Marko 5:38-42 “Wakafika nyumbani kwa yule
mkuu wa sinagogi, akaona ghasia, na watu wakilia, wakifanya maombolezo
makuu. Alipokwisha kuingia, akawaambia,
Mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana hakufa, bali amelala tu. Wakamcheka sana.
Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na
wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo yule kijana. Akamshika mkono
kijana, akamwambia, TALITHA, KUMI; tafsiri yake, Msichana, nakuambia, Inuka.
Mara akasimama yule kijana, akaenda; maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi
na miwili. Mara wakashangaa mshangao mkuu.”
Utangulizi:
Leo tutachukua muda kujifunza kwa
kina na mapana na marefu kuhusu Vazi maalumu la kiyahudi liitwalo TALLIT, Vazi hili huvaliwa na wanaume
wa kiyahudi na baadhi ya Wakristo walio na ufaamu wa kutosha kuhusiana na vazi
hilo, Vazi hilo maalumu mfano wa
(mtandio) lilitengenezwa kwa Pamba au Sufu nyeupe, Ni vazi lenye umbo la
Mstatili na huvaliwa mapegani na kiasi kidogo sehemu za kifuani kwa kujitanda,
kwa kawaida ni vazi Jeupe lenye mistari ya blue nyeusi (Dakr Blue) au Nyeusi inayotoka upande mmoja waa chini na juu
kutoka mwanzo mpaka mwisho, Vazi hili ni
moja ya Nyenzo muhimu sana ya kiroho iliyotumiwa tangu zamani na wayahudi na
baadhi ya manabii n ahata Yesu mwenyewe, Vazi hili linaaminika kuwa na nguvu za
Kiroho na huvaliwa kwaajili ya kufanyia maombi pamoja na kupata ulinzi wa
Mungu, Asili ya vazi hili ni kutokana na maagizo ya Mungu katika Torati kitabu
cha
Hesabu 15:37-40 “Kisha Bwana akasema na
Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli, na kuwaagiza ya kwamba wajifanyie
vishada katika ncha za nguo zao, katika vizazi vyao, tena ya kwamba watie
katika kila kishada cha kila ncha nyuzi za rangi ya samawi; nacho kitakuwa
kwenu ni kishada, ili mpate kukiangalia, na kuyakumbuka maagizo yote ya Bwana,
na kuyafanya; tena kwamba msiende kutanga-tanga kuandama mioyo yenu wenyewe, na
macho yenu wenyewe, ambayo mlikuwa mkiyaandama kwa uasherati hapo kwanza; ili
mpate kukumbuka na kuyafanya maagizo yangu yote, na kuwa watakatifu kwa Mungu
wenu.”
Wayahudi wenye asili ya ASHKENAZ wanaliita vazi hilo TALLIS Ni vazi ambalo linachochea moyo
wa utii na maombi na linalotaka uwe na uhusiano wako binafsi na Mungu, kama
watu watajifunza na kufahamu umuhimu wa vazi hili na wakalitumia vema wanaweza
kuchochea uhusiano wao na Mungu kwa njia ya maombi na utii kwa Mungu hivyo
kuzaliwa watu wenye nguvu za kiroho za kupita kawaida. Tutajifunza somo hili THALITHA KUMI Kwa kuzingatia vipengele
vinne vifuatavyo:-
·
Ufahamu kuhusu
Asili ya TALLIT
·
Mambo ya kujifunza katika vazi la TALLIT
·
Nguvu ya
kiroho kwa matumizi sahihi ya TALLIT
·
Thalitha
Kumi ( TALITHA CUMI)
Ufahamu kuhusu Asili ya TALLIT
Tallit ni Vazi au Mtandio maalumu unaotumika wakati wa kuomba ni
moja ya alama Muhimu sana ya kiroho na Nyenzo ya kiroho ambayo Wakristo wengi
hawafahamu umuhimu wake, watumishi wengi wa Mungu hawajawahi kupewa ufahamu wa
kutosha kuhusu vazi hilo, Lakini kujifunza juu ya vazi hilo na umuhimu wake na
matumizi sahihi ya vazi hilo na kusha kuyatendea kazi, kunaweza kutuletea
uamsho mkubwa sana katika maisha ya maombi kwa waktristo bila ya kutumia nguvu,
kuwa na ufahamu kuhusu umuhimu wa vazi hili sidhani kama inawahusu Wayahudi
peke yao kwani ni fundisho la kibiblia kuanzia na agano la kale mpaka agano
jipya, hivyo kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu Tallit kutatuleta katika kiwango
kingine kizuri cha kujenga uhusiano wetu na Mungu na kuleta matokeo
yanayokusudiwa katika maisha yetu na ya wengine!
Tallit ni Vazi au mtandio maalumu vazi la ibada linalotumiwa na
wayahudi na Baadhi ya Wakristo kwa kusudi la kuiungamanisha na Mungu hususani
wakati wa Maombi ya Alfajiri, au siku za sabato kwa wayahudi na siku takatifu, Tallit pia huvaliwa wakati wowote mtu
anapokua anahitaji kumuomba Mungu hususani anapokuwa bali na Sinagogi ua
hekalu.
Nguo hii mara nyingi hutengenezwa
kwa kitani nyeupe na huwa na umbo la mstatili na huvaliwa kama mtandio wa
mabegani lakini pia huwekwa kichwani wakati wa maombi, Nguo hiyo Nyeupe huwa na
michirizi au mishari ya Rangi ya bluu Nyeusi katika upande wa chini na wa juu
inayotoka mwanzo wa nguo mpaka mwisho wa Nguo, Aidha vazi hili maalumu huwa na
Nyuzi nyuzi zinazofungwa mbili mbili zinazoning’inia katika pindo la vazi hilo,
Nyuzi nyuzi hizo zinazoning’inia mwishoni mwa ncha za vazi hilo huitwa TZITZI kwa kiyahudi
Jina hilo Tallit kwaasili linatokana na neno la KIARAM TALLIT ikiwa na maana ya TO COVER kujifunika au
kujitanda na kwaasili ilitokana na agizo la Mungu katika Toarati kama
tulivyoona katika
Hesabu 15:37-40 “Kisha Bwana akasema na Musa, na kumwambia, Nena na wana
wa Israeli, na kuwaagiza ya kwamba wajifanyie vishada katika ncha za nguo zao,
katika vizazi vyao, tena ya kwamba watie katika kila kishada cha kila ncha
nyuzi za rangi ya samawi; nacho kitakuwa kwenu ni kishada, ili mpate
kukiangalia, na kuyakumbuka maagizo yote ya Bwana, na kuyafanya; tena kwamba
msiende kutanga-tanga kuandama mioyo yenu wenyewe, na macho yenu wenyewe,
ambayo mlikuwa mkiyaandama kwa uasherati hapo kwanza; ili mpate kukumbuka na
kuyafanya maagizo yangu yote, na kuwa watakatifu kwa Mungu wenu.”
Vazi hili kwa mujibu wa
masimulizi ya kiyahudi linawekwa ahadi za Mungu ndani yake pamoja na amri kumi
za Mungu, maandiko hayo huwekwa kwa ufundi sana katika vazi hilo moja na
kufikisha ahadi za Mungu 613 Awali
katika maelekezo ya Mungu Nyuzi nyuzi zilitakiwa kuwa nne tu yaani katika kila
ncha ta TALLIT nyuzi moja Kumbukumbu 22:12 “Ujifanyizie
vishada katika pembe nne za mavazi yako ya kujifunika.” Hata hivyo baadaye marabi walizifanya
nyuzi nyuzi hizo kuwa nyingi kwaajili ya kuwakilisha ahadi za Mungu na maagizo
yote ya USI na Yale mtu anayopaswa
kutenda. Kuusi kubwa la nyuzi nyuzi hizo ni kujikumbusha amri zote na maagizo
yote ya Mungu nyuzi nyuzi hizo huitwa TZITZI
Kuvaa vazi hili hakukuwa kwaajili
ya mapambo bali kuolikuwa kunaashiria kuwa mtu huyo hana utani na maswala yote
kuhusu Mungu, lilikuwa ni vali linalomkumbusha mtu kujitoa kwa Mungu na kwamba
anawajibika kuishika sharia yote ya Musa, Mafarisayo waliyavaa sana mavazi hayo
lakini hata hivyo wakiwa na nia ya kujionyesha kwa watu kuwa ni wenye haki,
walisahau kabisa kuwa Mungu huangalia moyo na haangalii kama wanadamu
waangaliavyo na kwa sababu ya tabia yao mbaya Yesu aliwachana na wala
hakuwaacha salama
1Samuel 16:7 “Lakini Bwana akamwambia Samweli,
Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana
haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali
Bwana huutazama moyo.”
Mathayo 23:25-28 “Ole wenu waandishi na
Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani
yake vimejaa unyang'anyi na kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu, safisha
kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi. Ole wenu, waandishi
na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa,
nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na
uchafu wote. Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye
haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi.”
Unaona vazi hilo ni agizo la utii
kwa Mungu na hivyo halipaswi kuvaliwa kinafiki na kwa klusudi la kujionyesha ua
kukubalika ni vazi ambalo ukilivaa kama unamuomba Mungu unaomba kwelikweli na
kama unazishika mari zake unazitii hasa kwa hiyo halipaswi kuvaliwa ili mradi,
bali linapaswa kuvaliwa na watu waliomaanisjha kwelikweli kutka moyoni na wale
waliomaanisha wakilivaa uweza na nguvu za Mungu huambatana nao sio hivyo tu
watu wakigusa TZI TZI wanapokea
uponyaji na nguvu za kiungu kwa mujibu wa mahitaji yao kama tutakavyoona katika
somo hili
TALLIT ni mojawapo ya vazi la thamani kubwa sana duniani na huuzwa
kwa bei karibu mara nne ya bei ya suti kali nchini Israel vazi hili huuzwa kati
ya fedha ya kitanzania laki nne mpaka laki tano hivi, Vazi hili kwa wastani
linaweza kuwa na urefu wa inchi 72 katika kona zeke kuu nne kuliandikwa SHEMA,
sikie ee Israel Bwana Mungu wako ni Bwana mmoja, mistari yake ilitakiwa
kuchorwa kwa wino wa samaki aina ya Ngisi
Mambo ya kujifunza katika vazi la TALLIT
Bila shaka unaanza kupata picha
sasa kwamba vazi hili sio la kawaida kwani kuanzia matengenezo yake mpaka
matumizi yake ni maelekezo ya neo la Mungu, hata hivyo ukiacha kuwa vazi hili
hutumika kwa maombi ya ahadi za Mungu, bado pia mvaaji anapaswa kujifunza mambo
kadhaa ambayo yanapaswa kuonekana katika maisha yake kupitia matumizi ya vazi
hili, vazi hili lina mafunzo muhimu makubwa ya kujifunza kama ifuatavyo:-
1.
Utawala
wa Mungu katika maisha Yetu
Asili ya vazi
hili ni maandiko na Mungu aliagiza vzazi hili kwa jamii ya wayahudi na dunia
nzima ili watu watambue kuwa Mungu ndiye anayetawala maisha yetu, unapojifunika
vazi hili maana yake unatambua ukuu wa Mungu kuwa Mungu yuko juu yako hata
pamoja na kila unachikionea fahari Duniani, sawa tu na mtu anavyovaa kibandiko
au Barakashia, na zile nyuzi nyuzi zinatufundisha
ya kuwa Mungu nanataka wakati wote tukumbuke sharia zake na kuzitii, kwa hiyo
vazi hili lnadai utii kwa Mungu, haitoshi tu kutambua kuwa Mungu yuko juu ya
yote kisha ukawa unaenda kama utakavyo
1Yohana 2:3-6 “Na
katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake. Yeye
asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani
yake.Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika
kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake. Yeye asemaye ya kuwa
anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda.”
Mtu anayevaa
vazi hilo ni lazima awe anamjua Mungu, anatambua ukuu wake na kuwa yeye
anawajibika kwake na kuwa yuko juu ya yote kwa hiyo anayevaa Tallit ni lazima aenende kama yeye
alivyoendenda!
2.
Mungu
ni Mtakatifu Sana
Mtu anapojifunika
na vazi hilo humaanisha kuwa hastahili kumwangalia Mungu, wala hustahili
kumuona yeye kwa macho ya nyama kwa sababu Mungu ni mtakatifu sana hakuna mtu
anaweza kumuona Mungu akaishi
Kutoka 33:19-20 “Akasema,
Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza jina la BWANA mbele
yako; nami nitamfadhili yeye nitakayemfadhili; nitamrehemu yeye
nitakayemrehemu. Kisha akasema, Huwezi kuniona uso wangu, maana mwanadamu
hataniona akaishi.”
Tallit ni vazi Jeupe na michirizi yake
ya blue huwakilsha mbingu ambayo ni makao makuu ya Mungu, na Mungu wetu ni
Mtakatifu sana kwa hiyo mtu awaye yote anayeivaa TALLIT au kikofia kama baraghashia anapaswa kuishi maisha
matakatifu, kwa sababu kuvaa vazi hilo kuna maanisha kuwa wewe umejitoa muhanga
kuishi kama vile apendavyo Mungu
1Petro 1:15-16 “bali
kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika
mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni
mtakatifu.” Kwa msingi huo uvaaji wa Tallit ni tangazo kuwa Mungu ni
Mtakatifu na kwamba nasi tunapaswa kuwa watakatifu katika mwenendo wetu wote
3.
Utii
kwa Mungu ni Muhimu sana
Nyuzi nyuzi
katika vazi lile inakumbusha juu ya sharia za Mungu na kuwa sharia hizo zinadai
utii kutoka kwetu ili Mungu aweze kututimizia ahadi zake, kwa hiyo kuvaa vazi
hilo halafu ukawa hauna utii kwa Mungu ni kuvaa ufarisayo tu, Makusudi makubwa
ya vazi hili ukiacha kuomba na kustawisha uhusiano wetu na Mungu vazi hili
linatukumbusha wajibu wa kumtii Mungu, Mungunanapendezwa na utii kwake, wote
tunafahamu Mungu alimkataa Sauli kwa sababu ya kukosa utii, maandiko yanaagiza
tumtii Mungu
1Samuel 15:22-23 “Naye
Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa
na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia
kuliko mafuta ya beberu.Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama
ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa
wewe usiwe mfalme.”
Watu
waliomuamini Yesu kama bwana na mwokozi wa maisha yao huitwa watoto wa kutii,
maana yake Mungu anategemea tutaishi maisha ya utii kwake hivyo mtu anapotamani
kuwa na vazi hili maalumu na akafanikiwa kuwa nalo halitakuwa na faida kwako
kama hutaishi maisha ya utii
1Petro 1:14 “Kama
watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu;”
Tunapomtii
Mungu, katika mkaisha yetu na kutambua jinsi kutii kulivyo Muhimu, itatusaidia
katika maisha yetu kuwa na nguvu dhidi ya shetani na kazi zake
Yakobo 4:7-10 “Basi
mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni Mungu, naye
atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha
mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka
kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu. Jidhilini mbele za
Bwana, naye atawakuza.”
4.
Kuwa
mbali na kiburi
Vazi la Tallit
linapovaliwa huvunika kichwa na mabega yetu, wakati huo tunatambua kuwa Mungu
ndiye mtawala wa kila kitu, na tunakubali kuwa yuko juu ya yote tukiwemo sisi
na kuinyesha kuwa tunamtii yeye, hata hivyo kuvaa vazi hili pia kuna maanisha
unyenyekevu kama mtu anataka Baraka za Mungu ni muhimu sana mtu huyo akawa
mnyenyekevu, Hakuna dhambi ambay Mungu huihukumu kwa haraka sana kama kiburi,
huwezi kusema kuwa umejitoa sana kwa kumaanisha kwa Mungu kisha alama za kiburi
zinaonekana kwako, unyenyekevu kwa Mungu kwanza na unyenyekevu kwa wanadamu,
pale wakati wote tunapojihesabu kuwa sisis sio kitu kwa Mungu na sio bora
ukilinganisha na wanadamu wengine, Vazi hili ni ishara ya kujinyenyekeza kwa
Mungu, na hivyo unapokwenda mbele zake na vazi hili maana yake umejinyenyekeza
kwake
Isaya 66:2 “Maana
mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema
Bwana; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho
iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu.”
1Petro 5:6-7 “Basi
nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;
huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa
mambo yenu.”
Yakobo 4:6 “Lakini
hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao,
bali huwapa neema wanyenyekevu.”
Unaona ni wazi
kabisa kuwa kijapo kiburi ndipo ijapo aibu, Mungu huwapinga wenye kiburi bali
huwapa neema wanyenyekevu, kwa hiyo vazi hili linawakilisha kuwa tumenyenyekea
kwa Mungu, unapohitaji maombi kwake anakusikia kutokana na mwenendo wako wa
unyenyekevu
5.
Ulinzi
wa Mungu
Vazi hili
vilevile ni ishara ya kuwa unazingirwa na uwepo wa Mungu, kwa kuwa Tallit
vilevile inawakilisha Hema ya kukutania ni vazi ambalo unapolileta kichwani
humaanisha kuwa umeingia katika patakatifu na uko tayari kusema na Mungu kama
vile unavyokuwa umeingia hekaluni, Tallit ni Hekalu binafsi, na TZITZI ni Pazia la hekalu lililopasuka
unapojifunika maana yake umeingia katika uwepo wa Mungu na hivyo uwepo huo
unakufunika ni ishara ya kuzingirwa na ulinzi wa Mungu pande zote
1Petro 1:3-5 “Ahimidiwe
Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa
mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo
katika wafu; tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka,
uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu. Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia
ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.”
6.
Kuishi
kwa Neno la Mungu
Tallit ni vazi
ambalo linawakilisha neno la Mungu, ahadi za Mungu na amri zake, Vazi hili
linawakilisha neno la Mungu linamkumbusha mvaaji kuwa anapaswa kusoma neno la
Mungu hii inakusaidia kutokusahau wema wa Mungu, linakukumbusha kutiokuwa
mawindo kwa haraka katika mitego ya adui,
kwa hiyo kuvaa vazi hili kunakutaka sio tu kuwa na ujuzi wa neno la
Mungu bali kuishi kwa neno na ndio maana
Vazi hili linahesimiwa sana na wayahudi kwa sababu lilikuwa ni vazi
linalosaidia kuwaleta watu karibu na Mungu katika maisha yao ya kila siku.
Luka 4:3-12 “Ibilisi
akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate. Yesu
akamjibu, Imeandikwa ya kwamba mtu hataishi kwa mkate tu. Akampandisha juu,
akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja. Ibilisi akamwambia,
Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami
humpa ye yote kama nipendavyo. Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa
yako. Yesu akajibu akamwambia, Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu
yeye peke yake. Akamwongoza mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya kinara cha
hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini; kwa maana
imeandikwa, Atakuagizia malaika zake wakulinde; na ya kwamba,mikononi mwao
watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Yesu akajibu akamwambia, Imenenwa, Usimjaribu
Bwana Mungu wako.”
7.
Kuwa
mbali na Unafiki
Mtu anayevaa Tallit hapaswi kuishi maisha ya
kinafiki, ukivaa Tallit katika jamii
ya kiyahudi, watu watakuja kwako na kukusogelea kwa kusudi la kulishika vazi
hilo kwa Imani ili Mungu aweze kukutana nao, TALLIT ni nyumba binafsi ya Mungu, ni Nyumba ya sala ni hema yako
binafsi ya kukutania, hivyo watu wenye ujuzi kuhusu vazi hilo na hawana uwezo
wa kulinunua au viwango vya kutosha kulivaa watakimbilia kwako kwa uponyaji
kwani vazi hilo ni Ishara ya Masihi ni Ishara ya kuwa wewe ni mtu wa Mungu, ni
Ishara ya kuwa una Mungu wa Israel
Zakaria 8:22-23 “Naam,
watu wa kabila nyingi na mataifa hodari watakuja Yerusalemu kumtafuta Bwana wa
majeshi, na kuomba fadhili za Bwana. Bwana wa majeshi asema hivi, Siku hizo
watu kumi, wa lugha zote za mataifa, WATAUSHIKA UPINDO WA NGUO YAKE YEYE ALIYE
MYAHUDI; naam, wataushika wakisema, Tutakwenda pamoja nanyi, kwa maana
tumesikia kwamba Mungu yu pamoja nanyi.”
Unaona ukivaa TALLIT kwa watu wanaojua maandiko,
watu waliovunjika moyo, watu wenye shida watakluzingira wakihitaji huduma kutoka
kwako, Ndio maana kuvaa vazi hilo kwa nia ya kujionyesha huku ukiwa hauna nguvu
za Mungu halisi kunakemewa vikali na Yesu Mwenyewe, kwani Mafarisayo
waliyatanua mavazi yao na kuziongezea urefu TZITZI
Mathayo 23:2-5 “Waandishi
na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa; basi, yo yote watakayowaambia,
myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao
hunena lakini hawatendi. Wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani
mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao.Tena matendo yao yote huyatenda
ili kutazamwa na watu; kwa kuwa hupanua hirizi zao, huongeza matamvua yao;”
Angalia Mstari
wa 5b kwa makini Mstari huu katika kiingereza unasomeka hivi, …. “They make
their Phylacteries wide and the tassels on their garments lon;” neno
hilo TASSELS katika kiingereza Ndio TZITZI yaani hirizi au matamvua, ni
nyuzi nyuzi zinazoning’inia mwishoni mwa pindo la vazi hilo liitwalo TALLIT Kwa hiyo mafarisayo waliyafanya
manyuzi nyuzi ya TALLIT zao kuwa
marefuuuu ili iwe rahisi watu kuyashika lakini hayakuwa na majibu ya kutosha
kwa watu kukutana na mahitaji yao, Kristo alikuja kuonyesha kuwa kwake hakuna
miujiza ya kuigiza au fake kwa hiyo watu waliposhika upindo wa vazi lake
walipata msaada, kama utakusudia kuvaa vazi hili achilia mbali maisha na tabia
za kuigiza uwe halisi, ulifanyie kazi zinazolingana sio kwaajili ya kuonekana
bali kwaajili ya kuwakutanisha watu na Mungu wa Israel, Mtakeni bwana na nguvu
zake, Ni lazima ukiwa unaivaa TALLIT
basi tuje tushike upindo wa vazi lako na kukutana na Mungu, Ni Tallit ndio vazi
la miujiza, Shetani leo amedanganya watu siri iliyoko katika vazi hili na
wahubiri wanatumia makoti yao eti kuachilia upako na kuangusha watu, sikatai
kuwa koti lako linaweza kuwa na nguvu za Mungu Lakini usisahau Mungu hajaagiza
koti aliagiza TALLIT nachelea kuwa
kutumia koti inaweza kuwa sawa tu na Walawi walioacha kulibeba sanduku mabegani
mwao wakatumia Mkokoteni wa kukokotwa na ng’ombe., jambo lililopelekea Uza
kuawa, ni vazi hili ndilo linatakiwa kufanya kazi hiyo na sio suti yako ya
polista
Kuna mambo mengi
ya kujifunza kuhusiana na vazi hilo lakini muda usingeliweza kutosha kuchambua
moja baada ya jingine hata hivyo hayo ni ya msingi niliyokuainishi kwaajili ya
kumfanya mvaaji kuwa na uwepo wa Mungu katika maisha yake n ahata kuweza kuleta
athari kwa wengine, hata hivyo vazi hilo likivaliwa kwa kanuni hizo kuna mambo
mengi sana ya kushangaza ambayo yanaweza kufanyika kupitia vazi hilo.
Nguvu ya kiroho kwa matumizi sahihi ya TALLIT
Nguvu za Uponyaji:
Vazi hili liitwalo TALLIT likiwa limevaliwa na mtu sahihi
na akazingatia mafundisho sahihi niliyoeleza hapo juu, uwepo wa nguvu za Mungu
hutenda kazi kupitia mtu huyo na vazi hilo, Vazi hili linalovaliwa sana na
wayahudi, nikukumbushe tu pia lilivaliwa sana na baadhi ya manabii na pia
lilivaliwa na Bwana wetu Yesu Kristo, baadhi ya manabii na wafalme na Hata Yesu
mwenyewe ambaye aliishika Sheria yote ni wazi kuwa alikuwa na vazi hili na
kutokana na maisha yeke ya utii kwa Mungu vazi hili kupitia pindo za vazi yaani
TZI TZI kulikuwa na miujiza kadhaa
iliyofanyika kupitia vazi hili, moja ya stori ya kusisimua kuhusu nguvu za
kiroho pale mtu alipotumia TALLIT Ni
pale wakati Mwanamke aliyekuwa na kansa alipoamua kulishika vazi hilo
lililokuwa mabegani mwa Yesu! Ona
Marko 5:25-36 “Na mwanamke mmoja mwenye
kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili,
na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote
alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya, aliposikia
habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana
alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona. Mara chemchemi ya damu yake
ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule. Mara Yesu,
hali akifahamu nafsini mwake kwamba nguvu zimemtoka, akageuka kati ya mkutano,
akasema, Ni nani aliyenigusa mavazi yangu? Wanafunzi wake wakamwambia, Je!
Wawaona makutano wanavyokusonga-songa, nawe wasema, Ni nani aliyenigusa?
Akatazama pande zote ili amwone yule aliyelitenda neno hilo. Na yule mwanamke
akaingiwa na hofu na kutetemeka, akijua lililompata, akaja akamwangukia,
akamweleza kweli yote. Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya, enenda zako
kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena. Hata alipokuwa katika kunena,
wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha
kufa; kwani kuzidi kumsumbua mwalimu? Lakini Yesu, alipolisikia lile neno
likinenwa, akamwambia mkuu wa sinagogi, Usiogope, amini tu.”
Katika injili ya Marko hapo
tunaona mwanamke huyu akiyashika mavazi ya Yesu kama unavyoweza kuona hata
hivyo ni ukweli usiopingika kuwa Mwanamke huyu hakushika mavazi yote ya Yesu
yeye alishipa PINDO la vazi la Yesu PINDO hapa ndio TZITZI yaani zile nyuzi nyuzi zilizokuwa zikining’inia katika hilo vazi, wayahudi waliamini kuzishika
hizo ni Kumshika Mungu mwenyewe au neno lake au YESHUA yaani masihi, kwa kuwa mwanamke huyu alikuwa amesikia kuwa
Yesu ni Masihi na alisikia kazi nyingi alizozifanya Yesu yeye alikuwa na Imani
kuwa akiigusa TALLIT inayotumiwa na
mtu huyu maarufu yeye angepona Luka
anaelezea kwa kina kuwa alichoshika mwanamke huyu ni Upindo wa vazi lake
yaani alishika TZITZI na kanisa ile
iliyomsumbua kwa miaka 12 ilikata mara moja
Luka 8:43-46 “Na mwanamke mmoja, ambaye
ametokwa na damu muda wa miaka kumi na miwili, [aliyekuwa amegharimiwa mali
zake zote kwa kuwapa waganga] asipate kuponywa na mtu ye yote, alikwenda nyuma
yake, akaugusa upindo wa vazi lake; na mara hiyo kutoka damu kwake kulikoma.
Yesu akasema, Ni nani aliyenigusa? Basi, watu wote walipokana, Petro alimwambia,
Bwana mkubwa, makutano haya wanakuzunguka na kukusonga. Yesu akasema, Mtu
alinigusa, maana naona ya kuwa nguvu zimenitoka.”
Mwanamke huyu alipokea uponyaji
kwa sababu alifahamu Nguvu ya kiroho ya vazi lile alilokuwa analitumia Yesu,
kwa nini kwa sababu Yesu hakuvaa ili mradi tu, alivaa akiwa anaitiis heria ya
Mungu, kwa hiyo unaposikia uponyaji kwa kupitia upindo wa vazi haimaanishi
upindo wa vazi la suti au dela hapana ni vazi maalumu la matumizi ya ibada kwa
wayahudi na wakristo wanaoelewa, kwa msingi huo kama Yesu alivaa vazi hili
hakuna sababu kwa wakristo kuacha kulitumia vazi hili kwani linahamasisha mambo
yote ya muhimu yanayoweza kuleta uamsho mkubwa na kurejesha uhusiano mkubwa na
Mungu.
Nguvu za miujiza na upako maradufu
Vazi la Tallit pia kwa mujibu wa
tamaduni za kiyahudi lilikuwa linaweza kurithiwa, hasa kama lilikuwa linatmiwa
na mtu mwema, na kulirithi vazi hilo kulimaanisha kurithi upako na miujiza ya
mtu huyo, tunafahamu kuwa vazi hili pia lilitumiwa na nabii Eliya ambaye
baadaye alipotwaliwa alimuachia vazi hilo Elisha na akalitumia kufanya miujiza
mbalimbali angalia maandiko
2Wafalme2:5-10. “Basi wana wa manabii,
waliokuwako Yeriko, wakamkaribia Elisha, wakamwambia, Je! Unajua ya kuwa Bwana
atamwondoa bwana wako leo, asiwe mkubwa wako? Akajibu, Naam, najua, nyamazeni. Eliya
akamwambia, Tafadhali kaa hapa; maana Bwana amenituma niende mpaka Yordani.
Akasema, Kama Bwana aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Wakaendelea
mbele wote wawili. Basi watu hamsini wa wale wana wa manabii wakaenda
wakasimama, kuwakabili kwa mbali; na hao wawili wakasimama karibu na Yordani. Eliya
akalitwaa vazi lake la juu, akalikunja, akayapiga maji, yakagawanyika huku na
huku, na hao wawili wakavuka pakavu. Hata ikawa, walipokwisha kuvuka, Eliya
akamwambia Elisha, Omba kwangu lo lote utakalo nikutendee, kabla sijaondolewa
kwako. Elisha akasema, Nakuomba, sehemu maradufu ya roho yako na iwe juu yangu.
Akasema, Umeomba neno gumu; lakini, ukiniona nitakapoondolewa kwako, utalipata;
la hukuniona, hulipati.”
Bila shaka kuna kitu unajifunza
kuhusiana na vazi hilo, ukweli ni kuwa Eliya aliponyakuwaliwa na Mungu kwenda
mbinguni vazi hili lilimuangukia Elisha na akalitmia tena kwa matumizi kama
yale kuuvuka mto Jordani, lakini sio hivyo tu upako zaidi kama ule wa Eliya na
mamlaka yake ikawa juu ya Elisha
2Wafalme 2:11-15 “Ikawa, walipokuwa
wakiendelea mbele na kuongea, tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa
moto, likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa
kisulisuli. Naye Elisha akaona, akalia, Baba yangu, baba yangu, gari la Israeli
na wapanda farasi wake! Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe,
akayararua vipande viwili. Kisha akaliokota lile vazi la Eliya lililomwangukia,
akarudi, akasimama katika ukingo wa Yordani. Akalitwaa lile vazi la Eliya
lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, Yuko wapi Bwana, Mungu wa Eliya? Naye
alipoyapiga maji, yakagawanyika huku na huku, Elisha akavuka. Na hao wana wa
manabii, waliokuwako Yeriko wakimkabili, walipomwona, walisema, Roho ya Eliya
inakaa juu ya Elisha. Wakaja kuonana naye, wakainama kifudifudi mbele yake.”
Unaweza kuona mamlaka ya kiungu
iliyokuwa juu ya Eliya ilimkalia Elisha kupitia vazi hilo, vazi hili likitumiwa
na mtu kwa ufasaha lina uponyaji, lina ufufuo, lina upako na faida nyingi za
kiroho.
Nguvu ya kuondoa mamlaka
Kwa mujibu wa masimulizi ya
kiyahudi wanasema mtu anapofariki dunia mwili wake au jeneza lake hufunikwa na
vazi hili la TALLIT na zile nyuzi
nyuzi yaani TZITZI hukatwa
kumaanisha kuwa ndio mwisho wake wa kushika sharia yaani amefariki dunia au
amekataliwa, kwa hiyo katila lugha ya kinabii ukiishika vazi hili na TZITZI zake zikakatika humaanisha
mwisho wa mamlaka yako, Tulio hili lilitokea wakati Nabii Samuel akiwa amevaa
Vazi hili na alipokuwa akimkemea Sauli kwa kukosa utii wakati anageuka kuondoka
sauli aliushika upindo wa vazi hili na likamchanikia hii ilimaanisha mwisho
wake umefika
1Samuel 15:25-28 “Basi sasa, nakuomba,
unisamehe dhambi yangu; rudi pamoja nami, nipate kumwabudu Bwana. Samweli
akasema, Sitarudi pamoja nawe; kwa sababu umelikataa neno la Bwana, Bwana naye
amekukataa wewe, usiwe mfalme wa Israeli. Naye Samweli alipogeuka, aende zake,
SAULI AKAUSHIKA UPINDO WA VAZI LAKE, nalo likararuka. Basi Samweli akamwambia,
Leo Bwana amekurarulia ufalme wa Israeli, naye amempa jirani yako, aliye mwema
kuliko wewe.”
Unaweza kuona kumbe vazi lile pia
linanguvu ya kinabii, linaishara ya uwepo wa Mungu kuondoka juu ya mtu kama mtu
huyo hatakuwa mtii, Sauli alijitabiria vibaya kwa kushika TZITZI nyuzi nyuzi hizi na lile vazi lilararuka kumbe mamlaka
yakemimefikia ukingoni
Nguvu ya kupokonywa mamlaka
Kama mtu akikukatia vazi hili
huashiria pia amechukua mamlaka yako katika ulimwengu war oho na amekufikisha
mwisho, katika mapigano baridi
yaliyokuwepo kati ya Sauli na Daudi ukweli ilikuwa Sauli alikuwa
akimtafuta Daudi ili aweze kumuua, na huenda katika kabi ya Daudi kulikuwa na
unabii kuwa iko siku Bwana atamtia adui yako mikononi mwako, na siku hiyo
ilifika na watumishi wa Daudi walimkumbusha Daudi kuhusu ujumbe huo, hata hivyo
katika namna ya kushangaza sana Daudi aliukata tu Upindo wa Vazi la sauli
badala ya kumuua, kukatiwa hizo ilikuwa ni Ishara ya kifo katika ulimwengu wa
Roho jambo ambalo kwakweli lilimuuma sana Daudi na kumfadhaisha sana Sauli
kwani alijua wazi kabisa kinabii anakufa
1Samuel 24:1-12. “Ikawa, Sauli aliporudi
baada ya kuwafuatia Wafilisti, aliambiwa ya kwamba, Daudi yuko katika nyika ya
Engedi. Ndipo Sauli akatwaa watu elfu waliochaguliwa katika Israeli wote,
akaenda kumtafuta Daudi na watu wake juu ya majabali ya mbuzi-mwitu. Akafika
penye mazizi ya kondoo kando ya njia, na huko kulikuwa na pango; Sauli akaingia
ndani ili kuifunika miguu. Na Daudi na watu wake walikuwa wakikaa mle pangoni
ndani sana. Nao watu wa Daudi wakamwambia, Tazama, hii ndiyo siku ile
aliyokuambia Bwana, Angalia, nitamtia adui yako mikononi mwako, nawe utamtenda
yo yote utakayoona kuwa mema. Basi Daudi akainuka, AKAUKATA UPINDO WA VAZI LAKE
SAULI KWA SIRI. Lakini halafu, moyo wake Daudi ukamchoma, kwa sababu amekata
upindo wa vazi lake Sauli. Akawaambia watu wake, Hasha! Nisimtendee bwana
wangu, masihi wa BWANA,neon hili,kuunyosha mkono wangu juu yake,kwa maana yeye
ni masihi wa BWANA. Basi Daudi akawazuia watu wake kwa maneno hayo, asiwaache
kumwondokea Sauli. Kisha Sauli akatoka pangoni, akaenda zake. Daudi naye
akainuka baadaye, akatoka pangoni, akamwita Sauli, akisema, Bwana wangu,
mfalme. Na Sauli alipotazama nyuma, Daudi akainama uso wake hata nchi,
akamsujudia. Daudi akamwambia Sauli, Kwa nini unasikiliza maneno ya watu
wasemao, Tazama, Daudi anataka kukudhuru? Tazama, leo hivi macho yako yameona
jinsi Bwana alivyokutia mikononi mwangu pangoni, na watu wengine wakaniambia
nikuue; lakini nikakuacha; nikasema, Sitaki kuunyosha mkono wangu juu ya bwana
wangu; kwa maana yeye ni masihi wa BWANA Tena, baba yangu, tazama, tafadhali,
tazama upindo wa vazi lako mkononi mwangu; maana ikiwa nimeukata upindo wa vazi
lako, nisikuue, ujue, na kuona ya kuwa hakuna uovu wala kosa mkononi mwangu,
wala sikukukosa neno; ingawa wewe unaniwinda roho yangu ili kuikamata.Bwana
atuamue, mimi na wewe, na Bwana anilipizie kisasi changu kwako; lakini mkono
wangu hautakuwa juu yako.”
Nguvu ya kugawanywa kwa ufalme
Tunaona pia vazi hilo hilo likiwa
katika mabega ya Ahiya nabii ambaye alilikata kata kumaanisha kugawanyika kwa
ufalme katika Israel maana yake ni kuwa vazi hilo linapochana chanwa kinabii
huashiria kuraruliwa kwa mamlaka au ufalme
1Wafalme 11:29-35 “Ikawa zamani zile Yeroboamu
alipokuwa akitoka katika Yerusalemu, nabii Ahiya, Mshiloni, alikutana naye
njiani; naye Ahiya amevaa vazi jipya, na hao wawili walikuwa peke yao
mashambani. Ahiya akalishika lile vazi jipya alilokuwa amelivaa, akalirarua
vipande kumi na viwili. Akamwambia Yeroboamu, Twaa wewe vipande kumi, maana
Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nitaurarua ufalme, na kuuondoa katika
mkono wa Sulemani, nami nitakupa wewe kabila kumi, (lakini yeye atakuwa na
kabila moja kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya Yerusalemu mji
ule niliouchagua katika miji yote ya kabila za Israeli);kwa sababu wameniacha
mimi wakaabudu Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni, na Kemoshi, mungu wa Wamoabi,
na Milkomu, mungu wa wana wa Amoni wala hawakuenda katika njia zangu, kutenda
mema machoni pangu, kuzishika sheria zangu na hukumu zangu, kama Daudi baba
yake. Walakini sitauondoa ufalme wote katika mkono wake; lakini nitamfanya awe
mkuu siku zote za maisha yake, kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi niliyemchagua
kwa maana alizishika amri zangu na sheria zangu, lakini nitauondoa ufalme
katika mkono wa mwanawe, nami nitakupa wewe kabila kumi.”
Kwa hiyo unakubaliana nami kuwa
vazi hili lina nguvu za kiroho na miujiza mbalimbali kama tulivyojifunza katika
neno la Mungu, nadhani kama manabii wengi na walimu wa neno la Mungu wataweka
mkazo mkubwa kwenye matumizi ya TALLIT na
kuwaelekeza watu namna na jinsi ya kutumia unaweza kuondosha kabisa matumizi ya
sabuni za upako na nyenzo nyingine za kiroho zisizo za kimaandiko, badala ya kukanyaga mafuta watu wangekuwa
wanatumia TALLIT wangekua kiroho,
wangevuta uhusiano wao na Mungu na baraka nyingi zingeweza kuambatana na maisha
ya wakkristo na kusababisha ukaribu na Mungu, hakuna nyenzo ya kiroho inaweza
kumleta mtu karibu na Mungu kama TALLIT hii
hata rozari haiingii yeye aliye na sikio na alisikie neno hili.
Sasa swali kubwa sana ni kwanini
kichwa cha somo hili ni neno THALITHA
KUMI? je kuna uhusiano wowowte kati ya TALLITH
na TALITHA KUMI ? jibu ni ndio na uko uhusiano mkubwa sana wa
matamshi ya Bwana Yesu alipokuwa akimfufua Binti Yairo na fundisho zima la TALLIT hilo linatupa nafasi ya
kujifunza kwa kina katika kipengele kinachofuata
Thalitha Kumi (TALITHA CUMI)
Marko 5: 38-42 “Wakafika nyumbani kwa yule
mkuu wa sinagogi, akaona ghasia, na watu wakilia, wakifanya maombolezo
makuu. Alipokwisha kuingia, akawaambia,
Mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana hakufa, bali amelala tu. Wakamcheka
sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa babaye yule kijana na mamaye,
na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo yule kijana. Akamshika
mkono kijana, akamwambia, TALITHA, KUMI; tafsiri yake, Msichana, nakuambia,
Inuka. Mara akasimama yule kijana, akaenda; maana alikuwa amepata umri wa miaka
kumi na miwili. Mara wakashangaa mshangao mkuu.”
Neno Thalitha Cumi neno TALLIT yote ni maneno ya KIARAMU na ni maneno
yenye mzizi mmoja, Kutokana na
Matumizi ya TALLIT kwaajili ya
Maombi, kama mtu aliomba Mungu ampe mtoto ndani ya TALLIT yake na Mungu akampa mtoto wa kike mtoto huyu angeitwa THALITHA, kwa hiyo katika Lugha ya
Kiaramu Binti mdogo wa kike mwenye umri ambao haujafikia kuolewa aliitwa THALITHA, kwa hiyo THALITHA linaweza kuwa ni jina kamili la mtoto wa kike, au Jina la
Jumla la mtoto wa kike au Msichana, kwa
Msingi huo linapounganishwa na neno CUM
– KOOM , Yaani RISE au AMKA, unapata
sentensi MSICHANA AMKA au
Kijana Amka. Hivyo Yesu alipotamka maneno THALITHA CUM aidha alikuwa amesema MSICHANA AMKA au alitaja jina la Msichana moja kwa moja ambaye
aliitwa THALITHA. Kama Jina la msichana huyu aliitwa THALITHA basi ni wazi kwa kuwa Petro
alikuwepo miongoni mwa wanafunzi watatu walioshuhudia tukio hili basin aye
wakati ameitwa kumsaidia Dorcas ambaye naye aliitwa THABITHA ambalo nalo
lilikuwa jina la KIARAMU lakini sasa
ni kwa Mwanamke mtu mzima THABITHA kwa KIARAM maana yake ni
GRACIOUS au Neema unaweza kuona katika
Matendo 9:36-42 “Na mwanafunzi mmoja
alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa);
mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. Ikawa siku zile
akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani. Na kwa kuwa mji
wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko
huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu. Petro
akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote
wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona
Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao. Petro akawatoa nje wote, akapiga
magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, ondoka. Naye
akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi. Akampa mkono,
akamwinua; hata akiisha kuwaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao,
hali yu hai. Ikajulikana katika mji
mzima wa Yafa; watu wengi wakamwamini Bwana.”
Unaona Kwa msingi huo THALITHA lilikuwa jina la Kiaramu la
Mtoto wa kike linalotokana na imani ya mtu aliyeomba kupitia TATLIT, au kuonyesha furaha kwa kupata
Binti mdogo. Huo ni moja ya uwezekano
huo
Kwa msingi huo maneno haya TALLIT na THALITHA yana uhusiano wa Karibu na ni Marko pekee katika injili
ndiye aliyeyatumia maneno haya. Yesu
aliyatumia maneno haya wakati anamfufua mtoto wa Yairo na ilikuwa siku ileile
na muda uleule ambapo kulikuwa na tukio la kuponywa kwa mwanamke yule aliyekuwa
ameugusa upindo wa vazi la Yesu yaani
TZITZI, mwanammke huyu aliteseka kwa miaka 12 na binti aliyefufuliwa alikuwa na umri wa miaka 12. siku ile kulikuwa na nini hasa?
Kwa nini siku hii miujiza mingi mikubwa ilifanyika kupitia vazi hili la Yesu?
Kimsingi ni siku ambayo Yesu
alikuwa akifanya miujiza kwa kutumia
TALLIT na bila shaka kwa maelekezo ya ROHO
MTAKATIFU na kimsingi huyu BINTI ndiye aliyekuwa mlengwa kwani Yesu alikuwa akielekea
kwenda kumuombea na mwanamke mwenye kutokwa Damu aliingilia kati tu na
kuhudumiwa, kisha taarifa zilikuja kuwa kijana huyu msichana alikuwa amefariki,
lakini Yesu alikwenda na kumuinua.
Kama umefuatilia somo hili vizuri
kuhusu TALLIT utagundua kuwa Vazi
lile lina nguvu sana na hapa tunaona likihusika katika maombezi ya kumfufua
binti aliyewakuwa amekufa tayari, katika muujiza huu watu wengi wamezingatia
tafasiri ya Marko kwamba Yesu alisema msichana amka THALITHA KUMI ni kweli, lakini kuna maswala makuu mawili hapa ambayo
yamejificha ni hivi:-
Kumbuka kuwa mtu akifa katika
Israel mwili wake ufunikwa na TALLIT na
TZITZI (Nyuzi nyuzi) hukatwa kumaanisha mwisho wa kuzishika mari za Mungu
na Sheria, kwa hiyo katika mazingira ya muujiza huu ni aidha mwili wa msichana
ulikuwa umefunikwa kwa TALLIT na
Yesu hakuita tu, wala hakushika mkono, Yesu aliifunua TALLIT na kusema maneno
TALLITHA CUMI, TALLIT INUKA na
kijana akainuka huu ndio uwezekano mmojawapo wa namna na jinsi muujiza huu
ulivyofanyika
Namna nyingine ambayo inawezakuwa
ilifanyika hapa ni aidha Yesu aliitumia
TALLIT yake mwenyewe ile ambayo iliguswa na mwanamke aliyekuwa anatokwa
damu, na kuifunika ile maiti na kisha
kuifunua huku akisema TALITHA CUMI akimaanisha TALLIT INUKA na mara msichana yule
akainuka huu ni uwezekano mwingine
Kwa hiyo katika muujiza huu mkubwa
sana tunaona tena Nguvu ya TALLIT ikitumiwa
sio tu kuponya mtu mwenye Kansa bali pia kiunua mtu aliyekufa hii ni kwa sababu
neno TALLIT na TALITHA ni neno moja,
Kwa hiyo Yesu alitumia kifaa au nyenzo hii ya kiroho katika kufanya muujiza
mikubwa siku ile, Wakristo tunaweza kutumia
TALLIT japo Bei ni ghali lakini ni Dhahiri ni vazi linaloweza kusaidia
kuleta uamsho mkubwa katika kanisa la Mungu, vazi hili ni la thamani kubwa sana
na Yesu alilitumia na siku ile alipokuwa anasulubiwa ilionekana sio vema
kulipasua na badala yake walilipigia kura ili liweze kuchukuliwa na askari mmoja
kwanini kwa sababu walijua nguvu iliyokuwa ikitenda kazi kwa Yesu na
waliiheshimu TALLIT aliyokuwa
anaivaa kwa hiyo vazi lililopigiwa kura lilikuwa ni TALLIT
Mathayo 27:35 “Walipokwisha kumsulibisha,
waligawa mavazi yake, wakipiga kura; [ili litimie neno lililonenwa na nabii,
Waligawa nguo zangu kati yao, na juu ya vazi langu walipiga kura.]”
Kwa msingi huo basi katika shule
za kinabii, wale wenye kupenda kutumia vifaa vya kiroho, hakuna kifaa cha
kiroho cha muhimu na ambacho tunaona Yesu anakitumia kama TALLIT, Hatumuoni Yesu akitumia chumvi wala Mafuta, wala sabuni,
wala maji ya upako, Lakini vazi hili Yesu alilitumia kwa maelekezo ya Roho wa
Mungu, Vazi hili ni la kinidhamu na ni chuo cha mafunzo, vazi hilo ni la msingi
na la muhimu na sidhani kama itakuwa ni vibaya likitumiwa na wakristo kama
urithi wa moja ya mambo ya msingi kutoka katika dini ya kiyhaudi, TALLIT ni tofauti na NAIVERA Kanzu maalumu ambayo huvaliwa na makuhani. Kumbuka hilo.
Hitimisho - Tuombe
Baba Katika jina la Yesu Leo nasema Katika jina la Yesu Inuka ewe
uliyekufa, inuka ewe uliyelala, na ninakutangazia kama biashara yako imekufa Utainuka, Ndoa yako ina viashiria vya uchungu amka, Yesu
alisema mtoto amka naamsha kila kitu kilichokufa katika maisha yako, nakausha
kila chemichemi ya uharibifu inayobubujika kwa miaka mingi katika maisha yako
Kwa jina la Yesu Kristo Thalitha KUM, inuka katika masomo, inuka katika uchumi,
inuka katika huduma, inuka katika hekima, inuka katika haki, katika jina la
Yesu Kristo, Bwana uliyenifunulia Somo hili leo wafungue na kuwainua wasomaji
wangu waliojifunza somo hili kwa kina na
mapana na marefu na kukuibaliana na mafundisho haya uliyomfunulia mtumwa wako
katika jina la Yesu THALITHA kum katika kile eneo la maisha yako, katika
ufahamu wako, katika kazi yako, katika uzao wako na sehemu zote za maisha yako
nilizozitaja na nisizo zitaja Amen
Na Rev. Innocent Mkombozi, Samuel Hamza, bin jumaa, bin Athumani
Sekivunga Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni