Alhamisi, 23 Machi 2023

Chanda cha Mungu !


Kutoka 8: 16 -19 “BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha fimbo yako, ukayapige mavumbi ya nchi, ili kwamba yawe chawa katika nchi yote ya Misri. Nao wakafanya; Haruni akaunyosha mkono wake na fimbo yake, na kuyapiga mavumbi ya nchi, nayo yakawa chawa juu ya wanadamu na juu ya wanyama; mavumbi yote ya nchi yakawa ni chawa katika nchi yote ya Misri. Hao waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao, ili kwamba walete chawa, lakini wasiweze; nako kulikuwa na chawa juu ya wanadamu, na juu ya wanyama. Ndipo wale waganga wakamwambia Farao, Jambo hili ni chanda cha Mungu; na moyo wake Farao ukawa mgumu asiwasikize; vile vile kama BWANA alivyonena.”




Utangulizi:

Neno Chanda cha Mungu limejitokeza au kutajwa katika Biblia ya Kiebrania kama neno “etsba” kimatamshi “ets-bah” na kutajwa katika Biblia ya kiingereza ya King James Version mara 32  na kwa lugha ya kiyunani ni “Daktulos” kimatamshi ni Dak-too-los  ambalo Katika Biblia ya kiingereza ya King James Version limetajwa mara 8, maneno yote hayo katika lugha ya kiibrania na kiyunani yanamaanisha kidole cha Mungu, Neno ambalo kinabii linahusiana na Utendaji wa Roho Mtakatifu, hata hivyo Pamoja na neno hilo kutajwa mara kadhaa, limeonekana kwa uwazi katika matukio kadhaa likitumika kwa namna kali zaidi ya maeneo mengine.

·         Kidole cha Mungu wakati wa Farao.

·         Kidole cha Mungu Katika mlima wa Sinai.

·         Kidole cha Mungu wakati wa Beltshaza.

·         Kidole cha Mungu na wakati wa Huduma ya Yesu.

Kidole cha Mungu wakati wa Farao!

Neno kidole cha Mungu linajitokeza kwa mara ya kwanza katika lugha za kinabii, kutokana na uandishi wa Musa katika kitabu cha kutoka mara baada ya Musa na Haruni kuamuriwa na Mungu kuachilia pigo la tatu, Mapigo haya yalikuwa ni amri ya Mungu ili kumlazimisha Farao kuwaachia wana wa Israel waende zao kwa sababu walikaa katika inchi ya Misri na katika hali ya utumwa kwa zaidi ya miaka 400, Mungu alimuelekeza Musa kumuamuru Haruni kunyoosha fimbo yake ili kuyapiga mavumbi ya nchi yapate kuwa chawa katika inchi yote ya Misri

Kutoka 8:16-17BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha fimbo yako, ukayapige mavumbi ya nchi, ili kwamba yawe chawa katika nchi yote ya Misri. Nao wakafanya; Haruni akaunyosha mkono wake na fimbo yake, na kuyapiga mavumbi ya nchi, nayo yakawa chawa juu ya wanadamu na juu ya wanyama; mavumbi yote ya nchi yakawa ni chawa katika nchi yote ya Misri.”

Kwa kawaida kila Muujiza ambao Musa na Haruni waliufanya kwa jina la Mungu, utaweza kuona wachawi wa kimisri nao waliigiza hasa kwa miujiza ya mwanzoni walipojaribu kuuigiza muujiza huu kwa uchawi wao na kushindwa ndipo walipotamka wenyewe kwa midomo yao kumueleza Farao kuwa hiki ni chanda cha Mungu,

Kutoka 8:18-19 “Hao waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao, ili kwamba walete chawa, lakini wasiweze; nako kulikuwa na chawa juu ya wanadamu, na juu ya wanyama. Ndipo wale waganga wakamwambia Farao, Jambo hili ni CHANDA CHA MUNGU; na moyo wake Farao ukawa mgumu asiwasikize; vile vile kama BWANA alivyonena.”  Hapo ndipo tunapouona uweza wa Mungu katika kutenda miujiza ya kupita kawaida dhidi ya miujiza ya kichawi na ya kimazingaombwe, Mungu ana uwezo mkubwa sana, anapukusudia kutukomboa katika utumwa wa anina yoyote ile ni lazima tumuitie yeye kwa uweza wa Roho wake Mtakatifu ambaye ndiye chanda cha Mungu atatutoa katika mikandamizo ya aina yoyote ile                            

Kidole cha Mungu Katika mlima wa Sinai.

Eneo lingine ambapo tunaona maandiko yakitaja chanda cha Mungu ni katika Mlima wa Sinai wakati Mungu alipokuwa anataka kumpa Musa Amri na sharia zake ili awafundishe watu wake, wakati Amri Kumi za Msingi zilipokuwa zinaandikwa tunaelezwa kuwa amri hizo ziliandikwa kwa kidole cha Mungu yaani Chanda cha Mungu

Kutoka 31:18 “Hapo BWANA alipokuwa amekwisha zungumza na Musa katika mlima wa Sinai, akampa hizo mbao mbili za ushuhuda, mbao mbili za mawe, zilizoandikwa kwa chanda cha Mungu.”

Musa analikumbuka tukio hilo la amri na sharia za Mungu kuandikwa kwa kidole chake wakati alipokuwa anawaandikia kitabu kingine cha kumbukumbu la Torati ona katika

Kumbukumbu la Torati 9:9 -10 “Na hapo nilipokwea mlimani kwenda kuzipokea mbao za mawe, nazo ni mbao za agano Bwana alilofanya nanyi, ndipo nikakaa mle mlimani siku arobaini usiku na mchana; sikula chakula wala kunywa maji. Bwana akanipa zile mbao mbili za mawe zimeandikwa kwa kidole cha Mungu; na juu yake yameandikwa maneno mfano wa yote aliyosema nanyi Bwana mle mlimani toka kati ya moto siku ya mkutano.”  

Haikuwa lazima kuwa labda Mungu aliandika ka ma wanadamu waandikavyo kwa kuwa Mungu ni Roho lakini haipingiki kuwa uwezo wake wa utendaji ROHO MTAKATIFU alisababisha kwa muujiza mkubwa sharia zake za msingi kuwepo katika mawe yale, ni ukweli usiopingika kuwa kama Roho Mtakatifu aliweza kuziandika sharia za Mungu katika mawe hashindwi kuziandika sharia zake katika mioyo yetu neno la Mungu linaeleza wazi kuwa uko wakati ambapo Mungu ataziandika sheria zake katika mioyo yetu  

2 Wakoritho 3:2-3  Ninyi ndinyi barua yetu, iliyoandikwa mioyoni mwetu, inajulikana na kusomwa na watu wote; mnadhihirishwa kwamba mmekuwa barua ya Kristo tuliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo ni mioyo ya nyama.”  

Unaona Roho Mtakatifu yaani utendaji wa Mungu ulioandika sharia kwa kidole cha Moto katika mlima wa Sinai yu aweza kuandika sheria zake na kuweka mwako wa moto katika mioyo yetu ili tumtii Mungu, tunaweza kusoma mapenzi ya Mungu leo kutoka Moyoni kwa kuelekezwa na kufundishwa na Roho Mtakatifu

1Yohana 3:21-24 “Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu; na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake. Na hii ndiyo amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri. Naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake yeye naye ndani yake. Na katika hili tunajua ya kuwa anakaa ndani yetu, kwa huyo Roho aliyetupa.”

 Utendaji wa Mungu ndani yetu unaweza kuihuisha sharia ya Mungu ndani yetu na kutugeuza kuwa mfano wa kuigwa kwa kila mtu duniani, hata kama ulimwengu unaweza kuwa umeharibika kwa kiwango gani Roho Mtakatifu ndani yetu atatuongoza na kutuhifadhi na kuionya mioyo yetu na kutuelekeza katika sharia ya Mungu wetu sharia ya kifalme sharia ya Roho wa Uzima kwa sababu hiyo sisi sasa hatuongozwi na sharia ile ya kimwili iletayo mauti bali twaongozwa na sharia ya Roho wa Uzima ulio katika Kristo Yesu.

Warumi 8:1-4Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti. Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili; ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.”      

Kidole cha Mungu wakati wa Beltshaza.

Eneo lingine ambapo tunauona utendaji wa Mungu kama Kidole chake ni wakati wa kipindi cha utawala wa mfalme Mpumbavu aliyeitwa Belshaza mfalme huyu hakujua ya kuwa Mungu ndiye anayeweka watu madarakani, yeye aliamuru vyombo vilivyokuwa vimetekwa kutoka Hekalu lililokuwako Yerusalem, na baba yake Mfalme mkuu Nebukadreza ambaye baadaye alimuheshimu sana Mungu wa Israel, lakini Belshaza yeye alikuwa na dharau hakuthamini vyombo vile vya Hekaluni ambavyo kimsingi vilikuwa vimewekwa wakfu, chombo kinapokuwa kimewekwa Wakfu maana yake Roho wa Mungu anakuwa amevitenga na kuviheshimu lakini Beslshaza badala yake yeye aliamua kuvidhalilisha kwa kuvinywea pombe ona katika

Daniel 5:1-4 “Belshaza, mfalme, aliwafanyia wakuu wake elfu karamu kubwa akanywa divai mbele ya elfu hao. Belshaza, alipokuwa akionja ile divai, akaamuru wavilete vile vyombo vya dhahabu na fedha, ambavyo baba yake, Nebukadreza, alivitoa katika hekalu lililokuwako Yerusalemu; ili kwamba mfalme, na wakuu wake, na wake zake, na masuria wake, wapate kuvinywea. Basi wakavileta vile vyombo vya dhahabu, vilivyotolewa katika hekalu la nyumba ya Mungu lililokuwako Yerusalemu; na mfalme na wakuu wake, na wake zake, na masuria wake, wakavinywea. Wakanywa divai, wakaisifu miungu ya dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe.”

Ukweli ni wazi kuwa tukio hili lilimuuzunisha sana Mungu wa Israel, Mungu hawezi kukubali vyombo vyake alivyovoweka wakfu kwa kuvitakasa vitumike kinyume na makusudi ya Mungu aliye hai, wakati tukio hili lililpokuwa likiendelea mfalme aliona katika ukuta kiganja cha mkono kikiandika kwa vidole vya kibinadamu kumtangazia mfalme huyu hukumu yake kwa haraka ona

Daniel 5:5-6 “Saa iyo hiyo vikatokea vidole vya mkono wa mwanadamu, vikaandika katika chokaa ya ukuta wa nyumba ya enzi ya mfalme, mahali palipokikabili kinara; naye mfalme akakiona kitanga cha ule mkono ulioandika. Ndipo uso wa mfalme ukambadilika; fikira zake zikamfadhaisha; viungo vya viuno vyake vikalegea; magoti yake yakagongana.”

 Jambo hili lilikuwa jambo la kutisha sana lugha ya kibiblia hapo VIUNGO VYA VIUNO VYAKE VIKALEGEA ni lugha ya kiungwana kuwa mfalme alijinyea na kujiharishia kwa hofu, tabia mbaya aliyokuwa nayo na dhadhau yake dhidi ya mambo ya Mungu ilikuwa sasa inashughulikiwa na utendaji wa Mungu mwenyewe, vidole hivyo vya Mungu vilikuwa vimentangazia hukumu ya Mungu na hukumu yake ilikuwa ni kifo kwa sababu amevuka mpaka Daniel ambaye ndiye alikuja kuyatafasiri maneno yale alisema

Daniel 5: 22-30 “Na wewe, mwanawe, Ee Belshaza, hukujinyenyekeza moyo wako, ijapokuwa ulijua hayo yote. Bali umejiinua juu ya Bwana wa mbingu; nao wamevileta vyombo vya nyumba yake mbele yako; na wewe, na wakuu wako, na wake zako, na masuria wako, mmevinywea; nawe umeisifu miungu ya fedha na ya dhahabu na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe; wasioona, wala kusikia, wala kujua neno lo lote; na Mungu yule, ambaye pumzi yako i mkononi mwake, na njia zako zote ni zake, hukumtukuza. Ndipo kile kitanga cha ule mkono kikaletwa kutoka mbele zake, na maandiko haya yameandikwa. Na maandiko yaliyoandikwa ni haya; MENE, MENE, TEKELI, NA PERESI. Na tafsiri ya maneno haya ni hii; MENE, Mungu ameuhesabu ufalme wako na kuukomesha. TEKELI, umepimwa katika mizani nawe umeonekana kuwa umepunguka. PERESI, ufalme wako umegawanyika, nao wamepewa Wamedi na Waajemi. Ndipo Belshaza akatoa amri, nao wakamvika Danieli mavazi ya rangi ya zambarau, wakatia mkufu wa dhahabu shingoni mwake, wakapiga mbiu kutangaza habari zake, ya kwamba yeye ni mtu wa tatu katika ufalme. Usiku uo huo Belshaza, mfalme wa Wakaldayo, akauawa.”

Ni ukweli usiopingika ya kuwa vidole vile vilikuwa ni vidole vya Mungu wazo hili katika Daniel lilikuwa ni wazo linalofanana kabisa na wazo la kile kidole kilichoandika Sheria za Mungu wakati wa Musa, lakini hapa chanda cha Mungu kinashughulika na mtawala mwenye kiburi na majivuno na dharau kuhusu Maswala ya Mungu, Mungu huwapinga wenye kiburi linapokuja swala la Mtu ana kiburi Roho wa Mungu na utendaji wake unafanya kazi ya kuhukumu na kupinga na wale wanaokataa mambo ya Mungu, wakati mwingine watu wanapingana na watumishi wa Mungu na kufikiri au kudhani kuwa watakuwa salama Mungu hawezi kukubali jambo kama hilo litendeke

Zaburi 105:14-15 “Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao. Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.” Wako watu wanadharau neno la Mungu, wanadharau ibada, wanadharau watumishi wa Mungu, wanadharau wakristo, wanadharau wokovu, wanadharau miujiza, na kila kazi zinazofanywa na Roho Mtakatifu ukweli ni wazi kuwa kidole cha Mungu chanda cha Mungu pia kitahusika katika kuleta hukumu haraka kwa wenye kiburi na majivuno Mungu huwapinga wenye kiburi bali huwapa wanyenyekevu neema.

Kidole cha Mungu na wakati wa Huduma ya Yesu.

Wakati wa Huduma ya Yesu Krito duniani neno chanda cha Mungu linaonekana kutumiwa na Bwana Yesu Kristo mwenyewe, Hii ni baada ya kuwa amemponya kwa muujiza mtu aliyekuwa na pepo bubu na kziwi, Mafarisayo na wapinzani wa Yesu Kristo walikosoa vikali miujiza iliyokuwa ikifanywa na Bwana Yesu na kudai kuwa anatoa pepo na kufanya miujiza kwa nguvu za Belzebuli ona

Mathayo 12:22-24 “Wakati ule akaletewa mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu akanena na kuona. Makutano wote wakashangaa, wakasema, Huyu siye mwana wa Daudi? Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo.”

Katika kuwajibu hoja yao Mafarisayo na wapinzani wa kazi za Mungu Roho Mtakatifu ambaye ndiye nguvu ya utendaji iliyokuwa ikitenda kazi ndani ya Kristo, Yesu alieleza wazi kuwa hakuna ufalme unaweza kujipinga wenyewe na hivyo shetani hawezi kuwatoa mashetani, Bali yeye anayafanya anayoyafanya kwa chanda cha Mungu akimaanisha miujiza yote na kazi zote za utoaji wa pepo ni matokeo ya kazi za Roho Mtakatifu atendaye kazi ndani yake na ndani yetu pia

Luka 11:20 “Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.” Mathayo 12:24-28 “Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo. Basi Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena mji au nyumba yo yote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama.  Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje? Na mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, je! Wana wenu huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo hao ndio watakaowahukumu. Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.”

Katika maandiko yote hayo ya injili Yesu anasisitiza kuwa anazifanya kazi za Mungu kwa utendaji wa Mungu ulioko ndani yake chanda cha Mungu, yaani Roho Mtakatifu, hii ndio nguvu ile ile iliyotenda kazi katika muujiza wa kusababisha chawa na ndio nguvu, iliyoandika amri za Mungu katika mbao za mawe, na ndio nguvu iliyoandika hukumu katika ukuta kushughulika na Belshaza, Kidole cha Mungu au chanda cha Mungu ni uweza wa Mungu usio na mipaka ni ngubvu za Mungu ni upako utendao kazi, Hakuna chombo cha kibinadamu kinachoweza kupingana na nguvu za kiungu zitendazo kazi za kiungu, hakuna wachawi wanaweza kushindana na nguvu hizo, hakuna utawala unaweza kupoingana na nguvu hizo, hakuna mwanasayansi anaweza kupinga a na nguvu hizo wala hakuna hekima inayozidi hekima ya Chanda cha Mungu ni chanda cha Mungu ndicho kinachotumika kuponya magonjwa kwa wenye shida za aina mbalimbali na kushughulika na mahitaji yote ya aina binadamu.

Kidole cha Mungu sio tu kinatenda miujiza ya uponyaji, lakini pia kinatangaza rehema na msamaha kwa wenye dhambi na kutukinga na wale waliotukusudia mabaya

Yohana 8:3-8Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati. Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje? Nao wakasema neno hilo wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi.”

Wakati watu wanapoorodhesha list ya dhambi zetu ili tuhukumiwe na Mungu, kidole cha Mungu kinaweza kunadika rehema kwaajili yetu kinaweza kuandika dhambi ya kila mmoja ya wale wanaotushitaki, kidole cha Mungu kina uwezo wa kubatilisha hati za mashitaka wakati wote Neno la Mungu linapoonesha kidole cha Mungu kimehusika mahali lazima tujue kuwa ni uweza wa Mungu ni utendaji wa Mungu Roho Mtakatifu akiwa kazini. Kamwe hatupaswi kuogopa kitu, wala kuhofia kitu. Wala hatupaswi kuwaogopa wale watupingao na kwanza wanaonywa waache kucheza na chanda cha Mungu! Aidha chanda cha Mungu kinahusika na uumbaji kuonyesha utendaji wa Mungu uliokuwako wakati wa uumbaji ona

Zaburi 8:1-3 “Wewe, MUNGU, Bwana wetu Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote! Wewe umeuweka utukufu wako mbinguni; Vinywani mwa watoto wachanga na wanyonyao Umeiweka misingi ya nguvu; Kwa sababu yao wanaoshindana nawe; Uwakomeshe adui na mijilipiza kisasi.Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako, Mwezi na nyota ulizoziratibisha;”

Hitimisho

Hivi nilivyo na hivyo ulivyo ni matokeo ya kazi yake Mungu wetu, adui zako wakikutisha waambie hivi nilivyo ni chanda cha Mungu, chanda cha Mungu kinaweza kutuelekeza katika sharia yake, katika hukumu zake, katika utendaji wake wa miujiza, katika utendaji wa nguvu zake na uwezo wake dhidi ya wapinzani wetu, wakati wote tunaweza kumkumbusha Mungu ya kuwa tunahitaji kidole chake kihusike katika kila eneo la maisha yetu na kuleta mpenyo kila amahali pale tunahitaji mpenyo

Na Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.  

Hakuna maoni: