Jumapili, 13 Julai 2025

Asizimie moyo mtu!


1Samuel 17:32-36 “Daudi akamwambia Sauli, Asizimie moyo mtu ye yote kwa ajili ya huyu; mimi mtumishi wako nitakwenda kupigana na Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Huwezi wewe kumwendea Mfilisti huyu upigane naye; maana wewe u kijana tu; na huyu ni mtu wa vita tangu ujana wake. Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo wa lile kundi, mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua. Mtumishi wako alimwua simba na dubu pia; na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa sababu amewatukana majeshi ya Mungu aliye hai.”


Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa katika maisha haya mara nyingi mimi na wewe kama wanadamu huwa tunakutana na changamoto mbali mbali ambazo nyinginezo zinaweza kutuvunja moyo na kutukatisha tamaa, sio hivyo tu pia zinaweza kutuogopesha na kutufanya tupoteze kujiamini au hata kuamini kuwa Mungu anaweza kutusaidia tena, Katika Israel wakati fulani waliwahi kukutana na hali kama hii unayoipitia wewe, walikuwa katika vita na wafilisti, na katika jeshi la wafilisti alijitokeza mtu mmoja mkubwa sana mwenye nguvu na mwenye kutisha ambaye alizungumza maneno ya propaganda za kivita na kuwatia hofu sana wana wa Israel kiasi ambacho jeshi lote la Israel wakiongozwa na Sauli mfalme wao waliogopa na kuzimia moyo, Neno “Asizimie” katika Lugha ya kiebrania linasomeka kama “Nรขphal” ambalo kwa kiingereza ni “fall” limetumika hivyo mara 318 likimaanisha kuanguka, au kupoteza matumaini, au kushuka chini kutoka katika hali yake ya awali, kwa Kiswahili kuvunjika moyo yaani asivunjike moyo mtu awaye yote  unapokutana na changamoto.

1Samuel 17:1-11 “Wakati huo Wafilisti walikusanya majeshi yao kwa vita, nao wakakusanyika huko Soko, ulio mji wa Yuda, wakatua kati ya Soko na Azeka, katika Efes-damimu. Naye Sauli na watu wa Israeli wakakusanyika, wakatua katika bonde la Ela, nao wakapanga vita juu ya hao Wafilisti. Wafilisti wakasimama juu ya mlima upande huu, na Waisraeli wakasimama juu ya mlima upande huu, napo palikuwa na hilo bonde katikati. Ndipo akatoka shujaa katika kambi ya Wafilisti, aliyeitwa Goliathi, wa Gathi, ambaye urefu wake ulikuwa mikono sita na shibiri moja. Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani, tena amevaa darii ya shaba; na uzani wake ile darii ya shaba ulikuwa shekeli elfu tano za shaba. Tena amevaa mabamba ya shaba miguuni mwake, naye alikuwa na mkuki wa shaba kati ya mabega; yake. Na mti wa fumo lake ulikuwa kama mti wa mfumaji; na kichwa cha mkuki wake kilikuwa shekeli mia sita za chuma uzito wake; na mtu aliyemchukulia ngao yake akamtangulia. Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupanga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi. Kama akiweza kupigana nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda yeye na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia. Yule Mfilisti akasema, Nayatukana leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane. Basi Sauli na Israeli wote waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana.”

Kutokana na maneno ya shujaa huyo wa wafilisti mwenye kutisha sana Israel waliogopa na kuzimia moyo, ni jambo la kawaida wakati mwingine kwamba linapotokea jambo la kutisha kutokana na propaganda za kishetani huwa tunasahau uweza wa Mungu na ukuu wake na kuitazama ile changamoto huku tukijiuliza kama tunaweza kutokaje katika changamoto hiyo, unajiuliza nitatoboa kweli au safari hii ndio nafariki, nitatokaje katika ugonjwa huu, nawezaje kukabiliana na deni hili kubwa namna hii, aibu inakaribia, nawezaje kutoka katika matatizo haya na kwa sababu ya utisho wa hali inayotuzunguka ni rahisi kwetu kuvunjika moyo au kuzimia moyo, Kijana mdogo sana katika Israel Daudi alisimama kwa ujasiri na kuwatia moyo taifa zima ya kuwa asizimie moyo mtu! Kwani yeye atapambana na hali inayowakabili kwa jina la Mungu wa Israel!. Leo kila changamoto unayokabiliana nayo, kila ukuta unaosimama kama kikwazo katika maisha yako, kila mlima na jaribu, na mateso, na ugonjwa na majini na mapepo na nguvu za giza zinazosimama kama changamoto katika maisha yako ambazo zimekufanya ukazimia moyo kwa jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai tunakwenda kukabiliana nazo na kuzisambaratisha kabisa haleluyaa Asizimie moyo mtu!.Tutajifunza somo hili Asizimie Moyo mtu kwa kuzuingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Sababu za watu kuzimia moyo!

·         Asizimie moyo mtu!

·         Kwanini asizimiye moyo mtu!

Sababu za watu kuzimia moyo!

Ni ukweli uliokuwa wazi kuwa Israel kama ilivyo kwa watu wengine walikuwa wamevunjika moyo na kuzimia kabisa kwa woga, mazingira waliokuwa wanakabiliana nayo, yalikuwa ni magumu na yenye kuogopesha sana, propaganda za kivita zilikuwa zimewatia hofu na kuwachosha, Goliath alikuwa akijitokeza kila siku asubuhi na jioni kwa siku 40 akiwatukana na kuwatisha sana, jambo lilolopelekea jeshi zima na mashujaa wakubwa wakiwepo kaka zake Daudi na mfalme Sauli kutishika na kufadhaika sana, Goliathi aliyatukana majeshi ya Israel waziwazi, hadharani kila mtu akishuhudia!

1Samuel 17:10-16 “Yule Mfilisti akasema, Nayatukana leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane. Basi Sauli na Israeli wote waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana. Basi Daudi alikuwa mwana wa yule Mwefrathi, wa Bethlehemu ya Yuda, aliyeitwa jina lake Yese; naye huyo alikuwa na wana wanane; na yeye mwenyewe alikuwa mzee siku za Sauli, na mkongwe miongoni mwa watu. Nao wale wana watatu wa Yese waliokuwa wakubwa walikuwa wamefuatana na Sauli kwenda vitani, na majina ya hao wanawe watatu waliokwenda vitani ni haya, mzaliwa wa kwanza Eliabu, na wa pili wake Abinadabu, na wa tatu Shama. Naye huyo Daudi alikuwa mdogo wa wote; na hao watatu waliokuwa wakubwa wakafuatana na Sauli. Basi Daudi alikuwa akienda kwa Sauli na kurudi ili awalishe kondoo za baba yake huko Bethlehemu. Naye yule Mfilisti hukaribia asubuhi na jioni, akajitokeza siku arobaini.”

Sisi nasi katika maisha yetu tunaweza kufadhaika na kutishika na hata kuvunjika moyo kutokana na uhalisia wa changamoto, ni ukweli uliokuwa wazi kuwa Golitahi lilikuwa jitu kubwa lenye nguvu na uzoefu wa kivita, na jeshi lote la Israel lilimuogopa, yako mambo ambayo yakikupata wewe mwenyewe na hata wataalamu wanaweza kukubaliana kuwa ni jambo zito na kubwa, ikiwa una ukimwi, ikiwa una sukari, ikiwa umepatwa na kiharusi, ikiwa una kansa ya damu, ikiwa una changamoto ya ini, kansa, figo, changamoto za mfumo wa fahamu, umeme katika mwili, moyo na kadhalika ni magonjwa ya kutisha ambayo hata wataalamu wa afya wenyewe wanayaogopa na una historia yake namna na jinsi yalivyoua watu mbalimbali kwenye jamii yako, familia yako na hata majirani, changamoto za mikopo umiza, madeni ya aibu, kufilisika, hasara za namna mbalimbali, kutapeliwa fedha nyingi, kuporomoka kwa biashara, hali mbaya ya kiuchumi, kutokujitosheleza kwa mahitaji mbalimbali na umasikini wa kutisha vinaweza kuwa sababu ya kuzimia moyo, Sio hivyo tu maneno unayoyasikia kutoka upande wa upinzani au wa adui yako na wakati mwingine wanaweza hata kusema kuhusu Mungu wako kwamba tuone kama Mungu wake anaweza kumsaidia hivyo vyote vinaweza kukufanya ukazimia moyo, wakati unapokuwa katika changamoto kali na ngumu sana maneno ya adui zako yanaweza kukuumiza sana, na hata maneno ya wale watu usiowatarajia, kama wapendwa wenzetu, Yesu alipokuwa msalabani adui zale walisema pia kuhusu Mungu kwamba amemtegemea Mungu na amwokoe sasa Msalabani nasi tutamwamini maneno ya kuumiza!

Mathayo 27:40-43. “Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka msalabani.Kadhalika na wale wakuu wa makuhani wakamdhihaki pamoja na waandishi na wazee, wakisema, Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe. Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu.”

Hatupaswi kamwe kukosa imani na kuvunjika moyo au kuzimia moyo wala kuyatazama mazingira na badala yake tunapaswa kumwangalia Mungu ambaye ni mkubwa kuliko changamoto yako, Daudi kamwe hakukubali kuwa na aibu ya kitaifa na wala hakukubali Mungu wake adhalilike na ndugu zake waaibike, akiwa amejaaa Imani, uzoefu, ujuzi kuhusu Mungu na ujasiri mkubwa ambao wengi walikuwa wameupoteza yeye alisema atapambana na hali hiyo na kwa sababu hiyo asizimie moyo mtu, usizimie moyo kwaajili ya ugonjwa wako, usizimie moyo kwaajili ya adui zako, usizimie moyo kwaajili ya umasikini wako, usizimie moyo kwaajili ya changamoto na matatizo ya kifamilia, haijalishi adui anatisha kwa kiwango gani sisi tutamjia kwa jina la Bwana Mungu wa Israel aliye hai.

Asizimie moyo mtu!

Wakati kila mtu akiwa ameingiwa na hofu fadhaa na kukata tamaa au kuzimia Moyo, Daudi alikuwa na mtazamo tofauti na wengine Yeye alikuwa amejifunza kuwa Mungu ni mkubwa kuliko changamoto ya aina yoyote ile, alikuwa amejifunza na kupata uzoefu na shuhuda namna na jinsi Mungu alivyompa ushindi dhidi ya  wanyama wakali wenye nguvu kuliko binadamu wanyama kama Dubu, Simba na kadhalika alitambua kuwa Mungu alikuwa pamoja naye hata alipokuwa akiwachunga kondoo wa baba yake na kwa sababu hiyo Golitahi kwake lilikuwa ni jambo dogo sana wala sio la kufadhaisha mtu na hivyo aliwapa tumani watu wote pamoja na mfalme Asizimie moyo mtu!

1Samuel 17:34-37 “Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo wa lile kundi, mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua. Mtumishi wako alimwua simba na dubu pia; na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa sababu amewatukana majeshi ya Mungu aliye hai. Daudi akasema, Bwana aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Enenda, na Bwana atakuwa pamoja nawe.”

Daudi aliamini kuwa sio kwa nguvu za kibinadamu atamkabili Goliath lakini ni kwa nguvu za Mungu na kwa msaada wa Mungu, alikumbuka shuhuda za ukuu wa Mungu na matendo yake na uaminifu wake, alitambua jinsi jina la Mungu linavyopaswa kutakaswa na kutukuzwa na alijua ya kuwa kwa jina hilo hakuna kinachoweza kusimama, alifahamu ya kuwa Mungu hawezi kutukanwa wala kudhalilishwa na jeuri na kiburi cha kibinadamu na kisha akakubali, Daudi alitambua kuwa kutukanwa kwa majeshi ya Mungu aliye hai ni kutukanwa kwa Mungu kwa hiyo alitaka kuitetea heshima ya Mungu, Daudi alitambua kuwa ushindi wake ni ushindi wa kitaifa na sio wa mtu mmoja na kuwa kushindwa kwa Goliathi ni kushindwa kwa wafilisti wote, Ni ukweli uliowazi katika ulimwengu wa roho vita ya Daudi na Goliati ilikuwa inawakilisha vita ya Yesu Kristo na Shetani, yule atakayeshindwa atakuwa mtumwa wa yule atakayeshindwa na watu wake na yule atakayeshinda atatawala yeye na watu wake kila mtu aliyeokoka ni mshindi kupitia ushindi wa Yesu Kristo, wakati Goliathi akiwa na kofia ya chuma na mabamba ya chuma kila mahali Daudi yeye hakuwa na kizuizi chochote na alikuwa na silaha laini yaani manati-kombeo na mawe matano tu laini

1Samuel 17:45-47.”Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana. Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli. Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana, naye atawatia ninyi mikononi mwetu.”

Wakati Goliathi alikuwa akitema propaganda tu na vitisho kwa kujiamini kwa kiburi na majivuno, Daudi alikuwa akizitamka shuhuda za Mungu na ukweli wa neno lake Mungu na uweza wake, ni ukweli ulio wazi kuwa siku ile Daudi alimpiga Goliathi na kwa kutumia upanga wa Goliathi mwenyewe alikata kichwa chake, tukio hili liliwapa nguvu Israel na waliwakimbiza wafilisti na kuwachinja kama walivyotaka na kujikusanyia nyara:-

1Samuel 17:48-52 “Ikawa, hapo Mfilisti alipojiinua, akaenda akamkaribia Daudi, ndipo Daudi naye akapiga mbio, akalikimbilia jeshi ili akutane na yule Mfilisti. Daudi akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingilia kipajini, akaanguka chini kifudifudi. Hivyo Daudi akamshinda yule Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akampiga Mfilisti, akamwua; walakini Daudi hakuwa na upanga mkononi mwake. Ndipo Daudi akapiga mbio, akasimama juu ya Mfilisti, akautwaa upanga wake, akaufuta alani mwake, akamwua, akamkata kichwa kwa upanga huo. Nao Wafilisti walipoona ya kuwa shujaa wao amekufa, wakakimbia. Nao watu wa Israeli na wa Yuda wakainuka, na kupiga kelele, nao wakawafuata Wafilisti mpaka ufikapo Gathi, na mpaka malango ya Ekroni. Nao majeruhi wa Wafilisti wakaanguka kando ya njia iendayo Shaarimu, mpaka Gathi, na mpaka Ekroni.”  
           

Kwanini asizimiye moyo mtu!

Daudi alikuwa na ufahamu kuwa ushindi wake hautokani na yeye mwenyewe bali ushindi wake unatokana na Mungu, sisi nasi hatuna budi kufahamu kwamba ushindi wetu unapatikana kupitia Yesu Kristo ambaye alishinda kifo na mauti, ushindi wowote tulio nao na tutakaokuwa nao ni ushindi unaotokana na ushindi wake Kristo Yesu mwana wa Daudi.  

1Wakorintho 15:57 “Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo.”

Maandiko yanatukumbusha tu kuwa hakuna changamoto kubwa kuliko Mungu wetu, kila mtu aliyeokolewa na anayemtegemea Mungu anapaswa kumtegemea Mungu na kumfanya kuwa ngao yake na kinga yake, tunapaswa kuwa na ujasiri na kuacha kupoteza matumaini, hatupaswi kamwe kuzimia moyo kama tumemfanya Bwana kuwa ngao yetu, hatupaswi kulia wala kufadhaika maana Mungu ndiye wokovu wetu, na ngome yetu na hakuna wa kutukaribia wala kutudhuru vyovyote vile!

Zaburi 27:1-3 “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini.”

Maandiko yanatukumbusha kuwa Mungu hutumia mambo manyonge sana, wakati ambapo Goliath anaonekana kuwa na silaha bora, mkuki mkubwa na uzoefu mkubwa vitani, huku mwili wake umezingirwa na mambamba ya shaba Daudi alikuwa ni kijana mdogo, mzuri macho mekundu lakini alijikinga kwa jina la Mungu na kumfanya Mungu kuwa tumaini lake, hii inatukumbusha kuwa Mungu anaweza kutumia chochote na kumtumia mtu yeyote bila kujali hali yake, historia yake na muonekano wake wa nje, unyonge wake au kupuuzwa kwake, Mungu hutumia vilivyodharaulika!  

1Wakorintho 1:26-29 “Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko; mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu.”

Maandiko yanatukumbusha kuwa Mungu ni mwaminifu na kuwa tunapokabiliana na changamoto za aina yoyote katika maisha yetu na tukumbuke namna na jinsi alivyotusaidia katika mambo mengine kumbuka matendo yake ya kale na hii itamuimarisha kila mmoja wetu kujua kuwa Mungu yule yule asiyebadilika aliyewasaidia baba zetu katika vita zao atajitokeza tena kwa namna nyingine kutusaidia

Zaburi 77:11-14 “Nitayakumbuka matendo ya Bwana; Naam, nitayakumbuka maajabu yako ya kale. Pia nitaitafakari kazi yako yote; Nitaziwaza habari za matendo yako. Ee Mungu, njia yako i katika utakatifu; Ni nani aliye mungu mkuu kama Mungu? Wewe ndiwe Mungu ufanyaye maajabu; Uliudhihirisha uweza wako kati ya mataifa.”

Ee Bwana usimuache msomaji wangu, na msikilizaji wangu na kila mtu duniani anayekutegemea wewe, usimwache akazimia moyo wakati wa taabu yake lakini umpe moyo wa ujasiri kama Daudi na nutupe ushindi katika vita zetu za maisha katika jina la Yesu Kristo amen!

Na. Rev Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni: