Jumamosi, 18 Machi 2023

Msaada na wokovu kwa njia nyingine!


Esta 4:13-14 “Naye Mordekai akawaagiza wampelekee Esta jibu la kusema, Wewe usijidhanie kuwa wewe utaokoka nyumbani mwa mfalme, zaidi ya Wayahudi wote. Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo?”   


          


Utangulizi.

Katika Historia ya Dunia moja ya watu au jamii au kabila au taifa la watu waliopitia katika mateso na mashambulizi makali sana duniani ni Wayahudi, Wayahudi wamekuwa watu wa kuchukiwa kila mahali Duniani, Mifumo yote ya kishetani duniani, imepangwa na kukusudia kuharibu kabisa mpango wa Mungu kupitia taifa hilo kuanzia na mpango wa ukombozi wa wanadamu ambao ulikuja pia kupitia Yesu Ktisto kupitia taifa hilo, lakini sio hivyo tu hata mpango wa Mungu wa baadaye. 

Katika maisha yetu vilevile wako watu wengine ambao Mungu ana mpango na makusudi makubwa na maisha yao kwaajili ya kuwahudumia watu wengine! Lakini hata hivyo wamekutana na mashambulizi makali sana kutoka kwa watu mbalimbali kwaajili ya kupambana na maisha yao, na kusudi lile ambalo Mungu ameliweka ndani yao, kokote kule waliko wanachukiwa na kupigwa vita nani tamaa ya shetani na maajenti wake kuona watu hao wanaharibikiwa wanakwenda mbali na nyuso zao na hata kuwaua, Mwalimu alisema kwamba sote tutachukiwa kwaajili ya jina lake. 

Yohana 16:1-3 “Maneno hayo nimewaambia, msije mkachukizwa. Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada. Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi.” 

Kama ilivyo kwa wayahudi na wanafunzi wa Yesu Kristo watachukiwa vilevile, na mtu mmoja mmoja kwa kadiri unavyompenda Mungu utachukiwa na wakati mwingine hata na wakristo wenzako, na au hata watumishi wenzako na wakati mwingine hata watu waliokuzidi kila kitu wanaweza kuchukizwa nawe kumbuka maneno ya Paulo mtume “Ndugu za uongo” hawa watakuchukia na kukuonea wivu na kukutengenezea zengwe ili yamkini uharibikiwe na kuangamizwa nah ii ndio furaha yao au kwa ujinga wakidhani wanafanya mapenzi ya Mungu, katika mazingira kama hayo bado tunapaswa kukumbuka kuwa Mungu yupo naye ndiye tumaini letu na tegemeo letu na ya kuwa ataleta msaada na wokovu kwa njia nyingine hata nje ya zile tunazozitegemea! 

Ni ahadi ya Mungu ya kuwa njia moja ikifungwa atafungua na njia nyingine 

1Wakoritho 10:13 “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.” 

Kuujia Ufalme kwa wakati. 

Kitabu cha Esta kiliandikwa kwa makusudi ya kuwafundisha wayahudi sababu ya kuwepo kwa sikukuu ya Purim,  Neno hilo Purim ni neno la Kiibrania ambalo kwa kiingereza ni “LOTS” kwa Kiswahili ni Kura au Muswada, ni sikukuu ya wayahudi kukumbuka au kufurahia ukombozi uliotokea karne tano hivi kabla ya Kristo kwa wayahudi wachache waliokuwa wakikaa huko uajemi ambao walipitishiwa Mswada na ukapigiwa kura kwamba watu wa kabila hilo wauawe, ni kutokana na wokovu mkubwa walioupata ndipo Mordekai akaamuru waikumbuke siku hiyo na kuiadhimisha kokote waliko 

Esta 9:20-26 “Basi Mordekai aliyaandika mambo hayo; naye akapeleka barua kwa Wayahudi wote waliokaa katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero, waliokuwa karibu na waliokuwa mbali, kuwaonya wazishike siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, na siku ya kumi na tano yake, mwaka kwa mwaka, ambazo ni siku Wayahudi walipojipatia raha mbele ya adui zao, na mwezi uliogeuzwa kwao kuwa furaha badala ya huzuni, na kuwa sikukuu badala ya kilio; wazifanye siku hizo ziwe za karamu na furaha, za kupeana zawadi na za kuwapa maskini vipawa. Nao Wayahudi wakakubali kufanya kama walivyoanza, na kama Mordekai alivyowaandikia; kwa sababu Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, adui ya Wayahudi wote, alikuwa amefanya shauri juu ya Wayahudi ili kuwaangamiza, akapiga Puri, yaani kura, ili kuwakomesha na kuwaangamiza pia; bali mfalme alipoarifiwa, aliamuru kwa barua ya kwamba hilo shauri baya alilolifanya juu ya Wayahudi limrudie kichwani pake mwenyewe; na ya kwamba yeye na wanawe watundikwe juu ya mti. Hivyo wakaziita siku hizo Purimu, kwa jina la Puri. Basi, kwa ajili ya maneno yote ya barua hiyo, na kwa yale waliyoyaona wenyewe juu ya jambo hilo, na mambo yenyewe yaliyowajia”, 

Katika wakati wa tukio hilo la ukombozi Mungu alikuwa ameinua binti wa kiyahudi akliyeitwa Esta kuwa malikia wa uajemi baada ya kuolewa na aliyekuwa mfalme kwa wakati huo, Mordekai mjomba wake alikuja kumtumia binti huyu kuwa sababu ya wokovu mkubwa wa wayahudi alipokuwa madarakani, kuingia kwake madarakani ulikuwa ni mpango wa Mungu ili kwamba aweze kuja kuwa msaada katika wakati mgumu wa saa ya kujaribiwa kwa Israel nani kupitia yeye kweli Mungu alileta wokovu mkubwa, baada ya Mjomba wake Mordekai kumfunulia mpango mbaya uliokuwa umepitishwa wa kuwaabngamiza wayahudi! Esta alikuwa tayari kuyatoa maisha yake kwaajili ya Ndugu zake kwani ilikuwa ni desturi ngumu kuwa kumuendea mfalme bila kibali chake hata kama wewe ni malikia kungekugharimi kifo isipokuwa kama mfalme atakunyooshea fimbo ya dhahabu 

Esta 4:15-16 “Basi Esta akawatuma ili wamjibu Mordekai,Uende ukawakusanye Wayahudi wote waliopo hapa Shushani, mkafunge kwa ajili yangu; msile wala kunywa muda wa siku tatu, usiku wala mchana, nami na wajakazi wangu tutafunga vile vile; kisha nitaingia kwa mfalme, kinyume cha sheria; nami nikiangamia, na niangamie” 

Kwa nini Esta alikubali kujitoa muhanga kwaajili ya watu wake ni baada ya Mordekai kumjulisha kuwa emekuwepo madarakani katika ufalme ule huenda kwa mpango wa Mungu ili awaletee watu wake wokovu, jambo ambalo pia lilimpa heshima kubwa mwanamke huyu! 

Ni muhimu kufahamu kuwa wako watu ambao wakiingia madarakani wanaweza kugeuka na kuwa Baraka kubwa sana kwa jamii na watu, na wako watu ambao wakiingia madarakani wanaweza kuwa sababu ya majutio makubwa sana kwa wengine, ashukuriwe Mungu kuwa esta alikubali kuwa Baraka kwa wengine, lakini wako viongozi ambao wewe na mimi tutaweza kuendelea kuwakumbuka katika maisha yetu katika mazingira yoyote yale iwe serikalini, au kwenye makanisa yetu, au idara zetu, au kazini kwako au kwenye biashara yako au bosi wako, kwamba wao walipoingia madarakani aidha walikuwa Baraka kubwa sana kwako kiasi ukashukuru na kusema wameujia ufalme kwa wakati, lakini wako viongozi wengine ndio wamekuja wakiwa hawajui kusudi la Mungu ndani yako na wote ni kama wakichukua mazoezi ya kufukuza wanataka kukufukuza wewe, wakitaka kuchukua mazoezi ya umbeya wanakufanyia wewe, wewe ndio unakuwa adui mkubwa wewe ndio unakuwa sababu ya vurugu na vujo na kupitishwa kwa miswada mibaya na mipango mibaya na vita za kila aina hwa ni watu wasiojua kwanini wameujia ufalme na wanadani wameujia ufalme ili wakutoe sadaka wewe wakidhani ya kuwa watajipatia heshima kumbuka Mordekai alimuonya Esta kuwa kama wewe hutatambua wajibu wako wakati huu ndipo utakapowajia wayahudi Msaada na wokovu kwa njia nyingine na wewe na mlango wa baba yako utaangamia, ninawatangazia wote ambao Mungu aliwaweka madarakani ili wawe Baraka kwako na kwangu ya kuwa kama hawajui ni kwa nini wameujia ufalme kwa wakati huu kuwa Mungu atatuletea Msaada na wokovu kwa njia nyingine       nao wataabika katika jina la Yesu! 

Msaada na wokovu kwa njia nyingine! 

Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu anatumia watu, na shetani pia anatumia watu, kila mtu aliyeko katika nafasi ya kuwafanyia mema wengine na awafanyie kwa nia njema na nia nzuri,  watu wengi sana wakishapewa nafasi badala ya kuzitumia nafasi hizo kwa kutenda, haki na kuwasaidia watu wa Mungu, kufikia ndoto zao na kutoa msaada wanaingiwa na choyo, wivu, dhuluma, kiburi na kutaka kuabudiwa kama miungu watu, wakati wote wanatafuta Heshima na kama huanguki kuwaabudu wanakasirika sana hiki ndicho kilichowafanya wayahudi kuchukiwa ona 

Esta 3:1-6 “Baada ya hayo mfalme Ahasuero alimwongezea cheo Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, akampandisha, akamwekea kiti chake juu ya maakida wote waliokuwapo pamoja naye. Nao watumishi wote wa mfalme, walioketi mlangoni pa mfalme, wakainama na kumsujudia Hamani, maana ndivyo alivyoamuru mfalme kwa habari zake. Bali Mordekai hakuinama, wala kumsujudia. Basi watumishi wa mfalme walioketi mlangoni pa mfalme wakamwambia Mordekai, Mbona wewe waihalifu amri ya mfalme? Ikawa, waliposema naye kila siku asiwasikilize, wakamwarifu Hamani, ili kuona kama mambo yake Mordekai yatasimama; maana alikuwa amewaambia ya kuwa yeye ni Myahudi. Hata Hamani alipoona ya kwamba Mordekai hainami wala kumsujudia, alighadhibika sana. Akaona si shani kumtia mikono Mordekai peke yake; maana wamemjulisha kabila yake Mordekai; kwa hiyo Hamani alitaka kuwaangamiza Wayahudi wote waliokuwa wakikaa katika ufalme wote mzima wa Ahasuero, yaani, watu wake Mordekai.” 

Unaona kwa sababu ya kutaka Heshima na kutaka kuabudiwa Hamani Mwagagi alikasirika sana na kutaka kuona mambo ya Mordekai yatasiamamaje kisa tu kwa mila na desturi za Kiyahudi hawaruhusiwi kutoa heshima ya Mungu kwa wanadamu, wako kina hamani kila kona katika maisha yetu ambao wamevimbaa, wana uchungu, wana hasira wana mipango mibaya imekusudiwa kwaajili yako pale kazini, pale shuleni, pale kwenye biashara, pale jirani, kila mahali wako watu wenye wivu wenye uchungu, wengine wana kila kitu lakini wivu umewajaa, wanatamani kuwa wao tu maisha yao yote, wako watu wengine wana vyeo kibao, kila taasisi yeye ni mtu mkubwa lakini unaweza kushangaa anakufuatilia wewe ambaye huna hata kuku wa mayaini jambo la kushangaza wako watu wanaotaka ukwame, wako wanaotaka uwe masikini, wako wanaotaka usitoke, wako wanaokuroga, wataroga mpaka na watoto wako, wanataka kuhakikisha kuwa kila kitu chako kinaharibika na hufanikiwi na hiyo ndio furaha yao! Hiyo ni roho ya Hamani, ni wao Mungu aliwaweka ili wawe msaada na wokovu katika maisha yako lakini hata kama wao hawako tayari kufanya hay oleo nataka nikutangazie kuwa uko Msaada na wokovu kwa njia nyingine, Mungu atafanya njia pasipo na njia, Mungu atakuinua sana, Mungu atakupeleka juu, sisi ni wale ambao msaada wetu hautoki kwa wanadamu Msaada wetu u katika Bwana aliyezuiumba mbingu na nchi 

Zaburi 121:1-8 “Nitayainua macho yangu niitazame milima, Msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu u katika Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi. Asiuache mguu wako usogezwe; Asisinzie akulindaye; Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli. Bwana ndiye mlinzi wako; Bwana ni uvuli mkono wako wa kuume. Jua halitakupiga mchana, Wala mwezi wakati wa usiku.  Bwana atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako. Bwana atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele.” 

Unaona wakati wote na kwa karne nyingi wayahudi na wakristo wametiana moyo kwamba wote wanaopitria magumu wasiwaangalie wanadamu, tunajua kuwa Mungu huwatumia wanadamu lakini na shetani pia huwatumia wanadamu, hivyo tunapopitia hatari na kukawa kuna mtu tyunamtegemea atusaidie mtu huyu anaweza kusahau, Yuko mtu ambaye Yusufu alimtafasiria Ndoto gerezani na akamwambia ya kuwa ndugu yangu utakaporudi katika kiti cha mfalme unikumbuke na mimi maana nimefungwa mahali hapa kwa uonevu lakini mtu huyo alisahau ona 

Mwanzo 40: 13-23 “Baada ya siku tatu Farao atakiinua kichwa chako, atakurudisha katika kazi yako; nawe utampa Farao kikombe mkononi mwake, kama desturi ya kwanza, ulipokuwa mnyweshaji wake. Ila unikumbuke mimi, utakapopata mema, ukanifanyie fadhili, nakuomba, ukanitaje kwa Farao, na kunitoa katika nyumba hii. Kwa sababu hakika naliibiwa kutoka nchi ya Waebrania, wala hapa sikutenda neno lo lote hata wanitie gerezani. Mkuu wa waokaji alipoona ya kwamba hiyo tafsiri ni ya mema, akamwambia Yusufu, Mimi kadhalika nilikuwa katika ndoto yangu, na tazama, ziko nyungo tatu za mikate myeupe juu ya kichwa changu. Na katika ungo wa juu, mlikuwa na kila namna ya chakula kwa Farao, kazi za mwokaji; ndege wakavila katika ungo juu ya kichwa changu. Yusufu akajibu, akasema, Tafsiri yake ndiyo hii Nyungo tatu ni siku tatu. Baada ya siku tatu Farao atakiinua na kukuondolea kichwa chako, na kukutundika juu ya mti, na ndege watakula nyama yako. Ikawa siku ya tatu, siku ya kuzaliwa kwake Farao, akawafanyia karamu watumwa wake wote; akakiinua kichwa cha mkuu wa wanyweshaji, na cha mkuu wa waokaji, miongoni mwa watumwa wake. Akamrudisha mkuu wa wanyweshaji katika kazi yake ya kunywesha, naye akampa Farao kikombe mkononi mwake. Bali akamtundika mkuu wa waokaji, kama Yusufu alivyowafasiria. Lakini huyo mkuu wa wanyweshaji hakumkumbuka Yusufu, alimsahau ” 

Nadhani unaweza kuona mioyo ya kibinadamu, wakati mwingine Mungu anafungua milango na kumuinua mtu ili aweze kuwa baraka kwako lakini badala ya Mtu huyo kuwa Baraka anajibariki yeye, hii ilimtokea Yusufu hata alipotoa maagizo unikumbuke mtu yule alimsahau, Biblia inasema lakini mkuu huyo wa wanyweshaji hakumkumbuka Yusufu , wakati mwingine Mungu atainua Mwanamke au mwanaume  katika mahali Fulani kwa kusudi fulani ili wabebe jukumu Fulani na kuyatimiza mapenzi ya Mungu kwako na wanaweza kujisahau au wanaweza kusaidia lakini yote katika yote ni ili Mungu atimize mpango wako kwake katika maisha yako wakikusahau usisikitike, wakikujali usisikitike Mungu ataleta Msaada na wokovu kwa njia nyingine, Mungu anaweza kumtumia kila mmoja wetu kwa nafasi yake kutimiza mpango wake katika maisha yetu nan i muhimu sana kujiangalia katika kila nafasi tulizo nazo tukijisahau basi tujue wazi ya kuwa makudui ya Mungu hayawezi kuzuilika yeye ataleta Msaada na wokovu kwa njia nyingine na sisi wahusika tunaweza kujikuta tunaaangamia  

Esta 4:14 “Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo?” 

Baraka Burton katika wimbo wake NAOMBA NIWE BARAKA Anaimba maneno muhimu sana ambayo Mungu ametaka yaaambatane na ujumbe wangu huu! Kama maombi ya sisi kukubali kutumiwa na Mungu kwa nia njema badala ya kuacha Mungu alete Msaada kwa njia nyingine! ~

Wimbo: Naomba niwe Baraka kwa wengine Na Burton King

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima!     

Hakuna maoni: