Zaburi 138:6-8 “Ingawa Bwana yuko juu, amwona mnyenyekevu, Naye amjua mwenye kujivuna tokea mbali. Nijapokwenda kati ya shida utanihuisha, Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu, Na mkono wako wa kuume utaniokoa. Bwana atanitimilizia mambo yangu; Ee Bwana, fadhili zako ni za milele; Usiziache kazi za mikono yako.”
Utangulizi:
Duniani ni mahali ambapo pana
changamoto za aina mbalimbali ambazo kila mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke
atakutana nazo, wakati mwingine tutakutana na hali ngumu sana ama upinzani
mzito sana, au magonjwa makubwa ya kusumbua au kuwa na ndoto kubwa ambazo tunatafuta namna ya kuzitimiza, na
changamoto nyinginezo nyingi, na wakati mwingine hali Fulani za kukatisha tamaa
na kuvunja moyo na ama wakati mwingine ukiwa katika vita kali sana, katika
ndoa, katika kazi, katika masomo, katika biashara, katika mashamba, katika
mifugo na katika mahusiano taabu hizi zote Yesu Kristo anazifahamu na anajua ya
kuwa tunazipitia na alitutaka tujipe moyo kwa sababu yeye amezishinda kwaajili
yetu.
Yohana 16:33 “Hayo nimewaambieni mpate kuwa
na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi
nimeushinda ulimwengu.”
Yesu anazungumza maneno haya kwa
sababu anatambua wazi kuwa wakati mwingine tunaweza kujiona kama tuna mapungufu
Fulani nani kama hatutoshi wala hatustahili hata kufanyiwa muujiza, lakini ni
muhimu sana kukumbuka ya kuwa Mungu yuko pamoja nasi yeye anaitwa Emmanuel
yaani Mungu pamoja nasi na wakati tunapopitia kila aina ya changamoto na mambo
yoyote yanayotukabili yeye yuko pamoja nasi, alikuwa pamoja na Yesu Kristo
katika mateso yake na alihakikisha anamfufua, na hakumuacha kaburini, wakati
Daudi anakabiliana na jitu kubwa kuliko uwezo wake Mungu alikuwa pamoja naye,
wakati Paulo na Sila wakiwa gerezani ni yeye aliyafungua milango ya gereza,
wakati Danieli anatupwa katika tundu la Simba ni yeye aliyekuweko kufunga
makanwa ya simba, na wakati Shadrak, Meshak na Abednego wakitupwa kwenye tanuri
la moto mkali ni yeye ndiye aliyejiunga nao wasiunguzwe jambo kubwa la msingi
ni kukumbuka tu ya kuwa Mungu yuko kati kati ya shida zako.
Zaburi 138:6-8 “Ingawa Bwana yuko juu,
amwona mnyenyekevu, Naye amjua mwenye kujivuna tokea mbali. Nijapokwenda kati
ya shida utanihuisha, Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu, Na mkono
wako wa kuume utaniokoa. Bwana atanitimilizia mambo yangu; Ee Bwana, fadhili
zako ni za milele; Usiziache kazi za mikono yako.”
Katika mistari hii ya msingi
hususani mstari ule wa saba yaani Zaburi
ya 138:7 “Nijapokwenda kati ya shida utanihuisha,
Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu, Na mkono wako wa kuume utaniokoa.” Mungu
nanatufundisha kupitia mtumishi wakeMwandishi wa zaburi hii ya kuwa yeye huwa
katikakati ya shida zetu mstari huu katika lugha ya kiingereza Biblia ya NIV
husomeka hivi “Though
I walk in the midst of trouble, you preserve my life you stretch out your hand
against the anger of my foes with your hand you save me” ambapo
katika tafasiri yangu naweza kusema Mstari huu unasema hivi NINAPOPITA KATIKATI YA TAABU/SHIDA UNANYOOSHA MKONO WAKO KUNIOKOA
NA HASIRA ZA ADUI ZANGU, Yaani maana yake katikati ya shida Mungu
anakuwepo, na anatoa msaada kwaajili ya utukufu wake hii maana yake ni nini ?
sio kila wakati Mungu atakutoa nje ya shida lakini wakati mwingine atakuacha
uingie katika shida na changamoto mbalimbali kisha ataweka mkono wake kwaajili
ya utukufu wake, kwa sababu hiyo jambo kubwa la Msingi na la kukumbuka ni kuwa
Bwana yuko pamoja nawe bila kujali hali unayoipitia, kuokolewa katika shida sio
jambo la Msingi sana kama Mungu kuwa pamoja nawe, Mungu kuwa pamoja nawe hilo
ndio jambo kubwa na la msingi,
Isaya 43:1-2 “Lakini sasa, Bwana
aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope,
maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu. Upitapo katika maji
mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika
moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.”
Unaona haijalishi kuna dhuruba
kiasi gani kama Mungu yuko pamoja nawe hakuna kitakachoshindikana kwaajili ya
utukufu wake, Mungu atatokeza muujiza kwa sababu yumo katikati ya shida yako
pamoja nawe
Kumbuka kuwa
1.
Wakati
Suleiman anaanza kutawala alikuwa na hofu kuwa anawezaje kuongoza taifa kubwa
na watu wengi kama wale, baba yake alikuwa mtu wa vita na mtu aliyemtegemea
Mungu, hivyo Mungu alimsaidia Suleimani kuwa na hekima ya namna ya kuingia na
kutoka na mambo yakawa shwari
2.
Mungu
hakumuwacha Yesu asisulubiwe lakini alimfufua siku ya tatu, hakumwacha
mtakatifu wake aonje uharibifu
3.
Mungu
hakumwacha Nyangumi asimmeze Yona na badala yake alimsababisha nyangumi
amtapike Yona siku ya tatu
4.
Mungu
hakumuacha Daniel asiingizwe kwenye tundu la Simba badala yake aliyafunga
makanwa ya simba
5.
Mungu
hakuwaacha Shadrak na Meshak na Abednego wasitupwe katika tanuru la Moto lakini
badala yake alijiunga nao katikati ya Moto ili usiwateteze
6.
Mungu
hakuwaacha Paulo na Silas wasipigwe na kutupwa gerezani lakini badala yake
aliwaacha wakafungwa gerezani na baadaye akayafungua malango ya magereza na
vifungo vyake
Changamoto kubwa katika maisha
yetu sio kutokupitia changamoto bali ni kumuomba Mungu awe pamoja nasi hili
ndilo jambo la Msingi Yesu aliahidi ya kuwa atakuwa pamoja nasi hata ukamilifu
wa dahari, na alihahidi kuwa tunapokutanika wawili au watatu kwa ajili ya jina
lake atakuwa pamoja nasi, Hakuna jambo la msingi duniani kama kuwa na Mungu,
Muulize jirani yako una Mungu ukiwa na Mungu una kila kitu!, Changamoto yako
sio kubwa kuliko Mungu tunayemtumikia na kumuabudu, Bwana ampoe neema kila
mmoja wetu kuwa na Mungu wakati tunapopita katika siku za kujaribiwa kwetu
katika jina la Yesu Kristo amen!
Na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni