Esta 3:8-11 “Basi Hamani
akamwambia mfalme Ahasuero, Kuna taifa moja waliotawanyika na kukaa mahali
mahali katikati ya mataifa walioko katika majimbo yote ya ufalme wako. Nao
sheria zao zimefarakana na sheria za kila taifa; wala hawazishiki amri za
mfalme; kwa hiyo haimpasi mfalme kuchukuliana nao. Basi, mfalme akiona vema, na
iandikwe kwamba waangamizwe; nami nitalipa talanta kumi elfu za fedha mikononi
mwao watakaosimamia shughuli hiyo, waziweke katika hazina ya mfalme. Ndipo
mfalme alipoivua pete yake mkononi, akampa Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, adui
ya Wayahudi. Kisha mfalme akamwambia Hamani, Hiyo fedha umepewa, na watu pia,
fanya uonavyo vema.”
Utangulizi:
Mungu anaposhika
kalamu ni usemi wa fumbo (Metaphor) unaotumika kuelezea uwezo na utendaji wa
Mungu katika kuamua mambo ya kitaifa, ulimwengu au mtu mmoja mmoja kuhusiana na
mpango wake wa baadaye, Mungu ndiye mshika dau wa maisha ya kila mtu na
anayeujua mwanzo na mwisho wa mtu au anayeamua kuwa hatima ya mtu itakuwaje,
uweza wake huo hauwezi kuingiliwa wala kuathiriwa na mpango wowote wa
kibinadamu wala Shetani, wakati wote yeye ndiye hubakia kuwa mwenye hatima ya
mwisho wa kila mtu, familia, taifa na ulimwengu!, Hakuna mwanadamu, wala serikali
wala ufalme wala mamlaka yenye uwezo wa kuamua hatima yako itakuwaje isipokuwa
Mungu peke yake! Ni yeye peke yake ndiye anayetuwazia mema kwa sababu yeye
ndiye aliye tuumba na kwa sababu hiyo anajua hatima yetu na sababu ya yeye
kutuumba! Ameandika kila kitu kutuhusu hakuna wa kufuta.
Yeremia 29:11 “Maana
nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya
mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.”
Kwa bahati mbaya
wako watu duniani ambao hufiriki ya kuwa wao wanaweza kuamua hatima ya maisha
yako au maisha yetu au kwamba hatima ya taifa letu iko mikononi mwao, na kwa
sababu hiyo kwa kutumia nafasi waliyo nayo wakati mwingine wameweza kuingilia
na kujaribu kuzuia au kuwakwamisha watu wengine katika mpango wa Mungu wakidhani
kwa mawazo mafupi kuwa wao wanaweza kufanya hivyo, Lakini hatimaye Mungu
huingilia kati na kubadilisha mambo ni mpango wake peke yake unaoweza
kuhitimisha mambo kinyume na matarajio na mipango ya wanadamu ni wazo lake na
shauri lake na kusudi lake pekee linaloweza kusimama.
Zaburi 33:8-11 “Nchi yote
na imwogope Bwana, Wote wakaao duniani na wamche. Maana Yeye alisema, ikawa; Na
Yeye aliamuru, ikasimama. Bwana huyabatilisha mashauri ya mataifa, Huyatangua
makusudi ya watu. Shauri la Bwana lasimama milele, Makusudi ya moyo wake vizazi
na vizazi.”
Leo basi
tutachukua muda mfupi, kujifunza kwa kina na mapana ujumbe huu wa muhimu “Mungu anaposhika kalamu”na tutajifunza
ujumbe huu kwa kuzingatia vipengele viwili muhimu vifuatavyo:-
·
Njama za kuharibiwa kwa hatima yako.
·
Mungu anaposhika kalamu.
Njama za kuharibiwa kwa hatima yako
Katika dunia hii
iliyojaa iliyojawa na watu wenye chuki, uadui, uchawi, wivu, hasira, faraka
uzushi, husuda, ulafi, tamaa mbaya, chuki zisizo hata na sababu majungu na fitina,
kuharibiana na kuchafuana, kuwindana na kutafutana watu wanaweza kwa sababu au
hata bila sababu kukutafutia namna ya kukutengenezea hatima mbaya, adui zako
watatamani wakati wote wasikie unaharibikiwa na mambo yako hayaendi na wakati
mwingine watakusudia uwe na hatima mbaya hata kinyume na mapenzi ya Mungu,
watatamani kuona ndoto zako, maono yako na matamanio yako uliyopewa na Mungu
hayatimii kwa mbinu na hila za kibinadamu, kwa hiyo unaweza kuwekewa mpango
mkakati na watu ili wahakikishe ya kuwa mambo yako yanakwama, kama haya yanakukuta
hilo sio jambo geni kwako wala kwetu, maandiko yanatutia moyo kuwa tusione kuwa
ni ajabu tunapopatwa na changamoto za aina mbalimbali
1Petro 4:12-13 “Wapenzi,
msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili
kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho. Lakini kama mnavyoyashiriki
mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa
shangwe.”
Nyakati za
Biblia walikuweko watu kama wewe na wanadamu kama wewe waliokutana na
changamoto kama zako watu wakiwakusudia kuwakwamisha kwaajili ya maslahi yao au
kwa sababu ya husuda ya kitu cha kiungu ambacho Mungu amekiweka ndani yako:-
1.
Yusufu – Mungu alimpa ndoto kubwa za
maisha yake ya baadae, na ya nduguze lakini
sio hivyo tu alipata kibali kwa Mungu na kwa baba yake, Mungu alimpenda Yusufu
na alikuwa pamoja naye, lakini pia baba yake alimpenda sana na Mungu alimpa
Yusufu ndoto kuhusu hatima yake lakini hata hivyo nduguze walichukizwa na ndoto
hizo na kuanza kula njama ya kutaka kumuangamiza.
Mwanzo 37:2-11 “Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, aliyekuwa mwenye
miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo pamoja na ndugu zake; naye alikuwa
kijana pamoja na wana wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu
akamletea baba yao habari zao mbaya. Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko
wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake
wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala
hawakuweza kusema naye kwa amani. Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake
habari, nao wakazidi kumchukia; akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii
niliyoiota. Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda
wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya
mganda wangu. Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe
utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno
yake. Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni,
nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja
zikaniinamia. Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea
akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako
tutakuja tukusujudie hata nchi? Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi
neno hili.”
Ni jambo la kushangaza kwamba Yusufu alichukiwa na ndugu zake na sio
kumchukia tu walimuhusudu walikuwa na wivu wenye uchungu mkubwa dhidi yake na
kwa sababu ya ndoto zake walihakikisha wanaweka mkakati wa kummaliza ili waone
ndoto zake zitatimiaje yaani walitaka kumuua!
Mwanzo 37:13-20 “Israeli akamwambia Yusufu, Je! Ndugu zako hawachungi
kondoo katika Shekemu? Njoo, nikutume kwao. Akamwambia, Mimi hapa. Akamwambia,
Enenda, basi, ukaone kama ndugu zako hawajambo, na kundi nalo li salama,
ukaniletee habari. Basi akampeleka kutoka bonde la Hebroni, akafika Shekemu.
Mtu mmoja akamkuta, naye alikuwa anazunguka-zunguka katika nyika; yule mtu
akamwuliza, akisema, Unatafuta nini? Akasema, Nawatafuta ndugu zangu; tafadhali
uniambie mahali wanakochunga. Yule mtu akasema, Wametoka hapa, maana
niliwasikia wakisema, Twendeni Dothani. Basi Yusufu akawafuata ndugu zake
akawakuta huko Dothani. Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya
shauri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa
ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi
tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake.”
Wanadamu bila kufahamu kuwa Mungu alikwisha kumuandikia mtumishi
wake Yusufu kuwa atakuwa mkuu, wao walikuwa wakijaribu kuandika kinyume na kile
ambacho Mungu alikuwa amekikusudia kwa Yusufu, ndugu yangu hayo unayoyapitia ni
kuwa wanadamu wanataka kujaribu kuandika hitoria yako kinyume na kile ambacho
Mungu amekikusudia katika maisha yako!
2.
Daniel – Alifanyiwa njama na Mawaziri
wenzake baada ya kuwa ameinuliwa sana na
Mungu na kupata kibali kwa mfalme ambaye aliamua kumuweka juu sana katika
madaraka ya nchi ya uhamishoni, Mawaziri wa kikaldayo walikuwa na mpango wa
kuharibu hatima ya Daniel na kwa kuwa alikuwa na uadilifu walikosa sababu,
wakaona watumie njama ya kuzuia maombi kwa Mungu aliye hai, jambo ambalo
lingesababisha Daniel ashindwe na kupata sababu ya kumhukumu kwa hiyo mawaziri
waliandika mswada na kuupitisha
Daniel 6:1-16 “Ilimpendeza Dario kuweka juu ya ufalme maliwali mia na
ishirini, wawe juu ya ufalme wote; na juu yao akaweka wakubwa watatu, na
Danieli alikuwa mmoja wao; ili maliwali hawa watoe hesabu kwao, mfalme asipate
hasara. Basi Danieli huyo alipata sifa kuliko wakubwa na maliwali, kwa kuwa
roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme akaazimu kumweka juu ya ufalme wote.
Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli
kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa
maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake. Ndipo
wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo, tusipoipata
katika mambo ya sheria ya Mungu wake. Basi wale mawaziri na maamiri
wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia hivi, Mfalme Dario, uishi
milele. Mawaziri wote wa ufalme, na manaibu, na maamiri, na madiwani, na
maliwali wamefanya shauri pamoja ili kuweka amri ya kifalme; na kupiga
marufuku, ya kwamba mtu ye yote atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa
mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme atatupwa
katika tundu la simba. Sasa, Ee mfalme, piga marufuku, ukatie sahihi maandiko
haya, yasibadilike, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi, isiyoweza
kubadilika. Basi mfalme Dario akayatia sahihi maandiko yale, na ile marufuku.
Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia
nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa
kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru
mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo. Basi watu hao
wakakusanyika pamoja, wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu
wake. Ndipo wakakaribia, wakasema mbele ya mfalme katika habari ya ile marufuku
ya mfalme; Je! Hukuitia sahihi ile marufuku, ya kwamba kila mtu atakayeomba dua
kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini,
ila kwako, Ee mfalme, atatupwa katika tundu la simba? Mfalme akajibu, akasema,
Neno hili ni kweli, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi isiyoweza
kubadilika. Basi wakajibu, wakasema mbele ya mfalme, Yule Danieli, aliye mmoja
wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda, hakujali wewe, Ee mfalme, wala ile marufuku
uliyoitia sahihi, bali aomba dua mara tatu kila siku. Basi mfalme aliposikia
maneno haya alikasirika sana, akakaza moyo wake ili kumponya Danieli;
akajitaabisha kumwokoa hata jua likachwa. Ndipo watu wale wakakusanyika pamoja
mbele ya mfalme, wakamwambia mfalme, Ee mfalme, ujue ya kuwa ni sheria ya
Wamedi na Waajemi, lisibadilike neno lo lote lililo marufuku, wala amri yo yote
iliyowekwa na mfalme. Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, wakamtupa
katika tundu la simba. Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Mungu wako
unayemtumikia daima, yeye atakuponya.”
3.
Wayahudi waliokuwa uhamishoni – Mungu alikuwa
amewabarikia sana wayahudi waliokuwa utumwani, wao walikuwa na moyo ule ule wa
kumcha Mungu wakiwa wamejifunza kwamba kupitia kuabudu miungu mingine wao
walihukumiwa kwenda utumwani kwa hiyo wayahudi waliokuwa uhamishoni hawakutaka
kuabudu sanamu wala mtu waliipeleka heshima yote kwa Mungu, Kwa sababu hiyo Hamani
ambaye alikuwa amemchukia Modrekai kwa sababu alikuwa hainami mbele zake
aliamua kupitisha mswada bungeni ili kwamba ipitishwe sheria ya kuwaangamiza
wayahudi wote na hivyo waliandika mswada wa maangamizi
Esta 3:8-11 “Basi Hamani akamwambia mfalme Ahasuero, Kuna taifa moja
waliotawanyika na kukaa mahali mahali katikati ya mataifa walioko katika
majimbo yote ya ufalme wako. Nao sheria zao zimefarakana na sheria za kila
taifa; wala hawazishiki amri za mfalme; kwa hiyo haimpasi mfalme kuchukuliana
nao. Basi, mfalme akiona vema, na iandikwe kwamba waangamizwe; nami nitalipa
talanta kumi elfu za fedha mikononi mwao watakaosimamia shughuli hiyo, waziweke
katika hazina ya mfalme. Ndipo mfalme alipoivua pete yake mkononi, akampa
Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, adui ya Wayahudi. Kisha mfalme akamwambia
Hamani, Hiyo fedha umepewa, na watu pia, fanya uonavyo vema.”
Hata hivyo katika namna isiyoweze kuelezeka sheraia za waamedi na
waajemi zilikuwa zikipitishwa haikuwa kitu rahisi kubatilisha isipokuwa tu kama
Mungu ataingilia kati kwani sharia zao zikipita zimepita
Esta 8:8 “Basi waandikieni Wayahudi pia vyo vyote mpendavyo, kwa
jina la mfalme, mkatie muhuri kwa pete ya mfalme; kwa kuwa andiko lililoandikwa
kwa jina la mfalme na kutiwa muhuri kwa pete ya mfalme hakuna awezaye
kulitangua.”
4.
Yesu Kristo – Ambaye alishitakiwa kwa
husuda na wakuu wa makuhani ili tu kumsambaratisha na wakidhani kwa kufanya
hizo njama watakuwa wamemmaliza kabisa, aliandikiwa hati ya hukumu ya kufa
msalabani
Mathayo 27:17-20 “Basi walipokutanika, Pilato akawaambia, Mnataka
niwafungulie yupi? Yule Baraba, au Yesu aitwaye Kristo? Kwa maana alijua ya
kuwa wamemtoa kwa husuda. Na alipokuwa ameketi juu ya kiti cha hukumu, mkewe
alimpelekea mjumbe, kumwambia, Usiwe na neno na yule mwenye haki; kwa sababu
nimeteswa mengi leo katika ndoto kwa ajili yake. Nao wakuu wa makuhani na wazee
wakawashawishi makutano ili wamtake Baraba, na kumwangamiza Yesu.”
Wakati
mwingine adui zako watafanya njama na kukushambulia kwa hila na njia mbalimbali
ilimradi tu wahakikishe kuwa wanakupoteza au wanaharibu hatima yako kama tunavyoona
katika mifano hiyo hapo juu katika maandiko, ndugu msomaji wangu na msikilizaji
wangu inawezekana kuwa mara kadhaa na wewe unaweza kuwa umekutana na changamoto
za aina mbalimbali ambazo zote zinalenga kumaliza au kuharibu hatima yako au
hata kukuua kwa makusudi yale yale ya kuua kitu cha kiungu ambacho kimewekwa
ndani yako! Lakini hata hivyo uzoefu wa kimaandiko unaonyesha ya kuwa Mungu
huingilia kati na kubadilisha mambo pale anaposhika kalamu yake. Mungu huwaacha
wanadamu waandike miswada yao kisha yeye kama mfalme wa wafalme huitangua,
Mungu anaposhika kalamu historia yote na matarajio yote ya adui hubatilika
Mungu anaposhika kalamu.
Mungu anaposhika
kalamu maana yake Mungu anauwezo wa kubadili historia ya mambo, wanadamu na
shetani wanapokusudia kuharibu na kusitisha kile kitu ambacho Mungu amekiweka
ndani yako au kuharibu hatima yako na kukupakazia ubaya au kukukusudia ubaya
Mungu anauwezo wa kubadili historia
ya mambo mabaya na kuigeuza kujwa njema, au uwezo wa kubadili maji machungu
kuwa matamu, anauwezo wa kuandika upya hatima yako ya familia yako na taifa
lako na hata ulimwengu kwa ujumla, Mungu anauwezo wa kurejesha heshima ambayo
imeharibiwa, ana uwezo wa kuharibu mipango mibaya ya adui na kuifanya kuwa myema
au kupitia mpango huo mbaya akatokeza jambo jema kwa uwezo wake mkuu na kwa
mkono wake wa nguvu ulionyooshwa
Warumi 8:28-30 “Nasi
twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao
katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale
aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana
wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale
aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki;
na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.”
Yusufu
aliyefanyiwa njama na kaka zake ili kwamba ndoto zake zisitimie Mungu aliitumia
njia iiliyoonekana kuwa ya uchungu na ya kuumiza kuleta wokovu kwa taifa zima,
Mungu alibadili hatima mbaya iliyokusudiwa na wanadamu kutimiza hatima yeke
iliyokusudiwa na yeye Mungu anaposhika kalamu mambo hubadilika.
Mwanzo 50:15-20 “Ndugu
zake Yusufu walipoona ya kwamba baba yao amekufa, walisema, Labda Yusufu
atatuchukia; naye atatulipa maovu yetu tuliyomtenda. Wakapeleka watu kwa Yusufu, kunena, Baba yako
alitoa amri kabla ya kufa kwake, akasema, Mwambieni Yusufu hivi, Naomba
uwaachilie ndugu zako kosa lao na dhambi yao, maana walikutenda mabaya; sasa
twakuomba utuachilie kosa la watumwa wa Mungu wa baba yako. Yusufu akalia
waliposema naye. Nduguze wakaenda tena, wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama,
sisi tu watumwa wako. Yusufu akawaambia, Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu?
Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee
kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo.”
Mungu aliingilia
kati maswala ya Daniel ambaye alishitakiwa kwa hila na Mungu aliona wazi kuwa hakuwa
na hatia na mfalme akabadili mawazo kwa kumtoa Daniel katika tundu la simba na
kuwaingiza washitaki wake na familia zao Ni kitu gani kilitokea Mungu alposhika
kalamu makanwa ya simba hayakumuweza Daniel na badala yake adui zake
walishughulikiwa!
Daniel 6:21-27. “Ndipo
Danieli akamwambia mfalme, Ee mfalme, uishi milele. Mungu wangu amemtuma
malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa
mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme,
sikukosa neno. Basi mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danieli katika lile
tundu. Ndipo Danieli akatolewa katika lile tundu, wala dhara lo lote
halikuonekana mwilini mwake, kwa sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake. Mfalme
akaamuru, nao wakawaleta wale watu waliomshitaki Danieli, wakawatupa katika
tundu la simba, wao, na watoto wao, na wake zao; na wale simba wakawashinda
wakaivunja mifupa yao vipande vipande, kabla hawajafika chini ya tundu. Ndipo
mfalme Dario akawaandikia watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote,
waliokaa juu ya uso wa dunia; Amani na iongezeke kwenu. Mimi naweka amri, ya
kwamba katika mamlaka yote ya ufalme wangu watu watetemeke na kuogopa mbele za
Mungu wa Danieli; maana yeye ndiye Mungu aliye hai, adumuye milele, na ufalme
wake ni ufalme usioharibika, na mamlaka yake itadumu hata mwisho. Yeye huponya
na kuokoa, hutenda ishara na maajabu mbinguni na duniani, ndiye aliyemponya
Danieli na nguvu za simba.”
Mungu alishika
kalamu na kuondoa mashitaka dhidi ya wayahudi waliokuwa uhamishoni na wakapewa
mamlaka ya kujilinda na kuwafanyia lolote adui zao, ingawa tunaona kuwa Hamani
alikuwa na mpango mbaya lakini Mungu alibadili mpango huo na hata msalaba ambao
Hamani alikuwa amemuandalia Mordekai ukweli ni kuwa alisulubiwa yeye
Esta 8:7-11 “Mfalme
Ahasuero akawaambia malkia Esta na Mordekai, Myahudi, kusema, Tazama,
nimekwisha kumpa Esta nyumba yake Hamani, naye mwenyewe wamekwisha kumtundika
juu ya mti, kwa sababu aliwatia mikono Wayahudi. Basi waandikieni Wayahudi pia
vyo vyote mpendavyo, kwa jina la mfalme, mkatie muhuri kwa pete ya mfalme; kwa
kuwa andiko lililoandikwa kwa jina la mfalme na kutiwa muhuri kwa pete ya mfalme
hakuna awezaye kulitangua. Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa pale pale, siku
ya ishirini na tatu ya mwezi wa tatu, ndio mwezi wa Siwani; na kama vile
Mordekai alivyoamuru, Wayahudi wakaandikiwa, pamoja na maakida na maliwali, na
wakuu wa majimbo toka Bara Hindi mpaka Kushi, majimbo mia na ishirini na saba,
kila jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; na Wayahudi kwa
mwandiko wao na kwa lugha yao. Akaandika kwa jina la mfalme Ahasuero, na kutia
muhuri kwa pete ya mfalme, akazipeleka barua kwa matarishi, wamepanda farasi,
wamepanda wanyama wepesi sana waliotumika kwa huduma ya mfalme, ndio
waliozalishwa katika zizi la mfalme. Katika barua hizo mfalme aliwaruhusu
Wayahudi wakusanyike katika kila mji na kuzisimamia maisha zao, kuangamiza, na
kuua, na kulifisha jeshi lote la watu na la jimbo watakaowaondokea, wao na
wadogo wao na wanawake; na kuyachukua mali yao kuwa nyara;”
Mungu alimfufua
Yesu Kristo ambaye wazee walimshulubisha wakidhani ya kuwa wamemaliza hatima
yake, walipomuua waliomba kwamba kaburi lake lilindwe na likawekwa na muhuri
kuwa lisibadilike neno lolote katika kile ambacho kimeagizwa na askari
waliwekwa kulinda lakini Yesu alifufuka siku ya tatu!
Matendo 3:14-18 “Bali
ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; mkamwua
yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi
wake. Na kwa imani katika Jina Lake, jina lake limemtia nguvu mtu huyu
mnayemwona na kumjua; na imani ile iliyo kwake yeye imempatia huyu uzima huu
mkamilifu mbele yenu ninyi nyote. Basi sasa, ndugu, najua ya kuwa mliyatenda
haya kwa kutokujua kwenu, kama na wakuu wenu walivyotenda. Lakini mambo yale
aliyohubiri Mungu tangu zamani kwa kinywa cha manabii wake wote, ya kwamba
Kristo wake atateswa, ameyatimiza hivyo.”
Mungu yule yule
ambaye alibadilisha historia za watau wake hapo juu anauwezo wa kubadilisha
historia yako, Mungu anaposhika kalamu anafungua ukurasa mpya katika maisha
yako na kusababisha kitu kipya katika
maisha yako kitokee, haijalishi unapitia katika mapito gani, Wanadamu wote
walikuwa wameandikiwa kifo na laana ya dhambi lakini kupitia kazi iliyofanywa
na Bwana wetu Yesu Kristo pale msalabani Yesu amekuandikia habari mpya , ameifuta
ile hati iliyoandikwa ya sheria iliyokuwa na shuhuda zetu na kesi iliyokuwa
inatukabili ameigongomelea msalabani isiwepo tena ile hati ya kutuhukumu
imefutwa, Mungu anaweza kukufanya kuwa kiumbe kipya leo kama uliandikiwa hukumu
hati ya hukumu imefutwa, kama uliandikwa katika kitabu cha hukumu mambo yako ya
kale yamepita na yamekuwa mapya leo, haijalishi wanadamu wamekusudia nini leo
katika maisha yako nakuletea Yesu Kristo mzima mzima ambaye atayabadilisha
maisha yako na kuyafanya upya, wale waliokuzomea na kukuandalia kaburi, wale
waliokushitaki na kukuandikia hukumu, Yesu anabadilisha maisha yako anabadili
hatima yako, hakuna mwanadamu mwenye hati miliki ya Mungu, Mungu ni wa wote ni
Mungu wa wote wenye mwili, na Mungu akiishika kalamu na hubadili maisha yako
kabisa na kukupa muelekeo mpya, Mungu anaposhika kalamu ndugu yangu kila kitu
kitakuwa kipya tofauti na matarajio yako, Mungu anaposhika kalamu hakuna
historia mbovu isiyoweza kubadilishwa, hakuna aliyechelewa sana asiyeweza
kusawazishiwa, hakuna aliye na doa kubwa lisiloweza kufutika, hakuna aliyekatwa
asiyeweza kuchipuliwa, hakuna aliyeachwa asiyeweza kurejezwa, Muda usingeliweza
kutosha kukupa shuhuda za Ayubu ambaye shetani alifilisi kila kitu lakini Mungu
aliposhika kalamu, Ayubu akawa tajiri mara mbili zaidi, Muda usingeliweza
kutosha kuleta habari za Petro na Paulo na Sila ambao walitiwa gerezani na
maadui zao wakitarajia kuwa watakuwa wamewaweza au kuwaweka kizuizini ili
yamkini wawaangamize baadaye lakini Mungu aliposhika kalamu hali ilibadilika na
mambo yakawa tofauti itakuwa hivyo pia kwako leo, katika maisha yako, katika ndoa yako, katika huduma yako, kwaajili ya watoto wako,
kabila lako, jamii yako, taifa lako, ukoo wako, biashara zako, masomo yako,
tumbo lako la uzazi na kadhalika, Ni swala la Muda tu Mungu anaposhika kalamu
kila kitu huwa tofauti, waliosema hutoboi Mungu nanaposhika kalamu wataisoma
namba, hakuna jambo lililogumu lisilowezekana kwa Mungu, Hatima yako iko
mikononi mwa Mungu, hakuna mchawi, wala mganga wala mzimu, wale pepop, wala
shetani. Wala jinni wala mtu yeyote yule anayeweza kukuandikia kinyume na kile
Mungu amekiandika leo ni siku yako ya kuwekwa huru, ni siku ambayo Mungu
ataweka sawa pale palipoyumba katika maisha yako Haleluyaaaa!
Dua!
Ee Bwana mtumwa
wako ninaomba! Katika jina la Yesu Kristo; nakusihi ushike kalamu sasa na
kubadilisha maisha ya kila mmoja wetu na kuandika hatima mpya, andika hatima
mpya ya ndugu yangu huyu, andika hatima mpya ya dada yangu huyu, andika hatima
mpya ya familia zetu, andika hatima mpya ya huduma zetu, andika hatima mpya ya
vizazi vyetu, andika hatima mpya ya taifa letu, andika ee Bwana tofauti na wanadamu
walivyoandika, andika ee Bwana kwaajili ya jina lako tafakatifu, andika ee Bwana
kupitia neema yako na upendo wako mkubhwa sana na wingi wa rehema zako
tafadhali Bwana mwandikie kila mmoja wetu ukurasa mpya wenye kufaa kama
ulivyokusudia toka mwanzo namwombea kila
mmoja anayesoma ujumbe huu katika jina la Mwanao Mpendwa Yesu Kristo ameeen!
Na Rev. Innocent Samuel Kamote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni