Jumatatu, 23 Oktoba 2023

Sitatwaa chochote kilicho chako!


Mwanzo 14:14-23 “Abramu aliposikia ya kwamba nduguye ametekwa mateka, akawapa silaha vijana wake, waliozaliwa katika nyumba yake, watu mia tatu na kumi na wanane, akawafuata mpaka Dani. Akajipanga apigane nao usiku, yeye na watumwa wake, akawapiga, akawafukuza mpaka Hoba, ulioko upande wa kushoto wa Dameski. Naye akarudisha mali zote, akamrudisha na Lutu nduguye na mali zake, na wanawake pia, na watu. Abramu aliporudi kutoka kumpiga Kedorlaoma na wale wafalme waliokuwa pamoja naye, mfalme wa Sodoma akatoka amlaki katika bonde la Shawe, nalo ni Bonde la Mfalme. Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana. Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi. Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote. Mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu, Nipe mimi hao watu, na hizo mali uchukue wewe. Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma, Nimeinua mkono wangu kwa BWANA, Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi, ya kuwa sitatwaa uzi wala gidamu ya kiatu wala cho chote kilicho chako, usije ukasema, Nimemtajirisha Abramu;”



Utangulizi:

Wale ambao wanadhani kuwa Abrahamu alikuwa mtu wa kawaida tu aliyetembea na Mungu aliye hai na ni baba wa Isaka na Ishmael na ni baba wa Imani ya kiyahudi, Kikristo na waislamu, na moja ya baba wa taifa a Israel nataka watambue leo kuwa sivyo wanavyofikiria kuhusu Abraham, Maandiko yanaonyesha wazi kuwa Abrahamu alikuwa ni mtu mkuu sana na hakuwa wa kawaida, Tangu Mungu alipokuwa anamuita Abrahamu alikuwa ni mtu ambaye amekulia mjini na ni moja ya watu waliotokea kwenye maendeleo makubwa sana! Tunaelezwa wazi kuwa Abraham alitokea katika nchi ya Uru wa ukaldayo huko Mesopotamia, Historia inaonyesha wazi kuwa ustaarabu wa kwanza kabisa wa kimaendeleo ulitokea huko Mesopotamia mahali ambapo mito mikubwa duniani mto Frati na mto Tigris inamwaga maji yake katika ghuba ya uajemi, na mji wa Uru ulikuwa ndio mji wenye bandari na mji uliokuwa na maendeleo makubwa sana Katika ghuba ya uajemi, na ndio kuotokea huku Mungu alimuita na kufanya badiliko kubwa sana la maisha yake, Abraham alitokea katika familia na mji wenye maendeleo makubwa na wala hakuwa mshamba! Alikuwa tajiri mno na anayetoka katika mtazamo wa kimaendeleo wa hali ya juu sana.

Mwanzo 13:2-6 “Naye Abramu alikuwa ni tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu. Akaendelea kusafiri kutoka kusini mpaka Betheli, mahali pale palipokuwapo hema yake kwanza kati ya Betheli na Ai; napo ndipo palipokuwa na madhabahu aliyofanya hapo kwanza; naye Abramu akaliitia jina la BWANA hapo. Na Lutu aliyesafiri pamoja na Abramu, yeye naye alikuwa na makundi ya ng'ombe na kondoo, na hema. Na ile nchi haikuwatosha, ili wakae pamoja; maana mali zao zilikuwa nyingi, hata wasiweze kukaa pamoja.”

Unaona licha ya kuwa amekulia kwenye mji mkubwa na uliokuwa na maendeleo makubwa sana Abraham aliitii sauti ya Mungu ya kumuita kwenda katika nchi atakayomuonyesha yaani nchi ya kanaani, Maandiko pia yanatuonyesha kuwa Abraham alikuwa tajiri sana Kiswahili kinasema tajiri sana lakini biblia ya kiingereza ya Berean Standard Bible inatumia neno HAD BECOME EXTREMELY WEALTHY, Extremely rich yaani alikuwa tajiri kwelikweli, alitajirika kupitiliza! Maandiko yanasema mpaka inchi ile haikuwatosha Yeye na Lutu ili wakae pamoja maana mali zao zilikuwa nyingi!

Kwanini Bibia imetumia neno Extremely rich  au tajiri sana, katika Biblia ya kiebrania neno hilo tajiri sana linasomeka kama KABAD KABED  linatamkwa kaw-bad kaw bade  ambalo tafasiri yake kupita kawaida, utajiri mzito, utajiri uliopitiliza, utajili uliotukuka, utajiri wenye kuleta heshima utajiri wenye kuonyesha uungwana, kuinuliwa mno, utajiri mzito sana  strong concordance imetumia pia neno grievous  na severe kwa lugha ya mtaani  ni UTAJIRI WA KUFA MTU  na kama haitoshi tunaambiwa wakati Lutu anatekwa na jumuiya ya wafalme walioungana  Abraham alikwenda na jeshi lake la vijana wapatao 318  na kusambaratisha wakorofi na kumuokoa Lutu ile opereshini ya kijeshi mimi ninaiita Operation Lot yaani ilikuwa vita ya kumkomboa Lutu,  ona hapa kwanza 

Mwanzo 14:14 “Abramu aliposikia ya kwamba nduguye ametekwa mateka, akawapa silaha vijana wake, waliozaliwa katika nyumba yake, watu mia tatu na kumi na wanane, akawafuata mpaka Dani.”        

Je unapata picha ya aina gani hapo? Abraham alikuwa Mfalme, He was a Prince, Abraham alikuwa ni serikali kamili, alikuwa na meneja, alikuwa na waajiriwa, alikuwa na Jeshi, alikuwa ni mtu mkubwa sana, alikuwa na wapelelezi, nani walimpa taarifa kuwa Lutu ametekwa? Alikuwa na waandishi wa habari, alikuwa na silaha, alikuwa na benki yenye akiba ya fedha na dhahabu,alikuwa na wapelelezi, kwa hiyo nini maana yake pia Abraham alikuwa na moyo wa ukarimu alikuwa tajiri moyoni na alikuwa mtu mkubwa anayetembea, serikali inayotembea, ufalme unaotembea, alistawi sana kwa hiyo huwezi kumtishia Abraham kwa habari ya mali, na utajiri wa ulimwengu huu kwa kuwa alikuwa na kila kitu! Na mali hazikumuendesha hata kidogo, aliheshimu watu wote wakubwa kwa wadogo na kusimamia haki, ufahamu wake ulikuwa mkubwa na wenye mtazamo mkubwa wa kimaendeleo kutokana na mji alikotokea, Mesopotamia nchi ya mito miwili, nchi yenye rutuba na ustaarabu mkubwa wa mwanzo. Abrahamu hakuwa limbukeni, wala hakuinua mabega yake na kujiona mungumtu pale Mungu alipombariki kwa mali nyingi!


·         Kiini cha mafanikio na utajiri wa Abraham.

·         Kiini cha mafanikio na utajiri wa Wakristo.

·         Sitatwaa chochote kilicho chako! 


Kiini cha mafanikio na utajiri wa Abraham.

Mungu alikuwa amekusudia kumbariki Abraham tangu mwanzo na kwa kawaida Mungu akiisha kukubariki mafanikio mengine yote ya kimwili na kiroho yanakuja kutoka kwake, Lakini lazima iwepo Baraka kwanza, Baraka hizo ndio zinazoleta ufunguo wa mafanikio na utajiri hata ule unaoonekana kwa macho, Mithali 10:22 “Baraka ya Bwana hutajirisha, Wala hachanganyi huzuni nayo.” Abraham alikuwa mtu aliyebarikiwa mtu aliyebarikiwa kwanza huwa na amani, huwa na afya nzuri, huwa na furaha, huwa na upendo, huwa na ukarimu huwa na moyo wa kitajiri, hujaa fadhili, hujawa na utulivu na huzingirwa na ulinzi wa Mungu, Mungu hufanyika ngao kwake na Mungu huwa ndio thawabu yake kubwa sana na mtu huyo huwa mbali na hofu, kabla ya utajiri huo wa nje ndani ya mtu kunakuwa na baraka za Mungu hivi ndivyo Abraham alivyobarikiwa sana

Mwanzo 12:1-3 “BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”

Mungu ndiye aliyekuwa sababu ya Baraka kubwa sana alizokuwa nazo Abraham, kwa hiyo kiini cha mafanikio na utajiri wa Abraham ni Baraka kutoka kwa Bwana, ulinzi na usalama na kila alichokuwa nacho kilikuwa ni kwa sababu Mungu alikuwa amembariki, zaidi ya yote Mungu alimtuma askofu mkuu wa Yerusalem (Kuhani Mkuu) ambaye alikuwa kuhani, mfalme na nabii ambaye alikuja kumtamkia Abraham Baraka kubwa sana hata alipokuwa ametoka kwenye operesheni komboa Lutu ona askofu huyu aliitwa Melekizedeki ona

Mwanzo 14:18-20 “Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana. Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi. Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote.”

Unaona Melkizedeki kuhani wa Mungu aliyejuu sana, alikuja kumlaki Abraham alipokuwa ameshinda vita, akatoa huduma ya kiroho kisha kwa mamlaka aliyokuwa nayo kama kuhani alimbariki Abraham, lakini akiwa na ujuzi kuwa hata ushindi wa Abraham yaani adui zake kutiwa mikononi mwake kumetokana na Mungu muumba wa mbingu na nchi, kwa hiyo Melkzedeki alimbariki Abraham huku akiwa na uelewa kuwa kila kitu hata ushindi ule mkubwa kwa Abraham ulitokana na Mungu, yaani ilieleweka wazi kuwa ukuu wa mtu huyu, nguvu na utajiri umetokana na Mungu sijui wewe kama watu wanajua kuwa Mungu amekubariki au moyo wako unajua kuwa umeiba? Heshima uliyo nayo umepewa na Mungu au umeipata kwa majungu, fitina na ujanja ujanaja? Lakini chanzo cha Baraka na mafanikio yote ya Ibrahimu ilikuwa ni Bwana Mungu wake na sio vinginevyo!

Mwanzo 15:1 “Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana.”

Mungu akifanyika thawabu yetu kubwa sana na kuwa ngao katika maisha yetu tutakuwa na mafanikio yenye ustawi katika kila eneo la maisha yetu kimwili na kiroho, Amani itatawala na mafanikio yatatatwala na tutakuwa ni wafame katika ardhi ya dunia tukiwa na afya njema, Amani na furaha na utulivu,  huku tukiwa wasimamizi wa haki na watetezi wa wanyonge na majibu ya wenye uhitaji, Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuwa na mafanikio makubwa sana na utajiri mkubwa sana ambao Bwana ndio chanzo na kiini cha utajiri huo!, Mungu alimbariki hivyo Abraham sio kwaajili yake tu na kwaajili ya mafanikio ya ulimwengu mzima na kila anayemkubali Abraham na Mungu anayejitambulisha Duniani kupitia Abraham na mtoto wake wa ahadi yaani Bwana wetu Yesu Kristo!.

Kiini cha mafanikio na utajiri wa Wakristo.

Kama iivyokuwa kwa baba Yetu Ibrahimu baba wa Imani mafanikio na utajiri wa kila Mkristo kiini chake Ni Mungu wa Ibrahim, Isaka na Yakobo, na Baraka ile kubwa iliyokusudiwa kwa ulimwengu yaani Yesu Kristo, kila anayemuamini Yesu anapaswa kufahamu kuwa yeye ndio chanzo cha Baraka zetu, yeye ni kiini cha Mafanikio na utajiri Duniani kwa nini kwa sababu kwanza sisi ni warithi wa Baraka zote za Abraham!

Wagalatia 3:26-29 “Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.”

Unaona Mungu amekusudia kumbariki kila mtu anayemuamini Yesu bila kujali historia yake  na kumfanya kuwa mrithi wa ahadi na uzao wa Abraham kwa njia ya Imani, kwa hiyo kila mkristo amebarikiwa tayari, na hazina zote za utajiri zimekwisha kuwekwa wazi katika ulimwengu wa roho.

Waefeso 1:3-5 “Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo; kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake.”

Kila mtu aliyemwamini Bwana Yesu na kazi yake iiyofanyika pale msalabani amebarikiwa katika ulimwengu wa roho, wewe na mimi tuna Baraka zote za rohoni tayari kazi kubwa iliyoko mbele yetu ni kuzitafasiri Baraka hizo za rohoni ili kwamba ziweze kuonekana na kudhihirika katika ulimwengu wa mwili na ziko kanuni muhimu za kuzingatiwa

1.       Kiini cha Baraka zetu zote za rohoni na mwilini ni Yesu kristo naye tayari amekwisha kutubariki sasa ili tuweze kuziona Baraka zake hatuna budi kumpa yeye kipaumbele na hili ndilo alilolifanya Abraham Mathayo 6:31-33 “Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”

 

2.       Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote Mithali 3:5-6 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.”

 

3.       Mtumikie Bwana Mungu wako Kutoka 23:25-26. “Nanyi mtamtumikia BWANA, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako. Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza.”

4.       Fanya kazi kwa mikono yako na kwa bidi kumbukumbu 28:11-12 “Bwana atakufanya uwe na wingi wa uheri, katika uzao wa tumbo lako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako, katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako kwamba atakupa. Atakufunulia Bwana hazina yake nzuri, nayo ni mbingu, kwa kutoa mvua ya nchi yako kwa wakati wake, na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako; nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe.”

 

5.       Uwe na moyo wa ukarimu Mithali 28:27 “Mwenye kuwagawia maskini hatahitaji kitu; Bali afichaye macho yake atakuwa na laana nyingi.” Luka 6:38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.”

 

6.       Usipandishe mabega wala kuvimba kichwa Mungu anapokubariki Daniel 4:28-37 “Hayo yote yakampata mfalme Nebukadreza. Baada ya miezi kumi na miwili, alikuwa akitembea ndani ya jumba la kifalme katika Babeli. Mfalme akanena, akasema, Mji huu sio Babeli mkubwa nilioujenga mimi, uwe kao langu la kifalme, kwa uwezo wa nguvu zangu, ili uwe utukufu wa enzi yangu? Hata neno lile lilipokuwa katika kinywa cha mfalme, sauti ilikuja kutoka mbinguni, ikisema, Ee mfalme Nebukadreza, maneno haya unaambiwa wewe; Ufalme huu umeondoka kwako. Nawe utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni; utalishwa majani kama ng'ombe, na nyakati saba zitapita juu yako, hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, awaye yote. Saa iyo hiyo jambo hilo likatimizwa, likampata Nebukadreza; alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani kama ng'ombe, na mwili wake ulilowa maji kwa umande wa mbinguni, hata nywele zake zikakua, zikawa kama manyoya ya tai, na kucha zake kama kucha za ndege.Hata mwisho wa siku hizo, mimi, Nebukadreza, nikainua macho yangu kuelekea mbingu, fahamu zangu zikanirudia; nikamhimidi Yeye aliye juu, nikamsifu na kumheshimu Yeye aishiye milele; kwa maana mamlaka yake ni mamlaka ya milele, na ufalme wake hudumu toka kizazi hata kizazi;  na watu wote wanaokaa duniani wamehesabiwa kuwa si kitu, naye hufanya kama atakavyo, katika jeshi la mbinguni, na katika hao wanaokaa duniani; wala hapana awezaye kuuzuia mkono wake, wala kumwuliza, Unafanya nini wewe? Basi wakati uo huo fahamu zangu zikanirudia, na kwa ajili ya utukufu wa ufalme wangu, enzi yangu na fahari yangu zikanirudia; na mawaziri wangu, na madiwani wangu, wakaja kunitafuta; nami nikathibitika katika ufalme wangu, nikaongezewa enzi kupita kiasi. Basi mimi, Nebukadreza, namhimidi Mfalme wa mbinguni, namtukuza na kumheshimu; maana matendo yake yote ni kweli, na njia zake ni za adili; na wale waendao kwa kutakabari, yeye aweza kuwadhili.”

Mungu huwapinga wenye kiburi lakini huwapa neema wanyenyekevu, wako watu tena hasa wale wanaotoka kwenye hali duni zaidi wanakuwa malimbukeni kweli kweli, Mungu akiwafanikisha wanataka dunia nzima ijue, wanavimba kichwa na kusahau kuwa Mungu ndiye chanzo cha Baraka na utajiri wanadhani Mungu amewainua kunyanyasa watu, wanataka watawale kila kitu katika maisha yako mpaka hatima yako watoto wako na mkeo, wakifika eneo la tukio utasikia hiki ni changu, hiki ni changu, hiki ni change hawarudishi utukufu kwa Mungu, kuinuliwa kwao ndio kuwanza kupata shida kwa wengine, kuinuliwa kwao ndio kuanza kufukuzwa kwa watu wengine, kuteseka na kusemwa vibaya sikiliza Mungu hatubariki na kutuinua ili wengine wanyanyasike Mungu hutubariki na kutuinua ili tuweze kuwa Baraka kwa wengine na sio kutawala maisha ya watu wengine, Mungu alimbariki Abrahamu kwa sababu alikuwa anajua kuwa atawafaa wengine           

Kimsingi maagizo yote ya kibiblia yanayohusiana na kanuni za kubarikiwa utaweza kuyaona ndani ya maisha ya Ibrahimu na Isaka, na kanuni za ujanja ujanja utaweza kuziona ndani ya Yakobo, mpaka Mungu alipombariki na kumuita Israel, hakuna muujiza zaidi ya kumpata mtenda muujiza na hakuna ufame bila kumpata mfame kama tutamuweka Mungu mbele hakuna jambo litakalozuia mafanikio kwa mkristo awaye yote na wote wanaomtegemea             

Sitatwaa chochote kilicho chako!

Baada ya kuwa tumejifunza maswala kadhaa ya muhimu na kanuni za Mungu za kubarikiwa na jinsi Mungu alivyombariki Abraham sasa ni muhimu kwetu kurejea katika kiiini cha somo letu katika maneno ya Abraham kuwa hatatwaa chochote kilicho cha mfalme wa Sodoma

Abraham aliyasema maneno haya akimjibu mfalme wa Sodoma, Abraham alipigana vita hii akiwa na askari wake 318 sababu kuu ya kupigana kwake ni ili kumrejesha Lutu ndugu yake ambaye alikuwa ametekwa katika vita ile, Mungu alimpa Abraham ushindi mkubwa sana kwa kuwashinda wafalme kadhaa na alilazimika kumsaidia mfalme wa Sodoma kwa kuwa ndiko alikokuwa anakaa Lutu aliporejea na Ushindi Mara mfalme wa Sodoma, aligundua kuwa Abraham ana vijana hodari sana na kama akiwapata yeye haitaji mali, kwani atapata mali kwa kuwateka nyara wafalme wengine huko vitani kwa kutumia vijana waliofunzwa vita vyema na kwa weledi kupitia Abraham

Mwanzo 14: 1-12 “Ikawa siku za Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, na Kedorlaoma mfalme wa Elamu na Tidali mfalme wa Goimu, walifanya vita na Bera mfalme wa Sodoma na Birsha mfalme wa Gomora, na Shinabu mfalme wa Adma, na Shemeberi mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela, ndio Soari3. Hawa wote wakakutana panapo bonde la Sidimu, kwenye Bahari ya Chumvi. Miaka kumi na miwili walimtumikia Kedorlaoma, hata mwaka wa kumi na tatu wakaasi. Na mwaka wa kumi na nne akaja Kedorlaoma na wafalme waliokuwa pamoja naye, wakawapiga Warefai katika Ashteroth-karnaimu, na Wazuzi katika Hamu, na Waemi katika Shawe-kiryathaimu,na Wahori katika mlima wao Seiri, mpaka Elparani iliyo karibu na jangwa. Kisha wakarudi wakaja mpaka Enmisfati, ndio Kadeshi, wakapiga nchi yote ya Waamaleki, na Waamori waliokaa Hasason-tamari. Mfalme wa Sodoma, na mfalme wa Gomora, na mfalme wa Adma, na mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela, ndio Soari, wakatoka wakapanga vita panapo bonde la Sidimu; wapigane na Kedorlaoma mfalme wa Elamu, na Tidali mfalme wa Goimu, na Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, wafalme wanne juu ya wale watano. Na bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami. Nao wafalme wa Sodoma na Gomora wakakimbia, wakaanguka huko, nao waliosalia wakakimbia milimani. Wakachukua mali zote za Sodoma na Gomora na vyakula vyao vyote, wakaenda zao. Wakamtwaa Lutu, mwana wa nduguye Abramu, aliyekaa huko Sodoma, na mali yake, wakaenda zao..”

Mwanzo 14:21 “Mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu, Nipe mimi hao watu, na hizo mali uchukue wewe.”

Huenda mfalme huyu alipoona Abraham akibarikiwa na Mfalme wa Salem naye akatoa zaka yeye alifikiri kwamba Mfalme wa Salem amepokea mali kumbe alikuwa amepokea sadaka, Bera yeye aliamua kumshawishi Abraham ampe watu kisha Abraham achukue mali, hizi zote nyara pamoja na mali zizlizochukuliwa huko Sodoma kwa kutekwa na wafalme ambao Abraham aliwapiga na kuwashinda.

Lakini Abraham alikuwa amekusudia na kumuapia Mungu ya kuwa hatachukua uzi wala ukamba wa kiatu, Abraham hakutaka mtu awaye yote aje ajisifu kuwa ndio sababu ya Baraka za Abraham, Abrahama alitaka heshima yake na ya Mungu wake na hivyo alikataa kujitia unajisi kwa mali za watu wadhalimu Alijua Abraham kuwa watu wa Sodoma walikuwa waovu na hivyo mali zao pia ni za uovu, hivyo alishajifunga kwa kiapo mapemaaaa  kuwa hatajitia unajisi kwa mali za uovu mali za dhuluma na wizi ona

Mwanzo 14:22-23 “Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma, Nimeinua mkono wangu kwa BWANA, Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi, ya kuwa sitatwaa uzi wala gidamu ya kiatu wala cho chote kilicho chako, usije ukasema, Nimemtajirisha Abramu;”

Abraham alikuwa amekula kiapo kuonyesha kuwa amejikabidhi kwa Mungu na aliamua kuweka wazi kuwa kila analolifanya na kila alicho nacho kiini cha mafanikio yake ni Mungu na kwaajili ya utukufu wa Mungu, Abraham alikuwa anelewa kuwa kiini cha Baraka zake ni Mungu aliyejuu sana yeye ndiye anayempa ushindi yeye ndiye anayempa utajiri na mafanikio na ni yeye ndiye aliyemfanya Abraham kuwa na Heshima na utajiri mzito, Kwa hiyo sifa na utukufu wa mafanikio ya Abraham ni Mungu aliyejuu

Mtu wa Mungu huwa wakati mwingine ni muhimu kupokea ushauri, lakini wakati mwingine kataa kila kitu wanachokushauri watu kwaajili ya utukufu wa Mungu, wako watu watajisifu kuwa ni sisi tuliomshauri akafanikiwa ni sisi tuliompa mtaji, ni sisi tuliomsomesha, ni sisi tuliomfanikisha wakati iko wazi kabisa kuwa kiini cha Baraka zako kiko na Mungu, hatima ya maisha yako iko na Mungu wala sio wao wanaohusika, sio kila mtu anayekupinga anaweza kuwa “Destiny Helpers  yaani wasaidizi wanaokupeleka katika hatima yako, kama nduguze Yusufu walitaka kumuua au waliamua kumuuza au alipotiwa gerezani na Potifa ili kumfikisha kwenye hatima yake iliyokusudiwa wengine ni “Destiny killers” kama waameleki ambao walisimama kama kikwazo kutaka kuwazuia Israel wasifikie hatima yao, wengine ni kama Balaam wanaolaani  na kutoa mbinu za kuhakikisha unaharibikiwa, wengine ni kama Herode wanaotaka  nyota yako ichunguzwe ili wapate kumuua mtoto uliyemzaa moyoni mwako au maono yako!

Sitatwaa chochote kilicho chako Abraham alikuwa anamaanisha ana Mungu na hivyo ana kila kitu haitaji msaada wa mtu wala msaada wa kibinadamu isipokuwa watu sahihi walioletwa na Mungu mbele zake ili wawe Baraka kubwa katika maisha yake kama ilivyokuwa kwa Melkizedeki Abrahamu alikuwa anaujuzi wa kujua watu wabaya na watu wema wako watu wazuri katika maisha yetu na wako watu wabaya watu wabaya na wapotelee mbali na mali zao, na maono yao na utajiri wao wa dhuluma na wenye asili ya Sodoma, Mungu muumba wa Mbingu na nchi Mungu aliye hai aliyejuu sana ana uwezo wa kutembea na mimi na wewe bila msaada wa mtu mwovu, mwenye roho mbaya, hatutachukua lolote wala ushauri wala sadaka wala mali ya mtu mwovu, Mungu ana njia yake ya kumbariki Abraham kwaajili ya utukufu wake na sio kwaajili ya utukufu wa wanadamu!, leo hii iko misaada inayotoka katika nchi au vikundi vya watu wanaounga mkono ushoga, ni jambo la kusikitisha sana kuwa kwa sababu ya tamaa wako watu ambao wako radhi kuchukua fedha na mali za watu hao waovu  ili kuendesha huduma mbalimbali, nataka nikutie moyo ya kuwa chanzo cha Baraka zetu na awe Mungu wa Ibrahimu na Isaka na Yakobo, chanzo cha mafanikio yako iwe haki, unaonaje kama utafanikiwa kwa kufanya majungu, ukifanikiwa kwa uchawi, ukifanikiwa kwa fitina ukifanikiwa kwa uongo, ukifanikiwa kwa wizi je utamtukuza Mungu huku ukiwa unaelewa wazi chanzo cha Baraka zako ni uovu? Abrahamu akasema sitatwaa chochote kilicho chako, Mungu ndiye sababu ya Baraka zangu na zako mtu wa Mungu!

Na. Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi Mwenye hekima!

Hakuna maoni: