Mathayo 27:62-66 “Hata siku ya pili, ndiyo iliyo baada ya Maandalio, wakuu
wa makuhani, na Mafarisayo wakamkusanyikia Pilato, wakasema, Bwana, tumekumbuka
kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa akali hai, Baada ya siku tatu nitafufuka.
Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya tatu; wasije wanafunzi
wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika wafu; na udanganyifu wa
mwisho utapita ule wa kwanza. Pilato akawaambia, Mna askari; nendeni mkalilinde
salama kadiri mjuavyo. Wakaenda, wakalilinda kaburi salama, kwa kulitia lile
jiwe muhuri, pamoja na wale askari walinzi.”
Utangulizi:
Moja ya tukio
muhimu sana katika Imani ya Ukristo ni pamoja na tukio la Kusulubiwa, kufa na
kufufuka kwa Yesu Kristo, tukio hili halikuwa tukio la bahati mbaya na ndio
maana Yesu Kristo katika Hekima yake alilirudia tena na tena mara kwa mara
alipokuwa pamoja na wanafunzi wake na hii ni kwa sababu Mateso yake na kifo
chake ndio kilele cha juu zaidi cha huduma yake ya ukombozi kwa wanadamu, Na
ndio maana tunaona Yesu akizungumza juu ya tukio hili mara kadhaa na kila
wakati akijitaja kama Mwana wa Adamu ona :-
-
Mathayo 16:21-23 “Tangu
wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda
Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na
waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka. Petro akamchukua, akaanza
kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata. Akageuka, akamwambia Petro,
Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu,
bali ya wanadamu.”
-
Marko 8:31-32 “Akaanza
kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na
kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya
siku tatu kufufuka. Naye alikuwa akinena neno hilo waziwazi. Petro akamchukua,
akaanza kumkemea.”
-
Luka 9:21-22 “Akawaonya,
akawakataza wasimwambie mtu neno hilo; akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kupata
mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na
kuuawa na siku ya tatu kufufuka.”
-
Mathayo 17:22-23 “Nao
walipokuwa wakikaa Galilaya, Yesu akawaambia, Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa
katika mikono ya watu, nao watamwua, na siku ya tatu atafufuka. Wakasikitika
sana.”
-
Marko 9:30-32 “Wakatoka
huko, wakapita katikati ya Galilaya; naye hakutaka mtu kujua. Kwa sababu
alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake, akawaambia, Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa
katika mikono ya watu, nao watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu
atafufuka. Lakini hawakulifahamu neno lile, wakaogopa kumwuliza. “
-
Luka 9:43-45 “Wote
wakashangaa, wakiuona ukuu wa Mungu. Nao walipokuwa wakiyastaajabia mambo yote
aliyoyafanya, aliwaambia wanafunzi wake, Yashikeni maneno haya masikioni mwenu,
kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu. Lakini
hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao wasilitambue; wakaogopa kumwuliza
maana yake neno lile.”
Unaona Yesu
alikuwa na kusudi maalumu la kurejea tena na tena kuhusiana na tukio hili, na
anaeleza hivi mbele ya wanafunzi wake ili kwamba wapate kuamini litakapotukia.
Yohana 14: 28-29 “Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, Naenda zangu, tena naja
kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba, kwa maana
Baba ni mkuu kuliko mimi. Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi
litakapotokea mpate kuamini.”
Kwanini Yesu
alirejea tena na tena tukio hili sio tu wanafunzi wake wapate kumuamini lakini
pia ijulikane wazi kuwa alikuwa akiyatoa maisha yake yawe fidia ya wengi na
kuleta ukombozi wa Mwanadamu, kwa Msingi huo kuna uwezekano mkubwa sana maadui
wa Yesu Kristo walikuwa wamesikia Yesu akizungumza wazi wazi kuhusiana na swala
hili na hivyo alipokufa walitaka kuhakikisha kuwa wanalidhibiti kaburi la Yesu
ili wanafunzi wake wasije wakamuiba na kudai kuwa amefufuka kama alivyosema na
hapo ndipo kukawa na mikakati ya kuhakikisha Kaburi la Yesu linawekwa muhuri na
kuwekwa walinzi kuhakikisha kuwa halibatiliki neno. Kwa Msingi huo leo
tutachukua Muda kutafakari kwa kina somo hili lenye kichwa YULE MJANJA ALISEMA SIKU YA TATU NITAFUFUKA. Tutajifunza somo hili
muhimu kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Maana ya maneno yule mjanja.
·
Jinsi Kaburi la Yesu lilivyopewa Ulinzi mkali.
·
Yule Mjanja alisema siku ya tatu nitafufuka.
Maana ya maneno Yule mjanja.
Tunasoma katika
kifungu cha Msingi maneno haya Mathayo
27:62-66 “Hata siku ya pili, ndiyo iliyo baada ya
Maandalio, wakuu wa makuhani, na Mafarisayo wakamkusanyikia Pilato, wakasema,
Bwana, TUMEKUMBUKA KWAMBA YULE MJANJA ALISEMA, ALIPOKUWA AKALI HAI, BAADA YA
SIKU TATU NITAFUFUKA. Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya
tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika
wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza. Pilato akawaambia, Mna
askari; nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo. Wakaenda, wakalilinda kaburi
salama, kwa kulitia lile jiwe muhuri, pamoja na wale askari walinzi.”
Tunaona Neno yule
Mjanja likitumika hapa, kabla ya kuzungumza mambo mengine nataka tuchukue muda
mfupi kuangalia neno hili walilolitumia dhidi ya Yesu Kristo kwa kumuita mjanja
neno Mjanja linalotumika hapo katika kiingereza linatumika neno DECEIVER
Na katika kiyunani linatumika
neno PLANOS ambayo kwa ujumla yana
tafasiri mbaya na chafu, kwa kiingereza linatumika neno Misleader, Seducer, na Neno hili limetumika kama mara 4
katika biblia ya kiingereza, Kwa ujumla ni neno baya sana lililotumiwa kwa Yesu
Kinyume kabisa na Sifa Halisi alizokuwa nazo, Neno Deceiver ufafanuzi wake
katika kiingereza ni a Liar, Fraud,
Cheat, fake, betrayer, crook, Pretender na deluder Kwa ujumla wanazungumza Kwamba Yesu
alikuwa ni Tapeli au mtu anayepotosha
watu, kwa uwongo, kutunga, kudanganya, kupika majungu, kusaliti, kuigiza,
Mwongo, Haya yalikuwa ni maneno ya viongozi waliokuwa wamejawa na uchungu
sana na kutoa neno kali sana kwa Yesu licha ya kuwa wakati huu walikuwa
wamemuua kwa hila lakini bado waliendelea kuzungumza mambo mabaya kumuhusu kwa
kusudi la kuchafua utu wake na tabia yake Yesu anatajwa katika maandiko kama:-
Yohana 14:6 “Yesu
akamwambia, Mimi ndimi njia, na KWELI, na
uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.”
Yohana 1:14 “Naye
Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama
wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na KWELI.”
Yohana 16:13 “Lakini
yeye atakapokuja, huyo Roho wa KWELI,
atawaongoza awatie kwenye KWELI yote; kwa
maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena,
na mambo yajayo atawapasha habari yake.”
Ufunuo 3:14 “Na
kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye
Amina, Shahidi aliye MWAMINIFU NA WA KWELI,
mwanzo wa kuumba kwa Mungu.”
Muda
usingelitosha kuona jinsi maandiko yanavyomtaja Yesu kuwa ni kweli na
Mwaminifu, kwa msingi huo wivu na chuki za maadui wa Yesu Kristo, uliwasukuma
kushughulika naye wakimuita mjanja kwa kusudi la kumdhalilisha na
kumuhakikishia Pilato kuwa Yesu alikuwa Mzushi tu na hakuwa mkweli wakati Yesu alizaliwa kwa kusudi la
kuishuhudia kweli
Yohana 18:37-38 “Yesu akajibu, Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama
ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije
nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa. Basi Pilato
akamwambia, Wewe u mfalme basi? Yesu akajibu, Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni
mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na KWA AJILI YA HAYA MIMI NALIKUJA
ULIMWENGUNI, ILI NIISHUHUDIE KWELI. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti
yangu.Pilato akamwambia, Kweli ni nini? Naye akiisha kusema neno hilo
akawatokea Wayahudi tena, akawaambia, Mimi sioni hatia yo yote kwake.”
Hata hivyo
kutokana na ujinga waliokuwa nao na ufahamu waliokuwa nao Pilato aliwataka
walilinde kaburi kwa nguvu zote kwa kadiri wawezavyo na kuliwekea kaburi hilo
Muhuri ili huyo wanayedai kuwa ni mjanja yeye au wanafunzi wake wasiweze
kufanya jambo lolote kinyume na wanavyofikiri au kinyume na alivyosema !
Jinsi Kaburi la Yesu lilivyopewa
Ulinzi mkali
Kutokana na madai
ya wazee wa Sanhedrin (Mahakama ya juu ya kiyhahudi) kupeleka madai hayo kwa
Pilato tunaona amri ikitolewa kufanyika kwa ulinzi maalumu wa Kaburi la Yesu
ili isiwe kama alivyosema.
Mathayo 27:64-66 “Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya
tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika
wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza.PILATO AKAWAAMBIA, MNA
ASKARI; NENDENI MKALILINDE SALAMA KADIRI MJUAVYO. Wakaenda, wakalilinda kaburi
salama, kwa kulitia lile jiwe muhuri, pamoja na wale askari walinzi.”
Ni jambo la
kusikitisha sana na kushangaza kuwa maadui wa Yesu Kristo hawakuridhika kwamba
wamefanya fitina na kuhakikisha kuwa Yesu anakufa Msalabani, wakuu hawa wa
makuhani na wazee siku ile ya pili ilikuwa ni sabato, lakini jambo la
kusikitisha ni kuwa walikuwa tayari kuongeza dhambi juu ya dhambi siku ambayo
walipaswa kuishika sabato na wakati wanafunzi wa Yesu na watu wengine wametulia
wao walikuwa na mkakati wa kumdhibiti Yesu zaidi, mioyo yao ilikuwa imejawa na
uovu na chuki kubwa sana hata pale ambapo Yesu alikuwa amekufa, Dunia ya leo
pia imejawa na watu wanaopingana na maswala ya Mungu na kushindana na watumishi
wa Mungu wa kweli na hata pale unapoamua kunyamaza kimya bado wako watu
watatafuta kukuchafua, kumekuwako na watu waovu, wasiomcha Mungu, wasiotenda
haki, waliojawa na wivu na uovu wa kila aina ambao kazi yao kubwa ni kupingana
na Mungu na watumishi wake na wengine wakijifanya ni watumishi wa Mungu, ni
jambo la kusikitisha kuona Viongozi wa Dini tena siku ya sabato Yesu akiwa
kaburini bado wanaendelea kumfuatilia na kushitaki kwa Pilato na Pilato
aliamuru Kaburi lilindwe kwa kadiri iwezekanavyo, Ukiona bado watu wanakusema
vibaya hata baada ya wewe kuondoka au kufa ujue wewe umeacha historia ya kuigwa
aidha kwa wema au kwa ubaya, tunaweza kumkumbuka Hitler kwa sababu ya ukatili
wake wa kuua watu wengi, tunaweza pia kumkumbuka Idd Amin kwa ukatili wake
lakini vilevile tunaweza kuwakumbuka watu wema kupitia wema wao, lakini ukiona
mtu mwema anachafuliwa hata baada ya kifo chake au yeye mwenyewe akiwa hayupo
ujue mtu huyo ameacha rekodi (legacy) isiyokuwa ya kawaida na hata ingawa
hayupo bado ni tishio,
1.
Kaburi liliwekwa Muhuri – “Seal” – Ni muhimu kufahamu hapa tunapozungumza kuhusu
Muhuri hatuzungumzii ule muhuri ambao watu wamezoea, kizazi cha leo kinajua
Muhuri ule waliozoea kuiona ikiwepo Ofisini, na wino wake, Muhuri hii
inayotajwa katika Biblia ikiwepo kule katika kitabu cha Ufunuo ni aina ya Kamba
maalumu au nyororo maalumu inayofungwa na chuma katika kitu kinachomilikiwa na
Serikali ikiwa na alama ya marufuku kufunguliwa na mtu mwingine, Muhuri hiyo ni
alama ya ulinzi na usalama mfano serikali inapoweka umeme katika nyumba Mita ya
umeme ni mali ya shirika na hivyo
hufungwa na Kamba au waya maalumu na kubanwa ili kwamba mtu mwingine asiweze
kufungua, hali kadhalika mita ya maji, na ikiwa muhuri itaharibiwa maana yake
amri halali ya kiulinzi imehalifiwa, na hatua kali za kisheria zinaweza
kuchukuliwa dhidi ya mtu aliyevunja muhuri hiyo, wanaoweza kufungua Muhuri hiyo
ni wale tu waliofunga, kwa kiyunani
Muhuri hiyo huitwa SPHRAGIZO. Kwa
hiyo unaposikia kuwa Kaburi liliwekwa Muhuri maana yake kuna aidha kuna Kamba
maalumu zilihusika kulifunga kabisa kaburi, ili isitokee mtu akasogeza lile
jiwe na au lilisilibwa kwa simenti ili kuliunga kaburi hilo kusipatikane upenyo
wowote wa kitu kupita, au alama
inayowekwa kuthibitisha kuwa hakuna uharibifu wowote unaoweza kufanyika ni
tukio kama hili lilifanywa kwa nabii Daniel kuhakikisha kuwa anabaki katika
tundu la Simba ona
Daniel 6:15-17“Ndipo watu wale wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme,
wakamwambia mfalme, Ee mfalme, ujue ya kuwa ni sheria ya Wamedi na Waajemi,
lisibadilike neno lo lote lililo marufuku, wala amri yo yote iliyowekwa na
mfalme. Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, wakamtupa katika tundu
la simba. Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Mungu wako unayemtumikia daima,
yeye atakuponya. Likaletwa jiwe, likawekwa mdomoni mwa lile tundu; naye mfalme
akalitia muhuri kwa muhuri yake mwenyewe, na kwa muhuri ya wakuu wake,
lisibadilike neno lo lote katika habari za Danieli.”
Muhuri huu ulikuwa ni alama ya kuhakikisha
kuwa hakuna mabadiliko yoyote yanayoweza kufanyika kinyume na kile ambacho
serikali imekiamua na kuwa hakuna kutoka ndani ya kaburi au pango kwa msaada wa
kibinadamu isipokuwa kama mfalme au aliyetoa amri atabatilisha, kwa hiyo kitu kilipowekwa
muhuri ilimaanisha lisibatilike neno katika jambo lolote ambalo limeamuriwa
labda Mungu aingilie kati.
2.
Kaburi liliwekewa ulinzi mkali sana – Utafiti wa kibiblia na kihistoria unakubaliana
na ukweli kuwa hakuna askari walikuwa na utii kama askari wa Kirumi, na katika
tamaduni za kirumi kama askari waliagizwa kulinda kitu na kitu hicho
kikabainika kuwa hakikulindwa ipaswavyo hukumu yake ilikuwa ni kifo tu na kwa
sababu hiyo wakati mwingine askari waliweza kuamua kujiua wenyewe kuliko
kushughulikiwa na serikali angalia
-
Matendo ya Mitume 12:4-19 “Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi
mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka
kumtoa na kumweka mbele ya watu. Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa
likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake. Hata wakati Herode alipotaka
kumtoa, usiku ule ule Petro alikuwa analala katikati ya askari wawili,
amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakailinda gereza. Mara
malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani, akampiga
Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka
mikononi. Malaika akamwambia, Jifunge, kavae viatu vyako. Akafanya hivyo. Kisha
akamwambia, Jivike nguo yako, ukanifuate. Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua
ya kuwa ni kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani kwamba anaona maono. Na
walipopita lindo la kwanza na la pili, wakaja hata mlango wa chuma wa kuingilia
mjini, ukawafungukia wenyewe. Wakatoka nje, wakapita katika njia moja; mara
malaika akamwacha. Hata Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya
kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika
kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi. Na alipokuwa akifikiri haya akafika
nyumbani kwa Mariamu, mamaye Yohana, ambaye jina lake la pili ni Marko; na watu
wengi walikuwa wamekutana humo wakiomba. Naye alipobisha kilango cha lango,
kijakazi, jina lake Roda, akaja kusikiliza. Alipoitambua sauti ya Petro, hakukifungua
lango, kwa ajili ya furaha, bali alipiga mbio, akaingia ndani akawaambia kwamba
Petro anasimama mbele ya lango. Wakamwambia, Una wazimu. Lakini yeye akakaza
sana, akasema ya kwamba ndivyo hivyo. Wakanena, Ni malaika wake. Petro
akafuliza kugonga, hata walipokwisha kumfungulia wakamwona, wakastaajabu. Naye
akawapungia mkono wanyamaze, akawaeleza jinsi Bwana alivyomtoa katika gereza.
Akasema, Kampasheni Yakobo na wale ndugu habari hizi. Akaondoka, akaenda mahali
pengine. Hata kulipopambauka askari wakaingiwa na fadhaa nyingi, amekuwaje
Petro. Na Herode alipomtafuta, asimwone, aliwauliza-uliza wale walinzi,
akaamuru wauawe. Kisha akatelemkia kutoka Uyahudi kwenda Kaisaria, akakaa huko.”
-
Matendo ya Mitume 16:25-27 “Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa
wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa
wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza
ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa.Yule
mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka,
alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia.”
Kwa msingi huo
unaweza kupata picha kuwa licha ya kuwepo kwa Muhuri lakini vile vile kaburi la
Yesu lilikuwa na ulinzi mkali sana, kuna uwezekano walikuwepo askari zaidi ya
16 na kwa taratibu za kirumi askari asipotimiza wajibu alitakuwa kuuawa na ndio
maana unaona hata mkuu wa gereza aliyekuwa akiwashikilia Paulo na Sila alitaka
kujiua yeye mwenyewe kwa sababu ilieleweka wazi kuwa kama ameshindwa kutimiza
wajibu katika kulinda kile alichotakiwa kukilinda basi hukumu yake ni kifo, kwa
msingi huo tamaduni hii inatuhakikishia kuwa Kaburi la Yesu lililindwa bara
bara na ilipaswa kuwa hivyo maana wao waliona Yesu kuwa ni Mjanja, mwongo,
tapeli na mzushi kwa hiyo ulinzi wao ulikuwa ni wa kuhakikisha kuwa huyo mjanja
hatoki!
Yule Mjanja alisema siku ya tatu
nitafufuka
Ukweli ni kuwa
wazee wale walikuwa wanafanya ujinga, Mungu alikuwa anataka wao wenyewe ndio
wawe mashahidi wa Kwanza wa kufufuka kwake Kristo, Kumbuka pamoja na Yesu
kurudia rudia kuwa atasulubiwa na kuuawa na siku ya tatu atafufuka jambo hili
lilikuwa zito kueleweka kwa wanafunzi wa Yesu, lakini maadui wa Yesu walikuwa
wanakumbuka na sasa wanafanya makakati wa kulilinda kaburi kama tulivyoona
lilikuwa jambo jema kwao.
Hawakuwa wanajua
kuwa wanashughulika na mtu ambaye Kifo hakiwezi kumzuia, walikuwa wakishughulika
na Mwenyewe ambaye ni ufufuo na uzima, mwenye mamlaka ya mauti na uzima! Na ambaye makusudi yake hayawezi
kuzuiliwa kamwe
Yohana 11:24-25 “Martha akamwambia, Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo
siku ya mwisho. Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye
aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi;”
Huwezi kumuwekea
mipaka mwanaume mwenye funguo/Mamlaka ya mauti na uzima Ufunuo 1:17-18 “Nami nilipomwona,
nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu
yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami
nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo
za mauti, na za kuzimu.”
Yesu alifufuka,
kufufuka kwake kunatoa ujumbe kuwa hakuna kitu wala mtu anaweza kuzuia kusudi
la Mungu katika maisha yako, kama jinsi ambavyo hawakuweza kuzuia kusudi la
Mungu kumfufua Yesu Kristo, Mungu ni mwenye nguvu ya kufufua anauwezo wa
kuondoa lolote lililokufa na kulirudishia uhai, anauwezo wa kubadilisha huzuni
kuwa furaha, anauwezo wa kubadilisha maombolezo kuwa machezo, kama jinsi
ambavyo viongozi wa dini na askari na wazushi walishindwa kuzuia Yesu asifufuke
nataka nikutangazie kuwa Roho Mtakatifu amenituma nikutangazie kuwa haijalishi
wachawi wameweka muhuri ya namna gani, haijalishi kuwa wapiga majungu wamepiga
kwa kiasi gani, hauijalishi kuwa wafitini wamefitinisha kwa kiwango gani,
hajalishi kuwa umekandamizwa kwa kiasi gani, Mungu atamtuma malaika wake
aliyezivunja zile muhuri na kudongolosha lile jiwe linalosimama kama kizuizi
katika maisha yako na utatoka tena nasema utatoka tena nasema utainuka, adui
zako wanataka kuhakikisha ya kuwa unalala, wanataka kuharibu sifa na wema wako
uonekane kuwa wewe ni mjanja mjanja tu, wanatangaza mwisho wako na kudhani ya
kuwa wamekudhibiti na kuwa huwezekani kuinuka tena Lakini Roho Mtakatifu anatangaza mwanzo wako leo
katika jina la Yesu Kristo wa Nazareth aliye hai, hakuna jini, hakuna maimuna,
hakuna makata wala kinyamkera, hakuna pepo, hakuna mganga, hakuna mchawi,
hakuna hirizi, hakuna pembe, hakuna zindiko, hakuna uchawi, hakuna mamlaka,
hakuna jeshi, hakuna askari hakuna, hakuna hakuna kizuizi chochote
kitakachozuia kusudi la Mungu katika maisha yako, wakati ambapo ujanja
ulitumika kama neno la kejeli leo tunaligeuza kuwa sisi tulio ndani ya Yesu ni
wajanja kweli kweli, sisi sio wa kawaida, tumewekwa katika ulimwengu wa roho pamoja na Kristo, tumekufa
pamoja naye, tumefufuka pamoja naye, tunatawala pamoja naye hivyo ndivyo neno
la Mungu linavyotuambia:-
Waefeso 2:6 “Akatufufua
pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho”,
Katika Kristo Yesu;
kila anayemuamini Yesu yuko juu, ameinuliwa amefufuka pamoja naye sisi sio wa
kawaida, hakuna anayeweza kushindana na mapenzi ya Mungu katika maisha yetu,
hakuna anayeweza kuhakikisha kuwa tunabaki kaburini, hakuna wa kutuzuia, hakuna
wa kutuzibia, hakuna wa kulinda na kumzuia Mungu mwenye nguvu, Mungu wa baba zetu
anayahuisha tena maisha yetu na kutuweka mahali salama Kristo alitoka kwa
mkwara kaburi lilitetemeka muhuri zikavunjwa na malaika akalivingirisha jiwe na
akalikalia jiwe, walinzi wakawa kama wafu kiwewe kiliwashika, Yesu ni aliye hai
katika wafu, wewe na mimi tu hai leo haleluyaaa! Wakati adui zetu wakikesha
kuhakikisha hatuamki ni wao ndio watakaokuwa wafu wakati sisi tunafufuka!,
Maandiko yanaonyesha kuwa walinzi wa kirumi safari hii hawakuweza kutimiza
wajibu wao malaika wa Bwana alilivingirisha jiwe akalikalia, alivunja mihuri
yao, alibatilisha matakwa yao Yesu alifufuka na hakuibiwa mwanaume wa wanaume
kaburi halikumuweza, Alifufuka kwelikweli!, Nampenda Mungu nampenda Yesu
mipango yao huiweka wazi kabisa kwa sababu hakuna anayeweza kuzuia mpango wa
Mungu, Mtu mmoja aliniambia usiweke wazi mipango yako wala usimwambie mtu ndoto
zako kwa sababu wanadamu ni waovu wanaweza kwenda kuzuia mipango yako au kupigana
nayo, sielewi anatumia andiko gani lakini Tabia ya Mungu huweka wazi mipango
yake hueleza mapema siku ya tatu nitafufuka na hakuna wa kuzuia, Kama ndoto
zangu ni mpango wa Mungu hata nikiweka wazi hakuna wa kuzuia, kama mipango
yangu ni mipango ya Bwana hakuna wa kuzuia, mbona walijaribu kumuua mwenye
ndoto Yusufu ili kuua ndoto zake na Je ziliztimizwa hazikutimizwa? Hekima ya
Mungu sio kama hekima ya wapuuzi wa dunia hii, Mungu akiwa na mpango na jambo
lake hata mroge kwa ramba ramba, chaumbeya au tekelo, au uende kwa waganga kule
Pemba, au Newala kule Nchedebwa, au Nachingwea, au Lamu, au Kwasemangube, au
Kwamsisi huko Handeni, au Sumbawanga kokote unakoweza kwenda huwezi kuzuia
makusudi na mpango wa Mungu, Mungu ni mwenye nguvu angalia walipozuia na
kulilinda kaburi kwa ulinzi wao wote maandiko yanasema kulitoka tetemeko kubwa
la nchi, malaika alishuka akalivingirisha jiwe na kulikalia, wapinzani wakawa
kama wafu hivi ndivyo Mungu wentu anavyofanya mambo yake !
Mathayo 28:2-4 “Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa sababu
malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe
akalikalia. Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji.
Na kwa kumwogopa, wale walinzi wakatetemeka, wakawa kama wafu.”
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni