Yohana 4: 45-48 “Basi alipotoka Galilaya,
Wagalilaya walimpokea; kwa kuwa wameyaona mambo yote aliyoyatenda huko
Yerusalemu wakati wa sikukuu; maana hao nao waliiendea sikukuu. Basi alifika tena Kana ya Galilaya, hapo
alipoyafanya yale maji kuwa divai. Na palikuwa na diwani mmoja ambaye mwanawe
hawezi huko Kapernaumu. Huyo aliposikia ya kwamba Yesu amekuja kutoka Uyahudi
mpaka Galilaya, alimwendea, akamsihi ashuke na kumponya mwanawe; kwa maana
alikuwa kufani. Basi Yesu akamwambia, Msipoona ishara na maajabu hamtaamini
kabisa?”
Utangulizi:
Yesu alikuwa ni mtenda miujiza
mkubwa Zaidi kupata kutokea Duniani, Mungu alimpa neema kubwa sana ya kufanya
kazi ya uponyaji na kufundisha kwa uweza wa Roho Mtakatifu kila alikokwenda
Mathayo 4:23-25 “Naye alikuwa akizunguka
katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari
Njema ya ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu. Na
habari zake zikaenea katika Shamu yote; wakamletea wote waliokuwa hawawezi,
walioshikwa na maradhi mbalimbali na mateso, wenye pepo, na wenye kifafa, na
wenye kupooza; akawaponya. Na makutano mengi wakamfuata, kutoka Galilaya, na
Dekapoli, na Yerusalemu, na Uyahudi, na ng'ambo ya Yordani”
Sababu kubwa ya Yesu kusukumwa na
Roho Mtakatifu kufanyahuduma hizi zote ni kwa sababu aliwahurumia watu na
kusikitishwa na taabu zao na uonevu wa Shetani aliokuwa ameufanywa kwa wanadamu
hivyo alifanya kazi hiyo ya kuwaponya na
kuwafundisha neno la Mungu
Mathayo 9:35-36 “Naye Yesu alikuwa
akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na
kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila
aina. Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na
kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji.”
Kwa hiyo kazi zote alizozifanya
Kristo alizifanya kwa sababu ya moyo wake wa upendo kwa wanadamu, alitumia
karama zake na vipawa vyake kwa faida ya kuwajenga watu, kuwasaidia, kuwakwamua
na kuwatoa katika shida na changamoto kubwa zilizokuwa zikiwakabili, Hata hivyo
kwa upande wa watu waliokuwako nyakati zile wao walianza kumfuata Yesu kila
alikokwenda wakifurahi na kushangilia kwaajili ya kuona miujiza na kufurahia
ishara alizokuwa akizifanya, Kimsingi Isahara na maajabu sio kitu kibaya na
ndio maana Yesu alifanya, lakini kimsingi wanadamu wanatakiwa kujifunza
kumuamini Mungu na kujua ya kuwa Mungu anawajali na kuhusika na maisha yao hata
bila ya Ishara na maajabu nahiki ndicho kiwango ambacho Yesu alitamani watu
wakifikie:- tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Kusudi kuu la ishara na miujiza
·
Msipoona ishara na maajabu hamtaaamini kabisa
·
Jambo kubwa la msingi
Kusudi kuu la Ishara na miujiza.
Ishara na miujizaa ni mojawapo ya
matukio makubwa ya kushangazwa yanayoyanywa na Mungu kupitia watumishi wake
ambao amewapa karama mbalimbali kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kuwawezesha watu
hao kufanya mambo makubwa nay a kushangaza kwa idhini au kwa jina la Mungu, Tangu
zamani katika Israel na hata baadaye nyakati za kanisa la kwanza na siku zoa
leo katika jumuia nyingi za kikristo za uamsho kama Charismatic Movements na
Pentecostal movements Ishara na miujiza imekuwa ni moja ya sehemu muhimu sana
ya kiibada kwa kusudi la kuwaaminisha watu juu ya uwepo na utendani wa Mungu na
kudhihirisha kuwa mungu hayuko mbali na watu wake na kuwa yeye ni msaada ulio
karibu
Zaburi
46:1 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada
utakaoonekana tele wakati wa mateso.”
Kwa hiyo kumekuweko na msisistizo
mkubwa sana wa injili na huduma nyingi za ukombozi na uponyaji, ambavyo
kimsingi sio vibaya kwa sababu watu wanasaidiwa na kuponywa magiojwa yao na
kusaidiwa kimwili, kiroho na hata kisaikolojia unapoona makundi makubwa ya watu
wakitafuta uponyaji unaweza kuhisi huruma na hata kutamani kama ungekuwa na
uwezo wa kuwasaidia watu wote ungeweza kuwasaidia lakini hata hivyo ni muhimu
kufahamu kuwa kuna makusudi ya kuweko kwa ishara na miujiza , na ni muhimu
kujiuliza kwanini Mungu anafanya hizi ishara na miujiza ?
1. Kufunua ukuu wa Mungu - Ishara zote zilizofanyika katika agano la
kale na zinazofanyika hata sasa katika agano jipya makusudi yake makuu ni
kufunua ukuu wa Mungu, ni ili watu wenye kiburi wanaojifikiri kuwa wao ni ka a
miungu duniani wapate kutiishwa wajue ya kuwa Yuko Mungu anayetawala Dunia na kila mmoja aweze kumjua yeye na jina lake
na uweza wake na utendaji wake hatimaye waweze kumuabudu na kumuheshimu yeye
ona
Warumi 9:17 “Kwa
maana maandiko yasema juu ya Farao, ya kwamba, Nilikusimamisha kwa kusudi hili,
ili nionyeshe nguvu zangu kwako, jina langu likatangazwe katika nchi yote.”
Maana yake ni
nini kwamba miujiza yote ambayo Mungu aliitenda kuanzia wakati anawatoa wana wa
Israel Huko Misri na mingine mingi muda usingeweza kutosha kutaja yote lakini
kusudi mojawapo kubwa ni kuufunua ukuu wa Mungu ili dunia ipate kumuheshimu,
kumtukuza, kumshukuru, na kutambua kuwa yeye ndiye kila kitu.
2. Kuufunua utukufu wake – ishara zote
alizozifanya Mungu katika agano la kale na jipya hata kuanzia kazi zake za
uumbaji na maajabu yote na ishara ni kwaajili ya kuufunua utuklufu wake ni ili
watu wote wajue na kumsifu Mungu kuwa ndiye Mungu,
Zaburi 19:1 “Mbingu
zauhubiri utukufu wa Mungu, Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.”
Unaona Mungu
wetu anataka tumtukuze yeye, kumtukuza yeye ni sehemu ya ibada, ni sehemu ya
kutambua ukuu wake, ni sehemu ya heshima , ni sehemu ya shukurani ni sehemu ya
kuonyesha kuwa yuko mwenye serikali mbunguni na duniani na kuwa tunapaswa kumpa
yeye utukufu, hii ni mojawapo ya sababu kwanini Mungu hufanya ishara na miujiza
ona pia
Yohana 2:11 “Mwanzo
huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake,
nao wanafunzi wake wakamwamini.”
3. Kwaajili ya huruma na upendo wake
– Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai
na Baba wa Mbinguni ni wamoja kwa uweza wa Roho Mtakatifu Yesu alitenda kazi ya
uponyaji kwaajili ya kufunua huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu kama
tulivyoona katika utangulzizi kuwa alifanya yote aliyoyafanya kwaajili ya
huruma zake
Mathayo 9:35-36 “Naye
Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika
masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote
na udhaifu wa kila aina. Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu
walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji.”
Kazi hizi
alizozifanya Kristo ni kwaajili ya maelekezo yote kutokwa kwa baba yake hivyo
alifanya kile ambacho baba yake anakifanya
Yohana 5:19-20 “Mwana
hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana
yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile. Kwa kuwa Baba ampenda
Mwana, naye humwonyesha yote ayatendayo mwenyewe; hata na kazi kubwa zaidi
kuliko hizo atamwonyesha, ili ninyi mpate kustaajabu.”
Kwa hiyo kile
alichokitenda Bwana Yesu kwa neno au kwa tendo kinadhihirisha na kufunua Moyo
wa Mungu baba kwetu, Kristo Yesu ni chapa ya mng’ao wa utukufu wa Mungu kumuona
Yesu ni Kumuona baba, kwa sababu hiyo ni Dhahiri kuwa Yesu/Mungu alifanya
ishara na miujiza kwa kusudi la kufunua huruma na upenzo wake kwetu.
4. Kwaajili ya kulithibitisha neno – Neno la Mungu linapotoka kwake au kwa kinywa
cha nabii wake huwa haliendi bure naposema nabii hapa namiaanisha mtu anayesema
kwa niaba ya Mungu yaani walimu, wachungaji, wainjilisti manabii na mitume,
watmishi wote halali ambao wanazungumza kwa niaba ya Mungu wanapolisema neno
lake halitekwenda bure litazaa matunda
Isaya 55:10-11 “Maana
kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali
huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na
mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa
changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa
katika mambo yale niliyolituma.”
Kwa hiyo Mungu
hulithibitisha neno lake kwa ishara na
miujiza, watu wanapotoka kwenda kulitangaza neno lake Mungu hufanya ishara na
miujiza kwa kusudi la kulithibitisha neno lake ili watu wapate kusadiki ona
Marko 16L17-20 “Na
ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa
lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru
kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya. Basi Bwana
Yesu, baada ya kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa
Mungu. Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao,
na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.]”
Matendo 14:3 “ Basi wakakaa huko wakati
mwingi, wakinena kwa ushujaa katika Bwana, aliyelishuhudia neno la neema yake,
akiwajalia ishara na maajabu yatendeke kwa mikono yao.”
Waebrania 2:3-4 “Kwa
maana, ikiwa lile neno lililonenwa na malaika lilikuwa imara, na kila kosa na
uasi ulipata ujira wa haki, sisi je! Tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu
namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale
waliosikia; Mungu naye akishuhudu pamoja nao kwa ishara na ajabu na nguvu za
namna nyingi, na kwa magawanyo ya Roho Mtakatifu, kama alivyopenda mwenyewe.”
Kwa hiyo tunaona
wazi kuwa Mungu hufanya ishara na miujiza kwa kusudi la kulithibitisha neno
lake lengo kuu likiwa watu wapate kusadiki kuamini, waokolewe wawekwe huru,
waponye, wajengeke wakue katika Imani wakiamni kuwa yuko Mungu
5. Ili watu wapate kumuamini – Kusudi
kubwa na la juu Zaidi la Mungu kufanya ishara na miujiza ni ili watu wapate
kumuamini wakubali kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, wamwamini yeye ili wapate
wokovu wamjue Mungu na Yesu Kristo aliyemtuma
Yohana
20: 30-31 “Basi kuna ishara nyingine nyingi
alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki.
Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa
Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake.”
Kusudi kubwa na
la juu kabisa la ishara na miujiza ni ili watu wamamwini Mungu na wapate
kuokolewa wamwamini Yesu Kuwa ni Bwana na mwokozi ili waokolewe, na wayahudi
wapate kujua kuwa Yesu ndiye Masihi mwana wa Mungu aliye hai kwa hiyo kila
muujiza alioufanya Yesu pamoja na maneno yake na matendo yake hitimisho lake ni
ili watu wapate kumwamini kuwa yeye ni mwana wa mungu na ndiye njia na kweli na
uzima
Yohana 2:11 “Mwanzo
huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu
wake, nao wanafunzi wake wakamwamini.”
Yohana 2:23 “Hata alipokuwapo Yerusalemu kwenye sikukuu
wakati wa Pasaka, watu wengi waliamini jina lake, walipoziona ishara zake
alizozifanya.”
Msipoona ishara na maajabu hamtaaamini kabisa.
Baada ya kuwa tumejifunza na
kupata ufahamu kuhusu kusudi kuu la Isara na miujiza sasa swali kubwa la Msingi
ni kwanini Bwana Yesu alitoa maonyo kwa watu waliokuwa tu wanataka kusaidiwa na
kupata miujiza yao?
Yohana 4: 45-48 “Basi alipotoka Galilaya,
Wagalilaya walimpokea; kwa kuwa wameyaona mambo yote aliyoyatenda huko
Yerusalemu wakati wa sikukuu; maana hao nao waliiendea sikukuu. Basi alifika tena Kana ya Galilaya, hapo
alipoyafanya yale maji kuwa divai. Na palikuwa na diwani mmoja ambaye mwanawe
hawezi huko Kapernaumu. Huyo aliposikia ya kwamba Yesu amekuja kutoka Uyahudi
mpaka Galilaya, alimwendea, akamsihi ashuke na kumponya mwanawe; kwa maana
alikuwa kufani. Basi Yesu akamwambia, Msipoona ishara na maajabu hamtaamini
kabisa?”
Kimsingi sio kuwa Yesu alikuwa
anazungumza na diwani pekee hapana Yesu alikuwa anazungumza na diwani na watu
wote waliokuwa wamemkusanyikia mioyoni mwao wakiwa wanataka kuponywa na kuona
ishara na miujiza aliyokuwa akiifanya hata kabla hawajamuamini, yaani kismingi
watu walikuwa wana hamu na shauku ya kuona miujiza na ishara kuliko hata mwenye
kufanya hizo sihara na miujiza, Yesu aliwakemea maalumu kwaajili yao,
Hakumaanisha kuwa ishara na maajabu ni jambo baya kwao hapana lakini kuna kitu
cha ziada Zaidi ya muujiza nah ii sio mara ya kwanza Yesu kutoa maonyo
haya ona
Yohana 6:25-29 “Hata walipomwona ng'ambo ya
bahari, walimwambia, Rabi, wewe umekuja lini hapa? Yesu akawajibu, akasema,
Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali
kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. Msikitendee kazi chakula chenye
kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu
atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu. Basi
wakamwambia, Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu? Yesu akajibu,
akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu, mmwamini yeye aliyetumwa na yeye.”
Nadhani sasa tunaweza kuona
katika moja ya kemeo la Yesu kwamba watu walimfuata kwa sababu tu waliziona
ishara na jambo hilo liko wazi Yohana
6:1-2 “Baada ya hayo Yesu alikwenda zake ng'ambo ya
Bahari ya Galilaya, nayo ndiyo ya Tiberia. Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa
sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa.”
Kwa hiyo hoja ya Yesu Kristo ina
umuhimu na msingi sana hususani katiika nyakati za leo, kuna watu leo ambao
wameacha kumtafuta Mungu na mafundisho sahihi na badala yake wanatafuta ishara
na miujiza , wanashindwa hata kuamini injili nyepesi tu ya wokovu na kumjua Mungu wa kweli badala yake
wanatafuta ishara na miujiza hii inadhoofisha sana nafasi ya kanisa kuwahudumia
na kupata nafasi ya kuwajengea Imani sahihi, tumekuwa na wimbi kubwa la watu wanaotafuta
maombezi kila wakati, wakristo wamedumaa na hawafikii ngazi ya kukomaa na kukua
kiroho ili wao nao wawe na karama za Rohoni na kuwahudumia wengine badala yake
wanahangaika huko na huko kutafuta maombizi kila likija wimbi moja na lingine,
Yesu mwenyewe alikuwa anaonya hapa kwamba Imani hii ya kutaka kuhudumiwa tu kwa
ishara na miujiza japo hiana ubaya lakini haitoshi kuwafanya watu wawe na imani
ya kweli, Ishara na miujiza ni mwanzo tu wa swala zima la Imani ili tujenge
Imani yetu kwa mtenda miujiza ambaye ni Bwana Yesu, onyo la Yesu ni kwa watu
wote Msipoona na sio usipoona kwa hiyo kila mmoja wetu anakumbusha kuwa ishara
huwa ainatuongoza katika jambo moja kubwa na la muhimu sana ambalo ni Yesu
Jambo kubwa la msingi.
Ni muhimu kufahamu kuwa hakuna
watu ambao wamewahi kushuhudia miujiza mikubwa na utendaji mkubwa wa Mungu kama
wana wa Israel hivyo neno la Mungu linalalamika kuwa hawakuamini na hatimaye
wengi waliangamizwa jangwani
1Wakorintho 10:1-5 “Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa
baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; wote
wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari; wote wakala chakula
kile kile cha roho; wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana
waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo.Lakini
wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani.”
Wana wa Israel Jangwani waliona
muujiza mmoja baada ya muujiza mwingine Makusudi makubwa ya Mungu ni ili waoa
wamuamini, wamtukuze, wamuheshimu na kumuabudu, watambue ya kuwa yeye ndiye
anayemiliki, wamuamini yeye na neno lake na hatimaye waweze kuwa na badiliko la
ndani linalotokana na kuamini, lakini badala yake hawakuamini, walinungunika
roho zao hazikufanyika imara hawakumwamini na hivyo Mungu alichukizwa nao
Waebrania 3:14-19 “Kwa maana tumekuwa
washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu
mpaka mwisho; hapo inenwapo, Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu
mioyo yenu, Kama wakati wa kukasirisha. Maana ni akina nani waliokasirisha,
waliposikia? Si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Musa? Tena ni akina
nani aliochukizwa nao miaka arobaini? Si wale waliokosa, ambao mizoga yao
ilianguka katika jangwa? Tena ni akina nani aliowaapia ya kwamba hawataingia
katika raha yake, ila wale walioasi? Basi twaona ya kuwa hawakuweza kuingia kwa
sababu ya kutokuamini kwao.”
Kristo Yesu alikuwa anataka
kuwaepusha wana wa Israel na jambo kama hili, fundisho lake ni kwa watu wote
waaminio na hata wale ambao bado, muhimu tu kama kwetu sote Ishara na miujiza
ikatuongoza katika kumtii Mungu na kumuheshimu, Yesu anataka tmuamini yeye hata
tuspoona ishara na miujiza, Imani sahihi wakati wote hailazimishi Mungu atende
kila tunataka inalazimisha mioyo yetu iamini katika Mungu katika namna ya
iliyopitiliza na hiki ndicho Mungu anachokitaka
-
Ayubu 19:25-26
“Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai,
Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa
hivi, Lakini, pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu;”
-
Daniel
3:14-18 “Nebukadreza akajibu, akawaambia, Enyi
Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa makusudi hata hammtumikii mungu
wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati
mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na
zomari, na namna zote za ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha,
ni vema; bali msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuru iwakayo moto;
naye ni nani Mungu yule atakayewaokoa ninyi na mikono yangu? Ndipo Shadraka, na
Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hamna haja
kukujibu katika neno hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza
kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme.
Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu
yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”
Hitimisho:
Lazima ufikie wakati Imani yetu
iwe kwamba Mungu ni Mungu tu na atabaki kuwa Mungu na kwamba lazima aonyeshe
miujiza yake, na tunapaswa kumuamini iwe kuna muuiiza au hakuna muujiza, iwe
tuna kazi au hatuna kazi, iwe tumeponywa au hatujaponywa, iwe amaejibu maombi
aua amekataa, iwe amatuponya au hajatuponya iwe tumeolewa au hatujaolewa, iwe
tumechumbiwa au hatujachumbiwa, iwe tumepata au tumekosa, iwe tumefaulu au
tumefeli, iwe kuna raha au kuna shida, tuwe tunapata mema au mabaya tunamwamini
Mungu hata pasipo ishara na maajabu tunamwamini Mungu kuwa yeye ndiye anayetawala
kila jambo katika maisha yetu na tunaendelea kumuheshimu na kumpa utukufu
Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni