1Wakorintho 16:7-9 “Maana sipendi kuonana
nanyi sasa, katika kupita tu, kwa sababu nataraji kukaa kwenu muda kidogo, Bwana
akinijalia. Lakini nitakaa Efeso hata Pentekoste; kwa maana nimefunguliwa
mlango mkubwa wa kufaa sana, na wako wengi wanipingao.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa katika
maisha yetu ya kila siku duniani, hatupaswi kuwa na huzuni pale tunapoona jambo
moja katika maisha yetu limekwama, na ukajaribu na lingine likakwama, na
lingine likakwama, hii haimaanishi kuwa unatakiwa kukata tamaa, na kama ulikuwa
unamuomba Mungu au wewe ni mtu wa Mungu acha kufikiri kuwa ndio basi, Mungu
katika mpango wake ameweka majira na nyakati mbalimbali kwa makusudi maalumu
wakati mwingine tusiyoajua au tutakayoyajua baadaye kwa manufaa yetu
Muhubiri 3:1 “Kwa kila jambo kuna majira
yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu”
Kwa msingi huo kila changamoto
unayoipitia katika maisha yako kumbuka kuwa wewe sio wa kwanza, wako na wenzako
au na wengine waliopitia, alieleza dada mkoja ambaye aliwahi kufungwa gerezani
kwa kosa la kusingiziwa na akaa gerezani mwaka mmoja tena akiwa ananyonyesha
anasema kule gerezani hali aliyoiona alimsamehe hata mtu aliyemfikisha
gerezani, kwani alikutana na watu wenye changamoto kubwa kuliko zake na
waliofungwa miaka mingi Zaidi kuliko yake na walisingiziwa makossa makubwa Zaidi
na kudhulumiwa hata kuliko yeye, Maandiko yamejaa mifano ya watu kadhaa wa
kadhaa katika maandiko ambao walipitia changamoto za aina mbalimbali wengine
wakisingiziwa n ahata kufungwa gerezani lakini hatimaye walitoka au Mungu
alitafuta njia ya kuwatoa huko, Mungu atakutoa na wewe vilevile Haleluyaaa! Tutajifunza
somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Kufunguliwa mlango wa kufaa sana
·
Mifano ya watu waliofunguliwa milango ya kufaa
·
Jinsi ya kufunguliwa mlango wa kufaa
Kufunguliwa mlango wa kufaa sana
1Wakorintho 16:7-9 “Maana sipendi kuonana
nanyi sasa, katika kupita tu, kwa sababu nataraji kukaa kwenu muda kidogo, Bwana
akinijalia. Lakini nitakaa Efeso hata Pentekoste; kwa maana nimefunguliwa
mlango mkubwa wa kufaa sana, na wako wengi wanipingao.”
Paulo mtume anafunua mpango wake
uliokuwa moyoni mwake kwaajili ya Kanisa lililokuwako Korintho, anaelezea
mpango wake kuwa ilikuwa apate nafasi ya kwenda Korintho na kukaa nao kwa muda
wa kutosha hususani wakati wa baridi, hata hivyo vilevile alikuwa na makusudi
ya kukaa Efeso mpaka wakati wa Pentekoste, lakini hata hivyo ilikuwa ngumu pia
kuwaaachaWaefeso kwa sababu huko alikuwa amefunguliwa mlango mkubwa wa kufaa
sana, ni kwa jinsi gani Paulo anaelezea kuchelewa kwenda Korintho na kuendelea
kubaki Efeso sababu kubwa ni kuwa amefunguliwa mlango mkubwa wa kufaa sana !
Paulo anatumia mfano wa mlango
akimaanisha kuwa injili yake imepata kibali na watu wa Efeso wanalipokea neno
la Mungu kwa kiwango kikubwa sana na cha hali ya juu , Kila wakati Paulo mtume
alipopata nafasi na kibali cha kuihubiri injili mahali na mahali hapo pakawa na
moyo mkubwa wa kuikubali injili aliitqa swala hilo kufunguliwa mlango ona
2Wakorintho 2:12 “Basi nilipofika Troa kwa
ajili ya Injili ya Kristo, nikafunguliwa mlango katika Bwana”,
Hii ni kwa sababu ziko sehemu au
maeneo mengine ambayo kuipokea kwao injili kulikuwa ni kwa ugumu sana na wakati
mwingine kwa upinzani mkubwa sana, iko miji ambayo Paulo alitamani sana
aihubiri injili lakini shetani akiwatumia watu alipinga vikali sana na huduma
ya Paulo mtume, wakati mwingine alikimbia usiku kutoka mji mmoja kwenda mji
mwingine
Matendo 17:1-10 “Wakiisha kupita kati ya
Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambapo palikuwa na sinagogi la
Wayahudi. Na Paulo, kama ilivyokuwa desturi yake, akaingia mle walimo,
akahojiana nao kwa maneno ya maandiko sabato tatu, akiyafunua na kuwaeleza ya
kwamba ilimpasa Kristo kuteswa, na kufufuka katika wafu; na ya kwamba, Yesu
huyu ninayewapasha ninyi habari zake ndiye Kristo. Wengine miongoni mwao
wakaamini, wakashikamana na Paulo na Sila; na Wayunani waliomcha Mungu, wengi
sana, na wanawake wenye cheo si wachache. Na Wayahudi wakaona wivu,
wakajitwalia watu kadha wa kadha katika watu ovyo wasio na sifa njema, nao
wakakutanisha mkutano, wakafanya ghasia mjini, wakawaendea watu wa nyumba ya
Yasoni, wakataka kuwapeleka mbele ya watu wa mji; na walipowakosa, wakamkokota
Yasoni na baadhi ya ndugu mbele ya wakubwa wa mji, wakipiga kelele, wakisema,
Watu hawa walioupindua ulimwengu wamefika huku nako, na Yasoni amewakaribisha;
na hawa wote wanatenda mambo yaliyo kinyume cha amri za Kaisari, wakisema na
kwamba yupo mfalme mwingine, aitwaye Yesu. Wakafadhaisha ule mkutano na wakubwa
wa mji walipoyasikia hayo. Nao walipokwisha kumtoza dhamana Yasoni na wenziwe
wakawaacha waende zao. Mara hao ndugu wakawapeleka Paulo na Sila usiku hata
Beroya. Nao walipofika huko wakaingia katika sinagogi la Wayahudi.”
Kutokana na upinzani huu wa mara
kwa mara dhidi ya injili, Paulo mtume aliwaomba wakristo wa makanisa ya miji
mingine kuwa na maombi rasmi ya kumuombea ili kwamba afunguliwe mlangowa injili,
Wakolosai 4:2-3 “Dumuni sana katika kuomba,
mkikesha katika kuomba huku na shukrani; mkituombea na sisi pia, kwamba Mungu
atufungulie mlango kwa lile neno lake, tuinene siri ya Kristo, ambayo kwa ajili
yake nimefungwa,”
Katika mji wa Efeso mambo
yalikuwa ni tofauti sana na maeneo mengine, watu wa Efeso walipomuona Paulo
mtume kwa mara ya kwanza na kumsikia katika sinagogi hata wayahudi wa Efeso
walimtaka Paulo akae kwao siku nyingi Zaidi, Paulo alikuwa na safari ya kwenda
Syria (Shamu) na hivyo aliwaahidi kuwa angerejea tena ona
Matendo 18:18-19 “Baada ya hayo Paulo
akazidi kukaa huko siku nyingi, kisha akaagana na ndugu akaabiri kwenda Shamu;
na Prisila na Akila wakaenda pamoja naye, alipokwisha kunyoa kichwa chake huko
Kenkrea; maana alikuwa ana nadhiri. Wakafika Efeso, akawaacha huko. Yeye
mwenyewe akaingia katika sinagogi, akahojiana na Wayahudi. Walipomtaka akae
wakati mwingi zaidi, hakukubali;”
Paulo aliporejea Efeso baadaye
mlango mkubwa sana wa injili ulifunguka, watu walilipokea neno la Mungu kwa furaha
kubwa sana pamoja na kuwa injili huwa inapingwa lakini Pale Efeso alipata neema
ya kukaa muda mrefu zaidi na hivyo kuwa na kanisa imara sana, Katika mji huu
Paulo alitumiwa na Mungu kwa miujiza mikubwa sana na kupita kawaida, watu wengi
walikuja kwa Bwana na sio hivyo tu waliokuwa wachawi na waaguzi waliacha uchawi
na kuchoma moto vifaa vyao vya kiroho na vitabu vyao vya thamani kubwa sana na
kushikamana na Paulo
Matendo 19:8-11 “Akaingia ndani ya
sinagogi, akanena kwa ushujaa kwa muda wa miezi mitatu, akihojiana na watu, na
kuwavuta katika mambo ya ufalme wa Mungu. Lakini wengine walikaidi, wakakataa
kuamini, wakiitukana ile Njia mbele ya mkutano; basi, akaondoka akawaacha,
akawatenga wanafunzi, akahojiana na watu kila siku katika darasa ya mtu mmoja,
jina lake Tirano. Mambo haya yakaendelea kwa muda wa miaka miwili, hata wote
waliokaa Asia wakalisikia neno la Bwana, Wayahudi kwa Wayunani. Mungu akafanya
kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida;”
Matendo 19:18-20 “Na wengi wa wale
walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao. Na watu wengi katika
wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele
ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha
hamsini elfu. Hivyo ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda kwa nguvu.”
Ni kutokana na mafanikio makubwa
sana Paulo mtume anaelezea kuwa katika huduma yake ambayo kimsingi ilikuwa na
upinzani mkubwa sana anaona kuwa amefunguliwa mlango mkubwa wa kufaa sana Pale
Efeso licha ya kuwepo kwa upinzani wa hapa na pale, Muda alioutumia Pale Efeso
ulimkosesha Fursa ya kwenda Korintho kwa kusudi la kuwaimarisha huko nako na
ndipo alipowaandikia kuwa anatamani kuwa nao lakini alikuwa amefunguliwa mlango
mkubwa sana wa kufaa japo kuna upinzani mdogo
1Wakorintho 16:7-9 “Maana sipendi kuonana
nanyi sasa, katika kupita tu, kwa sababu nataraji kukaa kwenu muda kidogo, Bwana
akinijalia. Lakini nitakaa Efeso hata Pentekoste; kwa maana nimefunguliwa
mlango mkubwa wa kufaa sana, na wako wengi wanipingao.”
Mifano ya watu waliofunguliwa milango ya kufaa
Mungu alimfungulia mtume Paulo
mlango mkubwa wa kufaa sana kwaajili ya injili, kama tunavyoweza kuona katika
maandiko kwamba Upinzani dhidi ya injili ulimkabili Paulo mtume kila mahali
kiasi cha kuhatarisha maisha yake japo watu wengi walikuja kwa Bwana, Ni muhimu
kufahamu kuwa sio katika huduma tu watu hufungiwa mlango, lakini hata katika
maisha yetu ya kawaida kuna milango inaweza kufungwa yako mambo ambayo
ungetamani yakae sawa lakini yamefungwa, ni huduma yako bado haijapata nafasi
ya kutulia na kuwafikia wale ambao ulikuwa unawafikiri, ni tumbo lako na uzao wako umefungwa hushiki
mimba, au huwezi kumpa mwanamke mimba, biashara haijapata mpenyo unaokusudiwa, Hata
hivyo haupaswi kukata tamaa, Neno la Mungu linatukumbusha kuwa katika kila
jaribu Mungu huweka mlango wa kutokea
1Wakorintho
10:13 “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo
kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita
mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze
kustahimili.”
·
Yusufu alipitia katika mitihani ya namna
mbalimbali katika maisha yake hata kufungwa gerezani kwa kusingiziwa tu lakini
hatimaye Mungu alimfungulia mlango na akawa mtu mkubwa sana katika incho ya
Misri
-
Mwanzo
37:12-36 “Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za
baba yao huko Shekemu. Israeli akamwambia Yusufu, Je! Ndugu zako hawachungi
kondoo katika Shekemu? Njoo, nikutume kwao. Akamwambia, Mimi hapa. Akamwambia, Enenda, basi, ukaone kama ndugu
zako hawajambo, na kundi nalo li salama, ukaniletee habari. Basi akampeleka
kutoka bonde la Hebroni, akafika Shekemu. Mtu mmoja akamkuta, naye alikuwa
anazunguka-zunguka katika nyika; yule mtu akamwuliza, akisema, Unatafuta nini? Akasema,
Nawatafuta ndugu zangu; tafadhali uniambie mahali wanakochunga. Yule mtu
akasema, Wametoka hapa, maana niliwasikia wakisema, Twendeni Dothani. Basi
Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani. Wakamwona toka mbali, na
kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa
wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa
katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona
zitakuwaje ndoto zake. Reubeni akasikia akamwokoa katika mikono yao, akasema,
Tusimwue. Reubeni akawaambia, Msimwage damu; mtupeni katika birika hii iliyopo
nyikani, wala msimguse; ili apate kumwokoa katika mikono yao, akamrudishe kwa
baba yake. Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake,
kanzu ile ndefu aliyoivaa, wakamtwaa wakamtupa katika birika; na hiyo birika
ilikuwa tupu, hamna maji. Nao wakakaa kitako kula chakula; wakainua macho yao,
wakaona, msafara wa Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao,
wakichukua ubani na zeri na manemane, wakisafiri kuvichukua mpaka Misri. Yuda
akawaambia ndugu zake, Kwafaa nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake? Haya,
na tumwuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yetu isimdhuru, maana yeye ni ndugu
yetu, na damu yetu. Ndugu zake wakakubali. Wakapita wafanya biashara Wamidiani;
basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika, wakamwuza Yusufu kwa
Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri. Akarudi
Reubeni birikani, kumbe! Yusufu hayumo katika birika, akararua nguo zake. Akarudi
kwa ndugu zake, akasema, Mtoto hayuko, nami niende wapi? Wakaitwaa kanzu ya Yusufu, wakachinja
mwana-mbuzi, na kuichovya kanzu katika damu. Wakaenda nayo ile kanzu ndefu,
wakamletea baba yao, wakasema, Tumeona hii; basi, utambue kama kanzu hii ni ya
mwanao, ama siyo. Akaitambua, akasema, Ndiyo kanzu ya mwanangu, mnyama mkali
amemla; bila shaka Yusufu ameraruliwa. Yakobo akararua mavazi yake, akajivika
gunia viunoni, na kumlilia mwanawe siku nyingi. Wanawe wote, na binti zake
wote, wakaondoka wamtulize, lakini akakataa kutulizwa, akasema, La! Nitamshukia
mwanangu, nikisikitika, hata kuzimu. Baba yake akamlilia. Nao Wamidiani
wakamwuza huko Misri, kwa Potifa, akida wa Farao, mkuu wa askari.”
·
Ayubu alipitia mitihani migumu sana kufiwa na
watoto wote, kupoteza mali zake zote, kupata hasara ya mifugo yake yote na
wafanyakazi wake wote waliuawa na kutekwa na kubakiwa na watoa taarifa tu, kama
haitoshi yeye aliugua na kufilisika kwa kiwango kikubwa, hata hivyo Mungu
alimfungulia mlango wa kufaa baadaye
-
Yakobo
5:10-11 “Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina
la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu. Angalieni,
twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona
mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.”
Mpenzi
haupaswi kukata tamaa na kudhani ya kuwa wewe una nuksi au balaa, kila
changamoto unayoipitia kumbuka kuwa Mungu atafanya mlango wa kutokea, Mlango
ambao Mungu atakufungulia utakuwa ni mkubwa na wa kufaa Zaidi, Mungu
aliyewafungulia mlango watakatifu waliotutangulia na wale ambao wako leo na
tnasikia shuhuda zao hatakosa kukufungulia mlango mkubwa wa kukufaa Zaidi wewe
nawe katika maisha yako
Jinsi ya kufunguliwa mlango wa kufaa
Ni muhimu kufahamu kuwa hata sasa
Mungu anakuwazia mema, Paulo mtume hakukata tamaa kwa sababu ya magumu
aliyokuwa akiyapitia, aliendelea kuhubiri injili, kila alikokuwa akikataliwa
alikimbia katika mji mwingine na hatimaye kule Efeso Mungu alimfungulia mlango
mkubwa wa kufaa Zaidi, ziko sababu nyingi kwako kwanini Mungu atakufungulia
mlango
1. Mungu
tunayemwambudu na kumtumikia nidye mwenye funguo yeye anauwezo wa kufungua na
hakuna wa kufunga na ana uwezo wa kufunga na hakuna afunguaye kwa msingi huo ni
Mungu mwenyewe anayeweza kuingilia katika hali unayoipitia na kukufungulia
mlango na ni yeye anayeweza kukupa
mlango uliofunguliwa mbele yako ona
Ufunuo 3:7-8 “Na
kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye
mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala
hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye. Nayajua matendo yako.
Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye
kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala
hukulikana jina langu.”
2. Mungu
amelipa Kanisa mamlaka ya kushangaza sana wewe kama mtu uliyemwamini Bwana Yesu
wewe ni kanisa na Mungu amekupa uwezo na mamlaka ya kufungua lolote kiasi hata
mbinguni likafunguliwa na una uwezo wa kufunga lolote nahata mbinguni
likafungwa, kwa msingi huo katika kila jambo ambalo unahisi limefungwa unaweza
kumuomba Mungu na akakufungulia mlango ona
Mathayo 18:18 “Amin,
nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo
yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.”
3. Washirikishe
wale unaowaamini katika maombi yako, kuna nguvu kubwa sana kama watu wawili au zaidi
wakipatana na kuomba Mungu huwafanyia, kile walichokiomba, Mungu huwa kati kati
ya watu Zaidi ya wawili au watatu wakiungana katika maombi, hiki ndicho
alichosema Kristo ona
Mathayo 18:19-20 “Tena
nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote
watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo
wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.”
Na ndio maana Paulo
mtume alipoona changamoto zilizokuwa zinamkabili aliwaomba kanisa wamuombee
neema ili kwamba wamuombee ili afunguliwe mlango
Wakolosai 4:2-3 “Dumuni
sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani; mkituombea na sisi
pia, kwamba Mungu atufungulie mlango kwa lile neno lake, tuinene siri ya
Kristo, ambayo kwa ajili yake nimefungwa,”
Daniel
alipopata changamoto kazini wakati wenye hekima walipotakiwa kutafasiri na
kumkumbusha mfalme Nebukadreza kuhusu Ndoto aliyoiota akaisahau na kuwataka
wamkumbushe kwanza kisha wamuelezee maana vinginevyo angewaua Daniel aliamua
kumuomba Mungu na kuwashirikisha na wenzake na wakamuomba Mungu, shirikisha
watu muhimu unaowaamini ombeni pamoja kuhusu changamoto inayokukabili na Bwana
atakufungulia mlango mkubwa wa kufaa Zaidi.
Daniel 2:17-19 “Ndipo
Danieli akaenda nyumbani kwake, akawapasha habari kina Hanania, na Mishaeli, na
Azaria wenzake; ili waombe rehema kwa Mungu wa mbinguni kwa habari ya siri
hiyo, ili kwamba Danieli na wenzake wasiangamizwe pamoja na wenye hekima wa
Babeli. Ndipo Danieli alipofunuliwa siri hiyo katika njozi ya usiku. Basi
Danieli akamhimidi Mungu wa mbinguni.”
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni