Jumanne, 14 Novemba 2023

Wafariji wenye kutaabisha.


Ayubu 16:1-6 “Ndipo Ayubu akajibu, na kusema, Nimesikia maneno mengi mfano wa hayo; Ninyi nyote ni wafariji wenye kutaabisha. Je! Maneno yasiyo faida yatakuwa na mwisho? Au, kuna nini kinachokukasirisha, hata ukajibu? Mimi nami ningeweza kunena kama ninyi; Kama roho zenu zingekuwa mahali pa roho yangu, Ningeweza kutunga maneno juu yenu, Na kuwatikisia ninyi kichwa changu. Lakini ningewatia nguvu kwa kinywa changu, Na utuzo wa midomo yangu ungetuliza. Nijapokuwa nanena, huzuni yangu haitulizwi; Nijapokuwa najizuia, nimepunguziwa kitu gani?


Utangulizi:

Kitabu cha Ayubu ni moja ya kitabu kilichoandikwa kwaajili ya kutoa majibu kwa ulimwengu kuhusu falsafa ya mateso, kwanini maisha ya mwanadamu hukutana na changamoto za aina mbalimbali, lakini sio hivyo tu kujibu pia swali kwanini wenye haki nao wanateseka?  Ayubu alikuwa mtu mwenye haki mbele za Mungu, hata hivyo alikumbana na mateso makubwa ya aina mbalimbali, ambayo aliyavumilia na mwisho wake ukawa mwema, Ayubu leo amekuwa mfano mzuri na mwema wa kuigwa katika swala zima la kuvumilia mateso na kuonyesha wema wa Mungu kwetu pale tunapovumilia, Mungu ni mwingi wa rehema na mwenye huruma

Yakobo 5:10-11 “Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu. Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.”

Pamoja na mapito aliyokuwa akiyapitia Ayubu lakini vilevile Maandiko yanatufundisha kuwa wakati tunapopitia mambo magumu kwa kawaida wanakuwepo watu wanaokuja katika maisha yetu na kutoa ushauri/kufariji au kusema hili au lile kutokana na mapito tunayoyapitia wakati mwingine watu hao wakiwa na nia njema na wakati mwingine wakiwa hawajui wanachoweza kusema kuhusiana na mapito yako kama kiko sahihi au la kama ni mapenzi ya Mungu au la,  na wakati mwingine sio rahisi kujua siri ya mapito anayoyapitia mtu isipokuwa Mungu mwenyewe, wakati Ayubu alipokuwa akipitia wakati Mgumu neno linatueleza kuwa alitembelewa na rafiki zake watatu ambao walikuja kwa kusudi la kumfariji kutokana na mapito aliyokuwa anayapitia ona:-

 Ayubu 2:11-13 “Basi ikawa hao rafikize Ayubu watatu walipopata habari ya mabaya hayo yote yaliyomfikilia, wakaja kila mtu kutoka mahali pake; nao ni Elifazi Mtemani, na Bildadi Mshuhi, na Sofari Mnaamathi; wakapatana pamoja ili waende kumlilia Ayubu na kumtuliza moyo. Basi walipovua macho yao, nao wakali mbali, wasimtambue, wakainua sauti zao na kulia; kila mmoja akararua joho yake, wakarusha mavumbi juu ya vichwa vyao kuelekea mbinguni. Kisha wakaketi nchi pamoja naye muda wa siku saba, mchana na usiku, wala hapana mmoja aliyenena naye neno lo lote; kwa maana waliona ya kuwa mashaka yake aliyo nayo ni makuu mno.”                         

Elifazi Mtemani, Bildadi Mshuhi na Sofari mnaamathi walikuwa na nia njema na nzuri kabisa ya kumfariji Ayubu na mioyo yao na matendo yao yanadhihirisha kuwa walikuwa wako sahihi katika kutafuta namna ya kumfariji ndugu yao kutokana na mambo magumu aliyoyapitia, hata hivyo katika namna ya kushangaza sana baada ya wao kutoa hoja mbalimbali Ayubu aliwaita watu hao au rafiki zake kuwa ni WAFARIJI WENYE KUTAABISHA   angalia hapa Ayubu 16:2 “Nimesikia maneno mengi mfano wa hayo; Ninyi nyote ni wafariji wenye kutaabisha.” sasa swali kubwa kwetu na macho yetu ni kuliangalia jambo hili kwa kina na mapana na marefu kuwa wafariji wenye kutaabisha ni watu wa namna gani ?  na ni vipi tunaweza kukabiliana nao wanapojitokeza katika maisha yetu, na kama sisi nasi tunataka kuwa wafariji na washauri wa wengine ni tahadhari gani tunapaswa kuzizingatia. Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Maana ya Wafariji wenye kutaabisha

·         Jinsi Mtu anavyoweza kuwa mfariji mwenye kutaabisha

·         Namna ya kujiepusha na wafariji wenye kutaabisha au kuwa wafariji wenye kutaabisha

Maana ya Wafariji wenye kutaabisha:

Ayubu 16:1-6 “Ndipo Ayubu akajibu, na kusema, Nimesikia maneno mengi mfano wa hayo; Ninyi nyote ni wafariji wenye kutaabisha. Je! Maneno yasiyo faida yatakuwa na mwisho? Au, kuna nini kinachokukasirisha, hata ukajibu? Mimi nami ningeweza kunena kama ninyi; Kama roho zenu zingekuwa mahali pa roho yangu, Ningeweza kutunga maneno juu yenu, Na kuwatikisia ninyi kichwa changu. Lakini ningewatia nguvu kwa kinywa changu, Na utuzo wa midomo yangu ungetuliza. Nijapokuwa nanena, huzuni yangu haitulizwi; Nijapokuwa najizuia, nimepunguziwa kitu gani?

Moja ya swali muhimu la kujiuliza hapa ni kwanini Ayubu anawaita watu hawa kama wafariji wenye kutaabisha japo tunaweza kuwa na ufahamu kuwa walikuwa na nia nzuri na walijitahidi kwa kadiri ya hekima waliyokuwa nayo, kumtia moyo lakini mwisho wa yote walikuwa ni wafariji wenye kutaabisha na Mungu aliwakemea kuwa hawakunena sawasawa na Mungu wala sawasawa na Mtumishi wake Ayubu na hivyo walitakiwa kutoa dhabihu kuomba radhi kwa uovu wao!

Neno wafariji wenye kutaabisha kimsingi katika biblia ya kiingereza Mstari wa pili ambao ni wa msingi katika somo letu unasomeka hivi

I have heard many such things MISERABLE COMFORTERS  are ye all  neno MISERABLE   kwa kiibrania ni “AMAL” ambalo maana yake ni wenye kulaumu, wenye kukutendea vibaya, wenye unyanyasaji, wenye kuchosha, wenye kuumiza, wenye kuhuzunisha, wenye maumivu, wenye kuogopesha, wenye uovu, wenye kuchosha, wenye kutia uvivu, wenye kukatisha tamaa, wenye kuvunja moyo, wenye uovu, wasiyo na kweli, wenye kupotosha.  Neno hilo AMAL limetumika mara 55 Katika Biblia na katika mistari tofauti 54  

Kwa msingi huo Ayubu alikuwa anamaanisha kuwa ameshawasikia watu wengi kama hawa na kuwa katika faraja na ushauri waliokuwa wakijaribu kuutoa walikuwa wametoka nje ya makusudi na mpango wa Mungu kwa sababu hiyo badala ya kumfariji, walikuwa wakizungumza tu na kwa kweli walikuwa wametoka pia nje ya kusudi na ukweli kuhusu mtazamo wa Mungu, kwa ujumla walikuwa nje ya kweli ya Mungu, tena wala walikuwa hawawakilishi mfumo na sifa za Mungu, kwa hiyo Ayubu alipowasikiliza aliona wazi kuwa wanamkosea Mungu mno, walikuwa wanahisi tu jambo Fulani kuhusu utendaji wa Mungu wakati wa majaribu ya mtu lakini haikuwa kweli ya Mungu wala kusudi la Mungu na pia walikuwa wakimshutumu Mtumishi wa Mungu Ayubu kwamba ana kesi ya kujibu katika mabaya aliyokuwa anayapitia n ahata watoto wake waliokufa vibaya walikuwa na makosa Fulani na kwa sababu hiyo ingawa walikuja kwa wakati kwa kusudi la kumfariji na kumshauri  Ayubu walijikuta wanapotosha, wanamuumiza zaidi, wanamvunja moyo, wananena uovu, wanasema yasiyo kweli, wanamchosha na wanamuumiza hali kama hii inaweza kuwepo kwa watu wengi wanaotuzunguka katika nyakati zetu hata siku za leo!

Ayubu alikuwa amepitia majaribu makubwa na mazito mno kiasi cha kupatwa na mashaka makubwa sana, rafiki zake waliojitokeza kumfariji badala ya kumpunguzia maumivu aliyokuwa akiyapitia wao waliongeza huzuni na maumivu mtazamo wao kuhusu majaribu ulikuwa ukimtaka Ayubu akiri na kutubu dhambi zake ili Mungu aondoe adhabu aliyoiweka juu yake

Ayubu 11:14-17. “Ikiwa una uovu mkononi mwako, uweke mbali nawe, Wala usikubali upuzi kukaa hemani mwako; Hakika ndipo utakapopata kuinua uso pasipo ila; Naam, utathibitika, wala hutakuwa na hofu; Kwa kuwa utasahau mashaka yako; Utayakumbuka kama maji yaliyokwisha pita; Na maisha yako yatakuwa meupe kuliko adhuhuri; Lijapokuwa ni giza, litakuwa kama alfajiri.”

Ayubu 22:4-7 “Je! Ni kwa wewe kumcha yeye anakukemea? Na kuingia hukumuni nawe? Je! Uovu wako si mkuu? Wala maovu yako hayana mwisho. Kwa kuwa umetwaa dhamana kwa nduguyo bure, Na kuwavua nguo zao walio uchi. Hukumpa maji ya kunywa huyo aliyechoka, Nawe umemnyima chakula huyo mwenye njaa.”

Sio jambo la kushangaza hata katika siku zetu leo, pale tunapopatwa na mapito magumu, majaribu magumu na mitihani ya aina mbalimbali, wafariji wengi na washauri hukimbilia katika hatima ya kusema kuwa ni kwa sababu tu mefanya dhambi, au kuna kosa kubwa sana ambalo mtu amelifanya  na sio hivyo tu hata katika nyakati zetu leo watu wengi sana hufikiri kuwa mtu akiwa na mafanikio ya mwilini basi yuko vizuri na Mungu na mtu akiwa na majanga basi kutakuwa kuna shida katika mahusiano yake na Mungu  fikira za namna hii sio tu zinawakosesha amani wanaopita katika mapito bali pia zinaharibu mtazamo wa utendaji wa Mungu na kupotosha ukweli kuhusu utendaji wa Mungu!, badala ya watu kushauri vema na kukujenga wanakubomoa na kuichoma nafsi yako kiasi ambacho wanataka kukugombanisha wewe na Mungu, Wafariji wa namna hii huongezea Msiba wakati wa matatizo badala ya kukusaidia hao ndio wanaitwa wafariji wenye kutaabisha!

 

Jinsi Mtu anavyoweza kuwa mfariji mwenye kutaabisha

1.       Mtu anayefikiri kila mwanadamu anayeteseka ni kwa sababu amefanya dhambi -  Mfariji mwenye kutaabisha ni mtu awaye yote anayedhani kuwa kila taabu anayoipitia mtu ni kwa sababu aidha mtu huyo amefanya dhambi au wazazi wake, haya ndio yalikuwa mawazo ya wanafalsafa waliokwenda kumshauri na kumfariji Ayubu wao walikuwa na dhana inayoathiri wengi hata katika nyakati za leo, miongoni mwa watu wengi sana waliookoka leo wakiona mtu aliyeokoka anapatwa na mabaya wanadani kuwa mtu huyo ni mbaya au kuna dhambi ameifanya hajaitubia, au Mungu anashughulika naye anamuadhibu aina hii ya dhana ilikuwepo pia miongoni mwa wanafunzi wa Yesu na Yesu alikuwa tofauti na mtazamo wao? 

 

Yohana 9:1-3 “Hata alipokuwa akipita alimwona mtu, kipofu tangu kuzaliwa.  Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu? Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake.”

 

2.       Mtu anayefikiri kuwa kila mwanadamu anayeteseka anavuna alichokipanda – Ni ukweli ulio wazi kuwa maandiko yanazungumza juu ya kuwepo kwa kanuni ya kupanda na kuvuna

 

Wagalatia 6:7-9 “Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho.”

 

Wako watu duniani ambao wanadhani ya kuwa unapopita katika mapito Fulani basi ni kwa sababu ulipanda au kuna mtu kwenye ukoo wenu au baba zako alipanda ubaya Fulani na sasa unateseka kwa sababu unavuna au wewe ulifanya uovu Fulani na sasa unakujilia juu yako na wanaweza kumuhusisha Mungu katika jambo hilo kwamba Mungu analeta mabaya juu yako kwa sababu ya ubaya Fulani ulioutenda hii pia ilikuwa falsafa ya rafiki zake Ayubu walipokuja kumfariji, na watu wengi leo wana mtazamo kama huo wa KARMA lakini sio kila mapito yanatokana na Karma au mavuno Fulani.

 

3.       Mtu anayefikiri kuwa  wewe hufanikiwi au hupati muujiza kwa sababu huna Imani -  wako watu wengi sana ambao wakati mwingine wanaweza kuhukumu wenzao kuwa wewe hupati muujiza wako au Mungu hakufanyii jambo Fulani kwa sababu huna Imani, wakati wote wao wanafikiri tu kuwa Imani yao ndio imewasaidia kufikia hali waliyoifikia na wale wasio na imani wamebaki na michangamoto yao, falsafa na dhana ya namna hii pia inamuweka Mungu katika nafasi ya kufikiriwa kuwa anahusiana na wenye Imani pekee lakini maandiko yanamaanisha Imani ina pande mbili, na zote ni Imani.

 

Waebrania 11:35-39 “Wanawake walipokea wafu wao waliofufuliwa. Lakini wengine waliumizwa vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora; wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani; walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya; (watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi. Na watu hao wote wakiisha kushuhudiwa kwa sababu ya imani yao, hawakuipokea ahadi;”

 

Je watakatifu waliouawa kwaajili ya Imani, kina Stefano waliopigwa mawe na kufa kwaajili ya neno la uzima je walikuwa hawana Imani? Au Kristo mwenyewe mwenye haki aliyesulubiwa na kufa kifo kibaya msalabani je hakuwa na Imani?  Watakatifu waliopitia mateso na changamoto mbalimbali je walikuwa wamemkosea Mungu kuna haja ya kupanua mtazamo wako kuhusu changamoto mbalimbali wanazopitia watu wote duniani!

 

4.       Mfariji mwenye kutaabisha huzungumza zaidi ya kile anachokijua – Wafariji wengi wenye kutaabisha ni wepesi kuzungumza na ni wepesi kufikiri na kutoa maoni,  na sio wepesi kusikiliza, unaweza kuwa kwenye ndoa kama ya kwangu ina miaka 22 mimi ndio naishi na mke wangu, lakini kuna mtu anaweza kuja tu na kujifanya anatujua vizuri kuliko tunavyojijua kwa habari za kusikia tu, wafariji wenye kutaabisha hujifanya wanajua kila kitu, wanaweza kujifanya wanamjua mumeo kuliko wewe au wanamjua mkeo kuliko wewe au wanajua sana maisha yako au wana taarifa zako za miaka na siku nyingi au wanajua hata dhambi zako za zamani, hawajui kama ulitubu au la hawajui uhusiano wako na Mungu lakini wanaweza kujifanya wanajua na wakakizungumza kwa kujiamini na kwa uhakika kumbe wako mbali sana na mapenzi ya Mungu, Wako watu  wanaweza kujua hata kwanini unaugua figo, na wakawa na majibu yao, wanaweza kujua hata kwanini uliachishwa kazi na wakawa na majibu yao, wanaweza wakawa na jibu la kila kitu, Rafiki za Ayubu walikuwa na dhana kuwa dhambi inaleta changamoto za kila aina na haki inaleta thawabu na Baraka tele na mafanikio kwa hiyo hata kufa kwa watoto kumi wa Ayubu wao waliona kuwa huenda watoto hao walikuwa wamefanya dhambi na wakazungumza kwa uhakika ona

 

Ayubu 8:2-4 “Wewe utanena maneno haya hata lini? Maneno ya kinywa chako yatakuwa kama upepo mkuu hata lini? Je! Mungu hupotosha hukumu? Au, huyo Mwenyezi hupotosha yaliyo ya haki? Kwamba watoto wako wamemfanyia dhambi, Naye amewatia mkononi mwa kosa lao;”

 

Unaona Wafariji na washauri wa Ayubu walimwambia kuwa Mungu amewaua watoto wako kwa sababu walikuwa wamemfanyia Mungu dhambi na Mungu amewashughulikia kwaajili ya makossa yao! Wafariji wenye kutaabisha kwa ujumla huwa hawajui hata wanayoyazungumza, wao wanazungumza kwa uzoefu wa falsafa za dunia na hawawezi kuingia kwenye mashauri ya Mungu na kujua Mungu alikuwa anamaanisha nini na kwanini mambo yanatokea katika namna yanayotokea, lakini pia walikuwa wanadhani tu kwa kuunganisha mambo, na badala ya kumfariji Ayubu katika mapito yake walimuhukumu yeye na familia yake ! na badala ya kumpunguzia Msiba wake waliongeza huzuni zake!

 

5.       Mtu anayefikiri kuwa kikombe chako kimejaa  -  Kwamba Mungu huwa anahifadhi maovu anaandika mahali anakuangaliaaaaa afu kuna mstari mwekundu, kuna kikombe chako mahali siku kikijaaa sasa hasira zake zinawaka na anaanza kukushughulikia hii ni dhana ambayo imejengeka sana kwa watu wa Mungu kama wanajadili jambo kuhusu mapito yako wanaweza kusikika  na kusema aaa jamaa bhana kikombe chake kimejaa!:,  Hata sijui imeandikwa wapi au iko eneo gani katika maandiko ambapo Mungu emeeleza kuwa kuna matone ya dhambi yanaingia afu kikombe chako kikijaa anakushughulikia! Yaani tunaye baba Mbinguni ambaye anavizia maovu yetu yafikie kiwango Fulani alafu anamwaga mihasira yake ahaaaa ee kikombe kimejaa yaani kuna mambo kadhaa ulikuwa huyafanyi sasa Mungu ndio anashughulikna na wewe ulikuwa hutoi zaka, uliwaabisha wengine, uliwanyima chakula wenye njaa, hukuwajali wajane, hukuwajali yatima, hukwenda kuona wafungwa, uliwanyima maji wenye kiu, ulipendelea watu, uliwapuuzia yatima na wajane, ulikuwa na hiki ama kile kwa hiyo baada ya mlolongo huo mkubwa Mungu alikuwa anakucheki tu sasa kikombe kimejaa anakushughulikia ahaaa ona  dhana kama hii ilikuwa katika mioyo ya wafariji wa Ayubu waliokuja kumfariji na kumshauri n ahata leo wako watu wenye mitazamo kama hiyo

 

Ayubu 22::5-10 “Je! Uovu wako si mkuu? Wala maovu yako hayana mwisho. Kwa kuwa umetwaa dhamana kwa nduguyo bure, Na kuwavua nguo zao walio uchi. Hukumpa maji ya kunywa huyo aliyechoka, Nawe umemnyima chakula huyo mwenye njaa. Lakini huyo shujaa, nchi ilikuwa yake; Na huyo mwenye kusifiwa, yeye aliikaa. Umewafukuza wanawake wajane hali ya utupu, Na mikono ya mayatima imevunjwa. Kwa hiyo umezungukwa na mitego, Na hofu ya ghafula yakutaabisha,”

 

6.       Wafariji wenye kutaabisha hujiweka katika nafasi ya Mungu kuhukumu -  wakati ukiwa katika changamoto mbalimbali za maisha saa ya kujaribiwa kwako wafariji wenye kutaabisha hujisahau na kukaa katika nafasi ya Mungu  wakijifanya kuamua hatima ya maisha yako, au wakitaka kumsaidia Mungu kukuonjesha machungu zaidi, kumbe badala yake wanamkosea Mungu, waliokuja kumfariji Ayubu wote walihukumiwa na Mungu na ukweli ni kuwa Mungu alikasirishwa nao sana kwa kuwa hawakuwa sahihi kwa jinsi na namna walivyoshughulika na Ayubu

 

Ayubu 42:7-10 “Basi ikawa, baada ya Bwana kumwambia Ayubu maneno hayo, Bwana akamwambia huyo Elifazi Mtemani, Hasira zangu zinawaka juu yako, na juu ya hao rafiki zako wawili; kwa kuwa ninyi hamkunena yaliyo sawa katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu. Basi sasa, jitwalieni ng'ombe waume saba, na kondoo waume saba, mkamwendee mtumishi wangu Ayubu, mjisongezee sadaka ya kuteketezwa; na huyo mtumishi wangu Ayubu atawaombea ninyi; kwa kuwa nitamridhia yeye, nisiwatende sawasawa na upumbavu wenu; kwani ninyi hamkunena maneno yaliyonyoka katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu. Basi Elifazi, Mtemani, na Bildadi, Mshuhi, na Sofari, Mnaamathi, wakaenda, wakafanya kama vile Bwana alivyowaamuru; naye Bwana akamridhia Ayubu. Kisha Bwana akaugeuza uteka wa Ayubu, hapo alipowaombea rafiki zake; Bwana naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza.”

 

Wafariji hawa walikosea hawakusema sawasawa kwa habari ya Mungu wala kwa habari za mtumishi wake Ayubu, na hivyo walikuwa na hatia walipata dhambi ambayo ilihitaji tena watoe dhabihu kisha waombewe na Ayubu ili Mungu aweze kuwarehemu! Je unapenda sana kujishaua shaua na kuingilia mambo ya watu katika maisha yao? Je unadhani uko sahihi kila wakati unaponena neno juu ya Masihi wa Bwana na mapito yake?  Je unadhani uko salama unapoongezea mateso juu ya watu wa Mungu, Je unadhani uko sahihi wakati wote unapojifanya unatoa ushauri kuhusu maisha na huduma ya Mtu wa Mungu? Je wewe ndio Mungu je wewe ndiye uliyemuita, je wewe ndio unajua anakokokwenda?  Je wewe unajifanya una uelewa mkubwa sana wa neno la Mungu kuliko mtu anayepitia mateso? Je wewe kwenye raha zako unadhani una ukaribu na Mungu kuliko mtu anayepitia kwenye mateso? Au mtu aliyevunjika moyo?  Wengi wa watu wanaojifanya wafariji, au washauri ndio wanaoharibu maisha ya watu zaidi na kumkosea Mungu kuliko unavyodhani kwa msingi huo lazima kila mmoja achukue tahadhari na kuacha kuingilia mapito na njia za mtu, tuwe marafiki tu, tuombeane tu lakini huna mamlaka ya kuingilia na kumuamulia mtu mpango wa Mungu alioukusudia kwa watu wake na maisha yake na mapito yake, Mungu akulinde wewe na mimi ili tusiwe miongoni mwa watu watakaokuwa wafariji wenye kutaabisha

 

Namna ya kujiepusha na wafariji wenye kutaabisha au kuwa wafariji wenye kutaabisha

1.       Acha kumuwazia Mungu kwa upumbavu!

 

Ni vizuri kukaa kimya wakati changamoto zinapozuka katika maisha yetu na kuacha kabisa kumuwazia Mungu kwa upumbavu, hakuna jambo linaweza kuhatarisha maisha yetu kama kukimbilia kuzungumza mambo kana kwamba tunajua sana, duniani kuna watu ni wajuaji kila kitu wanadhani wanakijua na wana majibu ya kila kitu, maandiko yanatufundisha kuwa ni vizuri kukaa kimya na kujichunga sana tunapozungumza mambo na zaidi pia tunaloliwaza kuhusu Mungu.

 

Ayubu 1:20-22 “Ndipo Ayubu akainuka, akalirarua joho lake, kisha akanyoa kichwa chake, na kuanguka chini, na kusujudia; akasema, Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na libarikiwe. Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu.”

 

Kufikiri kuwa kila mwanadamua aneyeteseka duniani ni kwa sababu ametenda dhambi ni kumwazia Mungu kwa upumbavu, hivi wewe ni mkamilifu kiasi ya kwamba Mungu anakuacha? Kama Mungu anagekuwa anamtesa kila mtu kwa sababu ya dhambi basi wanadamu wote wangekuwa walelazwa kwa mateso na magonjwa kutokana na uovu tulio nao maandiko yanaonyesha kuwa watu wote wamefanya dhambi na hakuna mwenye haki hata mmoja wala hakuna anayemtafuta Mungu Ayubu anatajwa kuwa alikuwa Mcha Mungu

 

Warumi 3:10-12 “kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja.”

 

Kama unataka kuwa mshauri mzuri na mfariji mzuri uwe na uwezo mkubwa wa kulijua neno la Mungu na kumjua Mungu, na kuyajua mapenzi yake na njia zake, huwezi kuwa mfariji sahihi kama humjui Mungu wala neno lake na tabia zake na njia zake, tukilijua neno vema na tabia za Mungu na mapenzi yake tunaweza kufaa kuwa wafariji wazuri kwa kuwa tutawaelekeza watu katika kumuamini Mungu na kuwatia moyo wanapopitia katika changamoto mbali mbali, Mungu hana mahali ambapo anaweka rekodi ya uovu na kusubiri kikombe kijae, wala alishasema watoti hawatateseka kwa sababu ya dhambi za baba zao

 

 Zaburi 130:3-4 “Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama? Lakini kwako kuna msamaha, Ili Wewe uogopwe.”

 

Ezekiel 18:20 “Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe, haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake.”

 

2.       Usiwe na majibu ya suluhisho la tatizo moyoni mwako

Marafiki wa Ayubu walifanya mambo mazuri kama matatu hivi waliposikia kuwa Ayubu amepatwa na majanga walimtembelea ni tofauti kidogo na nyakati za leo ambapo watu hukukimbia kama walivyomkimbia watu wengine, pili walilia kwa sauti kuu na kurarua mavazi yao kuonyesha kuwa waliguswa na changamoto alizopitia jamaa yao  na mwisho walikaa pamoja naye tena walikaa kimya kwa siku saba.

Tatizo lao ni kuwa hawakuweza kukaa kimya walikuwa na tafasiri yao kuhusu mateso yaliyompata Ayubu na walikuwa wanamtaka atubu ili kwamba Mungu aweze kumsamehe na kumbariki tena hii ilikuwa ushauri na suluhisho, nimeshakutana na watu wengi sana ambao unapokutana na changamoto wao wanakuambia UTUBU ni kana kwamba wewe kuna makosa Fulani makubwaaa umemfanyia Mungu na ndio maana unapitia hali unayoipitia, wanadhani kuwa sifahamu umuhimu wa toba wanadhani labda ninajihesabia haki kama ilivyo kwa Ayubu maandiko yalionyesha wazi kuwa Ayubu alikuwa safi, na Mungu mwenyewe alikuwa amejivunia kuhusu Ayubu na Shetani pia alikiri kuwa Ayubu alikuwa mwadilifu, kwa msingi huo basi ni wazi kuwa mapito ya Ayubu hayakuwa na uhusiano wowote na tabia zake, aidha wako watu ambao ukikosea wanataka kuona unaadhibiwa na Mungu na unapitia mambo magumu hata adhabu wanatoa wao haya ni makosa makubwa sana ya kitheolojia na ujuzi hafifu kuhusu Mungu, na neno lake, Mungu ni mwema na huwapa jua lake na mvua yake wema na waovu,  linapokuja swala la mapito huwa halichagui

Ayubu 2:9-10 “Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Umkufuru Mungu, ukafe. Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake.”     

Hatupaswi kuhisi tu kuwa mtu Fulani anapitia hali Fulani kwa sababu Fulani kwani kufanya hivyo pia ni kuingilia UBWANA wa Mungu, na hili ndio sababu iliyopelekea Mungu akawakemea Rafiki za Ayubu

3.       Zingatia kanuni za ushauri au kufariji

Ziko kanuni ambazo mfariji anapaswa kuzizingatia anapokwenda kumfariji mtu na kumshauri ikiwa ni pamoja na kuvaa kiatu na yeye aliyepatwa na majanga Warumi 12:15 “Furahini pamoja nao wafurahio; lieni pamoja nao waliao.” Kila mfariji lazima awe na uelewa wa kutosha kuhusu mapito na njia za Mungu, achana kabisa na mitazamo yenye kuhukumu achana nayo, hakikisha unakuwa na usiri na sio kutangaza siri za Muhusika, zingatia tamaduni za wahusika, acha kwenda kuwasanifu, watie moyo unaowafariji sawa sawa na mtazamo wao au wa neno la Mungu na mapenzi ya Mungu, waunge mkono isipikuwa tu kama fikira zao haziko sawa na Mapenzi ya Mungu, hakikisha unamjua Mungu vizuri na njia zake, kumbuka kuna wanaopatwa na ubaya kwa sababu ya mabaya lakini si kila anayepatwa na mabaya ni mbaya, Panua mtazamo wako wa kitheolojia na upana wa mapito katika mtazamo wa Mungu, Inua macho yako na kuchukua tahadhari kuhusu wema wa Mungu.

Hitimisho:

Hatuna budi kumuomba Mungu ili siku zote tuweze kuwa marafiki wazuri, wafariji wasioleta misiba, na washauri wenye weledi ili kwamba wale wote wanaopitia mapito ya aina mbalimbali na huzuni na magumu na maumivu tuweze kujua namna ya kuwatia moyo katika Mungu, wakati mwingine kama hatuna ufumbuzi wa jambo ni vema kukaa kimya usijitie kimbelembele kama mzungumzaji, Tumuombe Mungu atusaidie kama tunataka kusema tuseme yaliyo kweli na yale tunayoyajua na yaliyoko kwenye mapenzi yake, kama watu wana dhambi tuwaongoze kwenye mema, tuwe wafariji wenye haki, na sio wafariji wenye kutaabisha.

Na Rev. Innocent Mkombozi Kamote

Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni: