Jumapili, 28 Julai 2024

Hukumu ya Mungu isiyoepukika!


Warumi 2:1-8 “Kwa hiyo, wewe mtu uwaye yote uhukumuye, huna udhuru; kwa maana katika hayo umhukumuyo mwingine wajihukumu mwenyewe kuwa na hatia; kwa maana wewe uhukumuye unafanya yale yale. Nasi twajua ya kuwa hukumu ya Mungu ni ya kweli juu yao wafanyao hayo. Wewe binadamu, uwahukumuye wale wafanyao hayo na kutenda yayo hayo mwenyewe, je! Wadhani ya kwamba utajiepusha na hukumu ya Mungu? Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa Mungu wakuvuta upate kutubu? Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu, atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake; wale ambao kwa saburi katika kutenda mema wanatafuta utukufu na heshima na kutokuharibika, watapewa uzima wa milele; na wale wenye fitina, wasioitii kweli, bali wakubalio dhuluma, watapata hasira na ghadhabu;”




Utangulizi:

Hukumu ya Mungu kwa wanadamu ni jambo lisiloepukika,Tangu mwanzo Mwanadamu na viumbe wengine walipokosea Mungu mara moja alitoa hukumu, alimuhukumu Shetani, alimuhukumu mwanadamu, Alimuhukumu mwanaume na alimuhukumu mwanamke kila mmoja kwa kadiri ya uhusika wake katika kosa lile la bustanini mwa Edeni, kwa hiyo hukumu ya Mungu ni jambo lisiloepukika, ukweli kuhusu hukumu ya Mungu ni jambo lenye kutisha sana kwa wanadamu, hata hivyo leo tutachukua Muda kutafakari kwa undani kuhusu hukumu ya Mungu na umuhimu wake katika mtazamo wa upendo wake na rehema zake na tabia yake ya uungu ambayo itakushangaza!

Warumi 2:12-16 “Kwa kuwa wote waliokosa pasipo sheria watapotea pasipo sheria, na wote waliokosa, wenye sheria, watahukumiwa kwa sheria. Kwa sababu sio wale waisikiao sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki. Kwa maana watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe. Hao waionyesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao, yenyewe kwa yenyewe, yakiwashitaki au kuwatetea; katika siku ile Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu, sawasawa na injili yangu, kwa Kristo Yesu.”

Swala zima la hukumu kwa mujibu wa maandiko Mungu hakuwapa wanadamu, na tumekatazwa kuhukumu, bali amepewa Yesu Kristo na Baba yake aliye mbinguni, kwa hiyo hakuna mtu awaye yote mwenye mamlaka ya kuhukumu isipokuwa mwana wa Adamu yaani Yesu Kristo mwenyewe, kuhukumu ni kukaa katika kiti cha Mungu. Fundisho kuhusu hukumu linatawala maandiko yote katika agano la kale na jipya, Utukufu wa Mungu unaonekana na kufunuliwa katika namna anavyohukumu, Mungu anamtaka kila mmoja awajibike na kwa sababu hiyo hakuna mwanadamu wala taifa litakaloweza kuiepuka hukumu ya Mungu na Yesu ndiye Mwamba wa hukumu hiyo:-

Yohana 5:22-30 “Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana hukumu yote; ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka. Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani. Amin, amin, nawaambia, Saa inakuja, na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai. Maana kama vile Baba alivyo na uzima nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na uzima nafsini mwake. Naye akampa amri ya kufanya hukumu kwa sababu ni Mwana wa Adamu. Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu.Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo; na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenipeleka.”

Kwa nini Masihi amepewa kuhukumu? Kwa sababu uwezo wake wa kuhukumu ni mkubwa sana na uko juu na sio wa kibinadamu, na kwa sababu yeye amepitia uanadamu anatujua vema lakini pia kwa sababu kuhukumu kwake hakutokani na yale yanayoonekana kwa macho, wala yale ayasikiayo kwa masikio yake lakini hukumu yake ni ya haki kama alivyosema mwenyewe na uwezo wake ni mkubwa sana kwa sababu ya Roho wa Mungu na hekima yake kuu

Isaya 11:1-5 “Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda.Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake;bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya. Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia.”

Kumbukumbu 1:17 “Msitazame nafsi za watu katika hukumu; mwasikize wadogo na wakubwa sawasawa; msiche uso wa mtu awaye yote; kwa kuwa hukumu ni ya Mungu; na lile neno liwashindalo mniletee mimi, nami nitalisikiza.”

Kumbukumbu 32:3-4 “Maana nitalitangaza Jina la Bwana; Mpeni ukuu Mungu wetu.Yeye Mwamba, kazi yake ni kamilifu; Maana, njia zake zote ni haki. Mungu wa uaminifu, asiye na uovu, Yeye ndiye mwenye haki na adili.”

Leo tutachukua muda moja kwa moja kutafakari kwa kina na mapana na marefu kuhusu hukumu za Mungu ambazo kimsingi ziko aina nne za hukumu ambazo tutaziangalia kwa kuzingatia vipengele vinne vifuatavyo sawa na ufunuo.

 

1.       Hukumu iliyoko sasa – Paroúsa Krisi

2.       Hukumu ya adhabu – Krima

3.       Hukumu isiyo ya adhabu – Krino

4.       Hukumu isiyotarajiwa – Aprosmenos   

 

Hukumu iliyoko sasa – Paroúsa Krisi

Hukumu hii kwa kiingereza inaitwa Present Judgement kwa kiyunani Paroúsa Krisi yaani hukumu hii inategemeana na mkao ulioko sasa wa hali ya kiroho za wanadamu, kama mwanadamu ameukubali mpango wa Mungu wa ukombozi kwa kumwamini Bwana Yesu kama Bwana na mwokozi wake huyo kwa sasa haukumiwi, na yule ambaye hajaukubali mpango wa Mungu wa ukombozi kupitia Yesu Kristo huyo amekwisha kuhukumiwa, Instant Judgement.au “Quckly Decision” “quicly judgemnt

Yohana 3:16-18 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.     Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.”

Yohana 5:24 “Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.”

Kwa hiyo katika ulimwengu huu wako watu ambao wamehukumiwa tayari yaani hivi tunavyozungumza hapa wako watu wa aina mbili duniani na wote wanaendelea na shughuli zao wakiwa wamehukumiwa yaani wale wasiomwamini Yesu na kundi la pili ni watu ambao hawako chini ya hukumu hawahukumiwi hawa ni wale waliomuamini Bwana Yesu na kumkubali kama Bwana na mwokozi wao, Hukumu hii inaendelea ikiendeshwa na Roho Mtakatifu kupitia kazi anayoifanya sasa ya kuwashuhudia watu kwa habari ya dhambi, haki na hukumu, kila wakati na kila siku injili ihubiriwapo mtu akimpokea Yesu anahama kutoka upande wa wale waliohukumiwa kwenda upande wa wale wasiohukumiwa,Injili ikihubiriwa ukaikubali sasa uko nje ya hukumu, na ukiikataa uko hukumuni.

Yohana 16:7-8 “Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu. Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.”
             

Hukumu ya adhabu – Krima

Hii ni moja ya kundi la hukumu (Judgement or Condemnation) ambayo inahusiana na siku ya mwisho wakati Kristo atakapokalia kiti cha enzi cha hukumu na kumuhukumu kila mmoja kwa kadiri ya matendo yake hukumu hii pia inaitwa hukumu ya adhabu au hukumu ya aibu, siku ya hukumu hii kila mtu atasimama mbele ya kiti hicho cha hukumu cha Mungu na kutoa hesabu yake mwenyewe. Hukumu hii kiyunani Krima au Krinete maana yake to Condemn, au making a negative assessment of a person or thing, kufanya maamuzi hasi dhidi ya mtu au kitu.

Warumi 14:10-12 “Lakini wewe je! Mbona wamhukumu ndugu yako? Au wewe je! Mbona wamdharau ndugu yako? Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu. Kwa kuwa imeandikwa, Kama niishivyo, anena Bwana, kila goti litapigwa mbele zangu; Na kila ulimi utamkiri Mungu. Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu.”

2Wakorintho 5:10 “Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.”


Daniel 12:2-3 “Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele. Na walio na hekima watang'aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang'aa kama nyota milele na milele.”

Muhubiri 12:14 “Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.”

Ufunuo 20:11-12 “Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana. Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.”  
     

Ufufuo huu ni wa hukumu ya adhabu,(Krima) na itakuwa ni hukumu ya aibu kwa sababu Neno Krima linalotumika kuelezea hukumu ya adhabu lina maana ya hukumu isiyohukumu matokeo tu bali inayohusu utafiti wa kina na uzingativu wa kila kilichofanyika kuanzia kwenye dhamiri na machakato mzima wa tukio pamoja na uzito wa ushahidi na mazingira  katika mtazamo wa kibinadamu, lakini katika mtazamo wa kiungu hukumu hii inahusisha hukumu iliyo sawasawa na Haki ya Mungu na tabia yake, na kwa kuwa Mungu ni mkamilifu hukumu yake itakuwa sahihi  na madhara au adhabu itakayoambatana na hukumu hii itakuwa ni sahihi, kwa hiyo hukumu yake itakuwa ni matokeo na ufunuo ulio sahihi ukiingia ndani katika dhamiri ya mwanadamu kwa hiyo itakuwa ni hukumu ambayo hata yeye anayehukumiwa atakubaliana na ile adhabu atakayopewa au ataridhishwa na maamuzi ya jaji mkuu Yesu Kristo.   
     

Hukumu isiyo ya adhabu – Krino

Hukumu hii isiyo ya dhabu ni hukumu inayowahusu wale wote ambao wamemuamini Yesu Kristo hawa kimaandiko hawahusiki katika hukumu ya adhabu (Krima), na badala yake hawa wana adhabu iitwayo Krino hii ni hukumu isiyo ya adhabu imetajwa na Paulo Mtume katika:-

Warumi 8:1-2 “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti

Warumi 8:33-34. “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki.Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea.”

Krino ni hukumu isiyo ya adhabu ambayo itawahusu watu waliookolewa, yaani wale waliomuamini Yesu hawatakutana na hukumu ya adhabu lakini watakutana na hukumu itakayofuatilia kwa haki, kwanini mtu Fulani alifanya jambo Fulani na thawabu yake itakuwa ni thawabu gani? Hukumu hii katika tamaduni za kiyunani Mgeni rasmi hukaa katika kiti kinachoitwa Bema au jukwaa au sehemu maalumu iliyoinuka kwaajili ya kutoa thawabu, za kimichezo ambapo wanamichezo wanapata thawabu au medali kulingana na kazi waliyoifanya na hakuna madhara kwa waliokosa medali. Hii ni hukumu ya watakatifu ni hukumu ya kutoa hesabu mbele za Kristo kwa kile tulichofanya. Katika somo la ufahamu kuhusu maswala ya hukumu The doctrine of Judgement Krino kiyunani kwa kiingereza ni to separate, put asunder, to pick out, Select, choose, to approve, esteem, to prefer, to give an opinion, to determine, resolve, decree, ni hukumu ya kutenganisha, kuchanganua, kuchagua, kuidhinisha, kuthaminisha, kupendelea, kutoa maoni, kuazimia, kuthibitisha, kwa hiyo itakuwa ni hukumu ya kuja kuthibitisha nani anafaa kuwa nini katika ufalme wa Mungu na sio kwa kusudi la kuadhibu.

1Wakorintho 3:12-15 “Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au majani au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa dhahiri. Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. Kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa, atapata thawabu. Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara; ila yeye mwenyewe ataokolewa; lakini ni kama kwa moto.”

Mathayo 25:14-28 “Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake. Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri. Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano. Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida. Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake. Baada ya siku nyingi akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao. Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana, uliweka kwangu talanta tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida. Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako. Akaja na yule aliyepokea talanta mbili, akasema, Bwana, uliweka kwangu talanta mbili; tazama, talanta nyingine mbili nilizopata faida. Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako. Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya;basi nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako. Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya; basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake. Basi, mnyang'anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi

Mathayo 24:45-46 “Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo.”

Hukumu hii ni hukumu ya watakatifu, kila mtu aliyeokolewa anapaswa kumtumikia Mungu, na Kristo atakapokuja kulinyakua kanisa, pale mawinguni itakuwepo nafasi ya kutoa taji na karamu ya mwana kondoo wakati huu kila mkristo atahukumiwa sawa na kazi aliyoifanya na jinsi na namna alivyoitumia talanta aliyopewa kwa uaminifu au vinginevyo na hapo thawabu zitatolewa, hakutakuwa na adhabu lakini kila mtu atastahili heshima yake kulingana na bidii, akili, muda na namna tunavyojitoa kwa Mungu ikiwa ni pamoja na kuwalisha watu wake, kwa hiyo kama sisi ni wachungaji tuwalishe watu chakula yaani neno la Mungu kwa wakati wake, kama una kipawa chochote kile kitumie kwa kadiri uwezavvyo na kwa kadiri ya neema huku ukiwa na dhamiri safi kwa sababu hukumu hii ni hukumu isiyoepukika pia katika hukumu hii hakuna mtu anayeweza kuwashitaki watu wa Mungu kwa sababu zozote wala hakuna mtu anayeweza kutuhukumu na kudai kuwa hawa ni wakosa, hukumu hii ni hukumu isiyo na madhara.        
    

Hukumu isiyotarajiwa – Aprosmenos

Katika hukumu zote zilizotajwa hapo juu, hii ndio hukumu itakayoshangaza watu kuliko hukumu zote, katika hukumu hii maamuzi atakayoyatoa Yesu Kristo yatadhihirisha uwezo wake mkubwa na hekima yake kubwa na ile hali ya kuwa yeye ni Bwana na hakuna mtu wa kumuamulia lolote wala kutabiri lolote, hukumu hii inadhihirisha kwamba Mungu mwenyewe ana haki ya kuamua na uwezo wake wa kuhukumu ni wa hali ya juu na wa tofauti sana.
 

Hukumu hii iko katika maamuzi ya Mungu mwenyewe na inaitwa hukumu isiyotabirika katika lugha ya kiyunani linatumika neno hilo Aprosmenos ambalo kwa kiingereza ni unanticipated, unforeseen, unexpected, difficulties  predicted kwa hiyo ni hukumu isiyotegemewa, ni hukumu isiyotarajiwa, ni hukumu isiyotabirika ni hukumu ambayo ni ngumu kimatazamio, hukumu hii iko chini ya maamuzi ya Mungu mwenyewe bila kujali kuwa kuna haki au hakuna haki mfano lakini iko haki ambayo Mungu mwenyewe katika mtazamo wake huiona lakini wanadamu hawawezi.

Warumi 9:10-16 “Wala si hivyo tu, lakini Rebeka naye, akiisha kuchukua mimba kwa mume mmoja, naye ni Isaka, baba yetu, (kwa maana kabla hawajazaliwa wale watoto, wala hawajatenda neno jema wala baya, ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua, si kwa sababu ya matendo, bali kwa sababu ya nia yake aitaye), aliambiwa hivi, Mkubwa atamtumikia mdogo. Kama ilivyoandikwa, Nimempenda Yakobo, bali Esau nimemchukia.Tuseme nini basi? Kuna udhalimu kwa Mungu? Hasha! Maana amwambia Musa, Nitamrehemu yeye nimrehemuye, nitamhurumia yeye nimhurumiaye. Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu.”

Warumi 9:20-21 “La! Sivyo, Ee binadamu; wewe u nani umjibuye Mungu? Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba, Kwani kuniumba hivi? Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima? 

Unaona ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua Maneno haya yanaonyesha kuwa mwanadamu awaye yote anapokuwa na kesi mahakamani awe amekosa au awe hajakosea bado anakuwa na mashaka kwa sababu mwenye maamuzi ya mwisho ni hakimu au jaji mwenyewe, kwa hiyo ni muhimu kufahamu kuwa iko mamlaka ya Mungu mwenyewe inayoweza kuamua na kuhukumu hata kama jambo linaonekana kuwa sawa machoni pako mfano;

1.       Luka 10 38-42 “Ikawa katika kuenenda kwao aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake.Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake.Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie.Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.”

Kwa mila na tamaduni za kimashariki wewe na mimi tunge muhukumu Mariamu kama binti mvivu na tungemkubali Martha kama mwanamke mchapakazi, lakini pale Martha alipoinua kinywa chake kumuhukumu Mariamu Bwana katika hukumu yake isiyotarajiwa anahukumu kuwa Martha ni changamoto kubwa sana na Mariamu ndiye yuko sahihi. Martha alikuwa na makosa makubwa sana kuliko Mariamu, Martha alikuwa akimfokea Yesu!  BWANA HUONI VIBAYA? Ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu?

Kumsikiliza Yesu ndio tukio la Heshima kubwa sana, na alikuwa akipokea Baraka kubwa za ushirika na Yesu, ambapo Martha kwa sababu ya kulalamika kwake alikuwa na msongo tu wa mawazo, haikuwa vibaya kuandaa kwaajili ya mgeni, lakini alijaa hukumu dhidi ya Yesu na Ndugu yake Mariamu, na kwa sababu hiyo alipoteza point katika hukumu kwa sababu ya manung’uniko

 

Wafilipi 2:14-15 “Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano,mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu,”

                 

Yesu hakumwambia Martha akae chini, kwani alikuwa anafanya jambo jema, na wala hakumwambia Mariamu inuka kwani naye alikuwa akifanya jambo jema, mmoja akimtumikia na mwingine akisikiliza,  wako wakristo na watumishi wa Mungu ambao hutumika sana, na wako ambao huomba sana na kutafakari wote wanaitenda kazi iliyo njema, kosa kubwa ni pale unapoanza kuwakosoa wengine na kufikiri kuwa wewe ndiye bora zaidi kwa sababu unafanya hicho unachikifanya, Jambo kubwa na la msingi na la muhimu ni uhusiano na Yesu Kristo, na Mariamu alikuwa ameligundua hilo, na hakuna mtu angeweza kumtenga na hilo, Mariamu kwa jicho la kibinadamu alionekana ni mvivu lakini kwa jicho la Yesu Mariamu alikuwa anampenda Yesu, alichukua muda kuwa na Yesu kwake Yesu alikuwa muhimu kuliko kupika, unalolifanya linaweza kuwa sio tatizo, lakini tatizo ni pale unapoanza kuamsha kinywa kwaajili ya wengine, Uhusiano wetu na Mungu ni jambo jema ambalo hakuna mtu anaweza kutuondolea. Mariamu alichagua fungu jema na hakuna wa kumuondolea, Ukichagua ushirika na Yesu hakuna mtu atakuondolea ushirika huo watakuondoa kwenye mengine lakini hakuna kitakachokutenga na Upendo wake Kristo.

 

2.       Marko 9:38-40 “Yohana akamjibu, akamwambia, Mwalimu, tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi. Yesu akasema, Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya;kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu.”

 

Hakuna mtu aliyekwenda kwa Yesu Kristo/Mungu akiwa anamshutumu mwingine na Yesu akakubaliana naye hata siku moja, kila wakati katika maisha ya Yesu alipoletewa kesi, Kesi hiyo iliwageukia walioleta, na hukumu kuwapata wao, katika tamaduni za kikanisa na madhehebu watu hujidhania kuwa wao ni wao na wao ndio wenye Yesu peke yao kama Yohana hapo, kwa hiyo walivyoona kuna anayetoa pepo kama wao lakini si wa dhehebu lao alitaka kuwazuia kuwanyima kibali, Lakini Yesu alikosoa vikali mtazamo wao.Wako watu wanaofikiri kuwa ni wao tu ndio wenye mamlaka au hatimiliki na Yesu, wao ndio bora, tabia ya aina hii inamuuzi sana Mungu, unaposhindana na kila mtu anayetumia jina la Yesu kwa kujifikiria kuwa wewe ndio wa muhimu na unapaswa kulitumia jina hilo unajiweka kwenye hatari ya kupingana na Yesu mwenyewe.

 

3.       Warumi 11:2-4 “Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali. Au hamjui yale yaliyonenwa na maandiko juu ya Eliya? Jinsi anavyowashitaki Waisraeli mbele za Mungu,Bwana, wamewaua manabii wako, wamezibomoa madhabahu zako, nami nimesalia peke yangu, nao wananitafuta roho yangu.Lakini ile jawabu ya Mungu yamwambiaje? Nimejisazia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali.”

 

Eliya alikuwa nabii mkubwa sana wa Mungu, aliwahukumu waisrael kuwa wamewaua manabii wote wa Mungu na kuvunja madhabahu, zote za Bwana na kuabudu baali na kuwa ni yeye pakee amesalia (1Wafalme 19:10) Lakini Mungu alimjibu kuwa wako wengi ambao hawajapiga goti lao kwa baali, Mungu alikuwa anamthibitishia Eliya kuwa asijidhanie kuwa yuko pake yake Mungu ana watu wengi, hukumu ya Mungu wakati wote huthibitisha kuwa sisi ni wanadamu na hatuko sawa katika mitazamo yetu, Mungu ana jicho lake la kipekee katika kuyatazama mambo na hivyo tunapaswa kuwa wanyenyekevu sana na kuacha kuwashitaki watu wengine kwa Mungu.

 

4.       Katika mifano ya ufalme wa Mungu pia ambayo imebeba siri nyingi za Mungu utaweza kuona imejaa hekima na maarifa na uweza wa kiungu katika maamuzi ya namna ya kuhukumu, Yesu anafunua kuwa kuhukumu kwake kutakuwa mara zote kukiwaacha watu midomo wazi yatakuwa ni maamuzi ambayo yatawashangaza wengi kwa matokeo yake.

 

a.       Farisayo na mtoza ushuruLuka 18:9-14 “Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”

 

Katika mfano huu tunajifunza juu ya watu wawili waliopanda kwenda hekaluni kusali, mmoja alikuwa farisayo kwa hiyo ni wazi kuwa alikuwa myahudi wa madhehebu ya mafarisayo, alikuwa mcha Mungu na mtu aliyemwamini Mungu, pia alikuwa mtii kwa sheria (Torati) na aliielewa vema, na alikuwa mtu wa haki, hakutii tu sheria lakini alifanya zaidi ya sheria, kwa mujibu wa torati waisrael walitakiwa kufunga mara moja tu siku moja kwa mwaka (Siku ya upatanisho) lakini yeye alifunga mara mbili kila wiki  kwa hiyo alizidisha na kufanya zaidi ya sheria, Sheria ilimtaka mtu atoe fungu la kumi angalau ya sehemu Fulani tu ya mapato yake lakini yeye alitoa sehemu ya kumi ya kila aina ya kipato (mapato yangu yote) kwa hiyo hakuwa na dhambi, hakuwa myang’anyi, wala hakuwahi kudhulumu mtu, wala hakuwahi kuzini, kwa msingi huu basi kama ingelikuwa ni wewe na mimi farisayo huyu ni peponi moja kwa moja au tungekubaliana na sala yake na katika hukumu hatungemuhesabia kuwa hana shida yoyote Lakini hitimisho la Hakimu mkuu ni kuwa ajikwezaye atatushwa na ajishushae atakwezwa, Farisayo alikataliwa tatizo lilikuwa ni nini katika hukumu hii? Alijihesabia haki, alijidhania ya kuwa yeye ni mtakatifu, alijivuna, alipata kiburi cha kidini, hakufikiri kuwa naye anahitaji msamaha wa Mungu na rehema zake, alijifikiri ya kuwa anaweza kununua rehema za Mungu kwa matendo yake, alipiga vita wengine na kujiona ni mkamilifu kwa sababu ya matendo yake na kiburi, Katika macho ya Mungu alikataliwa Mungu huwapinga wenye kiburi na kuwapa neema wanyenyekevu, sio hivyo tu moyo wake ulijaa dharau dhidi ya watu wengine na alikuwa hana upendo, na zaidi ya yote alikalia kiti cha Mungu kwa kujifanya ndiye muhukumu,  

 

Mathayo 7:1-5 “Msihukumu, msije mkahukumiwa ninyi. Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa.Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au utamwambiaje nduguyo, Niache nikitoe kibanzi katika jicho lako; na kumbe! Mna boriti ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako.”

 

Mathayo 23:23-24 “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache. Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia.”

 

Farisayo alikataliwa katika hukumu, hii ndio hukumu ya kushangaza na isiyoweza kutabirika, tuna watu wengi sana wanaopanda kwenda kusali, tuna watu wengi sana wanafunga, sio wazinzi, ni wasafi lakini usafi huo ni wakwao wenyewe mioyoni mwao Mungu atawakataa, hukumu isiyotarajiwa itatufunulia mengi sana, tutaona mambo ya ajabu ya watu wote wanaojifikiria kuwa hawahitaji toba wamekamilika na wako safi lakini Yesu atawakataa hii itatushangaza ni hukumu isiyotarajiwa. Wote wenye juhudi ya kutenda mema na kudharau wengine kwa kujifikiri kuwa wao ni safi kuliko wengine, mahubiri yao yamejaa hukumu, maneno yao yamejaa kuhukumu wengine na kujifikiri kuwa wao wako sahihi na ni wasafi mno kumbe katika macho ya Mungu tunahitaji kuwa wanyenyekevu, na ni muhimu kwetu kukumbuka kuwa matendo mema sio kitu cha kushangaza kwa Mungu, tuliumbwa tukiwa wema, kwa hiyo unaweza kukuta mtu jhajamuamini Yesu na akawa ana matendo mema, Mungu anataka tuipokee zawadi ya wokobu kwa neema na kwa Imani na kutembea kwa neema na Imani, pasipo hiyo huwezi kumpendeza Mungu.

 

Waefeso 2:8-10 “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.”    

 

b.      Wafanyakazi katika shamba za mizabibu – Mathayo 20:1-16 “Kwa maana ufalme wa mbinguni umefanana na mtu mwenye nyumba aliyetoka alfajiri kwenda kuajiri wakulima awapeleke katika shamba lake la mizabibu. Naye alipokwisha kupatana na wakulima kuwapa kutwa dinari, aliwapeleka katika shamba lake la mizabibu. Akatoka mnamo saa tatu, akaona wengine wamesimama sokoni wasiokuwa na kazi; na hao nao akawaambia, Enendeni nanyi katika shamba langu la mizabibu, na iliyo haki nitawapa. Wakaenda. Akatoka tena mnamo saa sita na saa kenda, akafanya vile vile. Hata kama saa kumi na moja akatoka, akakuta wengine wamesimama, akawaambia, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?  Wakamwambia, Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri. Akawaambia, enendeni nanyi katika shamba la mizabibu. Kulipokuchwa, yule bwana wa shamba akamwambia msimamizi wake, Waite wakulima, uwalipe ujira wao, ukianzia wa mwisho hata wa kwanza. Na walipokuja wale wa saa kumi na moja, walipokea kila mtu dinari. Na wale wa kwanza walipokuja, walidhani kwamba watapokea zaidi; na hao pia wakapokea kila mtu dinari. Basi wakiisha kuipokea, wakamnung'unikia mwenye nyumba, wakisema, Hao wa mwisho wametenda kazi saa moja tu, nawe umewasawazisha na sisi tuliostahimili taabu na hari za mchana kutwa.Naye akamjibu mmoja wao, akamwambia, Rafiki, sikudhulumu; hukupatana nami kwa dinari? Chukua iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe.Si halali yangu kutumia vilivyo vyangu kama nipendavyo? Au jicho lako limekuwa ovu kwa sababu ya mimi kuwa mwema? Vivyo hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho

 

Kuna mengi ya kujifunza pia kuhusu hukumu ya Mungu katika mfano huu, sitaki kueleza kila kitu kilichomo katika mfano huu lakini mfano huu unazungumzia mwenye nyumba, Biblia ya kiingereza inatumia neno landowner yaani mwenye shamba ambaye alikuwa amekusudia kazi yake iishe, alitoka kutafuta wafanya kazi, kwaajili ya shamba lile, siku zile malipo ya siku nzima yalikuwa ni dinari, mwenye shamba aliajiri yeye mwenyewe aliajiri watu wa saa 12 alfajiri, kisha saa 6 kisha Saa 9 na kisha saa 11,  na alipatana nao kuwalipa (zingatia malipo kwa siku ni Dinari) au unaweza kuweka Elfu kumi kwa siku, kwa kazi ya masaa 12.  Hawa wengine waliajiriwa tu kwa mapenzi ya mwenye shamba na aliwaahidi atawapa haki yao, ilipofika jioni aliamuru wote walipwe akianza na wale wa saa 11 ambao kimsingi walifanya kazi saa moja tu. Hii ni kwa sababu mwenye shamba ni mkarimu, lakini walipolipwa wale walioajiriwa wa saa 12 alfajiri walilalamika na kulaumu kuwa mwenye shamba hakuwa ametenda haki kwa sababu wako watu wamefanya kazi saa moja tu na amewalipa sawa na wao waliofanya kazi tangu asubuhi, Kwa hiyo walimuhukumu mwenye shamba kwa kuwa mkarimu na mwema. Hii inatufundisha nini? Mungu anauwezo wa kuamua na lolote atakaloliamua sawa na ukarimu wake huna haki ya kulalamika kwa sababu hajakudhulumu yeye huweza kuamua kumrehemu yeyote yule na hatupaswi kuwa na wivu?

 

Warumi 9:18-21 “Basi, kama ni hivyo, atakaye kumrehemu humrehemu, na atakaye kumfanya mgumu humfanya mgumu. Basi, utaniambia, Mbona angali akilaumu? Kwa maana ni nani ashindanaye na kusudi lake?La! Sivyo, Ee binadamu; wewe u nani umjibuye Mungu? Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba, Kwani kuniumba hivi? Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?

 

Waefeso 2:8-9 “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.”

 

Dinari inazungumzia wokovu, ambapo Mungu anaweza kumuokoa mtu wakati wowote na thawabu ikawa moja kama alivyomuokoa mwizi pale msalabani, lakini wale waliokuweko kazini wali lalamika mbona unatulipa sawa?  Mara kadhaa tumekasirika na kuona wivu pale Mungu anapombariki mwingine, na kumuinua kuliko sisi kwa mapenzi yake tunalalamika kwa sababu ya wivu, tunalalama na kumuona Mungu kama hayuko sawa vile ni kama anapendelea wakati tunapojilinganisha na wengine na wakati mwingine tumewapiga vita watu kwa sababu ya wivu wetu, tunafanya ujinga na Mungu anazo sababu za kutuhukumu kwa kuhukumu wema wake na ukarimu wake, wokovu ni kwa neema tu na kamwe hatuwezi kuutendea kazi, wale wanaofikiri kuwa kwa kazi zao watapata kibali kikubwa kwa Mungu wanajidanganya mfano huu unafunua vilevile hukumu isiyotarajiwa ya Mungu.

 

c.       Mfano wa yule kaka mkubwaLuka 15:11-32 “Akasema, Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake. Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati. Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu. Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana.Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena. Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia. Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo. Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini? Akamwambia, Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima. Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi. Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu;lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona. Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako.Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.”

 

Nauita mfano wa kaka mkubwa kwa sababu katika mtazamo wa Mungu ndiye aliyekuwa na matatizo makubwa zaidi ya Mwana mpotevu, Baba wa mwana mpotevu alikuwa anasikitika kumpoteza kijana wake na aliporejea nyumbani alilia akamkumbatia na kumvika mavazi mazuri kisha akamfanyia sherehe kubwa, Kaka mkubwa alikasirika, akasusa na kugoma kuingia ndani, akamuhukumu baba yake na mdogo wake, alimshutumu kuwa mdogo wake huyo ametapanya mali pamoja na makahaba, na baba yake ameonyesha ukirimu jambo ambalo hajawahi kulifanya kwa kaka mkubwa, kwa hiyo alijawa na hasira, na wivu na kulaumu ukarimu wa baba yake mfano huu kama mingine iliyotangulia unatahadharisha kuwa Mungu atakapohukumu wanadamu atafanya mapinduzi ambayo wale wanaojifikiria kuwa ni wenye haki watalia na kushangaa, wale wanaojifikiria kuwa hawajawahi kumkosea Mungu kwa lolote, basi wanaweza kumkosea Mungu kwa kuhukumu wengine, au kwa kumlaumu Mungu au maamuzi ya Mungu ya kikarimu, iko mifano Mingi ambayo muda usingeliweza kutosha kuichanganua lakini unaanza kuelewa

Kwaajili ya Hukumu hizi za kushangaza za Mungu, na tabia zake ni muhimu sana kuwa wanyenyekevu na kuogopa sana hukumu ya Mungu, hakuna kitu kinatisha kama hukumu ya Mungu, wakati wote kujifikiri kuwa sisi ndio tuko sawa na wenzetu hawako sawa, kunakuweka katika hatari ya kuingia katika hukumu isiyoepukika na hukumu za kushangaza kwaajili ya aina hii ya mtazamo ni lazima tukubali na kuelewa ya kuwa hata siku ya mwisho siku ya hukumu Mungu akisema nimekusudia kuwarehemu watu wote na watu wote nataka waingie peponi au katika ufalme wake je wewe na Mimi tutakubaliana na hukumu hiyo? Tutaona kuwa Mungu amehukumu kwa haki? au tutadhani kuwa Mungu ana upendeleo acha kujifikiri kuwa wewe ni bora zaidi kuliko wengine, acha kukomalia makosa ya wengine Mungu nadhani anataka tushughulike na maisha yetu zaidi kuliko ya wengine.

Mathayo 7:3-5 “Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au utamwambiaje nduguyo, Niache nikitoe kibanzi katika jicho lako; na kumbe! Mna boriti ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako.”

Je utaweza kuiepuka hukumu ya Mungu? Ni hukumu isiyoepukika inatutaka tuwe wanyenyekevu sana sisi kama wanadamu hatuna cha kujivuna katika jambo lolote lile, wakati wote tuombe rehema na neema ya Mungu na kuendelea kumtafuta bwana kwa mioyo yetu yote, na zaidi ya yote turuhusu wakati wote neno la Mungu lituhukumu na kutubu pale linaposhughulika na maovu yetu, Mungu atatubariki na kwa neema yake atatufunulia kweli yetu yote Bwana yu karibu na moyo uliopondeka tutembee kwa unyenyekevu na kujishusha mbele za Mungu aliye hai.

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima

Tafadhali naomba maoni yako 0718990796

Jumapili, 21 Julai 2024

Utamlilia Sauli hata lini?


1Samuel 16:1-3 “Bwana akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe. Samweli akasema, Nawezaje kwenda? Sauli akipata habari, ataniua. Basi Bwana akasema, Chukua ndama pamoja nawe, ukaseme, Nimekuja ili kumtolea Bwana dhabihu. Ukamwite Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonyesha utakayotenda; nawe utamtia mafuta yule nitakayemtaja kwako.”


Utangulizi:

Kaka zangu dada zangu Leo tutachukua muda kiasi kutafakari ujumbe wa Muhimu wenye kichwa “Utamlilia Sauli Hata lini?” Kama tulivyosoma katika kifungu cha msingi, ujumbe huu una maana kubwa na zaidi sana leo unatufundisha umuhimu wa kusahau mambo yaliyopita ambayo kimsingi yanaweza kuwa kikwazo cha kutupeleka katika mambo mapya au hatua nyingine ambayo Mungu ametuandalia. Wote tutakuwa tunakumbuka kuwa Mungu alimfunulia Samuel Nabii kuhusu Mfalme Mpya wa Israel na kumuagiza akampake mafuta.

1Samuel 9:15-17 “Basi Bwana alikuwa amemfunulia Samweli, siku moja kabla Sauli hajamwendea, akisema, Kesho, wakati kama huu, nitakuletea mtu kutoka nchi ya Benyamini, nawe mtie mafuta ili awe mkuu juu ya watu wangu Israeli, naye atawaokoa watu wangu na mikono ya Wafilisti; maana nimewaangalia watu wangu, kwa sababu kilio chao kimenifikilia.Hata Samweli alipomwona Sauli, Bwana akamwambia, Huyu ndiye niliyekuambia habari zake; huyu ndiye atakayewamiliki watu wangu.”                

Pamoja na kuwa ni kweli Sauli alikuwa ni chaguo la Mungu, Na Samuel alimtia mafuta Lakini ulifika wakati ambapo Mungu alikuwa na mpango mwingine, na hivyo alimkataa Sauli na kumtaka nabii Samuel ampake mafuta Mfalme mwingine mwenye nguvu zaidi na mwenye kuupendeza moyo wake na aliye mwema kuliko Sauli, Mfalme huyo alikuwako Bethelehemu katika nyumba ya Yese. Kukataliwa kwa Sauli kuliwekwa wazi mapema kwa neno la kinabii ona;-

1Samuel 15:26-28 “Samweli akasema, Sitarudi pamoja nawe; kwa sababu umelikataa neno la Bwana, Bwana naye amekukataa wewe, usiwe mfalme wa Israeli. Naye Samweli alipogeuka, aende zake, Sauli akaushika upindo wa vazi lake, nalo likararuka. Basi Samweli akamwambia, Leo Bwana amekurarulia ufalme wa Israeli, naye amempa jirani yako, aliye mwema kuliko wewe

Hata hivyo Samuel kama nabii inaonekana aliendelea Kumuombea neema Saul kwa majuma kadhaa, alimpenda, alitamani aendelee kuwa naye, ilikuwa ni tabia ya Samuel kuwaombea wana wa Israel na mfalme pia kwa mujibu wa maandiko Samuel kuacha kuwaombea Israel kwake ilikua ni kama kufanya dhambi

1Samuel 12:23 “Walakini mimi, hasha! Nisimtende Bwana dhambi kwa kuacha kuwaombea ninyi; lakini nitawaelimisha katika njia iliyo njema, na kunyoka

Kwa hiyo huenda Samuel aliendelea kumuombea Sauli kwa Mungu,  na hakuacha alisikitika moyoni kumpoteza kijana yule mzuri aliyemtia mafuta yeye mwenyewe shujaa, mtu mrefu Mzuri kutoka kabila la Benjamin lakini Mungu aliyakataa maombi ya Samuel kwa sababu alikuwa amekusudia kuwapa Israel Shujaa, kijana mzuri zaidi, anayeupendeza Moyo wa Mungu mtu aliye mwema na atakayekuwa bara kubwa kwa Israel, Hivyo Mungu alimkemea Samuel na kumuuliza utaendelea kumlilia Sauli mpaka lini ikiwa mimi nimemkataa, inawezekana ikawa ni stori nzuri sana na imenyooka haiitaji tafasiri yoyote, lakini leo hii katika kisa hiki, Mungu anataka kusema nasi kuhusu swala la kuachilia Mambo ya kale  ili aweze kutuingiza katika mambo mapya, hupaswi kukaa chini na kuyalilia mambo yaliyopia hata kama ni mazuri kiasi gani kwani kuyalilia hayo kunatufanya tusipige hatua katika kuuendea ukurasa mpya ambao Mungu anataka uufungue, ili tukue na kuelekea katika kiwango kingine, Tutajifuza somo hili Utamlilia Sauli Hata lini kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Umuhimu wa kusahau yaliyopia.

·         Umuhimu wa kutambua mapenzi ya Mungu.

·         Utamlilia Sauli hata lini?.


Umuhimu wa kusahau yaliyopita.

1Samuel 16:1 “Bwana akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe.”

Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu anapokuwa na mpango mpya katika maisha yetu, anapenda tuelewe na kusonga mbele na kuyasahau yaliyopita, siku zote kuendelea kulia lia kwaajili ya mambo ya zamani kunaweza kutuzuia kuona yale mapya ambayo Mungu ametuwekea mbele yetu, na siku zote mbele ni kuzuri zaidi, kwa hiyo ni lazima tuukubali kusahau yaliyopita, ni vigumu sana wakati mwingine kusahau yaliyo nyuma na wakati mwingine inaonekana kama ni jambo lisilowezekana lakini historia ya nyuma inaweza kuwa kikwazo kikubwa cha mpango na mapenzi ya Mungu kwaajili yetu na kwa sababu hiyo ni lazima tuyachuchumilie yaliyo mbele na kukubali kusahau yote yaliyopita.

Wafilipi 3:13-14 “Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.”

Paulo mtume aliyepitia dhiki na mateso mengi sana Hakubali hata kidogo kukaa katika hayo lakini wakati wote alikuwa akijitahidi kuwaza mbele, Ni mapenzi ya Mungu kwetu kusahau mambo yaliyopita hususani yale ambayo yametuletea maumivu makubwa katika maisha yetu,  au makosa amkubwa ambayo tumewahi kuyafanya huko nyuma, Mungu mwenye rehema na neema wakati wote hutupa nafasi ya pili, na ya tatu na ya nne na ya tano na ya sita na ya saba na ya nane na kadhalika yeye anatutaka wakati wote tusilie kwaajili ya yaliyopita na badaa yake tusonge mbele bila kujali kile ulichokipitia, iweni talaka, au uonevu, au umepoteza kazi, au umeingia katika changamoto zozote nzito, au umekosea sana, au umefiwa au ulifeli vyovyote vile Mungu anatutaka tusonge mbele na kuacha kumlilia Sauli kwa sababu ana mpango mpya nawe, Mwana riadha wakati wote anapaswa kuangalia mbele, na kuendelea na mbio, kwani kuangalia nyuma kunaweza kuwa kikwazo, kwa msingi huo usipoteze muda na maswala yaliyopita yawe mazuri au mabaya wewe angalia mbele, Mungu anayekuwazia mema na mpango mpya!

Isaya 43:18-19 “Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani. Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani.”

Ilikuwa ngumu kwa Samuel kuacha kumlilia Sauli, kwa kuwa alikuwa Mfalme Mzuri na alipewa na Mungu, Lakini sasa Mungu ana mpango mpya ulio bora zaidi, kwa hiyo, yuko Daudi mwana wa Yese kwaajili yako hivyo sahahu utawala na ufalme uliopita chukua chupa yako umtie mafuta yule ambaye Mungu atakuelekeza     

Umuhimu wa kutambua mapenzi ya Mungu

Mungu alikuwa na mpango mpya kwaajili ya Israel Kama alivyo na mpango mpya kwaajili yako, Mungu alikuwa amechagua mmoja wa wana wa Yese na alikuwa yuko tayari kumpaka mafuta Ili atawale baada ya Sauli na ulikuwa ni wajibu wa Samuel kwenda Bethelemu na Chupa yake ya mafuta  na kumtia mafuta yule ambaye Mungu alikuwa amemkusudia, hapa ulikuweko mtihani wa kuyajua mapenzi ya Mungu na ulikuwepo mpango unaohitaji subira, wakati huo ni lazima tuaachane na mambo tuliyoyazoea kwa sababu Mungu ana mpango mpya, sauti zinaweza kuwa nyingi sana wakati tunauendea mpango mpya wa Mungu na tunaweza kufikiri kuwa ni huu au ule  lakini hatimaye Mungu atakufunulia mpango wake kamili ambao huo Yesu yumo ndani yake, The best is yet to come !

1Samuel 16:6-11 “Ikawa walipokuja, alimtazama Eliabu, akasema, Yakini masihi wa BWANA yupo hapa mbele zake. Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo. Ndipo Yese akamwita Abinadabu, akampitisha mbele ya Samweli. Naye akasema, Bwana hakumchagua huyu. Ndipo Yese akampitisha Shama. Naye akasema, wala Bwana hakumchagua huyu. Yese akawapitisha wanawe saba mbele ya Samweli. Samweli akamwambia Yese, Bwana hakuwachagua hawa. Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja huku.”            

Kujua mapenzi ya Mungu kwaajili ya mpango mpya sio kazi nyepesi, ilimsumbua Samuel ilimsumbua Yese, hawakujua mfalme mpya ni nani, na kwakuwa hakuwepo pale walihitaji subira, tunahitaji subira kuyajua mapenzi ya Mungu, Katika maisha yetu tunaweza kukutana na changamoto kama hizi, wakati huu tunapaswa kuongeza uwezo wa kuisikia sauti ya Mungu, na kuwa na moyo wa Subira, ili kuachana na mazoea na kuyajua mapenzi yake kwa hiyo kuna umuhimu wa kuyatambua mapenzi ya Mungu, kuna mambo matatu tu tunaweza kuyafanya wakati huu

1.       Kujaza pembe Mafuta – hii inahusiana na kufanya maandalizi ya kiroho kwa hiyo ni muhimu kwetu kujitoa kwa Roho Mtakatifu, kwa kuomba na kujitakasa na kutubu, tendo hili litatuweka karibu na Roho Mtakatifu  na kutusaidia kuijua sauti yake  na zaidi ya yote inatusaidia kuyatii mapenzi yake na kuyajua

 

1Samuel 16:4-5  “.Samweli akafanya hayo aliyosema Bwana, akaenda Bethlehemu. Wakaja wazee wa mji kumlaki, wakitetemeka, nao wakasema, Je! Umekuja kwa amani? Naye akasema, Naam, kwa amani; nimekuja kumtolea Bwana dhabihu; jitakaseni; njoni pamoja nami kwenye dhabihu. Akawatakasa Yese na wanawe, akawaita kwenye dhabihu

 

Matendo 13:1-3 “Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.”

 

2.       Kutii maagizo ya Mungu – Samuel alitii maagizo ya Mungu na kukubalia kumsahau Sauli na akaenda kwa Yese ili kumtia mafuta Daudi, Tunapaswa kuyatii maagizo ya Mungu na kusonga mbele bila kuchelewa, ni muhimu kufahamu kuwa mambo ya zamani yanakamata sana na yanataka kuturudisha nyuma, Lakini Mungu ameruhusu tusonge mbele kwa hiyo hatuna budi kwenda pale Mungu anaposema twende Samuel akafanya hayo aliyoyasema Bwana, akaenda Bethelehemu kule Bwana atakakosema wende nenda na yale maagizo ambayo Bwana amekuagiza kuyafanya yafanye kwa kutumia Hekima chini ya neema yake.

 

3.       Ruhusu Mpango mpya wa Mungu -  Samuel na Yese walikubali mapenzi ya Mungu, alipokuja yeye aliyesubiriwa na asiyetazamiwa Samuel alimtia mafuta kwani Bwana alisema naye huyu ndiye, kwa hiyo walilazimika kumsahau Sauli na kumkubali Daudi, Mambo ya zamani ambayo hayana nafasi tena katika maisha yetu na ambayo hayako katiika mpango wa Mungu ni lazima tuyafukuzilie mbali, ili lile jipya ambalo Mungu amekusudia kulifanya liweze kuchukua nafasi.

 

1Samuel 16:12-13 “Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza. Bwana akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye. Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama.”                

Utamlilia Sauli hata lini?

Utamlilia Sauli hata lini? Ni swali ambalo Mungu alimuuliza Samuel na ni swali ambalo linatuita katika kutafakari maisha yetu, Je kuna jambo bado unalishikilia? bado una shikilia mambo ya zamani ambayo Mungu anataka tuyaache na kuyasahau? Je unajiandaa kwa mambo mapya?  Tunapotulia katika maombi hatuna budi kuendelea kumuomba Mungu atuongoze na kutuandaa na kutuweka tayari ili tukubali kuyatii mapenzi yake, na kupokea kile kipya ambacho Mungu amekikusudia katika maisha yetu  na Mungu ni mwema atakutendea mema usilie!

Kuacha mambo ya zamani kunahitaji ujasiri, na Imani, Samuel alihitaji ujasiri na kukubali mabadiliko kwa Imani, kwa sababu Mungu alimthibitishia kuwa ana mpango bora zaidi kwaajili ya Israel Mpango wenye manufaa sio kwaajili ya Israel tu  bali kwa ulimwengu mzima, Mungu alikuwa amemkusudia mwana wa Daudi kuja kukaa katika kiti cha Enzi milele na huyo ni Yesu Kristo, uwepo wa Mungu uko mbele, Mungu alikuwa amekwisha kumuacha Sauli na sasa Roho Mbaya ilikuwa inamkalia, Mahali ambapo uwepo wa Mungu umeondoka, Shetani na mapepo huchukua nafsi

1Samuel 16:14-15. “Basi, roho ya Bwana ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa Bwana ikamsumbua. Nao watumishi wa Sauli wakamwambia, Angalia, sasa roho mbaya kutoka kwa Mungu inakusumbua.”

Mungu alikwisha ondoa uwepo wake kwa Sauli na kuruhusu mashetani kumkalia, Mungu anapotushauri jambo ni vema kwenda nalo, kwa kuwa huko ndiko uwepo wake unakokwenda hatupaswi kujivunia Sauli tena kwani sasa ni nyumba ya mapepo na uwepo wa Mungu umehama, uwepo wa Mungu sasa ulikuwa uko juu ya Daudi kwa nguvu!

1Samuel 16:13 “Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama.”

Acha kulilia ya nyuma Songa mbele Mungu anampango mwema zaidi msahau Sauli, Mungu anaye Daudi wako je utaendelea kumlilia Sauli hata lini ikiwa mimi nimemkataa? Uwepo wa Mungu uko mbele!, Usilie kwaajili ya kazi uliyofukuzwa, usilie kwaajili ya nyumba uliyohama, usilie kwaajili ya mchumba ambaye ameondoka, usilie kwaajili ya mke aliyekuacha, usilie kwaajili ya mume aliyekuacha, usilie kwaajili ya bosi aliyekuacha Mungu anao mpango mwingine kwaajili yako, usilie kwaajili ya uhamisho uliohamishiwa kuna kusudi kubwa na jipya kwaajili ya Mungu. Na Kwaajili yako na familia yako na watu wako!

1Wafalme 9:5 “ndipo nitakapokifanya imara kiti cha ufalme wako juu ya Israeli milele; kama nilivyomwahidia Daudi, baba yako, nikisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Israeli.”

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!.

Jumamosi, 13 Julai 2024

Ninyi si wa ulimwengu huu!

 

Yohana 15:18-21 “Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia. Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu. Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka.”




Utangulizi:

Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Yesu alikuwa akimaanisha ulimwengu utatuchukia kabisa, kwa sababu kwanza ulimwengu ulimchukia Kristo, Kwa hiyo kila mwanafunzi wa Yesu Kristo hapaswi kuona jambo hilo kuwa ni jambo geni, Kama ulimwengu ulimchukia Kristo kwa vyovyote vile hauwezi kuwakubali wafuasi wake.

Mathayo 10:22-25 “Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Lakini watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya Israeli, hata ajapo Mwana wa Adamu. Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumwa hampiti bwana wake.Yamtosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumwa kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mwenye nyumba Beelzebuli, je! Si zaidi wale walio wa nyumbani mwake?

Ulimwengu unachukizwa sana na watu waliomwamini Yesu na kumfuata, kwa sababu sio wa ulimwengu huu, wakati wanafunzi wa Yesu watatambulikwa kwa upendo wao kwa watu, watu wa ulimwengu huu watajulikana kwa chuki na wivu dhidi ya watu wa Mungu, wanafunzi wa Yesu sio wa ulimwengu huu kwa sababu wameitwa kutoka ulimwenguni kuingia katika ufalme wa mwana wa pendo lake, na kuuacha ufalme wa giza, kwa hiyo tuwapo katika maisha haya sisi wenyeji wetu uko mbinguni, na kwa sababu hiyo mkuu wa ulimwengu huu hawezi kuwa na furaha na watu waliookolewa, kwa sababu wao wameuacha ufalme wake, na hivyo anachukizwa nao, wale walio wa ulimwengu huu wao ndio wenyeji wa ufalme wa shetani au ufalme wa giza na hivyo hauwezi kuweko urafiki kati ya nuru na giza, kweli na uongo, na hivyo hakuwezi kuweko kwa Amani na upendo wa kweli kutoka katika dunia hii inayoongozwa na mfumo wa yule muovu, wala watu wa Mungu wasitarajie ya kuwa dunia itawatendea haki, kwa sababu mfumo wa ulimwengu huu unawatema!, Mfumo wa ulimwengu huu uko chini ya Shetani ambaye kimsingi hana nguvu kama za Bwana wetu Yesu, lakini hata hivyo anatawala mfumo wa uasi wa dunia na kunyunyizia ushawishi wake duniani. 

Yohana 14:30-31 “Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu. Lakini ulimwengu ujue ya kuwa nampenda Baba; na kama vile Baba alivyoniamuru; ndivyo nifanyavyo. Ondokeni, twendeni zetu.”       

Tutajifunza somo hili ninyi si wa ulimwengu huu kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Ufahamu kuhusu mkuu wa ulimwengu huu.

·         Kuchukiwa kwa watu wasio wa ulimwengu huu.

·         Jinsi watu wasio wa ulimwengu huu wanavyopaswa kuishi.


Ufahamu kuhusu mkuu wa ulimwengu huu.

Ni muhimu kufahamu kuwa Shetani ana majina mengi yanayomtambulisha kama mwenye mamlaka na ulimwengu huu, Katika maandiko Yesu anamtaja kama mkuu wa ulimwengu huu Katika

Yohana 14:30 Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu.  

Katika biblia ya kiingereza maneno hayo yanasomeka “I will not speak with you much longer, for the PRINCE OF THIS WORLD is coming. He has no hold on me” kwa hiyo shetani anaitwa mkuu wa ulimwengu huu, au kwa jina lingine, mungu wa dunia hii angalia au mfalme wa dunia hii, Kwa hiyo kimsingi Shetani ni mtawala wa dunia hii.

2Wakorintho 4:3-4 “Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.”  

Unaona katika andiko hili Shetani anaitwa MUNGU WA DUNIA HII.  Aidha katika maandiko mengine Shetani anaitwa MFALME WA UWEZO WA ANGA “The Prince of the air” hili unaweza kuliona katika kitabu cha Waefeso

Waefeso 2:1-3 Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi; ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine.”

Hii ina maana gani? Ni muhimu kufahamu kuwa katika lugha ya Kiyunani neno Prince of this world, mkuu wa ulimwengu huu, god of this age, mungu wa dunia hii, ruler of the kingdom of air, mkuu wa uweza wa anga huyu kwa kwa kiyunani anaitwa KOSMOKRATOR  kwa kiingereza COSMOCRATOR  maana yake RULER OF THE WORLD  neno hilo Kosmokrator limetokana na lugha ya asili ya dini za kipagani hususani Wanostiki na Wamarcion wakimaanisha ni lugha ya kiufundi ya kumtambulisha Shetani kutokana na kazi zake za uendeshaji wa ulimwenguni kwa hivyo utaweza kuona jina hilo Kosmokrator ni mkuu wa anga, au mtawala wa dunia hii au mwenye ushawishi wa akili na tabia na mwenendo, malengo, matumaini, falsafa, elimu, biashara, mawazo, fikra, ujasusi, udhibiti, na utaratibu wa kila kitu hapa duniani. Katika ulimwengu wa watu wasiookolewa ni muhimu ikafahamika wazi kuwa ulimwengu uko chini ya huyu Kosmokrator yaani Shetani. Kwa hiyo mifumo yote ya uendeshaji wa dunia hii na ushawishi wake uko chini ya mkuu wa anga anayetenda kazi sasa kwa wana wa kuasi.

Yohana 12:31Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje”. Kwa hiyo Mkuu wa anga anaitwa Kosmokrator wakati ulimwengu na mfumo wake wote unaitwa Kosmos,  Mapambo  na vipodozi vyote vinaitwa Kosmetikos, yaani art of beautification kwa hiyo neno Kosmos lilitumika pia kuelezea mfumo wa ulimwengu na ndio maana nyakati za kanisa la Kwanza mtu aliyeonyesha kuupenda sana ulimwengu alifikiriwa pia amekuwa adui wa Mungu.

Yakobo 4:4 . “Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu.”

Kwa hiyo Maandiko yanapomtaja shetani kama mkuu wa ulimwengu huu, yanafunua ule ukweli ya kuwa katika ulimwengu huu wako watu wanaoongozwa na mfumo wake na wanaofuata mfumo wake na wako chini ya mfumo huo na pia wale waliomwamini Yesu wako katika mfumo mwingine wanaishi duniani lakini wakiwa wamehamishwa katika ufalme huo wa giza na kuingizwa katika mfumo wa ufalme wa mwana wa pendo lake yaani Pendo la Mungu. Hii ina maana gani ina maana ya kuwa watu waliookoka hawako chini ya utawala wa shetani, kwa hiyo wao sio wa ulimwengu huu

Wakolosai 1:13-14 “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi;”             

Kuchukiwa kwa watu wasio wa ulimwengu huu

Kwa sababu mtawala wa ulimwengu huu yaani shetani amepokonywa mateka yaani watu waliookolewa, wakahamishwa katika ufalme wa Mungu, Shetani amekuwa adui mkubwa sana wa watu wa Mungu na anachukizwa nao sana. Yesu akilijua hilo anatuwekea wazi, kuwa nasi tutachukiwa sana na ulimwengu na hii ni kwa sababu ulimwengu huo huo haukumkubali Bwana Yesu.

Yohana 15:18-21 “Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi.Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia. Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu. Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka.”

Yesu anaendelea kukazia kuwa mtumwa si mkubwa kuliko Bwana wake, maana yake hali ile ile ambayo watu wanamfanyia Bwana wako ni hali ile ile ndiyo watakayo mfanyia mtumwa wake, Hali anayofanyiwa mwenye nyumba, ndiyo hiyo hiyo watakayofanyiwa wale wa nyumbani mwake, ikiwa walimsulubisha Bwana wetu Yesu Kristo hali kadhalika wanafunzi wa Yesu Kristo watasulubiwa na kupata mateso mengi, kwa sababu nao wataishi na kufanya kazi kama zile zile alizozifanya Yesu Kristo, Yesu ni Nuru ya ulimwengu hali kadhalika watu wa Mungu ni nuru ulimwenguni, na watu wa dunia hii wanapenda giza na ndio maana walimsulubisha Yesu Kristo wote wapendao kuishi kwa hali itokanayo na Kristo Yesu wataudhiwa

2Timotheo 3:10-12 “Bali wewe umeyafuata mafundisho yangu, na mwenendo wangu, na makusudi yangu, na imani, na uvumilivu,na upendo, na saburi; tena na adha zangu na mateso, mambo yaliyonipata katika Antiokia, katika Ikonio, na katika Listra, kila namna ya adha niliyoistahimili, naye Bwana aliniokoa katika hayo yote.Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa.”

Kwa hiyo wapenzi msione kuwa ni ajabu watu waliompokea Yesu, wakikutana na vikwazo vingi, wakikataliwa, wakidharauliwa, wakichukiwa na dunia, wakifanyiwa fitina, wakizushiwa, wakidhulumiwa, wakifanyiwa hila, wakihuzunishwa kwa namna mbalimbali, wakibaniwa, wakisalitiwa, wakitafuta kuuawa, Wakristo watapata mateso na uonevu kwa sababu ya Imani yao, watakutana na vipingamizi kwa sababu ya mifumo ya kipinzani ya dunia hii,  watatengwa na jamii na familia zao na dini zao,  kwa sababu hawakubaliki na mfumo wa ulimwengu huu, mifumo ya Kosmokrator iko kuanzia ngazi ya ulimwengu, mabara, mataifa, mikoa, wilaya na kila kijiji, na katika kila eneo nguvu ya ushawishi wa mkuu wa anga katika eneo hilo atapingana vikali na wakristo wa eneo husika akitumia aina ya ushawishi wake, katika eneo husika kuwapiga vita wakristo na vita hii iko katika ulimwengu wa roho.

Waefeso 6:10-13 “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.”

Katika vita hivi na mfumo wa ulimwengu huu wakristo hawapaswi kuogopa kwa sababu mkuu wa ulimwengu huu hana kitu kwa Yesu Kristo na zaidi ya yote neno la Mungu limetuthibitishia wazi ya kuwa aliye ndani yetu ni mkuu kuliko yeye aliye ulimwenguni.

1Yohana 4:4-6 “Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia. Hao ni wa dunia; kwa hiyo wanena ya dunia na dunia huwasikia Sisi twatokana na Mungu. Yeye amjuaye Mungu atusikia; yeye asiyetokana na Mungu hatusikii. Katika hili twamjua Roho wa kweli, na roho ya upotevu.”

Watu wa Mungu wanapaswa kuwa hodari Duniani, wanapaswa kuwa na imani, wanapaswa kuwa wapambanaji, wanapaswa kutumia silaha zote walizopewa kushughulika na wakuu wa anga katika mazingira yetu na kuharibu nguvu ya ushawishi inayotenda kazi kulingana na mazingira yetu na kwa kufanya hivyo tutapata upenyo, aidha kila tunapoendelea kuihubiri injili tunaendelea kumpa shida mkuu wa anga na kumpokonya mateka wake.  

Jinsi watu wasio wa ulimwengu huu wanavyopaswa kuishi

1.       Kuishi kwa kiasi chini ya neema ya Mungu –  kila mtu aliyeokolewa, aliokolewa kwa neema na kwa sababu hiyo hiyo hatuna budi kuendelea kuishi kwa neema, shetani hatataka mtu aliyeokolewa kwa neema aendelee kufurahia neema hiyo na kwa vyovyote vile atatupandikizia falsafa za dunia hii za kututaka tupate kibali kwa Mungu kwa njia ya tendo au matendo fulani, ni muhimu kukumbuka na kufahamu kuwa dini zote za uongo duniani zina mfumo wa kukutaka upate kibali kwa Mungu kwa njia ya matendo, Uislamu unakazia matendo mema, Budha, Hindu, Confucianism, Sikhism,Taoism, Shintoism, Judaism n.k  au kuupata wokovu kwa kazi, au kwa matendo mema, jambo hilo ni kinyume na kweli ya Mungu kwa sababu wokovu, na uzima wa milele ni zawadi kutoka kwa Mungu, ni kipawa ni karama ambayo kamwe haitokani na nafsi zetu wala matendo yetu  bali neema ya Mungu, tunaokolewa kwa neema na tunaendelea kuishi kwa neema tukimpendeza na kusaidiwa na Roho wake Mtakatifu kumpendeza Mungu kwa neema yake.

 

Waefeso 2:8-9 “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.”

 

2.       Kuishi kwa Imani isiyotikisika -  watu wa Mungu watapitia dhiki na mateso mengi lakini mateso yao au yetu isiwe sababu ya kuyumba wala kuogopa mateso, watakatifu waliotutangulia waliishi kwa Imani isiyotetereka hata wakati wa majaribu Makubwa walichagua kupata mateso pamoja na watu wa Mungu badala ya kujifurahisha kwa anasa huku wakiikana Imani, Badala yake walikaza kumwangalia Mungu kwa matokeo.

 

Waebrania 11:24-27 “Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao; akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo; akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo. Kwa imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana.”

               

3.       Kuishi kwa uvumilivu na ustahimilivu - Hakuna jambo linauma kama kuteseka ili hali hujakosea kitu, hata hivyo maandiko yanatutaka kutokuogopa na kutokufadhaika na badala yake kuendelea kustahimili tukivumilia mateso na shida huku tukiiga mfano wa wenzetu ambao walidhihakiwa, walipigwa mijeledi, walifungwa kwa minyororo, walitiwa gerezani, walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno lakini kwaajili ya Imani katika Mungu na upendo wao kwa Kristo walikubali hata kuuawa kuliko kumkana Bwana.

 

1Petro 3:14 “Lakini mjapoteswa kwa sababu ya haki mna heri. Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike; bali mtakaseni Kristo Bwana mioyoni mwenu.”

 

Waebrania 11:35-38 “Wanawake walipokea wafu wao waliofufuliwa. Lakini wengine waliumizwa vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora; wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani; walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya; (watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi.”

 

4.       Kutokuifuta namna ya dunia hii –  Nyakati za kanisa la Kwanza wanafunzi wa Bwana walijitolea kuishi maisha ya uadilifu na kujitofautisha sana na mifumo ya ulimwengu huu, neno namna ya dunia hii maana yake  ni kushi chini ya kiwango, au chini ya uadilifu neno linalotumika hapo standard of this world au Pattern of this world kwa kiyunani suschēmatizo yaani Fashion au design au model, au alike  kwa hiyo lazima watu wa Mungu wajitofautishe na watu wa dunia hii katika mtindo wao wa maisha, neno la Mungu linaagiza hivyo na neema ya Mungu itatusaidia kutufundisha namna ya kuishi zaidi ya kiwango cha dunia hii nje ya muundo 

 

Warumi 12:2 “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”

 

Tito 11:11-12 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;”           

 

5.       Kuonyesha upendo uzidio – Pamoja na changamoto ambazo ulimwengu utatuletea kutokana na mfumo wake watu wa Mungu ambao wao sio wa ulimwengu huu wanapaswa kuendelea kuonyesha upendo mkubwa kwa wengine hususani wale wanaotuchukia na kufikiriwa kuwa ni adui zetu, kuwapenda maadui au kuwaombea wale wanaotuchukia na kuishi kwa kuonyesha upendo uzidio na hii sio hali ya kawaida kwa ulimwengu huu kwa kufanya hivyo tutawavuta wale watu wa ulimwengu huu kuona na kujua ya kuwa kuna kitu cha ziada katika Kristo.

 

Mathayo 5:43-46 “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?

 

Matendo 7:58-60 “wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli. Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu. Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake.”

 

6.       Kuvaa silaha zote za Mungu - watu wasio wa ulimwengu huu wako vitani, na hivyo maandiko yanaagiza kuwa wavae silaha zote za Mungu kama inavyoelezwa katika kitabu cha Waefeso

 

Waefeso 6:11-18 “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;”

 

Hiyo inaashiria kuwa tunapaswa kuwa tayari katika hali ya kiroho kukabiliana na utendaji wa mkuu wa anga na nguvu zake za ushawishi na uovu duniani, ili kujilinda katika vita tuliyonayo kiroho, Kila mkristo kwa kuwa anajua ya kuwa yuko katikati ya adui anapaswa kuwa na msimamo thabiti katika Imani na kupambana kwa ujasiri kwa neema ya Mungu kuweza kuzishinda hila zote za adui zinazozuia ukuaji wa ufalme wa Mungu kwa njia ya injili. Wewe mwenyewe pia ukiyalinda maisha yako kwa kuwa uko vitani, uongezewe neema!

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!