Jumanne, 7 Novemba 2023

Nafsi iliyoshiba taabu!


Zaburi 88:3-5 “Maana nafsi yangu imeshiba taabu, Na uhai wangu umekaribia kuzimu. Nimehesabiwa pamoja nao washukao shimoni; Nimekuwa kama mtu asiye na msaada. Miongoni mwao waliokufa nimetupwa, Kama waliouawa walalao makaburini. Hao ambao Wewe huwakumbuki tena, Wametengwa mbali na mkono wako.”



Utangulizi:

Mwandishi wa zaburi anazungumza maneno magumu sana kuelekea kwa Mungu Muumba, ni haki yake na ni haki ya watu wasiomjua Mungu na wanaomjua Mungu kusema maneno mazito kwa Muumba pale yanapokuwa yametukuta, Si kuwa mwandishi hakuwa mtu mwenye tumaini kwa Mungu hapana lakini alikuwa ni mtu aliyekata tamaa sana AMESHIBA TAABU na maisha yake yako hatarini kiasi ambacho ni kaburi tu ndio analoliona linamkabili, anajina amehesabiwa kama watu waliokufa tayari ingawa bado yuko hai, hana msaada, na anajiona kama ni miongoni mwa wafu basi yeye ni mfu aliyetupwa hana thamani hata ya kuzikwa, sawa tu na watu waliolala kaburini na wamesahaulika, sio na wanadamu tu hata Mungu ni kama hawakumbuki tena nje, mbali kabisa na uwepo wa Mungu, hali kama hii inawakuta wanadamu wote walioko duniani bila kujali una haki au hauna haki, unamcha Mungu au la, lakini tuwapo safarini hapa duniani sio kila jambo linaweza kuwa rahisi, wakati mwingine tunaweza kuwa na majanga mpaka nafsi zetu zikashiba taabu nini maana ya nafsi iliyoshiba taabu? Hilo ndio jambo la msingi tutakwenda kuliangalia katika somo hili !

Nafsi iliyoshiba taabu maana yake ni nafsi iliyoelemewa na hisia kali na za ndani sana za maumivu yanayopelekea mtu ajione kuwa hana matumaini tena ya kuishi, au kama mtu ambaye hawezi tena kupata msaada wowote kutoka kwa yeyote hapa duniani, unahisi uko mwenyewe na umekataliwa na huwezi kuunganishwa tena na yeyote, huwezi kushaurika na yeyote, huwezi kutiwa moyo na yeyote zaidi ya magumu yanayokukabili tu, kuwa katika hali ya nafsi kuugua, kuteseka, kusononeka na kuhuzunika au kushiba taabu kunakuweka katika nafasi ya kuhisi kuwa uko mwenyewe na hata wale uliowategemea wamekuacha ! na unachokiona katika maisha yako ni mauti tu ni kifo pekee ndicho kinachokukabili, huoni tumaini lolote unaona giza, heri hata wewe unaweza hata kusoma maandiko na au hata kufuatilia somo kama hili lakini nafsi iliyoshiba taabu huwa inajawa na huzuni nyingi kiasi cha kufa ona :-

Mathayo 26:37-39. “Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka. Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.”

Je hali kama hiyo imewahi kukutokea? Watumishi wengi wa Mungu wanakutana na hali kama hiyo, Bwana wetu Yesu Kristo alikutana na hali kama hii alipokuwa akiukabili Msalaba alihitaji msaada hata wa rafiki zake lakini walilala, alitamani hata wangekesha na kuomba kwaajili yake lakini hawakuweza hawakuweza kumsaidia kwa sala wala hata kwa maombi wala ushauri! Yeye alimuomba Mungu na ni malaika wa Bwana tu waliokuja kumtia nguvu, Lakini afadhali hata Yesu alitiwa nguvu na malaika wa Bwana, Lakini mwandishi wa zaburi yeye hakukuwa na mawasiliano ya aina yoyote na mbingu.

Tuwapo duniani tunaweza kukutana na changamoto na mapito magumu sana kiasi cha kutufikisha katika hali kama hii, uwe mtu unayemuamini Mungu au hata usiyemuamini Mungu, kuna vipindi ambavyo unaweza kukutana navyo vikakujaza huzuni kiasi cha nafsi yako kushiba, na ukakosa majibu na kuanza kumlilia Mungu, kwanini mimi? Kwanini mimi eee Bwana! Mungu wangu mbona mimi tuuuu!. Hivi Mungu yupo kweli jamani, hivi Mungu anaona, hivi huyu muumba aweza kweli kutoa haki katika hili? Tunaweza kulia na kufikia ngazi ya kufikiri kuwa ni Mungu ameamua kututaabisha ametutupa!, asante katika agano jipya angalau tuna ufunuo kuwa shetani yupo na tunaweza kufikiri kuwa changamoto nyingine zinasababishwa nay eye, Lakini nyakati za agano la kale hawakujua sana habari za shetani na hivyo Mungu tu alibeba lawama zote!  Ona:-

Zaburi 88:14-16 “Bwana, kwa nini kuitupa nafsi yangu, Na kunificha uso wako? Nateswa mimi hali ya kufa tangu ujana, Nimevumilia vitisho vyako na kufadhaika. Hasira zako kali zimepita juu yangu, Maogofyo yako yameniangamiza.”  

Unaona mwandishi wa zaburi hii alifikia hatua ya kufikiri Mungu amemtupa, Mungu ameficha uso wake, na aliona ni kama maisha yake yanapita katika hasira kali za Mungu na akachoka, huenda nawe msomaji na msikilizaji wangu unapitia hali kama hii, Nafsi yako imeshiba taabu, hakuna wa kukujali, uzito wa hali yako ni kama hakuna anayehisi, uko ulimwenguni kama umefutwa tu, Lakini ashukuriwe Mungu wetu ni Mungu anayejali, yeye hamtupi mtu na Bwana anataka kuinua nafsi yako kupitia ujumbe huu, Bwana akupe neema ya kufuatilia somo hili kwa kina ili tuweze kupata suluhu, nafsi zetu zikaponywe na kuacha kufadhaika katika jina la Yesu, Amen! Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

 

·         Maana ya nafsi iliyoshiba taabu!

·         Nafsi iliyoshiba taabu.

·         Mambo ya kufanya Nafsi inaposhiba taabu.

 

Maana ya nafsi iliyoshiba taabu.

Nafsi iliyoshiba taabu kama nilivyogusia kwenye utangulizi ni nafsi iliyoelemewa na hisia kali na za ndani sana za maumivu yanayopelekea mtu ajione kuwa hana matumaini tena ya kuishi, Na mwandishi wa zaburi anaonyesha kuwa alikuwa katika taabu iliyopitiliza kiasi cha kukata tamaa au kiasi cha kufa mwenyewe anasema MAANA NAFSI YANGU IMEJAA TAABU neno taabu linalotumika hapo katika lugha ya Kiebrania linatumika neno RAAH ambalo limetajwa katika maandiko mara 663  na kwa kiyunani ni PERILUPOS  ambalo tafasiri yake kwa kiingereza ni EXCEEDING SORROWFUL au AGONY ambalo maana yake kwa kiingereza ni Extreme physical, mental, and psychological suffering  yaani kwa lugha yetu ni Hatua ya juu na ya mwisho kabisa katika maumivu ya mwili, akili na nafsi kuelekea kufa ni huzuni ya kupita kawaida ni kuugua kwa ndani kabisa kama ingetokea mtu ni mgojwa wa mwili tungeweza kusema kuwa yuko mahututi!

Sa katika maisha haya ya dunia hii iliyojaa taabu kwa kawaida ziko taabu ambazo tunaweza kuvumilia lakini inapofikia hatua ya kushiba taabu, maana yake mtu amefikia hatua ya mwisho kabisa ya kuvumilia taabu hizo na anatamani katika akili yake afe! Yaani ni mtu aliyehemewa na kukata tamaa na amezidiwa amelemewa ametaabika kiasi cha kuona kifo ndio suluhu ya changamoto yake Nafsi inaposhiba taabu huwezi kamwe kuhisi uwepo wa Mungu, unakuwa tu na hisia kuwa Mungu amekutelekeza na kama unamcha Mungu unafikia ngazi ya kuchanganyikiwa kwamba Mungu anawezaje kuachilia hali ngumu na nzito kama hii? ukweli ni kwamba rafiki yako wa karibu anakuwa ni giza tu na unapoteza uwezo wa kufikiria kuwa utaokolewa, hata wanaojaribu kukutia moyo unaweza kushangazwa na Imani yao kwani wewe unaona tu yasiyowezekana kwa ujumla hakuna jambo baya duniani kama kuwa na nafsi iliyoshiba taabu, watu wengi wanaojiua ni wale ambao nafsi zao zilijaa taabu na wakakosa msaada au hata watu wa kuwatia moyo hii ni hali ngumu sana duniani

Mwandishi wa zaburi hii anaonyesha kuwa alikuwa amefikia kiwango cha juu kabisa cha taabu na huzuni na katika zaburi zinazoonyesha kiwango cha huzuni hii ni zaburi ya juu  zaidi katika zaburi zote zenye hisia kali za kuelemewa jambo kubwa la msingi ni kuwa zaburi hii imeandikwa kutundisha ya kuwa Mungu hawezi kuatuacha hata kama tunapita katika hali ngumu kwa kiasi gani  kama tunamtegemea yeye ni lazima atafanya njia na kutuokoa watoto wake bila kujali hali zetu

Kumbukumbu 31:6 “Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu; kwa maana Bwana, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha.”

Waebrania 13:5 “Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.”

Mungu hatakuacha katika hali yoyote ngumu endapo utaliitia jina lake, huyu ni baba anayejali, anayeona, anayefuatilia, anayefundisha na anayetuwazia mema hata katika mazingira yasiyo na matumaini, Mwandishi wa nyimbo za injili namba 122 anasema umechoka umeshushwa moyo, mwambie Yesu, wote tunajua kuwa tukimwambia Yesu hataweza kutuacha atashughulika nasi.

Nafsi iliyoshiba taabu.

Maisha sio kila wakati yana weza kuwa ya furaha, mateso na kupoteza ni moja ya fungu la maisha ya mwanadamu, Hata watu waliojitoa kwa Mungu na kutumiwa na Mungu kwa kiasi kikubwa walikutwa na maisha ya taabu wakati Fulani, mwandishi wa zaburi hii alikuwa katika kilele cha juu zaidi cha taabu yake, kwa kawaida kila mwanadamu kwa kiwango chake anapofikia katika kiwango cha kuwa na huzuni yajuu kabisa au nafsi yake kushiba taabu haoni nuru tena, anaona giza, haoni faida ya siku yake ya kuzaliwa na kilele cha juu kabisa cha suluhisho lake huona ni kifo, Kuwa na uhusiano mzuri au mbaya na Mungu sio sababu hata kidogo ya kukufanya usikutane na taabu, asili ya taabu na masumbufu ya maisha haya ni anguko la Mwanadamu, Tangu Adamu na Eva wazazi wetu walipoasi walifungua mlango wa kifo, mlango wa kifo hutafuta kuua kila kitu katika maisha yetu, kila kitu kina pigwa vita ya mauti, tangu unazaliwa, masomo yako, malezi yako, maisha yako, biashara zako, ndoa yako, kazini kwako, familia yako, mke wako, mume wako, watoto wako,  mazingira yako, chakula chako, biashara zako, kanisa lako na chochote kile kwa namna yoyote ile vitatafuta kupingana nawe na ndipo tunapojikuta tuko katika mazingira ya taabu, “Niliwahi kumwambia mke wangu hivi laiti ingekuwa maisha yanasomewa kwanza kisha ukihitimu ndio unaishi, basi watu wengi tungechagua kutokuzaliwa na kuishi duniani nadhani nikiwamo mimi!”, Lakini kwa bahati mbaya au njema maisha ni zawadi ambayo hatukuichagua, lakini ni zawadi ya thamani na hivyo kama tumepewa ni lazima tukubali kupambana na kila linalotukabili kwaajili ya utukufu wa Mungu,

Yakobo maisha yake yalijaa taabu alipoulizwa una miaka mingapi jibu lake lilikuwa refu kuliko swali lenyewe 

Mwanzo 47:7-9 “Yusufu akamleta Yakobo babaye ndani akamweka mbele ya Farao Yakobo akambariki Farao. Farao akamwuliza Yakobo, Je! Siku za miaka ya maisha yako ni ngapi? Yakobo akamjibu Farao, Siku za miaka ya kusafiri kwangu ni mia na thelathini; siku za miaka ya maisha yangu zimekuwa chache, tena za taabu, wala hazikufikilia siku za miaka ya maisha ya baba zangu katika siku za kusafiri kwao.”

Unaona huyu ni Mtumishi wa Mungu, Yakobo au Israel, anapoulizwa swali kuhusu maisha anajibu hapa akiwa na miaka 130 anaonyesha kuwa afadhali siku za baba zake wao waliishi sana na changamoto hazikuwa kubwa lakini yeye maisha yake YALIJAA TAABU, kwa lugha nyingine alishiba taabu, Neno taabu lililotumika hapo ni neno la Kiebrania RAAH, yaani mbaya, za taabu, za shida, za maumivu, za mateso, za kukatisha tamaa, zisizopendeza, zenye msongo wa mawazo, zenye huzuni, nzito, ngumu, sio za kupendeza, mbaya sana, njaatupu, za hovyo, za kilio, za masononeko, za vitisho, za misiba, za majanga, za bahati mbaya, zisizofaa, zenye madhara, hatarishi, huo ndio ufafanuzi wa neno hilo RAAH yaani kuhuzunisha kupita kawaida unaona

Akieleza kuhusu maisha Ayubu anasema katika kitabu chake Ayubu 14:1 “Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu.” Unaona Ayubu anatumia neno HUJAA TAABU kwa lugha ya Kiebrania kumetumika neno ROGEZ linalotamkwa ROGHEZ akimaanisha siku za maisha ya Mwanadamu hazina starehe, hazina utulivu, zinatisha, ni za hasira

Unajua Ayubu alikuwa Mcha Mungu aliishi maisha matakatifu, alikuwa kuhani wa Mungu wa ngazi yajuu sana, lakini hilo haliwezi kuwa sababu ya kutokuonja taabu naye maisha yake unafahamu nafsi yake ilishiba taabu anasehema ni kama mwanadamu anazaliwa ili akutane na mashaka tu

Ayubu 5:7-11 “Lakini mwanadamu huzaliwa ili apate mashaka, Kama cheche za moto zirukavyo juu. Lakini mimi ningemtafuta Mungu, Ningemwekea Mungu daawa yangu; Yeye afanyaye mambo makuu, yasiyotambulikana; Mambo ya ajabu yasiyo na hesabu; Yeye atoaye mvua inyeshe juu ya nchi, Na kuyapeleka maji mashambani; Awainuaye juu hao walio chini; Na hao waombolezao hukuzwa wawe salama.”

Unaona Bahati nzuri yeye anasema atamchagua Mung utu anapopita katika hali ngumu, wengine kwa sababu ya nafsi kutaabika na kukosa matumaini ndipo wanapoamua kwenda kwa waganga, na wachawi kutafuta msaada, wakati nafsi inapotaabika mtihani wa moyo unapita kupima kuwa utamwangalia nani?

               

 

jambo kubwa zaidi la kumshukuru Mungu mwandishi wa zaburi 88 hakuwahi kutaka kujiua, wala kuwaendea waganga,  lakini alikuwa anaona kuwa Mungu ana wajibika na taabu zote anazozipitia na kuwa ni yeye Mungu ambaye hajajibu maombi yake, wakati nafsi yake imekaribia kufa, Nafsi yake imeshiba taabu, na amekuwa kama mfu hata miongoni mwao waliokufa yeye ametupwa, ametengwa mbali na watu, watu wanamchukia, yupo kwenye kifungo asichoweza kutoka, na anaanza kuwa na shaka kama atamsifu Mungu na kusimulia matendo yake akiwa kaburini na inaonekana kuwa tangu ujana wake maisha yamejaa taabu tu  hii ndio hali ya mtu anapofikia ngazi ya nafsi kushiba taabu

Ndugu yangu nafsi yako inapojaa taabu wewe unakimbilia wapi? Nani anakuwa kuhani wako, je unadhani kujiua ndio suluhu? Je unadhani wewe ndio pekee unayapitia haya? Hapana wewe sio wa kwanza, wala wewe huko peke yako tofauti zetu ni kuwa wengine hawasimulii yanayowakuta lakini kila mwanadamu hata waliofanikiwa wakikuelezea wanayoyapitia utajua kuwa watu wengi wana nafsi zilizojaa taabu!

 

Mambo ya kufanya Nafsi inaposhiba taabu.

Najua kuwa umepitia changamoto ngumu sana na wako watu wamepitia hata mimi pia, kila mmoja anesema aelezee anayoyapitia nadhani kila mmoja sawa na mzani wake anaweza kukiri kuwa yeye ndiye mwanadamu aliyepitia changamoto nyingi zaidi kuliko mwingine, vyovyote iwavyo, masiha yangu pia yamekuwa na taabu zisizoweza kuelezeka, naweza kusema pia kama Yakobo nadhani ni afadhali ya siku za baba zangu, hata hivyo sijawahi kupungukiwa na wema wa Mungu, wakati wote nilipopoteza tumaini hata wakati wa mambo magumu sana, niliziona fadhili za Bwana hakika wema nza fadhili zake zinanifuata mimi siku zote za maisha yangu, nawe pia ndugu yangu Mungu hatapunguza wema wake kwako yeye atakupa kutoboa, na hatimaye ataandaa meza katikati ya watesi wako, nini unatakiwa kufanya wakati huu

1.       Mtumaini Mungu – Mithali 3:5-6 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.”

 

2.       Mkimbilie Mungu – Mwandishi wa zaburi 88 anaanza kwa kuliitia jina la Bwana hata pamoja na nafsi yake kushiba taabu hakuwaza kwenda kwa waganga na badala yake aliendelea kuliitia jina la Bwana kwaajili ya wokovu wake, Ni Yesu tu anayeweza kuwa jibu la taabu zetu zote Zaburi 46:1-3 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.”

 

3.       Ifundishe nafsi yako kuabudu – Wakati unapofikia ngazi ya kuzidiwa na taabu kwa kuwa ni nafsi ndiyo inayosumbuka nafsi hiyo useme nayo, uishirikishe kumuabudu Mungu, uishirikishe kukumbuka mambo kadhaa hata kama ni machache aliyoyafanya Mungu, ikumbushe nafsi isisahau kuwa na shukurani, ikumbushe nafsi matendo makuu ya Mungu

 

Zaburi 103:1-4 “Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote. Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote, Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema,”

 

4.       Usijiombee kufa – Maisha yetu ni zawadi, hatukuchagua kuzaliwa kwa hiyo unapokuwa katika wakati wa taabu ni rahisi kumshutumu Mungu na kumwambia inatosha niondoe HAPANA usiombe hivyo kuomba hivyo ni kukosa shukurani ni kumjibu Mungu kuwa ulituumba bure tu huna makusudi nasi, ni afadhali kujua kuwa taabu yako ina somo gani baada ya kumaliza na Mungu katika shule yake kuliko kujiombea kufa hata hivyo Mungu huwa hajibu dua za namna hiyo

 

-          Ayubu alijua kuwa baada ya moto wa taabu yake atatoka akiwa angaa zaidi kama dhahabu ona Ayubu 23:10-12 “Lakini yeye aijua njia niendeayo; Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu. Mguu wangu umeshikamana sana na hatua zake; Njia yake nimeishika, wala sikukengeuka. Sikurudi nyuma kuiacha amri ya midomo yake; Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu,”

 

-          Musa alijiombea kufa – alipozidiwa na majukumu na taabu za uongozi wa kuongoza watu wanaonung’unika Musa aliona taabu sana na akamuomba Mungu ikiwezekana afe ona Hesabu 11:4-15. “Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, N'nani atakayetupa nyama tule? Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu; lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu. Na hiyo mana ilikuwa mfano wa chembe za mtama na kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwake bedola. Watu wakazunguka-zunguka na kuikusanya, kisha wakaisaga kwa mawe ya kusagia, au kuitwanga katika vinu, kisha wakaitokosa nyunguni, na kuandaa mikate; na tamu yake ilikuwa kama tamu ya mafuta mapya. Umande ulipoyaangukia marago wakati wa usiku, hiyo mana ilianguka pamoja nao. Basi Musa akawasikia watu wakilia katika jamaa zao zote, kila mtu mlangoni pa hema yake; na hasira za Bwana zikawaka sana; Musa naye akakasirika. Musa akamwambia Bwana, Mbona umenitenda uovu mimi mtumishi wako? Kwa nini sikupata neema machoni pako, hata ukanitwika mzigo wa watu hawa wote juu yangu? Je! Ni mimi niliyewatungisha mimba watu hawa wote je! Ni mimi niliyewazaa, hata ikawa wewe kuniambia, Haya, wachukue kifuani mwako, mfano wa baba mwenye kulea achukuavyo mtoto anyonyaye, uende nao mpaka nchi uliyowaapia baba zao? Nipate wapi nyama ya kuwapa watu hawa wote? Kwani wanililia, wakisema Tupe nyama, tupate kula. Mimi siwezi kuwachukua watu hawa wote peke yangu, kwa kuwa ni mzigo mzito sana wa kunishinda. Na kama ukinitenda hivi, nakuomba uniulie mbali, kwamba nimepata fadhili mbele ya macho yako; nami nisiyaone haya mashaka yangu.”  Ni hali ya kawaida wakati mtu anapokuwa katika taabu na nafsi yakle ikalemewa huwa hawazi kuhusu uweza wa Mungu na hivyo hufikiri kuwa suluhisho ni kufikia mwisho kuliko kuona aibu au uchungu ulioko mbele lakini Musa hakujua kuwa Mungu alikuwa na mpango mwema nasema hivi usikufe wala usiombe kufa kwa sababu Mungu anataka kutukuzwa katika njia unayoipitia           

 

-          Eliya – alikuwa nabii aliyeweza kufanya mambo makubwa sana lakini ulipokuja mtihani wa taabu alikata tamaa sana alitishiwa tu na malikia Yezebeli kuwa atamkata kichwa, Eliya alikimbia mbio aligoma hata kula na maombi yake yakawa anataka tu afe ona

 

1Wafalme 19: 2-4 “Ndipo Yezebeli akampelekea Eliya mjumbe, kusema, Miungu wanifanyie hivyo na kuzidi, nisipokufanya roho yako kesho, panapo wakati huu, kama roho ya mmojawapo wa hao. Naye alipoona hayo, aliondoka, akaenda aihifadhi roho yake, akafika Beer-sheba, mji wa Yuda, akamwacha mtumishi wake huko. Lakini yeye mwenyewe akaendelea katika jangwa mwendo wa siku moja, akaenda akaketi chini ya mretemu. Akajiombea roho yake afe, akasema, Yatosha; sasa, Ee Bwana, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu.”

 

Unaweza kumcheka Eliya ukisoma kisa kizima cha ushujaa wake na mkwara kutoka kwa mwanamke, lakini zingatia kila mwanadamu ana kiwango chake cha mwisho cha uvumilivu huyu alipotumiwa ujumbe tu kuwa kesho nitakuua naapa kwa miungu yangu, Tayari aliogopa na kukimbia na kugoma kula na kulalal chini ya mti akisubiri kufa, Mungu ndiye anayetoa maisha na ni mpaka kusudi lake litimie ndani yetu Mungu hakukubali ombi hili, n ahata kifo kiliahirishwa kwake, hivyo usijiombee kufa wala usiogope

 

5.       Usiogope – kila wakati wito wa Mungu katika maandiko unatutaka tusiogope hii ni kwa sababu Mungu yuko pamoja nasi hata katika wakati tukiwa na hisia za kuwa peke yetu Mungu ni Roho kuna wakati anaruhusu tuhisi uwepo wake hivyo hata miili yetu inahisi kuwa yuko pamoja nasi lakini kuna wakati hatoruhusu tumhisi, tunahitaji Imani wakati huo, tunahitaji kutupilia mbali hofu, tunahitaji kutembea katika shuhuda zake tu tuikijua kuwa yupo na anashughulika na maisha yetu hata kama tunaiona mauti kumbuka yupo!

 

Zaburi 23:1-6 “Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika. Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.”

 

Hitimisho:

 

Mungu hatakusaliti – Mwandishi wa zaburi hii ya 88 ni HERMAN Mwana wa KORAH huyu ndiye mwandishi wa zaburi hii ni zaburi miongoni mwa zaburi zilizokuwa zinaimbwa wakati watu wanapopanda kwenda Hekaluni zinaitwa zaburi za KUPANDIA hii ndio zaburi chungu zaidi kuliko zote wayahudi waliita zaburi ya GIZA iliimbwa kwa machozi na watu waliokuwa wanahitaji msaada wa Mungu wakiwa hawajui maisha yatakuwaje, wakiwa na maswali mengi yasiyo na majibu wakifikiri kuwa Mungu pia amewaacha HERMAN anatuwakilisha sisi wote tunaweza kulalamika nadhani mimi ni mlalamikaji zaidi kuliko hata ninyi wasomaji wangu, nampenda Mungu lakini wakati mwingine simuelewi anaponipitisha katika magumu namuona kama ameniacha namuona kama amenisaliti, HERMAN mimi na wewe msomaji wangu tunamuona kama Mungu ametusaliti, na rafiki yetu ni giza tu nafsi imetupwa, maombi hayajibiwi, wanaotujua wametuacha, fadhaa zimetujaa? Je umewahi kufikia hali kama hii? Herman mwandishi wa zaburi hii Mwana wa kora aliifikia akidhani Mungu amemsaliti,

 

Zaburi 88:14-18 “Bwana, kwa nini kuitupa nafsi yangu, Na kunificha uso wako? Nateswa mimi hali ya kufa tangu ujana, Nimevumilia vitisho vyako na kufadhaika. Hasira zako kali zimepita juu yangu, Maogofyo yako yameniangamiza. Yamenizunguka kama maji mchana kutwa, Yamenisonga yote pamoja. Mpenzi na rafiki umewatenga nami, Nao wanijuao wamo gizani.”

 

Mungu ni mwaminifu katika ahadi zake kwa vyovyote vila haitakuja itokee akuache na asijali kuhusu maisha yako na yangu yeye hataweza kutusaliti wala kutuacha gizani yuko pamoja nasi hata ukamilifu wa Dahari, atatutia nguvu, atatusaidia na atatushika mkono na kutuinua hii ni ahadi yake na ndivyo itakavyokuwa katika maisha yetu siku zote Amen

 

Isaya 41:10 . “usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.”

 

Na. Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Rev. Innocent Mkombozi Kamote.         



Hakuna maoni: