2Timotheo 2:20-22 “Basi katika nyumba kubwa
havimo vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali na vya mti, na vya udongo; vingine
vina heshima, vingine havina. Basi ikiwa mtu amejitakasa kwa kujitenga na hao,
atakuwa chombo cha kupata heshima, kilichosafishwa, kimfaacho Bwana,
kimetengenezwa kwa kila kazi iliyo njema. Lakini zikimbie tamaa za ujanani;
ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa
moyo safi.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa asilimia
25 ya wanadamu waishio Duniani ni vijana, Idadi ya vijana duniani kwa sasa ni
Bilioni 1.7, na asilimia 86 ya vijana hao wanaishi katika inchi zinazoendelea,
Wastani wa umri wa vijana wanaoongezeka ni kati ya miaka 15-24 na wengi wao
wako Afrika, Asia na Amerika ya kusini, kwa hiyo utaweza kuona kundi hili
linakuwa na kuongezeka kwa kasi, aidha kundi la vijana ndio nguvu kazi kubwa ya
jamii na kanisa kwa ujumla, Vijana ni kundi muhimu sana kwaajili ya jamii na kanisa
la sasa na baadaye, Mungu amekuwa akiwahitaji vijana na amekuwa akiwatumia sana
katika kazi yake kama inavyoonekana katika maandiko, ni ukweli uliowazi
kibiblia kuwa wakati wa ujana ndio wakati muhimu sana wa kumcha Mungu na
kumtumikia kuliko wakati mwingine wowote,
Muhubiri 12:1-7 “Mkumbuke Muumba wako siku
za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka
utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo. Kabla jua, na nuru, na mwezi, Na
nyota, havijatiwa giza; Kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua;Siku ile walinzi
wa nyumba watakapotetema; Hapo wenye nguvu watakapojiinamisha; Na wasagao
kukoma kwa kuwa ni haba; Na hao wachunguliao madirishani kutiwa giza; Na
milango kufungwa katika njia kuu; Sauti ya kinu itakapokuwa ni ndogo; Na mtu
kusituka kwa sauti ya ndege; Nao binti za kuimba watapunguzwa; Naam, wataogopa
kilichoinuka Na vitisho vitakuwapo njiani; Na mlozi utachanua maua; Na panzi
atakuwa ni mzigo mzito; Na pilipili hoho itapasuka; Maana mtu aiendea nyumba
yake ya milele, Nao waombolezao wazunguka njiani. Kabla haijakatika kamba ya
fedha; Au kuvunjwa bakuli la dhahabu; Au mtungi kuvunjika kisimani; Au gurudumu
kuvunjika birikani; Nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, Nayo roho
kumrudia Mungu aliyeitoa.”
Pamoja na ushauri mzuri wa
kimaandiko kwa vijana kutoa muda wao wa ujana katika kumtumikia Mungu, kundi
hili linamashambulizi makali sana kutoka kwa Shetani, Dunia na miili yao,
kimsingi ni kundi ambalo linashambuliwa kwa kiwango kikubwa kupitia tamaa, kwa
hiyo hata wanapojitoa katika kumtumikia Mungu bado watazingwa na tamaa za
ujanani ambazo Paulo mtume anamsihi Timotheo kuhakikisha kuwa anazikimbia tamaa
hizo, Kwa msingi huo leo tutachukua Muda wa kutosha kujifunza jinsi ya
kukabiliana na changamoto hizo za ujanani kwa kuzingatia vipengele vitatu
vifuatavyo:-
·
Maana ya tamaa za ujanani.
·
Athari ya
tamaa za ujanani.
·
Jinsi ya kukimbia tamaa za ujanani
Maana ya tamaa za ujanani:
2Timotheo 2:22 “Lakini zikimbie tamaa za
ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao
Bwana kwa moyo safi.”
Neno tamaa za ujanani katika
Biblia ya kiingereza linasomeka Youthful
lusts au evil desires of Youth
yaani tamaa za ujanani au tamaa mbaya za ujanani katika Biblia ya kiyunani neno
tamaa linalotumika hapo ni Epithumia
ambalo kwa kiingereza tafasiri yake ni Longing
for what is forbidden au concupiscence
ambalo tafasiri yake strong sexual
desire, nymphomania, abnormally intense sexual desire, the tendence of human to sin, tamaa ya
kutenda dhambi.
Wakolosai 3:5-6 “Basi, vifisheni viungo
vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na
kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu.”
kwa hiyo tafasiri yake ni tamaa
ya kutaka kufanya kitu kilichokatazwa na Mungu, au tamaa kali ya ngono, au
tamaa isiyokuwa ya kawaida inayotaka utamani ngono, kiufupi ni tamaa kali na
inaweza kuwa ya ngono au ya mambo mengine ambayo huwasonga zaidi vijana, tamaa
hizi za ujanani zinaweza kuchukua umri kati ya miaka 15-70 hivi kwa wanawake na
15-80 hivi kwa wanaume. Kwa msingi huo utaweza kuona ni katika umri ule ule
Muhimu ambao Mungu anataka kumtumia mtu, kwa hiyo ili zisiingiliane na mapenzi
ya Mungu, au kuharibu mwenendo wa mtu wa Mungu, Paulo anamuasa Timotheo
kujihami nazo tamaa hizo tunaweza kuzianisha kama ifuatavyo:-
1. Tamaa ya mwili – Wakati wa ujana,
kipindi ambacho mwili wa kijana unajijenga na kuzalisha vichocheo vingi sana,
mahitaji ya kingono pamoja na mihemko mingine kwa vijana huwa yanawaka kwa
kiwango kikubwa sana na hayatajali kuwa umeokoa, unafunga sana na kuomba sana
na kuhudhuria sana ibada wakati wote unaweza kujikuta unamtumikia Mungu lakini
nguvu ya mwili, kuhitaji na kutamani ngono inakuwa iko pale pale, mihemko na
kushindwa kujitawala kihisia kunakuwepo vilevile, jambo hili limesumbua sana
vijana wengi mpaka wanachanganyikiwa, vijana wengi wanajichua, na wengi
wanaangalia picha za ngono, wakitafuta kwa kila namna kutimiza kiu yao ya
kingono ambayo inaonekana kama haina kitoshelezo taabu hii wanayoipitia vijana
ni kama watumishi wengi wa Mungu hawaijui au hawaijali, na wanachojua wao ni
kusubiri wasikie wamefanya uasherati na kuwatenga na kuwaharibu zaidi, na wala
kwa kufanya hivyo hawawezi kujiondoa katika kifungo hicho cha tamaa, kuwaka kwa
hasira, wivu, husuda, ulafi, uvivu na kadhalika kunawapelekesha sana kundi hilo,
kwa sababu vichocheo katika miili yao vinakuwa bado havijapata utengemavu wa
utulivu, kwa hiyo kundi hili linateseka sana bila kupata njia ya kujiokoa
katika hilo
1Petro 2:9-11 “Bali
ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya
Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie
katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa
la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.Wapenzi, nawasihi
kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho.”
Wagalatia 5:16-21 “Basi
nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu
mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi
zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka. Lakini mkiongozwa na Roho, hampo
chini ya sheria. Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati,
uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina,
faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika
hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao
mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.”
1Wathesalonike 4:3-4 “Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu,
mwepukane na uasherati; kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika
utakatifu na heshima;”
Vijana wanateseka
katika eneo hili, Watumishi wa Mungu wanapokwena katika vyuo vya Biblia huwa
tunawafundisha somo la kufanya UTAFITI,
Research, Somo hili linaelekeza kuwa kazi ya Mchungaji sio kuchunga na
kuhubiri tu, lakini lazima ufanye utafiti, na pia tunawafundisha somo la Saikolojia (Pyschology) ili kwa pamoja wafanye utafiti wa kisayansi kuhusu
tabia, jamani si tunashughulika na tabia za watu, wakati mwingine tufanye
utafiti kwanini kundi hili la watu au kabila hii, au wanaume au wanawake au
watoto wana tabia ya ina Fulani ili tujue namna ya kuwasaidia kila mmoja sawa
na uhitaji wake na kwa njia za kiroho tutaweza kuwasaidia na kutatua changamoto
zao na nyingine zinachukua muda mrefu, usiwe kama mjinga kila kitu unakimbilia
kukitangaza na kutenga tu, Fahamu Paulo alijua kuwa ziko tamaa za ujanani, na
alikuwa akimuonya Timotheo azikimbie kwa hiyo tabia hizo ni za kimaumbile na
kuwa rohoni haimaanishi uko nje ya.
2.
Tamaa
ya mali na vitu – Changamoto nyingine ya tamaa ya vijana ni mafanikio ya
haraka haraka, jambo ambalo linawaletea Matamanio ya kuwa na vitu vya anasa,
utajiri wa haraka na mali za dunia, jambo hili limesababisha mtego mkubwa kwa
vijana na maumivu katika mioyo yao na kukata tamaa au kutoka nje ya neema ya
Mungu pale wanapokosa, kuwa na mali na utajiri na Fedha sio dhambi kama utapata katika njia
halali, lakini wakati wa ujana spidi ya uhitaji wa mafanikio ya haraka hara
huwa kubwa kiasi ambacho unaweza kuingia mtegoni hilo ndilo ambalo maandiko
yanaonya.
1Timotheo 6:9-10 “Lakini
hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi
zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na
uharibifu.Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo
wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu
mengi.”
3.
Tamaa
ya mashindano – Changamoto nyingine katika tamaa za ujana ni kutaka
kujulikana ni tamaa ya kujifurahisha, ni tamaa ya ubinafsi, na kutaka
kushindana na wengine na kuwashinda ikiwezekana kwa njia yoyote, kugombea
ukubwa, kugombea nafasi, kuoneana wivu, kuwa na uadui, uchonganishi, kutafuta
cheo, kumchukia mtu mwenye kila kitu, na kadhalika.
Wafilipi 2:3-4 “Msitende
neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu
na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo
yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.”
4.
Tamaa
za Dunia – Ni changamoto ya kutaka kujihusisha na dunia na anasa zake,
katika njia ambayo taratibu inaweza kumuondoa mtu katika kumcha Mungu, tunataka
kujihusisha na burudani zisizo za kiroho, vyama visivyo vya kiroho,
kusheherekea vitu kupita kiasi, tamaa ya kunywa pombe, kudhamiria kuchukia
watu, ushirikina, mawasiliano na pepo, kujiunga na vyama vya kishetani,
uangaliaji wa picha za ngono, kujifurahisha kwa sinema za ngono, majarida ya
ngono, picha za maumbile yenye kuvutia, na anasa nyinginezo
1Yohana 2:15-17 “Msiipende
dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba
hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na
tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na
dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya
Mungu adumu hata milele.”
Kwa hiyo vijana wawapo duniani,
wawapo ulimwenguni, au tuwapo duniani, au tuwapo ulimwenguni, pamoja na ufahamu
mzuri, na kuelimishwa vema njia ya Bwana, na pamoja na wokovu, na kumpenda
Mungu, na kumshinda shetani adui mmojawapo mkubwa tunayekabiliana naye ni mambo
ya mwili na tamaa za ujanani, hizi ni muhimu vijana wakajua namna wanavyoweza
kutiisha miili yao na kujinasua kutoka katika mtego huu mkubwa kwani tamaa hizi
zina athari zake.
Athari ya tamaa za ujanani
Tamaa za ujanani zinaathari kubwa
sana kiroho, zinaunda tabia na mfumo ambao unaanza kumuweka mtu mbali na Mungu
taratibu bila kuelewa na hatimaye mwisho kumnyima mtu huyo nafasi ya uzima wa
milele ambao Mungu ameukusudia, kimsingi Mungu anapokuokoa hakusudii hata
kidogo kwamba uukose uzima wa milele, lakini kupitia tamaa za ujanani, dunia na
shetani taratibu tamaa hizi zinafanya kazi ya wewe mwenyewe kujiondoa katika
mpango huo wa Mungu, kwa kudumaa kiroho, kwa kupoteza uadilifu, kwa kukukosesha
Amani, kwa kuharibu uhusiano wako na Mungu na hatimaye kukuharibia mpango wa
Mungu wa umilele
1. Kutengana na Mungu – tamaa za ujanani
zikitimizwa mara moja ainaanza kuharibu ukaribu wetu na Mungu, zinavunja
uhusiano wetu na Mungu, kwa hiyo hata kama wanadamu hawatuoni lakini sisi
wenyewe tunapoteza urafiki na uhusiano wa karibu na Mungu na kuwa adui wa
Mungu, jambo ambalo litapunguza au kuondoa kabisa neema za Mungu katika maisha
yetu na mwili unapata nguvu ya kututawala
Yakobo 4:4-6 “Enyi
wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila
atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu. Au mwadhani ya
kwamba maandiko yasema bure? Huyo Roho akaaye ndani yetu hututamani kiasi cha
kuona wivu? Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu
huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu.”
Mwanzo 39:7-9 “Ikawa
baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala
nami. Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui
kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi
mwangu.Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu cho
chote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose
Mungu? ”
2.
Kudumaa
kiroho – Tamaa za ujanani huchukua muda mrefu sana kupambana na uwezo wa
kijana kukua kiroho na kumfuata Yesu kwa ukamilifu, na matokeo yake
inasababisha udumavu wa Kiroho, na badala ya kukua kiroho Mwili (Sarx) yaani ile asili ya mwanadamu na
tamaa mbaya inakuwa na nguvu kuliko utawala wa kiroho na hivyo kuathiri tabia
na mwenendo wa Mkristo, anakuwa wa mwilini na anakosa makuzi ya kiroho. Mtu wa
mwilini anashindana na mtu wa rohoni na kusababisha udumavu wa kiroho.
1Wakorintho 3:1-3 “Lakini,
ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni,
bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika
Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza.
Naam, hata sasa hamkiwezi, kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya
mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya
mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu?”
Waebrania 5:11-14 “Ambaye
tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na ni shida kuyaeleza kwa kuwa
mmekuwa wavivu wa kusikia. Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati
mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya
Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. Kwa maana kila
mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga.Lakini
chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa
kupambanua mema na mabaya.”
Luka 8:14 “Na
zilizoanguka penye miiba ni wale waliosikia, na katika kuenenda kwao husongwa
na shughuli na mali, na anasa za maisha haya, wasiivishe lo lote.”
3.
Kukosa
Amani – Tamaa za ujanani zinapoyatawala maisha yetu hutujengea mashaka,
wasiwasi na woga na wakati mwingine kupoteza Amani, na kusinyaa kwa Imani yetu katika wokovu na
Mungu, Japo Mungu ni mkuu na anatujua umbo letu. Lakini tunaweza kuwa
na watu ambao wanaonekana kuwa wako vizuri, katika idara zote, wako mstari wa
mbele na wanaimba na kuabudisha vizuri lakini kwenye mioyo yao hawana Amani,
nimefanya kazi na vijana kwa muda mrefu na mara nyingi nilijiwa na vijana ambao
walikuwa na dhambi za siri, wamezidiwa na tamaa, na wanapiga punyeto
zinawakosesha Amani, Amani hii ni tofauti na ile wanayoitafuta katika zile
tamaa, Amani hii wanakuhumiwa na dhamiri au Roho wa Mungu kuwaonya kuwa
wanapoteza Amani na Mungu, kwa hiyo kumbe wakati mwingine uhusiano wetu na
Mungu unapokuwa umeingiliwa na kitu cha tofauti mwanadamu anapoteza amani na Mungu
wake, furaha ya Roho Mtakatifu inatoweka, furaha ya wokovu inatoweka,
unajihukumu na kujiona mwenye hatia na unakuwa na uzito wa Moyo.
Zaburi 51:1-12 “Ee
Mungu, unirehemu, Sawasawa na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako,
Uyafute makosa yangu. Unioshe kabisa na uovu wangu, Unitakase dhambi zangu.
Maana nimejua mimi makosa yangu Na dhambi yangu i mbele yangu daima.
Nimekutenda dhambi Wewe peke yako, Na kufanya maovu mbele za macho yako. Wewe
ujulikane kuwa una haki unenapo, Na kuwa safi utoapo hukumu.Tazama, mimi
naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatiani. Tazama,
wapendezwa na kweli iliyo moyoni; Nawe utanijulisha hekima kwa siri, Unisafishe
kwa hisopo nami nitakuwa safi, Unioshe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji,
Unifanye kusikia furaha na shangwe, Mifupa uliyoiponda ifurahi. Usitiri uso
wako usitazame dhambi zangu; Uzifute hatia zangu zote. Ee Mungu, uniumbie moyo
safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu Usinitenge na uso wako, Wala
roho yako mtakatifu usiniondolee. Unirudishie furaha ya wokovu wako;
Unitegemeze kwa roho ya wepesi”
4.
Mtego
wa uadilifu – Kila mtu duniania anavutiwa na watu waadilifu, na kila
mwanadamu anapenda kuwa na sifa ya uadilifu, hata hivyo kupitia tamaa za
ujanani shetani amewaharibiwa watu
wengi sana sifa ya uadilifu kwa kutumia tamaa yao na kuwaingiza katika mtego
huo, Daudi alikuwa ni mtu aliyependwa na Mungu, na alimpenda Mungu upeo, Lakini
aliwahi kuingia katika mtego wa uadilifu bila shaka wakati wa ujana wake,
kijana anapokosa uadilifu katika Israel alihesabika kama mojawapo ya watu
wapumbavu
2Samuel 13:10-14 “Amnoni
akamwambia Tamari, Kilete chakula chumbani, nipate kula mkononi mwako. Basi
Tamari akaitwaa mikate aliyoifanyiza, akamletea Amnoni nduguye mle chumbani.
Naye alipokwisha kuileta karibu naye, ili ale, Amnoni akamkamata, akamwambia,
Njoo ulale nami, ndugu yangu. Naye akamjibu, La, sivyo, ndugu yangu, usinitenze
nguvu; kwani haifai kutendeka hivi katika Israeli; usitende upumbavu huu. Nami
nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli.
Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa. Walakini
yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye,
akamtenza nguvu, akalala naye.”
Tamaa za ujana
zinaposhindikana kudhidhibiti maana yake tunaweza kufanya mambo ya kipumbavu na
yakaleta aibu katika maisha yetu Bwana atupe neema ya kuwa mbali na upumbavu
katika jina la Yesu Kristo wa Nazareth aliye hai, Ni muhimu kumuomba Mungu
atusaidie na kuihuisha miili yetu tupate kuwa safi.
Jinsi ya kukimbia tamaa za ujanani
Ni muhimu kufahamu kuwa maandiko
hayataadharishi tu kuzikimbia tamaa za ujanani, lakini vile vie yanatupa na
njia za namna ya kutoka, na njia hizo ni muhimu sana kwa kila mtu kuzizingatia
ili tuweze kuishi maisha ya ushindi.
2Timotheo 2:22 “Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na
imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi.”
Ziko mbinu kadhaa ambazo
maandikio yanatoa lakini leo nitazungumzia sana moja ya muhimu sana na
kuichambua kwa undani sana na yenyewe ina maswala kadhaa ya kufanya
Kuenenda kwa Roho.
Wagalatia 5:16-18 “Basi nasema, Enendeni
kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani
ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana,
hata hamwezi kufanya mnayotaka.Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria.”
Ni Muhimu kufahamu kuwa tamaa za
ujanani hazina tofauti na tamaa za mwili, na iko namna ambayo watu wa Mungu
tunapaswa kuifahamu ili tuweze kupata ushindi katika maisha ya kiroho na ili
tuweze kuwa na ufahamu katika jambo ninalotaka kulisema na kulifundisha hapa ni
muhimu kufahamu kuwa mwanadamu ana sehemu kuu tatu katika asili ya uumbwaji
wake kuna utatu katika uumbwaji wa mwanadamu na nataka kufafanua kama
ifuatavyo:-
a.
Soma
– Neno la kiyunani kwa kiingereza The
body, the living body, the wholeness of human being, It’s a biological body
Mwili wa kibailojia, mwili unaotokana na baba na mama
b.
Sarx
– Neno la kiyunani kwa kiingereza
Flesh, human body, earthly body, sinful human nature, Sarks refers to the human
way of interacting with and responding to the world. Hii ndio inatafasiriwa
kama mwili katika Kiswahili, mwili wa kibinadamu, mwili wa duniani, mwanadamu
wa asili mwenye dhambi, mwili huu ndio unaotusaidia kuelewa mambo na kuyatambua mambo na kuitikia mambo
tukiwa hapa duniani. Maandiko yanaposema enendeni kwa roho wala hamtayatimiza
kamwe mambo ya mwili inamaanisha Sarx.
Kwa kiibrania (Nephesh) kwa
Kiswahili Nafsi. Sarx inatawaliwa na
ufahamu Nafsi, kwa uwezo wa kuona, kusikia, kunusa, kuonja, na kuhisi kwa
kutumia ngozi, Mtu anapofanya dhambi kama ya zinaa anafanya juu ya mwili wake
wote ni huu ndio unaozungumzwa kwamba ukifanya zinaa inakamata nafsi,
inaunganisha nafsi
1Wakorintho 6:18 “Ikimbieni
zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye
zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.”
c.
Pneumatikos
– Neno la kiyunani kuhusu roho ya mwanadamu, kwa kiingereza Soul a part of human that is relating to
human spirit, a part of man which is akin to God, the part of human being that
belongs to the Divine, it is Higher than man but inferior to God, inaitwa,
roho, ni sehemu ya mwanadamu inayohusiana na roho ya mwanadamu, ni sehemu ya
mwanadamu au mtu ambayo ni ya thamani au ni ya juu zaidi kuliko mwili, na iko
chini ya Mungu mahusiano yote na ulimwengu war oho hufanyikia kwenya nafsi na
kuamua roho iwe upande gani wa Mungu au shetani.
1Wakorintho 2:14-15 “Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho
wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa
yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala
yeye hatambuliwi na mtu”.
Kwa hiyo Soma – ni mwili, Sarx ni
Nafsi na Pneumatikos ni roho, Soma
kukua kwake na kuishi kwake kunategemea chakula, wanga, protins, mafuta,
vitamin, kupumzisha mwili, kunywa maji ya kutosha, kuchukua mazoezi na
kuzingatia kanuni za kiafya na kadhalika, Nafsi kulishwa kwake kunategemeana na
maarifa, kusikia, kuona na yote unayoyaingiza kupitia milango ya fahamu, na roho kulishwa kwake kunamtegemea Mungu au
maswala yote ya ibada, unapoilisha Soma unastawisha uhai wa nafsi na roho,
unapoilisha nafsi unastawisha akili na roho, kusinyaa kwa roho kunategemeana na
unailisha nini roho yako au nafsi yako, kukua kwako kiroho kunategemeana na
unailisha nini nafsi yako na roho yako!
Zaburi 103:1-2 “Ee nafsi yangu, umhimidi
Bwana. Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu.Ee nafsi
yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote.”
Mathayo 4:4 “Naye akajibu akasema,
Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa
cha Mungu.”
Wakati mkate ulikuwa unahusu
mwili huu wa kawaida, “Rhēma” neno la Mungu ni chakula cha
mtu wa rohoni, shetani alipoona Yesu anamlisha sana mtu wa rohoni, na mtu wa
mwilini ana njaa alimshawishi afanye mkate ili kumlisha mtu wa mwilini kwa
sababu ana njaa, na Yesu alikuwa akimjibu shetani kuwa atendelea kumlisha mtu
wa rohoni sawa na ufunuo wa kiungu, kwa sababu mtu sio mwili tu bali mtu pia ni
roho sasa maandiko yanamanisha nini
2Timotheo 2:22 “Lakini zikimbie tamaa za
ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao
Bwana kwa moyo safi.”
Wagalatia 5:16-18 “Basi nasema, Enendeni
kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani
ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana,
hata hamwezi kufanya mnayotaka.Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria.”
Lakini zikimbie tamaa za ujanani – Neno zikimbie kwa kiyunani
linasomeka kama neno “Pheugō” linalosomeka kimatamshi fyoo-go, ambalo kwa kiingereza Vanish – to
shun or to disappear from sight, especially quickly, became invisible, kwa
Kiswahili usionekane, jiepushe, usijitokeze, usitokee, kabisa kwenye tamaa za
ujanani, usiache tamaa za ujanani zikachomoza, zima kabisa tamaa za ujanani,
kwa hiyo kukimbia huku kunakozungumzwa hapo, yalikuwa ni mausia ya Paulo mtume
kwa Timotheo kuhakikisha ya kuwa wakati wote haruhusu au asiruhusu tamaa za
ujanani kumshinda katika maisha yake, swala hili linauhusiano na kila mmoja
wetu halikuwa tu agizo kwa Timotheo sisi nasi kwa neno hilo tunaagizwa
kutokuruhusu tamaa za mwili kabisa katika maisha yetu, hii maana yake ni nini
ni pamoja na kujitia nidhamu, na kuuweza mwili (Sarx) na (Soma)
1Wathesalonike 4:3-5 “Maana haya ndiyo
mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati; kila mmoja wenu ajue
kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima; si katika hali ya tamaa mbaya,
kama Mataifa wasiomjua Mungu.”
Neno kuuweza katika kiyunani “Ktaomai” ambalo maana yake ni “possess” kuutawala mwili sasa katika
hali ya kawaida ukiulisha sana mwili roho itazimia na mwili utakuwa na nguvu na
utatimiza mapenzi ya mwili, na ukiilisha sana roho utaenenda kwa roho, sasa ni
namna gani mtu anaweza Kuendenda kwa Roho hilo nalo sio jambo jepesi, lakini
pia sio kazi yetu, ni kazi ya Mungu Roho Mtakatifu hata hivyo tunao wajibu wa
kufanya, hatuwezi kuutawala mwili kwa ukali
lakini tunaweza kuutawala mwili kwa neema ya Mungu kwa kuruhusu Roho
Mtakatifu atawale.
Wakolosai 2:20-23 “Basi ikiwa mlikufa
pamoja na Kristo mkayaacha yale mafundisho ya awali ya ulimwengu, kwa nini
kujitia chini ya amri, kama wenye kuishi duniani, Msishike, msionje, msiguse;
(mambo hayo yote huharibika wakati wa kutumiwa); hali mkifuata maagizo na
mafundisho ya wanadamu? Mambo hayo yanaonekana kana kwamba yana hekima, katika
namna ya ibada mliyojitungia wenyewe, na katika kunyenyekea, na katika
kuutawala mwili kwa ukali; lakini hayafai kitu kwa kuzizuia tamaa za mwili.”
Kutiisha huko hakumaanishi ya
kuwa sasa unatumia nguvu au ukali kuutawala mwili na badala yake unajiachia
katika uwepo wa Mungu Roho Mtakatifu ili akusaidie, uhai wa kiroho wa kila mkristo na kanisa kwa
ujumla unategemea sana uwepo wa Roho Mtakatifu na utendaji wake katika maisha
yetu, kwa bahati mbaya kanisa huwa linakazia ujazo wa Roho Mtakatifu, kunena
kwa lugha, Karama za Roho Mtakatifu huku wakisahau kabisa swala zima la
kuenenda kwa roho, yaani kuhakikisha kuwa Mungu Roho Mtakatifu anatuongoza na kutupa
msaada kila wakati na kila iitwapo leo katika maisha yetu tukiwa na yeye,
tunapofurahia neema juu ya neema maana yake neema ya wokovu na neema ile
inayotusaidia kuenenda katika Kristo, ushirika wetu wa kudumu na Roho wa Mungu
utatusaidia katika maisha yetu kuushinda mwili bila kutumia nguvu, ukiona
unapambana sana katika kushindana na dhambi wewe mwenyewe kwa miguvu yako uko
mwilini bado na bado uko chini ya sheria.
Wagalatia 5:16-18 “Basi nasema, Enendeni
kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani
ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana,
hata hamwezi kufanya mnayotaka.Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria.”
Sasa tunawezaje kuenenda kwa roho?
-
Ishi
kulingana na Neno la Mungu – Soma neno la Mungu na kulitafakari na kulitii,
Neno la Mungu ndilo dira yetu, katika kutembea na Mungu, tunapojifunza na
kulitafakari tunajiweka katika nafasi ya kuyajua mapenzi ya Mungu na wakati huo
tunampa Roho Mtakatifu nafasi ya kutuongoza katika kweli yote na haki yote,
Paulo alimtaka Timotheo kufuata haki, kufuata haki maana yake ni nini? Neno
haki katika Biblia linajitokeza karibu mara 92 na neno hilo kwa kiyunani ni Justfication au righteousness tunapomtii Mungu sawa na maagizo yake katika neno
tunafuata haki na hii inatuweka katika nafasi ya kutembelewa na Roho Mtakatifu
na kuanza kuongozwa na Roho na kuenenda kwa Roho.
Matthayo 3:13-17 “Wakati
huo Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe. Lakini
Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja
kwangu? Yesu akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo
kuitimiza haki yote. Basi akamkubali. Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara
akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu
akishuka kama hua, akija juu yake; na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema,
Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.”
Wakolosai 3:16 “Neno
la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na
kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa
neema mioyoni mwenu.”
-
Ishi kwa
Imani – Kudumisha uhusiano wetu na Mungu na kuishi kwa kumpendeza Mungu ni
pamoja na kuishi kwa Imani, tunaokolewa kwa Imani, na tunapaswa kudumisha
uhusiano wetu na Mungu kwa Imani, Pasipo Imani haiwezekani kumpendeza yeye,
watu wote waliokuwa mashujaa wa Imani na waliojaa Roho Mtakatifu walikuwa watu
walioishi kwa Imani, Paulo akamwambia Timotheo ukafuate haki, na imani, kwahiyo
kukimbia tamaa za dunia hii kunahitaji kuendelea kuamini na kuishi kwa Imani
Yohana 14:16-17 “Nami
nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele;
ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala
haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.”
Wagalatia 3:1-3 “Enyi
Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa
wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa? Nataka kujifunza neno hili moja
kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na
imani? Je! Mmekuwa wajinga namna hii? Baada ya kuanza katika Roho, mnataka
kukamilishwa sasa katika mwili? ”
Matendo 6:5 “Neno
hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa
imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na
Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia;”
Waebrania 11:6 “Lakini
pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima
aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.”
-
Ruhusu
hali ya kukua kiroho - Kusudi kuu la
kuitwa kwetu ni ili tumzalie Bwana matunda, tukiulisha mwili tutazaa matunda ya
mwili na kudumaa kiroho, tukilisha roho tutakomaa kiroho na kumzalia Bwana
matunda ya Roho, matunda ya roho ni Pamoja na upendo na amani Paulo Mtume akamwambia
Timotheo “Lakini
zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na Amani” hatuwezi
kuzaa matunda haya hasa la upendo na Amani
kama hatujakomaa kiroho!
Waefeso 4:11-15 “Naye
alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa
wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha
watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na
sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata
kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;
ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila
upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.
Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote,
yeye aliye kichwa, Kristo.”
Wagalatia 5:22-23 “Lakini
tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili,
uaminifu,upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.”
-
Uwe na
Ushirika – Hakuna jambo zuri duniani kama ushirika, ni katika ushirikia
ndipo tunapoweza kutiwa moyo hii ni kwa ushirika unaojitambua, tunasaidiana, na
kuwajibika kwaajili ya maisha ya kila mmoja, Paulo alimwambia Timotheo “Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate
haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo
safi”
Waebrania 10:24-25 “tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri;
wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali
tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.”
-
Enendeni
kwa Roho - hatua zote hapo juu zinatuandaa kuja katika eneo muhimu ambalo
kuenenda kwa Roho, ni muhimu kufahamu kuwa neno enendeni linasomeka katika lugha
ya kiyunani kama “Peripateō” kwa kiingereza go be Occupied ambalo limetumika mara 93 katika biblia ya KJV “be busy” au Be Active, au be used Kiswahili
tungesema uwe bize, uwe katika utendaji, ushughulishwe wakati wote au uingie
kazini na Roho Mtakatifu, tumika naye, hali hii huchochea moto wa utendaji wa
Roho Mtakatifu usizimike, Roho wa Mungu huonekana na kutenda kazi
tunapojishughulisha naye kila wakati na kila siku, kama umechunguza sana kwa
makini watumishi wengi wa Mungu wanaoshughulika na kufanya kazi na Roho
Mtakatifu huwa hawapoi na huwa ni vigumu kuona matunda ya mwili yakizaliwa,
Daudi alipoacha kwenda vitani ndipo, alipoona mwanamke anayeoga na kuvutiwa
naye aku kumtamani, na tamaa za ujanani zikachukua nafasi.
Luka 4:1 “Na
Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho
muda wa siku arobaini nyikani,”
Luka
4:14 “Yesu akarudi kwa nguvu za Roho, akenda
Galilaya; habari zake zikaenea katika nchi zote za kandokando.”
Matendo 4:8-10 “Ndipo
Petro, akijaa Roho Mtakatifu, akawaambia, Enyi wakubwa wa watu na wazee wa
Israeli, kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu,
jinsi alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina
la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua
katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye
jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la
pembeni.”
Matendo 6:8-10 “Na
Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika
watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la
Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na
kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo
Roho aliyesema naye”
Hitimisho:
Kutembea na Roho
Mtakatifu na kuwa karibu naye siku zote, kusikia uongozi wake sio kazi rahisi,
lakini ndio njia yenye thawabu ya kuutunza wokovu wetu na kumzalia yeye matunda
zaidi ya yote inatupa ushindi na kutufanya kuishi kwa Amani na furaha kwa
utimilifu wake, wakati huo hatutayaona tena matendo ya mwili yakiwa mwiba na
usumbufu mkubwa katika maisha yetu, tutaweza kuzikimbia tamaa za ujanani bila
kutumia nguvu wala kupambana na dhambi katika miili yetu, mwili hautatutawala
wala hautatuvuta, mtu wa mwilini atazikwa kabisa na mtu wa Rohoni atakuwa na
nguvu, wachungaji na walimu wa neno la Mungu tukiwaelekeza watu kuhusu kutembea
na Roho, kuongozwa na roho kuenenda kwa roho, hatutakuwa na kazi ya kukemea dhambi,
kutenga, kutishia kujifanya wakali wakati wewe na mimi sio Mwokozi, kuhukumu
watu, kote kutamalizwa kwa kuwaambia watu kwa urahisi tu hivyo enendeni kwa
Roho, wala hamtayatimiza KAMWE mambo
ya mwili Neno kamwe kiyunani “ou mē” Kiingereza “Not at All” maana yake haitakuja
itokee kamwe kwa hiyo suluhu ya dhambi ni Roho Mtakatifu ambaye tatizo kubwa
watu hawamtumii, katika maisha yao bali wanajaa, wananena, wana karama kisha
inaishia hapo tu ni Muhimu kujiongeza.
Warumi 8:5-10 “Kwa
maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho
huyafikiri mambo ya roho. Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni
uzima na amani. Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana
haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. Wale waufuatao mwili hawawezi
kumpendeza Mungu. Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi
hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho
wa Kristo, huyo si wake.Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa
sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya haki.”
Bwana ampe neema
kila mmoja wetu, aweze kuelewa somo hili na kufaidika na maswala ya rohoni
sawasawa na mapenzi ya Mungu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, naomba
kwaajili ya wote ambao mwili unawasumbua Mungu ukapate kuwafunulia na kuwasaidia
ili mwili na tamaa za ujanani zisiwasumbue tena katika jina la Yesu Kristo
mwana wa Mungu aliye hai ameen!
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni