Jumamosi, 31 Agosti 2024

Ubatizo wa Roho Mtakatifu:-


Mathayo 3:11-12 “Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.  Ambaye pepeto lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake; na kuikusanya ngano yake ghalani, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.”




Utangulizi:

Ubatizo wa Roho Mtakatifu ni uzoefu wa kiroho unaotokea kwa mtu aliyeokoka kumuwezesha mtu huyo kupokea uwepo wa Roho Mtakatifu unaoambatana na nguvu za Mungu na ujasiri unaomuwezesha mtu huyo kuzungumza neno la Mungu kwa ujasiri, huku akithibitishwa na kunena kwa lugha pamoja na kupokea vipawa na karama nyinginezo, Ubatizo wa Roho Mtakatifu umetajwa kwa mara ya kwanza na Yohana mbatizaji katika vitabu vya injili.

Mathayo 3:11-12 “Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.  Ambaye pepeto lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake; na kuikusanya ngano yake ghalani, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.”

Marko 1:7-8 “Akahubiri akisema, Yuaja nyuma yangu aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuinama na kuilegeza gidamu ya viatu vyake. Mimi niliwabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.”

Luka 3:16-17 “Yohana alijibu akawaambia wote, Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto; ambaye pepeo lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake, na kuikusanya ngano ghalani mwake, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.”  

Madhehebu mbalimbali ya Kikristo yanatafasiri ubatizo wa Roho Mtakatifu katika mitazamo tofauti tofauti kulingana na elimu zao za kitheolojia (Experimental Theology)

1.       Wapentekoste na wanacharismatic - kuwa ubatizo huu unatokea kwa mtu aliyeokoka yaani aliyemuamini Bwana Yesu na kumkubali kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yake na, kufuatiwa na kupokea uwepo na nguvu za Roho Mtakatifu ambazo kimsingi zinathibitishwa na kunena kwa lugha mpya hii ndio alama ya kwanza inayothibitisha uwepo wa Roho wa Mungu ndani ya mtu na umuhimu wa kuishi maisha yenye nguvu za Roho Mtakatifu na kupelekea kuwa bora katika nia zetu za kuabudu na kumtumukia Mungu.

 

2.       Madhehebu ya kiinjili na kiprotestant - wao wanaamini kuwa ubatizo huu unatokea mara tu mtu anapokuwa amempokea Yesu, mara mtu anapompokea Yesu, wanaamini kuwa ni kazi ya Roho Mtakatifu kusababisha kuzaliwa upya kwa mtu huyo na hivyo anakaa ndani yake na hawaamini kuwa wokovu na uwepo wa Roho au Ubatizo wa Roho Mtakatifu ni vitu vinaweza kutenganishwa.

 

3.       Wakatoliki  na waanglikana wa High Church wanaamini kumpokea Roho Mtakatifu tu ni tukio la kisakrament (Kipaimara), wao wanaona kuwa uwepo wa Roho Mtakatifu ni tukio endelevu la maisha ya kila siku na tukio la kukua na kukomaa katika utakatifu na huduma.               

 

Kibiblia ubatizo huu wa Roho Mtakatifu ni moja ya ahadi Muhimu sana aliyoiahidi Mungu baba na Bwana wetu Yesu Kristo, ambapo wanafunzi wa Yesu Kristo walipaswa kusubiri kwanza pale Yerusalem mpaka wavikwe uwezo huu kutoka mbinguni.

Luka 24:49 “Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.”     

Matendo 1:4-5, 8 “Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu; ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache.8 Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”

Kwa hiyo unaweza kuona kuwa ni ubatizo wa ahadi kimaandiko na ni tukio ambalo Yesu aliwaelekeza wanafunzi wake kulisubiria na Yesu alilitofautisha na wokovu pamoja na ubatizo wa maji,  na wanafunzi wa Yesu walisubiria ahadi hii  na walijazwa au walibatizwa kwa  Roho Mtakatifu na kuanza kusema kwa lugha nyingine.

Matendo 2:1-4 “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.”

Haikuishia hapo tu kwani baadaye tunawaona wanafunzi wakiwa na mabadiliko makubwa sana wakiwa pia na karama na vipawa mbalimbali na wakimtumikia Mungu kwa nguvu na ujasiri mwingi pia wakiwa moto sana kuanzia Matendo 3 na kuendelea, jambo lililopelekea watu wengi kuokoka na kukua kwa kanisa na uhai wa kanisa unaoendelea mpaka leo.

Kwa msingi huo basi leo tutachukua Muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu kuhusu Ubatizo wa Roho Mtakatifu kwa kuzingatia vipengele muhimu vitatu vifuatavyo:-



·         Maana ya ubatizo wa Roho Mtakatifu.

·         Mtu aliyebatizwa kwa Roho Mtakatifu.

·         Jinsi ya kupokea Ubatizo wa Roho Mtakatifu.



Maana ya ubatizo wa Roho Mtakatifu;

Maandiko yanatufundisha ya kuwa kila mtu aliyeokolewa anakuwa na Roho Mtakatifu ndani yake, hii ni kwa sababu tukio zima la mtu kumkiri Yesu na kumpokea kama bwana na mwokozi kupitia kazi aliyoifanya Msalabani ni tukio linalosababishwa na Roho Mtakatifu, kwa hiyo kuzaliwa mara ya pili ni kuzaliwa kwa roho na kuungwa katika mwili wa Kristo, kwa Msingi huo basi ni muhimu kufahamu kuwa, Ndani ya kila mtu aliyeokolewa Roho wa Mungu yupo na hivyo kila aaminiye amefanyika kuwa mali ya Mungu.

Yohana 16:7-11 “Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu. Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu. Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi; kwa habari ya haki, kwa sababu mimi naenda zangu kwa Baba, wala hamnioni tena; kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.”

Warumi 8:9 “Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake.”

Wagalatia 4:5-6 “Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba. Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu.”

Wakati huu Roho Mtakatifu atafanya kazi na mwamini katika kiwango tofauti tofauti kwa kadiri ya neema ya Mungu ndani ya waamini, viwango hivi ni sawa na ngazi za ujazo wa maji kutoka kiwango kimoja hadi kiwango kingine, viwango hivyo vinachangiwa na utii, kujitoa, maombi, kufunga na maisha kwa ujumla ambapo kila mmoja anakuwa na kiwango chake viwango hivi tunaweza kuelezea vizuri kwa kutumia maono ya mfano wa nabii Ezekiel.

Ezekiel 47:1-5 “Baadaye akanileta tena mpaka lango la nyumba; na tazama, maji yalitoka chini ya kizingiti cha nyumba, kwa njia ya mashariki, maana upande wa mbele wa nyumba ulielekea upande wa mashariki; nayo maji yakashuka toka chini ya upande wa kuume wa nyumba, upande wa kusini wa madhabahu. Ndipo akanileta nje kwa njia ya lango upande wa kaskazini, akanizungusha kwa njia ya nje mpaka lango la nje, kwa njia yake iliyoelekea mashariki; na tazama, maji yalitoka upande wa kuume. Na alipotoka mtu yule, mwenye uzi wa kupimia mkononi mwake, kwenda masharikini, akapima dhiraa elfu, akanivusha maji yale; maji yakafika mpaka viweko vya miguu. Kisha akapima dhiraa elfu, akanivusha maji yale, maji yakafika mpaka magoti. Kisha akapima dhiraa elfu, akanivusha, maji yakafika mpaka viuno. Kisha akapima dhiraa elfu, yakawa mto nisioweza kuuvuka; maana maji yamezidi, maji ya kuogelea, mto usiovukika.”

Ezekiel Katika maono haya anajaribu kuelezea kiwango au viwango mbalimbali vya ujazo wa Roho Mtakatifu kutofautisha na ubatizo wa Roho Mtakatifu, viwango hivyo vinategemeana na ukuaji wa kila mwamini kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine, na kila mwamini anaweza kuongezea kiwango chake yeye mwenyewe kwa kujitoa kwa Mungu kwa hiyo uko uhusiano wa ukuaji wa kiroho na ujazo wa Roho Mtakatifu, mfano ni kutoka maji ya kiwango cha viwiko vya miguu, kisha maji ya magotini, kisha maji ya kiunoni, kisha mto usioweza kuvukika  Ezekiel alikuwa anazungumzia ukuaji wa kiroho wa muumini na uhusiano wake na ujazo wa Roho Mtakatifu, kwa hiyo mtu anaweza kuwa na Roho Mtakatifu tangu alipookoka kwa sehemu, lakini akawa hajajazwa au hajabatizwa katika kiwango cha kufurika ambacho ndio kinaitwa Ubatizo. Mtu anayebatizwa kwa Roho Mtakatifu ni mtu mwingine ni mtu wa tofauti sana ni mtu wa viwango vya juu sana , ni mtu ambaye uungu unakaa ndani yake kama tutakavyoona.

Wanafunzi wa Yesu walikuwa na kiwango cha uwepo wa Roho Mtakatifu wakati wakiwa na Yesu Kristo, kwa hiyo yako mambo waliweza kuyafanya, lakini katika kiwango cha chini na cha kawaida mfano kutoa Pepo, kufunuliwa kumjua Yesu, kusikiliza mafundisho yake na kadhalika walimpokea Roho Mtakatifu kwa sehemu, kwa hiyo walifanya kazi mbalimbali za Mungu kwa kiwango hicho.

Yohana 20:21-22 “Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu.”

Luka 9:1-2 “Akawaita wale Thenashara, akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi. Akawatuma wautangaze ufalme wa Mungu, na kupoza wagonjwa.”

Luka 10:1,17-19 “1.Basi, baada ya hayo Bwana aliweka na wengine, sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe.” 17-19 “Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.”

Mathayo 16:15-17 “Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni”  

Kwa hiyo utaweza kuona kuwa wanafunzi wa Yesu walipokea Roho Mtakatifu wakati wakiwa na Yesu, walitumwa kuhubiri, walitoa pepo, walitetemesha utawala wa shetani, waliweza pia kupokea mafunuo mbalimbali kwa sababu walikuwa na Roho wa Mungu ndani yao, na Yesu aliwatumia lakini ilikuwa katika kiwango cha chini sana, kiwango cha kawaida na ni wanafunzi hao hao Yesu anawagiza wasianze kuifanya kazi hiyo mpaka wamepokea uwezo kutoka juu, mpaka wamejiliwa na Roho Mtakatifu, mpaka wamebatizwa kwa Roho Mtakatifu ona

Luka 24:49 “Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.”     

Matendo 1:4-5, 8 “4-5,Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu; ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache.” 8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”

Kwa hiyo ubatizo wa Roho Mtakatifu ni zaidi ya ujazo, ni zaidi ya kuvikwa, ni zaidi ya kupokea, ujazo una viwango vya viwiko, magoti, kiuno, lakini ubatizo unahusisha maji yasiyovukika ni aidha uzame na ufie humo uzikwe humo, mtu anapobatizwa kwa maji huwa anazamishwa analowekwa kila kitu chake mwili wake, nafsi yake, roho yake na mpaka nguo zake analowa chapa chapa, anafia kwenye maji anazikwa kwenye maji, anazamishwa, kwa hiyo ubatizo wa Roho Mtakatifu maana yake ni nini  Neno ubatizo linatusaidia kwa sehemu kujua kinachozungumzwa hapo katika lugha ya kibiblia !

Neno ubatizo limetokana na neno la kiingereza Baptism ambalo kwa asili limetokana na neno la Kiyunani cha zamani Baptizein ambalo maana yake kuzamisha to immerse, dip in water, kuzamisha katika maji, kwa hiyo neno hilo ubatizo wa Roho Mtakatifu maana yake ni kuzamishwa katika Roho Mtakatifu!, aidha nguo za kitani nyeupe zilipokuwa zikilowekwa ili zipate rangi ya zambarau au nyekundu, zilizamishwa katika maji yaliyochemka na rangi hiyo na kutoka nguo hiyo ikiwa imebadilika rangi, yaani nguo ya kitani ingepoteza rangi yake nyeupe na kuwa na rangi ambayo nguo hiyo imechovya, kitendo hicho pia kinaitwa ubatizo, sasa maana ile ile inayotumika katika ubatizo wa maji sasa ndio inatumika katika ubatizo wa Roho Mtakatifu, kwa hiyo nawashauri walimu wa neno la Mungu kutumia neno ubatizo zaidi kuliko ujazo, au kuvikwa au kupokea nguvu au kujaa Roho Mtakatifu, japokuwa maneno hayo yote Ujazo na kuvikwa na kupokea yana maana moja lakini msamiati ulio bora zaidi utumike kubatizwa.

Kwa hiyo Neno ubatizo linapotumika pamoja na Roho Mtakatifu maana yake ni ile ile kuzamishwa katika Roho kwa hiyo kila kitu cha mtu anayebatizwa katika Roho Mtakatifu kina uwepo wa Mungu mtu analowa Roho Mtakatifu kwenye kila kitu mwili wake, nasfi yake, mavazi yake, mawazo yake, sauti yake, kivuli chake, jasho lake kila kitu, anafia ndani ya Roho Mtakatifu anabobea analowa maana yake mpaka mifupa ya mtu mwenye Roho wa Mungu ina jaa uwepo wa Mungu ndio maana Elisha alipokufa watu, walitupia mwili katika kaburi lake na ule mwili ulipogusa mifupa ya Elisha ukafufuka angalia:-

2Wafalme 13:20-21 “Elisha akafa, nao wakamzika. Basi vikosi vya Wamoabi wakaingia katika nchi mwanzo wa mwaka. Ikawa, walipokuwa wakimzika mtu, angalia, waliona kikosi; wakamtupa yule mtu kaburini mwa Elisha; mara yule maiti alipoigusa mifupa ya Elisha, alifufuka, akasimama kwa miguu.”

Kwa hiyo mtu aliyebatizwa kwa Roho Mtakatifu sio mtu wa kawaida, hawi wa kawaida, anaweza kupigwa mawe na akavumilia, hawi yeye anayeishi, anaweza kupaa kwenda mji mwingine, anaweza hata kivuli chake kikasababisha miujiza kwa sababu kila kitu kimelowa uwepo wa Mungu, wakati mwingine hata mazingira ya mtu aliyebatizwa kwa Roho Mtakatifu huwa na uwepo wa Roho Mtakatifu, Ubatizo wa Roho Mtakatifu ni kiwango cha maji yasiyovukika, unazama, unalowa, unapoteza uhai unapotea huwi wa ulimwengu huu hata kidogo watu wanaweza kudhani miungu imewashukia kwa jinsi ya kibinadamu sijui unanielewa?

Matendo 14:8-15 “Na huko Listra palikuwa na mtu mmoja, dhaifu wa miguu, kiwete tangu tumboni mwa mamaye, ambaye hajaenda kabisa. Mtu huyo alimsikia Paulo alipokuwa akinena; ambaye akamkazia macho na kuona ya kuwa ana imani ya kuponywa, akasema kwa sauti kuu, Simama kwa miguu yako sawasawa. Akasimama upesi akaenda. Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo wakapaza sauti zao, wakisema kwa Kilikaonia, Miungu wametushukia kwa mifano ya wanadamu. Wakamwita Barnaba, Zeu, na Paulo, Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji. Kuhani wa Zeu ambaye hekalu lake lilikuwa mbele ya mji, akaleta ng'ombe na taji za maua hata malangoni, akitaka kutoa dhabihu pamoja na makutano. Walakini mitume Barnaba na Paulo, walipopata habari, wakararua nguo zao, wakaenda mbio wakaingia katika makutano, wakipiga kelele, wakisema, Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamu hali moja na ninyi; twawahubiri habari njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo;”

Kwa hiyo watu waliobatizwa kwa Roho Mtakatifu wana kitu cha ziada  na ndio maana hata lugha inaweza kubadilika na wakaanza kusema kwa lugha mpya kwa nini uwepo wa Mungu unashuka katika kile eneo la mtu aliyebatizwa kwa Roho Mtakatifu, hiyo ndio maana ya ubatizo wa Roho Mtakatifu. Kama ukichukua chupa iliyojaa maji unakitumia kama kielelezo cha ujazo wa Roho Mtakatifu maana yake ujazo wa chupa hautoshi kuelezea ubatizo wa Roho Mtakatifu maana yake ni nini maana yake Roho anakuwepo mpaka kwenye chupa yenyewe na kifuniko chake !


Mtu aliyebatizwa kwa Roho Mtakatifu:

1.       Anakuwa na uhusiano wa ndani sana na Mungu – Kwa kawaida mtu ambaye amebatizwa kwa Roho Mtakatifu anaumbiwa kiu na hamu na shauku ya kuwa na uhusiano wa ndani sana na Mungu na kiu yake ya kumtafuta Mungu inakuwa kubwa anaweza kujisikia kuendelea kuutafuta uso wa Mungu hata kama ibada ya kawaida imeisha, wao watataka kuongea na Mungu watatafakari, wanakuwa kama hawana kiasi katika swala la kuutafuta uso wa Mungu wanakaa muda mrefu sana kwenye maombi, kiu yao ni uwepo wa Mungu.Roho wa Mungu ndani yao anawapa neema ya kuomba kwa kuugua kama waombolezaji.

 

a.       Yoshua Mwana wa Nuni: Kutoka 33:10-11 “Watu wote wakaiona nguzo ya wingu ikisimama penye mlango wa hema; watu wote wakaondoka wakasujudu, kila mtu mlangoni pa hema yake.Naye BWANA akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea hata maragoni; bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni kijana, hakutoka mle hemani.”

 

b.      Daudi – Zaburi 27:1-6 “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini. Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake.”

       

c.       Daniel: Daniel 6:4-11 “Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake. Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo, tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu wake. Basi wale mawaziri na maamiri wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia hivi, Mfalme Dario, uishi milele.  Mawaziri wote wa ufalme, na manaibu, na maamiri, na madiwani, na maliwali wamefanya shauri pamoja ili kuweka amri ya kifalme; na kupiga marufuku, ya kwamba mtu ye yote atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme atatupwa katika tundu la simba. Sasa, Ee mfalme, piga marufuku, ukatie sahihi maandiko haya, yasibadilike, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi, isiyoweza kubadilika. Basi mfalme Dario akayatia sahihi maandiko yale, na ile marufuku. Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu ;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo. Basi watu hao wakakusanyika pamoja, wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu wake.”

 

d.      Paulo mtume na timu yake ya umisheni: Matendo 16:12-16 “na kutoka hapo tukafika Filipi, mji wa Makedonia, mji ulio mkuu katika jimbo lile, mahali walipohamia Warumi; tukawa katika mji huu, tukikaa siku kadha wa kadha. Hata siku ya sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale. Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo. Hata alipokwisha kubatizwa, yeye na nyumba yake, akatusihi, akisema, Kama mmeniona kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani mwangu mkakae. Akatushurutisha.Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua.”

 

e.       Watu wa Mungu - Zekaria 12:10 “Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza.”

 

2.       Wanasumbuliwa sana kueneza injili: - Mtu aliyebatizwa kwa Roho Mtakatifu ndani yake kunakuwa na kiu ya kutaka kuieneza injili, kwa wengine hawahisi utulivu mioyoni mwao wanawiwa kwa hiyo wanasukumwa kushuhudia, wanasukumwa kulisema neno la Mungu na hawawezi kukaa kimya

 

a.       Matendo 17:14-17 “Mara hiyo wale ndugu wakampeleka Paulo aende zake mpaka pwani; bali Sila na Timotheo wakasalia huko. Lakini wale waliomsindikiza Paulo wakampeleka mpaka Athene; nao wakiisha kupokea maagizo kuwapelekea Sila na Timotheo, ya kwamba wasikawie kumfuata, wakaenda zao. Paulo alipokuwa akiwangojea huko Athene na kuona jinsi mji ule ulivyojaa sanamu, roho yake ilichukizwa sana ndani yake. Basi katika sinagogi akahojiana na Wayahudi na waliomcha Mungu, na wale waliokutana naye sokoni kila siku.”

 

b.      Apolo Matendo 18:24-26 “Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu. Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi.”

 

3.       Wanakuwa na uwezo mkubwa sana wa kukabiliana na changamoto – Mtu aliyebatizwa kwa Roho Mtakatifu anakuwa na uwezo mkubwa sana wa kukabiliana na changamoto yoyote inayokuja mbele zake na haogopi kitu na wako tayari hata kufa kwaajili ya injili

 

a.       Matendo 21:10-13 “Basi tulipokuwa tukikaa huko siku nyingi, nabii mmoja jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi. Alipotufikia akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa. Basi tuliposikia haya, sisi na watu wa mahali pale, tukamsihi asipande kwenda Yerusalemu. Ndipo Paulo alipojibu, Mnafanya nini, kulia na kunivunja moyo? Kwa maana mimi, licha ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika Yerusalemu kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu.”

 

b.      Matendo 4:18-20 “Wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu.Petro na Yohana wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe; maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.”          

 

4.       Wanafanya mambo makubwa ya kushangaza na kupita kawaida – watu waliobatizwa kwa Roho Mtakatifu wanakuwa na karama na vipawa na uweza wa kiungu unaowawezesha kufanya mambo ya kutisha na kushangaza katika viwango vikubwa sana

 

a.       Matendo 5:12-15 “Na kwa mikono ya mitume zikafanyika ishara na maajabu mengi katika watu; nao wote walikuwako kwa nia moja katika ukumbi wa Sulemani; na katika wote wengine hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao; ila watu waliwaadhimisha; walioamini wakazidi kuongezeka kwa Bwana, wengi, wanaume na wanawake; hata ikawa katika njia kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka juu ya majamvi na magodoro, ili Petro akija, ngawa kivuli chake kimwangukie mmojawapo wao.”           

 

b.      Matendo 6:8-10 “Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu.Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye.”

 

c.       Matendo 19:11-12 “Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka.”

 

d.      Paulo na Barnaba – Matendo 17:2-6 “Na Paulo, kama ilivyokuwa desturi yake, akaingia mle walimo, akahojiana nao kwa maneno ya maandiko sabato tatu, akiyafunua na kuwaeleza ya kwamba ilimpasa Kristo kuteswa, na kufufuka katika wafu; na ya kwamba, Yesu huyu ninayewapasha ninyi habari zake ndiye Kristo. Wengine miongoni mwao wakaamini, wakashikamana na Paulo na Sila; na Wayunani waliomcha Mungu, wengi sana, na wanawake wenye cheo si wachache. Na Wayahudi wakaona wivu, wakajitwalia watu kadha wa kadha katika watu ovyo wasio na sifa njema, nao wakakutanisha mkutano, wakafanya ghasia mjini, wakawaendea watu wa nyumba ya Yasoni, wakataka kuwapeleka mbele ya watu wa mji; na walipowakosa, wakamkokota Yasoni na baadhi ya ndugu mbele ya wakubwa wa mji, wakipiga kelele, wakisema, Watu hawa walioupindua ulimwengu wamefika huku nako,”

 

5.       Watu waliobatizwa kwa Roho Mtakatifu wanakuwa na ukarimu na uwezo wa kujitoa kwa hali ya juu, wanauwezo wa kutoa mali zao kwaajili ya injili, hutumii nguvu wala ushawishi kuwataka watoe, wanajua kujitoa, ukiona ni mpaka upige sarakasi ndio watu wajitoe ujue watu hao bado maji yao ni ya kisigino bado hayajajaa

 

a.       Matendo 4:31-37 “Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri. Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika. Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote. Wala hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye mahitaji; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile vilivyouzwa, wakaiweka miguuni pa mitume; kila mtu akagawiwa kwa kadiri ya alivyohitaji.Na Yusufu, aliyeitwa na mitume Barnaba, (maana yake, Mwana wa faraja), Mlawi, asili yake ni mtu wa Kipro, alikuwa na shamba akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni pa mitume.”

 

b.      Wafilipi 4:15-19 “Nanyi pia, ninyi wenyewe mnajua, enyi Wafilipi, ya kuwa katika mwanzo wa Injili, nilipotoka Makedonia, hakuna kanisa lingine lililoshirikiana nami katika habari hii ya kutoa na kupokea, ila ninyi peke yenu. Kwa kuwa hata huko Thesalonike mliniletea msaada kwa mahitaji yangu, wala si mara moja. Si kwamba nakitamani kile kipawa, bali nayatamani mazao yanayozidi kuwa mengi, katika hesabu yenu. Lakini ninavyo vitu vyote na kuzidi, tena nimejaa tele; nimepokea kwa mkono wa Epafrodito vitu vile vilivyotoka kwenu, harufu ya manukato, sadaka yenye kibali, impendezayo Mungu. Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu.”          

 

6.       Hawasumbuliwi na wachawi  na badala yake wao ndio huwa juu ya wachawi

 

a.       Wagalatia 5:18-21 Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria. Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.”

       

b.      Matendo 8:5-13 “Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule. Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa. Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, ule Mkuu. Wakamsikiliza, kwa maana amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake. Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake. Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa, akashikamana na Filipo; akashangaa alipoziona ishara na miujiza mikubwa inayotendeka.”

       

c.       Matendo 19:17-21 “Habari hii ikajulikana na Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawaingia wote, na jina la Bwana Yesu likatukuzwa. Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao. Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu. Hivyo ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda kwa nguvu. Mambo hayo yalipokwisha kumalizika, Paulo akaazimu rohoni mwake, akiisha kupita katika Makedonia na Akaya, aende Yerusalemu, akisema, Baada ya kuwako huko, yanipasa kuuona na Rumi pia.”


 Jinsi ya kupokea Ubatizo wa Roho Mtakatifu.

1.       Fahamu ya kuwa anayebatiza kwa Roho Mtakatifu Ni Bwana Yesu mwenyewe, Na ubatizo huu ni mpango wa Mungu, ni ahadi ya Mungu kwa waaminio kwa hiyo kila mmoja anastahili kupokea kwa Imani na kufungua moyo wake kuhakikisha kuwa maisha yake yanajaa na kufunikwa na uwepo wa Mungu Roho Mtakatifu sawa na neno lake lisemavyo:-

 

a.       Mathayo 3:11 “Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.”

 

b.      Ubatizo huu ni ahadi ya Mungu mwenyewe kwa kila mtu amwaminiye

Yoel 2:28 “Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono;”

       

Luka 24:49 “Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.”

 

Matendo 2:38-39 “Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.”

 

c.       Lazima uwe na nia ya kutumika – Ubatizo wa Roho Mtakatifu ni kwaajili ya utumishi, Roho wa Mungu anatabia ya kutaharakisha watu kwaajili ya utumishi, Pale tunapokuwa tayari kwa huduma na kukubali kutumika huku na huko Roho Mtakatifu atakuwa radhi nasi, Ubatizo huu hauwafai watu ambao wakataa tu, unawafaa watu ambao wako tayari kwa kazi kwa sababu Roho Hatakupa kutulia

 

Waamuzi 13:24-25 “Basi yule mwanamke akamzaa mtoto mwanamume akamwita jina lake Samsoni, mtoto huyu akakua, Bwana akambarikia. Roho ya Bwana ikaanza kumtaharakisha katika Mahane-dani, katikati ya Sora na Eshtaoli.”

 

Yeremia 47:6-7 “Ee upanga wa Bwana, Siku ngapi zitapita kabla hujatulia? Ujitie katika ala yako; Pumzika, utulie. Utawezaje kutulia, Ikiwa Bwana amekupa agizo? Juu ya Ashkeloni na juu ya pwani, Ndipo alipoyaamuru hayo.”

 

d.      Kwa maombi bila kuchoka

Luka 18:9-13 “Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka? Au akimwomba yai, atampa nge? Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?

 

e.      Lazima uwe na imani

Maswala yote ya kiroho yanapokelewa kwa Imani, wakati wote mt akiwa na mashaka hawezi kupokea kitu kutoka kwa Mungu, kwani pasipo Imani haiwezekani kumpendeza Mungu, kwa hiyo Mtu anayemuhitaji Roho wa Mungu ni lazima aombe kwa Imani,

 

Waebrania 11:6 “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.”

 

Wagalatia 3:2 “Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?

 

Kwa hiyo baada ya kujifunza namna hii na kusikia neno la Mungu kuhusu Ubatizo wa Roho Mtakatifu unapaswa kuamini na kuatendea kazi yale yote ambayo umeyasikia na ninakuhakikishia hutakuwa ulivyo.

       

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi Mwenye hekima        

Jumamosi, 24 Agosti 2024

Chuo kikuu jangwani!


Kumbukumbu 8:11-16 “Jihadhari, usije ukamsahau Bwana, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo. Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; na makundi yako ya ng'ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka; basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa; aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu,aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako; apate kukutweza, apate kukujaribu, ili kukutendea mema mwisho wako.”


Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa pamoja na kujifunza neno la Mungu sana katika makanisa yetu, katika vyuo vya biblia na kwa kujitoa sisi wenyewe kwa kuisoma biblia wakati mwingine kila mwaka na wakati mwingine kila baada ya miezi sita na kuisoma wakati wa maandalizi ya neno, na kuhubiri na kufundisha  na hata kuhojiana na wenzetu bado ni Muhimu kufahamu kuwa iko shule ya Mungu au shule ya Roho Mtakatifu ambayo kwa kawaida Mungu hutupitisha kabla ya kututumia na kutubariki katika viwango vya juu, wakati wote Mungu anapotaka kukufundisha njia zake huwapeleka watumishi wake katika chuo chake kikuu ambacho leo nimekipa jina chuo kikuu cha jangwani angalia

Luka 1:76-80 “Nawe, mtoto, utaitwa nabii wake Aliye juu, Kwa maana utatangulia mbele za uso wa Bwana umtengenezee njia zake; Uwajulishe watu wake wokovu, Katika kusamehewa dhambi zao. Kwa njia ya rehema za Mungu wetu, Ambazo kwa hizo mwangaza utokao juu umetufikia, Kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti, Na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli.”

Luka 4:1-2 “Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani, (Jangwani) akijaribiwa na Ibilisi. Na siku hizo alikuwa hali kitu; hata zilipotimia, aliona njaa.”

Tunasoma kuwa Mungu aliwaongoza watoto wake wana wa Israel jangwani, lakini sio hivyo tu Yohana mbatizaji moja ya manabii waliokuwa na nguvu za Mungu za kupita kawaida alikaa jangwani siku zote za maisha yake mpaka alipojitokeza kuhubiria watu, Lakini Kristo Yesu Mwenyewe kabla ya kuanza kuhudumia watu aliongozwa jangwani. kwanini jangwani, kwa nini jangwani? Jangwani ni shule ya Roho Mtakatifu, jangwani kuna chuo, jangwani ni chuo kikuu cha maandalizi ya watumishi wa Mungu, kama hujapitishwa jangwani nidhamu yako katika kumtumikia Mungu, kumtegemea na kumtumikia kwa ufasaha inaweza kuwa na upungufu, leo tutachukua Muda basi kujifunza kwa kina na mapana na marefu somo hili muhimu Chuo kikuu jangwani kwa kuzingatia vipengele vinne vifuatavyo:-

 

·         Umuhimu wa kupitishwa chuo kikuu jangwani.

·         Mifano ya watumishi wa Mungu waliopitia chuo kikuu jangwani.

·         Mambo muhimu utakayopitia katika chuo kikuu Jangwani.

·         Chuo kikuu jangwani.  

 

Umuhimu wa kupitishwa chuo kikuu jangwani

Jangwa linajitokeza na kutajwa katika maandiko mara kadhaa, kama moja ya sehemu yenye matukio muhimu sana yanayohusiana na Mungu na watu wake, mara baada ya Mungu kuwaokoa wana wa Israel kutoka katika inchi ya utumwa Misri moja kwa moja tunaona hawapeleki katika inchi ya maziwa na asali aliyokuwa amewaahidi, na badala yake anawapeleka katika jangwa ambalo walilitembea kwa miaka kama 40 hivi, kwa nini jangwani? kwa ujumla swala la kupita jangwani halionekani kuwa ni lenye kuvutia au kupendeza hata kidogo, lakini kwanini watu wapelekwe jangwani? Jangwani ni mahali ambapo Mungu alikuwa na makusudi na watu wake na Mungu alikuwa na mpango mwema wa kujifunua kwao na kuwafundisha watu wake, Musa anaeleza kuwa halikuwa jangwa la matumaini, hakukuwa na kivuli, hakukuwa na maji, hakukuwa na chakula, jangwa lilikuwa na nyoka wenye sumu (Nyoka wa Moto) kulikuwa na nge, jangwa lina joto kali sana mchana, jangwa lina baridi kali sana usiku, jangwani huwezi kwenda kwa mwendo wa haraka, jangwani ni rahisi kupotea, jangwani hakuna makaburi, Musa analiita jangwa kubwa lenye kutisha, jua kali, ukavu, upweke, moyo na akili zinachoka na hata kuinua hatua jangwani kunahitaji uwe na moyo mkuu kwanini jangwani? Ni chuo kikuu cha Mungu ni shule ya Roho wa Mungu kwetu! Ni shule Muhimu yenye kutengeneza nidhamu ya hali ya juu kwa watumishi wa Mungu, ni shula ya huduma ni shule ya ukomavu.

Kumbukumbu 8:11-16 “Jihadhari, usije ukamsahau Bwana, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo. Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; na makundi yako ya ng'ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka; basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa; aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu,aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako; apate kukutweza, apate kukujaribu, ili kukutendea mema mwisho wako.”

Kaka zangu na dada zangu, hakuna mtu anayependa kuishi maisha ya taabu, wala ya umasikini, wala maisha yasiyofurahisha, kila mtu anapenda raha na mteremko, kwa hiyo kila mmoja anakwepa kupita kwenye mateso shida na maumivu, wakati mwingine tunafurahia sana wengine wakipita katika mapito na tunaweza kujifikiri kuwa labda sisi ni maalumu sana kuliko wao kwa sababu hatujalionja jangwa, lakini kama unaishi katika njia hii na utumishi huu na kama Mungu anakupenda ni muhimu ujue kuwa Mungu ataruhusu maisha yako yapite jangwani, ambako utakumbana na upweke, utakutana na ukavu, utakutana na nyoka, nge, njaa, kiu, na utachoka, utachoka akili mwili na roho na utahisi hakuna uhai, utapoteza marafiki na wakati mwingine utachagua kufa kuliko kuishi, jangwa halionyeshagi matumaini hata siku moja, Mungu hulitumia jangwa kutunyoosha watu wake, kutufundisha, jangwani ni chuo cha mafunzo, jangwani ni chuo cha unyenyekevu, jangwani ni chuo cha utii kwa hiyo kama kuna mapito unayapita umelia, umeomba na hakuna kitu kinatokea na huoni msaada wowote na unapoteza matumaini ujue ya kuwa hauko pake yako na mkuu wa chuo yuko pamoja nawe, programu zote na kozi anazotaka uzipitie anazo yeye kumbuka ni Mungu ndiye anayekusudia upite katika njia hiyo yeye mwenyewe, uelewa wako, utii wako na unyenyekevu wako ndio utakaokusaidia kumalizo chuo kikuu jangwani kwa ufanisi mkubwa huku ukimtukuza Mungu kwa wema wake. Kwa hiyo maana yake ni nini? Maana yake ni kuwa yako mapito mengine ambayo Mungu ndiye anayekuwa amekusudia upite na ndiye mwenye programu ya mateso hayo, ili kukufanya uwe mwenye nidhamu.

Kutoka 13:17-18 “Ilikuwa hapo Farao alipokwisha kuwaacha watu hao waende zao, Mungu hakuwaongoza kwa njia ya nchi ya Wafilisti, ijapokuwa ilikuwa ni ya karibu; maana Mungu alisema, Wasije wakaghairi watu hawa hapo watakapokutana na vita, na kurudi Misri; lakini Mungu akawazungusha hao watu kwa njia ya bara kando ya Bahari ya Shamu; wana wa Israeli wakakwea kutoka nchi ya Misri hali wamevaa silaha.”

Hakuna mtu au mtumishi wa Mungu au mwana wa Mungu atakayepita jangwani kwa bahati mbaya, liko kusudi kubwa sana ambalo ni la muhimu sana la kupitishwa jangwani, wayahudi wanapolitaja neno jangwa huwa wanatumia msamiati ambao una maana ya ndani sana kuliko jangwa lenyewe katika lugha ya kiibrania neno Jangwani ambalo limetumiwa mara nyingi zaidi ni neno MIDHBAR ambalo maana yake ni Jangwani au nyikani na neno la kibrania linalokaribiana na hilo ni  MEDABER  ambalo lina asili moja na la jangwani ambalo kimsingi halikuwa na herufi za kati kati MDBR neno hili ndio limezaa maneno hayo mawili MIDHBAR ambalo maana yake Jangwa na  MEDABER maana yake kwa kiingereza to Speak, yaani kuzungumza, au kusikia, kwa hiyo kwa waebrania mtu anapoongozwa na Mungu kwenda jangwani ni ili akapate kuisikia sauti ya Mungu, sawa kabisa na kwenda chuoni kumsikiliza Mwalimu na ndio maana somo hili nikaliita chuo kikuu jangwani, kwa nini kwa sababu ni eneo ambalo Mungu hukupeleka ili upate kumsikiliza yeye, kwa hiyo kila aliyepelekwa jangwani hakupelekwa si kama aliyepotea tu au kujikuta uko jangwani kwa bahati mbaya hapana unapokuwa jangwani maana yake Mungu anataka umsikilize na utamsikilizia wapi ni eneo ambalo utainua mikono kuhitaji msaada wake na sio kwingine ni jangwani, Ndugu hapo unapopita au ulikowahi kupitia ni jangwani na Mungu anamakusudi na wewe hivyo kubali kupita katika shule unayoipitia ili uweze kuhitimu vema utakapohitimu kutoka katika chuo hiki utamcha Mungu, utakuwa mnyenyekevu, na utayajua matendo makuu ya Mungu, Jangwani sio lazima liwe jangwa halisi, lakini ni njia ngumu za Mungu anazoruhusu uzipitie ili kwa nia njema akurekebishe ili kukuleta kwenye Baraka kubwa anazozikusudia. Na jwangwani sio lazima uisikie sauti ya Mungu moja kwa moja la hasha jangwa lenyewe linasema, lina sauti linafundisha, ukiwa mwanafunzi mzuri utaisikia sauti ya Mungu kwa upole sana ikisema na wewe na kukufunza.

Kumbukumbu 8:1-6 “Amri hii ninayokuamuru leo mtaishika kuitenda, mpate kuishi na kuongezeka, na kuingia katika nchi ile ambayo Bwana aliwaapia baba zenu; nanyi mtaimiliki. Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo. Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana. Mavazi yako hayakuchakaa, wala mguu wako haukuvimba, miaka hiyo arobaini. Nawe fikiri moyoni mwako, ya kuwa kama vile baba amrudivyo mwanawe, ndivyo Bwana, Mungu wako, akurudivyo.Nawe uzishike amri za Bwana, Mungu wako, upate kwenda katika njia zake, na kumcha.”     

Mifano ya watumishi wa Mungu waliopitia chuo kikuu jangwani

1.       Hajiri – Alikuwa akipitia changamoto katika nyumba ya bibi yake yaani Sara baada ya kuwa na ujauzito Kupitia Ibrahimu, mateso yalipomuelemea aliamua kikimbia, na kujikuta jangwani huko hali yake ilikuwa ngumu na akaelemewa na huzuni, malaika wa Bwana akamtokea na kumtia moyo na kumuelezea hali aliyo nayo na kumtaka arudi kwa bibi yake, lilikuwa jambo la busara kwa wakati ule kwani alikuwa na mtoto wa Ibrahimu tumboni mwake, Mungu alijifunua kwake na akamjua Mungu kama Mungu aonaye kwanini kwa sababu aliyaona mateso yake, akaliitia jina la Bwana huko. Hajiri alikuwa akisikia habari za Mungu katika nyumba ya Ibrahimu na Sara lakini hakuwahi kumuona Mungu akijihusisha na maisha yake Binafsi, siku alipokimbilia Jangwani alimjua Mungu kwa njia binafsi na kumtambua kama Mungu aonaye! Nimemwona yeye anionaye alisema Hajiri, sio hivyo tu kumbuka neno lile la malaika wa Bwana rudi kwa bibi yako ukanyenyekee maana yake ni nini Hajiri alikuwa na kiburi, malaika wa bwana hakumwambia una kiburi wewe  una majivuno humtii bibi yako badala yake alimwambia rudi kwa bibi yako ukanyenyekee jangwa lilimfunza Hajiri kwenda kuwa mnyenyekevu angalia

 

Mwanzo 16: 1-13 “Basi Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri.Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, BWANA amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai. Sarai mkewe Abramu akamtwaa Hajiri Mmisri mjakazi wake, baada ya kukaa Abramu katika nchi ya Kanaani miaka kumi, akampa Abramu mumewe, awe mkewe. Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba. Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bibi yake alikuwa duni machoni pake. Sarai akamwambia Abramu, Ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa mjakazi wangu kifuani mwako, naye alipoona kwamba amepata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake. BWANA na ahukumu kati ya mimi na wewe. Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake. Malaika wa BWANA akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri. Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, nawe unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai. Malaika wa BWANA akamwambia, Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono yake. Malaika wa BWANA akamwambia, Hakika nitauzidisha uzao wako, wala hautahesabika kwa jinsi utakavyokuwa mwingi. Malaika wa BWANA akamwambia, Tazama! Wewe una mimba, utazaa mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Ishmaeli, maana BWANA amesikia kilio cha mateso yako. Naye atakuwa kama punda-mwitu kati ya watu, mkono wake utakuwa juu ya watu wote na mkono wa watu wote utakuwa juu yake, naye atakaa mbele yao ndugu zake wote. Akaliita jina la BWANA aliyesema naye, Wewe U Mungu uonaye, kwani alisema, Hata hapa nimemwona yeye anionaye?

 

2.       Hajiri na Ishmael –  Hajiri na mwanae Ishamel walifukuzwa tena katika nyumba ya Ibrahimu kwa maagizo ya Sara kwa sababu ya changamoto kadhaa zilizojitokeza, hata hivyo walipotoka kwa bahati walipotea jangwani, maji yaliwaishia na hali ya kifo ndiyo iliyokuwa ikiwakabili, Mungu aliye mwingi wa rehema na asiye na upendeleo, aliwatokea na kuokoa maisha ya kijana na mama yake alitiwa moyo na Mungu aliahidi kumfanya kijana kuwa taifa kubwa na Mungu akawa pamoja na yule kijana, Hivyo Ishmael naye akamjua Mungu wa baba yake katika namna ya kipekee, alimjua kuwa ni Mungu anayejihusisha na maisha ya watu wake bila upendeleo, Ni Mungu aliyesababisha maji jangwani, Ni Mungu aliyewapa kisima cha maji, Ni Mungu aliyemfundisha Ishmael kushika upinde na kuwa mpiga upinde hodari, leo hii inchi ya Ishamel ina visima vikubwa vya mafuta na vinawapa utajiri mkubwa sana na mafanikio makubwa sana Jangwa limekuwa Mwalimu mzuri wa maisha yao.  

 

Mwanzo 21:14-20 “Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba. Yale maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja. Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia. Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko. Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana. Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde.”

 

3.       Musa -  Baada ya kumkimbia Farao, kule Misri baada ya kuua raia wake, Musa alikimbilia katika jangwa la Midian na kuishi huko kwa miaka 40, Huko ndiko alikoisikia sauti ya Mungu akisema naye na kumtaka kubadilika  (Kuvua viatu vyake) na kumtuma ili aende kuwaongoza wana wa Israel ambao aliwaongoza jangwani kwa miaka 40, Safari ya jangwani kwa Musa ilikuwa ni maandalizi makubwa ya kumuandaa Musa kwaajili ya wana wa Israel ukombozi wao na ujuzi wa jangwa lile lakini kubwa zaidi kumjua Mungu na kujifunza utii kwa sheria zake, Jangwa lilimfundisha Musa kuwa mpole yaani mnyenyekevu sana, Lilimfundisha Musa kuutafuta uso wa Mungu, lilimuweka mbali na starehe za ikuu, lilimuweka mbali na ndugu zake, lilimuweka ugenini, lilimfundisha upweke, lilimnyoosha na kumfanya kuwa mvumilivu na mtumishi wa Mungu wa ngazi ya juu na viwango vikubwa.

 

Kutoka 2:14-15 “Yule akasema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri? Musa akaogopa, akasema, Kumbe! Jambo lile limejulikana. Basi Farao alipopata habari, akataka kumwua Musa; lakini Musa akakimbia mbele ya Farao, akakaa katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na kisima.”

 

Kutoka 3:1-8 “Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu. Malaika wa BWANA akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea. Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei. BWANA alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa. Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu. Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu. BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi.”

      

4.       Wana wa Israel - Mungu aliwaongoza wana wa Israel jangwani kwa muda wa miaka 40, baada ya kuwa amewaokoa kutoka Misri, kipindi hiki hakikuwa kipindi rahisi, kilikuwa ni kipindi kigumu na kilikuwa kama adhabu kali kwa wana wa Israel, kilikuwa ni kipindi cha kuwajaribu, kuwafundisha na kuwarudi, walikutana na wakati mgumu na Mungu peke yake akawa ndio jibu la changamoto zao zote, huko aliwapa sheria, aliwafundisha na kuwatunza la kuwaadhibu walipokosea, Mungu alikuwa akijitafutia taifa lenye nidhamu na ustaarabu wa hali ya juu, taifa lenye akili, na kuwaandaa kabla ya kuingia katika inchi ya mkanaani.

 

Hesabu 14:33-34 “Kisha watoto wenu watakuwa wachungaji jangwani muda wa miaka arobaini nao watauchukua mzigo wa uasherati wenu, hata mizoga yenu itakapoangamia jangwani.Kwa hesabu ya hizo siku mlizoipeleleza ile nchi, yaani, siku arobaini kila siku kuhesabiwa mwaka, mtayachukua maovu yenu, ndiyo miaka arobaini, nanyi mtakujua kufarikana kwangu.”

 

Kumbukumbu 8:2-6 “Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo. Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana. Mavazi yako hayakuchakaa, wala mguu wako haukuvimba, miaka hiyo arobaini. Nawe fikiri moyoni mwako, ya kuwa kama vile baba amrudivyo mwanawe, ndivyo Bwana, Mungu wako, akurudivyo. Nawe uzishike amri za Bwana, Mungu wako, upate kwenda katika njia zake, na kumcha.”

 

5.       Daudi – Baada ya kupakwa mafuta na kufanya mambo makubwa ikiwa ni pamoja na kumuua Goliath maisha ya Daudi yalibadilika alianza kukimbia kutoka jangwa moja hadi jangwa lingine na kuishi katika mapango akimkimbia Sauli aliyekuwa na kusudi la kumuua, moyo wake ulishuka  na aliishi maisha ya chini sana ya nyikani lakini kule nyikani alijifunza kumtegemea Mungu na kujenga ukaribu mkubwa sana na Mungu, aliandika mashairi mengi ya kumsifu Mungu na kumuimbia Mungu akiamini kuwa Mungu anamsikia, alijifunza kumuomba Mungu na kumsikiliza Mungu pia alijifunza kumsifu na kumtegemea yeye, Jangwa liliendelea kutengeneza maisha ya unyenyekevu na moyo wa rehema hata ingawa alikuja kufanya dhambi, Moyo wake ulibaki kuwa mwelekevu kwa Mungu akijaa toba na Mungu alimsifu Daudi kama mtu wa kipekee sana. Aliyeupendeza moyo.

 

1Samuel 23:14-15 “Basi Daudi alikuwa akikaa nyikani ngomeni, akakaa katika nchi ya milima milima kwenye nyika ya Zifu. Naye Sauli alikuwa akimtafuta kila siku, lakini Mungu hakumtia mikononi mwake. Daudi akaona ya kwamba Sauli ametoka nje ili kutafuta roho yake; naye Daudi akawako katika nyika ya Zifu, huko Horeshi

 

6.       Eliya -  Inaonekana wazi kuwa alitokea jangwani, hasa kwa sababu mtindo wa maisha yake na huduma yake inafanana sana na ya Yohana mbatizaji, lakini baada ya kutenda mambo makubwa inaonekana alimkimbia malkia katili aliyeitwa Yezebeli aliyekuwa ameyatishia maisha yake, kule jangwani akiwa na hofu ya kuuawa na mwanamke huo katili, hata hivyo alipata somo, Mungu alimtunza na kumpa chakula, na maji, alitiwa nguvu ya kutembea siku 40  bila kula wala kunywa na mwisho aliisikia sauti ya Mungu, ikimuelekeza mambo ya kufanya, lakini pia alijifunza kuwa nabii bora hakuwa yeye peke yake, wala wacha Mungu hakuwa ni yeye tu, Mungu anawajua walio wake na waliojificha kwaajili yake ambao mioyo yao haijamuabudu baali, jangwa liliondoa kiburi cha Nabii huyu aliyewashitaki watu wa Mungu na kudhani ya kuwa yeye ni wa kipekee, Kwa huruma zake Mungu hakusikiliza maombi yake ya kutaka kufa na badala yake alimnyakua kwake Mbinguni. Jangwa lilimfundisha kuwa Mungu ana watu wengi, Jangwa lilimfundisha kuwa yeye sio peke yake anayemcha Mungu, jangwa lilimfundisha kuwa Elisha anaweza kubwa nabii bora kuliko yeye, Jangwa lilimfundisha kuwa hapaswi kujivuna, jangwa lilimfudhisha kuwa Mungu hapatakani kwenye mikwara na sauti zenye kelele nyingi, alijifunza kuwa sauti ya Mungu huja katika hali ya utulivu, Jangwa lilimfundisha kuwa hapaswi kuwashitaki au kuwahukumu wengine hata kama ni dhaifu, jangwa, jangwa, jangwa ni shule ni chuo cha Roho wa Bwana.

 

1Wafalme 19:1-18 “Ndipo Yezebeli akampelekea Eliya mjumbe, kusema, Miungu wanifanyie hivyo na kuzidi, nisipokufanya roho yako kesho, panapo wakati huu, kama roho ya mmojawapo wa hao.Naye alipoona hayo, aliondoka, akaenda aihifadhi roho yake, akafika Beer-sheba, mji wa Yuda, akamwacha mtumishi wake huko. Lakini yeye mwenyewe akaendelea katika jangwa mwendo wa siku moja, akaenda akaketi chini ya mretemu. Akajiombea roho yake afe, akasema, Yatosha; sasa, Ee Bwana, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu. Naye akajinyosha akalala chini ya mretemu; na tazama, malaika akamgusa, akamwambia, Inuka, ule. Akatazama, kumbe! Pana mkate umeokwa juu ya makaa, na gudulia la maji, kichwani pake. Akala, akanywa, akajinyosha tena. Malaika wa Bwana akamwendea mara ya pili, akamgusa, akasema, Inuka, ule; maana safari hii ni kubwa mno kwako. Akainuka, akala, akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu, mlima wa Mungu. Akafika kunako pango, akalala ndani yake. Na tazama, neno la Bwana likamjia, naye akamwambia, Unafanya nini hapa, Eliya? Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya Bwana Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu, waiondoe. Akasema, Toka, usimame mlimani mbele za Bwana. Na tazama, Bwana akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunja-vunja miamba mbele za Bwana; lakini Bwana hakuwamo katika upepo ule; na baada ya upepo, tetemeko la nchi; lakini Bwana hakuwamo katika lile tetemeko la nchi; na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; lakini Bwana hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto sauti ndogo, ya utulivu. Ikawa, Eliya alipoisikia, alijifunika uso wake katika mavazi yake, akatoka, akasimama mlangoni mwa pango. Na tazama, sauti ikamjia, kusema, Unafanya nini hapa, Eliya? Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya Bwana, Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu waiondoe. Bwana akamwambia, Enenda, urudi njia ya jangwa la Dameski; ukifika, mtie mafuta Hazaeli awe mfalme wa Shamu. Na Yehu mwana wa Nimshi mtie mafuta awe mfalme wa Israeli; na Elisha mwana wa Shafati wa Abel-Mehola mtie mafuta awe nabii mahali pako. Na itakuwa atakayeokoka na upanga wa Hazaeli, Yehu atamwua; na atakayeokoka na upanga wa Yehu, Elisha atamwua. Pamoja na hayo nitajisazia katika Israeli watu elfu saba, kila goti lisilomwinamia Baali, na kila kinywa kisichombusu.”

 

Warumi 11:1-4 “Basi, nauliza, Je! Mungu aliwasukumia mbali watu wake? Hasha! Kwa kuwa mimi nami ni Mwisraeli, mmoja wa wazao wa Ibrahimu, mtu wa kabila ya Benyamini. Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali. Au hamjui yale yaliyonenwa na maandiko juu ya Eliya? Jinsi anavyowashitaki Waisraeli mbele za Mungu, Bwana, wamewaua manabii wako, wamezibomoa madhabahu zako, nami nimesalia peke yangu, nao wananitafuta roho yangu. Lakini ile jawabu ya Mungu yamwambiaje? Nimejisazia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali.”

 

7.       Yohana mbatizaji – Ni kijana aliyekulia jangwani na alitokea jangwani akihubiri habari za toba na kukaribia kwa ufalme wa Mungu, jangwa lilimuandaa kihuduma na akaiva kweli kweli, lipewa sauti kubwa na ya kipekee, alipewa ujumbe mzito kwa watu na mahubiri yaliyonyooka yanayoashiria kuwa alitoka akiwa na nidhamu kubwa sana na ya hali ya juu, Yesu anamsifia Yohana mbatizaji kuwa katika uzao wa Mwanamke hakuna aliyemzidi huyu jamaa, kwanini kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye katika maisha yake ya kujikana huko jangwani!

 

Luka 1:76-80 “Nawe, mtoto, utaitwa nabii wake Aliye juu, Kwa maana utatangulia mbele za uso wa Bwana umtengenezee njia zake; Uwajulishe watu wake wokovu, Katika kusamehewa dhambi zao. Kwa njia ya rehema za Mungu wetu, Ambazo kwa hizo mwangaza utokao juu umetufikia, Kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti, Na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli.”

 

Mathayo 3:1- 5 “Siku zile aliondokea Yohana Mbatizaji akihubiri katika nyika ya Uyahudi, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. Kwa sababu huyo ndiye aliyenenwa na nabii Isaya, akisema, Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake. Naye Yohana mwenyewe alikuwa na vazi lake la singa za ngamia, na mshipi wa ngozi kiunoni mwake; na chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu.Ndipo walipomwendea Yerusalemu, na Uyahudi wote, na nchi zote za kandokando ya Yordani;”

 

Luka 7:24-28 “Basi, wajumbe wa Yohana walipokwisha ondoka, alianza kuwaambia makutano habari za Yohana, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini? Unyasi ukitikiswa na upepo? Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa mavazi mororo? Jueni, watu wenye mavazi ya utukufu, wanaokula raha, wamo katika majumba ya kifalme. Lakini, mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? Naam, nawaambia, na aliye zaidi ya nabii. Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako mbele yako. Nami nawaambia, Katika wale waliozaliwa na wanawake hakuna aliye mkuu kuliko Yohana; lakini aliye mdogo katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko yeye.”   

 

8.       Bwana Yesu -  Aliongozwa na Roho Mtakatifu kwenda jangwani akiwa amefunga kwa siku 40 huko alijaribiwa na shetani, jangwa lilikuwa ni sehemu ya maandalizi ya huduma, na kipimo cha kujitambua kwake, alishinda majaribu yote na Mungu alimtia nguvu na kumuandaa tayari kwa huduma ya hadharani, uweza wa Roho Mtakatifu juu yake, maombi ya kufunga na kuomba, utii wa maandiko, na ujuzi wake wa kuyatumia maandiko kwa usahihi ulimpa ushindi mkubwa kutoka jangwani na akarudi hali amejaa Roho Mtakatifu tayari kwa huduma

 

Mathayo 4:1-11 “Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Ibilisi. Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa. Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate. Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako. Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake, akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia. Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake. Kisha Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia.”

 

Luka 4:13-15 “Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda. Yesu akarudi kwa nguvu za Roho, akenda Galilaya; habari zake zikaenea katika nchi zote za kandokando. Naye alikuwa akifundisha katika masinagogi yao, akitukuzwa na watu wote.”

 

9.       Paulo Mtume – Inaonekana wazi kuwa injili aliyoihubiri hakufundishwa na wanadamu bali na bwana mwenyewe wala hakuipata kwa mitume wengine, na ili kuthibitisha ni wapi alipata injili hii na ni wapi Bwana Yesu mwenyewe alimfundisha, Paulo mtume anasema maneno haya

 

Wagalatia 1:11-20 “Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo. Maana mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba naliliudhi kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu. Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu. Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake, alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake; mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu; wala sikupanda kwenda Yerusalemu kwa hao waliokuwa mitume kabla yangu; bali nalikwenda zangu Arabuni, kisha nikarudi tena Dameski. Kisha, baada ya miaka mitatu, nalipanda kwenda Yerusalemu ili nionane na Kefa, nikakaa kwake siku kumi na tano. Lakini sikumwona mtume mwingine, ila Yakobo, ndugu yake Bwana. Na hayo ninayowaandikia, angalieni, mbele za Mungu, sisemi uongo.”

 

Paulo hapa anagusia kitu ambacho kitaalamu kinasumbua kidogo wanatheolojia kwa sababu Arabuni anayoitaja Paulo ni ngumu kueleweka kwa sababu unapotaja Arabuni leo wengi hufikiria ni Saud Arabia, lakini kwa mujibu wa nyakati za karne ya kwanza neno hilo pia lilitumika kuelezea jangwa lililokuwako kaskazini ambalo lilijulikana kama Syro Arabian derset  hili ni jangwa lililoko kaskazini ya Israel katika inchi ya Syria na Jordan, maelezo ya Paulo mtume yanathibitisha kuwa uko Muda ambao Paulo alipitia jangwani na huko alifundishwa na Bwana mwenyewe kwa habari ya injili aliyoihubiri, ukiacha kuwa alipandishwa katika maono makubwa hata mbingu ya tatu, huenda maono haya aliyapata akiwa jangwani, sio hivyo tu  huenda Paulo mtume aliutumia muda huo, kusoma, neno la Mungu, kuomba na kujifunza na kutafakari na kupata mafunuo ya injili aliyoihubiri, hivyo akawa na sifa za utume hata kabla ya kuonana na mitume, unaposoma kitabu cha matendo unaweza kuona ni kama baada ya kuokoka kule Dameski alianza injili mara moja na baadaye kuja Yerusalem lakini ni ukweli ulio wazi, ulikuweko muda wa maandalizi jangwani  na yalikuwa ni maandalizi ya kutosha kwaajili ya utumishi wake

 

Mambo muhimu utakayopitia katika chuo kikuu Jangwani

Kama umepitia kwa umakini maswala kadhaa tuliyojifunza hapo juu utaweza kugundua kuwa kuna maswala kadhaa muhimu ambayo Mungu alikuwa ameyakusudia kwa kila mtumishi wake aliyemtumia alimpeleka jangwani, kuna mambo maengi sana ya kujifunza kuhusu jangwa na uhusiano wake na Mungu, pamoja na mafunzo mengine yote ambayo kimsingi yana umuhimu wake, mafundisho kanisani ni muhimu, mafundisho shule za jumapili ni Muhimu, mafunzo chuo cha biblia ni muhimu, hata hivyo jangwani hapa namaanisha mapito, majaribu, mateso, na maswala kadhaa wa kadhaa ambayo kimsingi ndio yanalifanya jangwa hilo liwepo katika maisha yako linatimiza kusudi Fulani la uwepo wako na namna njema zaidi ya kuhudumu na kumtumikia Mungu kwa viwango anavyovikusudia, sasa katika chuo hicho cha jangwani tunajifunza nini haya ndio baadhi ya mambo tunayojifunza, kwanini unapita jangwani? Kwanini Mungu aruhusu uingine kwenye chuo chake kikuu, chuo kikuu jangwani hapa ziko sababu:-

a.       Kwa kusudi la kukuonyesha dhambi zako – Mungu hukupeleka jangwani kwa kusudi la kukufunulia jinsi ulivyo, ukaidi wako na ubishi wako na ujeuri wako na kutokustahili kwako na manung’uniko yako, na jinsi ambavyo wewe na mimi sio bora kuliko wengine, ili tuwe mbali na kiburi, hili linafanyika kwa kukupeleka kwenye chuo chake jangwani ili huko umjue mwokozi wako vizuri na pamoja na uasi wetu wote tulio nao yeye anaendelea kutuhudumia kwa mahitaji yetu yote huko jangwani, jangwa linaumiza sana unapolipitia lakini ndio njia pekee ya kuyaona makosa yetu na njia zetu, huku tukiufurahia uzuri wa Mungu na njia zake. na matokeo yake jangwa litatuumbia utakatifu nidhamu na ujuzi kuhusu Mungu kivitendo.

 

Kumbukumbu 9:12-16 “Bwana akaniambia, Ondoka huko, shuka upesi; kwa kuwa watu wako uliowatoa Misri wamejiharibu; wamekengeuka mara katika njia niliyowaamuru; wamejifanyia sanamu ya kusubu. Tena Bwana akasema nami zaidi, akaniambia, Nimeliona taifa hili; na tazama, ni taifa lenye shingo ngumu; niache, nipate kuwaangamiza, na kulifuta jina lao chini ya mbingu; nami nitakufanya wewe uwe taifa kubwa lenye nguvu kuwapita wao.Basi nikageuka nikashuka mle mlimani, mlima ukawaka moto; na zile mbao mbili za agano zilikuwa katika mikono yangu miwili. Nikaangalia, na tazama, mlikuwa mmefanya dhambi juu ya Bwana, Mungu wenu; mmefanya ndama ya ng'ombe ya kusubu; mmekengeuka upesi katika njia aliyowaamuru Bwana.”       

 

Nehemia 9:13-21 “Tena uliyaona mateso ya baba zetu katika Misri, ukakisikia kilio chao, huko kando ya bahari ya Shamu; nawe ukaonyesha ishara nyingi na mambo ya ajabu juu ya Farao, na juu ya watumishi wake wote, na juu ya watu wote wa nchi yake; kwa maana ulijua ya kuwa waliwatenda kwa kutakabari; ukajipatia jina kama vile ilivyo leo. Nawe uliipasua bahari mbele yao, hata wakapita katikati ya bahari katika nchi kavu; na wale waliokuwa wakiwafuatia ukawatupa vilindini, mfano wa jiwe katika maji makuu. Zaidi ya hayo ukawaongoza kwa nguzo ya wingu mchana; na kwa nguzo ya moto usiku; ili kuwapa mwanga katika njia iliyowapasa kuiendea.Tena ulishuka juu ya mlima Sinai, ukasema nao toka mbinguni, ukawapa hukumu za haki, na sheria za kweli, na amri nzuri na maagizo;”

 

Israel walikuwa wameokolewa kutoka Misri lakini walikuwa ni wakaidi, wenye kiburi, wanasahau fadhili za Mungu kwa haraka, kwa hiyo jangwa liliwahusu ili wapokee maagizo ya Mungu, wafundishwe kutenda haki, wafuate sheria na amri nzuri liwe taifa lenye uadilifu na nidhamu ya hali ya juu, kwa hiyo jangwa liliwahusu, ili liwe taifa takatifu, ukuhani mteule watu wa miliki ya Mungu

 

b.      Kwa kusudi la kukutenga uwe wake – Mungu hukuongoza jangwani kwenye chuo chake ili akutenge na watu wa ulimwengu huu, anataka kukufanya wewe kuwa wa-pekee, alipowachakua Israel alitaka kuwatenga na kila aina ya ushawishi wa Kimisri, alitaka kuwaumbia kiu ya kumtegemea yeye tu, naye awafundishe kuwa ni yeye peke yake anayejali, na kufadhili kwa mahitaji yao yote, anataka umtegemee yeye tu ajifunue kwako kama rafiki wa karibu, akuache uwe mpweke ili yeye abaki kuwa rafiki wa kweli, ataacha ujeruhiwe ili yeye awe amani yako, atakuacha uwe dhaifu ili yeye awe nguvu zako. Kusudi kubwa likiwa ni kupitisha mpango wake kupitia wewe, hii haimaanishi kuwa wewe ni bora kuliko wengine bali ili Mungu apitishe mpango wake lazima akuchonge kule chuoni kwake jangwani nawe utakuwa tunu yaani kitu cha kujionea fahari

 

Kutoka 19:4-6 “Mmeona jinsi nilivyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za tai, nikawaleta ninyi kwangu mimi. Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu, nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli.”   

 

c.       Kwa kusudi la kuinua Imani na kukujenga upate kumuamini – jangwa linafundisha kumwamini Mungu na kumtegemea yeye, pia linaikuza Imani yako, linakuandaa kwa kusudi la kukufanya umtegemee Mungu moja kwa moja na kuisikia sauti yake na kumtii na kufuata muongozo wake, Mungu hapendezwi na wale wasiomuamini, Neno lake linasema na pasipo imani haiwezekani kumpendeza, kwa nini Mungu anaipima imani yetu? Kila wakati Mungu atakapoijaribu imani yetu ana mpango wa kutupeleka katika kiwango cha juu zaidi na kiwango cha kumjua yeye na kumkubali kuwa ndiye Mungu wetu.  

 

Kutoka 6:6-8 “Basi waambie wana wa Israeli, Mimi ni YEHOVA, nami nitawatoa ninyi mtoke chini ya mizigo ya Wamisri, nami nitawaokoa na utumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyoshwa, na kwa hukumu kubwa; nami nitawatwaeni kuwa watu wangu, nitakuwa Mungu kwenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ni YEHOVA, Mungu wenu, niwatoaye mtoke chini ya mizigo ya Wamisri. Nami nitawaleta hata nchi ile ambayo naliinua mkono wangu, niwape Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; nitawapa iwe urithi wenu; Mimi ni YEHOVA.”

 

d.      Kwa kusudi la kutufundisha utii na uvumilivu – jangwani ndiko Mungu anakotufundisha kusubiri, hakuna jaribu gumu duniani kama kusubiri, jangwani utake usitake huwezi kwenda kwa mwendo unaoutaka wewe, michanga itakuzuia, utachelewa kufika utasubiri sana na kwa sababu hiyo utaenda si kama utakavyo wewe bali kwa muda na wakati wa Mungu, utafuata maelekezo ya Mungu hata kama njia zake zinaonekana kuwa ngumu kusudi kubwa tupate kujifunza kutii na kuvumilia na kuwa na subira kabla ya kufika katika inchi njema

 

Kumbukumbu 4:1-10 “Na sasa, Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu. Msiliongeze neno niwaamurulo wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za Bwana, Mungu wenu, niwaamuruzo. Macho yenu yameona aliyoyatenda Bwana kwa sababu ya Baal-peori; maana wote waliomfuata Baal-peori, Bwana, Mungu wako, amewaangamiza kutoka kati yako.Bali ninyi mlioambatana na Bwana, Mungu wenu, mnaishi kila mmoja wenu, hata leo. Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama Bwana, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwingiayo ili kuimiliki. Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili. Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo. Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako; siku ile uliyosimama mbele za Bwana wako huko Horebu, Bwana aliponiambia, Nikusanyieni watu hawa, nami nitawasikizisha maneno yangu, ili wajifunze kunicha mimi siku zote watakazoishi duniani, wakapate na kuwafundisha watoto wao.”     

 

e.      Kwa kusudi la maonyo – Mungu hutupeleka katika chuo cha jangwani kwa kusudi la kutuonya, wakristo wengi sana tuna matumizi mabaya ya neema, kuna mambo Mungu anataka tuyaache hata hivyo lakini wengi tunaendelea nayo kwa hiyo jangwani ni sehemu ya maonyo, unakumbushwa sio tu kujiona ni mwenye dhambi, lakini kuomba neema ya kuziacha na kubadilika na kumwamini, mwamini Mungu sio tu kwa wokovu wako lakini pia kwa mabadiliko ya tabia zako, Israel walitaka kwenda kanaani hivyo hivyo na changamoto zao Mungu hakupendezwa nao kwa hiyo aliwaangamiza jangwani unapokuwa jangwani kubali maonyo, sikiliza Sauti ya Mungu kwa bidi jihoji wapi anataka nirekebishe kisha rekebisha, ni kiburi kujifikiri umesimama!

 

1Wakorintho 10:1-12. “Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari; wote wakala chakula kile kile cha roho; wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani. Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani. Wala msiwe waabudu sanamu, kama wengine wao walivyokuwa; kama ilivyoandikwa, Watu waliketi kula na kunywa, kisha wakasimama wacheze.Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu ishirini na tatu elfu. Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka. Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika, wakaharibiwa na mharabu.Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke

 

f.        Kwa kusudi la kukutia nguvu na kukuchonga - Changamoto za jangwani zitakujengea utulivu na kukuchonga uweze kuwa na sifa njema  na viwango vya ubora unaokubaliwa na Mungu kwaajili ya uongozi na huduma, uwakilishi na kukuweka katika mstari ulionyooka yaani bwana anakurudi, anakuchapa anakutia nidhamu, na utanyooka tu na kuwa wake kweli kweli, kabla ya kupewa umiliki uliokusudiwa katika maisha yako, utajifunza kumcha Mungu na kumuhofu yeye hili ni moja ya kusudi la chuo kikuu jangwani.  

 

Kumbukumbu 8:2-6.“Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo. Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana. Mavazi yako hayakuchakaa, wala mguu wako haukuvimba, miaka hiyo arobaini. Nawe fikiri moyoni mwako, ya kuwa kama vile baba amrudivyo mwanawe, ndivyo Bwana, Mungu wako, akurudivyo.Nawe uzishike amri za Bwana, Mungu wako, upate kwenda katika njia zake, na kumcha.”

 

g.       Kwaajili ya maandalizi ya huduma – jangwani ndiko Mungu anakuandaa kwaajili ya utulivu, ukomavu na majaribio ya huduma kwaajili ya kazi yake, wote watakaopita katika shule ya Mungu, chuo kikuu jangwani watatoka huko wakiwa na nidhamu ya hali ya juu, kiburi kinavunjiliwa mbali, woga unavunjiliwa mbali, kutokujiamini kunavunjiliwa mbali, Mungu anakuwa Mungu wako, na imani inapanda, na kumtegemea kunaongezeka na unaona rehema zake na utakumbuka kuwa ni yeye aliyekutokea huko jangwani ulikokutana naye

 

Kumbukumbu 29:5-6 “Nami miaka arobaini nimewaongoza jangwani; nguo zenu hazikuchakaa juu yenu, wala kiatu chako hakikuchakaa katika mguu wako.Hamkula mkate, wala hamkunywa divai, wala kileo; ili mpate kujua kwamba Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.”

 

Kila eneo ambalo Mungu amelikusudia likue kwaajili ya utumishi wake litasitawi na kukua, ufunuo mkuu wa huduma yako utaupata ukipelekwa jangwani yeye ndiye atajua kuwa utakapohitimu jangwani utakuwa ni mtu wa namna gani, utasema nini utafanya nini na utakuwa na sifa za namna gani.

 

h.      Kwa kusudi la Mungu kujifunua kwako – Mungu ni Mungu mwenye wivu, anapoamua kukupeleka jangwani anataka kujifunua kwako, anataka wewe na mimi tumjue yeye kwa kina na mapana na marefu zaidi ili sisi tuwe wake na yeye awe wetu, Yesu alipowaita wanafunzi wake pamoja na kuwa alikuwa anataka kuwatuma ili waifanye kazi yake lakini alikuwa anataka kwanza wawe wenzake wawe mali yake, Chuo kikuu jangwani kinakutaka uwe mali ya Mungu uwe mwenzake na ndio maana jangwani utatengwa na watu wote  

 

Kutoka 19:2-6 “Nao walipokuwa wameondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, wakatua katika lile jangwa; Israeli wakapiga kambi huko wakiukabili mlima. Musa akapanda kwa Mungu, na BWANA akamwita toka mlima ule, akisema, Utawaambia nyumba ya Yakobo, na kuwaarifu wana wa Israeli, maneno haya; Mmeona jinsi nilivyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za tai, nikawaleta ninyi kwangu mimi. Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu, nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli.”           

 

Marko 3:13-15 “Akapanda mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea. Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri ya kutoa pepo.”

 

i.        Kwa kusudi la kutunyenyekesha – Mungu huwa anataka tuwe wanyenyekevu kwa sababu nyingi sana, lakini kusudi kubwa ni kutulinda na dhambi ya kiburi, kiburi huwa kinaleta maangamizi ya haraka sana na Mungu hataki tuangamie, Shetani pamoja na malaika zake waliangushwa na kiburi, kwa sababu ya upendo wa Mungu kwetu hushughulika na kiburi chetu katika chuo chake kikuu jangwani ili tusijivune na kumsahau yeye, Mungu anajua kuwa unyenyekevu unaleta utajiri na Mungu ana makusudi ya kututajirisha lakini hebu fikiri kama utajiri utabebwa na mtu mwenye kiburi, kijapo kiburi ndipo ijapo aibu Mungu hataki kamwe tujifikiri kuwa sisi ni bora kuliko wengine, au watakatifu kuliko wengine au tumeokoka kuliko wengine

 

Kumbukumbu 8:2-3 “Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo. Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana.”

 

Zaburi 75:5-7 “Msiiinue pembe yenu juu, Wala msinene kwa shingo ya kiburi. Maana siko mashariki wala magharibi, Wala nyikani itokako heshima. Bali Mungu ndiye ahukumuye; Humdhili huyu na kumwinua huyu.”

 

Mithali 16:18-19 “Kiburi hutangulia uangamivu; Na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko. Afadhali kuwa na roho ya unyenyekevu pamoja na maskini, Kuliko kugawanya nyara pamoja na wenye kiburi.”

 

Mithali 22:3-4 “Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; Bali wajinga huendelea mbele wakaumia. Thawabu ya unyenyekevu ambao ni kumcha Bwana Ni utajiri, na heshima, nayo ni uzima.”

 

Kwa hiyo ni muhimu kufahamu kuwa unapoona Mungu anayaingiza maisha yako jangwani basi moja ya jambo ambalo tunapaswa kujifunza ni unyenyekevu, kwa haraka sana nyenyekea na unapofanya hivyo njia yako ya jangwani itafupizwa kwa haraka, Mungu atasubiri akuinue mara moja unapoamua kunyenyekea.

 

Yakobo 4:10 “Jidhilini mbele za Bwana, naye atawakuza.”

 

Katika makanisa Mengi na madhehebu mengi ya Kikristo, moja ya changamoto kubwa inayowasumbua wengi hasa wa makanisa ya kipentekoste ni pamoja na tatizo la kiburi, na wanaoongoza kwa unyenyekevu ni wakatoliki, makasisi wengi au wote wa kikatoliki ni wanyenyekevu sana, na sifa hii ya unyenyekevu waliyo nayo sio ya kuigiza, wote tunaweza kukubaliana kuwa hakuna mwanadamu mkamilifu, na kila mwanadamu anaweza kuwa na udhaifu huu au ule lakini katika habari ya unyenyekevu tukubaliane wazi kuwa Wakatoliki wako vizuri katika swala la unyenyekevu kuliko madhehebu mengine, katika mafunzo yao hujifunza kupitia mabadiliko mbalimbali ambayo yana mkazo mkubwa sana katika unyenyekevu, huwezi kupita jangwani katika chuo kikuu cha Mungu kisha ukatoka na kiburi, Musa alikaa jangwani na  akawa na mabadiliko makubwa sana kutoka Musa yule mkali aliyekuwa anamuua Mmsri kwa mikono ywake na kumfukia mpaka kuwa mtu mpole zaidi kuliko wote

 

Hesabu 12:1-3 “Kisha Miriamu na Haruni wakamnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana, alikuwa amemwoa mwanamke Mkushi.Wakasema, Je! Ni kweli Bwana amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia? Bwana akasikia maneno yao. Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi.”

 

Kama maandiko yanatueleza kuwa Musa alikuwa mpole (Maana yake mnyenyekevu) zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi Je unadhani Yesu alikuwa mpole kiasi gani?

 

Isaya 53:7-9 “Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake. Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu.Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.”

 

Makasisi wa kikatoliki hujifunza njia ya unyenyekevu wakiishi kwa mfano huo na kukubali fundisho liitwalo “The Theological concepts of Kenosis” Fundisho linalokazia kujinyenyekeza kunakopita kawaida ili tu uwahudumie watu, Yesu Kristo akiwa kielelezo cha unyenyekevu huo, ukiacha kifo chake cha aibu, huruma zake na upole na tendo la kuwaosha miguu wanafunzi wake sio kwaajili ya kufundisha tu na kuonyesha kielelezo bali Yesu alikuwa anafanya kweli tukio lile ambalo Petro hakulikubali kwani aliona haishatihi Mwalimu kujishusha katika kiwango cha utumwa wa kupitakawaida

 

Wafilipi 2:4-8 “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine. Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba

 

Kwa hiyo unyenyekevu wa aina hii tunaweza kujifunza kwa kupitia chuo kikuu cha jangwani ambako tunajifunza kutambua kuwa hatuwezi jambo lolote bila Mungu, tunajifunza kumtegemea Mungu kwa kila kitu, tunajifunza kuwatumikia wengine kwa unyenyekevu, na tunajifunza kujilinda na kiburi na kuacha kabisa majivuno,  Unyeneyekevu ni nguzo muhimu sana kwaajili ya huduma na kwaajili ya kutengeneza uhusiano wa ndani sana na Mungu, kwa hiyo ukiwaona watu wanajivuna, wanajigamba, wanafokea washirika, wanajitutumua, wanajifanya mabwana katika makanisa yao, wanajifanya watawala machifu, watemi, wanatengeneza himaya na kutaka kukuza majina yao kuliko la Yesu ufahamu chuo hiki kwao bado sana, yaani mtumishi wa Mungu anakuwa kama Mungu kwenye kanisa lake na anajivika uhakimu siku zote akiwahukumu wengine Mungu na atupe neema sana na kuturehemu sana na kutusamehe sana 

 

1Petro 5:1-5 “Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye;lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo.Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi.Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka.Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.”

 

Ni wapi sasa Mungu anaweza kutufundisha shule hii ya unyenyekevu, usipojifunza mwenyewe kama wakatoliki wanavyojifunza na kujitia nidhamu kubwa sana tena huku wakiwa na elimu kubwa sana lakini wakiwa wanyenyekevu sana taaluma hii tunaweza kuipata na kujifunza vizuri, ikiwa Mungu ataruhusu tupite katika chuo chake kikuu jangwani.  

 

Jangwani ni eneo la mabadiliko, ni njia ya mpito ambapo watu wa Mungu hususani watumishi wanaandaliwa kwaajili ya kazi kubwa sana iliyoko mbele yao, kwa hiyo wakati mwingine utalazimika kupitia mapito magumu sana na majaribu mazito ili Mungu akulazimishe kukua kiroho na kukuandaa tayari kwa huduma na wakati mwingine atakuacha kwenye upweke mkubwa, kubwa zaidi jangwani ni sehemu ya usukivu MIDHBAR ni mahali ambapo kila kitu kinasema kila pito linasema, kila jambo linasema lakini vyote Mungu anavitumia kwaajili ya kukuchonga na kukuandaa kwa huduma na utumishi uliotukuka ambao utakufanya utembee bila kiburi wala majivuno wala utapeli, wala unafiki wala kuigiza, Kama Mungu angekuwa haruhusu watu kupitia Chuo kikuu jangwani matepeli wengi sana wangejiingiza katika kazi ya kuhubiri injili lakini ukimuona Muhubiri yeyote yule ana nidhamu ya hali ya juu, anahudumia watu kwa unyenyekevu, yeye mwenyewe akiwa kielelezo cha unyenyekevu huo ujue amepitia jangwani, na ukimuona muhubiri yoyote yule muhuni muhuni mambo yake hayaeleweki, anatapeli watu janja janja nyingi ujue hajapitia jangwani, jangwani ni chuo kikuu kinachohitimisha watu walioiva kihuduma na kiuadilifu, na kiimani na wanaomtegemea Mungu. Watu waliopitia chuo hiki cha siri ni watu wa tofauti sana waliojaa mamlaka ya kiungu. Na usemaji wao na utendaji wao na tabia yao na unyenyekevu wao unakuwa kama sare ya shule (Uniform).


Chuo kikuu jangwani 

Jangwani sio lazima liwe jangwa halisi lakini ninapozungumzia jangwa hapa nimechukua picha ya ukweli halisi kutoka katika maandiko na kukuleta katika ukweli halisi kuhusu mapito unayoyapitia au tunayoyapitia katika maisha haya, mapito haya ndio shule ya Mungu, ndio chuo kikuu jangwani ni chuo kikuu cha mafunzo ya kila aina ambayo Mungu anayaruhusu katika maisha yetu, wote tunafahamu kuwa leo hii dunia ina vyuo vikuu vya kila aina vilivyobora na vizuri sana na vinatoa kila aina ya degree, (Shahada) kwa hiyo kuna ubora wa hali ya juu sana wa elimu na kuna degree za kila aina zinazotoa mafunzo ya kila aina kwa hiyo tunamshukuru Mungu kuwa leo watu wanaweza kuwa na ujuzi na ufahamu na elimu ya kila aina na katika elimu ya Mungu kuna vyuo vingi vikuu vya Biblia na tunafurahia kuona watumishi wa Mungu wakiwa na PHD degree, watu wanapokea vyeti vya aina mbalimbali  yaani astashahada, Stashahada, Shahada, Shahada ya uzamiri, Shahada ya uzamivu na Shahada ya ubobevu  na vyuo hivyo vina ubora mkubwa wa kutosha, hata hivyo bila chuo kikuu cha Roho Mtakatifu mambo mengi yatakuwa ni nadharia tu. Mungu huwa ana namna yake ya kumuandaa mtumishi wake na kwa njia hizo huwa anamfundisha vile anavyopaswa kuwa, Mungu alipomuita Saul/Paulo mtume alimuandaa kuwa chombo chake kiteule, alimuandaa kuichukua injili kwa wafalme na alimuandaa kama mtu atakayekuwa tayari kuvumilia mateso kwaajili ya jina la Yesu, ona:-

Matendo 9:1-16 “Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu.Hata alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni. Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi?Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe. Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda. Na wale watu waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, wakiisikia sauti, wasione mtu.Sauli akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski. Akawa siku tatu haoni; hali, wala hanywi. Basi palikuwapo Dameski mwanafunzi jina lake Anania. Bwana akamwambia katika maono, Anania. Akasema, Mimi hapa, Bwana. Bwana akamwambia, Simama, enenda zako katika njia iitwayo Nyofu, ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu aitwaye Sauli, wa Tarso; maana, angalia, anaomba; naye amemwona mtu, jina lake Anania, akiingia, na kumwekea mikono juu yake, apate kuona tena. Lakini Anania akajibu, Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi aliyowatenda watakatifu wako Yerusalemu; hata hapa ana amri itokayo kwa wakuu wa makuhani awafunge wote wakuitiao Jina lako.Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli. Maana nitamwonyesha yalivyo mengi yatakayompasa kuteswa kwa ajili ya Jina langu

Changamoto kubwa sana inakuja endapo watu hawatapita katika chuo kikuu cha jangwani, hiki ni chuo cha kiroho ni chuo cha mabadiliko ya kitabia, ni chuo cha uadilifu, ni achuo cha utumishi, ni chuo cha kukuchonga na kuondoa kiburi, ni chuo cha unyenyekevu, ni chuo ambacho kitakufanya umjue yule unayemtumikia kivitendo, Ni chuo kitakacho kujulisha huduma uliyoitiwa na nini cha kufanya, Ni chuo ambacho utasikia sauti ikisema Sauli Sauli mbona waniudhi? Ni chuo ambacho utakutana na Kristo mwenyewe wazi wazi ukipitia chuo hiki hutafanya kazi ya Mungu kama unavyojisikia au unavyotaka, utaifanya kama ulivyofundishwa na Yeye mwenyewe, kama unabisha waangalie watumishi wote wa Mungu waliopitia chuo kikuu cha jangwani na kuleta mageuzi makubwa na uamsho mkubwa na kufanya mambo ya kushangaza duniani, na hawa tuliowaangalia katika maandiko utagundua kuwa  hawajawahi kwenda kwenye vyuo maarufu sana hapa duniani, lakini walikuwa kweli ni mdomo wa Mungu, walijulikana wazi kuwa wamepitia jangwani, hawakuishi wakati mmoja lakini walifanana kwa sababu Mwalimu wao ni mmoja, ni watu ambao watu hawakuwahi kuwawaza wala kuwaota, walikuwa wana jangwani hasa, hakuna mtu aliejua wanatokea wapi, lakini wakitokea unawakubali,  lakini ghafla waliinuka kuwa kinywa cha Mungu, walizunguka na kuzungumza kwa mamlaka na nchi na mataifa yalitetemeka, walizungumza kweli iliyonyooka, walitoboa siri za mioyo ya watu walipotokea hadharani hawakupwaya kila mtu alijua ya kuwa wameandaliwa hasa, na wanafaa kwa kazi hiyo, nyuso zao, maisha yao, mavazi yao, ujasiri wao, utayari wao, mamlaka yao, ishara zao, na miujiza yao ilikuwa imejawa na uhakika wa kiungu, walikuwa na uadilifu ulionyooka, hutasikia wameshika mtu chuchu, au wameshika mtu kalio au wanaropoka mambo yasiyofaa, walikuwa wamejawa na ujumbe wa kimilele,  mmoja tu wa wahitimu hao alikuwa na thamani ya jeshi zima la Israel, kumbuka alipokufa Elisha, mtu alilia baba yangu baba yangu magari ya Israel na wapanda farasi wake, yaani Jeshi la Israel limeondoka! haiwezekani watu wamuwakilishe Mungu alafu wawe hawaeleweki, mara wanaibia watu, mara wagonjwa wanaibiwa na kutapeliwa, mara kuwaona wao ni mpaka ulipie, mara ukiingia lazima uwasujudie, mara lazima uvue viatu kuna mbwembwe nyingi sana,  waliopitia chuo kikuu cha jangwani walikuwa ni watu walionyooka kama rula, hawakua na mizaha hata kidogo, hawakuwa na ubinafsi wala sio wapiga dili au wasaka fedha, sifa zao, akili zao, midomo yao, uadilifu wao ulionyesha wazi kuwa walikuwa wanamuwakilisha Mungu, kulikuwa na kila ushahidi unaoonyesha kuwa hawakuwa watu waliozuka tu kwa bahati mbaya! na wala hawakuumiza watu, wala kuwatawala watu kwa ukali lakini waliunguruma maneno ya Mungu kama simba!, Upako haukuwa wa kubahatisha, vinywa vyaio havikujaa majivuo, wafalme waliwatambua na raia waliwatambua, wajane walinufaika na yatima walitiwa moyo, walikemea dhuluma waliwaonya wafalme!

Walikuwa ni watu ambao maisha yao huwezi kusimulia, walikuwa tayari kwa lolote, walikuwa tayari kwa vita ya aina yoyote, waliijua dhambi, walijua siri za mioyo ya watu, walijua maarifa ya Mungu, walijaa hekima kama anga, wakati waliowajia walikuwa wamelala wao walikuwa ni sababu ya uamsho mkubwa, uamsho waliokuwa wakileta haukutegemea maombi ya kundi la watu ilikuwa ni Eliya mmoja tu, Ilikuwa Ni Yohana mmoja tu, ilikuwa ni Amosi mmoja tu, umati wa watu uligeuka kwa Yona mmoja tu, hawa walikuwa ni askari kweli kweli wakati watu waliowahudumia walikuwa wanaota ndoto, wao walikuwa na maono sahihi na neno sahihi la Mungu lilikuwa ndani yao, wakati wengine walikuwa wakipiga pesa, wao walijawa na uaminifu, na kuwa mbali na hila, wakati mamia ya watu wakiwa wanajifurahisha katika starehe  na kujifurahisha na anasa za dunia, kufanya biashara na kufuata namna ya dunia hii, huku shule za dunia hii zikiwa zimejawa na kila aina ya starehe za kuwatuliza na kuwafurahisha, wao walikuwa na ujumbe mpya na elimu mpya kutoka chuo kikuu jangwani wakiamsha nia za wahubiri na wananchi kumcha Bwana,  waliingia kila mahali walikotumwa na Mungu, kutoka kwa wafalme mpaka kwa wajane, waliamuru watu kurudi katika njia za Mungu, wakiwa na uwepo wa Mungu, hali ya kiroho ya juu, nguvu za Mungu zisizo na maswali, walijawa na silaha za kimbingu watu walinyamaza kimya waliponena, watu walitetemeka walipowaona, na waliwataka watu watubu na kuacha kuabudu sanamu na waliwahuisha watu kuishi kwaajili ya Mungu na kumtumikia Mungu, waliowaonya masikini kwa matajiri, wafalme kwa watumwa na walilikabili taifa lolote hata nje ya mipaka. Walikuwa kielelezo, walikemea dhuluma, rushwa na ubadhirifu, hawakupaka mtu mafuta kwa mgongo wa chupa.

Hawakuwahi kuwa na uongo mioyoni mwao wala midomoni mwao, walikuwa wanamuwakilisha Mungu wa kweli, waliandaliwa na walikuwa tayari wakitokea jangwani, walisimama katika zamu zao kwa uaminifu, na hawakuonekana kuwa labda wamechanganyikiwa walikuwa na akili, akili timamu na walikuwa na uwezo wa kujibu maswali yoyote ambayo yangeinuka, na kuulizwa na mtu yeyote haijalishi ni swali na namna gani na limetoka kwa nani, walikuwa na ujuzi wa kujibu kila aina ya hoja ziwe za askari, ziwe za raia, ziwe za masadukayo, ziwe za mafarisayo, ziwe na maherode, ziwe za waesene, waliweza kumkemea kila mtu hata mfalme alipokosea hawakumficha kitu, malikia waovu waliwaogopa, Chuo kikuu jangwani kilikuwa kimewaandaa kusema kweli bila hofu walikuwa wako tayari kukabiliana na yeyote yule kwa sababu zozote zile zilizo kinyume na mapenzi ya Mungu, waliwarejesha watu wa Mungu wakikemea kila njia mbaya, ibada mbaya, ibada za sanamu, uchawi, uasi, kupoa, ushirikina, na ukengeufu na waliwataka watu wasisahahu kuwa yuko Mungu mbinguni, hawa walishazoea kuwa peke yao walibaki na Mungu tu, waliomba, walihubiri, walikemea na kuonya, na walimleta Mungu mzima mzima katika mioyo ya watu kwa kweli walionyesha kila jinsi kuwa wamehitimu katika chuo kikuu cha Mungu chuo kikuu jangwani!, waliijua sheria ya Mungu, waliijua torati ya Musa walilijua neno la Mungu, waliwaonya manabii wa uongo, waliamuru wachawi kutokuliona jua, walikuwa watu wa kipekee, Unapopelekwa jangwani Mungu anataka muhitimu wa aina hii.

Chuo kikuu jangwani ni majaribu, ni mapito, ni nyakati ngumu, ni kila aina ya uchungu unaoupitia duniani katika kila unachokipitia acha kulia acha kulalamika na badala yake tulia usikilize sauti hiyo ya jangwani inataka nini baada ya hayo unayoyapitia jangwani utaisikia sauti ya Mungu, itakufundisha utii, itakufundisha unyenyekevu, Jangwa halionekani kuwa kitu kizuri, na unaweza kusema kwanini Mungu ameumba jangwa lakini jangwa lina ujumbe mzito kwetu kuwa linaweza kuwa Mwalimu mzuri wa maswala ya kiroho, jangwa linaonya, jangwa linafundisha adabu, jangwa linaelekeza, jangwa lina amri, jangwa linatia nidhamu, jangwa linaondoa kiburi, jangwa linakufundisha kuwa hutaishi kwa mkate tu, jangwa linakufudisha chakula cha mbinguni, jangwa linakufundisha kuwa shujaa wa vita, jangwa linakufundisha dhiki sio kitu kwa Mungu, Nyoka sio kitu kwa Mungu, Nge wake sio kitu kwa Mungu, miba zake ni uvumilivu, jangwa linakukumbusha kuwa ukiwa na Mungu hutapungukiwa na kitu, jangwa linakukumbusha kutokuogopa mabaya, jangwa linakukumbusha kuwa Mungu anaweza kutokeza maji kutoka katika mwamba mgumu, jangwa linakufanya uwe mtu wa miliki ya Mungu, angwa linakufanya uwe imara, jangwa linakufanya uwe mtumishi wa kipekee, jangwa linakupa kuifanya huduma uliyoitiwa kwa ufanisi, jangwa linakuimarisha, jangwa linaondoa shaka, jangwa linakufanya uwe na maamuzi, jangwa ni sauti ya Mungu kivitendo, jangwa linakufanya uwe mnyenyekevu, watu watakujua ukoje ukifunua kinywa chako na wanaweza kukudharau wakikuona, jangwa ni chuo!

Mwangalie Musa, mwangalie Eliya, mwangalie Yohana mbatizaji, wote hawa walikuwa wahitimu wa jangwani ona jinsi walivyokabiliana na wafalme, ona jinsi walivyosimamia uadilifu, ona walivyokuwa na mamlaka ya kiungu, ona jinsi ambavyo hawakuwa waoga ona jinsi Mungu alivyokuwa pamoja nao na ona jinsi Mungu alivyowatumia!

Kama watu wa Mungu na watumishi wote mnaowana leo wangepita katika shule hizo tungekuwa na watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao.  Je unajisikiaje unateseka, unaona kama Mungu amekuacha, unajihisi mpweke, unakabiliwa na njaa, unahisi watu wote wamekuacha, hauna msaada, unakata tamaa? Unajiona kama una laana? Unajiona umechelewa? Ni kama hauna bahati? Mambo hayakunyookei? Huna connection? unaona giza, Je umejawa na mashaka? Umejawa na msongo wa mawazo? Unahisi umetengwa na Mungu?, Mungu anaonekana yuko mbali?, Mungu anaonekana hayuko?, Mungu anaonekana hawajibiki? Umejawana mashaka tupu na hakuna imani? Unahisi uko peke yako? Ni kama umepotea, ni kama hauna ulinzi, Umejawa na hofu na kukosa matumaini? Unahisi umepoteza muelekeo? Umeachwa? Hakuna wa kukujali? Hupendwi tena? uko kama umechanganyikiwa ndugu yangu usiogope ukiona hayo unayapitia ujue uko chuo kikuu cha jangwani, hakuna Mkristo anayempenda Yesu ambaye atakwepa kabisa kupitia chuo hiki! mimi ninakijua nimepita kwenye chuo hicho, nimeishi kwenye chuo hicho, nimeelimisjhwa kwenye chuo hicho? Umewahi kutengwa wewe? Mimi nimewahi, umewahi kuchafuliwa wewe? Mimi nimewahi, Umewahi kukataliwa wewe mimi nimewahi, watu wamewahi kukuacha wote? Mimi nimewahi, umewahi kutungiwa uongo? Mwenzako nimewahi, umewahi kukosa kazi, mimi nimewahi, umewahi kuacha kutumiwa na Mungu kabisa mimi nimewahi, umewahi kufilisika, mimi nimewahi, umewahi kuteuliwa kisha kutenguliwa? Mimi nimewahi, umewahi kuahidiwa kitu na mtu kisha asikutekelezee, mimi nimewahi, umewahi kutengwa na mkeo, mimi nimewahi, umewahi kufanyiwa mabaya na watu wa karibu mimi nimewahi, umewahi kushauriwa vibaya mimi nimewahi, umewahi kutapeliwa fedha nyingi sana? Mimi nimewahi umewahi kumlaumu Mungu? Mimi nimewahi, ndio kwa sababu ni wakati ambao Mungu anaonekana hajali, hahesabu kama kuna kitu umewahi kukifanya, maandiko yake yote yanaonekana kana kwamba ni nadharia tu unajiuliza anawezaje kuruhusu haya kutokea maishani mwangu?, Hivi kweli yupo? Anaweza kuonekana kweli, au kila kitu kinakuwa kama batili hivi, Je umewahi kuranda randa? Mimi nimewahi umewahi kuhisi kuchanganyikiwa? Mimi nimewahi, umewahi kushindana na kitu Fulani mwilini mwako kikuachie na kikawa hakitaki mimi nimewahi, umewahi kuwa katika hali ya ukavu kabisa? Mimi nimewahi, umewahi kuhubiri mkutano siku tatu na mtu asiokoke? Mimi nimewahi na nilitamani niache kabisa injili? Umeahi kujisikia kutikula na chakula kipo? Mimi nimewahi, umewahi kuharibikiwa mipango yako yote? mimi nimewahi, umewahi kushindwa vita na adui zako? Mimi nimewahi umewahi kulia hadharani? Mimi nimewahi, umewahi kutukana hadharani? Mimi nimewhi, umewahi kufanyiwa hila na walokole wenzako? Mimi nimewahi, umewahi kufanya makosa makubwa sana? Mimi nimewahi, aibu yako imewahi kutawanyaika kila mahali mimi nimewahi, umewahi kuwasikia watu wakikuzungumza vibaya huku hawakujui? Mimi nimewahi kuwasikia watu wakizungumza mabaya kunihusu utadhani wananijua! ukiyaona hayo basi usijifikiri kuwa wewe ni mtu mbaya, au eti Mungu anakunyoosha hapana ujue uko chuo cha jangwani Mungu hutupeleka huko tuone ujinga wetu, tujifunze hekima yake, tuzijue njia zake, na kutambua jinsi alivyo mkuu na mwema! Unaweza kuwa na maswali meengi sana lakini majibu ndio haya anatupeleka katika jangwa la kutisha ili tuwe watu wake, anatupitisha katika tanuru la moto ili tutoke kama dhahabu iliyo safishwa, tayari kwa matumizi mengine baada ya kutoka jangwani utakuwa mtu wa namna nyingine, na ndugu zako watakuinamia, kila atakayekuona atakuheshimu utakuwa rafiki wa Mungu na utaongea na Mungu uso kwa uso huku ukiwa hauna majivuno na ukiwa mpole na mnyenyekevu kuliko watu wote. Matokeo ya uvumilivu wako yatakuleta katika kilele cha utumishi uiotukuka n ahata ukiondoka kazi yako itadumu duniani na kuwa msaada kwa watu wengi sana.  

2Wafalme 2:11-15 “Ikawa, walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea, tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli.Naye Elisha akaona, akalia, Baba yangu, baba yangu, gari la Israeli na wapanda farasi wake! Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe, akayararua vipande viwili.Kisha akaliokota lile vazi la Eliya lililomwangukia, akarudi, akasimama katika ukingo wa Yordani.Akalitwaa lile vazi la Eliya lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, Yuko wapi Bwana, Mungu wa Eliya? Naye alipoyapiga maji, yakagawanyika huku na huku, Elisha akavuka.Na hao wana wa manabii, waliokuwako Yeriko wakimkabili, walipomwona, walisema, Roho ya Eliya inakaa juu ya Elisha. Wakaja kuonana naye, wakainama kifudifudi mbele yake.”

Ayubu 23:2-10 “Hata leo mashitaka yangu yana uchungu; Pigo langu ni zito zaidi ya kuugua kwangu.Laiti ningejua mahali niwezapo kumwona, Nifike hata hapo anapokaa! Ningeiweka daawa yangu mbele yake, Na kukijaza kinywa changu hoja. Ningeyajua maneno atakayonijibu, Na kuelewa na hayo atakayoniambia. Je! Angeshindana nami kwa ukuu wa uwezo wake? La, lakini angenisikiliza. Hapo walekevu wangepata kuhojiana naye; Basi hivyo ningeachiliwa na mwamuzi wangu milele. Tazama, naenda mbele, wala hayuko; Narudi nyuma, lakini siwezi kumwona; Na mkono wa kushoto, afanyapo kazi, lakini siwezi kumwona; Hujificha upande wa kuume, hata nisimwone. Lakini yeye aijua njia niendeayo; Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.”

Mithali 3:5-6 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.”

Hitimisho

Chuo kikuu jangwani ni chuo cha changamoto nyingi lakini zenye faida kubwa sana katika maisha nya kiroho, kwani unapata uzefu wa kuishi maisha ya kumtegemea Mungu,  na kukupa nguvu na ujasiri mwingi katika kukabiliana na changamoto za maisha, aidha jangwa linamsaidia mtu wa Mungu kukua kiroho na kwenda katika nagzi ya juu kabisa ya uadilifu nidhamu na kuishi kwa kanuni, jangwa linakufanya uwe wa kipekee, na jwangwa linakufanya uwe makini na uthamini kila kitu katika maisha, utaona uthamani wa chakula, utaona uthamani wa maji, utajua uthamani wa makazi, utajua uthamani wa umoja, utaona uthamani wa uhusiano, utajifunza kukua, kuimarika kiroho, na utagundua kuwa kilikuwa kipindi cha Baraka kwa maisha yako na utumishi wako, Bwana akupe neema na uwezo wa kuvumilia shule anayokupitisha na kusaidie uweze kuhitimu salama.

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima  

+255 718 99 07 96