Luka 13:10-13 “Siku ya sabato alikuwa
akifundisha katika sinagogi mojawapo. Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa
na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi
kujinyosha kabisa.Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa
katika udhaifu wako. Akaweka mikono yake
juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu.”
Utangulizi:
Katika moja ya miujiza kadhaa mikubwa
aliyoifanya Bwana Yesu, Moja ya muujiza wa muhimu sana ni pamoja na huu wa
kuponywa kwa mtu mwenye kibiongo.(Ugonjwa wa kupindana kwa mgongo) Luka 13:10-13 “Siku
ya sabato alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo. Na tazama, palikuwa na
mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye
amepindana, hawezi kujinyosha kabisa. Yesu alipomwona alimwita, akamwambia,
Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako.
Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu.”
Ugonjwa huu wa kibiongo au
ugonjwa wa kupindana mgongo ni moja ya ugonjwa mbaya sana sana katika historia
ya magonjwa duniani, na kwa bahati nzuri
Yesu Kristo alikuwa haponyi ilimradi tu, utaweza kuona miujiza mingi
aliyoifanya Kristo aliifanya kimkakati, aidha kwa watu walioteseka sana na
kupoteza matumaini ili awasaidie, au kwa kusudi Mungu atukuzwe na watu wapate
kumuamini, na pia kwaajili ya kutufundisha!, Muujiza huu wa kuponywa kwa mtu
mwenye kibiongo, una maswala kadhaa ya kutufundisha yanayoonyesha namna Mungu
anavyoshughulika na watu wake hasa ambao wanapitia hali ngumu sana, leo
tutachukua Muda kuuangalia muujiza huu, kwa kuzingatia vipengele vitatu
vifuatavyo:-
·
Ufahamu
kuhusu ugonjwa wa kupindana mgongo (Kibiongo)
·
Kuponywa
kwa mtu mwenye kibiongo
·
Mambo ya
kujifunza kupitia muujiza huu
Ufahamu
kuhusu ugonjwa wa kupindana mgongo (Kibiongo)
Ugonjwa wa kupinda mgongo (kibiongo)
ni mojawapo ya magonjwa mabaya sana duniani, ugonjwa huu kitaalamu unaitwa CAMPTOCORMIA ambapo kwa kawaida
wanaopatwa na ugonjwa huu huwa na muonekano wa kupinda usiokuwa wa kawaida
anaposimama, na unaweza kuonekana zaidi anapotembea, ni ugonjwa unaotokana na
muundo mmbaya unaojitokeza kutokana na kupinda kwa mbele au kwa nyuma kwa uti
wa mgongo, Neno hilo CAMPTOCORMIA limetokana na
neno la Kiyunani KAMPTOS ambalo maana yake ni BENT FORWARD au BENT BACKWARD kwa
kawaida jina la kawaida kwa kiingereza ni
“Bent spine syndrome” kupinda kwa mgongo. Ni ugonjwa mbaya na unapoteza
kabisa “shape” muonekano wa mtu, Ugonjwa
huu sio tu kuwa haujulikani sababu zake lakini pia hauna matibabu maalumu zaidi
ya kuwaona wataalamu wa mifupa (Physiotherapy)
ambao watakuwa wakimpatia mgonjwa matibabu ya kimazoezi tu, ugonjwa huu sio tu
unaweza kujitokeza kwa mtu kufutukia kifuani na kudidimia sehemu ya nyuma ya
mgongo, au kuwa na umbile kama la upinde mgongoni unaofikia nyuzi 45 na
kumfanya mtu huyo kuinama hata asiweze kuiona mbingu au kumchungulia mtu usoni,
kwa ujumla ukiacha kuwa mtu mwenye ugonjwa huu hapandezi unapomuona, lakini
vilevile unaweza kuhisi maumivu anayoyapata mtu aliyepindana wakati mwingine
uti wa mgongo wa mtu mwenye ugonjwa huu unaweza kujichora kama umbo la S na
na wakati mwingine unaweza kusababisha bega moja la mtu huyo likawa juu
na lingine chini, au mbavu zake zikaonekana zimeinama upande mmoja, Nguo za
kawaida hazimkai vizuri mtu wa jinsi hiyo kwa ujumla ni ugonjwa wa kusikitisha,
madaktari wanasema ugonjwa huu unaweza kujitokeza kwa mtu anapoanza kubalehe
hasa wanawake na kwa sababu hiyo wanaoshambuliwa sana ni wanawake kwa wingi na
wanaume wa uchache, kwa kuwa mpaka sasa hakuna anayejua sababu za ugonjwa huu,
Lakini Luka kwa vile alikuwa ni tabibu anaelezea kuwa ugonjwa huu unatokana na UDHAIFU lakini Luka anaelezea wazi
kuwa ni udhaifu uliosababishwa na shetani
na tunaelezwa kuwa alikuwa katika hali hiyo kwa miaka 18, Ugonjwa huu
unaambatana kwa mbali na hali ya udumavu kwa ujumla wake ni ugonjwa mmbaya sana
ona:-
Luka 13:10-13 “Siku ya sabato alikuwa
akifundisha katika sinagogi mojawapo. Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa
na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi
kujinyosha kabisa. Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa
katika udhaifu wako. Akaweka mikono yake
juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu.”
Luka ni tabibu, ni Daktari wa
binadamu aliyeokoka hivyo anaelewa wazi kuwa kuna udhaifu wa kawaida na udhaifu
unaosababishwa na Shetani, au mapepo, na Luka aliweza kujua udhaifu ule
kitabibu hauwezi kuponyeka wala kuutibika lakini kujua kuwa ni Pepo inawezekana
ni kutokana na Tabibu mkuu Yesu Mwenyewe kuwafunulia watu kuwa mateso ya mama
yule yalitokana na kifungo cha shetani kumbuika maneno yale “Na huyu mwanamke, aliye
wa uzao wa Ibrahimu, ambaye Shetani amemfunga miaka kumi na minane” ona
Luka 13:11-17 “Na tazama, palikuwa na
mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye
amepindana, hawezi kujinyosha kabisa. Yesu alipomwona alimwita, akamwambia,
Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako. Akaweka mikono yake juu yake, naye
akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu. Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa
sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato, akajibu, akawaambia mkutano, Kuna
siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si
katika siku ya sabato. Lakini Bwana akajibu akasema, Enyi wanafiki, kila mmoja
wenu, je! Hamfungui ng'ombe wake au punda wake siku ya sabato katika zizi,
aende naye kumnywesha? Na huyu mwanamke, aliye wa uzao wa Ibrahimu, ambaye
Shetani amemfunga miaka kumi na minane hii, haikupasa afunguliwe kifungo hiki
siku ya sabato? Aliposema haya wakatahayari wote walioshindana naye; mkutano
wote wakafurahi kwa sababu ya mambo matukufu yaliyotendwa na yeye.”
Unaona maelezo ya Luka ya awali
yametokana na maelezo ya Yesu mwenyewe Kwamba mwanamke yule alikuwa amefungwa
na Shetani kwa miaka 18, tena Yesu anamtaja kuwa mwanamke wa Uzao wa Ibrahimu,
hii inaonyesha wazi kuwa kulikuwa na uonevu wa Ibilisi, tena bila kujali kuwa
huyu binti ni wa uzao wa Ibrahimu, maana yake nini unaweza kuwa Mkristo na bado
ukafungwa katika vifungo na uonevu wa ibilisi, unaweza kuwa wa uzao wa Ibrahimu
yaani mtu wa Imani, Binti huyu alikuwa na imani, angalia kuwa alikuwa
anahudhuria ibada alifika kwenye Sinagogi, siku ya sabato, lakini alikuwa
anaonewa, viongozi wake wa dini hawakuweza kumsaidia, Ashukuriwe Mungu kwamba
Mgeni rasmi alikuweko kwenye ibada siku ile, Yesu Kristo mtenda miujiza
alikuwepo kwenye singagogi, kuhudhuria ibada pekee hakutoshi, kuwa wa uzao wa
Ibrahimu pekee hakutoshi, kuwa na imani ya Ibrahimu pekee hakutoshi,
tunamuhitaji Yesu Kristo aliye hai, Tunamtaka Bwana na nguvu zake, yako mambo
kibinadamu sio ya kawaida hata kama tunayaona ya kawaida, yako mambo ambayo
yako juu ya uwezo wetu ni Yesu pekee ndiye anayeweza kujua sababu ya mambo hayo
kumbe mengine ni uonevu wa ibilisi unadhani nani angelijua, yako mambo hata
madaktari hawajui ni kwanini, Lakini maandiko yanatukumbusha kuwa Yuko Yesu
ambaye maalumu sana anaweza kuyachukua madhaifu yetu na kujitwika na kutupa
unafuu bila kujali wataalamu wanasemaje.
Mathayo 8:16-16 “Hata kulipokuwa jioni,
wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote
waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema,
Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu.”
Haijalishi una udhaifu wa namna
gani na umeteseka kwa miaka mingapi, lakini maandiko yanaonyesha kuwa ni kazi
yake Yesu kuponya madhaifu na magonjwa yetu, kwa hiyo kila mwanadamu bila
kujali historia yake, kabila lake, ana uzuri kiasi gani ana ubaya kiasi gani
maandiko yanatukumbusha leo kumwangalia Yesu kwa mambo ambayo madaktari na
matabibu wa kawaida wameshindwa, Yeye atakuweka huru na kukufungua kutoka
katika udhaifu wako
Kuponywa
kwa mtu mwenye kibiongo:
Nadhani baada ya kuelezea ugonjwa
aliokuwa nao mwanamke huyu wewe mwenyewe unaweza kupata hisia za mateso yake,
kwamba alikuwa anateseka kiasi gani, na chukulia kama mwanamke wa aina hii ni binti
yako! Au dada yako au mama yako! Au mkeo? Ungejisikiaje? Mateso haya sio tu
yalikuwa ya mwilini lakini vilevile na kisaikolojia huenda alichekwa na watu,
na sio hivyo tu hata familia yake huenda ilichekwa, au watu walimkwepa, au sio
rahisi kuchumbiwa na kuolewa kulikuwa na ndoto nyingi ambazo zilikufa kutokana
na maisha ya mateso aliyokuwa nayo mwanamke huyu, Ashukuriwe Mungu Yesu ni
mwenye huruma sana, Mwanamke huyu aliyekuwa amepindana na hawezi kuinuka Biblia
inasema Yesu alipomuona alimuita mbele, na akamwambia mama umefunguliwa katika
udhaifu wako, na kama haitoshi Yesu akamwekea mikono yake na mara moja mwanamke
yule aliponywa na akanyooka mara moja nakuanza kumtukuza Mungu, kulikuwa na
namna nyingi tu ambazo Yesu angeweza kufanya angelituma neno, angekemea pepo,
lakini Yesu akiwa amejawa na huruma, alimuita kitendo cha kuitwa mbele
kilimfanya mwanamke yule ajue wazi kuwa ile ilikuwa ni siku yake, na kuwa Yesu alionyesha kuwa anamjali, labda
alisikia habari za Yesu na matendo yake makuu, aliwaza ni lini na mimi nitakuja
kukutana na mtu huyo na aniponye? hakua na matumaini, lakini Hakuna jambo zuri
duniani kama kuitwa na mtu mkubwa wa kiwango cha Kristo na sio hivyo tu Yesu
alitamka neno na mwisho akaweka mikono yake juu yake, Mwanamke huyu aliponywa
kwa heshima kubwa sana sio lazima
wakati wote muhubiri akuwekee mikono, lakini Yesu alitaka kumuonyesha upendo
wake mtu huyu alitaka kuponya na nafsi yake iliyoumizwa, alitaka kuinyesha kuwa
yuko mmoja anayemjali, unaposoma juu juu utaweza kudhani kuwa Labda Yesu alifanya
muujiza huu kuonyesha nguvu yake juu ya sabato, au juu ya viongozi wa dini, au
kuonyesha nguvu yake juu ya shetani lakini stori hii ni kwajili ya upendo,
kwaajili ya mateso, kwaajili ya kumuhurumia mtu mwenye fadhaa kubwa na nzito
isiyo na tabibu kumtoa katika kifungo cha ibilisi angalia maneno yale UMEFUNGULIWA KATIKA UDHAIFU WAKO!, You are
set Free from your infirmity ! Kusudi
letu kubwa au langu kubwa kubwa ni kuonyesha kuwa ibada za maombezi haziko
kwaajili ya kuonyesha nguvu za Mungu au nguvu za Muhubiri, au kuonyesha kuwa ninasikiwa
na Yesu kwa kiwango gani, ua ninatymiwa na Mungu, au kujitafutia umaarufu,
nataka watu wawe huru kwa sababu sifurahii kuona mateso, Huu ndio ulikuwa moyo
wa Yesu Kristo, Roho Mtakatifu alikuwa amempaka mafuta na kumtumia kwa kusudia
la kuwafungua watu wanaoonewa!
Luka
4:18-19 “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana
amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia
wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru
waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”
Matendo
10:38 “habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu
alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko,
akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu
alikuwa pamoja naye.”
Nia kubwa ya Yesu Kristo ni kuwasaidia
watu, hakufurahi Mwalimu kuona watu wanaoonewa na Ibilisi, watu wa Mungu
tumtafute Mungu, tutafute nguvu zake ili watu wanaoonewa kila mahali na hata
makanisani mwetu na katika masinagogi, wapate kutoka katika uonevu wa ibilisi,
haiwezekani watu wa Mungu wawe wanadhalilika na sisi tupo na Mungu ametuweka
kwaajili ya kuwasaidia. Kristo Yesu alisikitishwa sana na viongozi wa dini na
sinagogi ambao hata ibada ya uponyaji wa mwanamke huyu kwao ilikuwa kama kwazo
ona
Luka
13:14-17 “Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa
sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato, akajibu, akawaambia mkutano, Kuna
siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si
katika siku ya sabato. Lakini Bwana akajibu akasema, Enyi wanafiki, kila mmoja
wenu, je! Hamfungui ng'ombe wake au punda wake siku ya sabato katika zizi,
aende naye kumnywesha? Na huyu mwanamke, aliye wa uzao wa Ibrahimu, ambaye
Shetani amemfunga miaka kumi na minane hii, haikupasa afunguliwe kifungo hiki
siku ya sabato? Aliposema haya wakatahayari wote walioshindana naye; mkutano
wote wakafurahi kwa sababu ya mambo matukufu yaliyotendwa na yeye.”
Unaweza kuona nia ya Yesu hapa wala
haikuwa shindano la sabato, Yesu alitaka kuonyesha uchungu aliokuwa nao kwa
mwanamke aliyekuwa amefungwa, siku sita za kufanya kazi sio siku za ibada ni
siku za watu kujitafutia mahitaji yao, na sabato ndio siku ya ibada watu
wanajihudhurisha nyumbani kwa Bwana, nadhani
Yesu anatuonyesha siku ya bwana inavyopaswa kutumika, siku ya ibada
yako, Leo hii unaweza kwenda kanisani na sio kibiongo, lakini ukawa tu
umevunjika moyo na unakutana na watumishi wa Mungu waliojaa hasira, wanafokea
watu, wanashushua watu, unatoka katika ibada ulikuja na majanga yako na badala
ya kugangwa unatoka ukiwa umeumizwa moyo, watumishi wa Mungu ni lazima tuchague
maneno ya kusema siku za ibada, kama unaona moyo wako hauko vizuri basi
afadhali uache kuhudumu, wazee mnaotangaza matangazo, hakikisha kuwa
mnazungumza kwa busara msiwaharibie watu ibada, Mwanamke huyu ilikuwa ni siku
yake ya furaha na hata watu wa kawaida walifurahi na kumtukuza Mungu anakuja
mtu kufunga ibada anabwatuka NABANA PUA
HAPA “Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi
njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato.” MWISHO
WA KUBANA PUA. Ashukuriwe Yesu ni kiongozi mzuri wa ibada alihakikisha watu
wanatoka ibadani wakimtukuza Mungu! Siku ya ibada ni lazima itumike kwa busara
kunganga mioyo ya watu na sio kuwakwaza, kuwainua walioinama na sio
kuwainamisha, Yesu alikuwa akionyesha matumizi sahihi ya siku ya Bwana,
haipaswi kuwa siku ya kukandamiza watu na tafasiri mbaya za sharia bali ni siku
ya kuweka watu huru kutoka katika majanga ya maisha yanayowasibu sikuhadi siku!
Mambo
ya kujifunza kupitia muujiza huu
1.
Tunajifunza kwamba Yesu Kristo aliongozwa na
upendo katika kila jambo alilolifanya, Yesu hakuwahi kufurahi hata siku moja
lolote lile lisimame kinyume na msukumo wake wa upendo, ni kupitia upendo
Karama na utumishi wetu kwa Mungu na kwa watu unapaswa kujengwa katika msingi
huo. 1Wakorintho 13:1-8 “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina
upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na
kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza
kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi.Tena nikitoa mali zangu zote
kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo,
hainifaidii kitu. Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo
hautakabari; haujivuni;haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni
uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli;
huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo
haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha,
zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika.”
2. Ugonjwa huu ulikuwa ni mbaya sana na uliambatana na ubaguzi wa hali ya juu watu wa jinsi hii kama walikuwa wanaume tena wa kabila la lawi hawakuruhusiwa kuwa makuhani kwani Torati iliwatenga na ilionekana ni kama watu waliokataliwa na Mungu ona Walawi 21:17-20 “Nena na Haruni, umwambie, Mtu awaye yote wa kizazi chako wewe katika vizazi vyao, aliye na kilema, asikaribie kusongeza chakula cha Mungu wake. Kwa kuwa mtu awaye yote aliye na kilema hatakaribia; mtu kipofu, au kiwete, au mtu aliye na pua iliyoharibika, au aliye na kitu kilichozidi vimpasavyo mwili, au mtu aliyevunjika mguu, au aliyevunjika mkono, au aliye na kijongo, au aliye kibeti, au aliye na kilema cha jichoni, au aliye na upele, au mwenye buba, au aliyevunjika mapumbu;” Yesu alithibitisha kuwa yuko kwaajili ya watu wa namna hii, alikuwa anafunua wazi kuwa hali ile kamwe sio kazi za Mungu bali ni uonevu wa shetani na kuwa Mungu yuko kinyume na aina zote za uonevu, Kristo alichukizwa na aina hii ya uonevu na akamfungua
3.
Kiongozi wa Sinagogi mwenye roho mbaya –
kutokana na Yesu kutenda mema yeye alikasirika ndivyo maandiko yanavyotuambia,
mtazamo wake kuhusu uponyaji na utendaji wa miujiza anaona kama ni kazi
inayotakiwa kufanyika siku za kawaida na sio siku ya sabato, haishangazi kuwa
na watu wenye ufahamu finyu kuhusu namna na jinsi Mungu anavyofanya kazi, ni
hao hao ambao walikuwa wakifungulia punda kunywa maji au kuokoa mnyama
asidumbukie shimoni siku ya sabato, lakini wanaona mtu kuponywa siku ya sabato
ni ishu, Yesu alikemea tabia hii mbaya, watumishi wa Mungu wanapaswa kuwa na
roho nzuri, huruma na upendo na ufahamu mkubwa kuliko hata wanaowaongoza,
wakati watu wanafurahia matendo makuu ya Mungu inashangaza kuona mkuu wa
sinagogi anakasirika, washirika wa siku hizi wana ufahamu mkubwa sana wa neno
la Mungu hivyo viongozi hawana budi kujiongeza, na kuwa makini kwa
wanachokiongea na hija wanayoijenga kuhusu utendaji wa Mungu na matendo yake ya
huruma kwa watu
4.
Shetani anahusika kuwafunga watu ni kazi ya
watumishi wa Mungu kuutafuta uso wa Bwana na karama za rohoni kwa kusudi la
kuwasaidia watu kwa upendo, aidha katika upendo wake Yesu anaonyesha kuwa
anaweza kuponya changamoto yoyote hata kama ni ya Muda mrefu, kumbuka mwanamke
yule alionewa na ibilisi kwa miaka 18 lakini alipokutana na Yesu ukawa mwisho
wa changamoto zake! Changamoto zako zitafikia mwisho hata bila kujali imechukua
muda mrefu kwa kiasi gani!
5.
Wako watu ambao katika hali ya kawaida
wamenyooka lakini roho zao zimepindana wana kibiongo nao wanahitaji kuhudumiwa
roho zao, Kristo Yesu yupo tayari kuwahudumia watu wake leo, yeye hajabadilika
yeye ni yeye yule jana leo na hata milele, kama moyo wako na roho yako imeinama
huwezi hata kuangalia mbinguni leo kwa mamlaka niliyopewa kama mtumishi wa
Mungu nakutangazia uzima katika jina la Yesu Kristo wa Nazareth aliye hai Bwana
akutane na wewe katika kila eneo la maisha yako, bwana akuinue kutoka katika
kupindana kwako.Bwana akuinue kutoka katika hali ya kuinama kwako kwa namna
yoyote ile Katika jina la Yesu!
6.
Hakuna ugonjwa usiotibika kwa Yesu!, kama
jinsi ambavyo tumejifunza kuhusu ugonjwa wa kibiongo au kupindana kwa mgongo ni
ugonjwa mbaya haujulikani Dhahiri sababu zake na pia hauna tiba, Lakini kufumba
na kufumbua Yesu alipomuombea mwanamke huyu Mwenye kibiongo alisimama pale
pale, hii inatufundisha na kutufunulia kuwa hakuna uogonjwa wwowote ambao
unaweza kusimama mbele za Yesu, uwe unaeleweka kitaalamu, au uwe haueleweki,
uwe una tiba au hauna tiba, linapokuja swala la Yesu kujihusisha na tatizo lako
hakuna linaloshindikana, Yote yawezekana kwa Mungu, Katika jina la Yesu Kristo
tatizo lako leo kwa mamlaka niliyopewa kama Mtumishi wake nakutangaza kuwa
umefunguliwa kutoka katika udhaifu wako kwa jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu
aliye hai Ameeeen!
Na Rev. Innocent Samuel Bin Hamza Bina
Jumaa, Bin bin Athuman Sekivunga Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni