2Samuel 16:5-12 “Basi mfalme Daudi
alipofika Bahurimu, tazama, kulitoka huko mtu wa jamaa ya nyumba ya Sauli, jina
lake akiitwa Shimei, mwana wa Gera; alitoka, akalaani alipokuwa akienda. Tena
akamtupia Daudi mawe, na watumishi wote wa mfalme Daudi; na watu wote na
mashujaa wote walikuwako mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto. Na
Shimei alipolaani, alisema hivi, Nenda zako! Nenda zako! Ewe mtu wa damu! Ewe
mtu usiyefaa! Bwana amerudisha juu yako
damu yote ya nyumba ya Sauli ambaye umetawala badala yake; naye Bwana ametia
ufalme katika mkono wa Absalomu mwanao; kisha, angalia, wewe umetwaliwa katika
uovu wako mwenyewe, kwa sababu umekuwa mtu wa damu. Ndipo Abishai mwana wa Seruya, akamwambia
mfalme, Mbona mbwa mfu huyu amlaani mfalme bwana wangu? Na nivuke, nakusihi,
nikaondoe kichwa chake. Mfalme akasema, Nina nini na ninyi, enyi wana wa
Seruya? Kwa sababu yeye analaani, na kwa sababu Bwana amemwambia, Mlaani Daudi,
basi, ni nani atakayesema, Mbona umetenda haya?Daudi akamwambia Abishai, na
watumishi wake wote, Angalieni, huyu mwanangu, aliyetoka viunoni mwangu,
anautafuta uhai wangu; si zaidi Mbenyamini huyu sasa? Mwacheni alaani, kwa
sababu Bwana ndiye aliyemwagiza. Labda
Bwana atayaangalia mabaya yaliyonipata, naye Bwana atanilipa mema kwa sababu ya
kunilaani kwake leo”
Utangulizi:
Absalom Mwana wa Daudi alikuwa
ameinuka kinyume na baba yake kwa kusudi la kumpindua na kumuua na kuchukua
utawala wake, Hivyo ilimuazimu Daudi na majeshi yake kukimbia kwanza, akiwa
njiani anakutana na mtu anaitwa Shimei yeye ni wa jamaa ya familia ya Sauli,
Mtu huyu ghafla anaanza kurusha mawe na mavumbi akimlaani Daudi na kumtukana
kama mtu aliyechukua madaraka baada ya Sauli, akimshutumu ya kuwa ni Mungu
amesababisha machafuko kwa sababu ya Damu ya Sauli na watu wake (Damu ya nyumba
ya Sauli), Baadhi ya mashujaa wa Daudi walimkemea na kumuomba Daudi waondoe
kichwa cha mbwa mfu huyu, anayemtukana na kumlaani mfalme jambo hili lilikuwa ni kinyume cha sheria na
kinyume cha maagizo ya torati Kutoka
22:28 “Usimtukane Mungu, wala usimlaani mkuu wa
watu wako.”
Kumlaani mfalme au kumtukana ni
kosa ambalo kwa mujibu wa torati lilikuwa linahalalisha hukumu ya kifo, kama
mtu akikubambikizia kesi ya kumtukana mfalme katika Israel pia ilihesabika kuwa
umemtukana Mungu unaona?
1Wafalme 21:8-14. Basi, akaandika
nyaraka kwa jina la Ahabu, akazitia muhuri yake, akazipeleka zile nyaraka kwa
wazee, na kwa watu wenye nguvu waliokuwa katika mji wake, waliokaa pamoja na
Nabothi. Akaandika katika zile nyaraka, akasema, Pigeni mbiu ya watu kufunga,
mkamweke Nabothi juu mbele ya watu,
mkainue watu wawili, watu wasiofaa, ili wamshitaki, na kumshuhudia,
kunena, Umemtukana Mungu na mfalme. Kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili
afe. Wale wazee wa mji wake, na walio wenye nguvu waliokaa mjini mwake,
wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza, kama ilivyoandikwa katika nyaraka
alizowapelekea. Wakapiga mbiu ya watu kufunga, wakamweka Nabothi juu mbele ya
watu. Na hao watu wawili, watu wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale
watu wasiofaa wakamshuhudia Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana
Mungu na mfalme. Ndipo wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa.
Wakampelekea Yezebeli habari, wakasema, Nabothi amepigwa kwa mawe, amekufa.”
Pamoja na kuwa ilikuwa halali
kabisa kwa mujibu wa Torati mtu huyo kuuawa na ingekuwa ni makosa kwa mfalme
kumuachia kwani naye angekuwa hajaitimiza torati, lakini kwa amri ya kifalme
Daudi alimkinga mtu huyo na kuamuru kuwa aachiwe alaani kwa sababu Bwana ndiye
aliyeagiza! Daudi hakutaka mtu huyo alipwe apatwe na mabaya wakati ule kwani
alikuwa anaamini katika uaminifu wa Mungu, Yeye aliyetoa sheria ana haki ya
kuhukumu kwa sheria yake “mwacheni
alaani kwa sababu Bwana ndiye aliyemtuma”! Tutajifunza somo hili kwa
kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Puuzia
laana zisizo na maana au sababu
·
Kufuata
njia ya Mungu
·
Kanuni ya
Mungu kuhusu laana na Baraka.
Puuzia laana zisizo na maana au sababu.
Wote tunakubalina ya kuwa tukio
kama hili halikuwa tukio rahisi, mara nyingi kama mtu anakulaani au kukutukana
wengi wetu tungependa kujibu mapigo mara moja
na wakati huo huo tungeweza kutukana au kulaani mara moja au tungemuomba Mungu amshughulikie mara moja
hili ni jambo la kawaida la kibinadamu hata mimi napenda!
Lakini haikuwa hivyo kwa Daudi,
mwana wa Yese yeye alimsamehe mtu huyu, na kuipuuzia laana yake na matukano
yake na aliamini katika Mungu ya kuwa Mungu atamlipia na alitazamia kuwa Mungu
atamrehemu yeye Daudi na rehema zake zitakuwa juu yake, Daudi aliiona laana ya
Shimei na mabaya anayomtakia hayakuwa na mashiko kiasi cha kumfanya Mungu
ashawishike kumlaani Daudi kwani laana hiyo haikuwa na maana wala sababu za
haki, kwani Daudi hakufanya kosa katika familia ya Sauli iliyokuwa na mashiko
ya yeye kulaanika kwa hiyo matusi na laana
za Shimei alizozitoa ilikuwa kama mbayuwayu tu katika kuruka kwake ona
Daudi hakuwahi kuinua upanga wake njuu ya Sauli wala familia yake, Ni sauli
ndiye aliyekuwa anataka kumuua Daudi lakini Daudi hakufanya hivyo hata kidogo!
Mithali 26:6 “Kama shomoro katika
kutanga-tanga kwake, Na kama mbayuwayu katika kuruka kwake; Kadhalika laana
isiyo na sababu haimpigi mtu.”
Shomoro na mbayu wayu ni ndege
wadogo sana ndege hawa huwa na tabia aidha ya kufukuza wadudu au wakati
mwingine kucheza kwa kukimbia hewani na kugeuka geuka unaweza kudhani kuwa
wataanguka au kutua lakini huishia kugeuka ama unaweza kudhani wataenda moja
kwa moja kumbe wanarudi, ukweli kama huu ndivyo ilivyo laana isiyo na maana au
sababu, laana ni sawa na uchawi ni
hukumu, Ni tamko ni shambulizi linaloweza kutolewa na mtu na inaweza kumpata
mtu kama ziko sababu za haki za kufanyika
hivyo, Daudi alikuwa na ujuzi huo wazi kuwa hakuna mtu anaweza kumlaani
akalaanika yeye alianza harakati yake ya kwanza kabisa kwa kulaaniwa na Goliath
ona
1Samuel 17:42-43 “Hata Mfilisti alipotazama
huku na huku, akamwona Daudi akamdharau; kwa kuwa ni kijana tu mwekundu, tena
ana sura nzuri. Mfilisti akamwambia Daudi, Je! Mimi ni mbwa hata umenijia kwa
fimbo? Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake.”
Hata pamoja na Goliath kumlaani
Daudi kwa miungu yale laana hiyo haikuweza kufanya kazi na kinyume chake akiwa
anapigana vita kwa jina la Bwana ni Goliath ndiye aliyeishia kupigwa vibaya yeye
na wafilisti wakifuatia
1Samuel 17:45-50 “Ndipo Daudi akamwambia
yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi
ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli
uliowatukana. Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na
kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi
mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu
katika Israeli. Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba Bwana haokoi kwa
upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana, naye atawatia ninyi mikononi
mwetu. Ikawa, hapo Mfilisti alipojiinua, akaenda akamkaribia Daudi, ndipo Daudi
naye akapiga mbio, akalikimbilia jeshi ili akutane na yule Mfilisti. Daudi
akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake,
akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingilia kipajini,
akaanguka chini kifudifudi. Hivyo Daudi akamshinda yule Mfilisti kwa kombeo na
jiwe, akampiga Mfilisti, akamwua; walakini Daudi hakuwa na upanga mkononi mwake.”
Hakuna mtu anaweza kukulaani, ni
Mungu pekee mwenye uwezo wa kufanya hayo, hakuna mwanadamua anaweza kukutakia
mabaya ni Mungu tu, Adui au mtu awaye yote anapokulaani Mungu ana uwezo wa
kuigeuza laana hiyo kuwa Baraka ona
Zaburi 109:27-28. “Nao wakajue ya kuwa ndio
mkono wako; Wewe, Bwana, umeyafanya hayo. Wao walaani, bali Wewe utabariki,
Wameondoka wao wakaaibishwa, Bali mtumishi wako atafurahi.”
Kumbukumbu 28:20 “Bwana atakuletea laana na
mashaka, na kukemewa, katika yote utakayotia mkono wako kuyafanya, hata
uangamie na kupotea kwa upesi; kwa ule uovu wa matendo yako, uliyoniacha kwayo.”
Unaona kwa msingi huo hakuna
manadamu ana mamlaka ya kulaani kile ambacho Mungu amekibariki, Daudi alikuwa
na uhakika kuwa laana ya Shimei na matukano yake yote kinyume na Mfalme
Havingeweza kuathiri lolote katika maisha ya Daudi, hata hivyo kisheria Shimei
alipaswa kuuawa lakini Daudi alichagua rehema na alichagua kuachia kesi kwa
Mungu, msomaji wangu mpendwa usiogope hakuna mtu anaweza kubadili mwenendo wa
maisha yako kwa maneno yake yasiyo na maana, wako watu duniani ambao ni wepesi
sana kulaani, ukimuudhi kidogo tu anamwaga laana nyingi na wengi wetu tunadhani
kuwa laana hizo zimefanya kazi katika maisha yetu n ahata watu wengine wanadani
kwa kukubali kuwa ulilaaniwa, nataka nikueleze ukweli wa kibiblia Hakuna laana
inaweza kuwa na nguvu juu yako isipokuwa kama tutamuasi Mungu, au kuhusika
katika dhuluma au kama kuna mashiko katika hilo
1Petro 3:13-17 “Naye ni nani
atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema? Lakini mjapoteswa kwa sababu ya
haki mna heri. Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike; bali mtakaseni Kristo
Bwana mioyoni mwenu. Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za
tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu. Nanyi mwe na dhamiri
njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao
mwenendo wenu mwema katika Kristo. Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema,
ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya.”
Kufuata njia ya Mungu.
Ni muhimu kufahamu kuwa tuwapo
hapa duniani wako watu wanaweza kuinuka kama shimei katika maisha yetu na
kujiweka katika nafasi ya uadui katika maisha yetu, Hatukuja duniani
kutengeneza maadui lakini wako watu kutokana na matukio kadha wa kadha duniani
wanaweza kujiweka katika nafasi ya adui wao wenyewe linapokuja swala la namna
hii ni muhimu kama ilivyokuwa kwa
Daudi kuchagua njia ya Mungu, Shimei alikuwa amemlaani Daudi na kumlaumu kama
mtu wa damu, lakini ni ukweli ulio wazi kuwa Sauli aljaribu kumuua Daudi karibu
mara saba na Daudi alijaribu kuokoa maisha yake mara kadhaa, akiacha kila kitu
kiwe katika mikono ya Mungu yeye aliamini kuwa Mungu ana njia iliyo bora zaidi
ya kushughulika na wote wanaojiweka katika njia ya maisha yake kama adui zake
na ndio Maana Yesu mwana wa Daudi alifundisha kuwa inatupasa kuwaombea maadui
zetu na kuwapenda Mwalimu alikuwa na maana gani hapa, kwa
vyovyote vile alikuwa na maana ya kuwaacha katika mikono ya Mungu, kumuachia
Mungu hakimu mwenye haki na mwenye hekima yake kuamua namna njema na nzuri
itakayofaa Kwa adui zetu!
Mathayo 5:43-44 “Mmesikia kwamba imenenwa,
Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni
adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,”
Yesu mwenyewe alituachia
kielelezo, hata waliokuwa wakimsulubisha aliwaombea rehema kwa Mungu kwa sababu
ni Mungu pekee ndiye anayeweza kulaani, na sio kila mtu anaweza kulaanika kwa
sababu wako ambao Mungu alikusudia kuwabariki tu uweza huo uko katika mikono ya
Mungu hakuna mtu anaweza kukulaani bila Mungu kutoa kibali au wewe mwenyewe
kuvunja maagizo kadhaa ya kiungu yanayoweza kuruhusu kanuni ya kuvuna na
kupanda ikafanya kazi katika maisha yako, lakini ukweli unabaki wazi kuwa Mungu
hana kigeugeu akimbariki mtu amembariki
Hesabu 23:8 “Nimlaanije, yeye ambaye Mungu
hakumlaani? Nimshutumuje, yeye ambaye Bwana hakumshutumu?”
Hesabu 23:12 “Naye akajibu, akasema, Je!
Hainipasi kuangalia, niseme neno lile Bwana atialo kinywani mwangu?”
Daudi alikuwa na ufahamu huu wote
kuhusu Neno la Mungu alielewa wazi kuwa hakuna mtu anaweza kumlaani na kuwa
kama mtu atafanya hayo anaweza kufanya hayo kwa kibali kutoka kwa Mungu, na
ndio maana akawa na ujasiri wa kusema mwacheni alaani Bwana ndiye aliyemuagiza,
alijua wazi kuwa kama ni Bwana sawa lakini kama si Bwana hakuna mtu anayeweza
kuudhuru kwa sababu zozote zile
Kunaweza kuwako nyakati katika
maisha yetu ambapo watu wanaweza kupandisha kichaa na kuanza kutulaani laana hizo zote zitakuwa ni maneno ya mkosaji
tu yatakuwa ni maneno ya kusema mabaya yanaweza kutoka kwa ndugu, jamaa
majirani, kazini na hata kanisani, watu wanaweza kukushambulia hadharani au
sirini na vyovyote vile lakini tuna njia ambayo tunaweza kuichagua tusiwe kama
watu wa ulimwengu huu, ambao wanaweza kujibu tukio kama hilo kwa mtindo
wanaotaka wao, au tunaweza kuchagua njia ya Mungu kwa kuiga mfano wa Daudi na
Yesu mwana wa Daudi, na kupuuzia maneno
ya kipuuzi na kuonyesha upendo kwa kumuachia Mungu tukijua wazi kuwa hawana
madhara yoyote katika maisha yetu!
Kanuni ya Mungu Mtu kuhusu laana na Baraka.
Daudi alikuwa ni mfalme wakati
anatukanwa mtu aliyemtukana alikuwa anastahili kufa, Daudi alionyesha
kushughulika na kuhitaji Rehema zaidi kwa Mungu kuliko kuruhusu hukumu kwa mtu aliyemtukana,
alionyesha uvumilivu, alionyesha unyenyekevu, alitarajia Mungu mwenyewe anaweza
kuigeuza laana yake kuwa Baraka kutakiwa mabaya kuwa neema na rehema za Mungu,
Mungu atatulipia sio tu huduma tunazofanya bali hata mateso tunayoyapitia hivyo hatuna budi kumuamini Mungu kuwa
atatulipia 2Wathesalonike 1:6 “Kwa
kuwa ni haki mbele za Mungu kuwalipa mateso wale wawatesao ninyi ” Daudi
alitambua kuwa ziko kanuni za kiungu mtu anapolaani alijihisi kuwajibika yeye
kwa makosa yake na kukubali mapenzi ya
Mungu kuliko kushughulika na wengine, Yeye kama Mwanadamu alikosea sana na
Mungu alikuwa amesema upanga hautaondoka nyumbani mwako sasa ulikuwa ni wakati
ambapo mtoto wake mwenyewe ameinuka kinyume naye, na kama mtu baki tu
anamtukana si shani sana ukilinganisha kuwa hata mwana wake wa kumzaa amefanya
mapinduzi:-
-
Kuna
wakati ambapo ni vema tukashughulika sana na changamoto zetu, kuliko kutaka
kuna wengine wakiadhibiwa, wakati sisi tunapoangukia katika mikono ya Mungu na
kunyooshwa, sio vema sana katika wakatio huo huo kutaka Mungu awanyooshe
wengine, hatuna budi kutafuta kibali cha kiungu kwaajili ya maisha yetu na
kumuhitaji Mungu awe msaada wetu zaidi, atupe rehema, aondoe kiburi,
atunyenyekeshe, aondoe ile hali ya kujiona bora kuliko wengine, atupe utambuzi
ya kuwa sisi sio wa thamani sana kuliko wengine, Hata hivyo uelewa katika neno
la Mungu ulimsaidia sana Daudi kutambua kuwa maneno ya Shimei hayana nguvu
kwake Hawezi mtu wa Mungu kulaaniwa na mtu awaye yote bila kibali cha Mungu
Hesabu 22:10-12 “Balaamu
akamwambia Mungu, Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, amewatuma kwangu,
akisema, Tazama, kuna watu waliotoka Misri, wanaufunika uso wa nchi; basi njoo
unilaanie watu hawa; labda nitaweza kupigana nao, na kuwafukuza. Mungu
akamwambia Balaamu, Usiende pamoja nao; wala usiwalaani watu hawa, maana
wamebarikiwa.”
-
Mungu
mwenyewe atambariki kila mtu anayetubarikia na atamlaani kila anayetulaani kwa
sababu tumekusudiwa kuwa Bwaraka kwa mataifa yote Mwanzo 12:3 “nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye
nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”
-
Watu wote
wanaopenda kulaani kwa mujibu wa maandiko wanajiweka katika hatari ya kupatwa
wao na laana hizo na ndio maana maandiko yanatutaka tupendezwe na kubariki
Zaburi 109:17-20 “Naye alipenda kulaani, nako
kukampata. Hakupendezwa na kubariki, kukawa mbali naye, Alijivika laana kana
kwamba ni vazi lake. Ikamwingilia moyoni kama maji, Na kama mafuta mifupani
mwake. Na iwe kwake kama vazi ajivikalo, Na kama mshipi ajifungao daima. Ndiyo
malipo ya washitaki wangu toka kwa Bwana, Na ya hao wanaoisingizia nafsi yangu
mabaya.”
-
Hakuna
silaha inayoweza kufanikiwa juu yakow ewe na mimi na hakuna ulimi au laana
inayoweza kuinuka juu yetu kwani laana hiyo itahukumiwa Isaya 54:17 “Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila
ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi
wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.”
-
Laana
isiyo na mashiko yaani sababu haimpigi mtu “Mithali 26:6 “Kama shomoro katika kutanga-tanga kwake, Na kama
mbayuwayu katika kuruka kwake; Kadhalika laana isiyo na sababu haimpigi mtu.”
-
Mungu
anauwezo wa kutangua laana hata iliyotoka kwa mzazi, Mwanzo 49: 3-4 “Reubeni, u mzaliwa wangu wa kwanza, Nguvu zangu, na
malimbuko ya uwezo wangu. Umewapita wengine kwa ukuu na kwa nguvu. Umeruka
mpaka kama maji, basi usiwe na ukuu, Kwa sababu ulikipanda kitanda cha baba
yako, Ukakitia unajisi; alikipandia kitanda changu.” Maandiko
yanaonyesha wazi kuwa Yakobo hakumbariki Reubeni kwa sababu alivuka mpaka
alikipanda kitanda cha baba yake ni wazi kuwa kulikuwa na laana iliyojificha na
hivyo ukoo huu ungefutika kabisa katika Israel na kuwa dhaifu sana lakini
katika jicho la Rohoni baba wa
kiroho Musa alitamka Baraka kuwa reubeni asife lakini angalau awe na watu
wachache ona Kumbukumbu 33:6 “Reubeni
na aishi, asife; Lakini watu wake na wawe wachache.” Baba wa kimwili
alimlaani Reuben na huenda alimfuta katika Hesabu zake lakini baba wa kiroho
alibadilisha kauli na kutamka Baraka kuwa Reuben na aishi
-
Usilitumie
jina la Mungu kwa kulaani Kutoka 20:7 “Usilitaje
bure jina la BWANA, Mungu wako, maana BWANA hatamhesabia kuwa hana hatia mtu
alitajaye jina lake bure.” Neno usilitaje bure jina la Bwana Mungu
wako katika lugha nyingine linamaanisha pia usilitumie jina lake kulaani No Using the
name of God, your God, in curses or silly banter”
-
Endapo
tuliwahi kulaani watu ni vema ukatubu na kufuta laana hizo, kwa sababu kama
watu hao walihesabiwa haki na Mungu kuliko wewe yanaweza kukurudia
Yakobo 3:10-11 “Katika
kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa
hivyo. Je! Chemchemi katika jicho moja hutoa maji matamu na maji machungu?”
Kristo
anawatarajia wakristo kuwa watu wenye moyo kama wa Daudi, japo tunafahamu
katika mazingira Fulani tunaweza kuzitumia zaburi kama zile zaburi za kulaani,
lakini hata hivyo haipaswi kuwa jambo jepesi sana kukimbilia kulaani, na badala
yake tunaweza kuonyesha wema wa Mungu kwa wale wanaotupinga ili yamkini
ikiwezekana Mungu aweze kulete rehema kwetu pale tunapokuwa na rehema kwa
wengine Mathayo 5:7 “Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema.”
-
Kataa
kurudisha laana kwa anayekulaani – Warumi 12:14 “Wabarikini
wanaowaudhi; barikini, wala msilaani.” Na 17-21 “Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote.
Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote. Wapenzi,
msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi
ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana. Lakini, Adui yako akiwa na njaa,
mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto
kichwani pake. Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.”
-
Jifunze
kubariki – Kubariki ni tabia ya uungu, Mungu alipokuwa anauumba ulimwengu
mara kwa mara alikibariki kila alichokiumba, kubariki ni unabii, unatamka
maneno mazuri ili yaweze kuwapata na wengine
unatamka kwa Imani, unahakikisha kuwa kile unachokiamuru kama Baraka
kinakuwa kwa wengine nawe utabaki kama nabii wa Bwana kwa sababu unachokitamka
kizuri kitawapata wengine,
Waebrania 11:20-21 “Kwa imani Isaka akawabariki Yakobo na Esau, hata katika habari ya
mambo yatakayokuwa baadaye.Kwa imani Yakobo, alipokuwa katika kufa, akambariki
kila mmoja wa wana wa Yusufu, akaabudu akiegemea kichwa cha fimbo yake.”
Ukiyajua hayo Heri wewe ukiyatenda!
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni