Kumbukumbu 8:11-16 “Jihadhari, usije
ukamsahau Bwana, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na
sheria zake, ninazokuamuru leo. Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na
kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; na makundi yako ya ng'ombe na kondoo
yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu
ulicho nacho kitakapoongezeka; basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana,
Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa;
aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na
nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba
mgumu,aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako; apate kukutweza,
apate kukujaribu, ili kukutendea mema mwisho wako.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa pamoja na
kujifunza neno la Mungu sana katika makanisa yetu, katika vyuo vya biblia na
kwa kujitoa sisi wenyewe kwa kuisoma biblia wakati mwingine kila mwaka na
wakati mwingine kila baada ya miezi sita na kuisoma wakati wa maandalizi ya neno,
na kuhubiri na kufundisha na hata kuhojiana
na wenzetu bado ni Muhimu kufahamu kuwa iko shule ya Mungu au shule ya Roho
Mtakatifu ambayo kwa kawaida Mungu hutupitisha kabla ya kututumia na kutubariki
katika viwango vya juu, wakati wote Mungu anapotaka kukufundisha njia zake
huwapeleka watumishi wake katika chuo chake kikuu ambacho leo nimekipa jina
chuo kikuu cha jangwani angalia
Luka 1:76-80 “Nawe, mtoto, utaitwa nabii
wake Aliye juu, Kwa maana utatangulia mbele za uso wa Bwana umtengenezee njia
zake; Uwajulishe watu wake wokovu, Katika kusamehewa dhambi zao. Kwa njia ya
rehema za Mungu wetu, Ambazo kwa hizo mwangaza utokao juu umetufikia,
Kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti, Na kuiongoza miguu yetu kwenye
njia ya amani. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani
hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli.”
Luka 4:1-2 “Na Yesu, hali amejaa Roho
Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini
nyikani, (Jangwani) akijaribiwa na Ibilisi. Na siku hizo alikuwa hali kitu;
hata zilipotimia, aliona njaa.”
Tunasoma kuwa Mungu aliwaongoza
watoto wake wana wa Israel jangwani, lakini sio hivyo tu Yohana mbatizaji moja
ya manabii waliokuwa na nguvu za Mungu za kupita kawaida alikaa jangwani siku
zote za maisha yake mpaka alipojitokeza kuhubiria watu, Lakini Kristo Yesu
Mwenyewe kabla ya kuanza kuhudumia watu aliongozwa jangwani. kwanini jangwani,
kwa nini jangwani? Jangwani ni shule ya Roho Mtakatifu, jangwani kuna chuo,
jangwani ni chuo kikuu cha maandalizi ya watumishi wa Mungu, kama hujapitishwa
jangwani nidhamu yako katika kumtumikia Mungu, kumtegemea na kumtumikia kwa
ufasaha inaweza kuwa na upungufu, leo tutachukua Muda basi kujifunza kwa kina
na mapana na marefu somo hili muhimu Chuo kikuu jangwani kwa kuzingatia
vipengele vinne vifuatavyo:-
·
Umuhimu wa kupitishwa chuo kikuu jangwani.
·
Mifano ya watumishi wa Mungu waliopitia chuo
kikuu jangwani.
·
Mambo muhimu utakayopitia katika chuo kikuu
Jangwani.
·
Chuo kikuu jangwani.
Umuhimu wa kupitishwa chuo kikuu jangwani
Jangwa linajitokeza na kutajwa
katika maandiko mara kadhaa, kama moja ya sehemu yenye matukio muhimu sana
yanayohusiana na Mungu na watu wake, mara baada ya Mungu kuwaokoa wana wa
Israel kutoka katika inchi ya utumwa Misri moja kwa moja tunaona hawapeleki
katika inchi ya maziwa na asali aliyokuwa amewaahidi, na badala yake
anawapeleka katika jangwa ambalo walilitembea kwa miaka kama 40 hivi, kwa nini jangwani?
kwa ujumla swala la kupita jangwani halionekani kuwa ni lenye kuvutia au
kupendeza hata kidogo, lakini kwanini watu wapelekwe jangwani? Jangwani ni
mahali ambapo Mungu alikuwa na makusudi na watu wake na Mungu alikuwa na mpango
mwema wa kujifunua kwao na kuwafundisha watu wake, Musa anaeleza kuwa halikuwa
jangwa la matumaini, hakukuwa na kivuli, hakukuwa na maji, hakukuwa na chakula,
jangwa lilikuwa na nyoka wenye sumu (Nyoka wa Moto) kulikuwa na nge, jangwa
lina joto kali sana mchana, jangwa lina baridi kali sana usiku, jangwani huwezi
kwenda kwa mwendo wa haraka, jangwani ni rahisi kupotea, jangwani hakuna
makaburi, Musa analiita jangwa kubwa lenye kutisha, jua kali, ukavu, upweke,
moyo na akili zinachoka na hata kuinua hatua jangwani kunahitaji uwe na moyo
mkuu kwanini jangwani? Ni chuo kikuu cha Mungu ni shule ya Roho wa Mungu kwetu!
Ni shule Muhimu yenye kutengeneza nidhamu ya hali ya juu kwa watumishi wa
Mungu, ni shula ya huduma ni shule ya ukomavu.
Kumbukumbu 8:11-16 “Jihadhari, usije
ukamsahau Bwana, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na
sheria zake, ninazokuamuru leo. Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na
kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; na makundi yako ya ng'ombe na kondoo
yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu
ulicho nacho kitakapoongezeka; basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana,
Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa;
aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na
nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba
mgumu,aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako; apate kukutweza,
apate kukujaribu, ili kukutendea mema mwisho wako.”
Kaka zangu na dada zangu, hakuna
mtu anayependa kuishi maisha ya taabu, wala ya umasikini, wala maisha
yasiyofurahisha, kila mtu anapenda raha na mteremko, kwa hiyo kila mmoja
anakwepa kupita kwenye mateso shida na maumivu, wakati mwingine tunafurahia
sana wengine wakipita katika mapito na tunaweza kujifikiri kuwa labda sisi ni
maalumu sana kuliko wao kwa sababu hatujalionja jangwa, lakini kama unaishi
katika njia hii na utumishi huu na kama Mungu anakupenda ni muhimu ujue kuwa
Mungu ataruhusu maisha yako yapite jangwani, ambako utakumbana na upweke,
utakutana na ukavu, utakutana na nyoka, nge, njaa, kiu, na utachoka, utachoka
akili mwili na roho na utahisi hakuna uhai, utapoteza marafiki na wakati
mwingine utachagua kufa kuliko kuishi, jangwa halionyeshagi matumaini hata siku
moja, Mungu hulitumia jangwa kutunyoosha watu wake, kutufundisha, jangwani ni
chuo cha mafunzo, jangwani ni chuo cha unyenyekevu, jangwani ni chuo cha utii
kwa hiyo kama kuna mapito unayapita umelia, umeomba na hakuna kitu kinatokea na
huoni msaada wowote na unapoteza matumaini ujue ya kuwa hauko pake yako na mkuu
wa chuo yuko pamoja nawe, programu zote na kozi anazotaka uzipitie anazo yeye
kumbuka ni Mungu ndiye anayekusudia upite katika njia hiyo yeye mwenyewe,
uelewa wako, utii wako na unyenyekevu wako ndio utakaokusaidia kumalizo chuo
kikuu jangwani kwa ufanisi mkubwa huku ukimtukuza Mungu kwa wema wake. Kwa hiyo
maana yake ni nini? Maana yake ni kuwa yako mapito mengine ambayo Mungu ndiye
anayekuwa amekusudia upite na ndiye mwenye programu ya mateso hayo, ili
kukufanya uwe mwenye nidhamu.
Kutoka 13:17-18 “Ilikuwa hapo Farao
alipokwisha kuwaacha watu hao waende zao, Mungu hakuwaongoza kwa njia ya nchi
ya Wafilisti, ijapokuwa ilikuwa ni ya karibu; maana Mungu alisema, Wasije
wakaghairi watu hawa hapo watakapokutana na vita, na kurudi Misri; lakini Mungu
akawazungusha hao watu kwa njia ya bara kando ya Bahari ya Shamu; wana wa
Israeli wakakwea kutoka nchi ya Misri hali wamevaa silaha.”
Hakuna mtu au mtumishi wa Mungu
au mwana wa Mungu atakayepita jangwani kwa bahati mbaya, liko kusudi kubwa sana
ambalo ni la muhimu sana la kupitishwa jangwani, wayahudi wanapolitaja neno
jangwa huwa wanatumia msamiati ambao una maana ya ndani sana kuliko jangwa
lenyewe katika lugha ya kiibrania neno Jangwani ambalo limetumiwa mara nyingi
zaidi ni neno MIDHBAR ambalo maana
yake ni Jangwani au nyikani na neno la kibrania linalokaribiana na hilo ni MEDABER ambalo lina asili moja na la jangwani
ambalo kimsingi halikuwa na herufi za kati kati MDBR neno hili ndio limezaa maneno hayo mawili MIDHBAR ambalo maana yake Jangwa na MEDABER
maana yake kwa kiingereza to Speak, yaani
kuzungumza, au kusikia, kwa hiyo kwa waebrania mtu anapoongozwa na Mungu kwenda
jangwani ni ili akapate kuisikia sauti ya Mungu, sawa kabisa na kwenda chuoni
kumsikiliza Mwalimu na ndio maana somo hili nikaliita chuo kikuu jangwani, kwa nini kwa sababu ni eneo ambalo
Mungu hukupeleka ili upate kumsikiliza yeye, kwa hiyo kila aliyepelekwa
jangwani hakupelekwa si kama aliyepotea tu au kujikuta uko jangwani kwa bahati
mbaya hapana unapokuwa jangwani maana yake Mungu anataka umsikilize na
utamsikilizia wapi ni eneo ambalo utainua mikono kuhitaji msaada wake na sio
kwingine ni jangwani, Ndugu hapo unapopita au ulikowahi kupitia ni jangwani na
Mungu anamakusudi na wewe hivyo kubali kupita katika shule unayoipitia ili uweze kuhitimu vema utakapohitimu
kutoka katika chuo hiki utamcha Mungu, utakuwa mnyenyekevu, na utayajua matendo
makuu ya Mungu, Jangwani sio lazima liwe jangwa halisi, lakini ni njia ngumu za
Mungu anazoruhusu uzipitie ili kwa nia njema akurekebishe ili kukuleta kwenye
Baraka kubwa anazozikusudia. Na jwangwani sio lazima uisikie sauti ya Mungu
moja kwa moja la hasha jangwa lenyewe linasema, lina sauti linafundisha, ukiwa
mwanafunzi mzuri utaisikia sauti ya Mungu kwa upole sana ikisema na wewe na
kukufunza.
Kumbukumbu 8:1-6 “Amri hii ninayokuamuru
leo mtaishika kuitenda, mpate kuishi na kuongezeka, na kuingia katika nchi ile
ambayo Bwana aliwaapia baba zenu; nanyi mtaimiliki. Nawe utaikumbuka njia ile
yote Bwana, Mungu wako aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze,
kukujaribu kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo.
Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba
zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali
huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana. Mavazi yako hayakuchakaa,
wala mguu wako haukuvimba, miaka hiyo arobaini. Nawe fikiri moyoni mwako, ya
kuwa kama vile baba amrudivyo mwanawe, ndivyo Bwana, Mungu wako,
akurudivyo.Nawe uzishike amri za Bwana, Mungu wako, upate kwenda katika njia
zake, na kumcha.”
Mifano ya watumishi wa Mungu waliopitia chuo kikuu jangwani
1. Hajiri – Alikuwa akipitia changamoto
katika nyumba ya bibi yake yaani Sara baada ya kuwa na ujauzito Kupitia
Ibrahimu, mateso yalipomuelemea aliamua kikimbia, na kujikuta jangwani huko hali
yake ilikuwa ngumu na akaelemewa na huzuni, malaika wa Bwana akamtokea na
kumtia moyo na kumuelezea hali aliyo nayo na kumtaka arudi kwa bibi yake,
lilikuwa jambo la busara kwa wakati ule kwani alikuwa na mtoto wa Ibrahimu
tumboni mwake, Mungu alijifunua kwake na akamjua Mungu kama Mungu aonaye
kwanini kwa sababu aliyaona mateso yake, akaliitia jina la Bwana huko. Hajiri
alikuwa akisikia habari za Mungu katika nyumba ya Ibrahimu na Sara lakini
hakuwahi kumuona Mungu akijihusisha na maisha yake Binafsi, siku alipokimbilia
Jangwani alimjua Mungu kwa njia binafsi na kumtambua kama Mungu aonaye!
Nimemwona yeye anionaye alisema Hajiri, sio hivyo tu kumbuka neno lile la
malaika wa Bwana rudi kwa bibi yako ukanyenyekee maana yake ni nini Hajiri
alikuwa na kiburi, malaika wa bwana hakumwambia una kiburi wewe una majivuno humtii bibi yako badala yake
alimwambia rudi kwa bibi yako ukanyenyekee jangwa lilimfunza Hajiri kwenda kuwa
mnyenyekevu angalia
Mwanzo 16: 1-13
“Basi Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye
alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri.Sarai akamwambia Abramu, Basi
sasa, BWANA amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata
uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai. Sarai mkewe Abramu akamtwaa
Hajiri Mmisri mjakazi wake, baada ya kukaa Abramu katika nchi ya Kanaani miaka
kumi, akampa Abramu mumewe, awe mkewe. Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata
mimba. Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bibi yake alikuwa duni machoni
pake. Sarai akamwambia Abramu, Ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa
mjakazi wangu kifuani mwako, naye alipoona kwamba amepata mimba, mimi nimekuwa
duni machoni pake. BWANA na ahukumu kati ya mimi na wewe. Naye Abramu
akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema
machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake. Malaika wa
BWANA akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika
njia ya kuendea Shuri. Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi,
nawe unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai.
Malaika wa BWANA akamwambia, Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono
yake. Malaika wa BWANA akamwambia, Hakika nitauzidisha uzao wako, wala
hautahesabika kwa jinsi utakavyokuwa mwingi. Malaika wa BWANA akamwambia,
Tazama! Wewe una mimba, utazaa mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake
Ishmaeli, maana BWANA amesikia kilio cha mateso yako. Naye atakuwa kama
punda-mwitu kati ya watu, mkono wake utakuwa juu ya watu wote na mkono wa watu
wote utakuwa juu yake, naye atakaa mbele yao ndugu zake wote. Akaliita jina la
BWANA aliyesema naye, Wewe U Mungu uonaye, kwani alisema, Hata hapa nimemwona
yeye anionaye? ”
2. Hajiri na Ishmael – Hajiri na mwanae Ishamel walifukuzwa tena
katika nyumba ya Ibrahimu kwa maagizo ya Sara kwa sababu ya changamoto kadhaa
zilizojitokeza, hata hivyo walipotoka kwa bahati walipotea jangwani, maji
yaliwaishia na hali ya kifo ndiyo iliyokuwa ikiwakabili, Mungu aliye mwingi wa
rehema na asiye na upendeleo, aliwatokea na kuokoa maisha ya kijana na mama
yake alitiwa moyo na Mungu aliahidi kumfanya kijana kuwa taifa kubwa na Mungu
akawa pamoja na yule kijana, Hivyo Ishmael naye akamjua Mungu wa baba yake
katika namna ya kipekee, alimjua kuwa ni Mungu anayejihusisha na maisha ya watu
wake bila upendeleo, Ni Mungu aliyesababisha maji jangwani, Ni Mungu aliyewapa
kisima cha maji, Ni Mungu aliyemfundisha Ishmael kushika upinde na kuwa mpiga
upinde hodari, leo hii inchi ya Ishamel ina visima vikubwa vya mafuta na
vinawapa utajiri mkubwa sana na mafanikio makubwa sana Jangwa limekuwa Mwalimu
mzuri wa maisha yao.
Mwanzo 21:14-20
“Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate
na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu;
naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba. Yale maji yakaisha katika
kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja. Akaenda akakaa akimkabili,
mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa;
naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia. Mungu akasikia sauti ya
kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini,
Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko. Ondoka,
ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa
kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza
kiriba maji, akamnywesha kijana. Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye
akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde.”
3. Musa - Baada ya kumkimbia Farao, kule Misri baada
ya kuua raia wake, Musa alikimbilia katika jangwa la Midian na kuishi huko kwa
miaka 40, Huko ndiko alikoisikia sauti ya Mungu akisema naye na kumtaka
kubadilika (Kuvua viatu vyake) na
kumtuma ili aende kuwaongoza wana wa Israel ambao aliwaongoza jangwani kwa
miaka 40, Safari ya jangwani kwa Musa ilikuwa ni maandalizi makubwa ya
kumuandaa Musa kwaajili ya wana wa Israel ukombozi wao na ujuzi wa jangwa lile
lakini kubwa zaidi kumjua Mungu na kujifunza utii kwa sheria zake, Jangwa
lilimfundisha Musa kuwa mpole yaani mnyenyekevu sana, Lilimfundisha Musa
kuutafuta uso wa Mungu, lilimuweka mbali na starehe za ikuu, lilimuweka mbali
na ndugu zake, lilimuweka ugenini, lilimfundisha upweke, lilimnyoosha na kumfanya
kuwa mvumilivu na mtumishi wa Mungu wa ngazi ya juu na viwango vikubwa.
Kutoka 2:14-15
“Yule akasema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu
wetu, na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri?
Musa akaogopa, akasema, Kumbe! Jambo lile limejulikana. Basi Farao alipopata
habari, akataka kumwua Musa; lakini Musa akakimbia mbele ya Farao, akakaa
katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na kisima.”
Kutoka 3:1-8 “Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro
mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka
mlima wa Mungu, hata Horebu. Malaika wa BWANA akamtokea, katika mwali wa moto
uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto,
nacho kijiti hakikuteketea. Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya
makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei. BWANA alipoona ya kuwa amegeuka ili
atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa!
Akasema, Mimi hapa. Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni
mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu. Tena akasema, Mimi ni
Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa
akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu. BWANA akasema, Hakika
nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa
sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili
niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema,
kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na
Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi.”
4. Wana wa Israel - Mungu aliwaongoza wana
wa Israel jangwani kwa muda wa miaka 40, baada ya kuwa amewaokoa kutoka Misri,
kipindi hiki hakikuwa kipindi rahisi, kilikuwa ni kipindi kigumu na kilikuwa
kama adhabu kali kwa wana wa Israel, kilikuwa ni kipindi cha kuwajaribu,
kuwafundisha na kuwarudi, walikutana na wakati mgumu na Mungu peke yake akawa
ndio jibu la changamoto zao zote, huko aliwapa sheria, aliwafundisha na kuwatunza
la kuwaadhibu walipokosea, Mungu alikuwa akijitafutia taifa lenye nidhamu na
ustaarabu wa hali ya juu, taifa lenye akili, na kuwaandaa kabla ya kuingia
katika inchi ya mkanaani.
Hesabu 14:33-34
“Kisha watoto wenu watakuwa wachungaji jangwani
muda wa miaka arobaini nao watauchukua mzigo wa uasherati wenu, hata mizoga
yenu itakapoangamia jangwani.Kwa hesabu ya hizo siku mlizoipeleleza ile nchi,
yaani, siku arobaini kila siku kuhesabiwa mwaka, mtayachukua maovu yenu, ndiyo
miaka arobaini, nanyi mtakujua kufarikana kwangu.”
Kumbukumbu
8:2-6 “Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu
wako aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu
kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo. Akakutweza,
akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako
hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali
huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana. Mavazi yako hayakuchakaa,
wala mguu wako haukuvimba, miaka hiyo arobaini. Nawe fikiri moyoni mwako, ya
kuwa kama vile baba amrudivyo mwanawe, ndivyo Bwana, Mungu wako, akurudivyo.
Nawe uzishike amri za Bwana, Mungu wako, upate kwenda katika njia zake, na
kumcha.”
5. Daudi – Baada ya kupakwa mafuta na
kufanya mambo makubwa ikiwa ni pamoja na kumuua Goliath maisha ya Daudi yalibadilika
alianza kukimbia kutoka jangwa moja hadi jangwa lingine na kuishi katika
mapango akimkimbia Sauli aliyekuwa na kusudi la kumuua, moyo wake ulishuka na aliishi maisha ya chini sana ya nyikani
lakini kule nyikani alijifunza kumtegemea Mungu na kujenga ukaribu mkubwa sana
na Mungu, aliandika mashairi mengi ya kumsifu Mungu na kumuimbia Mungu akiamini
kuwa Mungu anamsikia, alijifunza kumuomba Mungu na kumsikiliza Mungu pia alijifunza kumsifu na kumtegemea yeye,
Jangwa liliendelea kutengeneza maisha ya unyenyekevu na moyo wa rehema hata
ingawa alikuja kufanya dhambi, Moyo wake ulibaki kuwa mwelekevu kwa Mungu akijaa
toba na Mungu alimsifu Daudi kama mtu wa kipekee sana. Aliyeupendeza moyo.
1Samuel
23:14-15 “Basi Daudi alikuwa akikaa nyikani ngomeni,
akakaa katika nchi ya milima milima kwenye nyika ya Zifu. Naye Sauli alikuwa
akimtafuta kila siku, lakini Mungu hakumtia mikononi mwake. Daudi akaona ya
kwamba Sauli ametoka nje ili kutafuta roho yake; naye Daudi akawako katika
nyika ya Zifu, huko Horeshi”
6. Eliya - Inaonekana wazi kuwa alitokea jangwani,
hasa kwa sababu mtindo wa maisha yake na huduma yake inafanana sana na ya
Yohana mbatizaji, lakini baada ya kutenda mambo makubwa inaonekana alimkimbia
malkia katili aliyeitwa Yezebeli aliyekuwa ameyatishia maisha yake, kule
jangwani akiwa na hofu ya kuuawa na mwanamke huo katili, hata hivyo alipata
somo, Mungu alimtunza na kumpa chakula, na maji, alitiwa nguvu ya kutembea siku
40 bila kula wala kunywa na mwisho
aliisikia sauti ya Mungu, ikimuelekeza mambo ya kufanya, lakini pia alijifunza
kuwa nabii bora hakuwa yeye peke yake, wala wacha Mungu hakuwa ni yeye tu,
Mungu anawajua walio wake na waliojificha kwaajili yake ambao mioyo yao
haijamuabudu baali, jangwa liliondoa kiburi cha Nabii huyu aliyewashitaki watu
wa Mungu na kudhani ya kuwa yeye ni wa kipekee, Kwa huruma zake Mungu
hakusikiliza maombi yake ya kutaka kufa na badala yake alimnyakua kwake
Mbinguni. Jangwa lilimfundisha kuwa Mungu ana watu wengi, Jangwa lilimfundisha
kuwa yeye sio peke yake anayemcha Mungu, jangwa lilimfundisha kuwa Elisha
anaweza kubwa nabii bora kuliko yeye, Jangwa lilimfundisha kuwa hapaswi
kujivuna, jangwa lilimfudhisha kuwa Mungu hapatakani kwenye mikwara na sauti
zenye kelele nyingi, alijifunza kuwa sauti ya Mungu huja katika hali ya
utulivu, Jangwa lilimfundisha kuwa hapaswi kuwashitaki au kuwahukumu wengine
hata kama ni dhaifu, jangwa, jangwa, jangwa ni shule ni chuo cha Roho wa Bwana.
1Wafalme
19:1-18 “Ndipo Yezebeli akampelekea Eliya mjumbe,
kusema, Miungu wanifanyie hivyo na kuzidi, nisipokufanya roho yako kesho,
panapo wakati huu, kama roho ya mmojawapo wa hao.Naye alipoona hayo, aliondoka,
akaenda aihifadhi roho yake, akafika Beer-sheba, mji wa Yuda, akamwacha
mtumishi wake huko. Lakini yeye mwenyewe akaendelea katika jangwa mwendo wa
siku moja, akaenda akaketi chini ya mretemu. Akajiombea roho yake afe, akasema,
Yatosha; sasa, Ee Bwana, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba
zangu. Naye akajinyosha akalala chini ya mretemu; na tazama, malaika akamgusa,
akamwambia, Inuka, ule. Akatazama, kumbe! Pana mkate umeokwa juu ya makaa, na
gudulia la maji, kichwani pake. Akala, akanywa, akajinyosha tena. Malaika wa
Bwana akamwendea mara ya pili, akamgusa, akasema, Inuka, ule; maana safari hii
ni kubwa mno kwako. Akainuka, akala, akanywa, akaenda katika nguvu za chakula
hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu, mlima wa Mungu.
Akafika kunako pango, akalala ndani yake. Na tazama, neno la Bwana likamjia,
naye akamwambia, Unafanya nini hapa, Eliya? Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa
ajili ya Bwana Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano
yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami
nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu, waiondoe. Akasema, Toka,
usimame mlimani mbele za Bwana. Na tazama, Bwana akapita; upepo mwingi wa nguvu
ukaipasua milima, ukaivunja-vunja miamba mbele za Bwana; lakini Bwana hakuwamo
katika upepo ule; na baada ya upepo, tetemeko la nchi; lakini Bwana hakuwamo
katika lile tetemeko la nchi; na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto;
lakini Bwana hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto sauti ndogo, ya
utulivu. Ikawa, Eliya alipoisikia, alijifunika uso wake katika mavazi yake,
akatoka, akasimama mlangoni mwa pango. Na tazama, sauti ikamjia, kusema,
Unafanya nini hapa, Eliya? Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya Bwana,
Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na
kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi
peke yangu; nao wanitafuta roho yangu waiondoe. Bwana akamwambia, Enenda, urudi
njia ya jangwa la Dameski; ukifika, mtie mafuta Hazaeli awe mfalme wa Shamu. Na
Yehu mwana wa Nimshi mtie mafuta awe mfalme wa Israeli; na Elisha mwana wa
Shafati wa Abel-Mehola mtie mafuta awe nabii mahali pako. Na itakuwa
atakayeokoka na upanga wa Hazaeli, Yehu atamwua; na atakayeokoka na upanga wa
Yehu, Elisha atamwua. Pamoja na hayo nitajisazia katika Israeli watu elfu saba,
kila goti lisilomwinamia Baali, na kila kinywa kisichombusu.”
Warumi 11:1-4 “Basi, nauliza, Je! Mungu aliwasukumia mbali watu wake?
Hasha! Kwa kuwa mimi nami ni Mwisraeli, mmoja wa wazao wa Ibrahimu, mtu wa
kabila ya Benyamini. Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali.
Au hamjui yale yaliyonenwa na maandiko juu ya Eliya? Jinsi anavyowashitaki
Waisraeli mbele za Mungu, Bwana, wamewaua manabii wako, wamezibomoa madhabahu
zako, nami nimesalia peke yangu, nao wananitafuta roho yangu. Lakini ile jawabu
ya Mungu yamwambiaje? Nimejisazia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali.”
7. Yohana mbatizaji – Ni kijana aliyekulia
jangwani na alitokea jangwani akihubiri habari za toba na kukaribia kwa ufalme
wa Mungu, jangwa lilimuandaa kihuduma na akaiva kweli kweli, lipewa sauti kubwa
na ya kipekee, alipewa ujumbe mzito kwa watu na mahubiri yaliyonyooka
yanayoashiria kuwa alitoka akiwa na nidhamu kubwa sana na ya hali ya juu, Yesu
anamsifia Yohana mbatizaji kuwa katika uzao wa Mwanamke hakuna aliyemzidi huyu
jamaa, kwanini kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye katika maisha yake ya
kujikana huko jangwani!
Luka 1:76-80 “Nawe, mtoto, utaitwa nabii wake Aliye juu, Kwa maana
utatangulia mbele za uso wa Bwana umtengenezee njia zake; Uwajulishe watu wake
wokovu, Katika kusamehewa dhambi zao. Kwa njia ya rehema za Mungu wetu, Ambazo
kwa hizo mwangaza utokao juu umetufikia, Kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli
wa mauti, Na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani. Yule mtoto akakua,
akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa
Israeli.”
Mathayo 3:1- 5
“Siku zile aliondokea Yohana Mbatizaji akihubiri
katika nyika ya Uyahudi, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni
umekaribia. Kwa sababu huyo ndiye aliyenenwa na nabii Isaya, akisema, Sauti ya
mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake. Naye
Yohana mwenyewe alikuwa na vazi lake la singa za ngamia, na mshipi wa ngozi
kiunoni mwake; na chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu.Ndipo walipomwendea
Yerusalemu, na Uyahudi wote, na nchi zote za kandokando ya Yordani;”
Luka 7:24-28 “Basi, wajumbe wa Yohana walipokwisha ondoka, alianza
kuwaambia makutano habari za Yohana, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini?
Unyasi ukitikiswa na upepo? Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa
mavazi mororo? Jueni, watu wenye mavazi ya utukufu, wanaokula raha, wamo katika
majumba ya kifalme. Lakini, mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? Naam, nawaambia,
na aliye zaidi ya nabii. Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, namtuma mjumbe
wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako mbele yako. Nami
nawaambia, Katika wale waliozaliwa na wanawake hakuna aliye mkuu kuliko Yohana;
lakini aliye mdogo katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko yeye.”
8. Bwana Yesu - Aliongozwa na Roho Mtakatifu kwenda
jangwani akiwa amefunga kwa siku 40 huko alijaribiwa na shetani, jangwa
lilikuwa ni sehemu ya maandalizi ya huduma, na kipimo cha kujitambua kwake,
alishinda majaribu yote na Mungu alimtia nguvu na kumuandaa tayari kwa huduma
ya hadharani, uweza wa Roho Mtakatifu juu yake, maombi ya kufunga na kuomba,
utii wa maandiko, na ujuzi wake wa kuyatumia maandiko kwa usahihi ulimpa
ushindi mkubwa kutoka jangwani na akarudi hali amejaa Roho Mtakatifu tayari kwa
huduma
Mathayo 4:1-11
“Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili
ajaribiwe na Ibilisi. Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona
njaa. Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe
haya yawe mikate. Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu,
ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. Kisha Ibilisi akamchukua
mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe
Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na
mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Yesu
akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako. Kisha Ibilisi
akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na
fahari yake, akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia. Ndipo Yesu
alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu
wako, umwabudu yeye peke yake. Kisha Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja
malaika wakamtumikia.”
Luka 4:13-15 “Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda
zake kwa muda. Yesu akarudi kwa nguvu za Roho, akenda Galilaya; habari zake
zikaenea katika nchi zote za kandokando. Naye alikuwa akifundisha katika
masinagogi yao, akitukuzwa na watu wote.”
9. Paulo Mtume – Inaonekana wazi kuwa
injili aliyoihubiri hakufundishwa na wanadamu bali na bwana mwenyewe wala
hakuipata kwa mitume wengine, na ili kuthibitisha ni wapi alipata injili hii na
ni wapi Bwana Yesu mwenyewe alimfundisha, Paulo mtume anasema maneno haya
Wagalatia
1:11-20 “Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo
niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa
sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa
Yesu Kristo. Maana mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya
Kiyahudi, kwamba naliliudhi kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu. Nami
naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika
kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu. Lakini
Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake,
alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari
zake; mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu; wala sikupanda kwenda
Yerusalemu kwa hao waliokuwa mitume kabla yangu; bali nalikwenda zangu Arabuni,
kisha nikarudi tena Dameski. Kisha, baada ya miaka mitatu, nalipanda kwenda
Yerusalemu ili nionane na Kefa, nikakaa kwake siku kumi na tano. Lakini
sikumwona mtume mwingine, ila Yakobo, ndugu yake Bwana. Na hayo
ninayowaandikia, angalieni, mbele za Mungu, sisemi uongo.”
Paulo hapa anagusia kitu ambacho kitaalamu kinasumbua
kidogo wanatheolojia kwa sababu Arabuni anayoitaja Paulo ni ngumu kueleweka kwa
sababu unapotaja Arabuni leo wengi hufikiria ni Saud Arabia, lakini kwa mujibu
wa nyakati za karne ya kwanza neno hilo pia lilitumika kuelezea jangwa
lililokuwako kaskazini ambalo lilijulikana kama Syro Arabian derset hili ni
jangwa lililoko kaskazini ya Israel katika inchi ya Syria na Jordan, maelezo ya Paulo mtume yanathibitisha kuwa uko
Muda ambao Paulo alipitia jangwani na huko alifundishwa na Bwana mwenyewe kwa
habari ya injili aliyoihubiri, ukiacha kuwa alipandishwa katika maono makubwa
hata mbingu ya tatu, huenda maono haya aliyapata akiwa jangwani, sio hivyo tu huenda Paulo mtume aliutumia muda huo, kusoma,
neno la Mungu, kuomba na kujifunza na kutafakari na kupata mafunuo ya injili
aliyoihubiri, hivyo akawa na sifa za utume hata kabla ya kuonana na mitume,
unaposoma kitabu cha matendo unaweza kuona ni kama baada ya kuokoka kule
Dameski alianza injili mara moja na baadaye kuja Yerusalem lakini ni ukweli
ulio wazi, ulikuweko muda wa maandalizi jangwani na yalikuwa ni maandalizi ya kutosha kwaajili
ya utumishi wake
Mambo muhimu utakayopitia katika chuo kikuu Jangwani
Kama umepitia kwa umakini maswala
kadhaa tuliyojifunza hapo juu utaweza kugundua kuwa kuna maswala kadhaa muhimu
ambayo Mungu alikuwa ameyakusudia kwa kila mtumishi wake aliyemtumia alimpeleka
jangwani, kuna mambo maengi sana ya kujifunza kuhusu jangwa na uhusiano wake na
Mungu, pamoja na mafunzo mengine yote ambayo kimsingi yana umuhimu wake,
mafundisho kanisani ni muhimu, mafundisho shule za jumapili ni Muhimu, mafunzo
chuo cha biblia ni muhimu, hata hivyo jangwani hapa namaanisha mapito,
majaribu, mateso, na maswala kadhaa wa kadhaa ambayo kimsingi ndio yanalifanya
jangwa hilo liwepo katika maisha yako linatimiza kusudi Fulani la uwepo wako na
namna njema zaidi ya kuhudumu na kumtumikia Mungu kwa viwango anavyovikusudia,
sasa katika chuo hicho cha jangwani tunajifunza nini haya ndio baadhi ya mambo
tunayojifunza, kwanini unapita jangwani? Kwanini Mungu aruhusu uingine kwenye
chuo chake kikuu, chuo kikuu jangwani hapa ziko sababu:-
a.
Kwa
kusudi la kukuonyesha dhambi zako – Mungu hukupeleka jangwani kwa kusudi la
kukufunulia jinsi ulivyo, ukaidi wako na ubishi wako na ujeuri wako na
kutokustahili kwako na manung’uniko yako, na jinsi ambavyo wewe na mimi sio
bora kuliko wengine, ili tuwe mbali na kiburi, hili linafanyika kwa kukupeleka
kwenye chuo chake jangwani ili huko umjue mwokozi wako vizuri na pamoja na uasi
wetu wote tulio nao yeye anaendelea kutuhudumia kwa mahitaji yetu yote huko
jangwani, jangwa linaumiza sana unapolipitia lakini ndio njia pekee ya kuyaona
makosa yetu na njia zetu, huku tukiufurahia uzuri wa Mungu na njia zake. na
matokeo yake jangwa litatuumbia utakatifu nidhamu na ujuzi kuhusu Mungu
kivitendo.
Kumbukumbu 9:12-16 “Bwana akaniambia, Ondoka huko, shuka upesi; kwa kuwa watu wako
uliowatoa Misri wamejiharibu; wamekengeuka mara katika njia niliyowaamuru;
wamejifanyia sanamu ya kusubu. Tena Bwana akasema nami zaidi, akaniambia,
Nimeliona taifa hili; na tazama, ni taifa lenye shingo ngumu; niache, nipate
kuwaangamiza, na kulifuta jina lao chini ya mbingu; nami nitakufanya wewe uwe
taifa kubwa lenye nguvu kuwapita wao.Basi nikageuka nikashuka mle mlimani,
mlima ukawaka moto; na zile mbao mbili za agano zilikuwa katika mikono yangu
miwili. Nikaangalia, na tazama, mlikuwa mmefanya dhambi juu ya Bwana, Mungu
wenu; mmefanya ndama ya ng'ombe ya kusubu; mmekengeuka upesi katika njia
aliyowaamuru Bwana.”
Nehemia 9:13-21 “Tena
uliyaona mateso ya baba zetu katika Misri, ukakisikia kilio chao, huko kando ya
bahari ya Shamu; nawe ukaonyesha ishara nyingi na mambo ya ajabu juu ya Farao,
na juu ya watumishi wake wote, na juu ya watu wote wa nchi yake; kwa maana
ulijua ya kuwa waliwatenda kwa kutakabari; ukajipatia jina kama vile ilivyo
leo. Nawe uliipasua bahari mbele yao, hata wakapita katikati ya bahari katika
nchi kavu; na wale waliokuwa wakiwafuatia ukawatupa vilindini, mfano wa jiwe
katika maji makuu. Zaidi ya hayo ukawaongoza kwa nguzo ya wingu mchana; na kwa
nguzo ya moto usiku; ili kuwapa mwanga katika njia iliyowapasa kuiendea.Tena
ulishuka juu ya mlima Sinai, ukasema nao toka mbinguni, ukawapa hukumu za haki,
na sheria za kweli, na amri nzuri na maagizo;”
Israel walikuwa
wameokolewa kutoka Misri lakini walikuwa ni wakaidi, wenye kiburi, wanasahau
fadhili za Mungu kwa haraka, kwa hiyo jangwa liliwahusu ili wapokee maagizo ya
Mungu, wafundishwe kutenda haki, wafuate sheria na amri nzuri liwe taifa lenye
uadilifu na nidhamu ya hali ya juu, kwa hiyo jangwa liliwahusu, ili liwe taifa
takatifu, ukuhani mteule watu wa miliki ya Mungu
b.
Kwa
kusudi la kukutenga uwe wake – Mungu hukuongoza jangwani kwenye chuo chake
ili akutenge na watu wa ulimwengu huu, anataka kukufanya wewe kuwa wa-pekee,
alipowachakua Israel alitaka kuwatenga na kila aina ya ushawishi wa Kimisri,
alitaka kuwaumbia kiu ya kumtegemea yeye tu, naye awafundishe kuwa ni yeye peke
yake anayejali, na kufadhili kwa mahitaji yao yote, anataka umtegemee yeye tu
ajifunue kwako kama rafiki wa karibu, akuache uwe mpweke ili yeye abaki kuwa
rafiki wa kweli, ataacha ujeruhiwe ili yeye awe amani yako, atakuacha uwe
dhaifu ili yeye awe nguvu zako. Kusudi kubwa likiwa ni kupitisha mpango wake
kupitia wewe, hii haimaanishi kuwa wewe ni bora kuliko wengine bali ili Mungu
apitishe mpango wake lazima akuchonge kule chuoni kwake jangwani nawe utakuwa
tunu yaani kitu cha kujionea fahari
Kutoka 19:4-6 “Mmeona
jinsi nilivyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za
tai, nikawaleta ninyi kwangu mimi. Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli
kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko
makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu, nanyi mtakuwa kwangu
ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa
Israeli.”
c.
Kwa
kusudi la kuinua Imani na kukujenga upate kumuamini – jangwa linafundisha
kumwamini Mungu na kumtegemea yeye, pia linaikuza Imani yako, linakuandaa kwa
kusudi la kukufanya umtegemee Mungu moja kwa moja na kuisikia sauti yake na kumtii
na kufuata muongozo wake, Mungu hapendezwi na wale wasiomuamini, Neno lake
linasema na pasipo imani haiwezekani kumpendeza, kwa nini Mungu anaipima imani
yetu? Kila wakati Mungu atakapoijaribu imani yetu ana mpango wa kutupeleka
katika kiwango cha juu zaidi na kiwango cha kumjua yeye na kumkubali kuwa ndiye
Mungu wetu.
Kutoka 6:6-8 “Basi
waambie wana wa Israeli, Mimi ni YEHOVA, nami nitawatoa ninyi mtoke chini ya
mizigo ya Wamisri, nami nitawaokoa na utumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono
ulionyoshwa, na kwa hukumu kubwa; nami nitawatwaeni kuwa watu wangu, nitakuwa
Mungu kwenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ni YEHOVA, Mungu wenu, niwatoaye mtoke
chini ya mizigo ya Wamisri. Nami nitawaleta hata nchi ile ambayo naliinua mkono
wangu, niwape Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; nitawapa iwe urithi wenu; Mimi ni
YEHOVA.”
d.
Kwa
kusudi la kutufundisha utii na uvumilivu – jangwani ndiko Mungu
anakotufundisha kusubiri, hakuna jaribu gumu duniani kama kusubiri, jangwani
utake usitake huwezi kwenda kwa mwendo unaoutaka wewe, michanga itakuzuia,
utachelewa kufika utasubiri sana na kwa sababu hiyo utaenda si kama utakavyo
wewe bali kwa muda na wakati wa Mungu, utafuata maelekezo ya Mungu hata kama
njia zake zinaonekana kuwa ngumu kusudi kubwa tupate kujifunza kutii na
kuvumilia na kuwa na subira kabla ya kufika katika inchi njema
Kumbukumbu 4:1-10 “Na
sasa, Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende;
mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu.
Msiliongeze neno niwaamurulo wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za Bwana,
Mungu wenu, niwaamuruzo. Macho yenu yameona aliyoyatenda Bwana kwa sababu ya
Baal-peori; maana wote waliomfuata Baal-peori, Bwana, Mungu wako, amewaangamiza
kutoka kati yako.Bali ninyi mlioambatana na Bwana, Mungu wenu, mnaishi kila
mmoja wenu, hata leo. Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama
Bwana, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwingiayo ili
kuimiliki. Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili
zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika
taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili. Kwa maana liko taifa gani
kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu, alivyo, kila
tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama
torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo. Lakini, jihadhari nafsi yako,
ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho
yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto
wako na watoto wa watoto wako; siku ile uliyosimama mbele za Bwana wako huko
Horebu, Bwana aliponiambia, Nikusanyieni watu hawa, nami nitawasikizisha maneno
yangu, ili wajifunze kunicha mimi siku zote watakazoishi duniani, wakapate na
kuwafundisha watoto wao.”
e.
Kwa
kusudi la maonyo – Mungu hutupeleka katika chuo cha jangwani kwa kusudi la
kutuonya, wakristo wengi sana tuna matumizi mabaya ya neema, kuna mambo Mungu
anataka tuyaache hata hivyo lakini wengi tunaendelea nayo kwa hiyo jangwani ni
sehemu ya maonyo, unakumbushwa sio tu kujiona ni mwenye dhambi, lakini kuomba
neema ya kuziacha na kubadilika na kumwamini, mwamini Mungu sio tu kwa wokovu
wako lakini pia kwa mabadiliko ya tabia zako, Israel walitaka kwenda kanaani
hivyo hivyo na changamoto zao Mungu hakupendezwa nao kwa hiyo aliwaangamiza
jangwani unapokuwa jangwani kubali maonyo, sikiliza Sauti ya Mungu kwa bidi
jihoji wapi anataka nirekebishe kisha rekebisha, ni kiburi kujifikiri
umesimama!
1Wakorintho 10:1-12. “Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa
baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; wote
wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari; wote wakala chakula
kile kile cha roho; wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana
waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. Lakini
wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani.
Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya,
kama wale nao walivyotamani. Wala msiwe waabudu sanamu, kama wengine wao
walivyokuwa; kama ilivyoandikwa, Watu waliketi kula na kunywa, kisha wakasimama
wacheze.Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku
moja watu ishirini na tatu elfu. Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao
walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka. Wala msinung'unike, kama wengine wao
walivyonung'unika, wakaharibiwa na mharabu.Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa
jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya
zamani. Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie
asianguke”
f.
Kwa
kusudi la kukutia nguvu na kukuchonga - Changamoto za jangwani zitakujengea
utulivu na kukuchonga uweze kuwa na sifa njema
na viwango vya ubora unaokubaliwa na Mungu kwaajili ya uongozi na huduma,
uwakilishi na kukuweka katika mstari ulionyooka yaani bwana anakurudi,
anakuchapa anakutia nidhamu, na utanyooka tu na kuwa wake kweli kweli, kabla ya
kupewa umiliki uliokusudiwa katika maisha yako, utajifunza kumcha Mungu na
kumuhofu yeye hili ni moja ya kusudi la chuo kikuu jangwani.
Kumbukumbu 8:2-6.“Nawe
utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako aliyokuongoza miaka hii arobaini
katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba
utashika amri zake, au sivyo. Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa
mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa
mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha
Bwana. Mavazi yako hayakuchakaa, wala mguu wako haukuvimba, miaka hiyo
arobaini. Nawe fikiri moyoni mwako, ya kuwa kama vile baba amrudivyo mwanawe,
ndivyo Bwana, Mungu wako, akurudivyo.Nawe uzishike amri za Bwana, Mungu wako,
upate kwenda katika njia zake, na kumcha.”
g.
Kwaajili
ya maandalizi ya huduma – jangwani ndiko Mungu anakuandaa kwaajili ya
utulivu, ukomavu na majaribio ya huduma kwaajili ya kazi yake, wote watakaopita
katika shule ya Mungu, chuo kikuu jangwani watatoka huko wakiwa na nidhamu ya
hali ya juu, kiburi kinavunjiliwa mbali, woga unavunjiliwa mbali, kutokujiamini
kunavunjiliwa mbali, Mungu anakuwa Mungu wako, na imani inapanda, na kumtegemea
kunaongezeka na unaona rehema zake na utakumbuka kuwa ni yeye aliyekutokea huko
jangwani ulikokutana naye
Kumbukumbu 29:5-6 “Nami
miaka arobaini nimewaongoza jangwani; nguo zenu hazikuchakaa juu yenu, wala
kiatu chako hakikuchakaa katika mguu wako.Hamkula mkate, wala hamkunywa divai,
wala kileo; ili mpate kujua kwamba Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.”
Kila eneo ambalo
Mungu amelikusudia likue kwaajili ya utumishi wake litasitawi na kukua, ufunuo
mkuu wa huduma yako utaupata ukipelekwa jangwani yeye ndiye atajua kuwa utakapohitimu
jangwani utakuwa ni mtu wa namna gani, utasema nini utafanya nini na utakuwa na
sifa za namna gani.
h.
Kwa
kusudi la Mungu kujifunua kwako – Mungu ni Mungu mwenye wivu, anapoamua
kukupeleka jangwani anataka kujifunua kwako, anataka wewe na mimi tumjue yeye
kwa kina na mapana na marefu zaidi ili sisi tuwe wake na yeye awe wetu, Yesu
alipowaita wanafunzi wake pamoja na kuwa alikuwa anataka kuwatuma ili waifanye
kazi yake lakini alikuwa anataka kwanza wawe wenzake wawe mali yake, Chuo kikuu
jangwani kinakutaka uwe mali ya Mungu uwe mwenzake na ndio maana jangwani
utatengwa na watu wote
Kutoka 19:2-6 “Nao
walipokuwa wameondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, wakatua katika lile
jangwa; Israeli wakapiga kambi huko wakiukabili mlima. Musa akapanda kwa Mungu,
na BWANA akamwita toka mlima ule, akisema, Utawaambia nyumba ya Yakobo, na
kuwaarifu wana wa Israeli, maneno haya; Mmeona jinsi nilivyowatendea Wamisri,
na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za tai, nikawaleta ninyi kwangu
mimi. Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano
langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana
dunia yote pia ni mali yangu, nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa
takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli.”
Marko 3:13-15 “Akapanda
mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea. Akaweka watu kumi na
wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri
ya kutoa pepo.”
i.
Kwa
kusudi la kutunyenyekesha – Mungu huwa anataka tuwe wanyenyekevu kwa sababu
nyingi sana, lakini kusudi kubwa ni kutulinda na dhambi ya kiburi, kiburi huwa
kinaleta maangamizi ya haraka sana na Mungu hataki tuangamie, Shetani pamoja na
malaika zake waliangushwa na kiburi, kwa sababu ya upendo wa Mungu kwetu
hushughulika na kiburi chetu katika chuo chake kikuu jangwani ili tusijivune na
kumsahau yeye, Mungu anajua kuwa unyenyekevu unaleta utajiri na Mungu ana
makusudi ya kututajirisha lakini hebu fikiri kama utajiri utabebwa na mtu
mwenye kiburi, kijapo kiburi ndipo ijapo aibu Mungu hataki kamwe tujifikiri
kuwa sisi ni bora kuliko wengine, au watakatifu kuliko wengine au tumeokoka
kuliko wengine
Kumbukumbu 8:2-3 “Nawe
utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako aliyokuongoza miaka hii arobaini
katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba
utashika amri zake, au sivyo. Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa
mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa
mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha
Bwana.”
Zaburi 75:5-7 “Msiiinue
pembe yenu juu, Wala msinene kwa shingo ya kiburi. Maana siko mashariki wala
magharibi, Wala nyikani itokako heshima. Bali Mungu ndiye ahukumuye; Humdhili
huyu na kumwinua huyu.”
Mithali 16:18-19 “Kiburi
hutangulia uangamivu; Na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko. Afadhali
kuwa na roho ya unyenyekevu pamoja na maskini, Kuliko kugawanya nyara pamoja na
wenye kiburi.”
Mithali 22:3-4
“Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; Bali
wajinga huendelea mbele wakaumia. Thawabu ya unyenyekevu ambao ni kumcha Bwana
Ni utajiri, na heshima, nayo ni uzima.”
Kwa hiyo ni
muhimu kufahamu kuwa unapoona Mungu anayaingiza maisha yako jangwani basi moja
ya jambo ambalo tunapaswa kujifunza ni unyenyekevu, kwa haraka sana nyenyekea
na unapofanya hivyo njia yako ya jangwani itafupizwa kwa haraka, Mungu
atasubiri akuinue mara moja unapoamua kunyenyekea.
Yakobo 4:10 “Jidhilini
mbele za Bwana, naye atawakuza.”
Katika makanisa
Mengi na madhehebu mengi ya Kikristo, moja ya changamoto kubwa inayowasumbua
wengi hasa wa makanisa ya kipentekoste ni pamoja na tatizo la kiburi, na
wanaoongoza kwa unyenyekevu ni wakatoliki, makasisi wengi au wote wa kikatoliki
ni wanyenyekevu sana, na sifa hii ya unyenyekevu waliyo nayo sio ya kuigiza,
wote tunaweza kukubaliana kuwa hakuna mwanadamu mkamilifu, na kila mwanadamu
anaweza kuwa na udhaifu huu au ule lakini katika habari ya unyenyekevu
tukubaliane wazi kuwa Wakatoliki wako vizuri katika swala la unyenyekevu kuliko
madhehebu mengine, katika mafunzo yao hujifunza kupitia mabadiliko mbalimbali
ambayo yana mkazo mkubwa sana katika unyenyekevu, huwezi kupita jangwani katika
chuo kikuu cha Mungu kisha ukatoka na kiburi, Musa alikaa jangwani na akawa na mabadiliko makubwa sana kutoka Musa
yule mkali aliyekuwa anamuua Mmsri kwa mikono ywake na kumfukia mpaka kuwa mtu
mpole zaidi kuliko wote
Hesabu 12:1-3 “Kisha
Miriamu na Haruni wakamnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa
amemwoa; maana, alikuwa amemwoa mwanamke Mkushi.Wakasema, Je! Ni kweli Bwana
amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia? Bwana akasikia maneno yao. Basi huyo
mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso
wa nchi.”
Kama maandiko
yanatueleza kuwa Musa alikuwa mpole (Maana yake mnyenyekevu) zaidi ya wanadamu
wote waliokuwa juu ya uso wa nchi Je unadhani Yesu alikuwa mpole kiasi gani?
Isaya 53:7-9 “Alionewa,
lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye
machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake;
Naam, hakufunua kinywa chake. Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha
yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai;
Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu.Wakamfanyia kaburi pamoja na
wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala
hapakuwa na hila kinywani mwake.”
Makasisi wa
kikatoliki hujifunza njia ya unyenyekevu wakiishi kwa mfano huo na kukubali
fundisho liitwalo “The Theological
concepts of Kenosis” Fundisho
linalokazia kujinyenyekeza kunakopita kawaida ili tu uwahudumie watu, Yesu
Kristo akiwa kielelezo cha unyenyekevu huo, ukiacha kifo chake cha aibu, huruma
zake na upole na tendo la kuwaosha miguu wanafunzi wake sio kwaajili ya
kufundisha tu na kuonyesha kielelezo bali Yesu alikuwa anafanya kweli tukio
lile ambalo Petro hakulikubali kwani aliona haishatihi Mwalimu kujishusha
katika kiwango cha utumwa wa kupitakawaida
Wafilipi 2:4-8 “Msitende
neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu
na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo
yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine. Iweni na nia iyo hiyo
ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo
alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu
cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya
mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama
mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba”
Kwa hiyo
unyenyekevu wa aina hii tunaweza kujifunza kwa kupitia chuo kikuu cha jangwani
ambako tunajifunza kutambua kuwa hatuwezi jambo lolote bila Mungu, tunajifunza
kumtegemea Mungu kwa kila kitu, tunajifunza kuwatumikia wengine kwa
unyenyekevu, na tunajifunza kujilinda na kiburi na kuacha kabisa majivuno, Unyeneyekevu ni nguzo muhimu sana kwaajili ya
huduma na kwaajili ya kutengeneza uhusiano wa ndani sana na Mungu, kwa hiyo
ukiwaona watu wanajivuna, wanajigamba, wanafokea washirika, wanajitutumua, wanajifanya
mabwana katika makanisa yao, wanajifanya watawala machifu, watemi,
wanatengeneza himaya na kutaka kukuza majina yao kuliko la Yesu ufahamu chuo
hiki kwao bado sana, yaani mtumishi wa Mungu anakuwa kama Mungu kwenye kanisa
lake na anajivika uhakimu siku zote akiwahukumu wengine Mungu na atupe neema
sana na kuturehemu sana na kutusamehe sana
1Petro 5:1-5 “Nawasihi
wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya
Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye;lichungeni kundi la Mungu
lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu
atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo.Wala si kama wajifanyao
mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi.Na
Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile
isiyokauka.Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni
unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini
huwapa wanyenyekevu neema.”
Ni wapi sasa
Mungu anaweza kutufundisha shule hii ya unyenyekevu, usipojifunza mwenyewe kama
wakatoliki wanavyojifunza na kujitia nidhamu kubwa sana tena huku wakiwa na
elimu kubwa sana lakini wakiwa wanyenyekevu sana taaluma hii tunaweza kuipata
na kujifunza vizuri, ikiwa Mungu ataruhusu tupite katika chuo chake kikuu
jangwani.
Jangwani ni eneo la mabadiliko,
ni njia ya mpito ambapo watu wa Mungu hususani watumishi wanaandaliwa kwaajili
ya kazi kubwa sana iliyoko mbele yao, kwa hiyo wakati mwingine utalazimika kupitia
mapito magumu sana na majaribu mazito ili Mungu akulazimishe kukua kiroho na
kukuandaa tayari kwa huduma na wakati mwingine atakuacha kwenye upweke mkubwa,
kubwa zaidi jangwani ni sehemu ya usukivu MIDHBAR
ni mahali ambapo kila kitu kinasema kila pito linasema, kila jambo linasema
lakini vyote Mungu anavitumia kwaajili ya kukuchonga na kukuandaa kwa huduma na
utumishi uliotukuka ambao utakufanya utembee bila kiburi wala majivuno wala
utapeli, wala unafiki wala kuigiza, Kama Mungu angekuwa haruhusu watu kupitia Chuo
kikuu jangwani matepeli wengi sana wangejiingiza katika kazi ya kuhubiri injili
lakini ukimuona Muhubiri yeyote yule ana nidhamu ya hali ya juu, anahudumia
watu kwa unyenyekevu, yeye mwenyewe akiwa kielelezo cha unyenyekevu huo ujue
amepitia jangwani, na ukimuona muhubiri yoyote yule muhuni muhuni mambo yake
hayaeleweki, anatapeli watu janja janja nyingi ujue hajapitia jangwani, jangwani
ni chuo kikuu kinachohitimisha watu walioiva kihuduma na kiuadilifu, na kiimani
na wanaomtegemea Mungu. Watu waliopitia chuo hiki cha siri ni watu wa tofauti
sana waliojaa mamlaka ya kiungu. Na usemaji wao na utendaji wao na tabia yao na
unyenyekevu wao unakuwa kama sare ya shule (Uniform).
Chuo kikuu jangwani
Jangwani sio lazima liwe jangwa
halisi lakini ninapozungumzia jangwa hapa nimechukua picha ya ukweli halisi kutoka
katika maandiko na kukuleta katika ukweli halisi kuhusu mapito unayoyapitia au
tunayoyapitia katika maisha haya, mapito haya ndio shule ya Mungu, ndio chuo
kikuu jangwani ni chuo kikuu cha mafunzo ya kila aina ambayo Mungu anayaruhusu
katika maisha yetu, wote tunafahamu kuwa leo hii dunia ina vyuo vikuu vya kila
aina vilivyobora na vizuri sana na vinatoa kila aina ya degree, (Shahada) kwa
hiyo kuna ubora wa hali ya juu sana wa elimu na kuna degree za kila aina
zinazotoa mafunzo ya kila aina kwa hiyo tunamshukuru Mungu kuwa leo watu
wanaweza kuwa na ujuzi na ufahamu na elimu ya kila aina na katika elimu ya
Mungu kuna vyuo vingi vikuu vya Biblia na tunafurahia kuona watumishi wa Mungu
wakiwa na PHD degree, watu wanapokea vyeti vya aina mbalimbali yaani astashahada, Stashahada, Shahada,
Shahada ya uzamiri, Shahada ya uzamivu na Shahada ya ubobevu na vyuo hivyo vina ubora mkubwa wa kutosha,
hata hivyo bila chuo kikuu cha Roho Mtakatifu mambo mengi yatakuwa ni nadharia
tu. Mungu huwa ana namna yake ya kumuandaa mtumishi wake na kwa njia hizo huwa
anamfundisha vile anavyopaswa kuwa, Mungu alipomuita Saul/Paulo mtume
alimuandaa kuwa chombo chake kiteule, alimuandaa kuichukua injili kwa wafalme
na alimuandaa kama mtu atakayekuwa tayari kuvumilia mateso kwaajili ya jina la
Yesu, ona:-
Matendo 9:1-16 “Lakini Sauli, akizidi
kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka
ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa
Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu.Hata alipokuwa
akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka
mbinguni. Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi?Akasema,
U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe. Lakini
simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda. Na wale watu
waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, wakiisikia sauti, wasione mtu.Sauli
akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika
mkono wakamleta mpaka Dameski. Akawa siku tatu haoni; hali, wala hanywi. Basi
palikuwapo Dameski mwanafunzi jina lake Anania. Bwana akamwambia katika maono,
Anania. Akasema, Mimi hapa, Bwana. Bwana akamwambia, Simama, enenda zako katika
njia iitwayo Nyofu, ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu aitwaye Sauli, wa Tarso;
maana, angalia, anaomba; naye amemwona mtu, jina lake Anania, akiingia, na
kumwekea mikono juu yake, apate kuona tena. Lakini Anania akajibu, Bwana,
nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi aliyowatenda
watakatifu wako Yerusalemu; hata hapa ana amri itokayo kwa wakuu wa makuhani
awafunge wote wakuitiao Jina lako.Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana
huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na
wafalme, na wana wa Israeli. Maana nitamwonyesha yalivyo mengi yatakayompasa
kuteswa kwa ajili ya Jina langu”
Changamoto kubwa sana inakuja
endapo watu hawatapita katika chuo kikuu cha jangwani, hiki ni chuo cha kiroho
ni chuo cha mabadiliko ya kitabia, ni chuo cha uadilifu, ni achuo cha utumishi,
ni chuo cha kukuchonga na kuondoa kiburi, ni chuo cha unyenyekevu, ni chuo
ambacho kitakufanya umjue yule unayemtumikia kivitendo, Ni chuo kitakacho
kujulisha huduma uliyoitiwa na nini cha kufanya, Ni chuo ambacho utasikia sauti
ikisema Sauli Sauli mbona waniudhi? Ni chuo ambacho utakutana na Kristo
mwenyewe wazi wazi ukipitia chuo hiki hutafanya kazi ya Mungu kama
unavyojisikia au unavyotaka, utaifanya kama ulivyofundishwa na Yeye mwenyewe,
kama unabisha waangalie watumishi wote wa Mungu waliopitia chuo kikuu cha
jangwani na kuleta mageuzi makubwa na uamsho mkubwa na kufanya mambo ya
kushangaza duniani, na hawa tuliowaangalia katika maandiko utagundua kuwa hawajawahi kwenda kwenye vyuo maarufu sana
hapa duniani, lakini walikuwa kweli ni mdomo wa Mungu, walijulikana wazi kuwa
wamepitia jangwani, hawakuishi wakati mmoja lakini walifanana kwa sababu
Mwalimu wao ni mmoja, ni watu ambao watu hawakuwahi kuwawaza wala kuwaota,
walikuwa wana jangwani hasa, hakuna mtu aliejua wanatokea wapi, lakini
wakitokea unawakubali, lakini ghafla
waliinuka kuwa kinywa cha Mungu, walizunguka na kuzungumza kwa mamlaka na nchi
na mataifa yalitetemeka, walizungumza kweli iliyonyooka, walitoboa siri za
mioyo ya watu walipotokea hadharani hawakupwaya kila mtu alijua ya kuwa
wameandaliwa hasa, na wanafaa kwa kazi hiyo, nyuso zao, maisha yao, mavazi yao,
ujasiri wao, utayari wao, mamlaka yao, ishara zao, na miujiza yao ilikuwa imejawa
na uhakika wa kiungu, walikuwa na uadilifu ulionyooka, hutasikia wameshika mtu
chuchu, au wameshika mtu kalio au wanaropoka mambo yasiyofaa, walikuwa wamejawa
na ujumbe wa kimilele, mmoja tu wa
wahitimu hao alikuwa na thamani ya jeshi zima la Israel, kumbuka alipokufa
Elisha, mtu alilia baba yangu baba yangu magari ya Israel na wapanda farasi
wake, yaani Jeshi la Israel limeondoka! haiwezekani watu wamuwakilishe Mungu
alafu wawe hawaeleweki, mara wanaibia watu, mara wagonjwa wanaibiwa na
kutapeliwa, mara kuwaona wao ni mpaka ulipie, mara ukiingia lazima uwasujudie,
mara lazima uvue viatu kuna mbwembwe nyingi sana, waliopitia chuo kikuu cha jangwani walikuwa ni
watu walionyooka kama rula, hawakua na mizaha hata kidogo, hawakuwa na ubinafsi
wala sio wapiga dili au wasaka fedha, sifa zao, akili zao, midomo yao, uadilifu
wao ulionyesha wazi kuwa walikuwa wanamuwakilisha Mungu, kulikuwa na kila
ushahidi unaoonyesha kuwa hawakuwa watu waliozuka tu kwa bahati mbaya! na wala
hawakuumiza watu, wala kuwatawala watu kwa ukali lakini waliunguruma maneno ya
Mungu kama simba!, Upako haukuwa wa kubahatisha, vinywa vyaio havikujaa
majivuo, wafalme waliwatambua na raia waliwatambua, wajane walinufaika na
yatima walitiwa moyo, walikemea dhuluma waliwaonya wafalme!
Walikuwa ni watu ambao maisha yao
huwezi kusimulia, walikuwa tayari kwa lolote, walikuwa tayari kwa vita ya aina
yoyote, waliijua dhambi, walijua siri za mioyo ya watu, walijua maarifa ya
Mungu, walijaa hekima kama anga, wakati waliowajia walikuwa wamelala wao
walikuwa ni sababu ya uamsho mkubwa, uamsho waliokuwa wakileta haukutegemea
maombi ya kundi la watu ilikuwa ni Eliya mmoja tu, Ilikuwa Ni Yohana mmoja tu,
ilikuwa ni Amosi mmoja tu, umati wa watu uligeuka kwa Yona mmoja tu, hawa
walikuwa ni askari kweli kweli wakati watu waliowahudumia walikuwa wanaota
ndoto, wao walikuwa na maono sahihi na neno sahihi la Mungu lilikuwa ndani yao,
wakati wengine walikuwa wakipiga pesa, wao walijawa na uaminifu, na kuwa mbali
na hila, wakati mamia ya watu wakiwa wanajifurahisha katika starehe na kujifurahisha na anasa za dunia, kufanya
biashara na kufuata namna ya dunia hii, huku shule za dunia hii zikiwa zimejawa
na kila aina ya starehe za kuwatuliza na kuwafurahisha, wao walikuwa na ujumbe
mpya na elimu mpya kutoka chuo kikuu jangwani wakiamsha nia za wahubiri na
wananchi kumcha Bwana, waliingia kila
mahali walikotumwa na Mungu, kutoka kwa wafalme mpaka kwa wajane, waliamuru
watu kurudi katika njia za Mungu, wakiwa na uwepo wa Mungu, hali ya kiroho ya
juu, nguvu za Mungu zisizo na maswali, walijawa na silaha za kimbingu watu
walinyamaza kimya waliponena, watu walitetemeka walipowaona, na waliwataka watu
watubu na kuacha kuabudu sanamu na waliwahuisha watu kuishi kwaajili ya Mungu
na kumtumikia Mungu, waliowaonya masikini kwa matajiri, wafalme kwa watumwa na
walilikabili taifa lolote hata nje ya mipaka. Walikuwa kielelezo, walikemea
dhuluma, rushwa na ubadhirifu, hawakupaka mtu mafuta kwa mgongo wa chupa.
Hawakuwahi kuwa na uongo mioyoni
mwao wala midomoni mwao, walikuwa wanamuwakilisha Mungu wa kweli, waliandaliwa
na walikuwa tayari wakitokea jangwani, walisimama katika zamu zao kwa uaminifu,
na hawakuonekana kuwa labda wamechanganyikiwa walikuwa na akili, akili timamu
na walikuwa na uwezo wa kujibu maswali yoyote ambayo yangeinuka, na kuulizwa na
mtu yeyote haijalishi ni swali na namna gani na limetoka kwa nani, walikuwa na
ujuzi wa kujibu kila aina ya hoja ziwe za askari, ziwe za raia, ziwe za
masadukayo, ziwe za mafarisayo, ziwe na maherode, ziwe za waesene, waliweza kumkemea
kila mtu hata mfalme alipokosea hawakumficha kitu, malikia waovu waliwaogopa, Chuo
kikuu jangwani kilikuwa kimewaandaa kusema kweli bila hofu walikuwa wako tayari
kukabiliana na yeyote yule kwa sababu zozote zile zilizo kinyume na mapenzi ya
Mungu, waliwarejesha watu wa Mungu wakikemea kila njia mbaya, ibada mbaya,
ibada za sanamu, uchawi, uasi, kupoa, ushirikina, na ukengeufu na waliwataka
watu wasisahahu kuwa yuko Mungu mbinguni, hawa walishazoea kuwa peke yao
walibaki na Mungu tu, waliomba, walihubiri, walikemea na kuonya, na walimleta
Mungu mzima mzima katika mioyo ya watu kwa kweli walionyesha kila jinsi kuwa
wamehitimu katika chuo kikuu cha Mungu chuo kikuu jangwani!, waliijua sheria ya
Mungu, waliijua torati ya Musa walilijua neno la Mungu, waliwaonya manabii wa
uongo, waliamuru wachawi kutokuliona jua, walikuwa watu wa kipekee,
Unapopelekwa jangwani Mungu anataka muhitimu wa aina hii.
Chuo kikuu jangwani ni majaribu,
ni mapito, ni nyakati ngumu, ni kila aina ya uchungu unaoupitia duniani katika
kila unachokipitia acha kulia acha kulalamika na badala yake tulia usikilize
sauti hiyo ya jangwani inataka nini baada ya hayo unayoyapitia jangwani
utaisikia sauti ya Mungu, itakufundisha utii, itakufundisha unyenyekevu, Jangwa
halionekani kuwa kitu kizuri, na unaweza kusema kwanini Mungu ameumba jangwa
lakini jangwa lina ujumbe mzito kwetu kuwa linaweza kuwa Mwalimu mzuri wa
maswala ya kiroho, jangwa linaonya, jangwa linafundisha adabu, jangwa
linaelekeza, jangwa lina amri, jangwa linatia nidhamu, jangwa linaondoa kiburi,
jangwa linakufundisha kuwa hutaishi kwa mkate tu, jangwa linakufudisha chakula
cha mbinguni, jangwa linakufundisha kuwa shujaa wa vita, jangwa linakufundisha
dhiki sio kitu kwa Mungu, Nyoka sio kitu kwa Mungu, Nge wake sio kitu kwa Mungu,
miba zake ni uvumilivu, jangwa linakukumbusha kuwa ukiwa na Mungu hutapungukiwa
na kitu, jangwa linakukumbusha kutokuogopa mabaya, jangwa linakukumbusha kuwa
Mungu anaweza kutokeza maji kutoka katika mwamba mgumu, jangwa linakufanya uwe
mtu wa miliki ya Mungu, angwa linakufanya uwe imara, jangwa linakufanya uwe
mtumishi wa kipekee, jangwa linakupa kuifanya huduma uliyoitiwa kwa ufanisi,
jangwa linakuimarisha, jangwa linaondoa shaka, jangwa linakufanya uwe na
maamuzi, jangwa ni sauti ya Mungu kivitendo, jangwa linakufanya uwe
mnyenyekevu, watu watakujua ukoje ukifunua kinywa chako na wanaweza kukudharau
wakikuona, jangwa ni chuo!
Mwangalie Musa, mwangalie Eliya,
mwangalie Yohana mbatizaji, wote hawa walikuwa wahitimu wa jangwani ona jinsi
walivyokabiliana na wafalme, ona jinsi walivyosimamia uadilifu, ona walivyokuwa
na mamlaka ya kiungu, ona jinsi ambavyo hawakuwa waoga ona jinsi Mungu
alivyokuwa pamoja nao na ona jinsi Mungu alivyowatumia!
Kama watu wa Mungu na watumishi
wote mnaowana leo wangepita katika shule hizo tungekuwa na watu ambao ulimwengu
haukustahili kuwa nao. Je unajisikiaje
unateseka, unaona kama Mungu amekuacha, unajihisi mpweke, unakabiliwa na njaa,
unahisi watu wote wamekuacha, hauna msaada, unakata tamaa? Unajiona kama una
laana? Unajiona umechelewa? Ni kama hauna bahati? Mambo hayakunyookei? Huna
connection? unaona giza, Je umejawa na mashaka? Umejawa na msongo wa mawazo?
Unahisi umetengwa na Mungu?, Mungu anaonekana yuko mbali?, Mungu anaonekana
hayuko?, Mungu anaonekana hawajibiki? Umejawana mashaka tupu na hakuna imani?
Unahisi uko peke yako? Ni kama umepotea, ni kama hauna ulinzi, Umejawa na hofu
na kukosa matumaini? Unahisi umepoteza muelekeo? Umeachwa? Hakuna wa kukujali?
Hupendwi tena? uko kama umechanganyikiwa ndugu yangu usiogope ukiona hayo
unayapitia ujue uko chuo kikuu cha jangwani, hakuna Mkristo anayempenda Yesu
ambaye atakwepa kabisa kupitia chuo hiki! mimi ninakijua nimepita kwenye chuo
hicho, nimeishi kwenye chuo hicho, nimeelimisjhwa kwenye chuo hicho? Umewahi
kutengwa wewe? Mimi nimewahi, umewahi kuchafuliwa wewe? Mimi nimewahi, Umewahi
kukataliwa wewe mimi nimewahi, watu wamewahi kukuacha wote? Mimi nimewahi, umewahi
kutungiwa uongo? Mwenzako nimewahi, umewahi kukosa kazi, mimi nimewahi, umewahi
kuacha kutumiwa na Mungu kabisa mimi nimewahi, umewahi kufilisika, mimi
nimewahi, umewahi kuteuliwa kisha kutenguliwa? Mimi nimewahi, umewahi kuahidiwa
kitu na mtu kisha asikutekelezee, mimi nimewahi, umewahi kutengwa na mkeo, mimi
nimewahi, umewahi kufanyiwa mabaya na watu wa karibu mimi nimewahi, umewahi
kushauriwa vibaya mimi nimewahi, umewahi kutapeliwa fedha nyingi sana? Mimi
nimewahi umewahi kumlaumu Mungu? Mimi nimewahi, ndio kwa sababu ni wakati ambao
Mungu anaonekana hajali, hahesabu kama kuna kitu umewahi kukifanya, maandiko
yake yote yanaonekana kana kwamba ni nadharia tu unajiuliza anawezaje kuruhusu
haya kutokea maishani mwangu?, Hivi kweli yupo? Anaweza kuonekana kweli, au
kila kitu kinakuwa kama batili hivi, Je umewahi kuranda randa? Mimi nimewahi
umewahi kuhisi kuchanganyikiwa? Mimi nimewahi, umewahi kushindana na kitu
Fulani mwilini mwako kikuachie na kikawa hakitaki mimi nimewahi, umewahi kuwa
katika hali ya ukavu kabisa? Mimi nimewahi, umewahi kuhubiri mkutano siku tatu
na mtu asiokoke? Mimi nimewahi na nilitamani niache kabisa injili? Umeahi
kujisikia kutikula na chakula kipo? Mimi nimewahi, umewahi kuharibikiwa mipango
yako yote? mimi nimewahi, umewahi kushindwa vita na adui zako? Mimi nimewahi
umewahi kulia hadharani? Mimi nimewahi, umewahi kutukana hadharani? Mimi
nimewhi, umewahi kufanyiwa hila na walokole wenzako? Mimi nimewahi, umewahi
kufanya makosa makubwa sana? Mimi nimewahi, aibu yako imewahi kutawanyaika kila
mahali mimi nimewahi, umewahi kuwasikia watu wakikuzungumza vibaya huku
hawakujui? Mimi nimewahi kuwasikia watu wakizungumza mabaya kunihusu utadhani
wananijua! ukiyaona hayo basi usijifikiri kuwa wewe ni mtu mbaya, au eti Mungu
anakunyoosha hapana ujue uko chuo cha jangwani Mungu hutupeleka huko tuone
ujinga wetu, tujifunze hekima yake, tuzijue njia zake, na kutambua jinsi alivyo
mkuu na mwema! Unaweza kuwa na maswali meengi sana lakini majibu ndio haya
anatupeleka katika jangwa la kutisha ili tuwe watu wake, anatupitisha katika
tanuru la moto ili tutoke kama dhahabu iliyo safishwa, tayari kwa matumizi
mengine baada ya kutoka jangwani utakuwa mtu wa namna nyingine, na ndugu zako
watakuinamia, kila atakayekuona atakuheshimu utakuwa rafiki wa Mungu na
utaongea na Mungu uso kwa uso huku ukiwa hauna majivuno na ukiwa mpole na
mnyenyekevu kuliko watu wote. Matokeo ya uvumilivu wako yatakuleta katika
kilele cha utumishi uiotukuka n ahata ukiondoka kazi yako itadumu duniani na
kuwa msaada kwa watu wengi sana.
2Wafalme 2:11-15 “Ikawa, walipokuwa
wakiendelea mbele na kuongea, tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa
moto, likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa
kisulisuli.Naye Elisha akaona, akalia, Baba yangu, baba yangu, gari la Israeli
na wapanda farasi wake! Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe,
akayararua vipande viwili.Kisha akaliokota lile vazi la Eliya lililomwangukia,
akarudi, akasimama katika ukingo wa Yordani.Akalitwaa lile vazi la Eliya
lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, Yuko wapi Bwana, Mungu wa Eliya? Naye
alipoyapiga maji, yakagawanyika huku na huku, Elisha akavuka.Na hao wana wa
manabii, waliokuwako Yeriko wakimkabili, walipomwona, walisema, Roho ya Eliya
inakaa juu ya Elisha. Wakaja kuonana naye, wakainama kifudifudi mbele yake.”
Ayubu 23:2-10 “Hata leo mashitaka yangu
yana uchungu; Pigo langu ni zito zaidi ya kuugua kwangu.Laiti ningejua mahali
niwezapo kumwona, Nifike hata hapo anapokaa! Ningeiweka daawa yangu mbele yake,
Na kukijaza kinywa changu hoja. Ningeyajua maneno atakayonijibu, Na kuelewa na
hayo atakayoniambia. Je! Angeshindana nami kwa ukuu wa uwezo wake? La, lakini
angenisikiliza. Hapo walekevu wangepata kuhojiana naye; Basi hivyo
ningeachiliwa na mwamuzi wangu milele. Tazama, naenda mbele, wala hayuko;
Narudi nyuma, lakini siwezi kumwona; Na mkono wa kushoto, afanyapo kazi, lakini
siwezi kumwona; Hujificha upande wa kuume, hata nisimwone. Lakini yeye aijua
njia niendeayo; Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.”
Mithali 3:5-6 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako
wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye,
Naye atayanyosha mapito yako.”
Hitimisho
Chuo kikuu jangwani ni chuo cha
changamoto nyingi lakini zenye faida kubwa sana katika maisha nya kiroho, kwani
unapata uzefu wa kuishi maisha ya kumtegemea Mungu, na kukupa nguvu na ujasiri mwingi katika kukabiliana
na changamoto za maisha, aidha jangwa linamsaidia mtu wa Mungu kukua kiroho na
kwenda katika nagzi ya juu kabisa ya uadilifu nidhamu na kuishi kwa kanuni,
jangwa linakufanya uwe wa kipekee, na jwangwa linakufanya uwe makini na
uthamini kila kitu katika maisha, utaona uthamani wa chakula, utaona uthamani
wa maji, utajua uthamani wa makazi, utajua uthamani wa umoja, utaona uthamani
wa uhusiano, utajifunza kukua, kuimarika kiroho, na utagundua kuwa kilikuwa
kipindi cha Baraka kwa maisha yako na utumishi wako, Bwana akupe neema na uwezo
wa kuvumilia shule anayokupitisha na kusaidie uweze kuhitimu salama.
Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
+255 718 99 07 96
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni