Zaburi 39:7-9 “Na sasa ninangoja nini, Ee
Bwana? Matumaini yangu ni kwako, Uniokoe na maasi yangu yote, Usinifanye laumu
ya mpumbavu. Nimenyamaza, sitafumbua
kinywa changu, Maana Wewe ndiwe uliyeyafanya.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu ya kwamba
tuwapo duniani kama wanadamu tunakutana na changamoto nyingi, na changamoto
hizi vyovyote iwavyo ni za kawaida tu wala usiogope, hakuna jambo jipya
linalokupata kila jambo linalokupata ni la kawaida, na wala hauko peke yako
wako wengi wanapitia au wamekwisha kupitia hivyo usiogope.
1Wakorintho 10:13 “Jaribu halikuwapata
ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye
hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na
mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.”
Daudi alikuwa mojawapo ya watu wa
Mungu ambaye alipitia changamoto nyingi sana
na katika zaburi zake utaweza kugundua maswala kadhaa wa kadhaa ambayo
sisi nasi tunayapitia katika maisha yetu, uko wakati ambapo Daudi alikuwa laumu yaani alifanywa LAUMU au alikuwa
akilaumiwa kwa njia mbalimbali na kusemwa au kufanywa kuwa mfano wa matukio
mabaya na yasiyofaa, au mfano wa watu ambao Mungu ni kama alikuwa akishughulika
naye au kumuadhibu, alilaumiwa sana
Daudi kiasi cha kufikia kuvunjika moyo, aliumia au kuugua sana na hakukuwa na
mtu wa kumuhurumia wala kumsaidia
hatimaye aliamua kumlilia Mungu kama
msaada wake ili asaidike naye ona:-
Zaburi 69:16-20 “Ee Bwana, unijibu, maana
fadhili zako ni njema, Kwa kadiri ya rehema zako unielekee. Wala usinifiche uso
wako, mimi mtumishi wako, Maana mimi nimo taabuni, unijibu upesi. Uikaribie
nafsi yangu, uikomboe, Kwa sababu ya adui zangu unifidie. Wewe umejua kulaumiwa
kwangu, Na kuaibika na kufedheheka kwangu, Mbele zako Wewe wako watesi wangu
wote. Laumu imenivunja moyo, Nami ninaugua sana. Nikangoja aje wa kunihurumia,
wala hakuna; Na wa kunifariji, wala sikumwona mtu.”
Yawezekana nawe pia unapitia hali
kama ya Daudi mwana wa Yese, unalaumiwa kila mahali, unaonekana kama sababu ya
mabaya yaliyotokea katika jamii, na
hivyo unalaumiwa unaweza kulaumiwa kwa sababu ya ndoa yako kuvunjika, unaonekana kama wewe
ndio sababu ya kifo cha yule mgonjwa, unaonekana kama wewe ni sababu ya
migogoro, unaonekana kuwa wewe ndio sababu ya ubadhirifu, unaonekana kama wewe
ndio uliye changia ajali ile kutokea, au wewe ndio sababu ya mambo kwenda
vibaya, unaweza kulaumiwa kwa sababu zozote zile, lawama wanafunzi wakifeli,
lawama kwaya ikiharibu, lawama mboga ikiungua, chumvi ikizidi lawama, chumvi
ikipungua, lawama, sukari ikizidi lawama, sukari ikipungua, lawama kwa sababu
ya anguko la mtu Fulani, lawama ya kufukuzwa kazi kwa mtu Fulani, lawama timu
yako imefungwa, lawama wewe ni kocha, lawama wewe ni kiongozi, lawama lawama
lawama Daudi alipoona lawama zimeuvunja moyo wake alimuomba Mungu amsaidie
lakini vilevile asiruhusu yeye kuwa laumu au mithali hata kwa watu wapumbavu!,
tuwapo duniani hatuwezi kukwepa lawama, lakini si kila mtu ana haki ya
kutulaumu, tutajifunza somo hili zuri
kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Maana ya
Laumu
·
Mambo
yanayoweza kusababisha lawama
·
Usinifanye
Laumu ya mpumbavu
Maana ya Laumu
Zaburi 39:7-9 “Uniokoe na maasi yangu yote,
Usinifanye laumu ya mpumbavu. Nimenyamaza, sitafumbua kinywa changu, Maana Wewe
ndiwe uliyeyafanya.”
Neno laumu au lawama linalotumika
katika maandiko hususani katika biblia ya kiebrania ambayo ndiyo iliyoleta
tafasiri ya biblia kwetu upande wa agano la kale linatumika neno “CHERPAH”
kimatamshi KHER- PAW unaweza
kutamka KEPAH neno hili maana yake KUZUNGUMZWA VIBAYA, KUSEMWA VIBAYA KWA
SABABU FULANI, KUSEMWA KWA KULAUMIWA, KUSUKUMIZIWA LAWAMA, KUSHUTUMIWA,
KUFANYWA KUWA MFANO WA TABIA MBAYA KWA, KUSEMWA VIBAYA KWA SABABU WEWE NDIO
UNAEONEKANA UMESABABISHA JAMBO BAYA KUTOKEA, KUSEMWA KWA SABABU YA MATUKIO YA
AIBU, KUSEMWA KWA MAKUSUDI YA KUSHUSHA NA KUHARIBU HESHIMA YAKO, KUSEMWA NA
KUSHUTUMIWA KWA KUSUDI LA KUKUHARIBIA SIFA Kiingereza Shame, au reproach, Neno
Reproach linatafasiriwa kama Disapproval, Kushutumiwa kwa makusudi
ya kukataliwa, na hii sio kwa sababu tu ulifanya jambo baya hapana wakati
mwingine hata kwa sababu ya ubora au uzuri au mafanikio au muonekano wako,
kutokana na mvuto mkubwa ulionao na jinsi jamii inavyokukubali au wanavyokubali
huduma yako na kazi zako na nyimbo zako na lolote lile unalolifanya, wako watu
kwa sababu zao moyoni wanaweza kutafuta namna ya kukulaumu tu, wanatafuta cha
kusema kwa kusudi la kukuharibia sifa ambazo Mungu amekupa
Mfano Luka 23:35-39 “Watu wakasimama
wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa
wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake. Wale
askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki, huku wakisema,
Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe. Na juu yake palikuwa na
anwani; HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI. Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa
alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.”
Unaona lawama wakati mwingine
inakuja tu kwa sababu ya wivu, Yesu hakuwa amefanya lolote baya lakini
alilaumiwa, alishutumiwa alidhihakiwa na kukosolewa hata mtu aliyekuwa
anasulubiwa pamoja naye alisema kama wewe ndiye Masihi basi jiokoe nafsi yako
na sisi pia, hii ilikuwa ni lawama, siku ya mateso yake Yesu alilaumiwa,
alilaumiwa kwa mambo mengi ya uongo, alilaumiwa kwa nukuu mbaya kutoka katika
mahubiri yake, alilaumiwa kuwa alisema anaweza kulijenga katika siku tatu! na
lawama nyingine nyingi zikiwa na makusudi ya kumvunjia heshima, kumdhihaki, kumuaibisha,
kumfedhehi, na kuharibu sifa zake
aonekane mbaya, hafai na anatahili kuuawa
Je umewahi kukwepa maisha ya
lawama? Mimi sijawahi kuyakwepa, lakini sio hivyo tu wakati mwingine hata sisi
wenyewe huwalaumu watu wengine na kuwaona kama wao ndio sababu ya kushindwa kwetu, mume anaweza kumlaumu
mkewe kwa sababu ya tabia za watoto, watoto wanaweza kuwalaumu walimu kwa
sababu ya kufeli kwao, na walimu pia wanaweza kuwalaumu wanafunzi kwa
kusingizio kuwa ni wazito, lawama ziko kila mahali, Kanisani, katika ndoa,
kazini, na hata ukiwa rais wa nchi watu watalaumu, maisha yakiwa magumu
wanaweza kudhani kuwa wewe ndio sababu, hata ukiwa waziri wa Nishati umeme ukikatika
watu wanaweza kukulaumu na hata kukutukana wakisema tayari waziri keshatuzimia
umeme, katika maisha haya ni lawama lawama lawama, kukwepa maisha ya lawama kwa
kiyunani ni ANEPILEPTON – blameless, kutokushutumiwa au
kulaumiwa! Jambo hilo sio jepesi hata
kidogo tuwapo duniani, tutalaumiwa sana jambo hili ni jambo la kawaida tu na
hupaswi kuvunjika moyo!
Mambo yanayoweza kusababisha lawama.
Lawama ni tabia ya kibinadamu,
lawama haitakuja iishie mpaka tunapoondoka Duniani, Hata mwanadamu anapofariki
dunia watu wengi sana huuliza sababu ya kifo chake na kitu fulani kitabebeshwa
lawama ya kifo hicho, maralia, presha, sukari, HIV, ajali uzembe, ujinga na
kadhalika lazima kitakuwepo kitu cha kubebeshwa lawama ndipo mwanadamu aweze
kupumua, mwanadamu hawezi kusikia Amani mpaka apate kitu cha kukisingizia, na
kukipa lawama, mwanadamu analaumu ili kujisikia nafuu, kutupia lawama wengine ni tatizo la kiroho na
kisaikolojia ni njia ya kutafuta unafuu, Nini kinaweza kusababisha lawama?
Lawama ilijitokeza kwa mara ya
kwanza kabisa baada ya anguko la Mwanadamu katika bustani ya Edeni Mara baada
ya Mungu kuhoji sababu ya anguko la mwanadamu na kwanini Adamu na Eva
walijificha walimpomsikia ona
Mwanzo 3:9-13 “BWANA Mungu akamwita Adamu,
akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa
kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi?
Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo
mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala.
BWANA Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema,
Nyoka alinidanganya, nikala.”
Kila mwanadamu mwenye upungufu,
huwa anatafuta kujazilizia udhaifu wake kwa kutafuta visingizio, wanadamu wote
katika uchanga wao na udhaifu wao hawako tayari kubeba lawama za wengine, marazote
watu hutafuta wa kulaumu, ni wanadamu wachache sana ambao wanaweza kukubali
kubeba adhabu au kuwajibika kwaajili ya watu wengine, ukomavu wa juu zaidi wa
kiroho unatupeleka katika kiwango cha kufunika lawama za wengine na sisi kuwa
mstari wa mbele katika kukubali kuzibela lawama. Bwana wetu Yesu ni kielelezo
cha kubeba lawama sio za wanafunzi wake tu na lawama zetu zote wakati wote
amekubali kuwajibika kwaajili yetu hata mbele za baba yake ona:-
Mathayo Luka 22:50-51 “Mmoja wao akampiga
mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume. Yesu akajibu akasema, Mwe radhi
kwa hili. Akamgusa sikio, akamponya.”
Yesu hakutaka moja ya wanafunzi
wake bila shaka (Petro) alaumiwe na
kuwajibishwa kuwa alimkata mtu sikio na badala yake aliomba radhi kwa niaba
yake na kumponya mtu aliyekatwa sikio, huku ni kuwajibika kwa kiwango kikubwa
na cha juu zaidi katika hali ya ukomavu wa mtu wa rohoni, aidha alipokuwa
Msalabani hakutaka kuwalaumu Askari kwa kitendo cha kumsulubisha na badala yake
alijitishwa lawama na kuwaombea msamaha kwa baba yake!
Lawama nyingine tunaweza
kusababisha sisi wenyewe kwa sababu ya makosa yetu na dhambi zetu Mfano Daudi
alipofanya dhambi na Bathsheba Nabii nadhani alimweleza wazi kuwa kosa lake
linaweza kuwapa adui zake na adui za Bwana sababu ya kulaumu/kukufuru ona
2 Samuel 12: 13-14 “Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia Bwana dhambi.
Nathani akamwambia Daudi, Bwana naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa. Lakini,
kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za Bwana nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto
atakayezaliwa kwako hakika yake atakufa.”
Unaona Neno kukufuru linalotumika hapo Kiebrabia ni NAATS
ambalo maana yake umewapa kudhihaki, umewapa kutukana umewapa kusema
vibaya umewapa sababu za kulaumu, unaona
hapo ni kutokana na makosa aliyokuwa ameyafanya hapa, watu walipata nafasi ya
kulaumu au kukufuru, watu hawakumlaumu Daudi tu bali walimlaumu na Mungu wake
kwa sababu Mungu alijivunia Daudi kuliko mtu mwingine yeyote alisema nimemwona
Daudi mwana wa Yese mtu anayeupendeza moyo wangu, wakati mwingine kwa sababu ya
neema na rehema za Mungu zilizo juu yetu na wakati mwingine kwa sababu ya
uhusiano wetu ulio karibu sana na Mungu adui wanaweza kupata sababu ya kulaumu,
uko wakati wanaweza kutafuta hata namna ya kukuchafua ili mradi tu wapate
sababu ya kukulaumu, hata hivyo Daudi alikuwa mtu wa toba alikwisha tubu na
Mungu alikubali kumsamehe lakini kwa kuwa adui zake hawajui njia za Mungu ni
wajinga ni wapumbavu hawajui njia za Mungu Yeye alimuomba Mungu asimfanye kuwa
laumu ya mpumbavu.
Tuwapo duniani hatuwezi kukwepa
lawama kwa sababu yako mambo mengi sana tunayoweza kuyafanya au kufanyiwa,
kusababisha au kusababishiwa lawama, kuishi kwa kukwepa lawama sio jambo jepesi
hata ukijifungia sana ndani watu wanalaumu kuwa unajitenga na watu, na kwa bahati mbaya sasa wako watu wengine
kama ilivyokuwa kwa Daudi wanaongoza kwa kulaumiwa, wakati mwingine unaweza
kulaumiwa hata bila ya sababu na wakati mwingine kwa sababu, Daudi alikuwa
anapitishwa na Mungu katika shule Fulani ili aweze kuwa bora zaidi, katika
wakati huo wa mapito yake alikuwa akilaumiwa kila sehemu na kila mahali mpaka
akazidiwa na lawama, naye aligundua kuwa anapaswa kumuomba Mungu kwaajili ya
lawama anazokutana nazo, alihesabu kuwa ni Mungu ameruhusu yeye awe lawama na
anamuomba Mungu asimfanye kuwa lawama alimsihi
Mungu mara kadhaa asimuache akawa lawama wala asiabike, Mungu hatakuacha
ulaumiwe hata milele tangu zamani Mungu alikuwa amekusudia kumkomboa mwanadamu
kutoka katika lawama, lawama zinazotokana na sisi, au jamaa zetu wanaotuzunguka
ama lawama za aina yoyote ile, lawama ni
alama ya madhaifu kibinadamu.
Usinifanye Laumu ya mpumbavu
Kwa nini Daudi alimuomba Mungu
asimfanye kuwa Laumu ya Mpumbavu? Daudi jambo la kwanza Kabisa alikuwa
akimlilia Mungu ili kwamba mapito anayoyapitia yasifikiriwe kuwa anapita kwa
sababu yeye ni mwenye dhambi, Daudi anamuomba Mungu kuwa ni wachache sana
wanaomjua Mungu wanaoweza kuzielewa njia za Mungu na kujua sababu ya mapito
yake, lakini wengi na hasa watu wajinga na wapumbavu wanaweza wasielewe njia za
Mungu na hivyo wanaweza kufikiri kuwa Mungu anamfanya Daudi kuwa somo la mtu
aliyeivunja torati na hivyo Mungu
anamnyoosha au anamfanyia kama mtu mwenye dhambi au kama mtu ambaye
hajasamehewa! Au mtu ambaye Mungu ameondoa mkono wake kwake, au mtu ambaye
Mungu anaona hasira juu yake, badala yake yeye ni mtu mwenye kibali kwa Mungu Zaburi 39:8 “Uniokoe
na maasi yangu yote, Usinifanye laumu ya mpumbavu.”
Mpumbavu ni mtu ambaye kwa mujibu
wa maandiko hana hekima au ufahamu kuhusu njia za Mungu, au mtu ambaye amekataa
maarifa au mtu asiyemcha Mungu Mithali 1:7
“Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu
hudharau hekima na adabu.” Mpumbavu
ni mtu asiyemjua Mungu au hata kuamini kuwa Mungu yupo, Zaburi 14:1-3 “Mpumbavu amesema moyoni,
Hakuna Mungu; Wameharibu matendo yao na kuyafanya chukizo, Hakuna atendaye
mema. Toka mbinguni Bwana aliwachungulia wanadamu, Aone kama yuko mtu mwenye
akili, Amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema,
La! Hata mmoja.” Mpumbavu pia anaweza kuwa mtu aliyeamini lakini
hazijui njia za Mungu!
Wapumbavu ni watu wenye dhambi,
wasiomcha Mungu watu wenye sifa mbaya, wenye kutenda machukizo, wasiotenda
mema, wasio na akili, wasiomtafuta Mungu, au waliopotoka hawa hueneza lawama
kwa kusudi la kumshutumu Mungu kupitia udhaifu wa kibinadamu, walio nao
watumishi wake, Mungu ni baba kwetu uhusiano wetu na baba hakuna anayeweza
kuuvunja, kwani we inakuuma nini Baba wa nyumba ya jirani akiwa anamuadhibu
mwanaye? Kuadhibiwa kwa Daudi na Mungu
hakukuwa na maana kuwa Mungu hakuwa amesamehe dhambi zake bali Mungu alikuwa na
kusudi la kutengeneza nidhamu kwa Daudi, Mungu alikuwa anashughulika na mtoto
wake lilikuwa ni jambo jema sana kwani alitakiwa kufa lakini hata adhabu ya
kifo ilifutwa, dhambi yake ilifutwa lakini Mungu alimuingiza katika shule ya
Nidhamu tu, Mungu alikuwa anamkemea Daudi asirudie kufanya madudu, Mungu
alikuwa anamkumbusha kuwa mnyenyekevu, anamkumbusha kutikutumia madaraka yake
vibaya, anamkumbusha kuwa anaye baba wa kimbingu ambaye hataruhusu Israel iwe
na wafalme wanaofanana na wafalme wa dunia hii
Waebrania 12:6-11 “Maana yeye ambaye Bwana
ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye. Ni kwa ajili ya kurudiwa
mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na
babaye? Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa
wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali. Na pamoja na hayo tulikuwa na
baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawastahi; basi si afadhali sana kujitia
chini ya Baba wa roho zetu na kuishi? Maana ni hakika, hao kwa siku chache
waliturudi kama walivyoona vema wenyewe; bali yeye kwa faida yetu, ili
tuushiriki utakatifu wake. Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha
furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda
ya haki yenye amani.”
Wakristo pamoja na watumishi wa
Mungu wanaaswa katika maandiko, kutokuwa laumu, au wasiwe wenye kulaumiwa hata
pamoja nakuishi katika ulimwengu huu wenye kizazi cha ukaidi na kilichopotoka
ona
1Timotheo 3:2 “Basi imempasa askofu awe mtu
asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu,
mkaribishaji, ajuaye kufundisha;”
Wafilipi 2:14-15 “Yatendeni mambo yote
pasipo manung'uniko wala mashindano, mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama,
wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka;
ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu,”
Katika nyakati zetu ni muhimu
zaidi kuwa na maombi kama ya Daudi ya kumsihi Mungu asituifanye kuwa laumu kwa
wapumbavu na pia kwa wenye hekima, ni
muhimu kuomba maombi kama haya kama hayajawahi kukuta Mshukuru Mungu lakini
wenzako mara kadhaa watu wasio na nia njema wametutafuta sana ili watuchafue
wapate cha kulaumu, Lakini ashukuriwe Mungu kwa neema yake ametutunza, Lakini
nasema kama ilivyo kwa Daudi maombi yake yalikuwa ni muhimu sana na yanatufunza kitu cha ziada katika nyakati
zetu, Hii ni dua yangu na ninakuombea na wewe Mungu akutunze usiwe na lawama
katika maisha yako na huduma ambayo bwana ameiweka ndani yako, waimbaji,
wahubiri, viongozi, na wasanii pamoja na watumishi wote wa Mungu na wakristo
kwa ujumla mtu asitulaumu!, Mungu amtunze kila mmoja wetu ili kwamba
asipatikane mtu wa kutulaumu kwa habari ya utumishi wetu kwa Mungu, na kwa
habari ya karama hii tunayoitumikia, kama tutakuwa na nidhamu na Munu
ametufunza nidhamu kamwe Bwana hatatuacha tuangukie katika lawama za wapumbavu,
2Wakorintho 8:20-21 “Tukijiepusha na neno
hili, mtu asije akatulaumu kwa habari ya karama hii tunayoitumikia;
tukitangulia kufikiri yaliyo mema, si mbele za Bwana tu, ila na mbele ya
wanadamu.”
Wapumbavu, tukitoa pepo watasema
tunatoa kwa mkuu wa pepo, wapumbavu tukifanikiwa watasema sisi ni freemason,
wapumbavu ukipitia changamoto mbalimbali wanasema tuna dhambi, hawajui njia za
Mungu!, Daudi alikuwa na uhusiano na Mungu kama mtu na baba yake na Mungu
alikuwa ameahidi kuwa akikosea atashughulika naye mtu mpumbavu hawezi kuelewa
Daudi aliomba kwamba asifanyike laumu ya mpumbavu, mtu asiyeelewa njia na
uhusiano alionao Daudi na Mungu
2Samuel 7:14-15 “Mimi nitakuwa baba yake,
naye atakuwa mwanangu; akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo ya binadamu na kwa
mapigo ya wanadamu; lakini fadhili zangu hazitamwondoka, kama vile
nilivyomwondolea Sauli, niliyemwondoa mbele yako.”
Daudi au mwana wa Daudi awaye
yote anaposhughulikiwa na Mungu mpumbavu na anyamaze, kwani haimaanishi kuwa
Mungu ameondoa fadhili zake, kwa mtumishi wake lakini baba yuko kwenye chuo cha
Nidhamu na mtumishi wake
1Wakorintho 11:32 “Ila tuhukumiwapo, twarudiwa na Bwana, isije ikatupasa
adhabu pamoja na dunia.” Katika kiingereza mstari huu unasomeka hivi 1Corinthians 11:32 “But when we are judged by the Lord we are being
disciplined so that we will not be condemned with the world” kwa
msingi huo Mtu wa Mungu anapopita katika majaribu ni Mungu mwenyewe ndiye
anayejua kwanini anapitia hayo, labda Mungu anampa mtu shule ya nidhamu ili
asihukumiwe na watu wa dunia au kama watu wa dunia hii, Hivyo Daudi alikuwa na
uelewa kuwa anapitia njia ngumu lakini bado ana uhusiano mzuri na Mungu, na
hivyo wasio haki wanyamaze kimya hawana hadhi ya kumlaumu Daudi, Ndugu yangu
Hakuna mtu mwenye hadhi ya aina yoyote ile mwenye haki ya kuinua mdomo wake
kuhusu maisha yako, mtu akikushutumu ajue wazi kuwa hana haki, wala hadhi ya
kuinua kinywa chake kuhusu maisha yako, Mungu sio wa mtu Fulani tu Mungu ni
Mungu wa wote wenye mwili, ninapochapwa na baba yangu wewe inakuhusu nini, kila
mmoja na familia yake na kila famuilia na sharia zake, mwache kuwashutumu
wengine kama hamuwaombei, wala kuwashauri, wala kuwatakia Amani, kwani hakuna
mtu awaye yote ajuaye uhusiano wako na Mungu, siri ya mapito yako iko kati yako
wewe na baba yako wa mbinguni,
USINIFANYE LAUMU YA MPUMBAVU!
Na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni