Jumatatu, 21 Julai 2025

Je, Mungu wako anaweza kukuokoa?

 

Zaburi 34:15-18 “Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao. Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani. Walilia, naye Bwana akasikia, Akawaponya na taabu zao zote. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa.”




Utangulizi:

Mojawapo ya sifa kubwa ya Mungu aliye hai ni pamoja na kuokoa! Mungu wa kweli ni lazima awe na sifa ya kuokoa na uwezo wa kufanya hivyo, Watu wengi wanafahamu kuwa Moja ya kazi ya Mungu ni kumuokoa mwanadamu na dhambi zake pamoja na matokeo ya dhambi hizo, hata hivyo sio tu kuwa Mungu hutuokoa na dhambi na matokeo yake yaani athari zake lakini pia hutuokoa na hatari za namna mbalimbali kwa hiyo Mungu hutuokoa na hatari za aina zote. Mungu ni mwokozi.

Zaburi 68:19-22 “Na ahimidiwe Bwana, Siku kwa siku hutuchukulia mzigo wetu; Mungu ndiye wokovu wetu. Mungu kwetu sisi ni Mungu wa kuokoa; Na njia za kutoka mautini zina YEHOVA Bwana. Naam, Mungu atakipasua kichwa cha adui zake, Utosi wenye nywele wa mtu afulizaye kukosa. Bwana alisema, Kutoka Bashani nitawarudisha, Nitawarudisha kutoka vilindi vya bahari;

Kimsingi kila mwanadamu anahitaji wokovu, katika maeneo mbalimbali, Tangu anguko la Adamu katika bustani ya Edeni mambo yetu wanadamu yamekuwa hayatuendei kwa ukamilifu kama ilivyokuwa mwanzo na kwa sababu hiyo tunamuhitaji Mwokozi, maisha ya mwanadamu yamejawa na taabu na safari yetu haijanyooka, maisha yetu yamekuwa ya milima na mabonde, mchanganyiko wa huzuni na furaha, uchungu na utamu, hatuna utulivu wa kutosha hatuwezi kufurahia maisha moja kwa moja, Amani ya kweli imeingia mushikeli, fadhaa zimetuzunguka kila upande, kukikucha ni kama hatuifurahii asubuhi, hata wale tunaowaona kwa macho kuwa ni kama wanaonekana wana mafanikio makubwa wengine wana changamoto kubwa zaidi kiasi cha kuwahurumia, tunamuhitaji Mungu atakayetuokoa, tunamuhitaji atakayetuokoa mikononi mwa adui zetu ili hatimaye tumuabudu Mungu pasipo hofu!, Watu waliomcha Mungu tangu mwanzo walikuwa wakitazamia wokovu wake, walikuwa wanajua ya kuwa Mungu ameahidi kumleta kiongozi atakayekuwa na msaada Mkubwa kwa wanadamu kifurushi kamili cha wokovu kingekuwa juu yake yani huyu ni Yesu!

Luka 1:69-75 “Ametusimamishia pembe ya wokovu Katika mlango wa Daudi, mtumishi wake. Kama alivyosema tangu mwanzo Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu;Tuokolewe na adui zetu Na mikononi mwao wote wanaotuchukia; Ili kuwatendea rehema baba zetu, Na kulikumbuka agano lake takatifu; Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu, Ya kwamba atatujalia sisi, Tuokoke mikononi mwa adui zetu, Na kumwabudu pasipo hofu, Kwa utakatifu na kwa haki Mbele zake siku zetu zote.”

Luka 2:25-31 “Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote;”

Baba zetu walikuwa wakiutumainia wokovu, wokovu ambao kwa kiyunani ni “SOTERIA” ni kifurushi cha ukombozi ambacho ndani yake kuna msamaha wa dhambi, kuna ushindi dhidi ya dhambi, kuna kutokulipwa sawaswa na makosa yetu, kuna faraja na amani ya kweli, kuna kuponywa magonjwa, kuna kushindiwa vita, kuna kuokolewa kutoka utumwani, kuna nguvu ya kushinda umasikini, na kuharibiwa kwa laana zote ni nani asiye hitaji wokovu? Kila mmoja anahitaji wokovu na kwa sababu hiyo kila mmoja anamuhitaji mwokozi na ni Mungu pekee anayeweza kuokoa, wokovu ni kazi ya Mungu peke yake! Leo basi tutachukua muda kidogo kujikumbusha juu ya somo hili muhimu lenye swali Je Mungu wako aweza kukuokoa? Na tutajifunza hivyo kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo!


·         Je Mungu wako aweza kukuokoa?

·         Mungu awezaye kuokoa!

·         Je wewe una Mungu anayeweza kuokoa?


Je Mungu wako aweza kuokoa?

Kwa kuwa wanadamu wanapitia changamoto za aina mbalimbali katika maisha! Mara nyingi sana wanadamu wamekuwa wakijiuliza swali Je Mungu anaweza kuokoa? Kwa maana ya kuwa katika kila changamoto tunazokutana nazo tunaweza kujiuliza kuwa je Mungu anaweza kunitoa katika hali hii? Je Mungu anaweza kukushindia katika hali hiyo unayoipitia? Unaweza wakati mwingine kupita katika hali na mazingira magumu sana ya kusikitisha, kutisha, kuhuzunisha, kuvunja moyo na kukatisha tamaa na ukadhani ya kuwa Mungu hashughuliki na hali hiyo au hawezi kushughulika na hali unayoipitia Je Mungu wako anaweza kukuokoa? Katika maandiko tunapewa mifano ya watu mbalimbali ambao walikuwa wanakabiliwa na hali za kutisha na katika kutishiwa huko ilifikiriwa kuwa hawataweza kabisa kupata wokovu, shetani vilevile kupitia maajenti wake alitaka kujua kuwa watu hao wataokolewa namna gani katika kona ambayo walikuwa wamekabwa? Na kutishiwa ikifikiriwa ya kuwa hakuna mungu anayeweza kuwaokoa!

Hezekia - 2Wafalme 19:10-14 “Mwambieni Hezekia, mfalme wa Yuda, maneno haya, mkisema, Asikudanganye Mungu wako unayemtumaini, akisema, Yerusalemu hautatiwa katika mikono ya mfalme wa Ashuru. Tazama, umesikia ni mambo gani wafalme wa Ashuru waliyozitenda nchi zote, kwa kuziangamiza kabisa; je! Utaokoka wewe? Je! Miungu ya mataifa wale, ambao baba zangu waliwaangamiza, imewaokoa? Yaani, Gozani, na Harani, na Resefu, na wana wa Adini waliokuwa katika Telasari? Yuko wapi mfalme wa Hamathi, na mfalme wa Arpadi, na mfalme wa mji wa Sefarvaimu, na wa Hena, na wa Iva? Basi Hezekia akaupokea waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma; kisha Hezekia akapanda, akaingia katika nyumba ya Bwana, akaukunjua mbele za Bwana.”

Shadraka, Meshaki na Abednego - Daniel 3:13-15 “Basi Nebukadreza akatoa amri kwa hasira na ghadhabu, waletwe hao Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Basi wakawaleta watu hao mbele ya mfalme. Nebukadreza akajibu, akawaambia, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa makusudi hata hammtumikii mungu wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuru iwakayo moto; naye ni nani Mungu yule atakayewaokoa ninyi na mikono yangu?

Daniel - Daniel 6:19-20 “Asubuhi mfalme akaondoka mapema, akaenda kwa haraka mpaka penye lile tundu la simba. Naye alipolikaribia lile tundu, akamlilia Danieli kwa sauti ya huzuni; mfalme akanena; akamwambia Danieli, Ee Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu wako, unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa?

Hezekia, Shadraki Meshaki na Abednego pamoja na Daniel katika nyakati tofauti waliwahi kuwa na wakati Mgumu ambao ulihitaji, wokovu na kila wakati walioupitia walipaswa kuonyesha kama Mungu wanayemuamini anaweza kuwaokoa, zilikuwa ni nyakati ngumu kwani ni mpaka uwe na imani katika Mungu wa kweli, anayeweza kuokoa ili uweze kupita katika hali hiyo!, Wapinzani wako na wale wanaokupa changamoto za Mungu uliye naye wanataka tu kujua kuwa katika hali uliyoko je Mungu wako anaweza kukuokoa? Watataka kuona kama Mungu wako anaweza kukusaidia kama unamwamini Mungu wa kweli Muumba wa mbingu na ardhi kwa hakika yeye anaweza kuokoa!

Yesu Kristo alipokuwa ameshitakiwa kwa husuda na kuhukumiwa kuuawa msalabani adui zake walimsanifu wakitaka ashuke msalabani ili yamkini ikiwezekana nao waweze kumuamini, alipolia Mungu wangu Mungu wangu mbina umeniacha, walimdhihaki wakisema anamuita Mungu aje kumuokoa walidhani kuwa Msalaba ni hatua ya mwisho na ya kuwa kama wamemtundika msalabani hawezi kuchomoka tena, walisema amemtegemea Mungu na amwokoe sasa!  

Mathayo 27:39-43 “Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisa-tikisa vichwa vyao, wakisema, Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka msalabani. Kadhalika na wale wakuu wa makuhani wakamdhihaki pamoja na waandishi na wazee, wakisema, Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe.Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini. Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu.”

Wakati mwingine adui atakuweka mahali ambapo anadhani kwamba huwezi kuchomoka na ya kuwa hata Mungu unayemuamini hawezi kukuokoa na atakuchungulia na kukudhihaki akifikiri ya kuwa hakuna anayeweza kukuokoa, Lakini jambo moja la kufurahia ni kuwa kama unamwamini Mungu aliye hai tambua ya kuwa Mungu mwenyezi, Mungu wa baba zetu Mungu wa Ibrahimu, na Isaka na Yakobo ni mwokozi na hatashindwa kukuokoa hata kidogo, Imeandikwa hatamwacha mtakatifu wake aone uharibifu, Mungu hatatuacha katika uharibifu hata kidogo! Atakuokoa yeye ni mwokozi!


Mungu awezaye kuokoa!

Mungu anayeweza kuokoa ni yule ambaye anaweza kumuokoa mtu au taifa au jamii katika shida zao zote, Ni Mungu ambaye hawezi kuvumilia mateso na huzuni, Ni Mungu anayeweza kukuepusha na majanga ya kila aina, majaribu ya kila aina na mateso ya kila aina, matisho ya kila aina, mitego ya kila aina, Magonjwa ya kila aina, hatari za kila aina na hata kifo, sio tu kuwa Mungu anaweza kuokoa lakini vile vile anauwezo wa kulinda na hata kuingilia kati maswala mbalimbali yanayoonekana kuwa magumu katika maisha yetu.Yeye anatujua vema wakati tunapohitaji msaada wake na hujitokeza mara na kuuleta wokovu kwa wakati anajua muda na wakati sahihi wa kukutetea na kufanya hivyo:-

Wakati Hezekia alipokuwa akitishiwa kuhusu mji wa Yerusalem kuwa utapigwa na Ashuru na kupewa shuhuda jinsi mfalme wa Ashuru alivyoangamiza miji mingine na miungu, hata kuandikiwa barua ya vitisho yeye aliichukua barua hiyo na kuipeleka mbele za Mungu wake hekaluni na kisha akaishitakia mbele za Bwana Mungu wake awezaye kuokoa, katika namna ya kushangaza sana Mungu aliyajibu maombi yake na hali ya mambo ikawa tofauti, Mungu alimuokoa Hezekia na watu wake na mji wa Yerusalem lakini pia Senekarebu mfalme wa Ashuru aliuawa mbele ya mungu wake asiye na msaada.

2Wafalme 19:15-19 “Naye Hezekia akaomba mbele za Bwana, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia; wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi. Tega sikio lako, Ee Bwana, usikie; fumbua macho yako, Ee Bwana, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, ambayo amemtuma mtu aje nayo ili kumtukana Mungu aliye hai. Ni kweli, Bwana, wafalme wa Ashuru wamewaharibu mataifa na nchi zao, na kuitupa miungu yao motoni; kwa maana haikuwa miungu, bali ni kazi ya mikono ya wanadamu; ilikuwa miti na mawe tu, ndiyo sababu wakaiharibu. Basi sasa, Ee Bwana, Mungu wetu, utuokoe na mkono wake, nakusihi, ili kwamba falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe Bwana Mungu, wewe peke yako.”

2Wafalme 19:32-37 “Basi Bwana asema hivi katika habari za mfalme wa Ashuru, Yeye hatauingia mji huu, wala hatapiga mshale hapa, wala hatakuja mbele yake kwa ngao, wala hatajenga boma juu yake. Njia ile ile aliyojia, kwa njia iyo hiyo atarudi zake, wala hataingia ndani ya mji huu, asema Bwana. Maana nitaulinda mji huu, niuokoe, kwa ajili yangu mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu. Ikawa usiku uo huo malaika wa Bwana alitoka, akakiingia kituo cha Waashuri, akawapiga watu mia na themanini na tano elfu. Na watu walipoondoka asubuhi na mapema, kumbe! Hao walikuwa maiti wote pia. Basi Senakeribu mfalme wa Ashuru akaondoka, akaenda zake, akarudi akakaa Ninawi. Ikawa, alipokuwa akiabudu nyumbani mwa Nisroki, mungu wake, Adrameleki na Shareza wakampiga kwa upanga; wakaikimbilia nchi ya Ararati. Na Esar-hadoni mwanawe akatawala mahali pake.”

Wakati Daniel alipofanyiwa fitina na mawaziri wenye wivu kiasi cha Daniel kutupwa katika tundu la simba wenye njaa, jambo la kushangaza ni kuwa wakati mfalme alipojaribisha kuwatupa wale waliofanya fitina katika tundu la simba ni ukweli ulio wazi kuwa walitafunwa juu juu hata kabla miili yao haijagusa chini na tangu wakati huo mfalme aliamuru watu wote katika utawala wake wamuabudu na kumtumikia Mungu wa Daniel kwa sababu ni Mungu aliye hai na mwenye uweza wa kuokoa!

Daniel 6:21-27 “Ndipo Danieli akamwambia mfalme, Ee mfalme, uishi milele. Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno. Basi mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danieli katika lile tundu. Ndipo Danieli akatolewa katika lile tundu, wala dhara lo lote halikuonekana mwilini mwake, kwa sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake. Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale watu waliomshitaki Danieli, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto wao, na wake zao; na wale simba wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande vipande, kabla hawajafika chini ya tundu. Ndipo mfalme Dario akawaandikia watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, waliokaa juu ya uso wa dunia; Amani na iongezeke kwenu. Mimi naweka amri, ya kwamba katika mamlaka yote ya ufalme wangu watu watetemeke na kuogopa mbele za Mungu wa Danieli; maana yeye ndiye Mungu aliye hai, adumuye milele, na ufalme wake ni ufalme usioharibika, na mamlaka yake itadumu hata mwisho. Yeye huponya na kuokoa, hutenda ishara na maajabu mbinguni na duniani, ndiye aliyemponya Danieli na nguvu za simba.”

Wakati Shadraka na Meshaki na Abednego walipotupwa katika tanuru la moto uliokolezwa sana huku mfalme Nebukadreza akidhania ya kuwa hakuna Mungu anayeweza kuwaokoa ni ukweli uliowazi kuwa vijana hao wa kiyahudi walimuamini Mungu aliye hai na hata walipotupwa kwenye moto muujiza mkubwa ulitokea kwani walikuwa akipiga stori na malaika kwenye moto wakiwa salama bila kuungua tukio na mujiza uliopelekea mfalme kuamuru kuwa watu wote wamuabudu Mungu aliyeweza kuwaokoa watu wake katika tanuru la Moto kwa sababu hakuonekana Mungu anayeweza kuokoa kwa namna kama ile.

Daniel 3:19-29 “Ndipo Nebukadreza akajaa ghadhabu, na sura ya uso wake ikabadilika juu ya Shadraka, na Meshaki, na Abednego, basi akatoa amri watie moto ile tanuru mara saba kuliko desturi yake ya kutiwa moto. Kisha akawaamuru baadhi ya watu mashujaa wa jeshi lake kuwafunga Shadraka, na Meshaki, na Abednego, na kuwatupa katika ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto. Basi watu hao wakafungwa, hali wamevaa suruali zao, na kanzu zao, na joho zao, na mavazi yao mengine, wakatupwa katikati ya ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto. Basi kwa sababu amri ya mfalme ilikuwa ni kali, na ile tanuru ilikuwa ina moto sana, mwako wa ule moto ukawaua wale watu waliowashika Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Na watu hao watatu, Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakaanguka, hali wamefungwa, katikati ya ile tanuru iliyokuwa inawaka moto. Ndipo Nebukadreza akastaajabu, akainuka kwa haraka; akanena, akawaambia mawaziri wake, Je! Hatukutupa watu watatu, hali wamefungwa, katikati ya moto? Wakajibu, wakamwambia mfalme, Kweli, Ee mfalme. Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu. Kisha Nebukadreza akaukaribia mdomo wa ile tanuru iliyokuwa inawaka moto. Akanena, akasema, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye juu, tokeni, mje huku. Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakatoka katika ule moto. Na maamiri, na manaibu, na maliwali, na mawaziri, waliokuwa wamekusanyika pamoja, wakawaona watu hao, ya kuwa ule moto ulikuwa hauna nguvu juu ya miili yao, wala nywele za vichwa vyao hazikuteketea, wala suruali zao hazikubadilika, wala harufu ya moto haikuwapata hata kidogo. Nebukadreza akanena, akasema, Na ahimidiwe Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego; aliyemtuma malaika wake, akawaokoa watumishi wake waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa miili yao ili wasimtumikie mungu mwingine, wala kumwabudu, ila Mungu wao wenyewe. Basi mimi naweka amri ya kuwa kila kabila ya watu, na kila taifa, na kila lugha, watakaonena neno lo lote lisilopasa juu ya huyo Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watakatwa vipande vipande, na nyumba zao zitafanywa jaa; kwa kuwa hakuna Mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.”

Yesu Kristo ambaye alidhihakiwa na kusulubiwa msalabani na kusanifiwa na adui zake na kupewa maneno ya kejeli walidhani ya kuwa Mungu hawezi kumsaidia, Neno la Mungu linasema, Mungu alimsikiliza na alimuokoa na mauti na hakumwacha Mtakatifu wake aone uharibifu kwani Kristo Yesu huyo Mungu alimfufua

Matendo 2:32 “Basi kwa kuwa ni nabii, akijua ya kuwa Mungu amemwapia kwa kiapo, ya kwamba katika uzao wa viuno vyake atamketisha mmoja katika kiti chake cha enzi; yeye mwenyewe akitangulia kuyaona haya, alitaja habari za kufufuka kwake Kristo, ya kwamba roho yake haikuachwa kuzimu, wala mwili wake haukuona uharibifu. Yesu huyo Mungu alimfufua, na sisi sote tu mashahidi wake.”

Matendo 4:9-12 “kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”      

                          

Je wewe una Mungu anayeweza kuokoa?

Tumejifunza kutoka katika mifano ya kibiblia ya wenzetu ambao walikuwa na Mungu anayeweza kuokoa na aliwaokoa walipokuwa na changamoto za aina mbalimbali, ukiwa na Mungu mwenye nguvu na anayeweza kuokoa unaweza kutembea katika hii dunia ukiwa na Amani na furaha na kiburi ya kuwa una Mungu anayeweza kutumainiwa, Mungu anayeweza kutegemewa, Mungu aliye hai, Mungu anayetetea, Mungu anayejali, Mungu anayelinda, Mungu anayejishughulisha sana na Mambo yetu, ukiwa na Mungu wa aina hii ni raha iliyoje duniani. Watakatifu waliotutangulia walikuwa na Mungu wa aina hii anayeweza kuokoa na waliufurahia wokovu wao katika mazingira na maeneo mbalimbali ni Mungu wa pekee anayeweza kutumainiwa ni yeye peke yake anayeokoa, Mungu mwenyewe amejifunua kwetu na kutamba kuwa anaweza kuokoa na kuwa hakuna Mungu mwingine

Isaya 43:11-15 “Mimi, naam, mimi, ni Bwana, zaidi yangu mimi hapana mwokozi. Nimetangaza habari, nimeokoa, nimeonyesha, na hapakuwa mungu wa kigeni kati yenu; kwa sababu hiyo ninyi ni mashahidi wangu, asema Bwana, nami ni Mungu. Naam, tangu siku ya leo, mimi ndiye; wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu; mimi nitatenda kazi, naye ni nani awezaye kuizuia? Bwana, Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Kwa ajili yenu nimetuma ujumbe Babeli nami nitawashusha wote mfano wa wakimbizi, naam, Wakaldayo, katika merikebu zao walizozifurahia. Mimi ni Bwana, Mtakatifu wenu, Muumba wa Israeli, mfalme wenu.”

Sisi wakristo tunamuamini Mungu anayeweza kutuokoa na hakuna mwingine duniani wala mbinguni awezaye kuokoa isipokuwa yeye peke yake na kwa jina lake Yesu Kristo ukiliitia Mungu amekusudia kutupa wokovu kwa yeye, kila mmoja anapaswa kujitathimini kama je kweli ana Mungu anayeweza kuokoa? Mimi ninaye Mungu anayeweza kuokoa, sisi tunaye Mungu anayeweza kuokoa, Maandiko yanamtaja Yesu, kuwa ni Yesu Peke yake mwenye uwezo huo! Nje ya Yesu hakuna mwokozi

Matendo 4:10-12 “jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”

Waebrania 7:25-27 “Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee. Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lo lote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu; ambaye hana haja kila siku, mfano wa wale makuhani wakuu wengine, kwanza kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za hao watu; maana yeye alifanya hivi mara moja, alipojitoa nafsi yake.”

Je wewe unaye Mungu anayeweza kukuokoa? Shida na changamaoto zako hazikomi wala haziondoki kwa sababu huna Mungu anayeweza kuokoa, huna Mungu anayeweza kukusikia wala huna Mungu anayeshughulika na mambo yako, Mungu asiye na msaada ni wa nini? je wewe una Mungu wa aina gani? Sisi Mungu wetu yuko hai, yuko mbinguni na uwezo anao alitakalo hulitenda.Na ni kimbilio letu

Zaburi 115:3-9 “Lakini Mungu wetu yuko mbinguni, Alitakalo lote amelitenda. Sanamu zao ni fedha na dhahabu, Kazi ya mikono ya wanadamu. Zina vinywa lakini hazisemi, Zina macho lakini hazioni, Zina masikio lakini hazisikii, Zina pua lakini hazisikii harufu, Mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi, Wala hazitoi sauti kwa koo zake. Wazifanyao watafanana nazo, Kila mmoja anayezitumainia. Enyi Israeli, mtumainini Bwana; Yeye ni msaada wao na ngao yao.”

Zaburi 46:1-5 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake. Kuna mto, vijito vyake vyaufurahisha mji wa Mungu, Patakatifu pa maskani zake Aliye juu. Mungu yu katikati yake hautatetemeshwa; Mungu atausaidia asubuhi na mapema.”

Nakutangazia ya kuwa mimi nina Mungu aliye hai, nina shuhudua nyingi za ajabu na za kutisha jinsi na namna Mungu aliye hai aliyonishindia na kunipigania, Ikiwa unataka kuona uhai wa Mungu wangu wewe jaribu kushughulika nami na ujichanganye unikorofishe katika habari za Mungu wangu, I tell you the truth you will be eliminated! Do tot mess up with me or my God! Kama unataka kupotea chezea mimi cheza na Mungu wangu ni Mungu ambaye anaokoa na kubariki na ameahidi sio tu kunibariki lakini pia yeye ni ngao yangu na thawabu yangu kubwa sana ninakusihi msomaji wangu na msikilizaji wangu hakikisha ya kuwa una uhusiano na Mungu aliye hai Mungu wa kweli na hutakuja kujuta. Yeyote atakaye jaribu kushindana nawe atasambaratishwa vibaya, ni Mungu ambaye haruhusu uonevu hata kidogo, haogopi wafalme wala mtu mwonevu wote anawakemea kwa sababu ya aina ya mafuta aliyokupaka onja habari za Bwana Mungu wangu utembee kifua mbele Mwamini Bwana Yesu utetewe, Mwamini mfanye kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako na utaokolewa onja uone ya kuwa Bwana ni mwema! Yesu Kristo hana mzaha na mali yake ikiwa unamuamini na kumtegemea jua ya kuwa kwa jina lake Mungu ameruhusu watu wote waokolewe kila atakayeliitia jina la Bwana yaani Yesu Kristo ataokoka, Ni vema kumtegemea Mungu ambaye ni mwokozi, acha kutegemea miungu mingine isiyokuwa na msaada, sisi tunaye Mungu anayeokoa leo hii kama utamuamini na kumsadiki na kutegemea kwa hakika hutatahayarika, kama ilivyoandikwa ya kuwa kila amuaminiye yeye hatatatahayarika kamwe, Mungu na akuokoe katika kila changamoto unayoipitia katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai amen!

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima 

Hakuna maoni: