoagiza, leo hii ili uweze kufanikiwa ni lazima uwe na connection na watu au mtu Fulani, uwe kwenye kundi au chama Fulani, watu wanapendelea watu au kundi Fulani la watu kwa sababu ni ndugu, au ni wa jinsia yake, au ni masikini, au amepokea rushwa au ni wa ukoo wake, au shemeji zake, au ana hadhi Fulani au ana hela, au wanafahamiana kwa muda mrefu na kadhalika hivyo kuna namna watu wanapewa heshima au upendeleo kwa sababu Fulani, Fulani kama uko na upendeleo leo hii ni lazima utubu na kuelewa kuwa upendeleo ni dhambi mbaya kama zilivyo dhambi nyingine! 

Maana ya upendeleo.

Neno upendeleo katika biblia ya kiyunani husomeka kama PROSOPOLEPSIA ambalo kiingereza linasomeka kama FAVORITISM  ambalo maana yake ni “respect of persons” au “to give judgement with the respect of outwards circumstances of a man” pia inaweza kutafasirika kama giving unfair treatment of a person or group on basis of prejudice kwa Kiswahili Upendeleo ni hali ya kutoa haki au kipaumbele kwa mtu asiyestahili kutokana na maslahi ya mtoa haki, ni hali ya kutoa kipaumbele kwa mtu kulingana na mazingira ya nje au ya muonekano, au kuonyesha heshima kwa mtu au kundi la watu katika mtazamo au maoni yasiyo sahihi, au yasiyo sawa kimsingi upendeleo ni sawa na hakimu anayetoa haki mahali pasipostahili haki, au mwamuzi refa anapowapa watu penalty ambayo kimsingi na kiyushahidi haikupaswa kuwa penalty ni tabia ambayo kibiblia haikubaliki na wala haitokani na Mungu wetu  tunaelezwa kuwa Mungu wetu hana upendeleo na watu wa Mungu wanaonywa kutokuwa na Upendeleo kwa sababu zozote zile Yakobo anajaribu kutioa mfano ulio hai kuhusu upendeleo alipokuwa anajaribu kufafanua somo lake kuwa watu wasiwe na upnendeleo ona 

Yakobo 2:2-5 “Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni pangu, je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu? Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao? Bali ninyi mmemvunjia heshima maskini. Je! Matajiri hawawaonei ninyi na kuwavuta mbele ya viti vya hukumu?”

Upendeleo sio tabia ya uungu wala haipaswi kuwa tabia ya watu wa Mungu, kama watu wa Mungu wanaonyesha upendeleo je wana tofauti gani na watu wa dunia hii, ni ukweli usiopingika kuwa dunia inatarajia kujifunza kitu kutoka kwa watu wa Mungu na Mungu mwenyewe kama Mungu mwenyewe hana upendeleo wewe unayefanya upendeleo huoni ya kuwa una kesi ya kujibu, Maandiko yanatuelekeza kuwa Mungu hana upendeleo na kuwa tunapaswa kujifunza kutoka kwake na kwa neno lake kisha tuishi sawa na haki ya Mungu!. 

Mungu hana upendeleo!

Matendo ya mitume 10:34-35 “Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.”

Petro alitambua kuwa Mungu hana upendeleo, kuna wakati ambapo wayahudi walijidhani ya kuwa huenda wao ni wa Muhimu sana kuliko mataifa mengine dhana hii ilijengeka kwao wakasau kuwa Mungu alitaka kuwaandaa wao kama watumishi wake ili kutoka kwao injili ienee kwa mataifa yote , Lakini ni ukweli unaosmama wazi kuwa Mungu hana hati milikia ya mtu Fulani wako watu hudhani ya kuwa Mungu ni wao nan i wa kwao peke yao na hudhani ya kuwa Mungu anawawasikiliza wao tu nisikilize Mungu ni  wa watu wote yeye hana upendeleo wala hapokei uso wa mwanadamu  Mungu husimama upande wa kila mtu atendaye mema bila kujali ni wa kabila gani  ona

Warumi 2:10-11 “bali utukufu na heshima na amani kwa kila mtu atendaye mema, Myahudi kwanza na Myunani pia; kwa maana hakuna upendeleo kwa Mungu.”

Ndugu zangu hakuna kabila, wala mtu wala kiongozi anayeweza kudhani au kufikiri ya kuwa yeye ni wa muhimu sana kuliko wengine, wako watu wengine wamepata nafasi za uongozi na usimamizi wa mambo lakini hawatendi haki ya Mungu, na badala yake wanafanya upendeleo am,bao uko wazi wazi katika jamii au taasisi wanayoiongoza, Mungu anachukizwa wazi na jambo hilo, huo ni uwakilishi mbaya na mbovu wa kumtangaza Kristo, kila mtu aliyemjia Kristio na kubatizwa kwa Mungu ni sawa na hakuna upendeleo.  

Wagalatia 3:27-29 “Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.”

Unaona maandiko yanaonyesha kuwa sisi wote tumemvaa Kristo, sisi wote tumekuwa wamoja katika Kristo, haijalishi wewe myahudi, au myunani, haijalishi wewe mnyakyusa au mbondei, haijalishi wewe kijana au mzee, haijalishi wewe mtumwa au huru, haijalishi wewe ni wa namna gani sisi sote tunazo ahadi sawasawa na Ibrahimu na Isaka na Yakobo, kama Mungu alimlinda na kumtetea Abrahamu anatafanya hivyo kwa yeyote yule aliyemwamini mwana wake Yesu Kristo laizma ufikie wakati tuache kiburi na majivuno na kudhani kuwa mtu Fulani ana umuhimu sana kwa Mungu kuliko mwingine, Hakuna mtu ambaye anaweza kudhani ya kuwa amefanya makubwa sana kuliko mwingine au labda anasikilizwa sana na Mungu kuliko wengine kama mtu anajiona yuko hivyo nataka nikuambie wazi hicho ni kiburi, Mungu hapokei uso wa mwanadamu wala hapokei rushwa ona

Kumbukumbu la Torati 10:17 “Kwa maana Bwana, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa mabwana, Mungu mkuu, mwenye kuogofya, asiyependelea nyuso za watu, wala hakubali rushwa”.

Wakati mwingine tumeona watu wakitetewa waziwazi tena waliostahili hukumu tena wakiwa hawajatubu lakini kwa sababu wanajuana na wakubwa wanapewa upendeleo, kwa sababu wana connection wako tu, kuna watu ambao walifanya makosa madogo tu na wamehukumiwa vikali, kuna watu wana makosa makubwa lakini wako, kuna watu wako magerezani kwa sababu ya kusingiziwa tu, kuna watu kwa sababu wanachukiwa wanatafutiwa makosa hata ya kupakaziwa tu ili wahukumiwe hii ni tabia mbaya ya kibinadamu nadhani hakuna mtu ambaye ameishi kwenye jamii yenye upendeleo ambaye anaweza kuwa na furaha, wana michezo ambao timu zao wakati mwingine zimechezeshwa na marefarii wabaya wameonekana kukata tama sana pale timu nyingine inapobebwa na juhudi za wale waliotumia nguvu zao na akili zao zikipuuzwa na kutokuonekana kuwa kitu hapo ndipo utakapoelewa kuwa upendeleo sio kitu kizuri, katika ndoa vilevile pale ambapo wazazi wa upande mmoja wameonekana kupewa kipaumbele kuliko wazazi wa upande mwingine zimekuwa ni chachu na changamoto zenye kukatisha tamaa sana katika familia mbalimbali narudia tena hakuna mtu anayeweza kuwa na furaha na amani pale udhalimu wa upendeleo unapofanyika katika jamii yake, unakwenda mahakamani mahali ambapo unatarajia utapokea haki na unakuta hukumu inapotoshwa je unaweza kuwa na furaha na sehemu hiyo? Mwalimu anaposahihisha na kumuongezea marks mwanafunzi ambaye hakustahili je unaweza kufurahia kuweko katika jamii yenye upendeleo? Ashukuriwe Mungu hana upendeleo kwa Mungu kila mtu atahukumiwa sawa na matendo yake bila upendeleo ona

Wakolosai 3:23-25 “Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu, mkijua ya kuwa mtapokea kwa Bwana ujira wa urithi. Mnamtumikia Bwana Kristo. Maana adhulumuye atapata mapato ya udhalimu wake, wala hakuna upendeleo.”

Unapofanya upendeleo unaweza kudhani kama sio dhambi hivi, lakini ni ukweli ulio wazi kuwa unapofanya upendeleo unafanya dhuluma, unadhulumu wanaostahili, kwa wasiostahili, maandiko yanaonya kuwa adhulumuye atapata mapato ya udhalimu wake wala hakuna upendeleo,  ni Muhimu kwa kila mtu aliye katika nafasi ya maamuzi akajifunza kutenda kwa haki na kumcha Mungu Mungu anataka watu wote watendewe haki na kamwe kusiwe na aina yoyote ya upendeleo unaoshakiziwa na jambo lolote lile kifedha au uso wa mwanadamu ona

 2Nyakati 19:5 -7 “Akasimamisha makadhi katika nchi, katikati ya miji yote yenye maboma ya Yuda, mji kwa mji; akawaambia hao makadhi, Angalieni myafanyayo; kwa kuwa hammfanyii mwanadamu hukumu, ila Bwana; naye yupo pamoja nanyi katika neno la hukumu. Basi sasa hofu ya Bwana na iwe juu yenu; angalieni mkaifanye; kwa maana kwa Bwana, Mungu wetu, hapana uovu, wala kujali nafsi za watu, wala kupokea zawadi.”

Usifanye neno lolote kwa Upendeleo !

Nyakati za Kanisa la kwanza walijitahidi sana kuhakikisha kuwa wanakuwa mbali na upendeleomoja ya changamoto kubwa za kibinadamu zilizojitiokeza mapema nyakati za kanisa la kwanza ni pamoja na upendeleo jambo lililopeleka Mitume kuwa makini katika uchaguzi wa viongozi na mashemasi ambao kimsingi walipaswa kuwa watu wa haki watu wasio na upendeleo ona

Matendo 6:1-7 “Hata siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung'uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku. Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani. Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno. Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia; ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao. Neno la Mungu likaenea; na hesabu ya wanafunzi ikazidi sana katika Yerusalemu; jamii kubwa ya makuhani wakaitii ile Imani.”              

Haki inapotendeka katika jamii kunakuwa na baraka kubwa sana, lakini dhuluma inapotendeka watu huwa na manung’uniko Mungu anawataka watu wake wote kuwa mstari wa mbele katika kutenda haki na ndio maana utaweza kuona katika mstari wa Msingi Paulo akiagiza kwa kiapo akimwapisha Timotheo mbele za Mungu na mbele za malaika asifanye neno lolote kwa upendeleo hili sio agizo la mchezo maana yake Mungu na malaika mbinguni wanatutazamia tutende haki na huku ya Mungu iko pale pale kwa wasiotenda haki

1Timotheo 5:21 “Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, na mbele za malaika wateule, uyatende hayo pasipo kuhukumu kwa haraka; usifanye neno lo lote kwa upendeleo.”

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima!

Hakuna maoni: