Zaburi 27:9-11 “Usinifiche uso wako,
Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, Wala
usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu. Baba yangu na mama yangu wameniacha, Bali
Bwana atanikaribisha kwake. Ee Bwana, unifundishe njia yako, Na kuniongoza
katika njia iliyonyoka; Kwa sababu yao wanaoniotea;”
Utangulizi:
Watu wote tunaweza kuwa na ufahamu
wa kutosha kuhusiana na swala zima la Umuhimu wa Baba na Mama yaani wazazi wetu
na walezi wetu, kwa jinsi walivyo wa Muhimu sana Duniani, Wazazi wetu na walezi
wetu wana mchango mkubwa sana na wa muhimu sana katika kutuleta Duniani na
uangalifu wao mkubwa wa kuhakikisha tunapata malezi na kukua tukiwa na furaha
na Amani, wao pia hujitahidi sana katika kuhakikisha wanatutimizia mahitaji
yetu, wanatunza afya zetu wanaonyesha kujali na nafikiri hata kabla ya kumjua
Mungu kwa kawaida tunaanza kuwajua wao, wao ni wa Muhimu sana kama hujui
umuhimu wa wazazi baba na mama na walezi Hebu wapoteze siku moja ndipo
utakapoingia katika wimbi la kujua uchungu wa dunia, mimi nilipoteza mama yangu
nikiwa mdogo sana mpaka leo moyo wangu umejawa na majonzi makubwa mno siwezi
kumkufuru Mungu kwa kutokuwepo kwake lakini wakati mwingine hata katika utu
uzima huu huwa nasema laiti mama yangu angelikuwepo nadhani unaelewa! Nataka tu
kuonyesha umuhimu wa watu hawa, na ndio maana Mungu katika Hekima yake anataka
watu hawa wapewe heshima maalumu na ya tofauti katika maandiko na kuwa kupitia
wao kunakuwa na Baraka kubwa sana katika maisha yetu ona
Waefeso 6:1-3 “Enyi watoto, watiini wazazi
wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki. Waheshimu baba yako na mama yako; amri
hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi,Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia.”
Unaona tuwapo Duniani wazazi ni
nguzo ya ulinzi na usalama wa maisha yetu duniani, kama utakuwa umeishi katika
nyumba ambayo baba na mama wameachana au kuna mafarakano yaliyopelekea mmoja
akaondoka au ukibaki yatima unaweza kujua umuhimu wa uwepo wa wazazi ndipo sa
Maandiko yanatuasa tuwaheshimu sana kwani kwa kufanya hivyo tunapata Baraka na
mafanikio na kupewa uwezo wa kuishi siku nyingi duniani, Hata hivyo katika
mazingira Fulani wazazi wetu wanaweza kutuacha na tukajikuta tumebaki wenyewe
na ni mmoja tu anayeweza kubaki na uaminifu wake mpaka dakika ya mwisho yaani
Mungu wetu wa Mbinguni, hilo ndilo ambalo Mwandishi wa zaburi anataka
kutuonyesha leo:-
·
Maana ya neno kuachwa
·
Baba yangu
na mama yangu wameniacha!
·
Bali Bwana
atanikaribisha kwake !
Maana ya neno Kuachwa!
Zaburi 27:9-11 “Usinifiche uso wako,
Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, Wala
usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu. Baba yangu na mama yangu wameniacha, Bali
Bwana atanikaribisha kwake. Ee Bwana, unifundishe njia yako, Na kuniongoza
katika njia iliyonyoka; Kwa sababu yao wanaoniotea;”
Ni Muhimu kufahamu kuwa neno
kuachwa linalotumika hapo katika maandiko ya Kiebrania linasomeka kama AZAB
ambalo kwa kiingereza wanatumia neno FORSAKEN Lakini kimsingi neno linalopaswa kutumika
hapo ili kuleta maana inayokusudiwa ni neno ABANDONED ambalo ufafanuzi wake ni cease to support or look after someone kwa Kiswahili ni KUTELEKEZA wakati neno Forsaken ni kuacha, kwa hiyo kimsingi
neno ambalo Daudi analimaanisha hapo ni KUTELEKEZWA
kwa hiyo kuachwa ni jambo lingine na
kutelekezwa ni swala lingine na ni zaidi ya kuachwa!, Kama mtu aliyekuwa
amejenga nyumba ya thamani sana kisha akaacha kuihudumia na kuiacha ikawa ka ma
gofu au mahame!
Neno kutelekeza linatumika katika
Kiswahili kumaanisha Mtu anayetegemewa kutoa msaada wa matumizi, malezi, chakula
mavazi na matibabu, makazi ulinzi pamoja na mahitaji yote ya msingi anapopotea
au kuacha kutoa huduma hizo au kuacha kujihusisha na wale wanaomtegemea na
kuwaacha wakiwa hawana msaada. Wzazi wetu wa kiroho pia wanaweza kufanya hivyo
yaani kututelekeza!
Baba yangu na mama yangu wameniacha!
Zaburi 27:9-11 “Usinifiche uso wako,
Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, Wala
usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu. Baba yangu na mama yangu wameniacha, Bali
Bwana atanikaribisha kwake. Ee Bwana, unifundishe njia yako, Na kuniongoza
katika njia iliyonyoka; Kwa sababu yao wanaoniotea;”
Kimsingi hatuna uhakika kama kuna
mahali ambapo Daudi aliwahi kutelekezwa na baba yake na mama yake, Japo
tunaweza tu kukumbuka tukio la Daudi kuachwa akiwachunga kondoo wa babaye
wakati Samuel alipokuja kutawadha mtu atakayekuwa mfalme kutoka katika familia
ya Yese ona
1Samuel 16:11-13 “Kisha Samweli akamwambia
Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama,
anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa
sababu hatutaketi hata atakapokuja huku. Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao.
Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza.
Bwana akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye. Ndipo Samweli akaitwaa
pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana
ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake
Rama.”
Hapa tunaweza tu kupata mwanga
kwamba Daudi alipuuziwa ukilinganisha na ndugu zake wengine japo ukweli ni kuwa
Mungu alikuja kumchagua yeye, hatuwezi kusema kuwa Daudi alitelekezwa, aidha
wakati wa taabu zake alikimbia pamoja na wazazi wake na baadaye aliona ni vema
akawahifadhi kwa Mfalme wa Moabu yaani kwa ndugu wa bibi yake RUTHU ambako aliwahifadhi wazazi wake
kwa muda ili wasikutane na misukosuko ya kukimbia huku na huko
1Samuel 22:3-4 “Kutoka huko Daudi akaenda Mispa ya Moabu; akamwambia
mfalme wa Moabu, Tafadhali ukubali baba yangu na mama yangu watoke huko waliko,
wakakae kwenu, hata nitakapojua Mungu atakalotenda kwa ajili yangu. Akawaleta
mbele ya mfalme wa Moabu, nao wakakaa pamoja naye wakati wote Daudi alipokuwa
ngomeni.”
Hapa pia hatuoni ushahidi wa Daudi
kuachwa au kutelekezwa na Familia yake kwanini Daudi anazungumza katika zaburi
hii kuwa baba yangu na mama yangu wameniacha Lakini Bwana atanikaribisha kwake
? hii ilikuwa ni lugha ya kimashairi ambayo Daudi aliitumia kutufundisha jambo
kuhusu utendaji wa Mungu, Daudi anataka kuonyesha wasikilizaji wake kuwa hata
pamoja na ukaribu mkubwa walio nao wazazi wetu na walezi wetu na uwezo wao na
uchungu wao mkubwa wa kutuhudumia, bado Mungu anabaki kuwa msaada ulio karibu
zaidi kuliko msaada wa wazazi, anataka kuonyesha kuwa utendaji wa Mungu katika
maisha yetu unazidi ule wa wazazi, kwani wao pamoja na kujitoa kwao na kujidhabihu
kwao kuna wakati wanaweza kuacha kuwa na huruma dhidi yetu lakini sivyo alivyo
Bwana Mungu wetu, wale wote wanaodhani ya kuwa Mungu amewatelekeza wanapaswa
kujua kuwa wazazi baba na mama wanaweza kufanya tukio hilo lakini sio ilivyo
kwa Bwana Mungu wetu ona
Isaya 49:14-16. “Bali Sayuni alisema, YEHOVA
ameniacha, Bwana amenisahau. Je!
Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo
lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. Tazama, nimekuchora
katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima.”
Na ndio maana inapotokea Mtu
amepoteza mume, au amepoteza wazazi na kuwa yatima Mungu mwenyewe huchukua
nafasi hiyo na kuwa mume wa wajane na baba wa yatima ona
Zaburi 68:5-6 “Baba wa yatima na mwamuzi wa
wajane, Mungu katika kao lake takatifu. Mungu huwakalisha wapweke nyumbani;
Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa; Bali wakaidi hukaa katika nchi kavu.”
Wakati wote katika maisha yetu,
tunapohisi kutelekezwa, au kuachwa au kuwa peke yetu hakuna sababu ya kuumia na
kuteseka tukijuliza kuwa Msaada (wokovu) wetu utatokea wapi Mungu aliye baba wa
wapweke baba wa Yatima mwamuzi wa wajane atatuletea wokovu mkuu
Hosea 14:3 “Ashuru hatatuokoa; hatutapanda
farasi; wala hatutaiambia tena kazi ya mikono yetu, Ninyi ndinyi miungu yetu;
maana kwako wewe wasio na baba hupata rehema.”
Mungu atachukua jukumu la baba na
mama au walezi kwa kila anayemuamini, ataonyesha upendo wake usiokoma na ataonyesha kujali katika namna ambayo mwanadamu hawezi
kuifanya, kimsingi katika lugha hii kwa sababu ni ya kimashairi Daudi katika
lugha ya kawaida anazungumza kuwa HATA
KAMA baba yangu na mama yangu
wataniacha Mungu atachukua nafasi na ni
mwenye nafasi ya kuonyesha anajali zaidi ya ukaribu walio nao wazazi wetu yeye hatakuja kutuacha wala kutupungukia na
tunaweza kuliitia jina lake katika mazingira magumu kama hayo!, na sio baba na
mama peke yao awaye yote tunayemtegemea katika maisha haya akitutelekeza Mungu
aliyetuumba na aliye baba mwema anachukua jukumu kubwa la kutuweka mabegani
mwake katika ulimwengu wa roho na kuonyesha kujali kuliko karibu zaidi ya
mwanadamu wa kawaida
Bali Bwana atanikaribisha kwake !
Kwa kawaida Bwana hukaribisha kwake
watu wa aina yoyote ile hata wale ambao
wamekataliwa kwa sababu zozote zile katika jamii, hakuna mtu mwema na mzuri
sana kiasi cha kumshawishi Mungu kumkubali wala hakuna mtu mbaya sana kiasi cha
kumshawishi Mungu kumkataa, yeye alisema katika neno lake kuwa yeyote ajaye
kwake hatamtupa nje kamwe
Yohana 6:37 “Wote anipao Baba watakuja
kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe.”
Kristo Yesu alipokuwa duniani
aliwakaribisha watu wengi sana kwake hata wale waliokuwa wamekataliwa na jamii
Luka 15:1-2 “Basi watoza ushuru wote na wenye
dhambi walikuwa wakimkaribia wamsikilize. Mafarisayo na waandishi
wakanung'unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao.”
Neno kukaribisha katika biblia ya
kiyunani linasomeka kama neno PROSLAMBANO/PROSDECHOMAI
na kwa Kiebrania ni ASAPH ambalo maana zake ni Kuhudumia, kukubali,
kuwaangalia, kuwapokea, kuwatambua, kuwakusanya, Wakati wote milango ya Mungu iko wazi
kutukaribisha kwake na tukawa kwake watoto wake na wanae, Kuachwa kwa aina
yoyote ile kutakakokupata Duniani kusikufanye wewe ukajisikia kuwa una bahati
mbaya, kutelekezwa kwako kwa aina yoyote ile kusikufanye wewe ukajisikia kuwa
huna thamani yuko Mungu mbinguni ambaye ndiye aliyekuumba yeye anakuthamini
kuliko unavyoweza kufikiri alishatuahidi ya kuwa hatatuacha wala hatatupungukia
Yoshua 1:5 “Hapatakuwa mtu ye yote
atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa
pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala
sitakuacha.”
Zamani sana tulikuwa tunaimba Baba
na mama wawezakuniacha, lakini Yesu hawezi kuniacha, Rafiki zangu waweza
kuniacha lakini Yesu hawezi kuniacha!
Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni