Zaburi 57:1-3 “Unirehemu, Ee Mungu,
unirehemu mimi, Maana nafsi yangu imekukimbilia Wewe. Nitaukimbilia uvuli wa
mbawa zako, Hata misiba hii itakapopita. Nitamwita MUNGU Aliye juu, Mungu
anitimiziaye mambo yangu. Atapeleka toka
mbinguni na kuniokoa, Atukanapo yule atakaye kunimeza. Mungu atazipeleka
Fadhili zake na kweli yake”
Utangulizi:
Hakuna jambo lililozuri kulipokea
duniani kama Rehema, Kila mwanadamu anapenda kurehemiwa na ndio maana katika
zaburi hii ya 57 tunamuona Daudi, akiomba rehema kwa Mungu, kwa mujibu wa
historia ya kimaandiko zaburi hii ilitokana na Maisha ya Daudi nyikani wakati
alipokuwa katika miaka ya kumkimbia Sauli, ambaye alikuwa anataka kumuua kwa
sababu ya wivu, Daudi alikuwa akikimbia kuyaokoa maisha yake na kujificha
katika mapango huko Engedi magharibi mwa pwani ya bahari iliyokufa. Ni katika mazingira ya aina hiyo
yaliyokuwa magumu katika maisha ya Daudi ndio tunaona akimuomba Mungu katika
zaburi hii akihitaji rehema za Mungu kwake!
1Samuel 24:1-3 “Ikawa, Sauli aliporudi
baada ya kuwafuatia Wafilisti, aliambiwa ya kwamba, Daudi yuko katika nyika ya
Engedi. Ndipo Sauli akatwaa watu elfu (tatu) waliochaguliwa katika Israeli
wote, akaenda kumtafuta Daudi na watu wake juu ya majabali ya mbuzi-mwitu.
Akafika penye mazizi ya kondoo kando ya njia, na huko kulikuwa na pango; Sauli
akaingia ndani ili kuifunika miguu. Na Daudi na watu wake walikuwa wakikaa mle
pangoni ndani sana.”
Kuomba rehema za Mungu
hakuhitajiki tu wakati ambapo tumetenda dhambi na tuko katika toba na basi
kwaajili hiyo tunaomba Rehema Hapana hapa Daudi kuna kitu kingine cha tofauti
anatufundisha kuhusu utajiri wa rehema, tunaweza kumuomba Mungu rehema hata
wakati wa mapito yetu na mahitaji yetu, wote tunakumbuka ombi la Batrimayo kwa
Yesu Kristo Mwana wa Daudi aliomba arehemiwe lakini kwaajili ya nini kwaajili
ya ukarabati wa macho yake ili aweze kuona ona
Luka 18:35-43 “Ikawa alipokaribia Yeriko,
mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya njia, akiomba sadaka; na alipowasikia
makutano wakipita, aliuliza, Kuna nini? Wakamwambia, Yesu wa Nazareti anapita.
Akapiga kelele, akisema, Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu. Basi wale
waliotangulia wakamkemea ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza sauti,
Ee Mwana wa Daudi, unirehemu. Yesu akasimama, akaamuru aletwe kwake; na
alipomkaribia, alimwuliza, Wataka nikufanyie nini? Akasema, Bwana, nipate
kuona. Yesu akamwambia, Upewe kuona; imani yako imekuponya. Mara hiyo akapata
kuona, akamfuata, huku akimtukuza Mungu. Na watu wote walipoona hayo walimsifu
Mungu.”
Kwa hiyo tunaweza kuinua macho
yetu katika mtazamo mwingine na kujifunza umuhimu wa rehema za Mungu katika
maisha yetu na utaweza kufurahia mpango wa Mungu katika maisha yetu na kujua
kuwa kila wakati katika changamoto yoyote tunayokutana nayo tunahitaji rehema
za Mungu na zitatupa upenyo tunaouhitaji siku zote katika maisha yetu.
Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia maswala matatu muhimu yafuatayo:-
1. Umuhimu
wa rehema za Mungu
2. Madhara ya kukosekana kwa rehema
3. Unirehemu
maana nafsi yangu imekukimbilia wewe
Umuhimu wa rehema za Mungu.
Ni muhimu kufahamu kuwa hakuna
jambo muhimu duniani Kama rehema! Rehema inapokosekana katika dunia kila kitu
kinaweza kuharibika na picha la kutisha likajitokeza Duniani, kwa kuelewa
umuhimu wa rehema Daudi anaomba rehema wakati akiwa anapita katika mateso na
majaribu makali sana
Rehema ni nini? Neno rehema
alilolitumia Daudi katika zaburi ya 57 katika biblia ya kiebrania linasomeka
kama CHANAN kimatamshi Khaw-nan ambalo maana yake ni kuomba
kuhurumiwa katika wakati wa mgandamizo wa mawazo, hususani wakati unapitia hali
ngumu au mateso, au kuomba kuhurumiwa kutoka kwa mtu mwenye uwezo na mamlaka na
nguvu ya kukuadhibu au kukudhuru, Neno hilo kwa kilatini ni Merced au merces kwa kiingereza Mercy
Daudi alihitaji rehema za Mungu
wakati alipokuwa amekimbilia katika nyika ya Engedi ambayo ilikuwa na mapango
mengi yeye alikuwa na watu wapatao mia sita tu wakati Sauli alikuwa akimtafuta
na askari wapatao 3000 tena hawa walikuwa ni wateule yaani watu hodari na
wataalamu wa vita kama ungekuwepo katika uwanja wa vita ungeweza kuona mapango
kila mahali na upelelezi ulikuwa umeonyesha wazi kuwa Daudi yuko huko na hivyo
Sauli alikuwa na uhakika wa kumpata na kumla nyama au kumfanya akitakacho!
Daudi alisali sala hii katika
zaburi 57 Yeye alihitaji rehema alijua kuwa Mungu atatuma rehema zake na kuwa
rehema hiyo hiyo ndiyo itakayomuokoa na majanga yanayomkabili, Mungu alijibu
vipi Mungu alimpiga Sauli upofu yeye na majeshi yake walifanya mapumziko katika
pango lilelile ambalo Daudi na watu wake walikuwa kwa ndani zaidi ona
kilichojitokeza
1Samuel 24:3-6 “Akafika penye mazizi ya
kondoo kando ya njia, na huko kulikuwa na pango; Sauli akaingia ndani ili
kuifunika miguu. Na Daudi na watu wake walikuwa wakikaa mle pangoni ndani sana.
Nao watu wa Daudi wakamwambia, Tazama, hii ndiyo siku ile aliyokuambia Bwana,
Angalia, nitamtia adui yako mikononi mwako, nawe utamtenda yo yote utakayoona
kuwa mema. Basi Daudi akainuka, akaukata upindo wa vazi lake Sauli kwa siri.
Lakini halafu, moyo wake Daudi ukamchoma, kwa sababu amekata upindo wa vazi
lake Sauli. Akawaambia watu wake, Hasha! Nisimtendee bwana wangu, masihi wa
BWANA,neno hili,kuunyosha mkono wangu juu yake,kwa maana yeye ni masihi wa
BWANA.”
Unaona matokeo ya kuomba rehema
yalisababisha majibu ya kushangaza Mungu alimleta Sauli katika pango lilelile
alilokuwepo Daudi na tayari kulikuwa na neno la unabii ya kuwa siku moja bwana
angentia Sauli mikononi mwa Daudi angalia sentensi hii - hii ndiyo siku ile aliyokuambia Bwana,
Angalia, nitamtia adui yako mikononi mwako Ilikuwa wazi kabisa kuwa
Mungu alikuwa ameshasema wazi kuwa Daudi afanye anachoweza kukifanya na washirika
wa Daudi walimkumbusha lakini yeye aliwakataza, Daudi alikumbuka rehema, yeye
alikuwa amemuomba Mungu rehema na hivyo aliziamini rehema za Mungu na fadhili
za Mungu kuwa zinaweza kumlipia. Rehema ni tabia ya uungu, Daudi alionyesha
ukomavu na alikuwa na ujuzi kuwa Mungu wa Ibrahimu Isaka na Yakobo ni Mungu wa
rehema Biblia inasema katika Maombolezo
3:22 “Ni huruma za Bwana kwamba hatuangamii, Kwa
kuwa rehema zake hazikomi.” Unaona hatuwezi kukwepa huruma na rehema
za Mungu kabisa hata wakati wa majanga maana hii ndio tabia ya Mungu ndio
rehema ndio jina lake kwa kweli na
Kutoka 34:5-7 “BWANA akashuka ndani ya lile
wingu, akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina la BWANA. BWANA akapita
mbele yake, akatangaza, BWANA, BWANA, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili,
si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli; mwenye kuwaonea huruma watu
elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia
mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao,
na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne.”
Bila rehema za Mungu hakuna
mwanadamu angestahili kuwepo, Bila rehema za Mungu hakuna mwanadamu angeweza
kuhesabiwa haki, Bila rehema za Mungu
tungeweza kuangamia, kila mmoja wetu anapaswa kukumbuka rehema, rehema zinabeba,
reheema zinafungua njia, rehema za Mungu zinatutunza rehema ni uhai wetu!
Madhara ya kukosekana kwa rehema
Ni ukweli uio wazi kuwa hakuna
mtu anaweza kumfikia Mungu na hata kuomba kama hakuna rehema, rehema za Mungu
zingekosekana hali ya kila mtu na kila mwanadamu ingekuwa mbaya sana duniani,
tunaweza kuona wakati wa agano a kale Mungu alipotaka kukaa kati kati ya
wanadamu kupitia hema ya kukutania alitoa maelekezo kwa Musa kutengeneza
Sanduku la agano ili ipatikane njia ya rehema za Mungu kuwafikia wana wa Israel
Mungu alielekeza kuwa ni lazima kiwepo kiti cha rehema, maelekezo haya ni
muhimu sana kwa sababu yanaonyesha wazi kuwa Mungu anakaa juu ya kiti cha
rehema, niseme hivi ofisini kwa Mungu anapokuwa kazini na kufanya kazi zake
zote kiti alichokikalia ni Rehema, bila rehema huwezi kufanikiwa kuwa na
mawasiliano yoyote na Mungu.
Kutoka 25:17-22 “Nawe fanya kiti cha rehema
cha dhahabu safi; urefu wake utakuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa
moja na nusu. Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu; uyafanye ya kazi ya kufua,
katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku. Weka kerubi moja mwisho
mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na
kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku. Na hayo makerubi yatainua mabawa
yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao
zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema. Weka
kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda nitakaokupa ndani
ya sanduku. Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya
kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la
ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli.”
Watu wa agano la kale waliweza
kumfikia Mungu kupitia kiti cha rehema, Mungu ni mtakatifu mno, usafi wake na
utakatifu wake unamtenga kwa wazi na kutoa sababu sahihi ya yeye kuwa mbali na
wanadamu na hata akitakiwa kutokujali, lakini watu wabaya wasiokombolewa na
damu ya Yesu waliweza kumfikia Mungu kwa damu za mafahari ya mbuzi na kondoo na
sadaka za kuteketezwa na damu ya kunyunyizwa iliyomwaga juu ya kiti cha rehema,
hii ilikuwa ni picha ya agano la kale yenye kutusaidia kufahamu umuhimu wa
rehema sisi watu wa agano jipya, kuvunjwa kwa amri kumi za Mungu kukosekana kwa
uadilifu kungepelekea kifo cha kila mtu lakini kabla Mungu hajaziangalia amri
zake tulizozivunja anaangalia
anatuangalia sisi kupitia kiti chake cha rehema ambacho unajua wazi kuwa
kwa damu ya Yesu Kristo iliyomwagiza pale msalabani tunawezeshwa kuwa na haki
ya kupata rehema
Waebrania 4:14-16 “Basi, iwapo tunaye
kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana
maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika
mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo
yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili
tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”
Unaona maandiko yako wazi kuwa
sisi katika agano jipya sasa tunaweza kukaribia kiti cha rehema na kupewa
rehema na neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji yetu, kwa hiyo utakubaliana
nami kuwa hatuhitaji rehema tu wakati tumefanya dhambi, lakini pia tunahitaji
rehema ya Mungu wakati wa mahitaji yetu, na tunaweza kuwasiliana na Mungu pia
kwa kupitia rehema, na hivyo
usishangazwe na Daudi kuomba rehema wakati akiwa anawindwa na adui au kuomba
rehema akiwa vitani, zaburi yake inatufunulia wazi umuhimu mkubwa wa rehema ya
Mungu na madhara makubwa ambayo yangetupata endapo Mungu angekuwa sio mwingi wa
rehema! Kama sio rehema za Mungu hali ya kila mmoja wetu ingekuwa mbaya. Mungu
alipokaa juu ya kiti cha rehema damu ilifunika madhaifu ya kibinadamu na
kusababisha Mungu asijali wala kuruhusu hasira yake kuwaka dhidi ya wanadamu,
unakumbuka ni alama ya damu katika miimo ya milango iliyowaokoa wanadamu wote
waliokuwa ndani ya nyumba zilizowekwa alama ya damu bila kujali ni jinsia gani
iko ndani, ni kabila gani iko ndani na nyumba zote misiri ambazo hawakuwa na
alama ya damu waliangamizwa, ni alama ya damu ndio iliyomuokoa kahaba Rahabu na
familia yake yote, wote waliokuwamo katika nyumba yake walisalimika kwa sababu
ya alama ya damu, asante sana Yesu kuhani mkuu kama sio damu yake aliyoimwaga
msalabani leo tungekuwa pabaya Yesu ndio kiti cha rehema damu yake ina nguvu,
ina uwezo wa kututetea kama sio damu yake leo hii tunapoigwa kwa hukumu, kwa
magonjwa, kwa laana, kwa hasira ya Mungu, kwa majini, kwa mapepo kwa wachawi
kwa nguvu za giza na changamoto nyingi sio hivyo tu hata tusingeweza kusamehewa
dhambi zetu pia
Waebrania 9:22-28 “Na katika Torati karibu
vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo. Basi
ilikuwa sharti nakala za mambo yaliyo mbinguni zisafishwe kwa hizo, lakini
mambo ya mbinguni yenyewe yasafishwe kwa dhabihu zilizo bora kuliko hizo. Kwa
sababu Kristo hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano
wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu
kwa ajili yetu; wala si kwamba ajitoe mara nyingi, kama vile kuhani mkuu
aingiavyo katika patakatifu kila mwaka kwa damu isiyo yake; kama ni hivyo,
ingalimpasa kuteswa mara nyingi tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu; lakini sasa,
mara moja tu, katika utimilifu wa nyakati, amefunuliwa, azitangue dhambi kwa
dhabihu ya nafsi yake. Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada
ya kufa hukumu; kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja
azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao
wamtazamiao kwa wokovu.”
Ni damu ya Yesu pekee inayoweza na
ambayo inalia kwake ili tupate rehema ndio yenye nguvu, inatupa kibali, inatupa
mamlaka dhidi ya uovu inatuthibitishia usalama, inavunja vifungo vya kila aina
inasafisha, inatupa uhakika wa kusamehewa na kuondolewa hatia zetu za mambo
yaliyopita yaliyopo na yajayo inavunja minyororo yote na misiba na huzuni,
inaondoa utumwa wa aina yoyote katika maisha yetu inawafanya majini na mapepo
kutuogopa ni damu ya Yesu ndio kiti cha rehema
Ikikosekana rehema maisha huwa na
majuto na uchungu mkubwa sana, visasi na
mikasa na maisha ya uadui kati ya wanadamu kwa wanadamu yanaweza kutokea pale
rehema inapokosekana, kama shetani anataka kuangamiza maisha yako moja ya njia
atakayoifanya ni kuhakikisha ya kuwa unakosa Rehema, anapoitwa mshitaki wetu na
kazi anayoifanya ya kushitaki ni kuhakikisha kuwa tunakosa rehema kwa Mungu alafu
tunaangamizwa au kupitia machungu na hali ngumu, ni jambo baya sana Mungu anapokubali kuacha
kutuangalia kupitia rehema zake
Zekaria 11:6 “Maana mimi sitawahurumia tena
wenyeji wa nchi hii, asema Bwana; bali, tazama, nitawatia, kila mmoja wao,
mikononi mwa mwenzake, na mikononi mwa mfalme; nao wataipiga hiyo nchi, wala
mimi sitawaokoa mikononi mwao.”
Ezekiel 7:8-9 “Basi hivi karibu nitamwaga
ghadhabu yangu juu yako, nitazitimiza hasira zangu juu yako, nami nitakuhukumu
sawasawa na njia zako; nami nitakupatiliza machukizo yako yote. Jicho langu
halitaachilia, wala sitaona huruma; nitakupatiliza njia zako na machukizo yako
yote yatakuwa katikati yako; nanyi mtajua ya kuwa mimi, BWANA, napiga.”
Unaweza kuona ulinzi wetu na
usalama wetu uko katika rehema za Mungu, Rehema zikikosekana utaweza kuona
tukipatilizwa, tukishughuikiwa, tukinyooshwa, ghadhabu ya Mungu itakuwa juu
yetu hasira zake zitawaka, tutahukumiwa, kila njia yetu itanyooshwa, tutalipia
kila dhambi, tutakosa msaaada tutakutana na machukizo, tutapigwa, tutaonewa,
tutakuwa hatarini, tutatiwa mikononi mwa adui zetu, tutadhalilishwa, na
kutendewa mabaya na uonevu wa kila aina kwa hiyo utakubaliana nami kuwa kuna
madhara makubwa sana ikikosekana rehema! Kanisani kukikosekana rehema,
waliookoka wakikosa rehema, taasisi zikikosa rehema, hospitali kukikosa rehema,
shuleni na nyumbani katika ndoa ikikosekana rehema hakuna kitu kinaweza
kusimama Daudi alielewa umuhimu wa Rehema akasema unirehemu ee bwana unirehemu
maana nafsi yangu imekukimbilia wewe!
Unirehemu maana nafsi yangu imekukimbilia wewe
Zaburi 57:1-3 “Unirehemu, Ee Mungu,
unirehemu mimi, Maana nafsi yangu imekukimbilia Wewe. Nitaukimbilia uvuli wa
mbawa zako, Hata misiba hii itakapopita. Nitamwita MUNGU Aliye juu, Mungu
anitimiziaye mambo yangu. Atapeleka toka
mbinguni na kuniokoa, Atukanapo yule atakaye kunimeza. Mungu atazipeleka
Fadhili zake na kweli yake”
Daudi alikuwa anajua anachokiomba
na sio tu alikuwa akiomba rehema kwa Mungu yeye mwenyewe alikuwa mstari wa
mbele kuishi kile anachokiomba, kama hujawahi kuishi maisha ya kuwa na maadui
nataka nikuambie hakuna jambo baya sana duniani kama kuwa na maadui, vilevile
kama hujawahi kuchukiwa nataka nikuambie hakuna jambo baya duniani kama
kuchukiwa, na pia kama hujawai kuona madhara ya kisasi nataka nikujulishe kuwa
hakuna jambo baya kama kulipa kisasi, Daudi alichagua rehema alijua kuwa rehema
inalipa Mwanaye mkuu baadaye Yesu Kristo mwana wa Daudi alikazia wazi kuwa rehema
kwa wengine inatuzalishia rehema kwa Mungu ona Mathayo 5:7 “Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema.” Rehema inatusaidia kutokulipa mabaya kwa
mabaya rehema ndio inayoongoza kusamehe, kuachilia maumivu yote, uwezo wetu wa
kutokuinua mkono wetu juu ya adui zetu ndio unaoonyesha ukomavu wetu wa kiroho
ni rehema, Daudi alimua kumuachia Mungu, kuhusu Sauli, alikuwa na uzoefu kuwa
hata Nabali aliyemtukana matusi pamoja na kuwa alimtendea wema alitaka kumuua
kwa mikono yake Mwenyewe lakini alipotulizwa na Abigaili Mungu alinyoosha mkono
wake juu ya Nabali yeye mwenyewe kwa niaba ya Daudi, chochote ambacho tunataka
Mungu atufanyie Yesu alionyesha kuwa Mungu anaweza kutupa kama pia tunawafanyia
wengine Mathayo 6:14-15 “Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa
mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu
hatawasamehe ninyi makosa yenu.”
Kwa lugha nyingine ili tupate
rehema kwa Mungu hatuna budi kuwa na rehema kwa wanadamu wenzetu, Daudi
aliifahamu siri hii, angeweza kumuua Sauli, angeweza kumdhuru kwa sababu
alipewa pia neno la unabii kuwa nitamtia adui yako mikononi mwako nawe
utamfanya vyovyote upendavyo hata hivyo aliamua kuchagua njia iliyobora zaidi
ambayo ni Kumuachia Mungu, anapoomba rehema yeye mwenyewe alielewa kuwa
anahitaji sana rehema , ndugu mpenzi msomaji wangu tunahitaji rehema sana,
rehema kila mahali, katika ndoa katika malezi katika maongozi ni rehema za
Mungu tu ndio maana hatuangamii kila mmoja wetu anahitaji rehema na rehema
inalipa.
Mithali 11:17-18 “Mwenye rehema huitendea
mema nafsi yake; Aliye mkali hujisumbua mwili wake. Mtu mwovu hupata mshahara
wa udanganyifu; Apandaye haki ana thawabu ya hakika.”
Kuwa na Rehema kwa Daudi dhidi ya
Sauli kulisababisha apate rehema pale alipokuja kufanya makosa makubwa, kuna
benki ya rehema mbinguni, na hivyo kila mmoja wetu ajifunze kutoka kwa Daudi na
kuachia rehema au kutunza rehema katika maisha yake hifadhi rehema ili baadaye
uje upate faida ya rehema kutoka benki ya mbinguni, rehema ni ufunguo wa kila
aina ya muujiza, tukikosa rehema tunajifungia Baraka zetu, liko gereza na taabu
ya kulipia katika ulimwengu wa roho kama tumekosa rehema ona mfano wa mtumishi asiye na rehema kuna
vitu vya kujifunza
Mathayo 18:21-35 “Kisha Petro akamwendea
akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara
saba? Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.
Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya
hesabu na watumwa wake. Alipoanza
kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Naye alipokosa cha
kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote
alivyo navyo, ikalipwe ile deni. Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia
akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Bwana wa mtumwa yule
akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni. Mtumwa yule akatoka, akamwona
mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia akamkamata, akamshika koo, akisema
Nilipe uwiwacho. Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema,
Nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa
kifungoni, hata atakapoilipa ile deni. Basi wajoli wake walipoyaona
yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote
yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu,
nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; nawe, je! Haikukupasa kumrehemu
mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika,
akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote. Ndivyo na Baba yangu
wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu
yake.”
Daudi anatufunza jambo kubwa sana
kuhusu rehema, hatuna budi kumuomba Mungu na kumshihi aturehemu, kila eneo la
maisha yetu lijawe na rehema na maisha yetu na kila tulifanyalo tukumbuke
umuhimu wa kujawa na rehema weka rehema katika maisha ya watu ili Mungu naye
akutunzie katika akaunti yako ya akiba za rehema maana ni rehema ya Mungu
inayohitajika kila wakati na zaidi sana wakati wa mahitaji yetu, Bwana ampe
neema kila mmoja wetu kuwa mtu aliyejaa rehema ili tuweze kupata rehema katika
jina la Yesu Kristo, Amen
Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni