1Timotheo 1:15-16 “Na neema ya Bwana wetu
ilizidi sana, pamoja na imani na pendo lililo katika Kristo Yesu. Ni neno la
kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja
ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi. Lakini kwa ajili
hii nalipata rehema, ili katika mimi wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe
uvumilivu wake wote; niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini baadaye, wapate
uzima wa milele.”
Utangulizi:
Ni muhimu kujikumbusha kuwa Yesu Kristo
mwana wa Mungu alikuja duniani kwa kusudi la kutafuta na kuokoa kile kilichopotea,
Maisha yake na huduma yake pamoja na mafundisho yake yalileta mabadiliko
makubwa sana ya kiroho na kijamii na uadilifu katika maisha ya watu wengi, mtu
mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.
Luka 19:2-10 “Na tazama, palikuwa na mtu,
jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri. Huyu
alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya
umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo. Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu
apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile. Na Yesu, alipofika mahali
pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa
kushinda nyumbani mwako. Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha.
Hata watu walipoona, walinung'unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu
mwenye dhambi.Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali
yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia
mara nne. Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu
naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa
kile kilichopotea.”
Alipokuwa duniani Yesu
alijichanganya na kuwaendea wenye dhambi kwa upendo heshima na kwa unyenyekevu
mkubwa sana na kuwafanya wao wampende na kumkubali, aliyabadilisha maisha yao
wakati mwingine wala sio kwa kuhubiri kwa nguvu bali kwa kuwaonyesha upendo na
kuwajali hususani wale waliokuwa wamekataliwa na kuonekana kuwa hawafai,
wapinzani wake wa kidini walimshutumu sana wakifiri ya kuwa alikuwa ni nabii aliyekosa kiasi kwa kuwa alikaa na kula
na kuongea na wenye dhambi, majibu yake kwa wapinzani wake yalikuwa yamejaa
hekima neema na mshangazo mkubwa sana kwani pia yalionyesha kuwa alikuwa na
ujuzi na mpango mkakati aliokuja nao ambao ni kuleta tiba kwa wenye dhambi
ambao walikuwa wakitubu kwa njia nyepesi sana na kupokea muujiza mkubwa muujiza
wa mabadiliko ya kitabia akijibainisha hivyo Yesu alisema
Luka 5:29-32 “Na Lawi akamfanyia karamu
kubwa nyumbani mwake; palikuwa na mkutano mkuu wa watoza ushuru na watu
wengineo waliokuwa wameketi chakulani pamoja nao. Ikawa Mafarisayo na waandishi
wao kuwanung'unikia wanafunzi wake, wakisema, Mbona mnakula na kunywa pamoja na
watoza ushuru na wenye dhambi? Yesu
akajibu akawaambia, Wenye afya hawana haja na tabibu, isipokuwa walio hawawezi.
Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu.”
Majibu yake Yesu na maneno yake
na matendo yanadhihirisha wazi kuwa Yesu Kristo alikuja duniani akiwa na mpango
na mkakati wa kuleta mabadiliko makubwa kwa jamii, Yesu anasifiwa kama mojawapo
ya wanafalsafa wakubwa sana duniani lakini moja ya sifa yake kubwa
inayomtofautisha na wanafalsafa wengine ni uwezo wake wa kubadilisha maisha ya
watu, kwa muda wa miaka zaidi ya 2000 kumekuwepo na wanafunzi wengi sana wa Bwana
Yesu na wanaoonyesha msimamo na mabadiliko makubwa ya kimaisha ya wale
waliokutwa na mafundisho yake hii maana yake ni kwamba hata pamoja na kuwa
amepaa mbinguni habari zake njema zimekuwa njema na dawa ya kipekee kwa jamii
kwa hiyo ni wazi kuwa mtu yeyote ayayehitaji mabadiliko ya mtindo wa maisha na
ikawa imeshindikana sehemu nyingine anamuhitaji Yesu, na sisi nasi kama watumishi wake hatuna budi
kumuuza Yesu kwa kumtangaza na kumuhubiri katika jamii kwaajili ya mabadiliko
ya kweli ya jamii yetu “Yesu Kristo kwa mabadiliko ya jamii!”, tutajifunza somo
hili Yesu kwa mabadiliko ya jamii kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Yesu
alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.
·
Mifano ya
watu waliokutana na Yesu na kubadilika.
·
Yesu
Kristo kwa mabadiliko ya jamii!.
Yesu alikuja kutafuta
na kuokoa kile kilichopotea
Kama tulivyoona katika utangulizi
wa somo hili ya kuwa Yesu Kristo alikuja duniani akiwa na mpango mkakati ulio
wazi ambao ni kuokoa kile kilichopotea, Kimsingi Yesu alikuja kusamehe watu dhambi
na kuyabadili maisha yao kabisa, alitajwa mapema katika maandiko kwamba yeye
ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao na pamoja na matokeo hasi
yaliyosababishwa na dhambi
Mathayo 1:21-23 “Naye atazaa mwana, nawe
utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi
zao. Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa
nabii akisema, Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita
jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi.”
Luka 19:9-10 “Yesu akamwambia, Leo wokovu
umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu.Kwa kuwa Mwana
wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”
Watu wote duniani wanafahamu kuwa
ni makosa kumteda Mungu dhambi na ndani ya mioyo yao wanajua na wako ambao
wanajitahidi kwa jitihada zao za kidini na kiimani lakini wanashindwa, dhambi
ni adui mkubwa wa mwanadamu analeta hatia na kuondoa ujasiri katika moyo, Dhambi pia inaweza ikakufanya
uishi kinafiki bila kupenda, inatawala na kuwafanya watu kuwa watumwa. Dhambi
ni adui yetu mkubwa kama alivyo shetani tu, tangu anguko la mwanadamu duniani
asili ya mwanadamu imeathiriwa na dhambi na kwa sababu hiyo wanadamu hawawezi
kufanya yale wanayoyapenda ikiwa ni pamoja na kumpendeza Mungu, umasikini wa kiroho na ukosefu wa tumaini umeingia, uhusiano na
Mungu umeingia mashakani na mwanadamu anapotea akijiona, Ni Yesu Kristo peke
yake aliyekuja kurejesha tumaini hilo, Ni yeye pekee aliyekuja kuonyesha upendo
wa Mungu kwetu na kwa njia ya msalaba
aliikamilisha kazi hiyo pana kwa sababu
hiyo sasa mlango uko wazi kwa jamii nzima, waliokataliwa, walevi, wachawi,
makahaba, wagonjwa, na jamii nzima inayotumikishwa bila kupenda tunapaswa
kuitumia huruma ya Mungu wetu kwa kuukubali upendo wake na kazi yake
aliyoifanya pale msalabani ili tusipotee, wajibu wetu mkubwa ni kumwamini na
tukimwamini hatutapotea na badala yake tutakuwa na uzima wa milele.
Yohana 3:16-18 “Kwa maana jinsi hii Mungu
aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye
asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni
ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye
hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la
Mwana pekee wa Mungu.”
Mifano ya watu waliokutana na Yesu na kubadilika.
Alipokuwa duniani mwokozi Yesu
Kristo alisababisha mabadiliko makubwa sana ambayo yanaendelea mpaka leo kila
inapohubiriwa injili na watu wakaikubali, Yesu alikuwa Mwalimu wa kipekee
ambaye hakufundisha tu bali mafundisho yake yalikuwa na nguvu na mamlaka
yakiambatana na uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha ya watu hata wale waliokuwa
wagumu kufikika, Yesu alibadilisha kila mtu aliyekutana naye na akawapa maisha
mapya na hapa iko mifano kadhaa:-
1. Paulo mtume - alikuwa moja ya watu
hatari sana mtu mwenye msimamo mkali katika dini yake aliyekuwa anaiona imani
ya kikrito kama imani potofu na inayoharibu mila na tamaduni za kiyahudi kwa
hiyo alitumia nguvu zake zote kuipinga na kuipiga vita imani hii, alisimamia
mauaji ya Stephano, na kwa hiyari yake aliomba kibali kwa kuhani mkuu
kuwafuatia na kuwakamata watu wote wa njia hii yaani (Waliookoka) na kuwaburuza
na kuwatia ndani.
Matendo 7:16-18 “Wakapiga
kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja, wakamtoa
nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa
kijana mmoja aliyeitwa Sauli.Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema,
Bwana Yesu, pokea roho yangu.Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana,
usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona
vema kwa kuuawa kwake.”
Matendo 9:1-5 “Lakini
Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani
Mkuu, akataka ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili
akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu. Hata
alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote
nuru kutoka mbinguni. Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli,
mbona waniudhi? Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu
unayeniudhi wewe.”
Mtume Paulo
aliyekuwa wa ajabu na adui mkubwa sana wa ukristo alipokutana na Yesu
mabadiliko makubwa sana yalitokea maishani mwake na uadui wake dhidi ya Yesu
Kristo na kanisa lake ulifikia mwisho na badala ya kuhukumiwa kuuawa Yesu
alimuamuru kuwa chombo chake cha kuihubiri injili na akawa mtu mwenye bidii na
juhudi kubwa na kuleta mchango mkubwa sana katika jamii, yeye anakumbuka jinsi
Mungu alivyomuokoa na baadaye maisha yake yakawa kielelezo kwa jamii ya wakati
ule na sasa.
1Timotheo 1:154-16 “Na neema ya Bwana wetu ilizidi sana, pamoja na imani na pendo lililo
katika Kristo Yesu. Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya
kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza
wao ni mimi. Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika mimi wa kwanza,
Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote; niwe kielelezo kwa wale
watakaomwamini baadaye, wapate uzima wa milele.”
2. Mwanamke msamaria – Alikuwa ni mwanamke
ambaye ametengwa na jamii kwa sababu ya maisha yake ya aibu, hata muda wake wa
kutembea na kwenda kuteka maji ulikuwa ni muda wa tofauti na wanawake wenzake
kijijini, Yesu alipokutana naye alizungumza naye moja kwa moja na akaweza
kushughulika na hali yake ya kiroho kimwili na kisaikolojia alimponya na kuitimiza
kiu yake ya kuhitaji maji ya uzima, baada ya muda mfupi wa kukutana na Yesu na
kuzungumza naye na kumfunulia yaliyokuwa yakiendelea moyoni mwake mwanamke huyu
aligeuka muhubiri wa injili ambaye aliwavuta wengi kuja kwa Yesu maisha
yake yalibadilika na kupitia yeye jamii
yake pia ilipata mwanga wa injili na giza likaondoka katika mji wao.
Yohana 4:3-42 “aliacha
Uyahudi, akaenda zake tena mpaka Galilaya. Naye alikuwa hana budi kupita
katikati ya Samaria. Basi akafika kunako mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu
na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe. Na hapo palikuwa na kisima
cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu amechoka kwa safari yake, akaketi vivi hivi
kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita. Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji.
Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe. Kwa maana wanafunzi wake wamekwenda mjini
kununua chakula. Basi yule mwanamke Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi
kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawachangamani
na Wasamaria.) Yesu akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye
ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji
yaliyo hai. Yule mwanamke akamwambia, Bwana, huna kitu cha kutekea, na kisima
ni kirefu; basi umeyapata wapi hayo maji yaliyo hai? Je! Wewe u mkubwa kuliko
baba yetu, Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na
wanawe pia, na wanyama wake? Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya
ataona kiu tena; walakini ye yote
atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji
nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa
milele. Yule mwanamke akamwambia, Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala
nisije hapa kuteka. Yesu akamwambia, Nenda kamwite mumeo, uje naye hapa. Yule
mwanamke akajibu, akasema, Sina mume. Yesu akamwambia, Umesema vema, Sina mume;
kwa maana umekuwa na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako; hapo
umesema kweli. Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii! Baba
zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni
mahali patupasapo kuabudia. Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja
ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu. Ninyi mnaabudu
msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa
Wayahudi.Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu
Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.
Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.
Yule mwanamke akamwambia, Najua ya kuwa yuaja Masihi, (aitwaye Kristo); naye
atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote. Yesu akamwambia, Mimi ninayesema
nawe, ndiye. Mara hiyo wakaja wanafunzi wake, wakastaajabu kwa sababu alikuwa
akisema na mwanamke; lakini hakuna aliyesema, Unatafuta nini? Au, Mbona unasema
naye? Basi yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake mjini, akawaambia
watu, Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda. Je! Haimkini
huyu kuwa ndiye Kristo? Basi wakatoka mjini, wakamwendea. Huko nyuma wanafunzi
wakamsihi wakisema, Rabi, ule. Akawaambia, Mimi ninacho chakula msichokijua
ninyi. Basi wanafunzi wake wakasemezana, Je! Mtu amemletea chakula? Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki,
niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake. Hamsemi ninyi,
Bado miezi minne, ndipo yaja mavuno? Tazama, mimi nawaambieni, Inueni macho
yenu myatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno. Naye
avunaye hupokea mshahara, na kukusanya matunda kwa uzima wa milele, ili yeye
apandaye na yeye avunaye wapate kufurahi pamoja. Kwa maana hapo neno hilo huwa
kweli, Mmoja hupanda akavuna mwingine. Mimi naliwatuma myavune yale
msiyoyataabikia; wengine walitaabika, nanyi mmeingia katika taabu yao. Na
katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke,
aliyeshuhudia kwamba, Aliniambia mambo yote niliyoyatenda. Basi wale Wasamaria
walipomwendea, walimsihi akae kwao; naye akakaa huko siku mbili. Watu wengi
zaidi wakaamini kwa sababu ya neno lake. Wakamwambia yule mwanamke, Sasa
tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe,
tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu.”
Ushuhuda wa
mwanamke msamaria unatukumbusha kazi ya Yesu ya kubadilisha jamii, na
tunajifunza jinsi ambavyo hata mtu mmoja tu aliyedharauliwa na kukataliwa
katika jamii na ambaye anaonekana hafai anaweza kabisa kubadilika na
kusababisha mabadiliko makubwa kwa jamii, Yesu anabadilisha maisha, Yesu
anabadilisha tabia, Yesu anabadilisha jamii.
3. Mathayo yule mtoza ushuru – Watoza
ushuru walikuwa mojawapo ya kundi
lililochukiwa na watu katika jamii ya wayahudi, kwanza wakihesabika kama
wasaliti kwa sababu walitoza kodi watu wa taifa lao kwa niaba ya taifa la
kigeni au la kikoloni la Warumi, lakini pia walionekana kama kundi la watu
wenye kudhulumu au wezi kwa sababu walijikusanyia mali kwa dhuluma au
kujitajirisha kwa fedha za haramu, kwa hiyo mafarisayo waliwaweka katika kundi
moja la watu najisi na wasiofaa na
kudharaulika au kuonekana kama ni wadhambi ona
Luka 18:9-14 “Akawaambia
mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine
wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili
mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu,
nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu,
wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa
zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala
hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema,
Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda
nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye
atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”
Tofauti na
mafarisayo ambao waliwabagua sana watoza ushuru na kujihesabia haki Yesu yeye
aliwaendea na kuwafanya rafiki zake akila na kufurahi pamoja nao ili hatimaye
awabadilishe maisha yao akiwepo Mathayo ambaye baadaye Yesu alimtumia kuandika
injili
Mathayo 9:9-13 “Naye
Yesu alipokuwa akipita kutoka huko aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye
Mathayo, akamwambia, Nifuate. Akaondoka, akamfuata. Ikawa alipoketi nyumbani
ale chakula, tazama, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuja wakaketi
pamoja na Yesu na wanafunzi wake. Mafarisayo walipoona, waliwaambia wanafunzi
wake, Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Naye
aliposikia, aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi.
Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si
sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”
Mifano hii inatuthibitishia na
kutuonyesha ya kwamba ni Yesu peke yake anayeweza kuleta mabadiliko ya kweli
katika jamii, na ni mabadiliko yanayoanzia moyoni na yasiyo na unafiki
yanayotokana na njia yake ya kuuendea ulimwengu kwa upendo na huruma na nguvu
za Mungu, kwa hiyo kupitia upendo wake huu aliweza kuwafikishia watu maisha
mapya bila kutumia nguvu aliwagusa watu kwa neema yake na upendo wake na kuwapa maisha mapya yaliyoathiri jamii
zao, hakuna mtume wala nabii yeyote ambaye alikuwa au amakuwa na uwezo wa
kuyabadili maisha ya watu wake na kuwafanya kuwa wema kama ilivyo kwa Bwana
wetu Yesu Kristo!.
Kwa msingi huo tunajifunza ya
kwamba hata sasa tunaweza kumpeleka Yesu kwa jamii na kumnadi kama biashara
inayoweza kuleta mabadiliko ya kila aina katika maisha yetu, Yesu atabadilisha
maisha ya watu kutoka kwenye uhalifu kuwa watu wema, kutoka kuwa wavuvi wa
samaki kuwa wavuvi wa watu, kutoka kwenye kundi la kudharaulika kwenda kwenye kundi
la kuheshimika na kutoka kwenye huzuni kwenda kwenye furaha, kanisa nini
tunapaswa kukifanya ni kuuza bidhaa Yesu na kuitangaza kwa ajili ya mabadiliko
ya jamii!, Kama alivyobadilisha wengine anaweza kumbadilisha yeyote yule hata ambaye anaonekana kushindikana
katika jamii, kama unaona ya kuwa jamii ni kama imekuchoka kwa maneno na
matendo yako Jaribu Yesu Kristo leo na utafurahi
Yesu Kristo kwa
mabadiliko ya jamii!
Katika jamii hii tuliyo nayo ambayo
inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ufisadi, ukosefu wa haki,
dhuluma uhalifu, umasikini, unyonge, mmomonyoko wa maadili, kukata tamaa na
msongo wa mawazo dunia inahitaji sana ujumbe wa Yesu Kristo ambao ndio pekee
unaobaki kuwa tiba ya kweli ya changamoto hizi ni lazima tuwapelekee watu
bidhaa hii na kuinadi kwao, Yesu Kristo kwa mabadiliko ya jamii, ni yeye pekee
ambaye anatoa mwaliko wa kuwapoza watu wote wenye kuelemewa na mizigo na kutoa
ahadi ya kweli kwamba atawapumzisha!
Mathayo 11:28-30 “Njoni kwangu, ninyi nyote
msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu,
mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata
raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”
Yesu anauwezo wa kubadilisha
mioyo ya wanadamu wote katika jamii mabadiliko ya watu kama mwanamke msamaria,
mabadiliko ya watu walioshikilia dini zao kama Paulo na mabadiliko ya watu waliokataliwa
na jamii kama kina Mathayo na Zakayo na mwanamke Msamaria, tukiwakutanisha na watu wa jinsi hiyo na Yesu
watapewa pumziko la kweli na maisha ya haki upendo na huruma zake
Kila mwanadamu aliyepoteza
tumaini na kukata tamaa katika jamii na anayehitaji kushinda changamoto za kila
siku za maisha ni aelewe na ajuzwe kuwa ni Yesu Kristo pekee anayeweza
kurejesha matumaini hayo, yeye pekee huelekeza watu kuishi maisha ya haki na
kutoa mwongozo wa maisha yanayoweza kubadilisha jamii, hutumii nguvu zako
kubadilika Ni Yesu anatumia damu yake na neema yake na trehema zake
kukubadilisha wewe unacho kihitaji ni Yesu tu!
Kwa hiyo ni lazima tumuhubiri
Yesu na kumpeleka Yesu kwa jamii yenye changamoto za aina mbalimbali tunaelezwa
kuwa nyakati za kanisa la kwanza wahubiri hawakuwa na ujumbe mwingine zaidi
walimuhubiri Yesu Kristo hawakuhubiri watu wala madhehebu yao wala makanisa yao
lakini walimuhubiri Yesu Kristo; Muhubiri Yesu tangaza bidhaa hii ieleze jamii
Yesu Kristo kwa mabadiliko, tukitaka kuwapelekea watu furaha ya kweli wapelekee
Yesu, wahubiri watu kuhusu Yesu waelekeze watu kwa Yesu, wape watu bidhaa iitwayo
Yesu Kristo; Yesu ndio sera inayouzika kuliko sera nyingine hakuna mbadala wa Yesu, Damu yake inatakasa, yeye mwenyewe
yuko hai ameketi mkono wa kuume wa Mungu waelezee watu kuhusu Yesu; Yesu
anaokoa, Yesu anaponya, Yesu anabadilisha maisha analeta tumaini, Yesu anatakasa,
Yesu anasamehe, Yesu habadiliki, Yesu haukumu mtu,Yesu ni mwaminifu, Yesu amejaa
neema na rehema na huruma hakua kama Yesu; Yesu ni yeye yule jana leo na hata
milele, tumuuze Yesu, tumnadi yetu, Tangaza uza bidhaa Yesu kwa mabadiliko ya
jamii
Matendo 8:5-8 “Filipo akatelemka akaingia
mji wa Samaria, AKAWAHUBIRI KRISTO. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza
maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa
akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia
kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha
kubwa katika mji ule.”
Yesu Kristo alikuja kutafuta na
kuokoa kile kilichopotea, na ni kupitia maisha yake na huduma yake na kazi yake
aliyoifanya pale msalabani alibadilisha maisha ya watu na anabadilisha maisha
ya watu hata leo ikiwa jamii yoyote inahitaji Amani na furaha basi jamii hiyo inapaswa
kumpokea Yesu, upendo wake, kujali kwake huruma yake na nguvu zake ziko
kutusaidia jamii yetu kwa sasa inamuhitaji Yesu zaidi kuliko kitu kingine chochote
atawaokoa na kuwasamehe na kuwapoza mioyo yao na kuwaletea nyakati za
kuburudishwa, na kuwapoza mioyo yao na kuishusha mizigo yao!
Zaburi 107:13-15 “Wakamlilia Bwana katika
dhiki zao, Akawaponya na shida zao. Aliwatoa katika giza na uvuli wa mauti,
Akayavunja mafungo yao. Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake, Na maajabu yake
kwa wanadamu.”
2Wakorintho 5:17 “Hata imekuwa, mtu akiwa
ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.”
Haijalishi maisha yako
yameharibiwa kwa kiasi gani, haijalishi ulirogwa kwa mchawi gani, haijalishi
adui zako wametambikia kwa kiwango gani, kutano moja tu na Bwana Yesu litabadilisha
maisha yako na mabadiliko makubwa yatakuwa ushahidi kwako, unamuhitaji Yesu kwa
mabadiliko ya maisha yako leo, mpe Yesu maisha
yako na hutakuwa mtu yule tena, maisha yoyote bila Yesu ni maisha
yasiyokamilika, maisha yoyote bila Yesu
ni maisha yenye kusikitisha sana, Maisha yoyote bila Yesu ni maisha yenye
upungufu, Kila mmoja wetu anamuhitaji Yesu, tunamuhitaji hata kwa ushindi wa
vita zetu, tunamuhitaji pia kwaajili ya maisha yetu yajayo, tunamuhitaji katika
ndoa zetu, kazini kwetu, biashara zetu, masomo yetu na popote, yeye hubadilisha maisha! Jaribu
leo!, omba sala hii pamoja nami endapo liko eneo katika maisha yako unahitaji
mabadiliko! Tuombe!
Bwana kama iekupendeza wewe kutubadilisha sisi, Basi nakuomba tufanye
kuwa mtu yule ambaye ungependa tuwe, tunatamani kubadilika, kwa sababu hiyo mpe
neema kila mmoja kuwa vile upendavyo wewe, nakushukuru kwa sababu
utawabadilisha wengi, hata Msomaji wangu na msikilizaji wangu utampa kuona wema
wako, asante kwa sababu utafanya zaidi ya jinsi nilivyokuomba kwa unyenyekevu
mkubwa katika jina la Yesu Kristo Amen!
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni