Jumapili, 26 Novemba 2023

Umuhimu wa kufanya Uinjilisti:


Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”              




Utangulizi:

Ni muhimu kujikumbusha kwamba moja ya agizo muhimu sana kwa wakristo wote duniani kutoka kwa Bwana wetu Yesu Kristo ni kuhakikisha kuwa watu wote duniani wanaisikia habari njema yaani injili, watu wengi sana huwa wanajisahaulisha kuhusu jambo hili la Muhimu, nimetumia miaka mingi sana kuwatia moyo, na kuwajenga kiimani na kuwafunulia neno la Mungu kama Mwalimu wa neno lake, lakini nitakuwa mchoyo wa fadhila kama nitasahau kukazia jambo hili  la Muhimu, najua kazi niliyokuwa nikiifanya ni sehemu ya injili lakini nasukumwa sana kuzungumzia injili kwa sababu kuna maonyo ya kimaandiko kwetu endapo tutaacha kusema kuhusu habari njema, kwa sababu ni sharti yaani ni lazima kuihubiri injili

1Wakorintho 9:16-17 “Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili! Maana nikiitenda kazi hii kwa hiari yangu nina thawabu; ila ikiwa si kwa hiari yangu, nimeaminiwa uwakili.”

Kazi ya kuhubiri injili imetoka katika agizo la kiongozi mkubwa zaidi Duniani na ni kazi ya Muhimu, kanisa yaani watu wa Mungu hawapaswi kwa namna yoyote kupuuzia agizo lake, pamoja na kuwajibishwa kwa watu wasiohubiri injili, lakini kuna madhara makubwa sana kwa ulimwengu kuharibiwa na kazi za shetani, mmomonyoko wa uadilifu, kukosa Nuru, kukosa chumvi, na kuingiliwa kwa ulimwengu na falsafa za giza zilizo kinyume na injili zitaenea na kuifanya dunia kuingia gizani kinyume kabisa na namna Yesu anavyotutarajia tufanye! Endapo tuntutapuuzia swala la kuihubiri injili,  Kwa hiyo tuna wajibu wa kuihubiri injili na hii ni kazi  ya kila muungwana aliyeamini  duniani!

Tutajifunza somo hili umuhimu wa kuihubiri injili kwa kuzingatia vipengele vinne  muhimu vifuatavyo:-

·         Maana ya neno injili.

·         Umuhimu wa kufanya uinjilisti.

·         Madhara ya kuacha kuhubiri injili.

·         Namna nyepesi ya kuifikisha injili


Maana ya neno Injili.

Neno injili limetokana na neno la kiingereza Evangelism ambalo kwa kiyunani ni EUANGELIUM  na kwa kilatini ni GOSPEL ambalo maana yake (Good Story) au (Good News)kwa Kiswahili Habari njema, au kuwaeleza watu habari nzuri, habari za matumaini au habari za kutia moyo.

Mfano Kama watu walikuwa na njaa mbaya sana kiasi cha kula kichwa cha punda au kiasi cha wanawake kula watoto wao kwa zamu, kisha ghafla watu hao wakatangaziwa kuwa mahindi, au ngano au unga au chakula kitapatikana kwa bei nafuu sana basi hiyo ni habari njema angalia mfano  ona

2Wafalme 6:24-30 “Ikawa baada ya hayo, Ben-hadadi mfalme wa Shamu akakusanya majeshi yake yote, akakwea akauhusuru Samaria. Njaa ikawa kuu huko Samaria; na tazama, wakauhusuru, hata kichwa cha punda kikapata kuuzwa kwa vipande themanini vya fedha, na kibaba cha mavi ya njiwa kwa vipande vitano vya fedha. Ikawa mfalme wa Israeli alipokuwa akipita ukutani, mwanamke mmoja akamwita akisema, Unisaidie, bwana wangu, mfalme. Akasema, Bwana asipokusaidia, nikusaidieje mimi? Ya sakafuni, au ya shinikizoni? Mfalme akamwambia, Una nini? Akajibu, Mwanamke huyu aliniambia, Mtoe mtoto wako, tumle leo, na mtoto wangu tutamla kesho. Basi, tukamtokosa mtoto wangu, tukamla; nikamwambia siku ya pili, Mtoe mtoto wako, tumle; naye amemficha mtoto wake. Ikawa, mfalme alipoyasikia maneno ya huyo mwanamke, aliyararua mavazi yake; (naye alikuwa akipita juu ya ukuta;) na watu wakaona, na tazama, alikuwa amevaa magunia ndani mwilini mwake.”

2Wafalme 7:1-11 “Elisha akasema, Lisikieni neno la Bwana; Bwana asema hivi, Kesho panapo saa hii, kipimo cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, langoni pa Samaria. Basi yule akida, ambaye mfalme alikuwa akitegemea mkono wake, akamjibu yule mtu wa Mungu, akasema, Tazama, kama Bwana angefanya madirisha mbinguni, je! Jambo hili lingewezekana? Akamwambia, Angalia, wewe utaliona kwa macho yako, lakini hutakula. Basi walikuwapo watu wanne wenye ukoma, penye lango la mji; wakasemezana, Mbona tunakaa hapa hata tufe? Tukisema, Tutaingia mjini, mjini mna njaa, nasi tutakufa humo; nasi tukikaa hapa, tutakufa vile vile. Haya! Twende tukaliendee jeshi la Washami; wakituhifadhi hai tutaishi; wakituua, tutakufa tu. Basi wakaondoka kabla ya mapambazuko, ili waende mpaka kituo cha Washami; na walipofika mwanzo wa kimo cha Washami, kumbe! Hapana mtu. Kwa maana Bwana alikuwa amewasikizisha Washami kishindo cha miendo ya magari, na kishindo cha farasi, kama kishindo cha jeshi kubwa; wakaambiana, Tazama, mfalme wa Israeli amewaajiri wafalme wa Wahiti, na wafalme wa Wamisri, waje wapigane nasi. Kwa hiyo wakaondoka, wakakimbia kungali giza bado, wakaziacha hema zao, na farasi zao, na punda zao, na kimo chao vile vile kama kilivyokuwa, wakakimbia wapate kujiponya nafsi zao. Basi wale wenye ukoma walipofika mwisho wa kituo, waliingia katika hema moja, wakala, na kunywa, wakachukua fedha, na dhahabu, na mavazi, wakaenda wakavificha; wakarudi, wakaingia katika hema ya pili, vile vile wakachukua vitu, wakaenda, wakavificha. Ndipo wakaambiana, Mambo haya tufanyayo si mema; leo ni siku ya HABARI NJEMA, na sisi tunanyamaza; mkingoja hata kutakapopambazuka, madhara yatatupata; basi twende tukawaambie watu wa nyumba ya mfalme. Basi wakaenda, wakawaita mabawabu wa mji; wakawaambia, Tulifika kituo cha Washami, na tazama, hapana mtu ye yote huko, wala sauti ya mtu, ila farasi wamefungwa, na punda wamefungwa, na hema zao kama walivyoziacha. Na mabawabu wakaita wakawaambia watu wa nyumba ya mfalme.”

Unaweza kuona ukilinganisha hapo juu habari mbaya ya njaa mbaya iliyokuwepo zamani za Nabii Elisha na tangazo la Nabii Elisha na muujiza wa wale wakoma waliovumbua kuweko kwa chakula uvumbuzi kuhusu kuweko kwa chakula katika Samaria wakati kukiwa na njaa mbaya iliyopelekea wanawake kula watoto ilikuwa ni habari njema!

Ulimwengu tulio nao umeharibika, shetani na malaika zake wameiharibu dunia, uadilifu wa mwanadamu umeathiriwa, uhusiano wa Mungu na mwanadamu umeharibika, wanadamu wote tunafahamu kuwa tumeharibikiwa hatustahili tena kuwa na uhusiano na Mungu, tunastahili hukumu ya Mungu, tunastahiki kifo tunastahili adhabu, tunastahili kutupwa motoni, tunastahili kuharibiwa, tunastahili kukataliwa hatufai kwa sababu hakuna mtu mwenye nia ya kutafuta uhusiano mwema na Mungu tumeharibika tumeoza wanadamu wote kama yasemavyo maandiko ona

Warumi 3:10-12 “kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja.”

Katika mazingira kama haya ya haribiko kubwa la mwanadamu anapotokea Mtu anatangaza kuwa Mungu amesamehe maovu yetu yote kwa sharti  moja tu na  sharti hilo ni kumuamini Mwanaye ambaye yeye alimtoa aadhibiwe yeye kwa niaba yetu pale msalabani na kuwa kazi tunayotakiwa sisi ni kuamini tu, na kuamini ni kukubali tu na kukiri na kushukuru na kwa kuamini huko hatutahukumiwa na tunahesabika kuwa watoto wa Mungu tukipewa haki sawa na mtoto wake aliyeishi maisha ya haki hizo sasa zinakuwa ni habari njema kwetu! unaona

Yohana 3:16-18 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.  Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.”

Unaona sasa kupitia kazi hii aliyoifanya baba kwa upendo wake tukimuamini mwana wake tumeokolewa, tunasamehewa hatuhukumiwi hizi ni habari njema ambazo kila mwanadamu zinapaswa kumfikia na ni kwa sababu ya haya Kristo alikuja ulimwenguni na kutoka katika kuamini tunasimama imara na kuokolewa, na kusamehewa na kubadilishwa mwenendo wa tabia na maisha yetu kwa neema tu kupitia nini kupitia kazi aliyoifanya Yesu pale msalabani

1Wakorintho 15:1-4 “Basi, ndugu zangu, nawaarifu ile injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri isipokuwa mliamini bure. Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko;”

Umuhimu wa kufanya uinjilisti.

Kusudi kubwa la Mungu kumtoa mwana wake wa pekee kuja ulimwenguni ni ili apate kuwaokoa wanadamu watakaomwamini, na wale wote ambao hawataamini watahukumiwa

Yoahana 3:16-18 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.  Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.”

Sasa ili watu waweze kukolewa ilikuwa ni lazima waisikie injili na wakiisha kuisikia injili, waiamini na wakiamini kwa maneno na vitendo yaani kubatizwa na kuwa wanafunzi wa Yesu na kusimama katika imani waokolewe, kwa hiyo tunajifunza ya kwamba watu hawawezi kuamini mpaka wasikie tena wasikie habari za Yesu

Marko 16:15-16 “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.  Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.”

Habari za Yesu Kristo ni lazima zihubiriwe kwa jamii ya watu wote ulimwenguni, kama watu wanamtii Yesu kristo hili ni agizo la muhimu mno, na Mungu anataka tuliangalie kwa jicho la kipekee Yesu mwenyewe hapa anasema aaminiye ataokoka asiyeamini Atahukumiwa ni Dhahiri kuwa hukumu ipo na kama hatutaki watu waangukie katika hukumu ya Mungu basi hatuna budi kuihubiri injili na kuhakikisha watu wote duniani na kila jamii na taifa na kabila na lugha wanafikiwa na injili, wajibu huu wa kuihubiri injili ni wa watu wote na sio watumishi pake yao, Nyakati za kanisa la kwanza walihubiri kila mahali, na walitimiza wajibu wao sisi nasi hatuna budi kufanya hivyo ona

Matendo 8: 4-5 “Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno. Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo.”

Ikiwa watu wa Karne ya kwanza waliweza kuihubiri injili kwa miguu yao, kwa majahazi, kwa punda na farasi, wakati wa leo tunaweza kuwafikiwa watu kwa njia nyingi na za rahisi zaidi, tunaweza kuifanya kazi hii kwa wepesi na kuwafikiwa watu wengi sana Duniani, shime kila mahali nawaomba wakristo tuamke na kuieneza habari njema ya Bwana wetu Yesu Kristo kwani mavuno yako tayari na ni sisi tu ambao tunaweza kuueneza moto wa injili kwa njia zozote zile ambazo Mungu ametupa katika karne hii, Tunaweza pia kutoa fedha zetu, kununua vyombo vya injili, vyombo vya usafiri, vyombo vya kuhubiria ndani na vile vya kuhubiria nje, kujenga makanisa, kununua mahema, kufadhili vipindi vya redio nan television zinazohubiri injili pamoja na fadhila nyingine za aina nyingi sana za kuhakikisha kuwa tunamtaja na kumueneza Yesu kwa kila mwanadamu, Baraka kubwa sana italifunika kanisa na taifa na jamii yoyote ile itakayotumia kila njia kuhakikisha kuwa injili inawafikia watu wote, hili ni agizo la Bwana wetu Yesu kwa kanisa lake kila mahali duniani, watu wa Mungu wako tayari na wana kiu lakini wanalisubiria kanisa liamke na kuupeleka moto wa injili haleluyaaa

Warumi 10:14-17 “Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri? Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema! Lakini si wote walioitii ile habari njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu? Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.”

Kuhubiri injili ni sawa na kuunga umeme katika miji yote isiyo na umeme, ni kuwasha nuru maeneo yote yenye giza, kama hatutaihubiri injili watu wataamini mambo ya giza, watafuata falsafa nyingine, watatambikia mizimu, wataabudu dini za uongo, watafuata mafundisho ya imani nyingine mbaya na zisizo na ustaarabu, wote tumekuwa mashahidi kuwa kila mahali injili ilipoingia kumekuwa na maendeleo makubwa ya kitaaluma, kiuchumi na kiuadilifu na ustaarabu na maeneo mengi ambayo injili haijafika kumekuwapo giza Kuu, kokote Yesu anakopelekwa ni dhahiri kuwa nuru kubwa iliwazukia watu wa jamii hiyo;-

Mathayo 4:13-16 “akatoka Nazareti, akaja akakaa Kapernaumu, mji ulioko pwani, mipakani mwa Zabuloni na Naftali; ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, Njia ya bahari, ng'ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa, Watu wale waliokaa katika giza Wameona mwanga mkuu, Nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti Mwanga umewazukia.”

Kwa msingi huo mpendwa hatuna budi kuipeleka nuru ya Yesu, kwa kuhakikisha kuwa tunawaeleza watu wote habari njema, acha kuhisi kuwa aaa siku hizi watu wanasikia bhana, hapana fanya wajibu wako wa kuihubiri injili na kama mtu yuko kimya muhubirie injili mpaka aseme mimi ni muamini mwenzako, eee kama umekaa kimya tutajuaje kuwa umeokoka tayari? Lihubiri neno.  Kumbuka kuwa katika wakati tulio nao ni rahisi zaidi kuhubiri injili

Tuige mifano ya watu mbalimbali ambao waliihubiri injili, Billy Graham anasemekana kuwa ndiye mwanadamu aliyeihubiri injili kwa watu wengi sana kiasi cha kuitwa muhubiri mkubwa wa karne ya 20, alihubiri mikutano mbalimbali ya ndani na nje huku mahubiri yake yakirushwa katika redio na television mbalimbali duniani  na matokeo yake Grahamu amekuwa Muhubri ambaye amehubiria watu wengi zaidi kuliko wote katika historia ya Ukristo na kwa rekodi za maafisa wake watu wapatao milioni 3.2 waliwahi kumpiokea Yesu katika mahubiri yake alihubiri injili katika maisha yeke tangu mwaka 1947 – 2005 alipostaafu. Amehubiria zaidi ya watu milioni 215 na amehubiri katika inchi zaidi ya 185, kwa mikutano zaidi ya 400 yeye anatupa changamoto leo kufanya kila tuwezalo kulifanya kuhakikisha kuwa dunia inajawa na injili, hakuwa na mbwembwe, alihubiri kwenye madhabahu akiwa na uso mkali na sauti yenye mamlaka akiwa na ushawishi mkubwa wa kuwafanya watu watubu na maelfu ya watu walikuwa wakitubu katika kila mkutano wake, alifariki Tarehe 21 February 2018 akiwa na umri wa miaka 99  

Madhara ya kuacha kuhubiri injili.

Kutokuihubiri injili ni UASI ni DHAMBI ni kwenda kinyume na maagizo ya Mungu!  Kwa sababu kwa namna moja ama nyingine tutakuwa tu mechangia uharibifu kwa dunia ambayo kama ingesikia habari njema Yesu angewaokoa, Nyakati za agano la kale Mungu alipowatuma manabii kufanya kazi ya kuonya na manabii hao walionywa pia kuwa wasiposema Mungu atawahukumu wao kwa sababu wameacha kuwa wasemaji kwa niaba ya Mungu,

Ezekiel 3:18 -19. “Nimwambiapo mtu mbaya, Hakika utakufa; wewe usimpe maonyo, wala husemi na huyo mtu mbaya ili kumwonya, kusudi aache njia yake mbaya na kujiokoa roho yake; mtu yule mbaya atakufa katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako. Lakini ukimwonya mtu mbaya, wala yeye hauachi ubaya wake, wala njia yake mbaya, atakufa katika uovu wake; bali wewe umejiokoa roho yako.”   

Ezekiel 33:7-9 “Basi wewe, mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi kwa nyumba ya Israeli; basi ulisikie neno hili kinywani mwangu, ukawape maonyo yangu.  Nimwambiapo mtu mbaya, Ewe mtu mbaya, hakika utakufa, nawe husemi neno la kumwonya mtu huyo, aiache njia yake, mtu mbaya huyo atakufa katika uovu wake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako. Walakini ukimwonya mtu mbaya kwa sababu ya njia yake, kusudi aiache; wala yeye asiiache; atakufa huyo katika uovu wake, lakini wewe umejiokoa roho yako.”             

Neno la Mungu bado linatuonya ya kuwa tunawajibu wa kuwaeleza watu habari njema, mtazamo unaweza kuwa tofauti na wakati wa Agano la kale ambapo manabii walipeleka maonyo tu na kusisitiza toba, lakini ujumbe wetu sisi ni mwepesi sana ukilinganisha na nyakati za agano la kale sisi tunapaswa kuwaeleza watu habari njema na sio za vitisho, kuwaeleza watu habari za upendo wa Yesu, habari za msamaha wa dhambi bure na kwa neema tu, Habari ya kuwa Yesu alisulubiwa akafa akazikwa kwa niaba yetu nao wataokolewa, lakini kwa kuwa Mungu habadiliki kama hatutaihubiri injili tunakuwa tumewafungia watu malango ya ufalme na tutawajibika na kuhukumiwa kwa kutokumtii Mungu kwa kufikisha agizo lake, ni nyepesi sana kwa sababu sio sisi tunaookoa anaeokoa ni yeye mwenyewe lakini sisi ni wajumbe wake, Kila kanisa kila mkristo aliye hai ana wajibu wa kuihubiri injili na tusipofanya hivyo tutawajibishwa na kuhukumiwa kama ilivyokuwa maonyo ya Mungu kwa Ezekiel na Paulo mtume

1Wakorintho 9:16-17 “Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili! Maana nikiitenda kazi hii kwa hiari yangu nina thawabu; ila ikiwa si kwa hiari yangu, nimeaminiwa uwakili.”

Ndani ya habari njema kuna uweza na nguvu za Mungu zenye kuokoa kwa hiyo wajibu wetu ni kuipeleka ni kusema ni kutangaza, muhubiri Yesu waeleze watu habari za Yesu na uweza wa kuokoa ni wake naye atafanya !.

Warumi 1:16- “Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia.”

Namna nyepesi ya kuifikisha injili

Muhubiri Kristo!, hubiri kazi yake ya huruma aliyoifanya pale msalabani, nyakati za kanisa la kwanza hawakuwa na maneno mengi zaidi ya kuthibitisha kuwa Yesu aliteswa kwaajili yetu alikufa na siku ya tatu akafufuka, huyu ni Mwana wa Mungu, huyu anaokoa, huyu anasamehe dhambi, bila kujali kuwa dhambi zetu zilikuwa nyekundu kama damu, yeye alijiadhibu mwenyewe msalabani kwaajili yetu.

Matendo 8: 4-5 “Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno. Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo.”

Zingatia misingi minne tu wakati unapoisema habari njema kwa njia rahisi ya kumuelezea mtu mmoja mmoja habari za kristo

1.       Wote tumefanya dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu Warumi 3:23-24 “kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu;”

2.       Afichaye dhambi zake hatafanikiwa aziungamaye na kuziacha atapata Rehema Mithali 23:13-14 “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema. Mwanadamu mwenye kicho yu heri sikuzote; Bali mshupavu wa moyo ataangukia madhara.”            

3.       Tukiziungama dhambi zetu yeye ni mwaminifu atatusamehe 1Yohana 1;9Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.”         

4.       Mwamini Bwana Yesu na utaokoka wewe pamoja na nyumba yako  yaani Familia yako na jamaa zako Matendo 16: 30-32. “kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako. Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake.”

Ikiwa mtu atakubali kujitambua kuwa sisi wote ni wakosaji, na kuwa tunahitaji rehema za Mungu, na kuwa rehema hizo zinapatikana kwa kazi aliyoifanya Yesu pale msalabani na kuwa wajibu wetu ni kuamini tu, mtu huyo akikubali kuamini atasema maneno haya

Bwana Yesu ninakushukuru kwa kuwa nimesikia neno lako, na nimeamini kazi uliyoifanya pale msalabani, nakushukuru kwa kuwa wewe ni bwana na kwa upendo wa Mungu umeniokoa na kunisamehe mimi nisiyestahili, nakuamini wewe kwa msamaha wa uovu wangu wote Amen

Kwa sala hii mtu huyo atakuwa amemuamini Bwana na atapaswa kuwa mwanafunzi wa Yesu kwaajili ya mafundisho na maelekezo mengine zaidi, Amen

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!.

Hakuna maoni: