1Wakorintho 11:23-32 “Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya
kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru
akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa
ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe
hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho
wangu. Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza
mauti ya Bwana hata ajapo. Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe
hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya
Bwana. Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe.
Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua
ule mwili. Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na dhaifu, na watu
kadha wa kadha wamelala. Lakini kama tungejipambanua nafsi zetu,
tusingehukumiwa. Ila tuhukumiwapo, twarudiwa na Bwana, isije ikatupasa adhabu
pamoja na dunia.”
Utangulizi:
Ni muhimu kwetu kufahamu, kuwa kushiriki meza
ya Bwana ni mojawapo ya agizo muhimu sana katika kanisa, ni agizo la kibiblia,
ambalo wanafunzi wa Yesu Kristo wanapaswa kulifanyia kazi, Meza ya Bwana au
Chakula cha Bwana ni Agizo lililotolewa na Yesu Kristo mwenyewe katika karamu
yake ya Mwishoaliposhiriki chakula cha pasaka na wanafunzi wake kabla kidogo ya
kukamatwa na kusulubiwa kisha kuuawa na kuzikwa na kufufuka na baadaye kupaa
mbinguni
Mathayo 26:17-28. “Hata siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi
wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, Ni wapi utakapo tukuandalie uile Pasaka?
Akasema, Enendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie, Mwalimu asema, Majira yangu
ni karibu; kwako nitafanya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu. Wanafunzi
wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa Pasaka. Basi kulipokuwa jioni
aliketi chakulani pamoja na wale Thenashara. Nao walipokuwa wakila, alisema,
Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti. Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza
mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana? Akajibu akasema, Yeye aliyetia mkono wake pamoja
nami katika kombe, ndiye atakayenisaliti. Mwana wa Adamu aenda zake, kama
alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu!
Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa. Yuda, yule mwenye kumsaliti,
akajibu, akasema, Ni mimi, Rabi? Akamwambia, Wewe umesema. Nao walipokuwa
wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake,
akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu Akakitwaa kikombe, akashukuru,
akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya
agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.”
Kwa msingi huo leo tutachukua Muda kujifunza
kwa kina na mapana na marefu kuhusiana na Meza ya bwana na tutajifunza somo
hili Meza ya Bwana na Karamu za Upendo! Kwa kuzingatia vipengele tisa
vifuatavyo:-
·
Meza
ya Bwana na karamu za upendo.
·
Chanzo
cha meza ya Bwana au chakula cha Bwana
·
Agizo
la kushiriki meza ya Bwana.
·
Sifa
za mshiriki wa meza ya Bwana.
·
Vitu
vinavyotumiwa na utaratibu wa kushiriki meza ya Bwana.
·
Maana
ya kiroho ya meza ya Bwana
·
Faida
nyingine za kushiriki meza ya Bwana.
·
Hasara
ya kushiriki meza ya Bwana isivyo stahili.
·
Mambo
yasiyo ya Kibiblia yanayihusiana na meza ya Bwana!
Meza ya Bwana na Karamu za Upendo !
Ni muhimu kufahamu kuwa nyakati za kanisa la
kwanza hawakuwa wanashiriki meza ya Bwana peke yake, Lakini walishiriki meza ya
Bwana pamoja na kufanya karamu za Upendo, Karamu hizo za upendo kwa kiyunani
ziliitwa KOINONIA ambapo watu waliungana pamoja na kushirikiana vyakula,
zawadi, ushirika, na changizo au kufurahia maswala mbalimbali, kwa hiyo baada
ya kushiriki meza ya Bwana vilevile watu walishirikiana vyakula kwa upendo kila
mmoja akimshirikisha mwenziwake kile alichikuja nacho kutoka nyumbani kwa hiyo
chakula hiki cha Bwana kilishirikishwa pamoja na karamu za Upendo, unaweza
kuona zikitajwa katika maandiko namna hiyo
Yuda 1:12-13 “Watu
hawa ni miamba yenye hatari katika karamu zenu za upendo walapo karamu pamoja
nanyi, wakijilisha pasipo hofu; ni mawingu yasiyo na maji, yachukuliwayo na
upepo; ni miti iliyopukutika, isiyo na matunda, iliyokufa mara mbili, na
kung'olewa kabisa; ni mawimbi ya bahari yasiyozuilika, yakitoa aibu yao wenyewe
kama povu; ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba yao waliowekewa
milele.”
2Petro 2:13 “Wakipatikana
na madhara, ambayo ni ujira wa udhalimu wao, wakidhania kuwa ulevi wakati wa
mchana ni anasa; wamekuwa ni mawaa na aibu wakifuata anasa zisizo kiasi katika
karamu zao za upendo, wafanyapo karamu pamoja nanyi;”
Hata hivyo pamoja na wazo zuri la kanisa la
kwanza kushiriki meza ya Bwana pamoja na karamu za upendo kulijitokeza kasoro
mbalimbali, ikiwapo karamu hizi kutumiwa na walimu wa uongo kueneza mafundisho
yao, na vilevile watu matajiri na wachoyo kuamua kula vyakula vyao badala ya
kushirikiana na wengine, aidha wengine waliamua kula vyakula vyao bila
kuwasubiria watu wengine na kwa sababu hiyo utaweza kuona kuwa mitume
walitahadharisha kuhusu kuvamiwa kwa karamu hizo za upendo, na walimu wa uongo,
vilevile Paulo mtume alikemea vikali tabia zilizokuwa zikijitokeza na ndipo
ilipofikia wakati ambapo Meza ya Bwana ambayo ilikuwa ni ibada maalumu
haikuweza tena kuwekwa pamoja na Karamu za upendo
1Wakorintho 11: 17-22 “Lakini katika kuagiza haya, siwasifu, ya kwamba
mnakusanyika, si kwa faida bali kwa hasara. Kwa maana kwanza mkutanikapo
kanisani nasikia kuna faraka kwenu; nami nusu nasadiki; kwa maana lazima kuwapo
na uzushi kwenu, ili waliokubaliwa wawe dhahiri kwenu. Basi mkutanikapo pamoja
haiwezekani kula chakula cha Bwana; kwa maana kila mmoja hutangulia kutwaa
chakula chake katika kule kula; hata huyu ana njaa, na huyu amelewa. Je! Hamna
nyumba za kulia na kunywea? Au mnalidharau kanisa la Mungu, na kuwatahayarisha
hao wasio na kitu? Niwaambieni? Niwasifu? La! Siwasifu kwa ajili ya hayo.”
Unaona kwa hiyo kutokana na hitilafu
zilizokuwa zimejitokeza Meza ya Bwana ilitenganishwa na Karamu za Upendo, na
kubaki Meza ya bwana pekee ambayo ndio moja ya agizo muhimu ambalo Yesu
aliagiza kanisa kulifanyia kazi. Hii haimaanishi kuwa KOINONIA ni dhambi bali kila kanisa linaweza kujiandalia KOINONIA yake bila kuiathiri meza ya
Bwana ambayo ni ibada inayopaswa kuheshimiwa sana!
Chanzo cha meza ya Bwana au Chakula
cha Bwana!
Nyakati za agano la kale wana wa Israel
waliagizwa kula chakula cha Bwana yaani Pasaka. Pasaka ya kwanza ilikuwa siku
ile wana wa Israel walipotoka Misri ambapo walikula mikate isiyotiwa
chachu:
Kutoka 12:3-20 “Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya
kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba
zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni wachache
kwa mwana-kondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na
watwae mwana-kondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu; kwa kadiri ya ulaji wa
kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwana-kondoo. Mwana-kondoo
wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika
mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko
lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni. Nao watatwaa baadhi ya damu yake
na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba
watakazomla. Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate
usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu. Msiile mbichi, wala ya
kutokoswa majini, bali imeokwa motoni; kichwa chake pamoja na miguu yake, na
nyama zake za ndani. Wala msisaze kitu chake cho chote hata asubuhi, bali kitu
kitakachosalia hata asubuhi mtakichoma kwa moto. Tena mtamla hivi; mtakuwa
mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi
mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya BWANA. Maana nitapita kati ya nchi
ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya
Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya
Misri; Mimi ndimi BWANA. Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba
mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo
lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri. Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi
mtaifanya iwe sikukuu kwa BWANA; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu
vyote, kwa amri ya milele Mtakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba; siku
hiyo ya kwanza mtaondoa chachu yote isiwe katika nyumba zenu kabisa; kwa kuwa
mtu ye yote atakayekula mkate uliochachwa tangu siku hiyo ya kwanza hata siku
ya saba, nafsi hiyo atakatiliwa mbali na Israeli. Siku ya kwanza kutakuwa kwenu
na kusanyiko takatifu, na siku ya saba kutakuwa kusanyiko takatifu; haitafanywa
kazi yo yote katika siku hizo, isipokuwa kwa hiyo ambayo kila mtu hana budi kula,
hiyo tu ifanyike kwenu. Nanyi mtaitunza ile sikukuu ya mikate isiyochachwa; kwa
kuwa katika siku iyo hiyo mimi nimeyatoa majeshi yenu katika nchi ya Misri; kwa
hiyo mtaitunza siku hiyo katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele. Mwezi
wa kwanza, siku ya mwezi kumi na nne, wakati wa jioni, mtakula mikate isiyochachwa,
hata siku ya mwezi ishirini na moja jioni. Muda wa siku saba isionekane chachu
katika nyumba zenu kabisa; kwa kuwa mtu ye yote atakayekula hiyo iliyotiwa
chachu, nafsi hiyo atakatiliwa mbali na mkutano wa Israeli, akiwa mwenye kukaa
hali ya ugeni, au akiwa mtu aliyezaliwa katika nchi. Msile kitu chochote
kilichochachwa; mtakula mikate isiyochachwa katika makao yenu yote.
Kwa msingi huo ukiacha kuwa siku ya Pasaka
wana wa Israel walichinja kondoo na kupaka damu yake katika miimo ya milango,
ili malaika wa bwana aweze kuruka kuipiga nyumba isiyo na damu, lakini ukiacha
mwana kondoo Pasaka aliliwa au kuadhimishwa pamoja na mikate isiyotiwa chachu
na ulaji wa mboga chunguchungu, Pasaka iliadhimishwa siku ya 14 katika Mwezi wa
Nisani kwa hiyo unaweza kuona kuwa meza ya Bwana au chakula cha Bwana ni agizo
la kibiblia hata kabla ya agano jipya
Mambo ya walawi 23:3-6 “Mtafanya kazi siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya
kustarehe kabisa, kusanyiko takatifu; msifanye kazi ya namna yo yote; ni Sabato
kwa BWANA katika makao yenu yote. Sikukuu za BWANA ni hizi, ni makusanyiko
matakatifu, ambayo mtayapigia mbiu kwa nyakati zake. Mwezi wa kwanza, siku ya
kumi na nne ya mwezi wakati wa jioni, ni pasaka ya BWANA. Na siku ya kumi na
tano ya mwezi ule ule ni sikukuu kwa BWANA ya mkate usiotiwa chachu; mtaila
mikate isiyochachwa muda wa siku saba.”
Pasaka ya Mwisho kabisa kabla ya angano jipya
ndio ambayo iliadhimishwa na Bwana Yesu pamoja na wanafunzi wake usiku ule
kabla Yesu hajatolewa na kusulubiwa kama Mwana kondoo wa wokovu
Luka 22:7-19 “Ikafika
siku ya mikate isiyotiwa chachu, ambayo ilipasa kuchinja pasaka. Akawatuma
Petro na Yohana, akisema, Nendeni, mkatuandalie pasaka tupate kuila.
Wakamwambia, Wataka tuandae wapi? Akawaambia, Tazama, mtakapoingia mjini
mtakutana na mwanamume akichukua mtungi wa maji; mfuateni mkaingie katika
nyumba atakayoingia yeye. Na mtamwambia mwenye nyumba, Mwalimu akuambia, Ki
wapi chumba cha wageni, nipate kula pasaka humo pamoja na wanafunzi wangu? Naye
atawaonyesha chumba kikubwa orofani, kimekwisha andikwa; andaeni humo.Wakaenda,
wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa pasaka. Hata saa ilipofika aliketi
chakulani, yeye na wale mitume pamoja naye. Akawaambia, Nimetamani sana kuila
pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu; kwa maana nawaambia ya kwamba
siili tena hata itakapotimizwa katika ufalme wa Mungu. Akapokea kikombe,
akashukuru, akasema, Twaeni hiki, mgawanye ninyi kwa ninyi; Maana nawaambia ya
kwamba tangu sasa sinywi mazao ya mzabibu hata ufalme wa Mungu utakapokuja.
Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu
unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Kikombe nacho
vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu
yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.] ”
Ni katika usiku huu Ndio Yesu aliamurukufanya
jambo hili kwa ukumbusho wake, kwa hiyo kimsingi katika wakati huu Yesu alikuwa
ameanzisha utaratibu mpya wa kuiandaa Pasaka bila mwana kondoo, na hivyo
kumbukumbu yake inafanyika kupitia miakate isiyotiwa chahu na juisi ya uzao wa
mzabibu nah ii ikawa ndio nnia mpya ya kumuadhimisha Kristo katika agano jipya na
kwa kufanya hivyo alibatilisha yote na
kutuanzia njia mpya
Ebra 10:19-20 “Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya
Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani,
mwili wake;”
Kwa kawaida Pasaka hii iliadhimishwa nyakati
za dhabihu ya jioni na ndio maana meza ya Bwana pia huitwa kwa kiingereza LORD SUPPER ambayo maana yake ni evening meal – Yaani chakula cha jioni
Marko 14:16-18 “Wanafunzi wakatoka, wakaenda mjini,
wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa pasaka. Basi ilipokuwa jioni yuaja
pamoja na wale Thenashara. Nao walipokuwa wameketi chakulani, wakila, Yesu
alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu, naye anakula pamoja nami, atanisaliti.”
Hata hivyo hii haimaanishi kuwa ni lazima Meza
ya bwana ifanyike jioni, Lakini kama inaweza kufanyika mida hiyo itapendeza
Zaidi lakini sio sharia
Agizo la kushiriki Meza ya Bwana!
Kwa msingi huo ni Muhimu kufahamu kuwa agizo
la kushiriki Meza ya Bwana linamuhusu kila mtu aliyeokoka, Meza ya bwana sio
utaratibu wa kidini ni agizo la kibiblia ni amri
Luka 22:19-20 “Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili
wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Kikombe
nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika
damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.] ”
1Wakorintho 11:23-25 “Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya
kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru
akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa
ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe
hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho
wangu.”
Kwa msingi huo unapoiangalia meza ya Bwana
unaweza kudhani kuwa ni kitu cha kipuuzi hizi lakini ni Agizo la Kristo kwa
kanisa na kwa sababu hiyo hatupaswi kamwe kupuuzia maagizo ya Mungu wala
kuchagua luipi la kulifanyia kazi na lipi la kuliacha, kwani kupouuzia baadhi
ya maagizo ya Mungu ni kujitafutia laana
Zaburi 119:6,21 “Ndipo mimi sitaaibika, Nikiyaangalia maagizo yako yote. Umewakemea wenye kiburi, Wamelaaniwa waendao mbali na maagizo yako.”
Haitupasi kuchagua maagizo Fulani na mengine kuchukia, inatupasa
kutii. Kutokuifanya maagizo Fulani ni kulaaniwa; Hivyo ni wajibu wetu kushiriki meza ya Bwana kila
inapopatiakana nafasi ya kufanya hivyo, kwa kuwa maandiko yameagiza kila
mkutanikapo, hii maana yake ni kila inapofanyika ibada na wakati mwingine
uongozi wa kanisa unaweza kuamua ni wakati gani wa kufanya hivyo kutokna na
Programu za kikanisa, makanisa mengine hufanya kila jumapili au kila
wanapokutanika au kila kunapokuwa na ibada, wengine hufanya mara moja kila
mwezi na kadhalika kila kanisa linaweza kujipangia utaratibu wake jambo la
msingi ni agizo hili la Bwana kufanyiwa kazi kama tu lilivyo agizo la ubatizo
kwa kuwa maandiko hayakupanga wakati
1Wakoritho 11: 24-26. “naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili
wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada
ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu
yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu. Maana kila mwulapo mkate
huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.”
Sifa za Mshiriki wa Meza ya Bwana!
Si kila mtu anaweza kuwa na sifa ya kushiriki
Meza ya Bwana, Meza ya bwana unaweza kuona kuwa Yesu aliishiriki akiwa na
wanafunzi wake wale 12 tu, hii maana yake ni kuwa kuna sifa maalumu za mtu
anayepaswa kushiriki meza ya Bwana, kwa sababu Meza ya Bwana inamshirikisha
Kristo au inamhitaji mtu mwenye ushirika na Kristo
Mtu anayeshiriki meza ya Bwana kwanza anapaswa
kuwa Mwanafunzi wa Yesu, na sio kila mtu au mtu yeyote Luka 22:10-11 “Akawaambia, Tazama,
mtakapoingia mjini mtakutana na mwanamume akichukua mtungi wa maji; mfuateni
mkaingie katika nyumba atakayoingia yeye.Na mtamwambia mwenye nyumba, Mwalimu
akuambia, Ki wapi chumba cha wageni, nipate kula pasaka humo pamoja na
wanafunzi wangu? ”
Kwa Msingi huo tunapata picha kuwa mshiriki wa
meza ya Bwana anapaswa kuwa Mwanafunzi wa Yesu, na Mwanafunzi wa Yesu ni lazima
awe na sifa zifuatazo:-
a. Awe ameokolewa yaani kama vile wale
walioshiriki kumla Pasaka katika agano la kale walikuwa ni jamii ya wana wa
Israel pamoja na jamii ya watu wengine waliookolewa kutoka Misri kwenda katika
nchi ya Kanaani, kwa hiyo ni lazima awe aliyetubu dhambi zake kwa kamaanisha
kuziacha, na kuishi maisha ya utauwa yaani utakatifu, katika kipindi hiki
cha kushiriki Meza ya Bwana tunakumbuka
jinsi tulivyookolewa kutoka katika utumwa wa dhambi
Kutoka 12: 39-42 “Nao
wakaoka mikate isiyochachwa ya ule unga waliouchukua walipotoka Misri, maana,
haukutiwa chachu, kwa sababu walitolewa watoke Misri, wasiweze kukawia, nao
walikuwa hawajajifanyia tayari chakula. Basi wana wa Israeli kukaa kwao, maana,
muda waliokaa ndani ya Misri, ulikuwa ni miaka mia nne na thelathini. Ilikuwa mwisho wa miaka hiyo mia nne na
thelathini, ilikuwa siku ile ile, ya kwamba majeshi yote ya BWANA yalitoka nchi
ya Misri. Ni usiku wa kuangaliwa sana mbele za BWANA kwa sababu ya kuwatoa
katika nchi ya Misri; huu ndio usiku wa BWANA, ambao wapasa kuangaliwa sana na
wana wa Israeli wote katika vizazi vyao.”
Kama wana wa Israel walivyotolewa misri kwenda Kanaani pia ukawa usiku wa kukumbukwa sana katika pasaka
ile ya kwanza washiriki, wa Meza ya Bwana wanapaswa kukumbuka kazi kubwa ya
ukombozi iliyofanywa na Yesu Kristo pale Msalabani kwaajili ya ulimwengu lakini
Zaidi sana wale wamuaminio! ni wakati wa kujichunguza na kuyaangalia maagizo ya
Bwana yaani wakati wa kushiriki meza ya Bwana ni wakati wa kuishi maisha ya
utakatifu nyaani kuwa mbali na chahu chahu katika maandiko huwakilisha
dhambi
Kutoka 13: 3 “Musa
akawaambia hao watu, Kumbukeni siku hii, mliyotoka nchi ya Misri, kutoka nyumba
ya utumwa; kwa kuwa BWANA aliwatoa mahali hapa kwa nguvu za mkono wake; na
usiliwe mkate uliochachwa.”
b. Awe amebatizwa kwenye maji tele sawa na
maandiko na ni kwa jina la Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Au mtu ambaye yuko
tayari kubatizwa baada ya kuwa ameokolewa, wote tunafahamu kuwa wana wa Israel
licha ya kuokolewa kutoka Misri lakini vilevile tunaelezwa kuwa walibatizwa
wawe wa Musa ona
1Wakorintho 10:1-4 “Kwa
maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote
chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; wote wakabatizwa wawe wa Musa
katika wingu na katika bahari; wote wakala chakula kile kile cha roho; wote
wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho
uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo.”
Unaona
Israel waliokula chakula cha kiroho, na kunywa kinywaji kile cha roho
walibatizwa wawe wa Musa, tunajifunza hapa vilevile kwa kuwa Meza ya Bwana ni
chakula cha kiroho na kinywaji cha kiroho basi wale wanaoshiriki wanapaswa kuwa
watu waliotii au watakaotii agizo la Ubatizo
Mathayo 28:19-20. “Basi,
enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba,
na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru
ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”
Yohana 3:22-23 “Baada
ya hayo Yesu na wanafunzi wake walikwenda mpaka nchi ya Uyahudi; akashinda huko
pamoja nao, akabatiza. Yohana naye alikuwa akibatiza huko Ainoni, karibu na
Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji tele; na watu wakamwendea, wakabatizwa.”
Yohana 4:1-2 “Kwa
hiyo Bwana, alipofahamu ya kuwa Mafarisayo wamesikia ya kwamba, Yesu anafanya
wanafunzi wengi kuliko Yohana, na kuwabatiza, (lakini Yesu mwenyewe hakubatiza,
bali wanafunzi wake,) ”
Wakolosai 2:11-12 “Katika
yeye mmetahiriwa kwa tohara isiyofanyika kwa mikono, kwa kuuvua mwili wa nyama,
kwa tohara ya Kristo.Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa
pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu.”
Matendo 2:41-42 “Nao
waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu
tatu. Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika
kuumega mkate, na katika kusali.”
Matendo 8:12 “Lakini
walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake
Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake.”
Kwa msingi
huo unaweza kuona kwamba Mshiriki wa Meza ya Bwana ni mwanafunzi wa Yesu yaani
mtu aliyeisikia injili na kuiamini kisha kubatizwa na anapokuwa anakaa katika
fundisho basi huyo ana sifa ya kushiriki meza ya Bwana au chakula cha Bwana
c. Asiwe mtu mwenye kuabudu Sanamu au miungu
mingine 1Wakorintho 10:15-21. “Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya
sanamu. Nasema kama na watu wenye akili; lifikirini ninyi ninenalo. Kikombe
kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule
tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio
wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja. Waangalieni hao Waisraeli walivyokuwa kwa
jinsi ya mwili; wale wazilao dhabihu, je! Hawana shirika na madhabahu? Basi
niseme nini? Ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? Au ya kwamba
sanamu ni kitu? Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa
mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani.
Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani. Hamwezi
kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani.”
d. Awe mume wa mke mmoja au mke wa mume mmoja yaani mtu asiyeishi katika maisha ya ukahaba
au ndoa ambayo haijahalalishwa katika jamii, au ndoa isiyohalali I Wakoritho
6:15-20 “Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo
vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba?
Hasha! Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana
asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja. Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni
roho moja naye. Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya
mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.
Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu,
mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa
thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.”
Tunaposhiriki
meza ya Bwana maana yake sisi ni washirika wa Yesu Kristo, mtu anapookolewa
mwili wake unakuwa kiuongo katika mwili wa Kristo, naye anakuwa ni hekalu la
Roho Mtakatifu kwa msingi huo basi uko umuhimu wa mtu huyu kuwa na maisha
matakatifu ikiwa ni pamoja na kujitenga na zinaa au ndoa isiyohalali, huwezi
kuishi maisha ya kikahaba kisha ukashiriki meza ya Bwana unaweza kupata madhara
au huwezi kuwa mshirikina kisha ukashiriki meza ya bwana unaweza kupata madhara
badala ya faida zinazokusudiwa, kimsingi maisha nsafi na matakatifu, kuwa mbali
na dhambi na ibada ya sanamu, na ushirikina na kuishi kiholela kunakufanya
usiwe mshirika wa Kristo na hivyo sio vema kushiriki meza ya Bwana
Vitu vinavyotumiwa na utaratibu wa
kushiriki meza ya Bwana.
Vitu vinavyotumiwa katika Meza ya bwana maana
yake ni nyenzo zinazotumika katika kuiandaa meza ya Bwana
-
Mkate usiyotiwa chachu:
Mikate
inayotumika katika maandalizi ya Meza ya bwana inapaswa kuwa ni mikate
isiyotumia hamira au Backingpoweder yaani iliyoumuliwa au mikate isiyotiwa chachu
Luka 22:7, 19-20 7. “Ikafika
siku ya mikate isiyotiwa chachu, ambayo ilipasa kuchinja pasaka.” 19-20
“Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa,
akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa
ukumbusho wangu. Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki
ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.]”
Mikate hii
siyo kama ile tunayoitumia kwa chai. Ingawa ni vema kutumia hiyo majumbani
lakini katika meza ya Bwana hairusiwi kwa nini? Sababu ni kuwa chachu ni mfano
wa uovu chachu ni mfano wa dhambi na kwa sababu Meza ya Bwana ni alama kivuli inayomwakilisha
Bwana wetu Yesu ambaye hakuishi masiha yandhambi hivyo mkate huo unapaswa kuwa
ni mkate usiotiwa chachu au kuumuliwa moja ya mifano ya mkate usiochachwa ni
chapati, aidha mafundisho ya uongo pia katika agano jipya huitwa chachu, Yesu
hakuwa na dhambi wala hakuwa mwongo
1Wakorintho 5:6-8 “Kujisifu
kwenu si kuzuri. Hamjui kwamba chachu kidogo hulichachusha donge zima? Basi,
jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile
mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka,
yaani, Kristo; basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu
ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli.”
Mathayo 16:11-12 “Imekuwaje
hamkufahamu ya kuwa si kwa sababu ya mkate naliwaambia? Ila jilindeni na chachu
ya Mafarisayo na Masadukayo. Ndipo walipofahamu ya kuwa hakuwaambia kujilinda
na chachu ya mkate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.”
Luka 12:1 “Wakati
huo, makutano walipokutanika elfu elfu, hata wakakanyagana, alianza kuwaambia
wanafunzi wake kwanza, Jilindeni na chachu ya Mafarisayo, ambayo ni unafiki.”
Waebrania 4:14-15 “Basi,
iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na
tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana
nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi
katika mambo yote, bila kufanya dhambi.”
Waebrania 7:26-27 “Maana
ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na
uovu, asiyekuwa na waa lo lote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko
mbingu; ambaye hana haja kila siku, mfano wa wale makuhani wakuu wengine,
kwanza kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya
dhambi za hao watu; maana yeye alifanya hivi mara moja, alipojitoa nafsi yake.”
Tunajifunza
nini kwamba Meza ya bwana inapaswa kuandaliwa kwa kutumia nyenzo ya mkate
usiotiwa chachu, na sio hivyo tu sisis wenyewe ni lazima tuwe mbali na chachu
yaani uovu au dhambi ya aina yoyote, wakati tunaandaa mkate usiotiwa chachu
waamini wanapaswa kujiandaa kwa toba na kuhakikisha kuwa hawaishi maisha ya
dhambi na unafiki na sio hivyo tu ni wakati wa kuhakikisha kuwa wanafunzi wa
Yesu wanakaa katika kweli kwani chachu pia huwakilisha mafundisho ya uongo,
mkate huo pia unapaswa kuwa mkate ambao unaweza kuvunjwa vunjwa kama vile watu
wanavyokata kata keko au wanvyogawana kitu Fulani kwa kufanya hivi tunaadhimisha na kutangaza
mauti ya Bwana ambapo mwili wake ulisulubiwa na kuvunjwa vunjwa na kuharibiwa
vibaya na kutundikwa msalabani
Isaya 52: 13-14 “Tazama,
mtumishi wangu atatenda kwa busara, atatukuzwa, na kuinuliwa juu, naye atakuwa
juu sana. Kama vile wengi walivyokustaajabia, (uso wake ulikuwa umeharibiwa
sana zaidi ya mtu ye yote, na umbo lake zaidi ya wanadamu),”
-
Uzao wa mzabibu
Meza ya
Bwana ina nyenzo kubwa mbili yaani mkate usiochachwa pamoja na kinywaji chake
ambacho kimsingi kinapaswa kuwa mzao wa mzabibu, Marko 14:23-25 “Akatwaa kikombe,
akashukuru, akawapa; wakakinywea wote.
Akawaambia, Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya
wengi. Amin, nawaambia ninyi, Sitakunywa tena kabisa uzao wa mzabibu, hata siku
ile nitakapounywa mpya katika ufalme wa Mungu.”
Kinywaji
hicho kinachotumika yaani mzao wa Mzabibu ua juisi ya mzabibu ndio huwakilisha
Damu ya Yesu
Mathayo 26:26-29 “Nao
walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi
wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa,
akisema, Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano,
imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. Lakini nawaambieni,
Sitakunywa kabisa tangu sasa uzao huu wa mzabibu, hata siku ile nitakapokunywa
mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.”
Luka 22:17-20 “Akapokea
kikombe, akashukuru, akasema, Twaeni hiki, mgawanye ninyi kwa ninyi; Maana
nawaambia ya kwamba tangu sasa sinywi mazao ya mzabibu hata ufalme wa Mungu
utakapokuja. Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio
mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.
Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya
katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.]”
Kinywaji
hiki kinawakilisha Damu ya Yesu iliyomwagika pale Msalabani ambayo ni takatifu
sana, ni kinywaji ambacho kilitokana na
mzao wa mzabibu, Katika misingi ileile ya kuwa Yesu hakuwa na chachu kinywaji
hiki vilevile hakipaswi kuwa kinywaji kilichochachwa yaani chenye pombe, “Fermented grape juice” na badala yake
inapaswa kuwa ni juisi ya mzabibu isisyochachwa “Unfermented grape juice” kwa hiyo ni lazima iwe juice ya Mzabibu
ambayo hajachachwa au isiyo na kilevi na mtu anaweza kuuliza swali kwanini iwe
juisi ya mzabibu na sio kitu kingine kama chungwa, mambibo na kadhalika nii ni
kwa sababu Yesu anaitwa katika maandiko Mzabibu wa kweli Yohana
15:1 “Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu
ndiye mkulima.”
Yesu anaitwa
Mzabibu wa kweli kwa sababu alizaa matunda ya haki, tofauti na wana wa
Israelambao Mungu aliwapanda kama mche mzuri wa mzabibu kutoka Misri na kuwaweka
katika nchi ya Mkanaani na badala yake wakazaa zabibu mwitu Zaburi 80:8 “Ulileta mzabibu kutoka Misri, Ukawafukuza mataifa
ukaupanda.”
Isaya 5:1-7 “Na
nimwimbie mpenzi wangu wimbo wa mpenzi wangu katika habari za shamba lake la
mizabibu. Mpenzi wangu alikuwa na shamba la mizabibu, Kilimani penye kuzaa
sana; Akafanya handaki kulizunguka pande zote, Akatoa mawe yake, Akapanda ndani
yake mzabibu ulio mzuri, Akajenga mnara katikati yake, Akachimba shinikizo
ndani yake; Akatumaini ya kuwa utazaa zabibu, Nao ukazaa zabibu-mwitu. Na sasa,
enyi wenyeji wa Yerusalemu, nanyi watu wa Yuda, amueni, nawasihi, kati ya mimi
na shamba langu la mizabibu. Je! Ni kazi gani iliyoweza kutendeka ndani ya
shamba langu la mizabibu nisiyoitenda? Basi, nilipotumaini ya kuwa litazaa
zabibu, mbona lilizaa zabibu-mwitu? Haya basi, sasa nitawaambieni
nitakalolitenda shamba langu la mizabibu; nitaondoa kitalu chake, nalo
litaliwa; nitabomoa ukuta wake, nalo litakanyagwa; nami nitaliharibu; wala
halitapogolewa wala kulimwa, bali litamea mbigili na miiba; nami nitayaamuru
mawingu yasinyeshe mvua juu yake. Kwa maana shamba la mizabibu la Bwana wa
majeshi ndilo nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni mche wake wa kupendeza;
akatumaini kuona hukumu ya haki, na kumbe! Aliona dhuluma; alitumaini kuona
haki, na kumbe! Alisikia kilio.”
Kwa msingi huo
washiriki wa meza ya bwana wanapoandaa juisi ya mzabibu isiyochachwa, wanapaswa
vilevile kuiandaa mioyo yao kumzalia Bwana matunda halisi na sio zabibu mwitu.
Maana ya kiroho ya meza ya Bwana!
Meza ya Bwana inatangaza mauti ya Bwana na
ushindi wake huku ikitukumbusha kuwa Kristo atakuja tena, na kwa sababu hiyo
inafanya kazi ya kutukumbusha ukombozi wetu kupitia kazi nzima iliyofanyika
pale msalabani na wajibu wetu wa kuishi maisha yanayompendeza, kimsingi ni kama
wana wa Israel wanavyoikumbuka Pasaka wakiadhimisha kuokolewa kwao katika nchi
ya Misri na kupelekwa katika inchi ya Kanaani, Meza ya bwana ni kama kambi ya
kujikumbusha namna tunapaswa kujitafakari na kuangalia safari yetu kwa kudumisha
ushirika na Yesu ili tusije tukawa watu wa kukataliwa
1Wakorintho 10:1-21. “Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa
baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; wote
wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari; wote wakala chakula
kile kile cha roho; wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana
waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. Lakini
wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani.
Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani
mabaya, kama wale nao walivyotamani. Wala msiwe waabudu sanamu, kama wengine
wao walivyokuwa; kama ilivyoandikwa, Watu waliketi kula na kunywa, kisha
wakasimama wacheze. Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya,
wakaanguka siku moja watu ishirini na tatu elfu. Wala tusimjaribu Bwana, kama
wengine wao walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka. Wala msinung'unike, kama
wengine wao walivyonung'unika, wakaharibiwa na mharabu. Basi mambo hayo
yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi,
tuliofikiliwa na miisho ya zamani. Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na
aangalie asianguke. Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya
wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo;
lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze
kustahimili. Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu.
Nasema kama na watu wenye akili; lifikirini ninyi ninenalo. Kikombe kile cha
baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si
ushirika wa mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili
mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja. Waangalieni hao
Waisraeli walivyokuwa kwa jinsi ya mwili; wale wazilao dhabihu, je! Hawana
shirika na madhabahu? Basi niseme nini? Ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa
sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni kitu? Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo
sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi
kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha
mashetani. Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya
mashetani.”
Wakati wa kushiriki Meza ya bwana ni wakati wa
kujitathimini kama wana wa Israel tumeambiwa sio wote waliingia Kanaani, ni
wajati wa kujikumbushankuimarisha uhusiano wetu na Bwana wetu Yesu Kristo,
hivyo ni wakati wa kujitafakari na kujikagua
na kuweka maazimio mapya ya kurudi na kukaa katika uwepo wa Bwana
Faida Nyingine za kushiriki Meza ya
Bwana !
Ni muhimu kufahamu kuwa katika meza ya Bwana
kuna faida nyingi sana za kiwmili na kiroho, tunaposhiriki kinywaji kile na
mkate ule na kutangaza mauti ya Bwana na kujiandaa kwaajili ya ujio wake mwili
wake ulisulubiwa kwaajili yetu na hivyo kuna nguvu kubwa sana ya uponyaji, Meza
ya bwana ni tangazo la aina ya mauti aliyiokufa Kristo na alikuwa kwaajili yetu
na hivyo tunaposhiriki inakuwa sawa kabisa na kusema kwa kupigwa kwake sisi
tumepona
Isaya 53:2-5 “Maana
alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana
umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani. Alidharauliwa na
kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye
watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika
ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa
amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu,
Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa
kupigwa kwake sisi tumepona.”
1Petro 2:21-25 “Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa
ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake. Yeye hakutenda dhambi,
wala hila haikuonekana kinywani mwake. Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano;
alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki. Yeye
mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa
mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa.
Kwa maana mlikuwa mnapotea kama kondoo; lakini sasa mmemrudia Mchungaji na
Mwangalizi wa roho zenu.”
Waebrania 13:12-13. “Kwa ajili hii Yesu naye, ili awatakase watu kwa damu yake
mwenyewe, aliteswa nje ya lango. Basi na tutoke tumwendee nje ya kambi,
tukichukua shutumu lake.”
Damu yake Yesu inatupa utakaso, magonjwa yetu
na madhaifu yetu yanaponywa, Roho zetu zimaimarika, ushirika wetu na Kristo
unaimarika, tunapata nafasi ya kumuabudu Yesu katika roho na kweli, tunaweka
mbali chachu zote, tunaanza upya safari ya kujihakikishia kuwa tunaushirika na
Kristo na tunaenda mbinguni, tunaishi maisha ya utakatifu na kufungua mlango wa
Baraka, wagonjwa ambao hawajaponywa katika maombezi ya kawaida hupokea uponyaji
kupitia meza ya Bwana hivyo kuna faida za kimwili na kiroho.
Hasara ya kushiriki Meza ya Bwana
isivyostahili
Tunaposhiriki meza ya Bwana inatupasa
kudhamiria kuacha dhambi. Yaani kuwa mbali na chachu, Sasa tunaposhiriki
na uovu au tukiwa na nia ya kutokuachana
na dhambi basi tunapata adhabu kali kwani tunakuwa tumeidharau kazi ya Mungu
iliyofanyika Msalabani na tunaweza kupata adhabu
Waebrania 10:28-29 “Mtu aliyeidharau sheria ya Musa hufa pasipo huruma, kwa neno la
mashahidi wawili au watatu. Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu
yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa
kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema? ”
Hivyo adhabu hiyo huanzia duniani na hata
inaweza kutupeleka Jehanamu milele japo lengo la adhabu hii ya Mungu ni ili
mwili wako uadhibiwe utubu na uweze kwenda mbinguni.
Pia tumaweza kuugua magonjwa yasiyoponyeka
hata kama tunaombewa namna gani hatuna uponyaji. Pia tunaweza kufa kabisa kwa
msingi huo inatupasa kujihoji kwanza kabla ya kushiriki. 1Wakoritho 11: 22-32 “kwa maana kila mmoja
hutangulia kutwaa chakula chake katika kule kula; hata huyu ana njaa, na huyu
amelewa. Je! Hamna nyumba za kulia na kunywea? Au mnalidharau kanisa la Mungu,
na kuwatahayarisha hao wasio na kitu? Niwaambieni? Niwasifu? La! Siwasifu kwa
ajili ya hayo. Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa
Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega,
akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho
wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni
agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.
Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya
Bwana hata ajapo. Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha
Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana. Lakini
mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe. Maana alaye na
kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua ule mwili. Kwa
sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na dhaifu, na watu kadha wa kadha
wamelala. Lakini kama tungejipambanua nafsi zetu, tusingehukumiwa. Ila
tuhukumiwapo, twarudiwa na Bwana, isije ikatupasa adhabu pamoja na dunia.”
Kushiriki mmeza ya Bwana isivyostahili na
ukapata adhabu maana yake ni kuwa ugonjwa utakaotokana na adhabu ya kushiriki
meza ya bwana isivyostahili hauwezi kupona kwa tabibu awaye yote wala maombezi
ya muhubiri yeyote kwanini kwa sababu ni mtu anaadhibiwa na Bwana
Mambo yasiyo ya Kibiblia yanayihusiana
na meza ya Bwana!
Madai ya mkate na Juisi ya Mzabibu kugeka kuwa
mwili na Damu ya Yesu halisi baada ya kubarikiwa hayo ni mafundisho ya uongo
kwani tendo hilo ni ukumbusho tu, hivyo mkate hubakia vile vile na juisi ya
mzabibu pia huwa vile vile na havuiwezi kugeuka kuwa Damu au mwili halisi wa
Bwana Yesu bali nguvu za Mungu za uponyaji wa mwili nafsi na roho huambatana na
meza ya Bwana.
-
Juisi
ya mzabibu kunywewa na Mchungaji tu kwa
niaba ya wote Hii sio kibiblia
kwani watu wote Wanaume kwa
wanawake wanapaswa kushiriki na sio mmoja kumiminiwa kombe
lote mtu mmoja peke yake Kumbuka
kuwa viko vifaa maalumu vinavyoweza kutumika kugawanya juice ya mzabibu na
kuigawa mikate hiyo iliyobarikiwa kwa kila mshirika mwenye sifa ya kushiriki
meza ya Bwana Mathayo 26:27 “Akakitwaa kikombe,
akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki;” Marko 14:23 “Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa; wakakinywea wote.”
-
Kutawadhana
kwa maji na kufutana miguu kabla ya kushiriki meza ya Bwana huu pia ni
upotovu: watu hawa hutumia maandiko ya Yohana 13: 2-12 “Kisha
akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa
kile kitambaa alichojifunga. Hivyo yuaja kwa Simoni Petro. Huyo akamwambia, Bwana!
Wewe wanitawadha miguu mimi? Yesu akajibu, akamwambia, Nifanyalo wewe hujui
sasa; lakini utalifahamu baadaye. Petro akamwambia, Wewe hutanitawadha miguu
kamwe. Yesu akamwambia, Kama nisipokutawadha, huna shirika nami. Simoni Petro
akamwambia, Bwana, si miguu yangu tu, hata na mikono yangu na kichwa changu
pia. Yesu akamwambia, Yeye aliyekwisha kuoga hana haja ila ya kutawadha miguu,
bali yu safi mwili wote; nanyi mmekuwa safi, lakini si nyote. Kwa maana alimjua
yeye atakayemsaliti; ndiyo maana alisema, Si nyote mlio safi. Basi alipokwisha
kuwatawadha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena, akawaambia, Je!
Mmeelewa na hayo niliyowatendea? ”
Hatuna budi kufahamu kuwa Yesu alitumia mifano
na mifano ya kinadharia na vitendo katika, kuwafundisha wanafunzi wake kama
Mwalimu na hapo alikuwa akifundisha kuhusu kuwa mkubwa katika ufalme wa Mungu
anapaswa mtumwa wa watu wote na kufanya kazi ya kitumwa nay a chini Zaidi kama
kutawadha miguu, hivyo kama unataka kufundisha somo hilo kiitendo ni vema
kufanya siku tofauti na hakuna ulazima wa nkuifanya kwenye meza ya bwana na
kufanya ibada kuwa ndefu na zenye kuchosha Yesu alitumia mfano huo wa kutawadha
wanafunzi wake miguu kwa sababu walikuwa na mawazo ya ukubwa badala ya utumishi
Luka
22:24-27 “Yakatokea mashindano kati yao, kwamba ni
nani anayehesabiwa kuwa mkubwa. Akawaambia, Wafalme wa Mataifa huwatawala, na
wenye mamlaka juu yao huitwa Wenye fadhili; lakini kwenu ninyi sivyo; bali
aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule
atumikaye.Maana aliye mkubwa ni yupi? Yeye aketiye chakulani, au yule
atumikaye? Siye yule aketiye chakulani? Lakini mimi kati yenu ni kama atumikaye.”
Hapo alikuwa anawafundisha kunyenyekea maana
kulikuwa na migongano ya kugombea ukubwa. Sasa kitendo cha Yesu kuwatawadha miguu
kilikuwa ni kitendo kinacho fanywa na mtumwa au mdogo kwa yule aliyemkubwa
Mwanzo
24:31-32 “Akasema, Karibu, wewe uliyebarikiwa na
BWANA, mbona unasimama nje? Kwa maana nimeiweka nyumba tayari, na nafasi kwa
ngamia. Na mtu yule akaingia katika nyumba, akawafungua ngamia; naye akatoa
majani na malisho kwa ngamia, na maji ya kuoshea miguu yake, na miguu ya watu
waliokuwa pamoja naye.”
1Samuel
25:41 “Naye akainuka na kujiinamisha kifulifuli
mpaka nchi, akasema, Tazama, mjakazi wako ni mtumwa wa kuwaosha miguu watumishi
wa bwana wangu.”
kwa msingi huo Yesu alikuwa
akiwafundisha unyenyekevu na kitendo chake cha kuwaosha miguu wanafunzi
wake kilikuwa ni ishara ya kuchukua nafasi ya chini ya utumwa na kujishusha akichukua
nafasi ya chini. Wafilipi 2:3-11 “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno;
bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi
yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya
wengine. Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo
Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa
sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana
utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;tena,
alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti,
naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia
Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu
vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa
YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”
Kwa hiyo kimsingi tukio la kutawadha miguu
haikuwa sehemu ya ibada ya meza ya Bwana bali ilikuwa ni fundisho kuhusu nafasi
ya juu katika utawala wa Mungu inapatikana kwa kujishusha na kuwa mtumwa wa
watu, Hatupaswi kufikiri kuwa kuna ulazima wa kutawadha miguu watu wakati
tunapotaka kushiriki meza ya Bwana asomaye na afahamu
Hitimisho:
Utaratibu wa
kufuatwa wakati wa kushiriki meza ya Bwana.
Kuhani
ataombea mkate kwanza
-
Mkate
– Baada ya maombi ya shukrani kwa kazi ya ukombozi aliyoifanya Yesu
msalabani kufanyika na Baraka
kisha watu wanafunzi humegewa
vipande vipande na kupewa mkononi na kupata
nafasi ya kujiombea
-
1Wakorintho 11:24 “naye
akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu;
fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.”
Kuhani
ataombea vikombe vya juisi ya mzabibu pia
-
Kikombe Baada ya Maombi yashukrani kwa kazi ya
ukombozi aliyoifanya Yesu Msalabani na Baraka watu wanaweza kunywa katika kikombe
kimoja au kugawanjwa katika vikombe vidogo vidogo na kila mtu kushiriki kikombe
chake.
-
1Wakorintho
11:25 “Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa
kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi
kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.”
Mratibu wa ibada ya meza ya Bwana anaweza
vilevile kutumia maandiko mengineyo yanayohusiana na meza ya Bwana na
wakashiriki na watu wake, kama Kanisa halijafundishwa somo kama hili unaweza
kuhubiri au kufundisha kwa ufupia kuhusiana na meza ya bwana na kisha
mkashiriki, kama wameshajifunza somo kama hili basi ufikapo wakati wa ibada ya
meza ya bwana unaweza tu kuendelea kwa kusoma andiko na kubariki vifaa vya
kiroho vya meza ya bwana na kisha watu wakashiriki, watu wanaweza kupata nafasi
ya kuomba na kuombeana au hata kusalimiana na kutiana moyo kwa dakika chache
wakati wa kushirikiana katika meza ya Bwana
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!