Kutoka 8: 16 -19 “BWANA akamwambia Musa,
Mwambie Haruni, Nyosha fimbo yako, ukayapige mavumbi ya nchi, ili kwamba yawe
chawa katika nchi yote ya Misri. Nao wakafanya; Haruni akaunyosha mkono wake na
fimbo yake, na kuyapiga mavumbi ya nchi, nayo yakawa chawa juu ya wanadamu na
juu ya wanyama; mavumbi yote ya nchi yakawa ni chawa katika nchi yote ya Misri.
Hao waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao, ili kwamba walete
chawa, lakini wasiweze; nako kulikuwa na chawa juu ya wanadamu, na juu ya
wanyama. Ndipo wale waganga wakamwambia Farao, Jambo hili ni chanda cha Mungu;
na moyo wake Farao ukawa mgumu asiwasikize; vile vile kama BWANA alivyonena.”
Utangulizi:
Neno Chanda cha Mungu
limejitokeza au kutajwa katika Biblia ya Kiebrania kama neno “etsba” kimatamshi “ets-bah” na kutajwa katika Biblia ya
kiingereza ya King James Version mara 32
na kwa lugha ya kiyunani ni “Daktulos” kimatamshi ni Dak-too-los ambalo Katika Biblia ya kiingereza ya
King James Version limetajwa mara 8, maneno
yote hayo katika lugha ya kiibrania na kiyunani yanamaanisha kidole cha Mungu, Neno ambalo kinabii
linahusiana na Utendaji wa Roho Mtakatifu, hata hivyo Pamoja na neno hilo
kutajwa mara kadhaa, limeonekana kwa uwazi katika matukio kadhaa likitumika kwa
namna kali zaidi ya maeneo mengine.
·
Kidole cha Mungu wakati wa Farao.
·
Kidole cha Mungu Katika mlima wa Sinai.
·
Kidole cha Mungu wakati wa Beltshaza.
·
Kidole cha Mungu na wakati wa Huduma ya Yesu.
Kidole cha Mungu wakati wa Farao!
Neno kidole cha Mungu
linajitokeza kwa mara ya kwanza katika lugha za kinabii, kutokana na uandishi
wa Musa katika kitabu cha kutoka mara baada ya Musa na Haruni kuamuriwa na
Mungu kuachilia pigo la tatu, Mapigo haya yalikuwa ni amri ya Mungu ili kumlazimisha
Farao kuwaachia wana wa Israel waende zao kwa sababu walikaa katika inchi ya
Misri na katika hali ya utumwa kwa zaidi ya miaka 400, Mungu alimuelekeza Musa kumuamuru Haruni kunyoosha fimbo yake
ili kuyapiga mavumbi ya nchi yapate kuwa chawa katika inchi yote ya Misri
Kutoka 8:16-17 “BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha fimbo yako,
ukayapige mavumbi ya nchi, ili kwamba yawe chawa katika nchi yote ya Misri. Nao
wakafanya; Haruni akaunyosha mkono wake na fimbo yake, na kuyapiga mavumbi ya
nchi, nayo yakawa chawa juu ya wanadamu na juu ya wanyama; mavumbi yote ya nchi
yakawa ni chawa katika nchi yote ya Misri.”
Kwa kawaida kila Muujiza ambao
Musa na Haruni waliufanya kwa jina la Mungu, utaweza kuona wachawi wa kimisri
nao waliigiza hasa kwa miujiza ya mwanzoni walipojaribu kuuigiza muujiza huu
kwa uchawi wao na kushindwa ndipo walipotamka wenyewe kwa midomo yao kumueleza
Farao kuwa hiki ni chanda cha Mungu,
Kutoka 8:18-19 “Hao waganga nao wakafanya
mfano wa hayo kwa uganga wao, ili kwamba walete chawa, lakini wasiweze; nako
kulikuwa na chawa juu ya wanadamu, na juu ya wanyama. Ndipo wale waganga
wakamwambia Farao, Jambo hili ni CHANDA CHA MUNGU; na moyo wake Farao ukawa
mgumu asiwasikize; vile vile kama BWANA alivyonena.” Hapo ndipo tunapouona uweza wa Mungu katika
kutenda miujiza ya kupita kawaida dhidi ya miujiza ya kichawi na ya
kimazingaombwe, Mungu ana uwezo mkubwa sana, anapukusudia kutukomboa katika
utumwa wa anina yoyote ile ni lazima tumuitie yeye kwa uweza wa Roho wake
Mtakatifu ambaye ndiye chanda cha Mungu atatutoa katika mikandamizo ya aina
yoyote ile
Kidole cha Mungu Katika mlima wa Sinai.
Eneo lingine ambapo tunaona
maandiko yakitaja chanda cha Mungu ni katika Mlima wa Sinai wakati Mungu
alipokuwa anataka kumpa Musa Amri na sharia zake ili awafundishe watu wake,
wakati Amri Kumi za Msingi zilipokuwa zinaandikwa tunaelezwa kuwa amri hizo
ziliandikwa kwa kidole cha Mungu yaani Chanda cha Mungu
Kutoka 31:18 “Hapo BWANA alipokuwa amekwisha
zungumza na Musa katika mlima wa Sinai, akampa hizo mbao mbili za ushuhuda,
mbao mbili za mawe, zilizoandikwa kwa chanda cha Mungu.”
Musa analikumbuka tukio hilo la
amri na sharia za Mungu kuandikwa kwa kidole chake wakati alipokuwa
anawaandikia kitabu kingine cha kumbukumbu la Torati ona katika
Kumbukumbu la Torati 9:9 -10 “Na hapo
nilipokwea mlimani kwenda kuzipokea mbao za mawe, nazo ni mbao za agano Bwana
alilofanya nanyi, ndipo nikakaa mle mlimani siku arobaini usiku na mchana;
sikula chakula wala kunywa maji. Bwana akanipa zile mbao mbili za mawe
zimeandikwa kwa kidole cha Mungu; na juu yake yameandikwa maneno mfano wa yote
aliyosema nanyi Bwana mle mlimani toka kati ya moto siku ya mkutano.”
Haikuwa lazima kuwa labda Mungu
aliandika ka ma wanadamu waandikavyo kwa kuwa Mungu ni Roho lakini haipingiki
kuwa uwezo wake wa utendaji ROHO
MTAKATIFU alisababisha kwa muujiza mkubwa sharia zake za msingi kuwepo
katika mawe yale, ni ukweli usiopingika kuwa kama Roho Mtakatifu aliweza
kuziandika sharia za Mungu katika mawe hashindwi kuziandika sharia zake katika
mioyo yetu neno la Mungu linaeleza wazi kuwa uko wakati ambapo Mungu
ataziandika sheria zake katika mioyo yetu
2 Wakoritho 3:2-3 “Ninyi ndinyi barua yetu, iliyoandikwa mioyoni mwetu,
inajulikana na kusomwa na watu wote; mnadhihirishwa kwamba mmekuwa barua ya
Kristo tuliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye
hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo ni mioyo ya nyama.”
Unaona Roho Mtakatifu yaani utendaji
wa Mungu ulioandika sharia kwa kidole cha Moto katika mlima wa Sinai yu aweza
kuandika sheria zake na kuweka mwako wa moto katika mioyo yetu ili tumtii
Mungu, tunaweza kusoma mapenzi ya Mungu leo kutoka Moyoni kwa kuelekezwa na
kufundishwa na Roho Mtakatifu
1Yohana 3:21-24 “Wapenzi, mioyo yetu
isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu; na lo lote tuombalo, twalipokea kwake,
kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake. Na hii
ndiyo amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, na kupendana
sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri. Naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake
yeye naye ndani yake. Na katika hili tunajua ya kuwa anakaa ndani yetu, kwa
huyo Roho aliyetupa.”
Utendaji wa Mungu ndani yetu
unaweza kuihuisha sharia ya Mungu ndani yetu na kutugeuza kuwa mfano wa kuigwa
kwa kila mtu duniani, hata kama ulimwengu unaweza kuwa umeharibika kwa kiwango
gani Roho Mtakatifu ndani yetu atatuongoza na kutuhifadhi na kuionya mioyo yetu
na kutuelekeza katika sharia ya Mungu wetu sharia ya kifalme sharia ya Roho wa
Uzima kwa sababu hiyo sisi sasa hatuongozwi na sharia ile ya kimwili iletayo
mauti bali twaongozwa na sharia ya Roho wa Uzima ulio katika Kristo Yesu.
Warumi 8:1-4 “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika
Kristo Yesu. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu
imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti. Maana yale yasiyowezekana
kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma
Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi,
aliihukumu dhambi katika mwili; ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu
sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.”
Kidole cha Mungu wakati wa Beltshaza.
Eneo lingine ambapo tunauona
utendaji wa Mungu kama Kidole chake ni wakati wa kipindi cha utawala wa mfalme
Mpumbavu aliyeitwa Belshaza mfalme huyu hakujua ya kuwa Mungu ndiye anayeweka
watu madarakani, yeye aliamuru vyombo vilivyokuwa vimetekwa kutoka Hekalu
lililokuwako Yerusalem, na baba yake Mfalme mkuu Nebukadreza ambaye baadaye
alimuheshimu sana Mungu wa Israel, lakini Belshaza yeye alikuwa na dharau
hakuthamini vyombo vile vya Hekaluni ambavyo kimsingi vilikuwa vimewekwa wakfu,
chombo kinapokuwa kimewekwa Wakfu maana yake Roho wa Mungu anakuwa amevitenga
na kuviheshimu lakini Beslshaza badala yake yeye aliamua kuvidhalilisha kwa
kuvinywea pombe ona katika
Daniel 5:1-4 “Belshaza, mfalme, aliwafanyia
wakuu wake elfu karamu kubwa akanywa divai mbele ya elfu hao. Belshaza,
alipokuwa akionja ile divai, akaamuru wavilete vile vyombo vya dhahabu na
fedha, ambavyo baba yake, Nebukadreza, alivitoa katika hekalu lililokuwako
Yerusalemu; ili kwamba mfalme, na wakuu wake, na wake zake, na masuria wake,
wapate kuvinywea. Basi wakavileta vile vyombo vya dhahabu, vilivyotolewa katika
hekalu la nyumba ya Mungu lililokuwako Yerusalemu; na mfalme na wakuu wake, na
wake zake, na masuria wake, wakavinywea. Wakanywa divai, wakaisifu miungu ya
dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe.”
Ukweli ni wazi kuwa tukio hili
lilimuuzunisha sana Mungu wa Israel, Mungu hawezi kukubali vyombo vyake
alivyovoweka wakfu kwa kuvitakasa vitumike kinyume na makusudi ya Mungu aliye
hai, wakati tukio hili lililpokuwa likiendelea mfalme aliona katika ukuta
kiganja cha mkono kikiandika kwa vidole vya kibinadamu kumtangazia mfalme huyu
hukumu yake kwa haraka ona
Daniel 5:5-6 “Saa iyo hiyo vikatokea vidole
vya mkono wa mwanadamu, vikaandika katika chokaa ya ukuta wa nyumba ya enzi ya
mfalme, mahali palipokikabili kinara; naye mfalme akakiona kitanga cha ule
mkono ulioandika. Ndipo uso wa mfalme ukambadilika; fikira zake zikamfadhaisha;
viungo vya viuno vyake vikalegea; magoti yake yakagongana.”
Jambo hili lilikuwa jambo la
kutisha sana lugha ya kibiblia hapo VIUNGO
VYA VIUNO VYAKE VIKALEGEA ni lugha ya kiungwana kuwa mfalme alijinyea na
kujiharishia kwa hofu, tabia mbaya aliyokuwa nayo na dhadhau yake dhidi ya
mambo ya Mungu ilikuwa sasa inashughulikiwa na utendaji wa Mungu mwenyewe,
vidole hivyo vya Mungu vilikuwa vimentangazia hukumu ya Mungu na hukumu yake
ilikuwa ni kifo kwa sababu amevuka mpaka Daniel ambaye ndiye alikuja
kuyatafasiri maneno yale alisema
Daniel 5: 22-30 “Na wewe, mwanawe, Ee
Belshaza, hukujinyenyekeza moyo wako, ijapokuwa ulijua hayo yote. Bali umejiinua
juu ya Bwana wa mbingu; nao wamevileta vyombo vya nyumba yake mbele yako; na
wewe, na wakuu wako, na wake zako, na masuria wako, mmevinywea; nawe umeisifu
miungu ya fedha na ya dhahabu na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe;
wasioona, wala kusikia, wala kujua neno lo lote; na Mungu yule, ambaye pumzi
yako i mkononi mwake, na njia zako zote ni zake, hukumtukuza. Ndipo kile
kitanga cha ule mkono kikaletwa kutoka mbele zake, na maandiko haya
yameandikwa. Na maandiko yaliyoandikwa ni haya; MENE, MENE, TEKELI, NA PERESI.
Na tafsiri ya maneno haya ni hii; MENE, Mungu ameuhesabu ufalme wako na
kuukomesha. TEKELI, umepimwa katika mizani nawe umeonekana kuwa umepunguka.
PERESI, ufalme wako umegawanyika, nao wamepewa Wamedi na Waajemi. Ndipo
Belshaza akatoa amri, nao wakamvika Danieli mavazi ya rangi ya zambarau,
wakatia mkufu wa dhahabu shingoni mwake, wakapiga mbiu kutangaza habari zake,
ya kwamba yeye ni mtu wa tatu katika ufalme. Usiku uo huo Belshaza, mfalme wa
Wakaldayo, akauawa.”
Ni ukweli usiopingika ya kuwa
vidole vile vilikuwa ni vidole vya Mungu wazo hili katika Daniel lilikuwa ni
wazo linalofanana kabisa na wazo la kile kidole kilichoandika Sheria za Mungu
wakati wa Musa, lakini hapa chanda cha Mungu kinashughulika na mtawala mwenye
kiburi na majivuno na dharau kuhusu Maswala ya Mungu, Mungu huwapinga wenye
kiburi linapokuja swala la Mtu ana kiburi Roho wa Mungu na utendaji wake
unafanya kazi ya kuhukumu na kupinga na wale wanaokataa mambo ya Mungu, wakati
mwingine watu wanapingana na watumishi wa Mungu na kufikiri au kudhani kuwa
watakuwa salama Mungu hawezi kukubali jambo kama hilo litendeke
Zaburi 105:14-15 “Hakumwacha mtu awaonee,
Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao. Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala
msiwadhuru nabii zangu.” Wako watu wanadharau neno la Mungu,
wanadharau ibada, wanadharau watumishi wa Mungu, wanadharau wakristo,
wanadharau wokovu, wanadharau miujiza, na kila kazi zinazofanywa na Roho
Mtakatifu ukweli ni wazi kuwa kidole cha Mungu chanda cha Mungu pia kitahusika
katika kuleta hukumu haraka kwa wenye kiburi na majivuno Mungu huwapinga wenye kiburi bali huwapa wanyenyekevu neema.
Kidole cha Mungu na wakati wa Huduma ya Yesu.
Wakati wa Huduma ya Yesu Krito
duniani neno chanda cha Mungu linaonekana kutumiwa na Bwana Yesu Kristo
mwenyewe, Hii ni baada ya kuwa amemponya kwa muujiza mtu aliyekuwa na pepo bubu
na kziwi, Mafarisayo na wapinzani wa Yesu Kristo walikosoa vikali miujiza
iliyokuwa ikifanywa na Bwana Yesu na kudai kuwa anatoa pepo na kufanya miujiza
kwa nguvu za Belzebuli ona
Mathayo 12:22-24 “Wakati ule akaletewa mtu
mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu akanena na kuona.
Makutano wote wakashangaa, wakasema, Huyu siye mwana wa Daudi? Lakini
Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa
pepo.”
Katika kuwajibu hoja yao
Mafarisayo na wapinzani wa kazi za Mungu Roho Mtakatifu ambaye ndiye nguvu ya
utendaji iliyokuwa ikitenda kazi ndani ya Kristo, Yesu alieleza wazi kuwa
hakuna ufalme unaweza kujipinga wenyewe na hivyo shetani hawezi kuwatoa
mashetani, Bali yeye anayafanya anayoyafanya kwa chanda cha Mungu akimaanisha
miujiza yote na kazi zote za utoaji wa pepo ni matokeo ya kazi za Roho
Mtakatifu atendaye kazi ndani yake na ndani yetu pia
Luka 11:20 “Lakini, ikiwa mimi natoa pepo
kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.” Mathayo
12:24-28 “Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema,
Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo. Basi Yesu akijua mawazo yao,
akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena
mji au nyumba yo yote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama. Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu
ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje? Na mimi nikitoa pepo kwa
Beelzebuli, je! Wana wenu huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo hao ndio
watakaowahukumu. Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa
Mungu umekwisha kuwajilia.”
Katika maandiko yote hayo ya
injili Yesu anasisitiza kuwa anazifanya kazi za Mungu kwa utendaji wa Mungu
ulioko ndani yake chanda cha Mungu, yaani Roho Mtakatifu, hii ndio nguvu ile
ile iliyotenda kazi katika muujiza wa kusababisha chawa na ndio nguvu, iliyoandika
amri za Mungu katika mbao za mawe, na ndio nguvu iliyoandika hukumu katika
ukuta kushughulika na Belshaza, Kidole cha Mungu au chanda cha Mungu ni uweza
wa Mungu usio na mipaka ni ngubvu za Mungu ni upako utendao kazi, Hakuna chombo
cha kibinadamu kinachoweza kupingana na nguvu za kiungu zitendazo kazi za
kiungu, hakuna wachawi wanaweza kushindana na nguvu hizo, hakuna utawala
unaweza kupoingana na nguvu hizo, hakuna mwanasayansi anaweza kupinga a na
nguvu hizo wala hakuna hekima inayozidi hekima ya Chanda cha Mungu ni chanda
cha Mungu ndicho kinachotumika kuponya magonjwa kwa wenye shida za aina
mbalimbali na kushughulika na mahitaji yote ya aina binadamu.
Kidole cha Mungu sio tu kinatenda
miujiza ya uponyaji, lakini pia kinatangaza rehema na msamaha kwa wenye dhambi
na kutukinga na wale waliotukusudia mabaya
Yohana 8:3-8 “Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa
katika uzinzi, wakamweka katikati. Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu
amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa
mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje? Nao wakasema neno hilo wakimjaribu, ili
wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake
katika nchi. Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na
dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. Akainama tena,
akaandika kwa kidole chake katika nchi.”
Wakati watu wanapoorodhesha list
ya dhambi zetu ili tuhukumiwe na Mungu, kidole cha Mungu kinaweza kunadika
rehema kwaajili yetu kinaweza kuandika dhambi ya kila mmoja ya wale
wanaotushitaki, kidole cha Mungu kina uwezo wa kubatilisha hati za mashitaka wakati
wote Neno la Mungu linapoonesha kidole cha Mungu kimehusika mahali lazima tujue
kuwa ni uweza wa Mungu ni utendaji wa Mungu Roho Mtakatifu akiwa kazini. Kamwe
hatupaswi kuogopa kitu, wala kuhofia kitu. Wala hatupaswi kuwaogopa wale
watupingao na kwanza wanaonywa waache kucheza na chanda cha Mungu! Aidha chanda
cha Mungu kinahusika na uumbaji kuonyesha utendaji wa Mungu uliokuwako wakati
wa uumbaji ona
Zaburi 8:1-3 “Wewe, MUNGU, Bwana wetu Jinsi
lilivyo tukufu jina lako duniani mwote! Wewe umeuweka utukufu wako mbinguni;
Vinywani mwa watoto wachanga na wanyonyao Umeiweka misingi ya nguvu; Kwa sababu
yao wanaoshindana nawe; Uwakomeshe adui na mijilipiza kisasi.Nikiziangalia
mbingu zako, kazi ya vidole vyako, Mwezi na nyota ulizoziratibisha;”
Hitimisho
Hivi nilivyo na hivyo ulivyo ni
matokeo ya kazi yake Mungu wetu, adui zako wakikutisha waambie hivi nilivyo ni
chanda cha Mungu, chanda cha Mungu kinaweza kutuelekeza katika sharia yake,
katika hukumu zake, katika utendaji wake wa miujiza, katika utendaji wa nguvu
zake na uwezo wake dhidi ya wapinzani wetu, wakati wote tunaweza kumkumbusha
Mungu ya kuwa tunahitaji kidole chake kihusike katika kila eneo la maisha yetu
na kuleta mpenyo kila amahali pale tunahitaji mpenyo
Na Rev. Innocent Samuel Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.