Yoshua 14:12-13 “Basi sasa unipe mlima huu,
ambao Bwana alinena habari zake siku hiyo; kwani wewe ulisikia siku hiyo jinsi
Waanaki walivyokuwa huko, na miji ilivyokuwa mikubwa yenye boma; yumkini yeye
Bwana atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza watoke nje, kama Bwana alivyonena.
Yoshua akambarikia, akampa Kalebu, huyo mwana wa Yefune, Hebroni kuwa urithi
wake.”
Utangulizi:
Leo tutakuwa na muda wa
kutafakari sehemu mojawapo muhimu ya kitabu cha Yoshua katika kifungu cha Yoshua 14:6-13, ambapo kimsingi
tunaweza kupata mafundisho ya kushangaza sana tunayoyapata kutoka kwa Kalebu
mmoja wa wapelelezi 12 waliotumwa na Musa kuichunguza nchi ya Kanaani. Ni jambo
la kushangaza kwamba Mungu hakuwa amemsahahu mtu huyu sawasawa na ahadi yake
aliyompatia kwa kinywa cha Musa mtumishi wake, kimsingi wakati mwingi sana
ulikuwa umepita na sasa Kalebu ana miaka 85
lakini bado anaonyesha imani thabiti kwa Mungu, uvumilivu na ukakamavu na kama mtu
mwenye subira kubwa na tumaini la maisha asiyekata tamaa, ambapo licha ya muda
mrefu kuwa umepita anaikumbushia ile ahadi, huku akiwa tayari kuipambania haki
yake aliyoahidiwa na Mungu, baada ya watu wengine wote kuogopa kuingia katika
nchi ya Mkanaani na kupambana na majitu yaliyokuwa yanaimiliki nchi hiyo na
Mungu akamuahidi Kalebu na Yoshua.
Hesabu 14:28-31 “Waambieni, Kama niishivyo,
asema Bwana, hakika yangu kama ninyi mlivyonena masikioni mwangu, ndivyo
nitakavyowafanyia ninyi; mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili, na wote
waliohesabiwa miongoni mwenu, kama jumla ya hesabu yenu, tangu waliopata umri
wa miaka ishirini na zaidi, hao walioninung'unikia, hakika yangu hamtaingia
ninyi katika nchi, ambayo niliinua mkono wangu ya kwamba nitawaketisha humo,
isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni. Lakini Watoto wenu,
ambao mlisema watakuwa mateka, ndio nitakaowaleta na kuwatia ndani, nao
wataijua nchi ninyi mliyoikataa.”
Tutajifunza ujumbe huu muhimu “Basi sasa unipe mlima huu” kwa
kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Sababu za
ahadi ya Mungu kwa Kalebu na Yoshua.
·
Basi sasa
unipe mlima huu.
·
Mambo ya
kujifunza kutoka kwa Kalebu.
Sababu za ahadi ya Mungu kwa Kalebu na Yoshua.
Ni muhimu kufahamu kwanza ni
kwanini Mungu aliwapenda na kuwaahidi Kalebu na Yoshua kwamba watairithi nchi
ya Kanaani tofauti na wenzao miongoni mwa wapelelezi 12 waliotumwa na Musa
kuipeleleza nchi ya Kanaani, ili tuweze kujifunza kutoka kwake na kuwa na moyo
kama wa Kalebu na Yoshua hatimaye nasi tuweze kuzifurahia Baraka za Mungu.
Kalebu na Yoshua walikuwa ni askari waaminifu na watiifu kwa Mungu, wote walikuwa
wametokea Misri katika nchi ya utumwa wakiwa vijana wadogo, na walipata bahati
ya kuchaguliwa miongoni mwa wapelelezi 12 waliotumwa kuipeleleza nchi ya Kanaani
zoezi la upelelezi lilichukua siku 40, waliporejea walitoa taarifa kwa Musa nao
walikiri kuwa inchi ile kweli ilikuwa ni nchi njema na ni kweli ilikuwa ni nchi
ya maziwa na asali, na miji yake ilikuwa ni mikubwa na yenye ngome na watu wake
walikuwa hodari lakini pia waliwaona wana wa Anaki, aidha pia walifanikiwa kuja
na vishada vikubwa vya zabibu kutoka nchi ya Mkanaani.
Hesabu 13:27-28 “Wakaenda wakafika kwa
Musa, na kwa Haruni, na kwa mkutano wote wa wana wa Israeli, katika jangwa la
Parani, huko Kadeshi; wakawaletea habari, wao na mkutano wote, wakawaonyesha
matunda ya nchi. Wakamwambia wakasema, Tulifika nchi ile uliyotutuma, na hakika
yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake.
Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma, nayo ni
makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko. Amaleki anakaa
katika nchi ya Negebu; na Mhiti, na Myebusi, na Mwamori wanakaa katika milima,
na Mkanaani anakaa karibu na bahari; na kando ya ukingo wa Yordani.”
Hata hivyo katika namna ya
kushangaza sana taarifa hii iliwatisha baadhi ya wana wa Israel wasiokuwa
thabiti katika imani, kwani wao badala ya kuona fursa waliogopa na kufadhaika
sana na kwa mawazo yao walikimbilia
kunung’unika na kulalamika badala ya kumuamini Mungu kwamba anaweza
kuwarithisha nchi ile kama alivyowaahidi, wapelelezi wengine 10, walikazia kuwa
haiwezekani kuirithi inchi ile kwa sababu zao za mitazamo ya kibinadamu, Lakini
Kalebu na Yoshua wao walikuwa na mtazamo tofauti kwani walirarua nguo zao na
kuwatia moyo watu Kuwa hawapaswi kuogopa kwani Mungu ni mwaminifu na angewapa
nchi ile na watu wale walikuwa ni kama chakula kwao.
Hesabu 13:31-33 “Kalebu akawatuliza watu
mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda
bila shaka. Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda
tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi. Wakawaletea wana wa
Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita
kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote
tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno. Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana
wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi;
nao ndivyo walivyotuona sisi.”
Hesabu 14:6-9 “Na Yoshua mwana wa Nuni, na
Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua
nguo zao; wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile
tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. Ikiwa Bwana
anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi
wa maziwa na asali. Lakini msimwasi Bwana, wala msiwaogope wale wenyeji wa
nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye
Bwana yu pamoja nasi; msiwaogope.”
Kutokana na ujasiri wa Kalebu
mwana wa Yefune na Yoshua mwana wa Nuni ambao walionyesha ujasiri mkubwa
uliochangiwa na uaminifu wao na imani yao kwa Mungu, Mungu aliapa kuwaangamiza
wengine waliolalamika na kunung’unika lakini aliahidi kuwa sivyo itakavyokuwa
kwa Kalebu na Yoshua kwa kuwa wao walikuwa na kitu cha ziada na cha tofauti na
hivi ndo walivyokua:-
-
Alimfuata
Bwana kwa moyo wake wote – Hesabu 14:23-24 “hakika
yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao, wala katika hao wote
walionidharau hapana atakayeiona; lakini mtumishi wangu Kalebu, kwa kuwa
alikuwa na roho nyingine ndani yake, naye AMENIANDAMA
KWA MOYO WOTE, nitamleta yeye mpaka nchi hiyo aliyoingia; na uzao wake
wataimiliki.”
Neno ameniandama
kwa moyo wote katika maandiko ya kiebrania linasomeka kama ‘achềr Rûach
ambalo kwa kiingereza ni wind by
resemblance yaani amekuwa na roho ya kufanana nami au punzi
inayonifanania, maana yake Kalebu alikuwa anaona mambo sawasawa na jinsi Mungu
anavyoona, wakati watu wengine wote wanaona mambo hayawezekani Kalebu na Yoshua
wao walikuwa wanaona mbona inawezekana, Mungu alimuahidi Kalebu inchi ile kuwa
atairithi yeye na watoto wake kwa sababu aliona kama Mungu anavyoona, aliona
yasiyowezekana kibinadamu yanawezekana kwa Mungu, alikuwa na mtazamo wa
yanayowezekana wakati wanadamu wakiona
yasiyowezekana.
-
Walimfuata
Bwana kwa kila neno – Kumbukumbu 1:34-36 “Bwana
akaisikia sauti ya maneno yenu, akaghadhibika, akaapa, akasema, Hakika yangu
hapana mmoja miongoni mwa watu hawa wa kizazi hiki kibaya atakayeiona nchi hiyo
nzuri, niliyowaapia baba zenu kuwapa,isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, huyo
ataiona; nami nitampa yeye na watoto wake nchi hiyo aliyoikanyaga; KWA KUWA AMEMFUATA BWANA KWA KILA NENO.”
Neno amemfuata
Bwana kwa kila neno kwenye lugha ya kiebrania linatumika neno Mâlềmâlâ ‘Achar ambalo katika kiingereza
ni neno Wholly Conjugation au Wholly Conjugate
ambalo kwa Kiswahili ni kuenda Sambamba, kufuata barabara, au kufanya au
kuungana kwa hiyo sifa nyingine aliyokuwa nayo Kalebu ni kuwa aliungana na Mungu katika neno lake lote,
kile kilichozungumzwa na Mungu yeye aliungana nacho kama kilivyosemwa, hakuwa
kinyume na neno, alilifuata, alilitenda aliungana nalo na kwa sababu hiyo Mungu
anaapa kuwa atairithi nchi.
-
Alimwandama
bwana kwa utimilifu – Yoshua 14:13-14 “Yoshua
akambarikia, akampa Kalebu, huyo mwana wa Yefune, Hebroni kuwa urithi wake. Kwa
hiyo Hebroni ukawa urithi wa Kalebu, mwana wa Yefune, Mkenizi, hata leo; kwa
sababu ALIMWANDAMA BWANA, MUNGU WA ISRAELI,
KWA UTIMILIFU.”
Neno alimuandama
kwa utumilifu katika maandiko ya kuiebrania linasomeaka kama Mâlềmâlâ kusomeka linasomeka maw-lay kwa kiingereza ni neno concecrate ambalo maana yake kwa utakatifu, kwa unyoofu, kwa kujiweka
wakfu, kwa njia tofauti na wengine yaani wakati wengine wanaasi
wanazungumza kinyume na ahadi ya Mungu Kalebu yeye alifanya kwa unyoofu kwa
utakatifu, kwaajili ya hili Mungu alimpa ahadi, Kalebu hafuati mkumbo
-
Walikuwa
na roho nyingine – Hesabu 14:22-24 “kwa sababu watu
hawa wote, ambao wameuona utukufu wangu na ishara zangu, nilizozitenda huko
Misri, na huko jangwani, pamoja na haya wamenijaribu mara hizi kumi, wala
hawakuisikiza sauti yangu; hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba
zao, wala katika hao wote walionidharau hapana atakayeiona; lakini mtumishi
wangu Kalebu, KWA KUWA ALIKUWA NA ROHO
NYINGINE ndani yake, naye ameniandama kwa moyo wote, nitamleta yeye mpaka
nchi hiyo aliyoingia; na uzao wake wataimiliki.”
Neno alikuwa na
roho nyingine katika maandiko ya kiebrania linasomeka kama Achềr rûach
ambayo kwa kiingereza “Strange Spirit”, roho nyingine, yaani
tofauti na wengine ambao walikuwa na roho ya hofu, roho ya woga, yeye alikuwa
na Roho Nyingine roho ambayo sio ya
kibinadamu, Roho kama ya Mungu, ukiwa na roho nyingine tofauti na wanadamu wa
kawaida wewe unakuwa na mtazamo mwingine, mtazamo wa tofauti, unaona kwa jinsi
nyingine na kutazama mambo kwa jicho lingine, jicho la kigeni.
Basi sasa unipe mlima huu
Kalebu huyu ambaye hakuwa mtu wa
kawaida na alikuwa na kitu cha ziada, akiwa na roho ya kufanana na Mungu, akiwa
na moyo wa unyoofu, akiwa anaungana na neno la Mungu, akiwa na roho nyingine
tofauti na wayahudi wengine yeye sasa anaidai nchi ya Kanaani aliyoahidiwa na
Mungu na anamkumbusha Yoshua kwamba sasa ni wakati wa kupewa urithi wake, na
kwa vile Yoshua alikuwepo anamkumbusha yale yote Mungu aliyokuwa ameahidi kwa
kinywa cha mtumishi wake Musa, mbele ya Yoshua walipokuwa pamoja naye ni miaka
45 imepita sasa ahadi ilitolewa alipokuwa na miaka 40 sasa anakumbushia kile
alichoahidiwa na Mungu, na hataki bure anasema yuko tayari kupigana kwaajili ya
ardhi ile tena pale pale wanapoishi majitu yaani wana wa Anaki hili ni jambo la
kushangaza sana
Yoshua 14:6-13 “Wakati huo wana wa Yuda walimkaribia Yoshua hapo Gilgali;
na Kalebu, mwana wa Yefune, huyo Mkenizi, akamwambia, Wewe wajua hilo neno
Bwana alilomwambia Musa, huyo mtu wa Mungu, katika habari zangu, na katika
habari zako wewe, tulipokuwa katika Kadesh-barnea. Mimi nilikuwa mtu wa miaka
arobaini umri wangu, hapo Musa mtumishi wa Bwana aliponituma niende kutoka
Kadesh-barnea ili kuipeleleza hiyo nchi; nami nilimletea habari tena, kama
ilivyokuwa ndani ya moyo wangu. Lakini wale ndugu zangu waliokwea kwenda pamoja
nami waliiyeyusha mioyo ya watu; ila mimi nilimfuata Bwana, Mungu wangu, kwa
utimilifu. Kisha Musa akaniapia siku hiyo, akasema, Hakika hiyo nchi ambayo
miguu yako imekanyaga itakuwa ni urithi kwako wewe, na kwa watoto wako milele,
kwa sababu wewe umemfuata Bwana, Mungu wako, kwa utimilifu. Sasa basi, angalia,
yeye Bwana ameniweka hai, kama alivyosema, miaka hii arobaini na mitano, tangu
wakati huo Bwana alipomwambia Musa neno hilo, wakati Israeli waliokuwa
wakienenda barani; na sasa tazama, hivi leo nimepata miaka themanini na mitano
umri wangu. Hata sasa mimi nina nguvu zangu hivi leo kama nilivyokuwa siku hiyo
Musa aliyonituma; kama nguvu zangu zilivyokuwa wakati huo, na nguvu zangu
ndivyo zilivyo sasa, kwa vita na kwa kutoka nje na kuingia ndani. Basi sasa
unipe mlima huu, ambao Bwana alinena habari zake siku hiyo; kwani wewe ulisikia
siku hiyo jinsi Waanaki walivyokuwa huko, na miji ilivyokuwa mikubwa yenye
boma; yumkini yeye Bwana atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza watoke nje,
kama Bwana alivyonena. Yoshua akambarikia, akampa Kalebu, huyo mwana wa Yefune,
Hebroni kuwa urithi wake.Kwa hiyo Hebroni ukawa urithi wa Kalebu, mwana wa Yefune,
Mkenizi, hata leo; kwa sababu alimwandama Bwana, Mungu wa Israeli, kwa
utimilifu. Basi jina la Hebroni hapo kwanza uliitwa Kiriath-arba; huyo Arba
alikuwa ni mtu mkubwa kupita wenziwe wote katika hao Waanaki. Hiyo nchi nayo
ikatulia, vita vikakoma.”
Miaka mingi imepita lakini Kalebu
bado yuko vile vile hakuna kuchuja, nguvu zake ziko vile vile na anataka ardhi
na kama ilivyo kawaida ya wanadamu wengi sio rahisi sana kuona faida za kukaa
mlimani, tunapenda nchi tambarare iliyonyooka, watu wengi hawapendi milima, na
zaidi ya yote mlima huu ulikuwa unamilikiwa na majitu makubwa wana wa Anaki,
katika namna ya kushangaza sana Kalebu yeye anautaka mlima huo na yuko tayari
kuupigania imani yake haijapoa miaka 45 imepita yeye yuko vile vile, moyo wake
uko vile vile anamuamini Mungu vile vile akiwa na nguvu zile zile, akiwa na
ujasiri ule ule hajachoka katika mapambano hii inatufundisha kitu kikubwa sana.
Hebroni ilikuwa ni safu ya milima
katika milima ya uyahudi kusini mwa Yudea,
ambako ni ukanda wa Magharibi leo, mji wa Hebroni ni moja ya mji
unaoheshimika sana na wayahudi kama moja ya miji mitakatifu walikozikwa wazee
wetu Ibrahim, Isaka na Yakobo katika pango la Makpela kwa hiyo ni eneo zuri kihistoria, wakati wa
Yoshua sasa eneo hilo lilikaliwa na majitu, lakini Kalebu alikuwa anaiona fursa
katika mlima aliouomba kuliko nchi tambarare, kiusalama na kiulinzi yeye angeishi
juu na kama askari angeweza kuwaona adui kwa mbali na kuwa salama, chini ya
milima kulikua na bonde zuri ambalo lingeweza kufaa kwa kilimo na mifugo na juu
ya mlima makazi salama, sasa Kalebu anataka hilo, Kalebu mtazamo wake ni wa
tofauti, ni kama ana moyo wa kufanya mambo kwa njia tofauti, ni kama mtu
anayesema wakati watu wanaogopa kuendesha ndege mimi nitaendesha, ni kama mtu
anayesema wakati watu wanaogopa hisabati mimi ninapenda hisabati, ni kama mtu
anayesema wakati watu wanaogopa masomo ya sayansi mimi nitachukua sayansi, Moyo
wa Kalebu ni moyo usioogopa mambo magumu, unaona fursa katika mambo
yasiyowezekana hauchagui mambo mepesi, unachagua mambo magumu, unaona fursa
katika mambo magumu, unawaza na kuyataja yanayoonekana hayawezekani kuwa yanawezekana
“BASI SASA UNIPE MLIMA HUU” haijalishi
umri umekwenda kiasi gani anataka MLIMA
HUU ni mzee lakini bado anawaza na kufikiri akiona maono kama kijana tu,
hasemi umri wangu umeenda, hasemi nguvu zangu zimeisha, ametunza Imani yake na
uwepo wake vilevile, Kalebu hapoi wala haboi, mtazamo wake kuhusu Mungu uko
vilevile wakati makanisa mengi yanapoa yanapofikia umri wa miaka 40, wakati
wakristo wengi wanapoa wanapokaa sana katika wokovu, Kalebu hapoi, Kalebu bado
anaona maono, Kalebu bado ana ndoto Kalebu bado anamuamini Mungu, haoni kuwa
Mungu amechelewa, wala hana muda wa kumlaumu Mungu, anakumbushia haki zake,
yuko tayari kwa mapambano, Kalebu hachoki mikesha, Kalebu hachoki kufunga, Kalebu
hachoki kuomba, Kalebu hachoki mikutano ya injili, Kalebu hachoki kuhubiri
vijijini, Kalebu hachoki kufungua makanisa,
Kalebu hachoki kusoma, Kalebu hachoki kujitoa, Kalebu hachoki kuishi maisha
matakatifu, Kalebu hachoki kulifuata neno, Kalebu hachoki kuwa na roho ile ile
ya Mungu, Kalebu hachoki kunena kwa lugha, Kalebu ana ujasiri ule ule wa kuhubiri
sokoni, Kalebu, ana moto uleule aliokuwa nao jangwani, Kalebu hachoki
kuvumilia, Kalebu hachoki kusubiria, Kalebu hachoki majaribu Kalebu hataki
kuweka silaha chini Kalebu Kalebu Kalebu una miaka 85 sasa umezeeka, nguvu zako
zimeisha, umestaafu sasa Kalebu si utulie, Kalebu si nikutafutie eneo tambarare,
Kalebu si ukae karibu na mimi? Kalebu anasema BASI SASA UNIPE MLIMA HUU Mungu wangu ni moyo wa namna gani huu
Kalebu? Umepigana vita vingi Kalebu, ukae chini utulie ule mema ya nchi
inatosha sasa Kalebu, Kalebu “BASI SASA
UNIPE MLIMA HUU” kuna waanaki huko Kalebu, Kalebu nitawafukuza huko, Bwana
atakuwa pamoja nami, nguvu zangu hazijapungua niko vilevile kama hapo Musa
aliponiapia “BASI SASA UNIPE MLIMA HUU”
“shakarabashata skarabatulabosolitasaka Kalebu sotoribakarashika sata rakata
risatika yekresatabsoliboso rokosotoka
sebetaolasiotifa “BASI SASA UNIPE MLIMA
HUU neno la Mungu linasema “KWA HIYO HEBRONI UKAWA URITHI
WA KALEBU, MWANA WA YEFUNE, MKENIZI, HATA LEO”
Mambo ya kujifunza kutoka kwa Kalebu.
-
Ni lazima
tuwe na Imani thabiti kwa ahadi za Mungu
- Kalebu alikuwa ni mtu wa imani
na hakuwahi kuchoka katika kumuamini Mungu ni miaka 45 imepita tangu alipokuja
kuichunguza na kuipeleleza nchi na hata ingawaje wapelelezi wengine walileta
habari chochezi kinyume na imani Kalebu tangu wakati ule aliamini kuwa Mungu
hawezi kuwaangusha anakumbuka ahadi za Mungu na hakua na lawama kuwa Mungu
amechelewa au amekawia anaendelea
kuipigania haki yake sawa na jinsi na namna ile ile aliyokuwa nayo awali.
Yoshua 14:9-12 “Kisha
Musa akaniapia siku hiyo, akasema, Hakika hiyo nchi ambayo miguu yako
imekanyaga itakuwa ni urithi kwako wewe, na kwa watoto wako milele, kwa sababu
wewe umemfuata Bwana, Mungu wako, kwa utimilifu. Sasa basi, angalia, yeye Bwana
ameniweka hai, kama alivyosema, miaka hii arobaini na mitano, tangu wakati huo
Bwana alipomwambia Musa neno hilo, wakati Israeli waliokuwa wakienenda barani;
na sasa tazama, hivi leo nimepata miaka themanini na mitano umri wangu. Hata
sasa mimi nina nguvu zangu hivi leo kama nilivyokuwa siku hiyo Musa
aliyonituma; kama nguvu zangu zilivyokuwa wakati huo, na nguvu zangu ndivyo
zilivyo sasa, kwa vita na kwa kutoka nje na kuingia ndani. Basi sasa unipe
mlima huu, ambao Bwana alinena habari zake siku hiyo; kwani wewe ulisikia siku
hiyo jinsi Waanaki walivyokuwa huko, na miji ilivyokuwa mikubwa yenye boma;
yumkini yeye Bwana atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza watoke nje, kama
Bwana alivyonena.”
Kalebu ni moja ya
mashujaa wa Imani aliyeweza kusubiria ahadi ya Mungu kwa muda mrefu bila kukata
tamaa, wakati Ibrahimu alimsubiri Isaka kwa miaka kama 25 hivi, na Daudi
alisubiria ufalme kwa miaka kama 20, Yakobo alivumilia kwa mjomba wake kwa
miaka 20 lakini Kalebu alivumilia kwa zaidi ya miaka 45 je wewe ni mvumilivu
kwa kiasi gani?
-
Kuwa
tayari kukabiliana na changamoto – Kalebu alikuwa na ujasiri wa hali ya
juu, hakuiomba Hebroni hivi hivi tu, Hebroni ulikuwa ni mlima na sio tambarare
na zaidi ya yote ulikuwa unamilikiwa na wana wa Anaki ambao kimsingi walikuwa
ni majitu, wale wale walioogopewa na wengine Yeye Kalebu hakuogopa alikuwa
tayari kukabiliana na hali hiyo huku akimtegemea Mungu kwamba angekuwa pamoja
naye akiamini kuwa atawafukuza.
Yoshua 14:12 “Basi
sasa unipe mlima huu, ambao Bwana alinena habari zake siku hiyo; kwani wewe
ulisikia siku hiyo jinsi Waanaki walivyokuwa huko, na miji ilivyokuwa mikubwa
yenye boma; yumkini yeye Bwana atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza watoke
nje, kama Bwana alivyonena.”
-
Hakuogopa
umri wake – Kalebu alikuwa mvumilivu sana na alikuwa na nguvu amefikisha
miaka 85 lakini anajisikia ndani yuko vile vile na uwezo ule ule wa kukabiliana
na changamoto zile zile alikuwa ni mbobezi katika maswala ya vita na jeshi,
jangwa lilikuwa limemuimarisha na kumfanya kuwa mtu mgumu, umri kwake haukuwa
kikwazo cha kuzirithi ahadi za Mungu na kuzipambania aliendelea kuwa na maono na
imani na matumaini.
Yoshua 14:11 “Hata
sasa mimi nina nguvu zangu hivi leo kama nilivyokuwa siku hiyo Musa
aliyonituma; kama nguvu zangu zilivyokuwa wakati huo, na nguvu zangu ndivyo
zilivyo sasa, kwa vita na kwa kutoka nje na kuingia ndani.”
-
Aliendelea
kuwa mwainifu siku zote – Kwa kweli maneno ya Kalebu yanaonyesha kuwa
alikuwa mwaminifu na aliendelea kuwa vile vile mpaka mwisho, uaminifu wake kwa
Mungu tangu ujana wake mpaka wakati huu
anaonekana kuwa alikuwa mtu asiyekata tamaa, shujaa na mtu aliyeendelea
kumtegemea Mungu huku akikumbuka ahadi zake na haki yake aliudai mlima huo kwa
sababu alikuwa na uhakika na Mungu wake kuwa hatomwangusha
Yoshua 14:7-8 “Mimi nilikuwa mtu wa miaka arobaini umri wangu, hapo Musa mtumishi wa Bwana aliponituma niende kutoka Kadesh-barnea ili kuipeleleza hiyo nchi; nami nilimletea habari tena, kama ilivyokuwa ndani ya moyo wangu. Lakini wale ndugu zangu waliokwea kwenda pamoja nami waliiyeyusha mioyo ya watu; ila mimi nilimfuata Bwana, Mungu wangu, kwa utimilifu.”
Hitimisho:
Kalebu anampa somo kila mmoja
wetu kuhusu imani, uvumilivu, subira, ujasiri, na uaminifu kwa Mungu, alikuwa
ni mtu asiyeogopa changamoto wala mtu wa kukata tamaa, hakukuwa na hata tone la
hofu maishani mwake kauli yake BASI SASA
UNIPE MLIMA HUU iwe changamoto kwetu kwamba tuteendelea kumuamini Mungu sio
kwa mambo mepesi tu bali hata kwa mambo magumu, na tutaendelea kuwa wavumilivu
bila kujali muda, na tutaendelea katika imani bila kupoa, na tutaendelea kuwa
na ujasiri wa kukabiliana na magumu bila kujali umri na kuwa tayari kumtumikia
Mungu mpaka siku zetu za mwisho!
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni