Mwanzo 26:12-16 “Isaka akapanda mbegu
katika nchi ile, akapata mwaka ule vipimo mia kwa kimoja, BWANA akambariki. Na
mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana. Akawa na mali ya
kondoo, na mali ya ng'ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu. Na
vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Ibrahimu babaye,
Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza kifusi. Abimeleki akamwambia Isaka,
Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi.”
Naliweka wakfu somo hili kwa
heshima ya Hayati Edward Ngoyai Lowassa waziri mkuu wa zamani wa Tanzania kwani
somo hili liliandaliwa siku ambayo yeye alikuwa anazikwa.
Utangulizi:
Ni Muhimu kufahamu kuwa wakati mwingine
vita na mapito tunayoyapitia kutoka kwa watu yanatokana na neema ya Mungu
iliyoko juu yetu, Mungu anapokupa kibali na baraka mbalimbali Baraka hizo au
neema hiyo hualika maadui!
Wakati Isaka alipokaa Gerari kwa
sababu ya njaa iliyotokea mashariki ya kati, kwa agizo la Mungu, Mungu alimbariki
sana Isaka, Mazao yake na mifugo yake iliongezeka sana kiasi ambacho wafilisti
walijawa na wivu wenye uchungu!
Maandiko yanaeleza wazi kwamba
wafilisti wakamhusudu! Neno Kuhusudu linalotumika hapo katika kiebrania
linatumika neno Qana mbalo maana yake ni Jealous au Zealous in a
bad sense kiswahili fasaha wivu wenye uchungu
Yakobo 3:14-16 “Lakini, mkiwa na wivu wenye
uchungu na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme uongo juu ya kweli.
Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya
kibinadamu, na Shetani. Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo
machafuko, na kila tendo baya.”
Kwaajili ya wivu wenye uchungu,
waliharibu visima alivyokuwa anatumia Isaka, Visima hivi vilichimbwa na
Ibrahimu baba yake miaka ya uhai wake, na visima hivi vilikuwa ndio chanzo cha
mfumo wa umwagiliaji na unyweshaji wa mifugo, na pasipo visima hivyo ni ngumu
kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji hususani wakati wa ukame, kwa hiyo
wafilisti walikusudia kumuharibu Isaka na walikusudia kuharibi kabisa vyanzo
vya Baraka zake, na walipoona majaribio yao yanashindikana mwisho wakamwambia
atoke kwao, na bila aibu walimweleza sababu kwanini aende
Mwanzo 26:16 “Abimeleki akamwambia Isaka,
Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi” kwa nini
walifanya hivyo Neema ya Mungu ilikuwa juu ya Isaka, alibarikiwa sana Mungu
alimpa akili ya kupata utajiri, familia yao walikuwa na ujuzi wa elimu ya
umwagiliaji, na ujuzi wa kuchimba visima hata kujua sehemu zenye maji, Jambo
hili liliwapelekea Wafilisti kujawa na wivu wenye uchungu kwaajili ya maisha ya
Isaka, Neema ya Mungu inapokuwa juu yako
na akaweka mkono wake kukubariki, ukawa na Nguvu, ukawa na bidii ya kazi, ukawa
na fedha, ukawa na ndoa nzuri, ukawa na watoto wenye mafanikio, ukawa na afya
nzuri ukastawi pande zote, ukawa na ustawi wa mwili nafsi na roho, hata hali
yako ya kiroho ikiwa vizuri, Shetani na majeshi yake ya pepo wabaya pamoja na
watu wabaya wataanza kukuonea wivu wenye uchungu, watu wataanza kukuchukia
pasipo sababu , kwanini kwa sababu ya neema ya Mungu iliyo juu yako
inayokuletea Baraka !
Kwa hiyo ni Lazima uelewe kama
wewe ni mtu mkubwa ndani, Mungu ameweka mkono wake juu yako, Mungu amekupa
kibali, na Baraka zake zikaanza kumiminika juu yako, Adui hatalala usingizi,
hataketi na kukuacha ufurahie Baraka za Mungu kwa Amani, ataanza kuchochea
shida na taabu. Leo basi tutachukua muda kujifunza somo hili Neema ya Mungu na
Mwaliko wa Maadui kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Mifano ya
watu waliopata Neema ya Mungu na kusababisha kuwa na Maadui
·
Neema ya
Mungu na mwaliko wa maadui
·
Ushauri
kutoka kwa Mungu
Mifano ya watu waliopata Neema ya Mungu na kusababisha kuwa na Maadui
Neno la Mungu limejaa mifano ya
watu waliopewa neema ya Mungu katika maisha yao na badala ya kupendwa na watu,
watu waliwachukia na kuwawashia moto, na kuwategea mitego ya aina mbalimbali
kuhakikisha kuwa wanakwama katika kila eneo la Maisha yao na ikiwezekana vyanzo
vya Baraka zao kuharibiwa!
1. Alichukiwa kwa sababu ya ndoto kubwa na
maono makubwa aliyokuwa nayo – Yusufu angalia katika Mwanzo 37:2-11 “Hivi ndivyo vizazi vya
Yakobo. Yusufu, aliyekuwa mwenye miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo
pamoja na ndugu zake; naye alikuwa kijana pamoja na wana wa Bilha, na wana wa
Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu akamletea baba yao habari zao mbaya. Basi
Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake,
akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko
ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani. Yusufu
akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; akawaambia,
Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. Tazama, sisi tulikuwa tukifunga
miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda
yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. Ndugu zake wakamwambia, Je!
Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa
ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake. Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia
ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi
na nyota kumi na moja zikaniinamia. Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba
yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako
na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi? Ndugu zake wakamhusudu; bali baba
yake akalihifadhi neno hili.”
Yusufu alipata
neema kutoka kwa Mungu, neema hii ilimfanya apate upendeleo kutoka kwa baba
yake, lakini nduguze walimchukia sana na Mungu akasema na Yusufu kwa habari ya Maisha
yake ya baadaye kwa njia ya Ndoto, Jambo hili lilipelekea nduguze wamchukie zaidi
na hata baadaye walikusudia kumuua,
kumbuka hapo Ndoto zilikuwa hazijatimia, lilikuwa ni ujumbe tu kutoka
kwa Mungu, watu wenye maono makubwa huchukiwa, Kimsingi kupitia kisa hiki wako
watu wanasema usimweleze mtu maono yako eti ufiche, kutokana na kisa hiki,
Lakini, Mungu hanaga tabia ya kuficha maono yake, huwa anaweka wazi, serikali
huwa haifichi mipango yake huwa inawekwa wazi, vyama huwa havifichi sera zake
huwa wanazinadi, kuficha maono ni woga, Mipango ya Mungu ya kumuokoa mwanadamu,
kuja kwa masihi iliwekwa wazi zamani sana Mungu mwenyewe aliiweka wazi, kwa
hiyo ukiona mpango umewekwa wazi kisha haukutimia ujue huo haukuwa mpango wa
Mungu, Mungu huweka wazi mipango yake na hakuna mtu anayeweza kusimama na
kuzuia kusudi lake na ndio maana Ndoto ya Yusufu iliwekwa wazi na Ndugu zake
walipigana nayo lakini ilikuja kutimia,.
Amosi 3:7 “Hakika
Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii
siri yake.”
Siri za Mungu
huwekwa wazi kwa watumishi wake hata kabla Hazijatimizwa, sijui wanaofundisha
ufiche siri zako wana maana gani, wanaogopa vita? wanaogopa maadui,? wanaogopa
wachawi? Mungu hana cha kuogopa yeye
anaweka wazi mambo yake na ndivyo alivyofanya kwa Yusufu, Mungu alitangaza
atakachomfanyia Yusufu hata kabla havijafanyika ni Mungu Bora anatangaza Mwisho
tangu mwanzo !
Isaya 46:9-10 “Kumbukeni
mambo ya zamani za kale; maana mimi ni Mungu, wala hapana mwingine; mimi ni
Mungu, wala hapana aliye kama mimi; nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu
zamani za kale mambo yasiyotendeka bado; nikisema, Shauri langu litasimama,
nami nitatenda mapenzi yangu yote”
Mungu haogopi
kutangaza mpango wake, na hakuna anayeweza kuzuia mapenzi yake, yanayoweza
kuzuiwa ni mapenzi ya wanadamu tu, lakini ya Mungu hayazuiliki, kusudi la Mungu
ni lazima lisimame, kwa hiyo uweke wazi usiweke wazi, Neema ya Mungu ikiwa juu
yako ndani yako kukiwa kuna kitu cha ziada ndani yako basi ni lazima kitaalika
maadui bila kujali kuwa kimesemwa au hakikusema kitaalika maadui tu na hii ni
kwa sababu gani ni kwa sababu ya wivu wenye uchungu! Walionao wanadamu kwa
uzito wa maono yako.
2. Alichukiwa kwa sababu ya Upako wa kifalme
na uwezo mkubwa aliokuwa nao – Daudi - angalia katika
1Samuel 18: 6-9 “Hata
ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti,
wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili
kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale
wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi
makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza;
akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena
awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile.”
Daudi alikuwa
amepakwa mafuta ya ufalme kichwani pake, lakini Muda wake ulikuwa bado
haujawadia, hata hivyo uweza wa kifalme ulitenda kazi ndani yake kwa kiwango
kikubwa sana alimpiga mfilisti na kujipatia umaarufu mwingi sana kwa sababu ya upako na uweza wa Mungu uliokuwa
juu yake, Angalia kuwa mfalme aliyekuwepo madarakani alianza kumpiga vita,
alitaka kumuua mara kadhaa kwa sababu alijua kuwa bila shaka ndiye atakayekuwa
mfalme, Mungu anapoweka ukubwa wowote ndani yako, hata kama wakati wake bado
watainuka wenye ukubwa kama wako watakupiga vita, hii ni kwa sababu hawafurahii
wewe uwe kama wao, hata unapotenda kwa busara ukiwa chini yao wanaogopa
wanadhani ni ile hali yako ya ukubwa inawaelemea, wanaweza kukuwinda, wanaweza
kukuwekea sumu, wanaweza kukusudia kukutendea mabaya wanapigwa upofu kwa sababu
ya nini Neema ya Mungu ya ukubwa wako inawatesa na kualika uadui, angalia Daudi
alikuwa na Adui ambaye ni Mfalme Sauli hivyo Sauli alikusudia kumuua Daudi,
Hata hivyo ukubwa wa Daudi usingeweza kuharibiwa kwa sababu Mungu alikusudia lakini
wote tunaelewa jinsi Sauli alivyosababisha maisha ya Daudi kuwa magumu sana
akikimbia huku na kule katika mapango na majabali na nyika kujificha na kuhami uhai wake kwaajili ya wivu
wenye uchungu wa Sauli.
3. Alichukiwa kwa sababu hawakuweza kushindana
na Hekima iliyokuwa juu yake – Stefano angalia katika
Matendo 6:8-10 “Na
Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika
watu.Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la
Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na
kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo
Roho aliyesema naye.”
Roho Mtakatifu
alikuwa amempaka mafuta Stefano, uweza wa Mungu ulikuwa juu yake akitumiwa na
Mungu kufanya ishara na miujiza mikubwa, lakini sio hivyo tu kichwani alikuwa
yuko vizuri, alikuwa na ujuzi wa maandiko na neno la Mungu lilikuwa limejaa,
watu wa masinagogi kama matano hivi
walikuja kujadiliana naye lakini hawakumuweza kwa sababu alikuwa na
hekima ya kupita kawaida na Roho wa Mungu alisema naye, tunajifunza hapa sio
mali tu, sio cheo tu hata hekima na uwepo wa Mungu unaoubeba unavutia maadui,
wanachukizwa na hali yako ya kiroho, wanatamani uchafuke, uonekane ulikuwa mtu
mbaya hufai, wewe ni kama kirusi tu, unatengenezewa skendo adui zako wanatamani
wapate sababu mbaya za kukuharibia walifanya hivyo kwa Stefano watafanya hivyo
na kwako bila kujali kuwa ni walokole wenzako au la angalia walitafuta
kumchafua Stefano kwa sababu za kizushi
Matendo 6:11 - 14 “Hata
wakashawishi watu waliosema, Tumemsikia mtu huyu akinena maneno ya kumtukana Musa
na Mungu. Wakawataharakisha watu na wazee na waandishi, wakamwendea, wakamkamata,
wakampeleka mbele ya baraza. Wakasimamisha mashahidi wa uongo waliosema, Mtu
huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa patakatifu na juu ya
torati; maana tumemsikia akisema kwamba Yesu huyo Mnazareti atapaharibu mahali
hapa, na kuzibadili desturi tulizopewa na Musa.”
Unaona?
Hamkuwahi kuona watu wakichafuliwa, hamkuwahi kuona watu wakizushiwa maneno ya
uongo katika jamii? Hamkuwahi kuona wakiitwa mafisadi, kumbe ni kwaajili ya
wivu wenye uchungu kutoka kwa maadui, watu wanachukizwa na utajiri ulio nao,
wanachukizwa na Neema ya Mungu iliyoko juu yako, wanachukizwa na Mali alizokupa
Mungu wanachukizwa na ndoto zako, wanachukizwa na uchungu na uzalendo na
msimamo wako wa dhati na uzalendo kwa watu wako lakini pia wanachukizwa na
Hekima iliyoko juu yako, akili kubwa uliyo nayo utendaji wako, uwajibikaji wako
kazini na kadhalika ndivyo walivyomfanyia Stefano wakampiga kwa mawe na kumuua,
wako watu wamedhurika na magonjwa, wamekufa vifo vyenye utata, wameumizwa mioyo
si kwa sababu walikuwa na hatia bali kwa sababu ya watu wenye wivu, wivu wenye
uchungu.
4.
Alichukiwa
kwa sababu tu alikuwa mkweli – Mungu anapokupa neema ya kuwa mkweli Neema
hiyo pia huwavutia maadui, Yohana mbatizaji alitiwa gerezani na kuuawa kwa
sababu Mungu alimpa neema na ujasiri wa kusema kweli!
Marko 6:17-28 “Kwa
maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata Yohana, akamfunga
gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake, kwa kuwa amemwoa; kwa
sababu Yohana alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo. Naye
yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asipate. Maana Herode alimwogopa
Yohana; akimjua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha
kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa akimsikiliza kwa furaha. Hata
ilipotokea siku ya kufaa, na Herode, sikukuu ya kuzaliwa kwake, alipowafanyia
karamu wakubwa wake, na majemadari, na watu wenye cheo wa Galilaya; ndipo binti
yake yule Herodia alipoingia, akacheza, akampendeza Herode na wale walioketi
pamoja naye karamuni. Mfalme akamwambia yule kijana, Niombe lo lote utakalo,
nitakupa. Akamwapia, Lo lote utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu.
Basi akatoka, akamwuliza mamaye, Niombe nini? Naye akasema, Kichwa cha Yohana
Mbatizaji. Mara akaingia kwa haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, Nataka
unipe sasa hivi katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. Mfalme akafanya
huzuni sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi karamuni,
hakutaka kumkatalia. Mara mfalme akatuma askari, akaamuru kuleta kichwa chake.
Basi akaenda, akamkata kichwa mle gerezani, akakileta kichwa chake katika kombe,
akampa yule kijana, naye yule kijana akampa mamaye.”
Yohana mbatizaji
aliuawa kwa sababu alikuwa Msemakweli, kweli iligharimu maisha yake maandiko
yanamtaja kuwa alikuwa mtu wa haki, alimkemea mfalme Herode kwa tendo la kuwa
na mke wa ndugu yake, akaamua kumtia gerezani, lakini mwanamke alifanya njama
ya kuhakikisha anauawa ili uovu wao uendelee, wakose mtu wa kuwakemea, hivi
ndivyo dunia inavyotaka, dunia haitaki watu wa kweli, haitaki watu wa haki,
haiitaji watu safi, kuwepo kwako kunawahukumu, hawafaidi maisha yao, ya dhambi,
hawataki mtu awe na kidomo domo watataka
wakunyamazishe ili nao wapige, aliyekuambia dunia inataka wasema kweli ni nani
hii ilimgharimu maisha ya nabii Yahaya au Yohana mbatizaji kama inenavyo injili
5. Alichukiwa kwa sababu kwa sababu ya husuda aliwazidi katika kila
idara – Yesu alikuwa mwema alifanya kazi njema umati mkubwa wa watu
ulimfuata walimuimbia hosanna mwana wa Daudi, ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina
Bwana
Mathayo 27:116-20 “Basi
palikuwa na mfungwa mashuhuri siku zile, aitwaye Baraba. Basi walipokutanika,
Pilato akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi? Yule Baraba, au Yesu aitwaye
Kristo? Kwa maana alijua ya kuwa wamemtoa kwa husuda. Na alipokuwa ameketi juu
ya kiti cha hukumu, mkewe alimpelekea mjumbe, kumwambia, Usiwe na neno na yule
mwenye haki; kwa sababu nimeteswa mengi leo katika ndoto kwa ajili yake. Nao
wakuu wa makuhani na wazee wakawashawishi makutano ili wamtake Baraba, na
kumwangamiza Yesu.”
Hivi umewahi
kujiuliza kwanini Yesu alichukiwa? Vikao vya siri vikakaliwa na mikakati ya
kuhakikisha anashughulikiwa ikafanyika? Sababu kubwa ni kuwa Yesu alikuwa
mashuhuri kuliko watu wote, alijizolea sifa zote, kutokana na huduma na
utumishi wake kwa kondoo wa Mungu waliotawanyika, alikuwa Mwalimu mwema,
alikuwa ni mchungaji mwema, aliponya watu, aliwahurumia, alikuwa na majibu ya
shida na matatizo yote ambayo jamii ilikuwa inakutana nayo, alilisha watu
wengi, alifufua alifuta misiba ya wengi alafu mshahara wake ni kusulubiwa?
Inakuwaje mtu mwema auawe? Inakuwaje watu wachague mtu muovu wamuache Yesu
asulubiwe? Maandiko yanasema Pilato alijua kuwa wamemtoa kwa sababu ya husuda
yaani wivu wenye uchungu, kila baya unalofanyiwa wakati mwingine ni kwa sababu
umewazidi adui zako katika idara zote Neema iliyokuwa juu ya Yesu ilikuwa
imewafunika viongozi wa dini, alikuwa akiwaumbua kwa kujawa na unafiki,
aliifundisha kweli na kunyosha mstari, aliwakosoa vikali, akiwatendea mema watu
na kuwafungua macho, akiruka vikwazo vyao, kwa hiyo walitafuta sababu za
kumsulubisha kwanini kwa sababu Neema ya
Mungu iliyokuwa juu yake iliwavutia maadui!, vaa vizuri, kula vizuri, jenga
nyumba nzuri, uwe na cheo kizuri utavutia watu wengi sana wawe karibu na wewe
lakini wengine ni nyoka ni watu waliojaa wivu wenye uchungu wanaotaka
kukuharibia maisha yako, watakuambia twende uwandani kisha huko watakuinukia
wakuue kama Habili kwanini kwa sababu
neema ya Mungu iliyoko juu yako inaalika maadui.
Neema ya Mungu na mwaliko wa maadui
Mwanzo 26:12-16 “Isaka akapanda mbegu
katika nchi ile, akapata mwaka ule vipimo mia kwa kimoja, BWANA akambariki. Na
mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana. Akawa na mali ya
kondoo, na mali ya ng'ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu. Na vile
visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Ibrahimu babaye,
Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza kifusi. Abimeleki akamwambia Isaka,
Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi.”
Tumeona katika utangulizi wa somo
letu, namna Isaka alivyochukiwa na wafilisti na sababu kubwa ni kuwa walimuonea
wivu, na wakaamua kuziba vyanzo vya Baraka zake yaani vile visima, Wakisahau
kuwa chanzo kikuu cha Baraka za Isaka ni neema ya Mungu iliyokuwa juu yake,
hata hivyo kama ipoipo tu, Mungu akishakuwa na mpango na mtu hakuna mwanadamu
anaweza kuzuia mpango wa Mungu, Ndugu yangu vita yote kubwa uliyo nayo ni kwa
sababu wewe u mzuri, unavaa vizuri, una neema ya Mungu juu yako, Mungu
amekusudia kukuweka juu na kukubariki, kwa hiyo usifadhaike unapokutana na
changamoto mbalimbali jua tu ya kuwa Mungu akiwa na mpango na wewe mipango yote
ya wanadamu inafikia ukingoni, na Mungu anakwenda kujitukuza katika maisha
yako, Isaka hakushindania visima na badala yake alichimba kingine na kingine na
kingine na mwisho wa siku wakaona aibu wakamwacha na Mungu akaweka mkono wake
na kuwapatia ahueni au nafasi Rehoboth wakati mwingine tuondoke na kwenda mbali
na maadui zetu ili Bwana atupe nafasi ya kupumua maana wanaumwa sana na wivu
wanaumwa mno wanadahani wakifukia visima na kudai kuwa ni vyao basi watatoboa
lakini ijulikane wazi ya kuwa Mungu ni Mungu na Mungu kwa neema yake ndio
chanzo kikuu cha Baraka zetu, Isaka angeweza kupigana vita lakini kwa kuwa
alikuwa ni mtu mwema na mpenda Amani aliamua kujiepusha ili kutafuta kwa bidi
kuwa na amani na watu wote!
Mwanzo 16:17-22. “Basi Isaka akatoka huko
akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko. Isaka akarudi akavichimbua
vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; maana wale
Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu; naye akaviita
majina kufuata majina alivyoviita babaye.Watumwa wa Isaka wakachimba katika
lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika.Wachungaji wa Gerari
wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita
jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye.Wakachimba kisima
kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna.Akaondoka huko
akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi,
akasema, Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi.”
Ushauri kutoka kwa Mungu.
Huu ni ushauri ambao Mungu
anautoa kwa watu wenye wivu, kwamba ili Mungu akubariki, wewe endelea kufanya
mema, basi, ukifanya vema naye atakubariki, Mungu amekusudia kumbariki kila
mmoja Mungu hana upendeleo hivyo
jitahidi usimuonee wivu nduguyo, acha kuwafanyia watu mabaya, usiwauwe kwa
ushahidi wa uongo, usiwachafue, usiwakasirikie ni neema ya Mungu iko juu yake
huwezi kushindana naye ikiwa mkono wa Bwana uko juu yake, Mungu baba alimshauri
Kaini ili asiingie dhambini kuwa afanye vema ! Mpango wa Mungu ni kumbariki
kila mtu, lakini Mungu anataka usiwe na uchungu anapombariki mwengine hakikisha
ya kuwa unakuwa mbali na kuumwa pale Mungu anapotoa kibali na neema yake kwa
nduguyo kwani ni swala la zamu tu usitende dhambi, usifanye hila usikasirike,
fanya vema nawe utabarikiwa pia usiwe na roho ya kaini aliyemuua nduguye
Mwanzo 4:2-11 “Akaongeza akamzaa ndugu
yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi.
Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA. Habili naye
akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA
akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake.
Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. BWANA akamwambia Kaini, Kwa
nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? Kama ukitenda vyema,
hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo
inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. Kaini akamwambia Habili nduguye,
[Twende uwandani]Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili
nduguye,akamwua. BWANA akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema,
Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya
ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. Basi sasa, umelaaniwa wewe katika
ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako;”
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni